*Sehemu ya 11*
Aliposhushwa kituo cha gerezani Isanga abiria wote waligundua kuwa harufu ile ilitokana na yeye, kwani waliona nguo zake zikiwa zimelowa mkojo.
“Hiloooo! Kubwa zima linajikojolea!” mpiga debe wa gari alimzomea.
Belinda aliumia sana moyo wake na kujikuta akilia machozi, hakupenda kuwa alivyokuwa ilikuwa ni bahati mbaya katika maisha, alikuwa ni mtoto wa tajiri kuliko mpiga debe aliyemzomea.
Alichechemea hadi gerezani ambako alijitambulisha kwa maaskari kama mke wa mfungwa Prosper, maaskari walimwambia siku hiyo ilikuwa si ya kuwaona wafungwa lakini alipowaeleza hali halisi iliyotokea na kwamba alikuwa akitokea hospitali maaskari walimwonea huruma na kumwingiza katika chumba alichokutana na Prosper mara kwa mara kabla ya kuugua na kulazwa hospitalini!
“Subiri tumwite!”
“Ahsante nasubiri!” Belinda alijibu.
Dakika chache baadaye Prosper aliingia chumbani akiongozana na mwanaume mwembamba mrefu aliyekuwa amemshika kiunoni, mtu huyo alionekana mgonjwa!
Alikohoa mfululizo na nywele zake zilikuwa nyepesi sana kichwani, alionekana ni kama mgonjwa wa Ukimwi, Belinda alipomwangalia vizuri mtu huyo alimtambua alikuwa ni Savimbi!
Belinda alishindwa kuelewa ni kwanini Savimbi alikuwa amekonda kiasi kile lakini hakutaka kuuliza, yeye na Prosper walikumbatiana na kusalimiana kwa furaha! Ulikuwa umepita muda mrefu sana bila kuonana.
“Huyu ndiye mtoto wako nimemleta umwone! Ila alitaka kunitoa roho, nashukuru Mungu leo niko hai!”
“Pole sana Belinda, ninajua unateseka sana kwa ajili yangu Mungu atakulipia!”
Waliongea mengi yaliyopita katikati yao, wakati Savimbi aliendelea kukohoa mfululizo na jasho jingi likimtoka! Hatimaye aliamua kutoka nje kwenda kupunga upepo.
“Kipenzi changu Pros, nipo nje napunga upepo mama!” Savimbi alisema na kunyanyuka kisha akampiga busu Prosper usoni na kutoka nje.
Belinda alipata uhakika wa kilichokuwa kikiendelea kati ya Prosper na Savimbi, alishindwa kujizuia na kuanza kulia mbele ya Prosper.
“Prosper tafadhali niambie ukweli nini kinaendelea kati yako na Savimbi nimejiuliza maswali mengi sana leo naomba unipe majibu!”
Prosper alimwangalia Belinda kwa macho ya huruma, alionekana mnyonge, alionekana kuwa na kitu moyoni alichotaka kukisema lakini alishindwa aanzie wapi.
“Tafadhali niambie Prosper vinginevyo mimi nakuacha narudi Dar es Salaam kwa baba yangu!”
“Usifanye hivyo Belinda!”
“Basi niambie!”
“Ninaweza kukuambia lakini tafadhali niahidi kitu kimoja!”
“Kitu gani?”
“Kwamba utanifichia siri na hutaniacha!”
“Itategemea Prosper! Lakini ni lazima unieleze vinginevyo naondoka nina wasiwasi kuna uhusiano mbaya kati yako na Savimbi kweli sio kweli?”
“Ni kw...eli Beli...nda! Nisa..mehe Beli..nda, Savi..mbi alinis..hawishi, alijifanya msamaria kwangu akawa ananipa chakula kizuri chenye mafuta, sukari nikafikiri ni mtu mwema lakini siku moja usiku niliamka na kukuta.....!”
Huku akilia machozi Prosper aliendelea kumsimulia Belinda kila kitu kilichotokea kati yake na Savimbi ndani ya gereza, lilikuwa jambo la aibu lakini alilazimika kuliweka wazi kwa sababu Belinda alitoka kufahamu.
“Ni kweli Belinda nisam...ehe mwenz’...angu, nisamehe mke wangu mtarajiwa, ni kweli Savimbi ananifanyia kitendo hiki! Alijifanya mweka kwangu tulipoingia gerezani akawa ananipa chakula kizuri, sukari, maji ya kunywa na kila nilipotaka kupigwa na wafungwa alinikingia kifua kwani mie ndiye nilikuwa mfungwa mdogo kuliko wote kwa wakati huo!
Kumbe alikuwa na nia mbaya ambayo mimi sikuifahamu tangu awali, hakuacha kunisifia eti nilikuwa na sura na umbile zuri, lakini mimi sikujali nilichukulia kitu cha kawaida kumbe alinitamani kimapenzi!”
“Halafu ikawaje?”Aliuliza Belinda kwa mshangao.
“SIku moja usiku nilizinduka usingizini na kumkuta akinipapasa mwili wangu, nilinyanyuka na kukaa huku nikimuuliza ni kitu gani alichotaka kufanya ndipo aliponieleza wazi kuwa alinitaka mapenzi mimi mwanaume mwenzake!”
