BASI LA SHETANI: Sehemu YA-28
Mtunzi: DEO MASSAWE
Ulikua usiku uliojaa mawazo katika kichwa cha Mainda,
“Mama kuna mtu anataka kuniingilia kimwili ili aweze kunipa msaada wa mimi na wewe kufika Dar es salam” Mainda alimwambia mama Winny lakini hakupewa jibu zaidi ya kumuona mama Winny akiinama na kulia kwa uchungu, alijiona mzigo kwa Mainda, manyunyu yaliyowanyeshea nje ya duka la wahindi yalilizidi kufanya hali ya ubaridi izidi kuwakamata, walijilaza sakafuni wakiwa wamekumbatiana,
“Potelea mbali, sitoi mwili wangu heri tufie hapa” alijisemea Mainda huku akilifuta wazo la kuenda kutoa rushwa ya ngono, alibaki akiombaomba hapo jijini Kampala kidogo alichopata alikitumia kumnunulia mama Winny dawa za kumkausha kidonda.
***
Licha ya msitu wa Amazon kuwa na wanyama wa kila aina pia kulikua na aina nyingi za miti, baadhi ya miti hizo kulikua na zenye uwezo wa kutengenezea dawa za kutibu magonjwa mbalimbali, pia kulikua na miti yenye sumu pamoja na miti ya maajabu, aina zote hizo za miti Mazengo alizijua, kwa mda alioshi msituni hapo aligundua dawa nyingi sana, siku baada ya siku alizidi kuzoeana na wanyama wakali, kitu kilichompa nafasi nzuri ya kukusanya mizizi ya dawa kwa ajili ya kuja kusaidia watu waliokua na magonjwa mbalimbali,
“Nataka nikasaidie watu wenye matatizo kama marehemu mke wangu,” Mazengo alijisemea huku akitokwa na machozi, kila alipomkumbuka mkewe aliinamisha kichwa chini na kumuombea kwani alimini kwa asilimia zote alikua marehemu.
***
Baada ya mwaka mmoja tangu Martin anze kutumikia kifungo gerezani, serikali ya Tanzania iliamua kufanya mabadiliko katika muundo wa mahakama, hivyo kila kitu kuhusiana na mahakama kikawa kimebadilishwa,
“Ah hapo sawa sahivi nitakua huru, mkuu wa magereza ni rafiki yangu,waziri wa mambo ya ndani ni rafiki yangu, mkuu wa jeshi la polisi Tanzania ni rafiki yangu, sasa mimi nitaishi gerezani kwa sababu gani?” Martin alijisemea pale alipopata taarifa juu ya mageuzi yaliyofanyika , asilimia kubwa ya watu waliopata nyadhifa za juu walikua marafiki zake wakubwa.
BAADA YA WIKI MOJA.
Tayari Martin aliachiwa huyu baada ya mkuu wamagereza kutembelea gereza la Segerea na kumuona rafiki yake,
“Lakini bwana Martin unatakiwa usafiri nje ya nchi, ukakae huko kwa kipindi chote ambacho ulitakiwa kukaa hapa gerezani”
“Hilo halina tatizo, nataka nikafanye kidogo mazoezi ya mwili, nataka kuenda kujifunza mbinu mbalimbli za kupigana , naskia Thailand ndio wako vizuri kuhusu hili” aliongea Martin na haraka alianza kupeleleza kuhusu waalimu wa Kung fuu, hapo ndipo alipata jina la VAJIRALONG kutoka BANGKOK, THAILAND, alifanya nae mawasilino kupitia Website (tovuti) walielewana na Vajiralong alikubali kumpa mafunzo . Safari ya kuelekea kisiwa cha Phayao iliandaliwa mara moja.
***
Wachina waliomuokoa Mazengo waliandaa sherehe kubwa ya kumuaga baada ya kuhitimu mafunzo, kila mmoja alikua tajiri kutokana na biashara walizobuni kutokana na mitaji ya kuuza madini, zawadi za kila aina zilinunuliwa magari zaidi ya mia moja yalinunuliwa kwa ajili ya mazengo, pamoja kiasi kikubwa cha pesa tofauti na ambazo aliwekewa katika account yake, Siku zilisogea taratibu Mazengo akiwa na Vajiralong,
“Kuna mwenzako anakuja kujifunza mafunzo kama ya kwako, anatarajia kuingia hapa kesho hivyo wakati kesho ukifanyiwa sherehe ya kuagana mimi nitakua napokea mwanafunzi mwingine, mimi nakubariki kwa mikono miwili, ukakae salama, umuamini Mungu ndiye anaweza kila kitu, usipigane bila sababu ya msingi, haya mafunzo niliyokupa ni yako ya kujilinda na sio kuanzisha vita au kuonea watu labda unaweza kumfundisha mtu wako wa karibu pia naamini katika msitu niliokupeleka kule Amazon umejifunza mambo mengi ikiwa ni pamoja na dawa za magonjwa mbali mbali, hapo ukizidisha ujuzi katika hayo madawa utapata hadi dawa za kutibu UKIMWI pamoja na dawa moja inayopatikana katika hiyo miti ya maajabu ambayo inaweza kurudisha umri wako nyuma au ukampa mtu yeyote na umri wake ukarudi nyuma lakini kama hujui hiyo dawa inaweza rudisha maisha ya watu watano pekee, sasa ni wewe utaangalia nani wa kumrudisha,” ulikua wosia wa Vajiralong kwa Mazengo.
