SoC03 Sheria za Vyombo vya Habari, Madhumuni na Athari zake katika Uwajibikaji na Uhuru wa Vyombo vya Habari Nchini Tanzania

Stories of Change - 2023 Competition
Nov 15, 2019
35
113
Utangulizi

Habari
ni taarifa au maelezo kuhusu tukio, jambo au matukio mbalimbali yanayotokea katika jamii, taifa, au dunia kwa ujumla. Halikadhalika, vyombo vya habari ni njia au nyenzo mbalimbali ambazo hutumiwa kuwasilisha habari kwa umma, kama vile Magazeti, Runinga, Redio na nyinginezo. Habari hizo huweza kuelimisha, kuburudisha na pengine kuhamasisha jamii juu ya masuala mbalimbali yanayojiri katika jamii.

Sheria za Vyombo vya Habari ni kanuni, sera na taratibu zinazotungwa na mamlaka za nchi (bunge) ili kuweza kuratibu mienendo, usimamizi, na utendajikazi wa Tasnia ya habari nchini.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 chini ya Ibara ya 18 imetoa uhuru na haki ya kila mtu kutoa maoni yake, ikiwa ni pamoja na haki ya kupata taarifa popote pale alipo ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. Hivyo basi, katiba hii na chini ya ibara hii ndipo msingi wa habari ulipoanzia kuwezesha sheria za habari kutungwa kama ilivyo wajibu wa bunge kufanya hivyo chini ya ibara ya 97(1) na 98 ya katiba hii.

Baadhi ya Sheria za Vyombo vya Habari, Madhumuni na Athari zake katika Uwajibikaji na Uhuru wa Vyombo vya Habari Nchini Tanzania

1. Sheria ya Huduma za Habari, 2016

Pamoja na majukumu mengine sheria hii inasimamia weledi katika tasnia ya habari, na inaunda Bodi ya Ithibati ya Habari, sambamba na Baraza Huru la Habari.

Katika sheria hii shida ipo katika kifungu cha 9 ambacho kimeeleza kuwa Mkurugenzi wa Habari (Maelezo) anaweza kufungia chombo cha habari pale anapodhani kuwa chombo husika kimekiuka sheria pamoja na kanuni zilizopo. Hapa shida siyo kanuni shida ni sababu zipi za kufunga na zimeainishwa wapi katika sheria?

Inawezekana kiongozi mwenye mamlaka ana kashfa ambayo umma wanapaswa kuifahamu, nisiitangaze hadharani eti kisa tu naogopa nitafungiwa huduma? Au pengine Serikali ina kashfa ya upotevu wa pesa ya umma kwa mfano kama ilivyo kwenye Taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali, nisitangaze tu kwa
kuogopa kufungiwa? Hapa ningependekeza sheria nyingine rafiki itungwe ambayo pamoja na mambo mengine itaainisha makosa ya msingi na siyo kuyafumbafumba katika kivuli cha “ Kanuni zilizopo”.

Pia, chini ya kifungu cha 10 cha sheria hii imetolewa haki ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa kufungiwa huduma kwa waziri mwenye dhamana ndani ya siku 30. Itoshe kusema kuwa hiki kifungu nacho ni dhaifu kwasababu kinachohitajika hapa ni mipaka yenye nidhamu ya kiutendaji kati ya mamlaka dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari na wamiliki wake. Hii itatujenga upya.

2. Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa, 2016
Katika sheria hii licha ya kuwa lengo na makusudi yake ni kuhakikisha raia wanapata taarifa, lakini kitu cha ajabu ni kuwa sheria hii imekaa kibaguzi. Chini ya kifungu cha 5(1) na (4) sheria hii inaminya haki ya kupata taarifa kwa kuruhusu raia pekee kupata taarifa. Kwa maana hiyo sasa mtu ambaye siyo raia wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania hana haki ya kupata taarifa.