Belinda alibubujikwa na machozi ya uchungu wakati akisikiliza maelezo ya Prosper jambo alilokuwa akilisikiliza haikuwa mara yake ya kwanza kulisikia alishalisikia kabla na alihisi lingekuwepo kati ya Prosper na Savimbi.
“Siku alipofanya hivyo ilikuwa ni usiku na wafungwa wote walikuwa usingizini, hakuna mtu aliyesikia kitu chochote, nilinyanyuka na kuanza kukimbia kwenda nje ambako Savimbi alinifuata na kuendelea kunishika ili aniingilie kwa nguvu.
“Aliweza?”Belinda hakuwa mvumilivu, alitaka kujua ni kitu gani kilitokea ingawa hakutaka kabisa mwisho wa habari hiyo uwe Prosper kufanya kitendo hicho.
“Hapana!”
“Afadhali, ulifanya kitu gani kujiokoa?”
“Nilichukua ubao mkubwa uliokuwepo na kumpiga nao usoni akaanguka chini na damu nyingi zikamtoka!”
“Kwa hiyo hakukufanya kitu?”
“Siku hiyo ndiyo!
Lakini asubuhi kulipokucha Savimbi alikuwa amenichukia sana hakusema na mimi kitu chochote na aliniambia kuwa ningekiona cha mtema kuni! Asubuhi hiyo sikupata chai aliyokuwa akinipa kila siku pia sikupata chakula wala maji!
Usiku ulipoingia nililala sakafuni kwani alininyang’anya godoro lake, hiyo haikutosha siku iliyofuata alitoa taarifa kwa mkuu wa gereza kuwa mimi nilimpiga kichwani na ubao baada ya kugoma kupasua kuni kitu ambacho hakikuwa kweli, kwa sababu yeye Savimbi alikuwa nyampara alisikilizwa zaidi na mkuu wa gereza kuliko mimi!
“Walikufanya nini baada ya hapo?”
“Nikaadhibiwa kwa kupigwa viboko ishirini na ni Savimbi huyohuyo aliyenichapa., niliumia sana!”Alisema Prosper kwa sauti ya upole.
“Pole sana Prosper sikujua kama ulipata mateso hayo yote sasa kwa nini hukuniambia?”
“Hukuwepo darling wakati huo wewe ulikuwa bado upo shule ulikuwa hujaja hapa Tabora!”
“Kiliendelea kitu gani baada ya hapo?”
“Gereza liligeuka Jehamanu kwangu!
Nilifanyishwa kazi ngumu, niliteswa kwa kunyimwa chakula na hata maji ya kunywa na katika muda wote wa mateso hayo Savimbi akawa anamhudumia kijana mwingine mwenye umri sawa na wangu ambaye aliingizwa gerezani muda mfupi baada ya mimi kukataa.
Kila mara Savimbi alinifuata na kuniambia kuwa nikitaka kuishi vizuri gerezani ilikuwa ni lazima tu nikubaliane na matakwa yake, bado nilikataa!”
“Hongera sana Prosper!”
“Ahsante lakini ngoja kwanza nimalizie kukusimulia kila kitu Darling!”
“Haya endelea?”
“Mwezi mmoja tu baadaye nilishangaa kuona savimbi akirejesha huduma zake kwangu tena! Nilishindwa kukataa kwa sababu ya shida na nikawa nakula chakula kizuri tena, akanipa godoro na kunipunguzia kazi gerezani, maisha yakawa mazuri, hakunieleza tena juu ya kufanya kitendo hicho lakini siku moja alinipa chai ya rangi jioni, baada ya kuinywa chai hiyo mwili ulilegea na nikapitiwa na usingizi na kumkuta Savimbi akinifanyia viba......!” Prosper alishindwa kumalizia sentensi yake na kuanza kulia, belinda nae alishindwa kuvumilia na kuanza kulia akiwa na mtoto wake mkononi!
“Nisamehe sana mke wangu! Nisamehe Belinda! Nililazimika kufanya hivyo kwa sababu ya shida, yalikuwa ni mateso makali mno!”Alisema prosper akiwa ameinamisha kichwa chini.
“Nini kilifuata?”
“Na baada ya hapo tuliendelea kufanya hivyo mara kwa mara, nisamehe belinda lakini pamoja na hayo yote bado nakupenda wewe pamoja na mtoto wangu na nitabadilika!”
“Prosper! Prosper! Ulishindwa nini kuvumilia mpenzi? Huwezi kuwa mwanaume wa kawaida tena!”Alisema Belinda huku akilia.
“Hapana Belinda nipo kawaida na ninakuahidi kubadilika na kama ikatokea nikatoka gerezani tuendelee na maisha yetu!”
“Prosper umeniumiza sana! Na kwa heri ya kuonana!”Alisema Belinda na kuanza kusimama wima alitembea hadi nje bila kugeuka nyuma, machozi yaliendelea kumbubujika na kulowanisha nguo zake, alikuwa ameumia kupita kiasi, hakutegemea kama mwanaume aliyempenda angeweza kutenda jambo hilo! Aliumia kiasi cha kuusahau hata ugonjwa uliokuwa ukimsumbua kwa muda mrefu!
*Je, nini kitaendelea?*