*MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN -- 036*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Akacheka haswa.
Lakini furaha yake hii haikudumu, akasikia sauti huko nje ya nyumba ikimuamuru atoke ndani upesi!
Walikuwa ni wanajeshi wa Phares wapo nje. Walishajua Rhoda amerejea himayani na sasa walikuwa hapo kutekeleza agizo la kumkamata mwanamke huyo mara moja kama vile walivyoagizwa.
ENDELEA
Venet akajiuliza kipi cha kufanya. Akaona ni kheri akaficha makucha yake kwa sasa. Atulie aone mchezo unaendaje hapa. Hakuona haja ya kujifanya mjuaji kwenye ngoma ya kigeni.
Basi taratibu akatoka ndani na kwenda kukutana na rundo kubwa la wanajeshi likiwa limemebelea kila aina ya silaha kana kwamba wamekuja kumkamata mhaini mwenye nguvu isiyo mithilika.
Venet akastaajabu jeshi hili! Asiongee kitu akasukumwa na teke mpaka chini. Akafungwa mikono akidhihakiwa kwa kuitwa mlozi mkubuhu, muuaji na shetani asiyestahili hata tone la huruma!
Japokuwa sifa hizi zilikuwa ni za kweli, Venet akaona amedharauliwa mno. Akajiona ameshushwa na sasa anafanana na taka shimoni. Si mwenye thamani. Lakini bado akavumilia.
Akiwa chini, Alphan akaweka mguu mgongoni mwake akimwambia:
"Ulidhani sitakukamata? Pole sana. Hatimaye mwisho wako umefika. Utatundikwa mbele ya kadamnasi kila mtu aone namna unavyopapatika ukitokwa na roho."
Alafu akamtemea kohozi ptuuh! Venet akatetemeka kwa hasira. Akajihisi moyo wake unasagwa na mche wa kinu. Akang'atameno kwa uchungu akimtazama Alphan kwa jicho la kizandiki, Alphan akatabasamu na kumkebehi.
Akifanya hayo wanajeshi wake wakawa wanashangilia kana kwamba bondia wa nyumbani anamshushia makonde bondia mgeni.
Mwishowe Venet, aliye katika mwili wa Rhoda, akafungashwa safari kuelekea lupango. Huko njiani akavutwa kama ng'ombe. Alikuwa peku akichomwa na miba na kutobolewa na mawe.
Watu njiani wakauliza kulikoni, wakaambiwa ni mlozi huyo. Basi nao wakaokota mawe na kumrushia, kama hayakuwepo wakamwagia mavumbi ama kumtemea mate!
Venet aliwezaje kuyavumilia yote haya?
Muda wote huo akawa anatazama chini akifunikwa na nywele. Alikuwa anautazama udongo anaoukanyaga. Mdomoni kuna kitu alikuwa anateta lakini hakikusikika.
Akafika lupango na kutiwa ndani akisukumiwa humo. Alikuwa peke yake katika chumba hiki, bila shaka walihofia kumchanganya na watu wengine kwasababu za usalama.
"Utakaa humo mpaka utakapokuja kuonja kitanzi!" Akasema Alphan akimuaga.
Basi huko nje kukawa sherehe kwenye kilabu cha pombe. Hatimaye mlozi amekamatwa! Watu wakanywa na kufurahi.
Habari zikasambaa ndani ya himaya nzima kwamba Rhoda ni mchawi na amekamatwa akitokea Tanashe. Habari hizi zikawashtua watu na kuwasisimua.
Mwaname yule mrembo, amekamatwa ulozi? Anhaa... basi ndo maana jengo lake likawa ghofu hivi ghafula? Ndiyo maana biashara yake ikatokomea kusikojulikana?
Watu sasa wakapata majibu. Kila mtu akawa anangoja kesho yake mwanamke huyo atundikwe kunyongwa kwenye uwanja wa hadhara. Wote waende kushuhudia!
**
"Mfalme, tumeshamtia nguvuni!" Akasema Alphan muda mfupi baada ya kuonana na mfalme, usoni akiwa na tabasamu pana.
Mfalme akatahamaki kidogo. Alikuwa yupo juu ya mgongo wa farasi akiwa ametoka safarini. Alimtazama vema Alphan aliyekuwa na pumbazo la furaha usoni, akamuuliza:
"Yupo wapi sasa?"
"Kule chimboni, unataka kumuona?"
"Ndio ila si kwa sasa. Naomba nipumzike kidogo, nadhani unaona nilipotokea."
Alphan akainamisha kichwa chake chini, mfalme akazama ndani alipopata kujimwagia maji na kisha kuketi mezani na mchumba wake, bibie Tattiana.
"Pole kwa safari," mwanamke akamkarimu.
"Ahsante, umeendeleaje hapa na upweke?" Mfalme akauliza kwa uso mtam.
"Upweke?" Tattiana akadakia kwa toni laini. "Sidhani. Nawezaje kuwa mpweke wakati kuna watu wengi hapa?"