Itoshe kusema kuwa sheria hii ni ya kibaguzi na pia inaenda kinyume na ibara ya 18(2) ya katiba ya nchi, lakini vile vile sheria hii inakinzana na Mkataba wa Haki za Binadamu na Haki za Watu wa Umoja wa Afrika, 1981 ambao Tanzania iliuridhia. Katika mkataba huo chini ya Ibara ya 9(1) imeelekeza wazi kuwa, nanukuu “Kila mtu atakuwa na haki ya kupokea taarifa”mwisho wa kunukuu. Hiki kitendo cha kuwajali raia wetu na kuwanyanyapaa raia wan je ni hatari siyo tu katika tasnia ya habari pia katika masuala mazima ya kiplomasia na kuitangaza nchi yetu.

Serikali yetu inapaswa kujifunza kwa mataifa mengine yalioyoendelea katika uga wa upashanaji taarifa ili kupitia kwao iweze kuona ni wapi panahitaji mabadiliko katika sheria zetu.

Kwa mfano, nchi kama Sweeden, Norway na New Zealand sheria za kupata taarifa zinampa nguvu msimamizi maalumu ambaye ni Afisa aliyeteuliwa na serikali kwa mujibu wa sheria zao, haki ya kusimamia utekelezaji wa sheria ikiwa ni pamoja na kuchunguza malalamiko yanayoyokuwa yakiletwa kwake kutoka kwa wananchi, serikali pamoja na watu wa vyombo vya habari. Hili limewafanikishia mengi na hadi sasa wana mawanda mapana ya upashanaji habari ulimwenguni.

Sambamba na hilo, serikali inapaswa kuvilea vyombo vya habari vilivyopo hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuvipatia sheria bora zitakazochochea ukuaji wa tasnia ya habari hapa nchi huku ikihakikisha taarifa za vyombo vya habari vya ndani vinapanua wigo wake hadi nje ya mipaka ya nchi hii. Tunapaswa kujifunza kwa mataifa ya jirani kwa mfano Kenya ambapo wao wamejitahidi kupanua wigo wa vyombo vyao vya habari kama vile vituo vya Runinga (CITIZEN na The East Africa ) , ambapo Afrika ya Kusini wao wamepanua wigo wa kituo chao cha Runinga kiitwacho SABC.

3. Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta, 2010
Sheria hii pamoja na mambo mengine inahusu udhibiti wa watoa huduma za mawasiliano ya kielektroniki na posta, usajili wa namba (laini) za simu, utoaji wa vibali kwa shughuli za mawasiliano pamoja na kushughulikia makosa yatokanayo na mawasiliano na posta.

Katika sheria hii binafsi shida nimeweza kuibaini chini ya kifungu cha 163 ambapo Maafisa wa polisi au wafanyakazi walioruhusiwa na Mamlaka ya mawasiliano wanaweza kuingia, kukagua, na kutwaa vifaa vya mawasiliano kutoka jengo au mahali popote pindi kutakapokuwa na sababu za msingi za kuamini kwamba sheria hii au kanuni zake zimekiukwa. Madhara ya hiki kifungu katika uwajibikaji wa vyombo vya habari ni kwamba, baada ya kuwa upekuzi umefanyika na nyaraka kuchukuliwa bila hata kuwepo kwa hati ya upekuzi siyo tu kutawadhoofisha waandaaji na wakusanyaji wa habari, vilevile hata vyanzo vya taarifa vitakosa imani na vyombo vya habari na havitoweza kuwapatia taarifa tena kwa kuhofia na kulinda faragha za taarifa zao.

Hitimisho
Serikali haina budi kuyatafakari yote niliyoyaandika katika andiko hili na kuhakikisha mamlaka husika zinayafanyia kazi na hatimaye kurejesha thamani ya Tasnia ya Habari nchini Tanzania.Uwajibikaji bora katika tasnia ya habari utategemea sana usawa wa sheria zilizopo na hapo ndipo tutaitangaza nchi yetu bila kusita. Tunatamani tuwe na akina SALIM KIKEKE wengi ambao wataipeperusha bendera ya nchi yetu huko nje. Kwa pamoja tutaijenga nchi yetu.​
 
Back
Top Bottom