Kujua matatizo ya wananchi kwa ukaribu ni msingi wa utatuzi wa kweli. Ni muhimu kwa viongozi kuwa karibu na waathirika moja kwa moja badala ya kutegemea tu ripoti kutoka kwa viongozi wa chini. Mara nyingi ripoti hizi huwa zimepunguzwa au kuhaririwa kwa nia ya kulinda maslahi ya viongozi hao wa chini, kundi kubwa zaidi hata hawafuatilii wala kujishughulisha (wavivu) wanasubiri mishahara wanatunga chochote, hivyo kuficha hali halisi ya matatizo yanayowakumba wananchi.
Katika mazingira haya, napenda kukiri kuwa Dkt. Dorothy Gwajima ni miongoni mwa viongozi wachache wanaojitahidi kuwasiliana moja kwa moja na wananchi ili kuelewa changamoto zao kwa undani. Anaonekana kuwa na dhamira ya dhati ya kufuatilia matatizo ya kijamii kutoka kwenye vyanzo vya moja kwa moja. Silaha yake kubwa imekuwa matumizi ya majukwaa ya mitandao ya kijamii, jambo ambalo linadhihirisha kuwa anaendana na wakati na ana nia ya kweli ya kusikiliza wananchi.
Kwa mfano, katika jukwaa la JamiiForums, mara kadhaa nimeona Dkt. Gwajima akianzisha mijadala, akichangia, na kureply maoni mengi ya wananchi. Hili si jambo rahisi kwa kiongozi wa ngazi yake, lakini linaonyesha jinsi anavyothamini maoni ya watu wa kawaida. Pia katika mitandao mingine kama Facebook, anaendelea kuwa na uwepo wa dhati, si tu kwa kutoa taarifa, bali pia kwa kujibu maswali na kutoa mrejesho wa moja kwa moja kwa wananchi.
Uwajibikaji wake unazidi mamlaka aliyopewa, jambo linalomtofautisha sana na viongozi wengi ambao wanajulikana zaidi kwa vyeo vyao kuliko kwa kazi wanazozifanya. Dkt. Gwajima ameonyesha kuwa cheo si pambo, bali ni nafasi ya kuwatumikia wananchi kwa uwazi, uwajibikaji na moyo wa dhati.