BASI LA SHETANI: SEHEMU YA-24
Saa nne kasoro dakika kumi, ukumbi wote ulitulia, ulikua wakati wa Martin kufunga sherehe kwa kutoa hotuba fupi,
“Ndugu zangu, natumai tumefurahia sherehe hii, naamini kila kitu kimeenda sawa na kama kuna mahali nilipokosea natumai wakati ujao nitarekebisha, wageni wangu kutoka Nigeria, na Zambia nawatakia safari njema mkakute kama mlivyoacha, lakini kabla ya kumalizia kabisa sherehe nataka niimalize kwa kuonesha roho ya kinyama mbele yenu, Mr James naomba aingizwe ndani” Martin aliongea hayo na mara moja msichana aliyefunikwa uso kwa kitambaa cheusi aliingizwa ndani, alikua akitetemeka kwa hofu, wanaume wawili wenye nguvu walimshika vizuri kiasi cha kutoweza kujigusa pale alipolazwa chali (KULALA KWA MGONGO) Martin alimtazama kwa makini kisha akaanza kuingiwa na mshangao, aligeuza uso na kumtizama James,
“Ni huyu ?”
“Ndio mkuu ni huyo, kwani huamini?”, james alijibu huku akiinama na kumfungua kitambaa kilichoufunika uso wake, Martin alichanganyikiwa na kuwafyetulia wale vijana risasi, ovyo, James alifanikiwa kutoka ukumbini na kupige kelele, watu pale ukumbini hawakuelewa kitu kilichosababisha Martin kuwa katika hali ile,
“ Hadi nyie wafanyakazi wangu mnaniletea mtu ambaye sijamuhitaji kwa sababu gani” Martin aliongea kwa hasira huku akitupa bunduki yake iliyoishiwa risasi,
“Je wewe ni nani ?” aliongea Martin huku akimsogelea mwanamke huyo aliyeletwa lakini kabla hajamfikia askari zaidi ya kumi waliingia na kumkamata Martin kwani kelele za James pamoja nna milio ya bunduki ziliwafanya askari wafike mapema,
“Chini ya ulinzi” ilikua sauti ya askari mmoja huku bunduki aina ya AK 47 ikimwelekea Martin, alinyoosha mikono juu pamoja na kupiga magoti, haraka alibebwa na kupakizwa ndani ya gari ya polisi pamoja na mwanamke aliyedhaniwa ni Winny,
miili ya waliouwawa ilipakiwa ndani ya gari lingine na kupelekwa hospitali ya Muhimbili kuchunguzwa na kuhifadhiwa.
“Hata kama nikifungwa gerezani lazima James nitakuuwa “, aliongea Martin gari likiwa linaondoka taratibu.
***
Baada ya Wiki tatu, kesi ya Martin ya kuuwa kwa kukusudia ilianza kusikilizwa katika mahakama ya kisutu akishtakiwa na Jamhuri, kwani hapakua na mtu yeyote aliyemshtaki Martin alitumia pesa kujaribu kuhonga lakini kulikua na vikwazo,
“We mzee sikia, mimi nakuhukumu miaka mitano lakini ukikaa mbili nakurudisha uraiani wewe ondoa shaka” yalikua maneno ya hakimu mkuu aliyetakiwa kutoa hukumu kwa Martin baada ya kupokea rushwa, Martin alikubali kufungwa miaka mitano lakini kabla ya kusafirishwa kwenda gereza la Segerea, aliomba kufanya kikao na baadhi ya wafanyabiashara waliokua wakisambaza dawa alizokua akiuza, kilikua kikao cha siri, ambapo alipata uhakika wa kutengeneza pesa akiwa bado gerezani .
“Bsi ndio kama hivyo vijana wangu, pigeni kazi kwa bidii nikitoka nawapa bonasi, nawaachia huyu Adeleka, kila kitu atakisimamia” alimaliza kwa kumkabidhi madaraka raia wa Nigeria aliyeitwa Adeleka, alimpa kazi ya kusafiri kila nchi ili kutafuta masoko, na baada ya hapo alipelekwa rasmi kutumikia kifungo huku kichwani kwake akimuweka James pamoja na Winny kiporo.
***
BAADA YA MWAKA MMOJA.
