SEHEMU YA 93...
Aliwachezea wanawake wengi, aliwaambia wanawake hao watoe mimba lakini wote hakuwakumbuka, mtu aliyemkumbuka zaidi alikuwa Sarafina. Picha aliyokutana naye barabarani ikamjia, hakuwa Sarafina yule wa kipindi cha nyuma, alikuwa mwingine kabisa, aliyechoka, ambaye alihitaji msaada mkubwa ila kwa kuwa alikuwa jeuri, akaondoa gari lake pasipo kumsikiliza kwa chochote kile.
Picha hiyo ilimuumiza kupita kawaida.
Alibaki kitandani pale akilia kwa uchungu. Ulikuwa ni muda wa kutubu dhambi zake, alijua kwamba alikuwa katika hatua ya mwisho ya kuvuta pumzi ya dunia hii, alitubu, Mungu amsamehe kwa yote aliyokuwa ameyatenda.
“Mtafute Sarafina umuombe msamaha!” aliisikia sauti ikizungumza moyoni mwake.
Hakujua mwanamke huyo alikuwa wapi, hakujua kama bado alikuwa akiendelea kukaa mitaani au wapi. Alimshirikisha mke wake juu ya jambo hilo, hakutaka kumficha, alimwambia ukweli juu ya kila kitu.
Ilipita miaka mingi nyuma lakini Gloria alikumbuka kila kitu. Moyo wake uliumia, haukuumia kwa sababu ya mwanamke mwingine bali uliumia kwa kuwa mwanamke mwenzake alifanyiwa jambo kama hilo, hakika alijiona kama yeye ndiye aliyefanyiwa.
“Namkumbuka. Ni miaka mingi imepita,” alisema Gloria.
“Ninaamini yeye ndiye chanzo cha kila kitu kilichotokea mke wangu! Nahitaji kumtafuta mwanamke huyu nimuombe msamaha,” alisema David huku akimwangalia mke wake.
Alidhamiria kwa moyo mmoja, siku iliyofuata, hakutaka kukaa hospitalini, wakaomba ruhusa kutoka, wakapewa na kuanza kumtafuta Sarafina. Kila alipokuwa akitembea, david hakutembea vizuri, alikuwa akichechemea na muda mwingi alihitaji kupumzika.
Kidonda kilimtafuta, kilimtesa, kilitoa usaha, kilinuka lakini hakutaka kuona akibaki hospitali, alitaka kumtafuta mwanamke huyo, amuone mtoto wake na kumlea lakini si kuona akifa pasipo kumuona mwanamke huyo.
Alimtafuta Sarafina kwa siku ishirini, alitembea sehemu kubwa na mkewe, mitaani lakini kote huku hakufanikiwa kumuona mwanamke huyo. Moyo wake uliuma, ulichoma, alijutia maisha yake, ni kweli alikuwa na pesa lakini amani ya moyo ilikuwa ni zaidi ya pesa alizokuwa nazo.
Itaendeea.