*MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN -- 022*
*Simulizi za series*
"Nani huyo anashindwa kubisha hodi?"
Aliropoka mzee wa baraza akishikilia dhakari yake inayokojoa. Alikunja shingo kutazama, uso kwa uso akakutana na pande la mwanaume aliyesimama kana kwamba mlinzi wa mfalme.
"Kumbe wewe!" Alifoka. "Pumbavu, huna adabu enh? Umechoka kazi!" Kibaraka wa Rhoda hakujibu kitu.
Alidaka koo la mzee huyo kama kuku akamnyanyua juu na kumbamizia ukutani kwanguvu. Kiganja chake kipana kilimeza shingo yote ya mzee aliyeishia kupata taabu kupumua. Alihangaika akitia huruma.
"Sikiliza na uelewe," alisema pande la jibaba. "Sina muda wa kupoteza hapa na wewe. Nimekufuata humu kukuambia juu ya jambo moja tu: mpigie kura Phares. Hakikisha anapita!" Mzee hakuweza kusema jambo kwasababu ya kukabwa.
Uso wake ulikuwa mwekundu mdomo akiutapanya. Mikono yake miwili ilishindwa kuondoa mmoja uliomkaba pasipo kujali namna gani alivyokuwa akihangaika.
"Endapo asipopita, kwa namna yoyote ile, basi jua hautabaki salama." Mwanaume huyo kijakazi wa Rhoda alipomaliza kusema hayo, alimuachia huru mzee. Alibandua kiganja chake kooni akamshudia mzee akidondoka chini akitafuta hewa.
Hakuketi kumsubiri, aligeuka akaondoka. Alipofika mlangoni, aliitwa na sauti iliyokuwa inatoka kwa taabu.
"Kijana!" Akasimama. "Unadhani utatumia mabavu yako kubatilisha kura yangu?" Mzee aliuliza. Bado alikuwa chini ashindwe kujinyanyua.
"Kamwe! Kama wataka kuniua, basi karibu. Nimeshakula chumvi za kutosha. Ila ukae ukijua kwamba, mawazo yangu ni yale yale na nitayasimamia milele kwa faida ya himaya ya Goshen, na si mtu mmoja!"
Mwanaume yule kibaraka wa Rhoda alifungua mlango. Kabla hajatoka ndani, alimtazama mzee huyo wa baraza na kisha akasema kwa sauti ya utulivu:
"Sawa kuhusu wewe, lakini vipi kuhusu mke wako, Rabina, na watoto wako wawili; Asilam na Poogi? Nao unataka wafe?" Kauli hiyo ilimgutua mzee. Hakutegemea kama familia yake ilikuwa bayana kiasi hicho. Alinyanyuka.
"Usije ukathubutu kugusa familia yangu!" Alifoka.
"Kama unataka kunijaribu, nenda kinyume na nilichokuambia. Utawakuta wote mizoga! Kuanzia mkeo aliye nyumbani, mpaka watoto wako wanaoishi upande wa Duke," alisema kibaraka wa Rhoda kabla hajatoka ndani na kuurudishia mlango.
Mzee allipatwa na uoga sasa. Alijihisi yu uchi. Kitendo cha kuambiwa mpaka makazi ya wanaye kilizidi kumzuzua na kumkatia pande hofu. Alisimama akaenda zake. Akiwa anakatiza kuingia ndani ya uwanja wa baraza, alitazamana na mwanaume yule kibaraka wa Rhoda. Mwanaume huyo akamuonyeshea ishara ya uangalizi kwa kunyooshea vidole vyake viwili machoni.
Mzee huyo alijirudisha kwenye kiti chake kikao kikaendelea kama ada. Muda wa kunywa ulikuwa umeshapita sasa na hivyo basi ukawa umewadia ule wa kufanya uteuzi.
Kati ya wazee watano wa baraza, ni wawili tu ndio walikuwa wazima. Wengine wote walikuwa hoi kwa kilevi. Kwa mujibu wa utaratibu, wazee hao wakawa wameshajitoa kwenye maamuzi ya siku. Hivyo basi uteuzi ukawa unaelekea kufanywa na wazee wawili tu.
"Basi na utaratibu uheshimiwe," alisema mzee wa baraza aliyeketi kando na yule aliyetoka kubanwa chooni. Wao pekee ndio walikuwa hai muda huo, pamoja na Phares ambaye aligusa glasi moja tu ya mvinyo kisha akaacha.