Hali ya mama Winny ilizidi kuwa mbaya , Mainda alichanganywa na mambo mawili,cha kwanza ni kuhusu hali ya ugonjwa uliomkabili mama Winny na kingine ni kuhusu kijana aliyewapa sehemu ya kuishi kwani ilikua imetimia mwaka mmoja tangu aondoke bila kurejea
“Kwani ina maana kasahau hapa au vipi, alisema atarudi lakini hadi sasa bado” Mainda aliwaza hilo mara kwa mara na hakupata majibu kuhusu Edson, kila siku alilala akijua atakuja kesho lakini hakutokea, kila siku aliendelea kulima mazao mbalimbali ndani ya geti, na mara nyingi alikua pembeni ya kitanda cha mama Winny akisali, harufu kali kutoka ka mama Winny ilizoeleka, hakuna hata mgeni mmoja aliyeingia ndani ya nyumba ile na hakuna mtu aliyejua ni watu wa aina gani wanaoishi humo.
Siku moja aliamua kuvunja chumba ambacho Edson aliingiza mabox, alitumia nyundo kuvunja kitasa, hakuamini macho yake, pesa nyingi zilizo ndani ya mabox yale zilimfanya afurahi kupita kiasi aliruka ruka kwa furaha lakini ghafla alitulia na kujiuliza swali,
“Hivi nafurahi kwani ni zangu?” alijiuliza swali hilo na kuanza kuzihesabu taratibu.
***
Winny alipata wakati mgumu sana kufanya kazi ya upishi kadri siku zilivyokua zinasonga alizidi kupata ujuzi lakini baada ya mezi sita tangu aanze kazi ile alianza kuumwa mara kwa mara, mwili wake ulikua ukichoka sana, huku mafua yasiyopona yakimuandama, alipoona hali hiyo alilazimika kuenda hospital ya Mwika Health Centre, hapo ndipo maisha yake yalibadilika ghafla baada ya kupokea majibu ya kuwa na virusi vya UKIMWI, alikiona kifo kikiwa mbele yake, mwili wake uliporomoka kwa kasi, hakupata hamu ya kula tena, alizitumia pesa zake kununua eneo na kujenga nyumba yake karibu na shule ya sekondari hapo mwika,
“Mungu kwa nini umeyaruhusu haya yatokee?’ Winny alikua akijisemea mara kwa mara.
***
Ilimchukua siku thelathini Mainda kukamilisha zoezi la kuhesabu pesa zile, lakini hakujua afanye nini, nafsi ilimsuta kuzitumia kwa kuwa hakujua aliyeziweka hapo alikua na malengo gani,
“Hivi mtu amenipa hifadhi alafu nije kutumia na pesa zilizo ndani kwake ?” haiwezekani hapa inabidi nikatangaze kanisani ili atafutwe na kama hayupo duniani basi tuzitumie” alijisemea Mainda huku akiikumbuka ndoto aliyoota siku moja kabla ya Edson kuondoka.
Baada ya siku tatu alisikia tangazo la mkutano wa injili, ulikua mkutano ambao ungedumu kwa siku tatu mfululizo,
“Hawa hawa wachungaji naenda kuwaomba ushauri wa nini cha kufanya na hizi pesa pia njia za kumpata Edson” alijisemea Mainda, japo ilikua vigumu kumuamini mchungaji yeyote kutokana na kitendo alichofanyiwa na mchungaji Paschal mwaka mmoja uliopita alijitahidi kuondoa imani mbaya juu ya wachungaji,
“Huyu hataweza kunifanyia vile vitu” alijisemea Mainda huku akielekea katika mkutano huo uliokua ukifanyika katika kiwanja kidogo cha chuo cha ustawi wa jamii.
Hakika mchungaji alitoa mahubiri mazuri, kila aliyesikiliza alirejewa na matumaini aliyokwisha poteza, pia kulikua na wachungaji wawili kutoka Nigeria,
“Mkutano utaendelea tena kesho, tukutane katika viwanja hivi hivi,mimi mchungaji Christian” yalikua maneno aliyofunga nayo mkutano na mara moja Mainda alianza kupenya katikati ya watu ili aweze kuomba kuonana na mchungaji huyo akiamini kuwa ndiye atakayemsaidia na kumshauri kuhusu pesa zilizoachwa na mtu aliyeondoka na kutorudi kwa mda mrefu.
