Yaani huku nako kuna arosto tena? Hongera madam S. Ingawa sijajua hatima ya Gabriel na watawa!
NYEMO CHILONGANI
SHAMBULIO LA DAMU
0718069269
Sehemu ya Kumi na Tano.
Scott na maofisa wengine wa CIA walikuwa wakifuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea, kwa Kennedy, mwanaume huyo alionekana kuwa muhimu kupita kawaida. Ilikuwa ni lazima wahakikishe kwamba anaingia nchini Marekani salana kabisa.
Muda ulizidi kwenda, siku ambayo waliwasiliana naye na kumwambia kwamba alikuwa njiani kwenda huko ndipo wakagundua kwamba kulikuwa na simu ambayo alipigiwa Kennedy kutoka nchini Uingereza. Hawakujua walizungumza nini lakini baada ya kuifuatilia sana kwagundua kwamba ilitoka katika Shirika la Kijasusi la MI6.
Mpaka kufikia hapo wakajua kabisa kulikuwa na mchezo. Kitu cha kwanza kabisa ambacho walijiuliza ni namna ambavyo MI6 walipata namba ya simu ya Kennedy, kwenye hilo hawakutaka kujiuliza sana kwani tayari waligundua kwamba Backnon alikuwa akifanya mawasiliano na watu hao hivyo kulikuwa na uhakika kwamba yeye ndiye aliyewapa watu hao namba hiyo.
Scott akaagiza watu hao wafuatiliwe kwani tayari alihisi kulikuwa na jambo kubwa ambalo lilitakiwa kutokea mahali hapo ambalo yeye kama yeye hakutaka kabisa kuona likitokea kwa sababu Kennedy alikuwa na karatasi ambazo zilikuwa muhimu mno.
Baada ya dakika kadhaa akaona akipigiwa simu na Kennedy na mwanaume huyo kuuliza kuhusu familia yake, alihitaji kujua kama ilikuwa salama au la. Hapo akapata kitu kwamba inawezekana kabisa kulikuwa na jambo kubwa lililokuwa likiendelea nyuma ya pazia.
Akawaagiza maofisa waende nyumbani kwake kuiangalia familia hiyo na walipofika huko, kitu ambacho waligundua ni kwamba familia hiyo haikuwepo. Wakampigia simu Scott na kumwambia kile kilichotokea, mwanaume huyo alichanganyikiwa, akahisi labda inawezekana mke wa Kennedy alimchukua mtoto wake na kuelekea kazini, akatuma watu huko, jibu walilolipata ni kwamba mwanamke huyo aliondoka muda mrefu sana.
Hilo likawachanganya kupita kawaida, hapo wakapata jibu kwamba inawezekana kabisa familia ya Kenney ilikuwa kwenye matatizo na ndiyo maana kitu cha kwanza kabisa ambacho mwanaume huyo alihitaji kufahamu ni kuhusu familia yake.
Hapo wakapata jibu kwamba inawezekana kabisa familia ya Kennedy ilitekwa na Waingereza na kumwambia kwamba alitakiwa kuhakikisha anapeleka karatasi hizo nchini humo. Ili kumuaminisha kwamba familia yake haikuwa imetekwa, Scott akazungumza naye na kumwambia kwamba hakukuwa na tatizo lolote lile, familia yake ilikuwa salama kabisa.
Alijua kulikuwa na kosa kumwambia hivyo lakini hakuwa na jinsi, karatasi zile alizokuwanazo zilikuwa muhimu kwao kuliko kitu chochote kile. Wakati akiwa amemwambia hivyo, aliwaambia maofisa wake wahakikishe familia ya Kennedy inapatikana haraka iwezekanavyo kwani bila hivyo kusingekuwa na uhakika wa kuzipata karatasi hizo.
Maofisa hao wakaondoka kwa lengo la kufanya kazi hiyo lakini pia alimtumia ujumbe Kennedy kwamba alitakiwa kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha anamuua Backnon kwani tayari alionekana kuwa adui wao ambaye hakutakiwa kuishi kabisa.
Kennedy aliwaambia ugumu wa kufanya hivyo ila walitakiwa kumtumia mtu mwingine kabisa kwa ajili ya kufanya kazi hiyo. Kwa Scott hakukuwa na tatizo, Wamarekani walijipanga, kwenye kila ndege ambayo ilikuwa ikikanyaga ardhi ya Marekani ilikuwa na mhudumu ambaye aliwekwa na CIA, hiyo ilitokana na shambulio la kigaidi ambalo lilitokea Septemba 11/2001.
Kennedy akawaambia kabisa kwamba kwa mazingira yaliyokuwepo ndani ya ndege lingekuwa suala gumu kufanya hivyo, walitakiwa kumtuma mtu ambaye alikuwa ndani ya ndege hiyo kama mhudumu kwa ajili ya kumuua mwanaume huyo.