***
Siku ya jumamosi asubuhi uwanja mkubwa ulio nje kidogo ya kisiwa cha Phayao kilitawaliwa na shamrashamra, matajiri wengi walifurika mahali pale, ulinzi uliiimariswa huku Mazengo akiwa ndiye mgeni rasmi wa sherehe hiyo, mda wote alionekana mwenye mawazo, kila alipofikiria jinsi maisha yake yanavyoelekea kuwa mazuri bila mkewe kuwepo aliona mali atakazopata hazina thamani, wala hatafurahia maisha yake. Saa nne kamili sherehe zilianza rasmi watu wengi walihutubia ikiwa ni pamoja na Mazengo kuonesha mafunzo aliyopata, wachina wote walifurahi kumuona mtu aliyewasababishia utajiri akiwa amepata mafunzo ya kutosha.
Kutokana na sababu zilizokua nje ya uwezo wa marubani ndege ambayo ilitakiwa kumfikisha Martin katika kisiwa cha Phayao ilichelewa hadi sherehe kuisha , hivyo wakati Mazego akiaga ndipo ndege iliyombeba Martin ilitua uwanjani hapo. Martin alipokelewa na Vajiralong huku kwa mbali Mazengo akiwa katika gari maalumu kwenye msafara wa kuelekeaa katika meli iliyokua imebeba zawadi zake, Meli hiyo ilikodiwa maalumu kuhakikisha Mazengo anafika nyumbani Tanzania.
***
GSG (Germany Security Group) kilikua kikundi maalumu kilichokua kinatoa huduma ya ulinzi nchini Tanzania huku makao makuu ya kikundi hicho yakiwa jiji Dar es salam nchini Tanzania, wajerumani hao walikua wakitoa huduma bora ya ulinzi, walikua na silaha za kutosha, mbwa wakali na wenye mafunzo ya hali ya juu, hakika kilikua kikundi namba moja cha ulinzi nchini Tanzania, kila kampuni au mtu binafsi aliyekodisha ulinzi kutoka katika kampuni hiyo alipewa mbwa mwenye mafunzo ya hali ya juu, pamoja na hayo makao makuu ya kikundi hicho ilikua nyumba ambayo Mainda aliachiwa na Edson.Siku moja katika hali ya kushangaza magaidi kutoka katika kikundi cha Al Queda waliweza kuvamia makao hayo makuu na kuiba silaha nyingi pia katika uvamizi huo waliweza kusababisha vifo vya walinzi kadhaa, pamoja na mbwa watano waliokua muhimu zaidi, kitendo hicho kiliwatia hasira wajerumani na kuamua kuagiza walinzi wenye mafunzo makubwa zaidi kutoka katika nchi za Urusi na Israel, ulinzi uliimarishwa katika jengo hilo, mbwa wakali na wenye mafunzo waliagizwa kutoka Marekani na China.
“Ilikua marufuku kwa mtu yeyote kuingia katika jengo hilo, matangazo yaliwekwa mtu kutosogelea nyumba hiyo kwa mita hamsini bila idhini.
***
Mazengo aliwasili nchini Tanzania baada ya wiki tatu, hakutaka kujulikana na watu moja kwa moja alienda hadi Kibaha huku magari yake pamoja na vitu vyote vikihifadhiwa katika ghala ya magari maeneo ya Posta, hakuona sababu ya kupoteza muda zaidi ya kuanza kutoa dawa kwa watu waliokua na matatizo mbalimbali,
“NABII ANAYEPONYA MAGONJWA MBALIMBALI AMETOKEA HUKO KIBAHA” zilikua habari zilizogonga vichwa vya habari kote duniani, Mazengo alitoa huduma pasipo malipo yoyote, mizizi aliyotoka nayo katika msitu wa Amazon ilichemshwa na kuwa dawa, watu walipeleka wagonjwa waliokua wamezidiwa na wote walipona, watu wengi kutoka kote duniani waliifuata tiba hiyo, foleni ilikua kubwa lakini hakuna hata mtu mmoja aliyejua kama ni mazengo kwani alivaa sura ya bandia, waandishi wa habari walipomfuata kumhoji alitishia kutokutoa dawa endapo atafuatiliwa,
“Mimi ni binadamu wa kawaida na nipo kuwasaidia binadamu wenzangu” lilikua jibu kutoka kwa Mazengo kila alipoulizwa na waandishi wa habari.
