NYEMO CHILONGANI
SHAMBULIO LA DAMU
0718069269
Sehemu ya Nane.
Viongozi wa vyuo mbalimbali vya utawa kutoka katika Kanisa la Living Christ waliwasiliana na kukubaliana kwamba ni lazima wafanye kila liwezekanalo kuhakikisha wanawamaliza wasichana wale ambao kiu yao kubwa ilikuwa ni kwenda kuzungumza na maaskofu kuwaambia uovu uliokuwa ukifanyika vyuoni.
Hawakutaka hilo litokee na ndiyo maana wakapanga mikakati ya kuwamaliza wote wawili. Wakaanza kumfuatilia Maria, walihitaji kufahamu mahali alipokuwa akiishi, ilikuwa ni lazima wamuue msichana huyo kwa sababu alikuwa mmoja wa watu hatari sana, yaani kumuacha hai lingekuwa kosa kubwa.
Vijana wao waliokuwa nchini Marekani ndiyo walikuwa kila kitu, waliwaambia jinsi mchezo ulivyotakiwa kuchezwa mpaka kuhakikisha Maria anaanza kufa na baadaye kufuata Nathalie.
Wakati wawili hao wakiagana katika mgahawa na kuondoka, vijana wawili ambao walikuwa na bastola zao wakaanza kufuatilia Maria ambaye aliondoka, akapanda treni na kuelekea huko kulipokuwa na apatimenti yake.
Ndani ya treni kichwa chake kilikuwa na mawazo tele, alijua kabisa kile walichokuwa wakienda kukifanya kilikuwa hatari na ilikuwa ni lazima wajipange mno na pia hawakutakiwa kumwamini mtu yeyote yule.
Hakujua katika treni aliyopanda kulikuwa na watu wawili waliotamani sana kuona akifa. Walikuwa humo, hawakuonyesha ishara zozote zile za kumfuatilia msichana huyo zaidi ya kujifanya nao abiria ambao walikuwa wakienda nyumbani kwao.
Maria alipofika katika kituo chake, akateremka na kuelekea nyumbani kwa kutembea. Vijana wale walikuwa nyuma yake, walitembea kwa mwendo wa taratibu huku wakijifanya kupiga stori na hawakuwa na muda naye.
Baada ya dakika kadhaa wakamuona akiingia ndani ya nyumba moja ambayo ilikuwa ni apatimenti, akaanza kupanda ngazi, nao wakaanza kupanda kwa nyuma yake mpaka kufika katika chumba alichokuwa akiishi ambapo walisikia tu mlango ukifungwa na kugundua kilikuwa ni chumba hicho.
Wakausogelea na kuanza kugonga kama watu waliokuwa na uhitaji fulani. Maria aliyekuwa ndani hata kabla ya kubadilisha nguo zake, akasikia hodi hiyo ambapo moja kwa moja akaelekea mlangoni na kuufungua.
Macho yake yakatua nyusoni mwa watu wawili, kwa kuwaangalia harakaharaka ilikuwa ni rahisi kugundua kama walikuwa watu wema, nyuso zao zilitawaliwa na tabasamu pana hali iliyoonyesha hakukuwa na tatizo lolote lile.
Ili kuwafanya wajisikie vizuri, naye Maria akaanza kutoa tabasamu lakini ghafla nyuso za watu hao zikabadilika na kuonekana katika hali nyingine kabisa na kutoa bastola zao.
Wakamsukumia Maria kwa ndani, akaanguka na kuumiza, akafutwa pale alipokuwa na kuchukuliwa, akafungwa kitambaa machoni na na kupelekwa nje huku akitakiwa kuwa kimya.
Hakujua watu hao walikuwa akina nani na walihitaji nini kutoka kwake. Moyo wake ulikuwa na hofu, alikuwa akilia huku akiomba msamaha kama kulikuwa na jambo baya alilifanya lakini watu hao hawakuongea kitu chochote kile.
Wakamchukua na kumpeleka ndani ya gari lao, wakaondoka mahali hapo huku Maria akiendelea kulia mfululizo. Wakiwa humo, mwanaume mmoja akachukua simu yake na kupiga sehemu, baada ya sekunde kadhaa, ikapokelewa na sauti ya mwanaume mmoja kusikika kutoka upande wa pili.
“Imekuwaje?” ilisikika sauti hiyo ikiuliza.
“Tunaye ndani ya gari! Kwa hiyo?”
