Serikali isipotii Mahakama nani atailazimisha? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Serikali isipotii Mahakama nani atailazimisha?

Discussion in 'Jukwaa la Sheria (The Law Forum)' started by Mzee Mwanakijiji, Jun 16, 2010.

 1. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #1
  Jun 16, 2010
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,362
  Likes Received: 6,393
  Trophy Points: 280
  Na. M. M. Mwanakijiji

  Serikali yetu haina nia ya kutii mahakama zetu. Labda niseme vingine, serikali yetu haina mazoea ya kutii maamuzi makubwa ya mahakama. Nitumie maneno mengine ili nieleweke vizuri zaidi, serikali yetu haina kusudio la dhahiri la kuhakikisha kuwa Mahakama halali ya nchi inapotoa uamuzi ni lazima serikali itii uamuzi huo hata kama watu binafsi kwenye serikali hiyo hawaupendi au unatishia maslahi yao. Zaidi ya yote, pale ambapo Mahakama imeamuru kuwa jambo fulani ni kinyume na Katiba basi ni jukumu la watunga sheria aidha kubadilisha Katiba hiyo na kuondoa kujipinga huko na kulifanya jambo hilo likubaliane na Katiba au kubadili sheria hiyo ili ikubaliane na Katiba. Hilo la kwanza, litasababisha wanasiasa kuchezea Katiba kwani kila Mahakama ikiamua jambo na kusema ni kinyume na Katiba basi wanasiasa wetu mahiri watabadili Katiba! (wameshafanya hivi mara kadhaa). Hilo la pili, ni gumu kufanya hasa kama sheria iliyopo inanufaisha wanasiasa waliopo au chama kilicho madarakani au makundi ndani ya serikali hiyo au watu fulani mashuhuri.

  Nimesema kuwa serikali yetu haina mazoea ya kutii amri ya mahakama hasa pale amri hiyo inagongana na maslahi ya watu wachache au kikundi fulani. Hivyo, badala ya kutii agizo la Mahakama, basi vyombo vyetu vya dola vinasuasua na kujifanya kana kwamba hakuna amri ya mahakama. Ninayo mifano mitatu ya jinsi gani serikali yetu imekuwa na ugoigoi usioelezeka wa kutii amri mbalimbali za mahakama zetu.

  Kesi ya kwanza inayoonesha jinsi ilivyo vigumu kwa serikali yetu kutii mamlaka ya Mahakama ni ile kesi ya Devram Valambhia ambaye mwaka 1985 aliingia mkataba na serikali kuiuzia magari na zana za kijeshi kwa ajili ya JWTZ/JKT. Mdau wa Valambhia Bw. Reginal Nolan alilipwa wakati Bw. Valambhia alianza kuzungushwa miaka nenda rudi kudai malipo yake. Alifungua kesi Mahakama Kuu kudai fedha zake karibu shilingi Bilioni 56. Licha ya maamuzi ya mahakama ambayo yote yalikubaliana na mfanyabiashara huyo, serikali ilitumia kila mbinu kutotaka kumlipa bwana huyo. Mwaka 2001 Mahakama ilitoa amri ya kukamatwa akaundi za Benki Kuu ili kumlipa mfanyabiashara huyo. Ikalazimu Jaji Salum Massati wa Mahakama Kuu kutoa amri ya kukamatwa Gavana wa Benki Kuu kwa kudharau amri ya mahakama (usiwe na shaka hakukamatwa, kwani wakubwa hawakamatwi hadi pale wanapotuhumiwa kufanya mauaji na hapo wanawaita mapolisi waje nyumbani kwao!) Kwa karibu miaka 20 serikali imekuwa ikipiga dana dana shauri hilo na kuifanya mahakama yetu kuwa ni mahakama isiyo na nguvu ikisimamia kesi za sungura wakati simba wanaendelea kana kwamba hakuna sheria ya wanyama wote msituni. Kwa mazingaombwe serikali yetu ikatunga sheria ambayo inakataza kukamatwa kwa akaunti za Benki Kuu huko mbeleni ili hata Benki Kuu wakigoma kumlipa mdai, hakuna mtu anachoweza kufanya. Kwa kumtumia Wakili Nimrodi Mkono serikali ilijaribu kutishia hata majaji kuwa endapo Benki Kuu italazimishwa kumlipa Bw. Valambhia basi itajikuta inashindwa kulipa mishahara, hata ya majaji! Mahakama yetu haikutishika iliendelea kusisitiza uamuzi wake. Huo ni mfano wa kwanza.

  Mwaka 1999 Mahakama ya Tanzania ilikubaliana na uamuzi wa Mahakama ya Zanzibar wa kuamuru usitishwaji wa ujenzi wa nyumba kwenye eneo la Bw. Ahmed Abdallah Shariff uliofanywa na vigogo wa CCM huko Zanzibar. Mahakama ya Zanzibar ilitoa amri ya nyumba hizo kuvunjwa na waliovamia kuondolewa. Vyombo vya dola vya Zanzibar vilikataa kutii uamuzi huo wa mahakama na vikafumba macho ili visiutekeleze. IkalazimuMahakama ya Mkoa wa Mjini Magharibi kutoa amri nyingine ya kukamatwa vigogo waliokiuga agizo hilo. Sina uhakika kama agizo hilo limetiiwa na waheshimiwa wetu au la.

