ATC yanusa kifo
Mattaka akataa wazo la kutakiwa ajiuzulu
na Mwandishi Wetu
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
SHIRIKA la Ndege la Tanzania (ATC), limesema litapata hasara ya sh milioni 300 kila wiki kutokana na kusimamishwa kwa huduma za ndege zake.
Hatua hiyo imefufua maumivu kwa shirika hilo ambalo limekuwa katika jitihada za kuboresha huduma zake baada ya kukabiliwa na matatizo ya kifedha ambayo yalilikumba wakati na baada ya kuingia ubia na Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA).
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, David Mattaka, alipokuwa akitoa ufafanuzi juu ya sababu zilizofanya shirika hilo lifungiwe kurusha ndege zake kwa kushindwa kutimiza masharti 482 ya usalama wa anga.
Mkurugenzi huyo alisema kusitishwa kwa huduma ya ndege za ATC, kunatokana na Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini (TCAA) kusimamisha huduma za shirika hilo baada ya ukaguzi uliofanywa na Jumuia ya Kimataifa ya Usalama wa Anga (IOSA) kupitia Kitengo chake cha ukaguzi wa usalama (AYATA), kubaini kuwa TCAA haikufuata taratibu katika kutoa cheti cha kurusha ndege kwa shirika hilo.
Mattaka alisema, ukaguzi huo uliofanywa Desemba, mwaka jana (2007), ulibaini kuwepo dosari 482 katika maeneo ya operesheni yaliyo chini ya TCAA.
Kwa mujibu wa Mattaka, dosari 39 zilibainika katika eneo la oganaizesheni na usimamizi, uongozaji wa ndege, dosari 206, matengenezo dosari 45, sehemu ya mizigo, dosari 44, ulinzi, dosari 36, kitengo cha utoaji, dosari 55, na uwanjani dosari 50.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa, Novemba mwaka huu, Shirika la Kimataifa Linalojishughulisha na Usalama wa Anga Duniani (ICAO), lilikuja kuifanyia ukaguzi TCAA kuhusiana na jinsi inavyosimamia mashirika ya ndege yanayofanya kazi nchini na kubaini kuwa vielelezo vya mashirika ya ndege vilivyokuwa TCAA, havikidhi masharti kwa mujibu wa taratibu zinazoongoza TCAA za mwaka 2006.
Kwa hiyo walibaini kuwa cheti kilichotolewa kwa ATC na ambacho muda wake ulikuwa umalizike Desemba 15, 2008, hakikuwa kimefuata taratibu. TCAA kwa hiyo iliamua kuiondolea ATC cheti hicho hadi hapo itakapokamilisha taratibu za kuwa na vielelezo vinavyokidhi masharti ya TCAA, alisema Mattaka.
Alisema kwa bahati nzuri, ATC iliweza kuwasilisha vielelezo vyote vilivyohitajiwa Desemba 10, 2008, na sasa shirika hilo linaisubiri TCAA ijiridhishe na vielelezo hivyo na kulirejeshea cheti ili liendelee kurusha ndege zake.
Kwa mujibu wa Mattaka, TCCA inatarajia kutumia takribani siku 10 kupitia nyaraka hizo za ATC na kurejesha huduma zake.
Alisisitiza kuwa mapungufu yaliyojitokeza ya kutokuwepo kwa vielelezo hivyo, hayana uhusiano wowote na suala la usalama wa ndege zake na hakuna kipindi ambacho wateja wake walikuwa katika hatari, kwa sababu ya ubovu wa ndege zake.
Tunajutia usumbufu wowote uliojitokeza kwa wateja wetu na tunawaomba watuvumilie wakati tukiendelea kulishughulikia suala hili, alisema.
Mattaka alisema hivi sasa shirika lake linarejesha nauli kwa abiria waliokata tiketi za kusafiri na ndege za shirika hilo katika siku za hivi karibuni, lakini waliomba kusafiri kwa tarehe za mbali, wataendelea kubaki nazo kwani wanaamini baada ya siku 10 kuanzia jana, watarejesha huduma zao.
Alipoulizwa kama yuko tayari kujiuzulu kutokana na kushindwa kuliendesha shirika hilo tangu alipokabidhiwa, Mattaka alisema hafikirii kufanya hivyo kwani anaamini bado anaweza na kutoa wito kwa serikali kuendelea kulisaidia shirika hilo linalochungulia kaburi.
Wakati Mattaka akitoa ufafanuzi huo, Waziri wa Miundombinu,Dk. Shukuru Kawambwa, alisema ATC imesimamishwa kutoa huduma kwa kutokidhi vigezo vya kimataifa vya usalama wa anga.
Alisema kufungiwa kwa shirika hilo hakutokani na ubovu wa ndege zake kama inavyofikiria na wengi bali kutokana na dosari zilizojitokeza wakati wa ukaguzi.
Wamesimamishwa kwa muda tu na tatizo si mwekezaji, bali kutofuata utaratibu uliopangwa na IATA, alisema Dk. Kawambwa.
ATC ni shirika pekee la ndege la umma na hadi Mei mwaka huu, lilikuwa na ndege sita, tatu ikiwa inazimiliki na nyingine za kukodi.
Hivi karibuni Kamati ya Miundombinu ya Bunge, ilisema kuwa kulikuwa na mpango wa shirika hilo la ndege kuingia ubia na shirika moja la ndege la China.