“Kammalizeni halafu fanyeni kazi ya kumpa mwingine wa mwisho,” alisikika mwanaume huyo.
“Sawa.”
Kwa jinsi watu hao walivyokuwa wameongea kwenye simu ilionyesha kabisa hakukuwa na uhakika wa Maria kupona. Aliendelea kulia huku akiomba msamaha lakini hakukuwa na mtu aliyemsikiliza.
Wao walichotaka kufanya ni kile walichoambiwa na mwanaume mmoja kwenye simu kwamba wamuue na wafanye kila liwezekanalo kumpata msichana mwingine.
Gari likaondoka mpaka sehemu fulani ambapo kulikuwa na jumba kubwa. Huko ndipo ambapo walitakiwa kufanya mauaji yao na ndiyo sehemu ambayo waliamua kuichukua kwa ajili ya kazi hiyo tu.
Walipofika, gari likaingizwa ndani na Maria kuteremshwa. Hakunyamaza, bado alikuwa akilia mfululizo, hakujua ni mahali gani alipokuwa kwani bado kitambaa kilikuwa machoni mwake.
Akaingizwa ndani ya jumba hilo na kupelekwa katika chumba kimoja kilichokuwa na michirizi ya damu.
Wakawapigia simu wakubwa wao na kuwaambia tayari walifika katika jumba la mauaji hivyo walikuwa wakitaka kusikia neno kutoka kwao.
“Huyo bakini naye kwanza, tutawaambia ni nini cha kufanya,” alisikika mwanaume kutoka upande wa pili.
“Sawa bosi!”
“Tutawasiliana nanyi, bado mmoja amebakia,” alisema mwanaume aliyesikika kutoka upande wa pili.
Viongozi hao waliokuwa nchi mbalimbali barani Ulaya wakapigiana simu na kupeana taarifa kwamba tayari Maria alikuwa ametekwa na kulikuwa na msichana mmoja, Nathalie ndiye ambaye alibaki na kwa namna yoyote ile ilikuwa ni lazima naye atekwe na kuuawa pamoja.
Bado waliendelea kudukua mawasiliano yake, walimsikia alivyokuwa akiongea na Gabriel na kumwambia mambo mengi kuhusu yale yaliyokuwa yametokea.
Walisikia mengi mpaka mpango wa kwenda nchini Ubelgiji kwenye sherehe ya utoaji wa vyeti kwa wanafunzi wote ambao walisoma katika vyuo mbalimbali vya Kanisa la Living Christ.
Walijua kabisa kwamba kama wangempata Nathalie na kumuua bado isingesaidia sana kwa sababu tayari kulikuwa na mtu mwingine ambaye naye alijua kile kilichokuwa kimetokea.
Wakati wakipanga mikakati ya kumteka Nathalie na kumuua ilikuwa ni lazima wajipange kwa ajili ya kumuua Gabriel ambaye naye pia aliambiwa kila kitu jambo ambalo lingeweza kuwa tatizo kubwa kama tu wangethubutu kumuacha mwanaume huyo.
Haraka sana mwanaume mmoja akachukua simu na kupiga nyumbani kwa akina Nathalie, simu iliita kwa sekunde chache, ilipopokelewa, sauti ya Gabriel ilikuwa ikisikika.
Alichokisema mwanaume huyo aliyepiga simu ni kwamba watu hao walikuwa na saa ishirini na nne tu za kuishi kwani ndani ya saa hizo ilikuwa ni lazima wauawe kama walivyouawa wengine.
“Nimewaambia,” alisema mwanaume huyo huku akiwaangalia wenzake.
Hawakutaka kuishia hapo, kwa kuwa walijua anuani ya mahali watu hao walipokuwa wakiishi, wakawapigia simu vijana wao na kuwapa amri ya kuwaua watu hao kama walivyowaua wengine.
“Tupeni saa mbili tu, tutaifanya kazi hiyo,” alisema mwanaume kutoka upande wa pili.
“Tena fanyeni haraka sana!”alisema na kukata simu.
Upande wa pili mara baada ya Gabriel kupokea simu hiyo na kusikiliza maneno aliyoambiwa na kukatwa, akabaki akimwangalia ndugu yake, moyo wake ulikuwa kwenye hofu nzito, aligundua kwamba kuwa watu ambao walikuwa nyuma ya kila kitu walikuwa hatari ambao wangeweza kuwamaliza muda wowote ule.