  Lakini hayo yote tisa, kumi ni jinsi serikali ya CCM ilivyodharau wazi uamuzi wa mahakama kuu kuruhusu wagombea huru na kwa kutumia sababu zisizo na mkia wala kichwa kuendelea kusuasua kutii uamuzi huo. Hivi sasa kuna kiti cha Ubunge kilichowazi cha Jimbo la Tunduru na Tume ya uchaguzi imeshatangaza tarehe ya kufanyika uchaguzi mdogo. Tatizo lililopo ni je uchaguzi mdogo wa Tunduru uruhusu wagombea binafsi kama Mahakama Kuu ilivyoiamuru ofisi ya Tume?

  Vyombo vya kiraia na Mchungaji Mtikila (aliyeleta kesi ya Kikatiba kuhusu jambo hili la wagombea huru) wanafikiri kuwa Tume iruhusu wagombea huru kwani mahakama imeshaamua kuhusu jambo hilo. Hata hivyo Mwenyekiti wa Tume Jaji Lewis Makame amesema kuwa sheria iliyopo hairuhusu wagombea huru, na ni sheria hiyo itafuatwa kwani licha ya Mahakama kutangaza kuwa sheria inayokataza wagombea huru ni kinyume na Katiba, sheria hiyo bado ina nguvu kwani Bunge halijaibadilisha.

  Hapa ndipo tatizo jingine tulilonalo linapojidhihirisha. Kama mahakama imeamua sheria fulani ni kinyume na Katiba, na Bunge halitaki na halina nia ya kurekebisha sheria hiyo, uhalali wa sheria hiyo uko wapi? Je, ni halali kutii sheria hiyo wakati mahakama imesema inakiuka Katiba? Je, kama mahakama haijatoa muda rasmi wa kubadilisha sheria hiyo, na Bunge halitaki kubadilisha, uhalali wa maamuzi ya mahakama uko wapi? Nitawaachia magwiji wa sheria kujaribu kuchambua hayo. Kwanini hata hivyo serikali ya CCM inaogopa kurekebiesha sheria ili wagombea huru waruhusiwe katika Tanzania wakati nchi zenye matatizo kama Uganda na Rwanda zimeruhusu?

  Kwanza, CCM inaogopa wagombea huru kwani kwa kuruhusu wagombea huru udhaifu mkubwa wa CCM utaonekana na kuanikwa hadharani na utadhihirisha jinsi chama hicho kilivyogawanyika ndani yake. Udhaifu huu wa CCM utaonekana pale chama hicho kitakapofanya mchakato wa kuchagua wagombea wa chama hicho wa nafasi mbalimbali na katika kufanya hivyo kuwaengua baadhi ya watu maarufu kama walivyofanya 1995, 2000, na 2005. Hatari ya kufanya hivyo ni kuwa wale wanachama maarufu walioenguliwa wanaweza kusimama na kushinda viti hivyo wakiwa wagombea huru. Hebu fikiria watu kama kina Njelu Kasaka ambao alienguliwa angesimama kama mgombea huru huko Chunya asingeshinda?

  Sababu ya pili ni kuwa CCM inajifanya baba wa Watanzania na hivyo kulazimisha Watanzania kujiunga na vyama ili wapate nafasi ya kuongoza. Kwa mawazo ya baadhi ya wakuu wa chama hicho viongozi wazuri, wenye uzalendo wa kweli na wanaojali wananchi wanapatikana kwenye vyama vya kisiasa peke yake. Wale watu wenye sifa hizo na ambao wangependa kushika nafasi za uongozi lakini hawataki kujiunga na chama chochote basi "wao walie" maana CCM inasema watu hao watarubuni wananchi, hawatawajibika, na watatishia maslahi ya usalama wa nchi kwani wanaweza kuwa mamluki wa mtu binafsi. CCM inataka watanzania waamini kuwa viongozi walioko kwenye vyama ndio walio "mahiri na majasiri"! Huu ni ulaghai wa mchana kweupe kwani matatizo mengi tuliyonayo Tanzania yameletwa na watu wenye kubeba kadi za vyama ya kisiasa ambavyo gwiji lao na mama lao ni CCM. Mahakama kuu iliona jambo hilo kama ilivyoamuriwa na jopo la majaji likiongozwa na Jaji Manento ambaye alitamka wazi kuwa "Tunaendelea kutangaza kuwa marekebisho hayo (marekebisho ya sheria Na. 34) yalikiuka Katiba pamoja na Azimio la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu ambalo Tanzania imeridhia".

