Serikali Kupunguza Gharama za Kusafisha Figo Kutoka 350,000 hadi Kati ya 90,000-150,000

benzemah

JF-Expert Member
Nov 19, 2014
1,504
3,034
Serikali imedhamiria kupunguza gharama za kusafisha figo kutoka Shilingi 350,000 mpaka Shilingi 90,000 hadi 150,000 kwa lengo la kuwapunguzia wananchi mzigo wa gharama za matibabu hasa kwa wenye vipato vya chini.

Taarifa hizo zimetolewa leo bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Mhe. Dkt. Godwin Mollel wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum kupitia Vijana, Mhe. Lucy Sabu lililohoji kuhusu mpango wa Serikali kupunguza gharama za kusafisha figo.

Naibu Waziri Mollel amesema kuwa, Serikali imekuwa ikitoa huduma za matibabu ikiwemo huduma ya kusafisha figo kwa wagonjwa wote bila kujali kipato cha mgonjwa husika ambapo huduma hizo kwa sasa zinatolewa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, hospitali za Rufaa za Kanda, Mikoa na Hospitali Maalum ikiwemo Hospitali ya Chuo Kikuu cha Dodoma.

"Katika eneo la huduma za kusafisha figo, wizara imegundua kuna uwezekano wa kupunguza gharama za huduma hiyo badala ya kuwa 350,000 kwa awamu moja, mgonjwa ataweza kutibiwa kwa gharama ya kuanzia 90,000 hadi 150,000 kwa awamu moja, hivyo kuna mpango wa kushusha gharama hizo, amesema Naibu Waziri Mollel.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi wenye kipato kidogo kufuata taratibu zinazopelekea wao kupata misamaha ya huduma (exemption) ikiwemo huduma hii ya usafishaji wa figo kwa kuwasilisha barua kutoka kwa Mtendaji wa Kata husika.
 
Back
Top Bottom