Ilikuwa ni lazima picha hizo zipelekwe nchini Ubelgiji lakini kitu ambacho mpaka muda huo kiliwapa maswali mengi ni juu ya namna watu hao walivyojua kila kitu kilichokuwa kikiendelea.
Walijitahidi kufanya mambo yao kwa siri sana lakini watu hao walifahamu kila kitu, hilo liliwapa hofu na kuhisi walikuwa wakifuatiliwa na watu hao pasipo kujua.
“Wamejuaje mambo haya yote? Mliwaambia?” aliuliza Gabriel.
“Hapana!”
“Sasa wamejuaje?” aliuliza Gabriel.
Wakati wali hilo likiwa halijajibiwa, mawazo yake yakakumbuka kuhusu filamu mbalimbali jinsi watu walivyokuwa wakidukua mawasiliano ya simu na kusikiliza kila kitu kilichokuwa kikiendelea.
Gabriel akaichukua simu ya Nathalie, akaanza kuiangalia kwa makini, alihisi kwamba watu hao walifanya hayo yote kwa kupitia simu hiyo.
“Hii simu uliinunua wapi?” alimuuliza Nathalie.
“Tulipewa vyuoni!”
“Wote watatu?”
“Ndiyo!” alijibu Nathalie.
Gabriel hakutaka kuchelewa, haraka sana akaondoka na kuelekea chooni ambapo huko akaitumbukiza na kuflashi. Nathalie alishtuka, hakujua sababu iliyomfanya ndugu yake huyo kufanya jambo kama hilo, akaanza kulalamika.
“Nathalie! Mawasiliano yenu yalidukuliwa, inawezekana walikuwa wakifuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea kupitia simu zenu,” alisema Gabriel.
“Hapana! Haiwezekani!”
“Sasa unahisi ilikuwaje mpaka watu hao wakafahamu kilichokuwa kikiendelea? Wenzako waliuawa, walijuaje kama Anna alikwenda nchini Ubelgiji? Mlimtuma mtu aje, mbona hakuja? Inawezekana naye wakawa wamemuua, walijuaje hayo yote? Uuh?” aliuliza Gabriel maswali ambayo yaliingia kichwani mwa Nathalie na kutengeneza maana kubwa.
“Kwa hiyo tulikuwa tukifuatiliwa?” aliuliza Nathalie!
“Hiyo ndiyo maana yangu!”
Nathalie alichoka, naye akaamini watu hao hawakuwa wa mchezo mchezo, walitakiwa wafanye kila liwezekanalo kujificha na mwisho wa siku kutoroka mahali hapo kwenda kujificha sehemu fulani.
“Nathalie! Ni lazima tuondoke mahali hapa,” alisema Gabriel.
“Sawa!”
Wakakubaliana, wakatoka na kuondoka mahali hapo huku wakiwa na picha zile zilizopigwa walipokuwa chuoni huku picha nyingine wakizificha ndani ya nyumba hiyo.
Lengo lao lilikuwa ni kwenda katika Mtaa wa Livingstone alipokuwa akiishi baba yao. Walitumia dakika ishirini njiani ndipo wakafika na kukaribishwa nyumbani huko.
Walikaa huko kwa dakika kadhaa ndipo baadaye simu ya Gabriel ikaanza kuita, haraka sana akaichukua na kuangalia kioo, ni namba ngeni ndiyo iliyokuwa ikionekana, akaipokea.
“Halo!” aliita.
“Halo! Gabriel, upo wapi? Nimekuja hapa nyumbani siwaoni, mmekwenda wapi?” aliuliza msichana aliyekuwa akiongea upande wa nyuma.
“Wewe nani?” aliuliza Gabriel.
“Maria!”
“Maria?” aliuliza Gabriel huku akionekana kushtuka, si yeye tu bali hata Nathalie aliyekuwa pembeni akashtuka.
“Ndiyo! Mbona umeshtuka?”
“Hakuna kitu!”
“Mpo wapi?”
“Tulitoka...” alijibu Gabriel na hapohapo Nathalie akampokonya simu ile.
“Maria! Upo wapi?” aliuliza Nathalie huku akionekana kuwa na hofu.
“Nipo kwenu! Kuna watu walikuwa wakinifuatilia na gari, nimekimbia! Walikuja nyumbani kwangu na kutaka kuniteka. Nathalie, naomba uniokoe...niokoeee...” alisema Maria huku akilia, hapohapo akakata simu.