Pamoja na watu waliopata taarifa hiyo ya kuponywa magonjwa ni Mainda , alitamani sana kuona mama Winny akipata huduma hiyo, lakini kilichomsumbua ni juu ya kufika Tanzania kutokana na kuomba msaada pasipo kupewa.
Mainda akiwa anaendelea kuzurura katika jiji la Kampala alifanikiwa kupewa msaada wa dola mia, alilia kwa furaha, alimshukuru mama wa kizungu kwa kumpa kiasi hichgo cha pesa lakini yote hayo ilikua baada ya kuokota mkoba uliodondoshwa na mzungu huyo na kumrudishia ndipo alipopewa kiasi hicho cha pesa.
“Asante Mungu sahivi nitarudi nyumbani na moja kwa moja mama Winny ataenda kupata tiba” alijisemea Mainda kwa furaha huku akiuangalia ufunguo wa nyumba aliyachiwa na Edson.
“Asante Mungu kwa haya yote unayotenda juu ya maisha yangu, naomba unifikishe nyumbani salama na mama Winny akapone tuendelee na maisha kama zamani” alijisemea moyoni huku akijiandaa na safari.
Winny nae hakua nyuma pale alipopata taarifa ya nabii aliyetokea huko Kibaha, alifurahi kusikia kuwa anaponya hadi ukimwi, mara moja alipanga safari baada ya kuamaini atapona aliamua kuuza nyumba yake aliyojenga huko Mwika ili aweze kurudi jijini Dar es kuanza maisha mapya, hivyo haraka alifanya mawasiliano na madalali.
***
Kwa kutumia basi lililokua linafanya safari zake kutoka katika jiji la Kampala hadi Dar es salam lijulikanalo kama Kampala Express Mainda na mama Winny walikaa siti za nyuma huku wote wakiwa na matumaini ya kuanza maisha mapya, furaha ilizidi baada ya kuona wakiingia katika jiji la Dar es salam majira ya saa tano usiku katika kituo cha mabasi Ubungo,
Kwa kuwa mama Winny alipoondoka nyumbani alikua hajitambui basi hakujua kitu chochote kuhusu nyumba aliyokua anakaa kabla ya kusafiri kwenda Kampala.
“Mama hakuna haja ya kulala hapa kituoni maana nyumba ambayo tulikua tunakaa ipo karibu tu hapo tunaweza chukua hata usafiri wa bajaji”
“Sawa mwanangu kama kuna usalama na una uhakika na tunapoenda basi sawa twende mwanangu, Mungu atatusaidia “baada ya kusema hayo walikodi bajaji lakini dereva aliwapa sharti la kuwaacha katika chuo cha Ustawi wa jamii mita chache kutoka nyumba ilipokuwa.
Baada ya dakika kumi tayari walikua wameshashuka katika bajaji, walitembea taratibu, Mainda aliikumbuka njia iliyoelekea katika nyumba hiyo lakini alishangaa jinsi kulivyokua na utulivu wa hali ya juu,Mita hamsini za mraba kuzunguka nyumba hiyo hakukuwashwa taa yoyote hivyo giza lilitawala.
Mbwa kiongozi wa kikundi hicho cha walinzi alikua na mafunzo ya kukariri harufu za watu katika nyumba ile, katika harufu alizokua amekariri ni pamoja na ya mama Winny pamoja na Mainda na hiyo ilitokana na kule ndani kubaki na baadhi ya nguo walizokua wakivaa hivyo Mainda na mama Winny walifanikiwa kufika hadi katika lango la nyumba hiyo bila mbwa kubweka. Walinzi zaidi ya watano walikua ndani ya geti, walikaa tayari kwa hali yoyote ya hatari na kikubwa walitegemea mbwa kubweka kwa hali yoyote ya hatari.
“Mainda alitoa funguo wa mlango mdogo wa geti, akaweka mkoba chini na kuupenyeza katika tundu, mlango ulifunguka lakini kutokana na giza bado hakuona kitu chochote.
Walinzi walishtuka sana mlango kufunguka pasipo mbwa kubweka, hivyo moja kwa moja midomo ya bunduki ilielekezwa mlangoni, pengine walihisi labda mbwa wao wameshalishwa sumu,
“Ingia mama ngoja nichukue huu mkoba”, Mainda alimpisha mama Winny apite ili yeye abaki nyuma kwa ajili ya kuingiza mizigo, lakini katika hali ya kushtukiza Mainda alishtuka kusikia milio mitano ya risasi pale mlangoni, alichanganyikwa na kupiga kelele, alisikia kishindo cha mtu kuanguka chini na moja kwa moja alijua ni mama Winny, taa ziliwashwa haraka uvumilivu ulimshinda na kuamua kuingia ndani na geti, kwa macho yake aliuona mwili wa mama Winny ukiwa ardhini huku ukivuja damu,mama Winny alikua akirusha mikono kuomba msaada, lakini Mainda alipojaribu kuinama kwa ajili ya kumsaidia nayeye alipigwa risasi ya mkono iliyompelekea kupoteza fahamu..
the Legend☆