Wakati akiwasiliana na Scott, Backnon alijifanya amelala lakini muda mwingi alikuwa akimfuatilia Kennedy kwa kujaribu kuangalia simu yake lakini alishindwa kabisa kuyaona mazungumzo yao. Alijua kabisa kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea na ilikuwa ni lazima afanye kitu chochote kile, wakitua Marekani tu akimbie zake na kutokomea kusipojulikana.
Huo ndiyo ulikuwa mpango wake lakini kwa upande wa Kennedy, tayari alikuwa na wasiwasi kwamba familia yake haikuwa salama kama alivyokuwa ameambiwa. Alihisi kabisa kulikuwa na tatizo mahali fulani na bosi wake, Scott hakutaka kumwambia ukweli.
Kilichomjia kichwani mwake ni kuondoka na kuelekea nchini Uingereza kama tu angegundua kwamba familia yake haikuwa salama kama alivyokuwa ameambiwa. Haraka sana akakata tiketi kwenye mtandao wakati ndege ikiwa imetulia angani ikiendelea na safari zake, katika anga ambayo waliruhusiwa kutumia huduma ya internet ndani ya ndege hiyo.
Akapata tiketi ya ndege ambayo ilikuwa ikiondoka ndani ya dakika saa moja na nusu baada ya ndege hiyo kutua nchini Marekani. Akawa nayo kwenye barua pepe yake na kitu pekee alichokuwa akikisikilizia ni kwa ndege hiyo kutua nchini Marekani na kuondoka zake kurudi nchini Uingereza.
Baada ya nusu saa, mhudumu mmoja wa kike akawasogelea pale walipokuwa huku akiwa na vinywaji kwenye chombo chake na kumuuliza Kennedy alikuwa akitumia kinywaji gani. Akasema hatumii chochote kile, akamuuliza Backnon ambaye alikuwa wa kwanza kabisa kwenye kiti kile cha watu wawili na yeye kusema kwamba hatumii chochote.
“Sawa,” alisema msichana huyo na kuanza kuondoka, alipoona amesimama pembeni ya Backnon kwa nyuma, akachukua sindano aliyokuwa nayo na kwa haraka sana kumchoma mwanaume huyo shingoni kwa nyuma.
Backnon akashindwa hata kupiga kelele, alishtuka tu na hapohapo usingizi mzito kumpata. Kennedy hakushtuka, alijua kilichokuwa kikiendelea, hivyo akatulia lakini akiwa makini kabisa kuhakikisha kwamba mchezo kama ule hauchezwi kwake hata kidogo.
Ndege iliendelea na safari, aliona kabisa kwamba kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea kuhusu familia yake hivyo ilikuwa ni lazima afanye kila liwezekanalo kuhakikisha anaiokoa familia hiyo popote pale ilipokuwa.
Wakati safari hiyo ikiendelea ndipo akakumbuka kwamba ni lazima afanye kitu kimoja kwa ajili ya kuondoka salama katika ndege hiyo kwani kwa jinsi hali ilivyokuwa, alihisi kabisa uwanja wa ndege kungekuwa na maofisa wa CIA ambao walikuwa wakimsubiri, wamchukue na kuelekea naye ofisini kwa ajili ya kuwakabidhi karatasi zilizokuwa na formula hiyo.
“Ni lazima nifanye kitu,” alisema Kennedy.
Hicho ndicho alichokifikiria, hakutaka kuona akishikiliwa na kupelekwa makao makuu na kukabidhi formula ile na wakati hakujua kuhusu familia yake.
Haraka sana akafungua begi lake dogo na kuchukua koti kubwa na kulivaa ambalo lilikwenda mpaka karibu na magoti yake, akaondoka na kuelekea chooni, huko ilikuwa ni lazima apange mipango mipya kuhakikisha hakuna mtu anayemshtukia kwa lolote lile. Kule chooni, akaufungua mlango kidogo na kuangalia upande mwingine, aliuona mlango ambao uliandikwa ‘Staff’ akajua tu humo kulikuwa na nini.
Akatoka chooni huku akiangalia huku na kule, akaufungua mlango huo na kuangalia ndani. Akakutana na nguo nyingi za wahudumu pamoja na za marubani. Kwa pembeni kabisa kulikuwa na sehemu ambayo ilitengwa kwa ajili ya mizigo ya abiria.
Haraka sana akaanza kuzifuata nguo za marubani, alipokaribia mahali zilipo, akamuona msichana mmoja akiendelea kupanga nguo nyingine, kwa kuwa hakuwa ameonekana na msichana yule alimpa mgongo, akamsogelea, alipomfikia, akamkaba kwa nyuma, si kwa lengo la kumuua bali kumzimisha kwa muda.
Ni ndani ya sekunde chache tu msichana huyo akatulia na kumuweka chini. Akachukua vazi moja la rubani, akalivaa, kwa juu akavaa na koti lake kama kulificha na kisha kutoka ndani ya chumba kile huku akiwa ameishika kofia yake kwa kificho.
