SHIRIKA la Ndege la Precision Air, limetangaza mkakati wa kuziba pengo lililoachwa na Shirika la Ndege la Air Tanzania (ATCL) kwa kuongeza safari zake za mikoani na kupunguza nauli kwa asilimia 15.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Alfonse Kioko alisema jana kuwa kuanzia Desemba 15, mwaka huu Precision itaongeza safari zake za anga kukidhi mahitaji ya wasafiri wanaozidi kuongezeka katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Tunaona ipo haja ya kuweka mazingira mazuri zaidi ya kuwahudumia na kukidhi mahitaji ya wateja wetu. Pamoja na kuongeza safari na kupunguza bei, bado tunaendeela kuangalia mahitaji yao mengine.
Wateja wetu wa mwanzo watakuwa katika nafasi nzuri zaidi kwa kuwa tunapeleka ndege yetu mpya aina ya ATR 72-500 iliyoingia nchini hivi karibuni, alisema Kioko. Akizungumzia utaratibu wa safari zao kwa sasa, Mkuu wa Kitengo cha Mipango na Mtandao cha shirika hilo, Patrick Ndekana, alisema kwa sasa wameongeza idadi ya safari kutoka Dar es Salaam kwenda Nairobi na kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza, na kwamba ndege zake zitaruka kuanzia saa 11:00 alfajiri hadi saa 1:00 usiku.
Kutoka Dar es Salaam kwenda Nairobi tumeongeza kutoka safari tatu hadi nne kwa siku na kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza tutakwua na safari tatu kwa siku kuanzia Jumamosi (leo) na za Kanda ya Kaskazini zitaendelea kuwa tano kama awali, alisema Ndekana.
Aliongeza kuwa ongezeko hilo litatoa fursa kwa wasafiri kufanya shughukli zao na kusafiri bila bughudha katika kipindi hicho ambacho, baada ya kuyumba kwa shirika la ndege la Air Tanzania ambalo limetangaza kufuta safari zake.
ATCL limefuta safari zake kwa muda wa siku 10, baada ya kunyanganywa cheti cha kuruka hewani na shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) tangu Desemba 08, mwaka huu. Hata hivyo, Ndekana alisema kuwa kutokana na ongezeko hilo la safari, kutakuwa na uwezekani wa kupata viti 210 kwa abiri wanaokwenda na kutoka Mwanza kurudi Dar es Salaam kwa kuwa watapeleka ndege mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 70 kwa safari moja, ambayo itafanya safari tatu kwa siku.
Wakati huo huo Boniface Meena anaripoti kuwa wakati Shirika la Ndege nchini (ATCL) juzi likieleza kuwa limeshawasilisha nyaraka zote za taratibu kwa Mamlaka ya Anga (TCAA) kwaajili ya marekebisho.
TCAA imeeleza kuwa hadi jana ATCL ilikuwa imewasilisha nusu ya nyaraka hizo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Margareth Munyagi, nyaraka hizo zilizotumwa tayari zimeshapitiwa na TCAA na kama ATCL ikifanya haraka katika uwasilishaji wa nyaraka zilizobaki ndani ya wiki mbili watakuwa wameshakamilisha mapitio yote.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, TCAA inakubaliana na jinsi Menejimenti ya ATCL inavyojituma katika kuhakikisha wanakwenda sawa na mahitaji ya yake ili waweze kurudishiwa cheti cha kuruka angani tena. Munyagi katika taarifa yake ameeleza kuwa kutokana na ATCL kutokuwa na kibali cha kuruka angani, kampuni ya Precision Air iko tayari kutoa huduma za safari za Mwanza itakapohitajika.
Ameeleza kuwa Precision wataongeza katika ratiba yao safari za Mtwara ili kuwaokoa abiria ambao walikuwa wasafiri kwa kutumia ndege za ATCL na wale ambao tayari walikuwa wamekata tiketi za safari. Alieleza kuwa kwa safari za Tabora na Kigoma Precision iatanya safari kama ilivyo katika ratiba zake hivyo abiria waliokuwa watumie ATC wataweza kutumia ndege hiyo.
Juzi ATCL ilikiri kuwa licha ya kukaguliwa na kitengo cha ukaguzi cha Chama cha Kimataifa cha Usafiri wa Anga (IOSA) tangu Desemba mwaka jana, lilishindwa kukidhi utashi wa viwango vipya vya usafiri huo na kusababisha linyang'anywe cheti cha kuendesha shughuli zake na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).
Kutokana na kunyang'anywa cheti hicho kinachoitwa AOC (Air Operations Certificate), shirika hilo lilisema kuwa, litakuwa likikosa karibu Sh300 milioni kwa wiki katika kipindi ambacho litakuwa halifanyi safari za anga kusubiri TCAA kufanyia kazi nyaraka zilizowasilishwa na ATCL Desemba 10 mwaka huu.
ATCL imezuiwa kufanya safari za anga baada ya TCAA kuinyang'anya cheti cha usafiri huo tangu Desemba 8, baada ya ICAO
kukagua shughuli za TCAA Novemba mwaka huu na kubaini nyaraka za ATCL hazikuwa zikiendana hata na sheria za TCAA za mwaka 2006 na hivyo kushauri linyanyang'anywe cheti hicho kwa muda usiojulikana.
Ukaguzi huo wa ICAO umekuja baada ya IOSA kufanya ukaguzi mwingine Desemba mwaka 2007 na kubaini jumla ya dosari 482 ambazo hazikufanyiwa kazi na ATCL hadi ukaguzi mwingine ulipofanyika mwezi uliopita.
"Novemba mwaka 2008, ICAO ilikuja nchini kukagua jinsi TCAA inavyofanya shughuli zilizo chini yake za kuangalia mashirika ya ndege yanayofanya kazi nchini," alisema Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, David Mattaka katika mkutano wake na waandishi wa habari juzi. "Katika kufanya hivyo, (ICAO) walibaini kuwa zile nyaraka za kiutaratibu ambazo zilikuwa TCAA, hazikulingana na sheria za TCAA za mwaka 2006.
Nyaraka hizo ndio zile ambazo zilikuwa zikiandikwa upya ili ziendane na sheria mpya," aliongeza Mattaka. " Naye Claud Mshana anaripoti kwamba mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amesema kufungiwa kwa ndege za ATCL kufanya safari zake kunatokana na serikali kukosa mikakati madhubuti ya kulijenga na kuliendesha shirika hilo.
Profesa Lipumba alisema makosa zaidi ya 400 yaliyogunduliwa hadi kusimamishwa kwa ATCL kufanya safari za TCAA, ni matokeo ya ubabaishaji wa serikali katika mambo ambayo alisema ni ya muhimu kwa nchi.
Akizungumza na Mwananchi jana Profesa Lipumba alisema, ni vema serikali ikajifunza utendaji kazi wa shirika la Precision Air ambalo linaubia na Shirika la Kenya Airways kwani limekuwa na huduma bora na za uhakika.
Ni vema hata sasa nguvu zikaelekezwa kwa Precision Air kwani ATCL haiwezi kufufuka tena alisema na kuongeza kuwa kama ni kuwa na mbia wa kuendesha shirika hilo basi anatakiwa asiwe mbabaishaji ili kuepusha hasara zisizo za lazima.
Kwa mujibu Profesa Lipumba, ni aibu kwa shirika nyeti kama hilo kufungiwa. ATCL imekuwa ikisuasua katika sekta ya usafiri wa anga tangu ubia wake na Shirika la Ndege la Afrika Kusini kuvunjika.