SEHEMU YA 60...
Hali haikubadilika, bado Sarafina alikuwa kimya pale chini alipokuwa amelala. Malaika akashtuka, akahisi kwamba kuna kitu kilikuwa kimetokea, akazidi kumwamsha mama yake lakini hakuamka, mbaya zaidi kila alipokuwa akimsukuma huku, alikwenda bila kubisha chochote kile.
Akashtuka, mapigo ya moyo yakaanza kumuenda mbio, akahisi kwamba mama yake alikuwa amekufa, machozi yakaanza kumtoka na kutiririka mashavuni mwake. Akaupeleka mkono wake katika upande wa moyo wa mama yake, haukuwa ukidunda, ulikuwa umetulia, hapo akawa na uhakika kwamba mama yake alikuwa amekuga.
Aliumia mno, machozi yaliyokuwa yakimtoka, yakaongezeka, akalia kwa kumuita mama yake, hakuamini kilichokuwa kimetokea, mwanamke ambaye kila siku alikuwa akimthamini, aliyekuwa akimpenda kwa mapenzi ya dhati, leo hii alikuwa naye kimwili lakini kiroho hakuwa naye.
“Mama! Mama! Mama amkaaaa…” alisema Malaika kwa sauti huku akimwamsha mama yake.
“Mama usiniache, mama amka uniangalie, mama nimekuja, mama nimekupikia, amka ule, amka mama yangu, naomba usife, mama usiniache, mama, mama, mama, mama yafumbue macho yako, mtoto wako nimerudi mama, naomba usiniache mama, nitaishi na nani? Nani atanipenda? Nani atanijali? Mama amka mama,” alisema
Malaika huku akiendelea kulia.
Sauti yake kali, kilio chake ndicho kikawaita watu wengine waliokuwa wakipita njia na kuingia humo ndani. Wakajua kwamba kulikuwa na tatizo, walipoingia, wakamkuta msichana huyo akimuamsha mama yake lakini hakuamka.
Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumtoa ndani na kumuweka nje huku mwanaume mwingine akimzuia kuingia ndani. Wanaume wale waliokuwa humo wakagundua kwamba mwanamke huyo alifariki dunia huku akinuka kuupita kawaida.
Walisikitika, hawakuamini kile walichokuwa wamekiona, kifuani mwa Sarafina, alikuwa ameoza, alitoa harufu kali hali ambayo wakati mwingine iliwafanya kuhisi kwamba mwanamke huyo alifariki muda mrefu na wakati huo alikuwa ameoza.
“Mbebeni tumpeleke hapo Amana,” alisema mwanaume mmoja na hivyo kumbeba.
Itaendelea.