Nathalie alichanganyikiwa, sauti aliyokuwa ameisikia alijua kabisa alikuwa Maria, hakujua ni kwa jinsi gani angeweza kumuokoa msichana huyo, alisema kwamba alikuwa nyumbani kwao, kama ni hivyo ilikuwa ni lazima aondoke kwenda huko.
Akamwambia Gabriel kwamba walitakiwa kwenda nyumbani kumchukua Maria, Gabriel hakukubali, alimwambia inawezekana hiyo ilikuwa mbinu ya watu hao kutaka kuwateka hivyo hawakutakiwa kwenda huko.
Nathalie hakukubali, Maria alikuwa rafiki yake mkubwa, alihitaji msaada kwa sababu kulikuwa na watu waliokuwa wakimfuatilia, alijua kabisa kwamba kama angemuacha huko basi watu hao wangeweza kumuua kama ilivyokuwa kwa Anna.
Akataka kwenda peke yake, Gabriel akamzuia. Huo haukuwa muda wa kuzuiliwa, akaporonyoka katika mkono wa Gabriel na kuondoka zake.
Mwanaume huyo akamuita, Nathalie hakutaka kurudi nyuma, katika kile kilichokuwa kikiendelea, ilikuwa ni lazima kuhakikisha wanakuwa pamoja ili kuongeza nguvu.
Alichukua gari la kaka yake, akamuacha mahali hapo na kuondoka kwa kasi kubwa. Njiani alikuwa akilia, hakuamini kama alikuwa akienda kuonana na Maria ambaye alikuwa akimuhitaji sana kipindi hicho.
Ni ndani ya dakika kumi tu akafika nyumbani kwao, haraka sana akateremka na kuelekea ndani ya nyumba hiyo ambapo aliamini kwamba tayari Maria alikuwa ndani kwani alijua mpaka mahali funguo zilipokuwa zikikaa.
“Maria....Maria...” aliita huku akifungua mlango wa sebuleni.
Nathalie akafika sebuleni na kuangalia huku na kule, hakuona mtu, kulikuwa na ukimya mkubwa kiasi kwamba akaanza kuogopa kwani hakuwahi kuiona nyumba hiyo ikiwa na ukimya kama ilivyokuwa kipindi hicho.
Hakuacha kuita, bado moyo wake ulimwambia kwamba Maria alifika nyumbani hapo hivyo kuendelea kumuita zaidi. Hakuitikia mtu yeyote lakini wakati amekwenda chumbani na kurudi tena sebuleni akakutana na watu ambao kwa kuwaangalia tu, hakuwatambua.
Hata kabla hajauliza swali walikuwa akina nani na walifika hapo kufanya nini, wakatoa bastola zao na kumnyooshea, akaogopa na kuhisi kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wake.
Akaamuriwa apige magoti na kunyoosha mikono juu, hakubisha, akafanya hivyo, mwanaume mmoja akamsogelea na kumfunga kamba mikononi mwake na kutoka naye ndani kuelekea nje.
Nathalie hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea mahali hapo, alikuwa na hofu tele na muda wote ule alihisi kabisa angeuawa kwani kwa jinsi alivyowaangalia wanaume wale, walionekana kuwa na hasira naye kupita kawaida.
Walipofika nje, wakaingia naye ndani ya gari na kuondoka mahali hapo. Kila kitu kilichokuwa kikitokea nje, Gabriel alikuwa akikifuatilia kwa ukaribu.
Katika kipindi ambacho ndugu yake huyo aliondoka kule kwa ndugu yao na kuelekea nyumbani, aliamua kumfuatilia kwa nyuma, hakutaka kugundulika lakini alihakikisha dada yake huyo anakuwa salama kabisa.
Mpaka alipoingia ndani, alikuwa akifuatilia na ghafla akawaona watu wakiingia humo na walipotoka walikuwa na msichana huyo, wakaingia ndani ya gari na kuondoka zao.
Alisikitika, aliumia lakini hilo halikuwa suluhisho la kuzuia picha zile kufika nchini Ubelgiji, ilikuwa ni lazima awahi katika sherehe hiyo na kuwakabidhi maaskofu na kuwaonyeshea kile kilichokuwa kikiendelea.