***
Mazengo alikua imara zaidi ya simba, mwalimu wake aliona kuwa Mazengo hawezi kupigwa na mtu yeyote duniani, hivyo alitoa taarifa kwa wachina waliompeleka, baada ya majadiliano na ili wachina kweli waamini kuwa mazengo amekua imara, ilimpasa afanyiwe mtihani, ulikua mtihani mgumu sana, alipaswa kusafiri hadi katikati ya msitu wa Amazon, aweze kuishi huko kwa miezi sita, bila silaha yoyote,
“Wewe kule nenda silaha utazikuta huko huko maana kuna watu wanaenda huko na silaha na wanakufa na kuziacha huko hivyo wewe nenda utakuta silaha zote huko”, yalikua maneno kutoka kwa mwalimu wake na bila ubishi haraka safari ilipangwa, alipanda ndege ya wachina hadi anga ya Brazil ambapo ni mojawapo ya nchi zilizopakana na msitu huo mnene na hatari kuliko msitu wowote duniani , wakiwa anga ya msitu Mazengo alikabidhiwa parachuti pekee, kisha akafunguyliwa mlango maalumu wa kurukia, hakuwa na hofu hata kidogo, ingawa aliamini msituni hapo kuna wanyama wakali na nyoka wa kila aina lakini aliamini ataushinda mtihani huo.
“All the best maaaaaaaaaaaaan, (Kila la heri mbaba)” lilikua neno la rubani wakati Mazengo akiwa anajirusha, aliteremka taratibu akisaidiwa na upepo, kwa mbali alishuhudia nyoka wakubwa wakitambaa msituni hapo.
“Mungu uwe na mimi, katika hii safari” alijisemea Mazengo huku hasira ikiwa ni kwa aliyeangamiza familia yake.
***
“Mainda na mchungaji Christian waliongea mengi, Mainda alimueleza kila kitu hadi kiasi cha pesa alichokua nacho,
“Unatania au ni kweli binti” mchungaji aliuliza kwa mshangao, hakika hakuamini kama kuna mtu anayeweza kuweka hela kiasi kile ndani kisha aondoke na akae zaidi ya mwaka mmoja bila kurudi nyumbani.
Binti naomba kaa nalo na iwe siri yako, hakika wewe ni binadamu wa kipekee sana kama angekua mtu mwingine asingetoa taarifa kama hii, sasa wewe cha kufanya ni kuitunza siri hii, yaani usimwambie mtu yeyote, hadi huu mkutano ukiisha basi tutapanga namna ya kumpata mwenye mali zake na najua hawezi kukuacha hivyo lazima atakutibia huyo mgonjwa wako hadi apone, nakusihi nenda kapumzike hadi kesho uje tena hapa”, mchungaji Christian aliongea huku akiwa haamini vitu alivyosikia kutoka kwa Mainda, baada ya hapo Mainda alimuelekeza mchungaji sehemu anayoishi.
“Jasiri haachi asili”lilikua neno la kwanza kutoka kwa mchungaji baada ya Mainda kuondoka,
“Kweli ni mimi Christian nimepata hii taarifa ??” alijiuliza Christian na kutabasamu,
***
Christian kabla ya kuokoaka na kufungua kanisa alikua jambazi mkubwa, ambaye alianza kufanya matukio ya wizi tangu akiwa shule ya msingi, kitu kilichopelekekea kutosoma sekondari, alijiunga na magenge ya wizi katika mitaa ya Ungalimited Arusha, alifanya matukio makubwa sana ya wizi wa kutumia silaha, alikua anauwa watu bila huruma, baadaye akahamia Dar es salam ambapo siku moja walifanya tukio la wizi katika Hotel ya Serena kwa bahati mbaya wenzake watano waliuwawa akapona peke yake, hapo alimua kuokoka lakini sio kwa ajili ya kuhubiri neno la Mungu bali ni kuiba kwa neno la Mungu, hapo alilazimika kusafiri hadi nchini Nigeria na kupewa mafunzo ya uchungaji, hapo kila mtu alitokea kumuamini, lakini kiuhalisia alijikusanyia sadaka kwa lengo la kunufaika yeye mwenyewe.
Hivyo siku aliyopewa taarifa kutoka kwa Mainda alikumbuka mambo yake ya zamani na moja kwa moja alitoa simu yake na kumpigia mmojawapo ea viongozi wa magenge ya ujambazi aliyeitwa Fork,
“Fork fanya tuonene leo leo kwa haraka,
“Mzee nipo Tarakea katika mpaka wa Tanzania na Kenya kuna mission tunaenda kufanya Nairobi” alijibu Fork
“Wewe nakuambia geuza msafara wako, usiku huu huu mfike Dar es salam kuna donge nono liko mahali” mchungaji Christian aliongea na mara moja safari ya Fork na kundi lake iligeuka.
INAENDELEA...
the Legend☆