Stories of Change - 2021 Competition

Rachel Nzengo

Member
Jul 29, 2021
13
17
1. Nawaandikia ninyi vijana, kwa maana mna nguvu,

Yalinenwa na Nabii Yohana, akijua mtafuzu,

Lakini kumbe hamjafana, fursa mwachezea ka’ fuvu,

Tena ujana mwautafuna, paso kuwekeza nguvu,

Amkeni mwokoe nyakati, kwani zakimibia ka’ mshale.


2. Eti mshikaji sina ishu, nimeamua kula gudi taimu,

Melegea ka tishu, kuamka asubuhi hutaki jihimu,

Mwenye kikali kisu, ndiye kula nyama huhitimu,

Wahenga vyema walisanifu, kuwa na kitu muhimu,

Amkeni mwokoe nyakati, kwani zakimbia ka’ mshale.


3. Fursa nyingi wakataa, eti hizo si yako hadhi,

Kutwa wazunguka kitaa, peke na bando kwa simati,

Hebu acha kupumbaa, hiyo simati nitosha mtaji,

Kuna dili zimezagaa, mtandaoni tena hadhi zimekidhi,

Amkeni mwokoe nyakati, kwani zakimbia ka’ mshale.


4. Kila siku Ati nitaanza kesho, nikisha kwisha jipanga,

Mara nangoja mrejesho, kutwa unatangatanga,

Amka anza na ulichonacho, kabla ningelijua haijakusonga,

Kesho bila leo ni mateso, kesho nzuri na leo hupangwa,

Amkeni mwokoe nyakati, kwani zakimbia ka’ mshale.



5. Kuna mitaji mitatu asili, mola alotupa paso ubahiri,

Nayo ni muda, mikono na akili, kuanza nayo paso mhariri,

Pia na huu mwigine utajiri , wa elimu darasani utajiri,

Kwanini sasa tunakariri, eti sina pa kuanzia na hili,

Amkeni mwokoe nyakati, kwani zakimbia ka’ mshale.


6. Muda ni leo usighairi, anza kusaka kipato,

Kwa kutumia hiyo akili, fanya wazo kuwa mchakato,

Tumia mikono kwa ujasiri, fanya mchakato kuwa mapato,

Nakazia muda ni mali, tendea kazi mapema yako ndoto,

Amkeni mwokoe nyakati, kwani zakimbia ka’ mshale.


7. Zipo nyingi fursa kwa mjini, paso nyingi kutoa fedha,

Na zingine kede vijijini, mali nyingi za asili wazibeza,

Naomba mnipe idhini, kuwarithisha hili nalowaza,

Kila mja wa mavumbini, mola kampa kusudi 'taloweza,

Amkeni mwokoe nyakati, kwani zakimbia ka’ mshale.


8. Kila mtu ana chake kipaji, na karama alojaliwa,

Usije mlaumu Mpaji, eti yule bahati kapendelewa,

Kazania kipawa kukichaji, unachokiweza ndo ulichopewa,

Tumia wakati kwa uhitaji, tena siogope kosolewa,

Amkeni mwokoe nyakati, kwani zakimbia ka’mshale


9. Twaimba kijana taifa kesho, wa kujenga nchi sahihi,

Na leo hutaki vuja jasho, eti wasosoma wawakebehi,

Ngoja nikupe mrejesho, shahada iso ujuzi haitakustahi,

Wote tuijenge kesho, tuanze leo bado asubuhi,

Amkeni mwokoe nyakati, kwani zakimbia ka’mshale.


10. Beti kumi nafunga kwa haki, nikiasa kijana na fursa,

Mbeleni tusije 'shtaki, eti walininyima fursa,

Kuna nyingi pia AZAKI, zakuza vipaji bila hisa,

Sauti yangu ni yangu haki, ujunbe 'mefikisha kwa wahusika,

Amkeni mwokoe nyakati, kwani zakimbia ka’ mshale.
 
Back
Top Bottom