Tumaini kubwa lilikuwa kwake, yeye ndiye ambaye alitakiwa kuamua kufuatilia suala hilo mpaka mwisho kwa sababu wale ambao walitakiwa kufanya hivyo, walitekwa na kuuawa na mbaya zaidi mpaka dada yake alitekwa mbele ya macho yake.
Moyo wake ulimuuma, alijua kabisa kitu ambacho kingefuata ni msichana huyo kuuawa, hakuwa na nguvu ya kwenda kushtaki polisi kwani aliamini hata kama angefanya hivyo ilikuwa ni lazima watu wale wamuue kwa sababu alikuwa amechelewa sana.
Haraka sana akakata tiketi, kitu pekee ambacho kingeonekana kuwa kama malipo kwa ndugu yake huyo na wasichana wengine wawili ilikuwa ni kuzifikisha picha zile sehemu husika na kuwaonyeshea unyama wote ambao wasichana wadogo walikuwa wakifanyiwa na viongozi wa makanisa ambao walipewa majukumu ya kusimamia vituo vilivyokuwa vikifundisha utawa.
Gabriel hakutaka kuchelewa, siku hiyohiyo akakata tiketi katika Shirika Ndege la Orange na hivyo kutakiwa kusafiri siku hiyohiyo na moja ya ndege kubwa ya shirika hilo iitwayo Airbus A350-900 iliyokuwa ya sita kwa ukubwa duniani.
***
Vijana ambao waliondoka na Nathalie nyumbani kwao wakaelekea katika jumba moja chakavu lililokuwa hapohapo New York tayari kwa kufanya mauaji ya mwanamke huyo.
Huko, wakamuunganisha na Maria ambaye alikuwa humo tayari, wawili hao walipoonana, wakaitana, wakakumbatiana na kuanza kulia pamoja.
Walijua kile ambacho kingetokea, walijua fika kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wao kwani watu wale hawakuonekana kuwa na masihara hata kidogo.
Pamoja na hayo yote hawakuacha kumuomba Mungu. Walimkumbusha jinsi walivyokuwa wamejitolea maisha yao yote kumtumikia, jinsi walivyohangaika kuhakikisha wanakuwa watawa na kumtumia maisha yao mpaka vifo vyao.
Walilia mno lakini hakukuwa na mtu aliyewasikiliza, ndiyo kwanza waliwaambia walitakiwa kubaki kimya kwani kelele zao zilikuwa chukizo mno masikioni mwao.
“Maria! Nimefurahi kukuona, hata kama tutauawa, tuuawe huku tukiwa tunamtumikia Mungu,” alisema Nathalie huku akimwangalia rafiki yake huyo ambaye alionekana kufarijika sana kumuona mwenzake mahali hapo.
“Mungu atutangulie, hata akina Yohana walikufa kwa kupata mateso makali, kama ni matendo makuu ya Mungu kwa kutaka kulibadilisha hili kanisa, ninaamini kwamba kuna siku ukweli utajulikana,” alisema Maria huku akimwangalia mwenzake.
“Ninaamini hilo.”
“Zile picha zipo wapi?”
“Anazo Gabriel! Najua atazifikisha tu, hata kama sisi tutauawa, ninaamini picha hizo zitafika katika mikono salama,” alisema Nathalie huku akimwangalia rafiki yake huyo.
Hawakuacha kulia, hawakuacha kumuomba Mungu kwa kila kitu kilichokuwa kikiendelea. Walishikilia rozali zao huku muda wote wakimshukuru Mungu kwa kila kitu kilichokuwa kikiendelea mahali hapo.
Baada ya dakika kadhaa wanaume wawili wakaingia huku wakiwa na mikanda ya suruali, walichokuwa wameambiwa ni kwamba walitakiwa kuwatesa wasichana hao, wawapige na mwisho wa siku wawaue kwa sababu waliwasumbua sana mpaka kutumia kiasi kikubwa cha pesa kuhakikisha wanakufa.
Hicho ndicho kilichofanyika, siku hiyo ilikuwa ni ya mateso makali, walichapwa mikanda, walivimba mpaka kutoka damu lakini hakukuwa na mtu yeyote yule aliyeonekana kujali.
Ni ndani ya nusu saa tu wasichana wote wawili walikuwa hoi, damu zilikuwa zikiwatoka, walivimba kila sehemu na hata kuongea hawakuwa wakiweza kabisa kutokana na mateso waliyokuwa wamepewa kuwa makubwa kupita kawaida.
