ANZA SIKU NA BWANA
KWA NENO NA MAOMBI.
NENO LA MUNGU LINA NGUVU KULIKO NENO LA MWANADAMU
ZABURI 1:1-3
1 Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.
2 Bali sheria ya BWANA ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.
3 Naye atakuwa kama mti uliopandwa Kandokando ya vijito vya maji, Uzaao matunda yake kwa majira yake, Wala jani lake halinyauki; Na kila alitendalo litafanikiwa.
Mpendwa jifunze;
■
Kusikiliza shauri la Bwana siku zote.
■
Kuketi barazani pa Mungu.
■
Kupendezwa na kutafakari sheria ya Bwana.
Mpendwa,
1.Je, wewe huwa
unapendezwa na nini
hasa?
2.Je, wewe unapenda
kutafakari sheria ya
Bwana?
3.Je, wewe unazaa
matunda kwa majira
yake?
TAFAKARI
Mpendwa, mafanikio yako na ustawi wako wa kiroho, kiakili, kiuchumi na kimwili hutegemea sana uhusiano wako na Mungu. Mungu hupendezwa na mtu wa namna hii,

Asiyekwenda katika shauri la wasio haki. Shauri la wasio haki lina ugomvi, fitina, chuki, uchonganishi, na masengenyo. Mambo ambayo ni chukizo mbele za Mungu.

Asiyeketi barazani pa wenye mizaha. Mpendwa mizaha ni chukizo mbele za Mungu kwani mwisho wake huzua matukano na ugomvi.

Mtu mwenye muda wa kutafakari sheria ya Bwana mchana na usiku. Sheria ya Bwana ina maagizo yote yakupasayo kuenenda kwayo, ndani ya neno la Mungu kuna uponyaji, baraka, amani, upendo, ushindi, ulinzi na ndiyo njia ya uzima wa milele.

Mpendwa, ukikaa na Mungu vizuri lazima utastawi, lazima utazaa matunda. Biashara zako, familia yako, kazi, mashamba, haviwezi kunyauka maana Bwana huachilia vijito vya maji. Na kila ulifanyalo litafanikiwa, wengine wanapolia hali ngumu ya uchumi, njaa, fedha hakuna kwako ni kicheko.

Mpendwa, kufanikiwa ni pamoja na kutimiza kile ambacho unapaswa kukifanya, na kusudi la wewe kuwepo hapa duniani. Unapoweza kulitimiza, basi wewe umefanikiwa. Kufanikiwa ni kuweza kushinda dhambi ambako huanzia pale unapoamua kumfuata
YESU KRISTO kuwa
BWANA NA MWOKOZI wa maisha yako.
WAFILIPI 4:19
19.Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu.
Barikiwa sana mtu wa Mungu.
Uwe na Jumatano njema sana.
27, Jan, 2021