"Kama ilivyo ada huu ni wasaa sasa wa kuteua kiongozi mkubwa wa Goshen; mfalme. Mfalme atakayekuwa juu ya nyumba zote ndani ya mipaka yetu, kuanzia kaskazini mpaka kusini, magharibi mpaka mashariki.
Mfalme atakayetuwakilisha nje ya mipaka na kutuongoza ndani ya mipaka. Ambaye neno lake litakuwa sheria, mkono wake utakuwa ngao." Baada ya kusemwa maneno hayo, alitajwa Phares peke yake kama mtu anayewania ama kupendekezwa kwa ajili ya nafasi hiyo. Hakukuwa na mwengine, hivyo basi wajumbe wakawa na fursa ya kupembua na kumchambua mlengwa, Phares.
Aliulizwa kuhusu historia yake, akashindwa kuitaja. Hakuwa anakumbuka kitu kuhusu historia yake. Si lolote, si chochote. Hakuona haja ya kuongopa, akasema ukweli.
"Tangu nipate fahamu zangu, sijawahi kujua kingine zaidi ya Goshen. Nimejikuta najua himaya hii nikiwa katika umri mkubwa.
Nilijikuta namjua Vedas kabla ya mtu mwingine yeyote. Hakuna aliyewahi nambia asili yangu, chimbuko langu. Kila niliyemuuliza kuhusu wazazi wangu, hakuwa anajua.
Nilipomuuliza Vedas, alisema yeye ndiye mama na baba yangu. Sikuwahi kumuelewa mpaka anakufa." Maneno hayo yalizaa tafakuri kwenye vichwa vya wajumbe. Walikosa cha kuuliza maana hakuwepo wa kumuuliza. Ilibidi kikao kiendelee.
Waliuliza kuhusu uzoefu wa mtahiniwa kwenye mambo ya uongozi, naye Phares akapata kuwaonyesha juu ya uwezowe kipindi chote cha utawala wa Vedas. Namna alivyofanikiwa kupambana na kuwashinda maadui.
Baada ya hapo kukawa hamna tena maswali, kura ikapigwa. Kila mdomo wa mjumbe ulikiri kuridhishwa na Phares, kwahiyo mtahiniwa huyo akawa amefaulu.
"Kwanzia sasa wewe ni mfalme mteuliwa. Utakuwa mfalme kamili pale utakapoapishwa mbele ya hadhara! Siku tano baada ya kikao cha uteuzi." Akadakia mzee mwingine, yule aliyekabwa chooni.
Sauti yake ilikuwa mfifia. Uso wake ulikuwa na ajizi na ayasemayo. "Kwa mujibu wa kanuni na taratibu, hakuna yeyote mwenye uwezo wa kutengua maamuzi ya baraza. Na hivyo basi maamuzi yake yaheshimiwe."
Baada ya hapo, kikao kikafungwa kwa kupeana mikono. Muda mfupi mbeleni tarumbeta kubwa likapulizwa kuihabarisha Goshen yote kwamba kiongozi mpya amepatikana.
Tarumbeta hili lililia mara tatu likigeuziwa kila pande. Basi kila kona ya Goshen wakajua nini kilikuwa kinaendelea. Walikuwa na hamu kubwa ya kumjua kiongozi wao mpya.
Sauti hiyo ya tarumbeta ilipofika masikioni mwa Rhoda, ilizaa tabasamu pana. Alijikuta akiangua kicheko yeye mwenyewe. Alisugua viganja uso wake uking'aa kwa furaha.
"Hatimaye," alijisemea. "Hatua moja baada ya nyingine. Sasa Goshen inakaribia kujaa kiganjani mwangu." Alichoropoa chupa ya mvinyo toka kabatini akagida. Alicheka tena.
"Ni punde ... si muda mrefu. Himaya zote zitakuwa chini yangu. Chini yangu mimi Rhoda," alisema kwa msisitizo kana kwamba kuna mtu alimkatalia.
Alikunywa na kunywa, akiwa anamalizia chupa ya mvinyo wake huo, kibaraka wake akiwa ameongozana na wanawake wawili wanafika nyumbani kwake. Wanawake hawa walikuwa juu ya farasi mmoja, wakati pande lile la mtu, kibaraka, akiwa juu ya farasiwe.