Hakukuwa na muda wa kupoteza, baada ya kuhakikisha wamewatesa vya kutosha, wakawasiliana na viongozi wao na kuwaambia kilichotokea hivyo kusikilizia ni kitu gani ambacho kilitakiwa kufanywa.
“Wamalizeni!” alisema mwanaume ambaye alipigiwa simu.
“Sawa.”
Hicho ndicho kilichofanyika, baada ya kuambiwa hivyo, hawakutaka kusubiri sana, wakawachukua na kuwapeleka katika chumba kingine, huko, kilichofanyika ni kupigwa risasi za vichwa na miili yao kufungwa kwenye makabati maalumu na kuchomwa moto humo.
Huo ndiyo ulikuwa mwisho wao, watekaji hao wakaondoka mahali hapo lakini wakapigiwa simu na kuambiwa kwamba kulikuwa na mtu mwingine ambaye naye alitakiwa kuuawa haraka iwezekanavyo.
Mwanaume huyo alikuwa Gabriel, ni kwamba taarifa zilisema alikata tiketi tayari kuanza safari ya kuelekea nchini Ubelgiji lakini wakawa na hofu inawezekana kabisa mwanaume huyo alikuwa na picha hizo hivyo ilikuwa ni lazima auawe haraka iwezekanavyo.
Wakati wakipiga simu na kuwaambia kuhusu hilo, walikuwa wamechelewa kwani hata walipokwenda uwanja wa ndege, waliambiwa kwamba tayari abiria walikuwa tayari ndani ya ndege.
Walitaka kukata tiketi na kuingia humo lakini ilishindikana, ndege ilijaa lakini pia isingewezekana kupata tiketi kwa haraka sana hasa kwa ndege ambayo ilikuwa ikiondoka muda huo.
Wakawapigia simu mabosi zao na kuwaambia kuhusu suala hilo, wao wakawaambia waachane nao kwani kungekuwa na mpango mwingine ambao wangeupanga kama mabosi kuhakikisha Gabriel anauawa hata kabla ndege haikutua nchini Ubelgiji.
Haraka sana kikao cha dharura kikaitishwa nchini Ubelgiji, ilikuwa ni lazima kuhakikisha mwanaume huyo anakufa haraka iwezekanavyo hata kabla ya kufika nchini humo.
Wale ambao walikuwa katika nchi nyingine wakashirikishwa kwa njia ya simu na kuendelea na kikao hicho huku mada kubwa ikihusu kummaliza Gabriel ndani ya ndege hiyo vinginevyo kila kitu walichokipigania kingefeli na kuonekana kufanya kazi ya bure kipindi chote hicho.
“Kama vipi ndege ipotezwe kwa ajili yake,” alisema mwanaume mmoja.
“Ipotezwe? Kivipi?”
“Yaani ipotee kama ile ya Malaysia!” alijibu mwanaume huyo ambaye alitoa wazo la kupotezwa kwa ndege hiyo.
Hilo lilikuwa wazo zuri ambalo lilitakiwa kufanyiwa kazi haraka sana. Wakakubaliana na hatimaye kupanga mipango ni kwa namna gani ndege hiyo ingepotezwa.
Wakawasiliana na Kundi la Yamong Tsu lililokuwa nchini Thailand na kuwaambia kile kilichotokea kwamba ndege hiyo kubwa ya abiria ilitakiwa kupotezwa.
Wakati mipango hiyo ikiwa imepangwa, upande wa pili tayari abiria katika ndege hiyo walikuwa wamekaa katika viti vyao na tayari safari ya kuelekea barani Ulaya na Asia kabla ya kuingia Afrika ikaanza.
Kila mmoja alikuwa kimya! Walifunga mikanda yao na ndege kuondoka katika ardhi ya Marekani. Gabriel alikuwa humo, naye alikuwa mmoja wa watu waliokuwa wakiondoka nchini humo.
Kwenye begi lake la mgongoni ambalo lilikuwa kwa juu aliweka picha zile zilizokuwa zikionyesha michezo michafu ambayo ilikuwa ikichezwa na watu waliopewa jukumu la kusimamia vyuo vya wasichana waliokuwa wakisomea utawa katika Kanisa la Living Christ.
Wakati safari hiyo ikianza, hakujua kama upande wa pili kulikuwa na watu waliokuwa na mpango wa kuipoteza ndege hiyo ili picha zile alizokuwanazo zisiweze kuonekana.
Je, nini kitaendlea?