Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,736
- 40,858
Na. M. M. Mwanakijiji
DAR-ES-SALAAM (ZAMAMPYA.COM) Katika hali ambayo inaonesha kufanyika kwa ‘cheupe chekundu’ au mchezo wa "karata tatu" Serikali ya Tanzania imeamua kuwabadilishia maombi madaktari waliojitokeza kuomba kazi Kenya baada ya kuamua madaktari hao waajiriwe katika Serikali hata kama hawakuomba ajira ndani ya Serikali.
Taarifa ya Wizara imesema kuwa “tarehe 18 Machi, 2017 Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilitangaza nafasi hizo za ajira kwa Madaktari wa Tanzania kwenda kufanya kazi nchini Kenya. Maombi hayo yalipokelewa ambapo hadi tarehe 27 Machi, 2017 ambapo jumla ya maombi takribani 496 yaliwasilishwa. Baada ya kufanya uchambuzi wa maombi haya ilibainika kuwa, Madaktari 258 walikidhi vigezo vilivyotakiwa kwenda kufanya kazi nchini Kenya.”
Kwa mujibu wa taarifa ya Bi. Mwalimu “wakati Serikali ya Tanzania ikiendelea kukamilisha utaratibu wa ajira za Madaktari wake nchini Kenya ikiwa ni pamoja na kutangaza nafasi hizo za kazi na kufanya uchambuzi wa maombi ya kazi, kuandaa Hati ya Makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Kenya kuhusu ajira hizo za Madaktari na Mkataba wa Ajira kwa Madaktari hao, wananchi (Madaktari) watano wa Kenya waliwasilisha pingamizi Mahakamani kuitaka Serikali ya nchi yao kusitisha kuajiri Madaktari kutoka Tanzania.”
Bi. Mwalimu alieleza kuwa “Kwa kuwa ratiba ya utekelezaji wa ajira hizi za Madaktari ilikubalika na pande zote mbili kuwa iwe imekamilika ifikapo tarehe 6 Aprili, 2017 na kuwa Madaktari hao wawe tayari kusafiri kwenda nchini Kenya kati ya tarehe 6-10 Aprili, 2017 na kwa kuwa hadi tarehe ya taarifa hii Mahakama nchini Kenya haijaondoa pingamizi lililofunguliwa kuhusu ajira za Madaktari wa Tanzania nchini Kenya.”
Kesi ya pingamizi lililotolewa na Mahakama ya Kenya kuzuia Serikali ya Kenya kuajiri madaktari wa kigeni inatarajiwa kuendelea huko Kenya siku ya Ijumaa wiki hii.
Tangazo la ajira za Kenya lilitolewa na Wizara kupitia Katibu Mkuu wake Dkt. Mpoki Ulusubisya ambapo lilieleza kuwa madaktari hao wanaotaka kwenda Kenya walikuwa waende kwa mkataba wa miaka miwili.
Hata hivyo Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kilipinga mpango huo na kudai kuwa kufanya hivyo ni kutowatendea haki madaktari wa Kitanzania na pia kutoitendea haki sekta ya afya Tanzania ambayo nayo ina upungufu wa madaktari. Katika tamko lao la kupinga mpango huo la tarehe 20/3/2017 chama hicho kilisema kuwa “Kwa kuwa MAT haikushirikishwa katika hatua yeyote na hivyo kukosa fursa yakufahamu lolote, Hivyo basi tungependa kupata ufafanuzi kuhusu masualayafuatayo ;Kwa nini Serikali ya Kenya imeshindwa kuajiri Madaktari wake na kuanza kutafuta Madaktari kutokaTanzania huku ikizingatiwa kwamba malipo ya Madaktari wa Tanzania yatakuwa makubwa zaidi ya wenyeji ?”
Uamuzi uliotangazwa leo na Waziri Mwalimu hata hivyo hausemi kama madaktari hao 254 ambao wataajiriwa Serikali wataajiriwa kwa mkataba wa aina gani na utakuwa na tofauti gani na madaktari ambao tayari wanafanya kazi nchini hasa ikizingatiwa kuwa wengi waliomba nafasi ya kwenda Kenya kwa sababu ya maslahi yao kwani walikuwa wanatarajiwa kulipwa kama wataalamu wa nje huku wakiahidiwa malipo manono na nyumba.
Hata hivyo, haijajulikana kama madaktari hawa ambao walikubaliwa kwenda Kenya na sasa wameamuliwa kufanya kazi Tanzania watakubali ajira hizi mpya ambao wao hawakuziomba au kama watalazimishwa hasa kwa vile Serikali katika taarifa yake imesema kuwa “majina ya Madaktari husika na vituo watakavyopangiwa kazi yatatangazwa katika tovuti ya Wizara www.ehealth.go.tz pamoja na wataalamu wengine wa Afya 11 walioleta maombi yao na kukidhi vigezo.”
Serikali imeendelea kuahidi kuwa itakuwa tayari kusaidia Kenya madaktari 500 baada ya mapingamizi yaliyowekwa kuondolewa lakini haijaeleza taarifa hiyo endapo nafasi hizo zitaanza tena hawa madaktari ambao watakuwa waajiriwa wa serikali ya Tanzania watapewa nafasi tena ya kwenda Kenya kutafuta maslahi zaidi au wakikubali ajira za serikali ndio nafasi ya kutafuta maslahi nje ya nchi zitakuwa zimepotea.