Wanawake hawa wawili ni miongoni mwa wale walikuwamo kwenye mkutano wa baraza la wazee wakihudumia. "Karibu sana!" Rhoda alipaza sauti. Aliwakarimu wageni wake kwa bashasha. Aliwahudumia kwa kuwamiminia mvinyo kwenye glasi ya kila mmoja.
"Ilikuwa ni kazi nyepesi, haikutuwia vigumu," alisema kibaraka kisha akaisindikizia na fundo kubwa la mvinyo.
"Ndani ya muda mfupi tulikuwa tumeshamaliza kila kitu.
"Bila shaka mlifanya kama nilivyowaagiza," alidakia Rhoda.
"Ndio, mam," akajibu mwanamke mmoja miongoni mwa wale wawili. "Punde baada ya mzee wa kwanza wa baraza kutoka, tulipata mwanya wa kuwatilia madawa kwenye vinywaji wale wawili uliotuagiza.
Tulipata shaka juu ya yule aliyeenda chooni, ila Nade alimalizana naye huko huko. Hivyo hakukuwa na shida kabisa." Rhoda akatabasamu.
"Hongereni sana kwa kazi nzuri. Ila si kwamba tumemaliza, hapana. Ni hatua moja tu katika safari ambayo ndio kwanza inaanza. Tuwe makini sana, nitawahitaji zaidi."
Aliposema hayo akabandika matabasamu kwenye nyuso za wageni wake kwa kusema;
"Ntawapa mara mbili ya ujira tuliokubaliana, maana mmenifurahisha."
.
.
.
.
.
.
***
.
.
.
.
.
.
Usiku ulikuwa umekua zaidi. Tungelinganisha na majira ya huku, basi tungesema ilikuwa ni saa saba ya usiku, tena yenye madakika zake, si changa.
Wakati wengine wakiwa wamejifunika na wapo juu ya vitanda kuitafuta asubuhi, vibaraka wawili wa Karim, mganga maarufu, walikuwa ndani ya msitu mkubwa wakijikunyata.
Hali ya hewa ilikuwa ya baridi msituni humo. Pia msitu ulikuwa umelowana kwa mvua zilizokuwa zinanyesha mara kwa mara. Hakukufaa kwa malazi ya binadamu. Sauti za vyura zilikuwa zinaita. Na hata wadudu walikuwa wakirandaranda huku na kule.
Vibaraka hawa wawili wa Karim walikuwa wamejifunika na blanketi moja zito. Ila chini walikuwa wamelalia kitambaa chepesi juu ya udongo mbichi, hivyo basi mwili wao bado ulikuwa unakosa joto jema kupambana na hali ya hewa ya muda huo eneo hilo.
Ila kutokana na uchovu mzito wa kutembea juu ya migongo ya farasi kwa siku kadha wa kadha, walikuwa hoi na mazingira hayakutosha kuwanyima usingizi. Walilala kando ya farasi zao.
Kuna muda fulani, vyura waliacha kulia, na wadudu waliacha kukatiza, kukawa kimya. Ila muda huo hakuwa unadumu sana, ni takribani kama dakika moja tu kisha mambo yanaendelea kama kawaida.
Hali hii ilitokea kwa mara tatu. Ilipotokea kwa mara ya nne, mambo hayakuwa kama awali. Kuna kitu cha kushangaza kilijiri. Kitu hichi hakikujulikana kama ni binaadam ama kiumbe kingine. Kilikuwa kinang'aa kwa kuwakawaka kimulimuli.
Umbo halisi la kitu hiki bado lilikuwa ni tenge. Kiliwasogelea vibaraka wa Karim katika hali ya kuwakawaka na kuumiza macho. Kilipokaribia, joto liliongezeka na punde vibaraka wakaanza kuvuja jasho kwa wingi kama vile wamemwagiwa maji.
Mmoja alikurupuka. Alitazama kando na kando, hakuona kitu. Sauti za vyura na wadudu zilikuwa zinaita kama kawaida. Alipotazama takribani kwa dakika moja pasipo kuona lolote, aliamua kujilaza.
Alilala kwa dakika mbili tu, hali ikaanza kubadilika tena kwa joto kuongezeka. Alikurupuka akaangaza. Mwili wake ulikuwa unavuja jasho mno, ila ajabu akiamka alikuwa anakuta hali ya hewa baridi kupita kiasi. Fika akajua mambo hayako sawa. "Saud, amka!" Alimkurupua mwenzake kwa kumsukumiza sukumiza mgongo.
"Nini bana..." Saudi akalalamika kimang'amung'amu.
