sanje
JF-Expert Member
- May 12, 2018
- 458
- 340
Kila baada ya miaka mia.lazima janga kubwa litokee.kuna mtu aliniambia hii habari janaMungu hubariki jitihada za mwanadamu pale anapotumia akili, nguvu na afya aliyopewa na mwenyezi Mungu.
Huombi Mungu akupe unga, mchele, au sukari. Wala huombi Mungu akupe flagyl au panadol ila unamwomba Mungu abariki jitihada zako za kilimo au kazi yako ili uwe na uwezo wa kula na kuilisha familia yako.
Unaomba ili dawa unayotumia ikafanye kazi katika mwili wa mgonjwa au Mungu awaongoze matabibu katika kumtafutia mgonjwa wako tiba sahihi, huku wewe ukihangaika kutafuta hela ya kulipia matibabu. Kushindwa kumlipia mgonjwa wako wakati una akili, nguvu na afya njema, ni kushindwa kutimiza wajibu wako. Ni dhambi.
Paulo alikuwa akishona nguo ili kupata hela ya matumizi. Pamoja na miujiza yote Mungu aliyoitenda kwa kupitia Paulo lakini Paulo alifanya kazi ili apate kuishi.
Mungu alimwokoa Nuhu na gharika kwa kumtaka atengeneze mashua. Nuhu aliokolewa na Mungu kwa kufanya kazi.
Mtoto Musa aliokolewa kwa kupitia Mama yake ambaye alitoroka naye. Akamtengenezea kikapu, akamhifadhi kwenye mto ambako binti ya Farao alizoea kwenda. Mama yake Musa ilibidi afanye kazi ili kupokea uokoaji wa Mungu.
Herode alipoamru watoto wote wa kiume wauawe, Mungu alimwambia Yusuf aondoke na Mariam kwenda Misri ili mtoto asiuawe. Mariam na Yusuf walifanya kazi ili kumwokoa mtoto Yesu.
Katika kuwaokoa Waisrael waliokuwa wakiuawa na Goliati, Daud alitengeneza kombeo alilolitumia kurushia jiwe. Na jiwe hilo Mungu akalipatia nguvu, na hata kumwua Goliati. Daud alifanya kazi ili kuwaokoa wana wa Israel.
Wakati mbalimbali Waisrael walipoonewa na maadui zao, waliandaa jeshi lao. Walienda mstari wa mbele. Walipigana, huku makuhani wakiomba. Mungu alibariki jitihada zao, hata wakaweza kushinda vita. Walifanya kazi.
Bikira Maria, alipewa nafasi ya kuwa mbarikiwa kuliko wanawake wote. Na baraka hiyo aliipata baada ya kukubali kubeba mimba, kutembea nayo kwa miguu umbali mrefu mpaka Betlehem, na kwenda kujifungulia kwenye zizi la wanyama. Hakushtukia mtoto yupo mkononi. Alifanya kazi. Alitumia akili pia.
Mungu wetu hutafuta mahali pa kuweka baraka na neema katika jitihada mbalimbali tunazozifanya. Kama hatujapatengeneza mahali pa Mungu kushushia baraka, neema na ulinzi wake, kamwe hatutapata baraka na wala hutapokea neema wala ulinzi wake.
Kutotimiza wajibu wako ni dhambi.
Kama wewe ni kiongozi mkuu wa nchi, wajibu wako mkuu ni upi katika kipindi hiki cha janga la Covid 19? Usipotimiza wajibu huo, unatenda dhambi.
Kama wewe ni kiongozi wa kiimani, wajibu wako kwa wakati huu ni upi? Usipoutimiza wajibu huo ni dhambi.
Kama wewe ni tabibu, wajibu wako mkuu wakati huu ni upi? Usipoutimiza wajibu huo, umetenda dhambi.
Kama wewe ni mfanyabiashara, mkulima, mkuu wa idara, mkuu wa majeshi, Polisi, n.k; wajibu wako ni upi? Usipoutimiza, hutapokea baraka wala ulinzi au neema za Mungu.
Mimi kama mwananchi wa kawaida, mwanataluma, mfanyakazi wa kawaida, mpiga debe wa daladala, mmiliki wa biashara mbalimbali, wajibu wangu ni upi? Usipoutimiza huwezi kupata ulinzi, kupokea neema zake wala baraka zake.
Kila mmoja ana wajibu wake. Ndiyo maana ya viungo ni vingi lakini mwili ni mmoja.
Mkuu wa nchi asifanye kazi ya unabii au ukuhani. Mkuu wa mkoa asijifanye mhubiri au mwombaji, daktari asijifanye kuhani. Kila mmoja atimize wajibu wake.
Tatizo letu kwa sasa, kwa kushindwa kutimiza wajibu wetu, kila mmoja anataka awe kuhani, nabii au mhubiri.
Kila mmoja aende kwenye wajibu wake. Maana Mungu atampima kila mmoja kwa wajibu aliomwekea.
Kusali na kuomba wakati wote ni jambo muhimu lakini tunaomba kitu gani?
Tunaomba ili siku moja tukiamka tuone ugonjwa haupo? Mbona haikuwa hivyo kwa ugonjwa wa plague (1720), kipindupindu (1820), Spannish Flu (1920), kifua kikuu, au ndui iliyoua zaidi ya watu 300m.
Sisi tunamwomba Muumba wetu abariki jitihada ambazo kila mmoja anazifanya kupambana na ugonjwa huu kama vike-
Mungu awaongoze wanasayansi wafanikiwe kupata chanjo ili ugonjwa utokomezwe kama ilivyotokomezwa ndui;
Mungu awaongoze wanaofanya tafiti kuujua ugonjwa huu vizuri, wapanuliwe ufahamu ili tujue kuenezwa kwake, kujikinga kwake, na tiba sahihi;
Mungu awajalie neema ya upendo wa kweli wanaowahudumia wagonjwa wetu ili waishi katika upendo na faraja mioyoni mwao wanapowahudumia wagonjwa wetu;
Mungu awajalie ufahamu wale wenye nafasi yoyote ya kusaidia, waongozwe kwenye utayari na kujua njia sahihi za kusaidia.
Mungu hashushi ulinzi na neema kwa watu wajinga. Ndiyo maana anasema, watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa. Mungu wetu hujivunia watu werevu, wenye bidii na wasiokata tamaa.