Mfalme akatabasamu.
"Kwahiyo ulikuwa na nani akikusaidia kusogeza muda?"
"Watu wengi tu ... Nilikuwa nikiongea na wale wamama."
"Wamama? Unamaanisha wale vijakazi?"
"Sijiskii vizuri kuwaita hivyo. Ni watu wazima kama mama yangu!"
Mfalme akaangua kicheko kisha akamshukuru Tattiana kwa kumfanya afurahi kwani alikuwa ametingwa sana kichwani na hakutegemea kama atapata kuonja hata tabasamu mpaka siku hiyo inakoma.
Habari hiyo ikamvutia Tattiana, akataka kujua nini kilimsibu mfalme. Mbona alitoka na furaha kasrini?
Mfalme akanywa kwanza mvinyo alafu akashusha pumzi ndefu. Akawaamuru vijakazi wake wote wawapatie faragha kabla hajafungua jumba lake la maneno. Wakamtii.
"Kulikuwa na kikao huko himaya ya Mamu. Wafalme wote wa ukanda huu walikuwa wamekutana huko, nami nilipokea ujumbe wa kuhitajika.
Sikutaka kuupuuzia huo wito, nikautii. Lakini niliyokutana nayo huko, yamenitia simanzi na kunitetemesha mwili!"
Tattiana akashindwa kungoja,
"Nini hiko?' Akawahi kuuliza.
Mfalme akaminya mdomo wake akitazama meza. Alafu kwa utulivu akiwa mbali fikirani, akasema:
"Mfalme wa himaya ya Maam anakaribia kufa. Hivi tuongeavyo, yupo hoi taabani kitandani, ni pumzi tu ndiyo wanamhesabia. Hawezi kupona abadani. Anatia huruma sana, haswa nikiwatazama wajane na watoto atakaowaacha bado wakiwa wanamhitaji.
Lakini inaniumiza zaidi na kunikosesha amani kwani kifo chake kina mahusiano na mikono yangu!"
Hapa Tattiana akaogopa. Akatoa macho akikunjama ndita, akamuuliza mfalme kivipi ahusike na kifo cha mfalme wa himaya nyingine? Lini alienda huko akamshikia upanga ama kumtumia maadui wammalize?
Mfalme akamwambia hakuna lolote kati ya hayo aliyoyaainisha amepata kulifanya. Mfalme wa Maam anaweza akawa na maadui ndani ama nje ya himaya yake, hilo halikujalisha. Hakuna mtu anayependwa na wote.
Ila shida inakuja kwamba mfalme huyo amejazwa sumu na tunda la Cedar! Hapa ndipo panamtia hatiani kwani tunda hilo linapatikana ndani ya Goshen pekee!
Ni kivipi tunda hilo likafika huko na hata kutumika kumdhuru mtu huyo mwenye nafasi ya juu ndani ya himaya?
Kwahiyo Goshen inatuhumiwa kwa haya mawili. Mosi, kurudia biashara ya kuuza matunda hayo haramu yaliyopigwa marufuku. Na pili, baya zaidi, kutuhumiwa kufanya jaribio la kumuua mfalme huyo wa Maam kwasabababu zisizojulikana.
"Amah!" Tattiana akaufunika mdomo wake kwa bumbuwazi.
"Kwahiyo hivi tunavyoongea," mfalme akaendelea kumwaga maneno. "Nimepewa takribani siku tano tu kutoa maelezo na ushahidi. Litakaposhindikana hilo, basi hatua stahiki na kubwa zitachukuliwa."
"Zipi hizo?" Tattiana akataka kujua.
"Mosi, Goshen kutengwa na himaya zote na huku wananchi wake wakifanywa kuwa haramu katika kila ardhi watakayokanyaga. Pili, himaya zote kuungana na kuiteketeza Goshen kwenye uso wa dunia. Ama tatu, mfalme wa Goshen kunyongwa mpaka kufa kwenye karamu ya mwaka!
Adhabu itateuliwa kutokana na maelezo yatakayotolewa."
Tattiana akahisi moyo wake umekuwa mzito ghafla. Hata akastaajabu ni kwa namna gani mfalme aliweza kukenua kwa kicheko muda mfupi hapo nyuma.
"Sasa tutaepukaje kikombe hiki?" Akauliza akijawa na woga.
"Kwa njia moja tu," akajibu mfalme. "Nayo ni kumpata mtu aliyepanda, kuchuma na kusafirisha Cedar kwenda huko."
"Hakuna mbadala mwingine!" Akamalizia.
- JE WATAMJUA MTU HUYO KABLA GOSHEN NZIMA HAIJAHUKUMIWA?
- NINI TATTIANA ATAFANYA AKIJA GUNDUA BABA YAKE ANAHUSIKA NA HILI? JE ATAHISI CHOCHOTE?
- VENET ATATIWA KITANZI MBELE YA KADAMNASI?
[emoji91][emoji91][emoji91]