"Amka tuondoke!"
"Twende wapi usiku wote huu? Tulale bana mie niko hoi mtepe," alisema Saud. Yote haya alikuwa ananena akiwa amefumba macho. Sauti yake ilikuwa ya kunguruma na mwili wake ukiwa teketeke dhoofu.
"Saud, tuko kwenye himaya ya watu," alisisitizia mwamshaji. Hakuonyesha lepe la masikhara hata kidogo. "Amka tusonge, hapa si salama!"
"Mie siendo popote bana ... we nenda! Niache!"
Alifoka Saud. Bado alikuwa yu usingizini. Macho yake hayakuwa yamefunguka. Hata mdomo wake ulikuwa umebanwa kivivu, alikuwa anaongea aking'ata meno.
Haraka mwamshaji aliamka akasimama. Alitazama kila pande. Japokuwa hakuona kitu, lakini moyo wake ulikuwa unapiga kwa kasi. Alikuwa anahisi kabisa kuna kitu. Kuna wakati vinyweleo vilikuwa vinamsimama! "Saud, mie naenda!" Alisema akimsukumiza mwenzake kwa mguu. Saud aliitikia kwa miguno pasipo kujihangaisha.
Mwamshaji alimfuata farasi wake akamfungua kamba apate kuondoka. Ila kabla hajayoyoma, aliona ni vema tena kumshitua Saud, mwenzake. "Saud, unakumbuka Karim alituambia nini tukiwa njiani? Tupo kwenye himaya ya wengine, tuwe makini. Ni vema tukaepusha shari kadiri tuwezavyo. Si kila mara kinga zetu zitafanya kazi." Mwamshaji alikuwa anaongea na sikio la kufa, hakueleweka. Mara hii Saud hakuonyesha muitikio, hata kwa kuguna. Alikaa kimya kana kwamba maiti.
Mwishowe, mwamshaji alijiondokea akiongozana na farasi wake. Punde hakuwa anaonekana. Saud alibakia peke yake sasa akikoroma kwa uroho wake wa usingizi. Alijikobeka blanketi mpaka shingoni. Alijikunyata vema kujipa joto.
Baada ya dakika kama tano hivi, milio ya chura ilikoma ghafla. Hata wadudu nao walinywea. Kulikuwa kimya mno kiasi kwamba unaweza kudhani umekuwa kiziwi. Kimya hiki kilidumu kwa muda. Kiumbe kile kiwakacho hakikuonekana, hatukujua kilikuwepo wapi.
Saud alikuwa ameachama mdomo akimwaga udenda. Hakuwa na habari yoyote. Akiwa anaendelea kulala, mara mdudu mmoja mweusi mwenye ukubwa wa mende, anajongea kuufuata mdomowe. Mdudu huyo anazama ndani ya mdomo wa Saud. Kisha kunaendelea kuwa kimya.
Hakuna lolote linalotukia kwa takribani sekunde tano. Baada ya hapo, Saud anakohoa mara moja. Mara tena ... mara tena na tena! Anakohoa mno mwishowe anaamka kwa kushindwa kulala.
Alishikilia kifua chake akiendelea kukohoa zaidi na zaidi. Alianza sasa kukohoa damu. Kikohozi hakikukoma abadani. Alikohoa mpaka akaanza kukosa hewa. Alisimama akikohoa. Matokeo yake, alipoteza fahamu. Alidondoka chini akilala ameachama.
Zilipita dakika tatu. Ghafla, Saud anaamka! Aliamka kana kwamba mzimu unafufuka kaburini. Macho yake yalikuwa ya kijani. Lips zake zilikuwa nyeusi kana kwamba kunguru. Aliachama mdomowe, mara wakatoka wadudu lukuki! Wadudu hawa walikuwa wote wa aina moja. Vilevile kama yule aliyemuingia mwanaume huyo hapo awali.
Saud alisimama akaangaza. Mara akaanza kuelekea kule alipoelekea mwenzake.
.
.
.
.
.
.
☆☆☆☆ LAKO JICHO ☆☆☆☆ USIKU HUU UMEKUWA MREFU, BADO HAKUJAKUCHA. NA UKIKUCHA KUMBUKA MALKIA ANAENDA KUTAFUTA MKUFU WAKE KWENYE HIMAYA YA GENGE LA WANYANG'ANYI. USIKOSE! ☆☆☆USIKOSE☆☆☆