  Kwa hali ilivyo sasa hata hivyo Jaji Lewis Makame yuko sahihi, Mahakama inapotangaza kifungu fulani cha sheria ni kinyume na Katiba kifungu hicho hakifutiki mara moja (automatic) kama ilivyo katika nchi nyingine kama Marekani bali kinaendelea kuwepo na kina nguvu hadi Bunge libadili sheria hiyo. Hilo peke yake haliwezi kusimamisha uchaguzi mdogo wa Tunduru kama Mtikila na baadhi ya vyama wanavyotaka. Nakubaliana na Mtikila kuwa suala la daftari la wapiga kura lililoenda na wakati ni hoja kubwa na ya msingi zaidi inayoweza kusimamisha uchaguzi huu kuliko suala la wagombea huru.

  Kwa maoni yangu suala la Mgombea huru ni suala ambalo Bunge lioneshe njia na kutii agizo la mahakama. Madai ya Mwanasheria Mkuu kutaka kukata rufaa hayana msingi kwani ni mchezo waliocheza kwenye kesi ya Valambhia. Mtu unapoamua kukata rufaa una mawazo kuwa una nafasi ya kushinda. Hata hivyo katika suala hili la wagombea huru hakuna mahakama Tanzania ambayo inaweza kukubaliana na serikali na kuona Katiba yenye kutoa haki kwa wananchi haina maana. Lengo la serikali ya CCM kupitia Mwanasheria Mkuu ni kupoteza muda kwani wanajua wazi kuwa kwa kadiri sheria hiyo bado ina nguvu (kama alivyodai Jaji Makame) hawana ulazima wowote wa kutii agizo la mahakama kwani hakuna mtu wa kuwalazimisha kutii!

  Na hilo nalo linatuleta kwenye tatizo jingine ambalo ndilo kiini cha makala hii. Nani anaweza kuilazimisha serikali au viongozi wa serikali kutii amri halali ya mahakama kama viongozi wenyewe wa serikali hawako tayari kufanya hivyo? Kama polisi wanagoma kwenda kumkamata mtu mkubwa (kama walivyofanya Zanzibar) nani atawalazimisha kufanya hivyo? Je Mahakama ikiamuru Gavana wa Benki akamatwe, na Polisi hawataki kufanya hivyo nani atamkamata Gavana huyo? Mahakama imetoa uamuzi kuhusu wagombea huru, uamuzi ambao wataalamu wa kisheria wanauhakika utasimama katika mahakama yoyote ya rufaa, ni lini Bunge la CCM litakuwa tayari kutii amri hiyo? Kama Bunge ndio linakuwa mfano wa chombo kisichotii mahakama, sisi raia wengine kwanini tukubali maamuzi ya mahakama hasa pale ambapo maamuzi hayo hayana maslahi kwetu?

  Inawezekana Jaji Makame ameshinda wakati huu kiufundi (technically) lakini hoja ya wagombea huru haiendi kokote kwani wapo Watanzania wengi ambao hawapendi vyama vya kisiasa lakini wananyimwa nafasi ya kuitumikia nchi yao kwa vile tu hawataki kujiunga na vyama vya kisiasa. Na Bunge la wabunge waoga wa CCM ambao hawataki kufanya kile ambacho waliapa kukifanya – kulinda na kutetea katiba, siku moja watajikuta wanawekwa pembeni ili Bunge ambalo halichezi ngoma za serikali na lenye kulinda Katiba ya Jamhuri yetu litakapoapishwa. Wasipoangalia vizuri, wanaharakisha ujio wa Bunge hilo, bunge ambalo litakuwa tayari kutii amri za Mahakama, kama vile mahakama zinafuata sheria zitungwazo na Bunge hilo. Siku hiyo watanzania wasiotaka kujifunga na vyama vya kisiasa wataweza kusimama na kugombea nafasi zote za uongozi kama wagombea huru. CCM wapende wasipende, lililopangwa kuwa, litakuwa kwani jogoo awike, au asiwike, kutakucha!!


  Iliandikwa: Feb 2007 Hapa
   
 2. Mwalimu

  Mwalimu JF-Expert Member

  #2
  Jun 16, 2010
  Joined: Aug 21, 2008
  Messages: 1,475
  Likes Received: 227
  Trophy Points: 160
  Mkuu Mwanakijiji haya ndio matatizo ya kulewa madaraka.
   
 3. Nemesis

  Nemesis JF-Expert Member

  #3
  Jun 16, 2010
  Joined: Feb 13, 2008
  Messages: 3,844
  Likes Received: 1,110
  Trophy Points: 280
  kweli maandishi hayafi, miaka 3 na zaidi lakini hakuna lililotendewa hii ndiyo inaleta maana kwanini hatutaweza kuendelea, no changes. Artcle hii inaweza kufufuliwa miaka 10 ijayo ikaonekana kama imeandikwa juma hilohilo, kwasababu matatizo yaleyale yanadumu daima.
   
 4. Mwalimu

  Mwalimu JF-Expert Member

  #4
  Jun 16, 2010
  Joined: Aug 21, 2008
  Messages: 1,475
  Likes Received: 227
  Trophy Points: 160
  Tuiombee mahakama yetu isilegeze kamba katika hili, dawa ni kuendelea kuwatandika rungu kila wakija mpaka watasalimu amri wenyewe!
   
Loading...