Alifanikiwa, hakuonekana, alitulia kwenye kiti na wakati huo ndege iliondoka nchini Canada na kuelekea Marekani baada ya kumaliza kuvuka katika Bahari ya Atlantiki.
Baada ya nusu saa, wakaambiwa wafunge mikanda, haraka sana akafanya hivyo na ndege kuanza kutua. Iliposimama, abiria wakaanza kuteremka, hakutaka kuwa na presha, akatoka na kurudi chooni, humo alisubiri kwa dakika kadhaa, alipohakikisha kwamba abiria wote wametoka, akavua koti lake, akabaki na mavazi ya rubani, akavaa kofia na kuanza kuteremka.
Kwa kumwangalia ilikuwa ni vigumu kugundua kama hakuwa rubani, alifanana vya kutosha, alikuwa akitembea kwa mwendo wa kawaida na kwenda kwenye mlango maalumu na kupita.
Maofisa kadhaa wa CIA walikuwa hapo, walimwangalia kila abiria aliyekuwa akiteremka, ilikuwa ni lazima wamchukue Kennedy na kuondoka naye mahali hapo lakini kitu cha ajabu kabisa mpaka abiria wanamalizika, mwanaume huyo hakuonekana.
“Vipi?” aliuliza Scott kwenye simu, alikuwa akimuuliza Kennedy.
“Hayupo!”
“Hayupo? Unamaanisha nini kusema hayupo?” aliuliza huku akiwa amechanganyikiwa.
“Yaani hatujamuona!”
“Hamjamuona? Kivipi?”
Kila swali alilouliza na kupewa jibu, aliibuka na swali jingine. Kile alichoambiwa hakukiamini kabisa, alichojua ni kwamba Kennedy alitoka Dubai akiwa amepanda ndege hiyo baada ya kubadilishwa, sasa ilikuwaje mwanaume huyo asiwepo.
Akahitaji kupata taarifa kutoka ndani ya ndege. Akaambiwa kwamba kulikuwa na tatizo, kuna mwanaume ambaye alichukuliwa na kukabidhiwa kwao, alikuwa Backnon lakini pia kulikuwa na jingine.
“Lipi?”
“Kuna mtu alivamia kwenye chumba cha nguo na kumzimisha mhudumu kwa muda,” alisema mwanaume huyo.
“Huyo ni Kennedy,” alisema Scott huku akishusha pumzi ndefu.
Wakafuatilia na kugundua kwamba kulikuwa na nguo za rubani zilikosekana humo, ilipotea katika mazingira ya kutatanisha lakini wakajua kabisa kwamba ni Kennedy ndiye ambaye alihusika kuzichukua nguo hizo.
Wakaondoka hapo na kuelekea katika chumba kimoja kwa lengo la kuangalia kwenye kamera ndogo za CCTV ili kuona kilichotokea. Huko, wakamuona Kennedy akitoka kwa kupitia mlango wa marubani, hakuonekana kuwa na hofu, alijiamini na alitembea kwa kujiamini kana kwamba alikuwa rubani kweli.
Mpaka kufikia hapo wakakubaliana kwamba walimkosa hivyo ilikuwa ni lazima wafanye kila liwezekanalo kuhakikisha anapatikana kwa sababu mtu huyo alikuwa muhimu mno.
Tayari maofisa wengine wa CIA walikuwa nyumbani kwake, waliizunguka kwa mbali kiasi kwamba ilikuwa ni vigumu kuonekana. Walikuwa wakimsubiria Kennedy ambaye waliamini ni lazima afike humo kwa lengo la kuangalia kama kulikuwa na familia yake ndani ya nyumba.
“Tuvamie?” aliuliza mwanaume mmoja.
“Hapana! Subirini mpaka atakapokuja,” alisikika Scott kutoka upande wa pili.
“Sawa. Tunasubiri! Tutakupa taarifa!” alisema mwanaume huyo huku kila mmoja akiwa na uhakika kwamba ni lazima Kennedy angefika nyumbani hapo kwa lengo la kuhakikisha kama familia yake ilikuwa humo kwani kila alipokuwa akimpigia simu mke wake, hakuwa akipatikana.
Je, nini kitaendelea?
Kwa sababu mambo ni mengi na muda mchache, naomba hadithi hii niitolee kitabu chake kwa sababu ni ndefu mnooooo.
Kitabu kitakuwa sh. 10,000 tu. Kuna watu wengine watatu....Boniface ambaye anawania urais Tanzania.
Kuna Diana ambaye alitumwa Uingereza kumpeleleza muuza madawa ya kulevya, Wayne.
Pia kuna Bianca ambaye alikuwa mpenzi wa bilionea wa Dubai aliyempa almasi iitwayo Waridi ambayo ilikuwa inakatazwa kuuzwa kwa kuwa ilihusika na kumwaga damu za watu huko Siera Leone.