Warioba ajitosa kumtetea Nape
2008-09-11 10:51:46
Na Simon Mhina
Baada ya mawaziri wakuu wawili wastaafu kujitokeza kumtetea mwanasiasa chipukizi, Nape Nnauye, dhidi ya adhabu ya kufukuzwa uanachama wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Jaji Joseph Warioba naye amejitosa kumtetea kijana huyo.
Warioba sasa anaungana na mawaziri wakuu wenzake, Clepa Msuya na Frederick Sumaye ambao wameelezea kushtushwa kwao na adhabu iliyotolewa na Baraza Kuu la Umoja huo dhidi ya Nape.
Baraza Kuu, Jumapili iliyopita lilimfukuza uanachama Nape kwa madai ya kuvunja kanuni za UVCCM. Pia lilipendekeza kwa Kamati Kuu ya chama hicho kumvua mwanasiasa huyo machachari nyadhifa zake zote ndani ya CCM.
Mbali ya kuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM, Nape pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho. Pia ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje ofisi ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba.
Warioba ambaye pia alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais chini ya utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi, alisema kama CCM ya siku hizi ukisema ukweli unafukuzwa kama Nape, basi kuna siku naye atafukuzwa, lakini akasisitiza hatishiki.
Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jana, kiongozi huyo anayeheshimika nchini, alisema haoni sababu za Nape kufukuzwa kwa kutoa maoni yake, bila kujali ni maoni gani.
``Unauliza kwamba wanaosema ukweli ndani ya CCM wamewashiwa indiketa? Ni kweli pengine kuna watu wenye lengo hilo, lakini hilo mimi haliniogopeshi kabisa.
Kusema ukweli ndio tabia anayotakiwa awe nayo mwana-CCM. Kiapo chetu cha uanachama kipo wazi kwamba nitasema kweli daima, fitina kwangu ni mwiko,`` alisema.
Jaji Warioba alisema hana haja ya kuingia kwa undani juu ya madai ya Nape yaliyosababisha afukuzwe UVCCM, lakini anachojua ni kwamba taratibu na kanuni za haki za UVCCM zimekiukwa.
Alisema japokuwa yeye ni kijana wa zamani, haamini kwamba kanuni za sasa za UVCCM zinaweza kuruhusu kuvunja demokrasia.
Hata hivyo, alisema anasubiri maamuzi ya vikao vya Kamati Kuu na NEC ili aweze kusema yaliyoko moyoni mwake.
``Ninaamini watatengua uamuzi huo wa ajabu. Wakitoa maamuzi ambayo yanaunga mkono, hapo sasa mnitafute ili nitoe na mimi yaliyo moyoni mwangu. Lakini ngoja kwanza tuwasikilize,`` alisema.
Vilevile, alisema licha ya kupigwa na butwaa aliposikia uamuzi huo, hakuamini macho yake, kwamba uamuzi huo umechukuliwa na jumuiya ya CCM anayoijua yeye.
Jaji Warioba alihoji ni kwa vipi wapinzani wanaoisema vibaya CCM na kuitukana mchana kweupe, wakitangaza kurejea CCM wanapokelewa kwa mbwembwe na kupewa vyeo, lakini waliopo kwenye chama hicho siku zote wakikikosoa chama, wanaonekana wabaya hata kufukuzwa?
``Mtu anakitukana CCM na kukisema vibaya kila siku. Akirudi anatukuzwa na kupewa vyeo. Lakini mwana-CCM akisema yale yale aliyokuwa anasema mpinzani (kama Nape) anafakuzwa, hii maana yake nini?`` Alihoji na kuongeza: ``Sasa kizuri ni kipi, Nape anayesema kwa nia ya kukikosoa na kukisaidia chama chake, au wapinzani wanaosema kwa lengo la kukibomoa CCM?.``
Warioba alisema suala la kumfukuza Nape halikuwa la kidemokrasia na limelenga kuwanufaisha watu wachache kwa lengo la kukiharibia sifa Chama. ``Hii ni aibu kubwa na fedheha kwa chama chetu,`` alisema.
Alisema hata ukiyaweka hayo mambo mawili kwenye mzani wa kawaida, yaani Nape kutoa madai ya ufisadi kwenye mradi wa Jengo la Vijana na Baraza Kuu la UVCCM kumfukuza, utakuta kitendo cha kumfukuza, ndicho kimeharibu sifa ya chama kuliko madai aliyotoa.
``Nimeshangaa kidogo, hivi kati ya Nape na waliomfukuza nani kaharibu sifa ya chama kinachowataka watu wake waseme kweli daima na fitina kwao iwe mwiko?`` Alihoji.
Warioba ni Waziri Mkuu mstaafu watatu kutoa kauli za kupinga hatua ya Nape kutimuliwa UVCCM.
Wa kwanza kutoa maoni yake ni Cleopa David Msuya ambaye alisema mazingira ya kumfukuza kijana huyo yalitawaliwa na jazba.
Alisema adhabu hiyo ni kubwa kwa Nape hata kama kweli alikosea.
Mwingine aliyejitokeza kutoa maoni yake juzi ni Frederick Sumaye ambaye alisema binafsi amesikitishwa na hatua hiyo na amekaririwa akisema atatoa dukuduku lake kwenye vikao vya CCM.
Sumaye alienda mbali zaidi na kusema: ``Kitendo cha kumfukuza Nape aliyekuwa mgombea wa uenyekiti wa taifa wa UVCCM, bila shaka ni njama zilizopangwa na maadui wake wa kisiasa, kwa lengo la kummaliza.``
Chanzo cha Nape kukumbwa na masahibu ya sasa ni hatua yake ya kukosoa mkataba wa ujenzi wa jengo jipya la UVCCM ambao alisema hauna maslahi ya umoja huo wala chama.
Alimlaumu Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la UVCCM, Edward Lowassa, kuwa ndiye aliyeshiriki kusaini mkataba huo ambao haukupitishwa na Baraza Kuu la UVCCM.
Nape alimtaka Lowassa kujiuzulu wadhifa huo kwa kuwa alikuwa ameuingiza umoja huo kwenye mkataba tata.
Kauli ya Nape aliitoa siku ametangaza nia yake ya kuwania uenyekiti wa UVCCM taifa, nafasi ambayo alipewa alama E katika mchakato wa kupitisha majina.
SOURCE: Nipashe