Sakata la Nape: Kila mmoja CCM anasema lake
Na Michael Uledi, Dodoma
KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) amesema alitangaza kuwa mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Nape Nnauye, kuwa hawezi kukata rufaa "mbinguni na duniani" kwa ubabe.
Wakati akisema hayo, viongozi wa chama hicho wamezidi kutoa taarifa zinazopingana kuhusu hatua ya kumvua Nape uanachama wa UV-CCM, huku mwenyekiti wa jumuiya hiyo ya vijana ya chama tawala akilazimika kutoa taarifa kufafanua jinsi suala lake lilivyoshughulikiwa katika Baraza Kuu la vijana na hatimaye Halmashauri Kuu ya CCM.
Baada ya Baraza Kuu la UV-CCM kutangaza kumvua Nape uanachama na kupendekeza mtoto huyo wa mwanasiasa wa zamani wa CCM, Moses Nnauye avuliwe nyadhifa zake zote kwenye chama hicho tawala, Makamba, akiongea na waandishi kwa nyakati tofauti alisema Nape "hawezi kukata rufaa mbinguni na duniani".
Lakini mwenyekiti wake wa CCM, Rais Jakaya Kikwete alibatilisha kauli hiyo na kusema Nape, ambaye anagombea uenyekiti wa UV-CCM, anayo haki ya kukata rufaa ili kupigania haki yake na kwamba CCM inamtambua kama mwanachama wake na nyadhifa zake zote anazoshikilia kwenye chama hicho.
Akizungumza na Mwananchi jana, Makamba alionekana kutotaka kuzungumzia suala hilo alipolizungumzia kwa kifupi, akirejea maneno ya Rais Kikwete.
Makamba alisema: "Nape anayo haki kukata rufaa kupinga maamuzi ya Baraza Kuu kwa kuzingatia kanuni na taratibu na katika hali iliyopo anaendelea kuwa mtumishi wa chama katika idara ya Mambo ya Nje," alisema Makamba kabla ya kujibu kwa kifupi swali la mwandishi aliyetaka kujua sababu za kusema kijana huyo hawezi kukata rufaa mbinguni na duniani.
"Ilikuwa ni ubabe," alisema Makamba akizungumzia kauli hiyo iliyosababisha kizaazaa miongoni wapenda demokrasia.
Wakati Makamba akisema hayo, mkurugenzi wa uchaguzi wa UV-CCM, Francis Isaack alikaririwa jana akisema kuwa hata kama Nape atakata rufaa, hataweza kujumuishwa kwenye mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa CCM kwa kuwa wagombea ni lazima wawe wanachama wa umoja huo wakati Nape amevuliwa uanachama.
Isaack alisema mchakato wa uchaguzi utakuwa umefika mbali wakati rufaa ya Nape, ambaye ameripotiwa kupewa alama E na vyombo vya juu vya UV-CCM kumaanisha kuwa hafai kwa kiongozi, itakapotolewa maamuzi iwapo kijana huyo atakata rufaa na hivyo hatarejeshwa kwenye mchakato huo
Lakini jana, naibu katibu mkuu wa CCM Zanzibar, Saleh Radhaman Ferouz aliliambia gazeti hili kuwa UV-CCM haina mamlaka kukwamisha fomu ya mgombea kwa sababu yoyote yule katikati ya mchakato wa uchaguzi, anaripoti Kizito Noya.
Jana Ferouz alisema: "Nape hawezi kuondolewa katika mchakato wa uchaguzi huo na UV-CCM kwa kuwa jumuiya hiyo sio yenye maamuzi ya mwisho juu ya wagombea.
"Hatma ya Nape katika kinyang'anyiro cha uchaguzi kilichokwishaanza, itatolewa na NEC ambayo ndio kikao cha mwisho katika mchakato wowote wa uchaguzi ndani ya chama hicho na jumuiya zake na sio UV-CCM.
"UV-CCM haiwezi kuitupa fomu ya mgombea aliyekwishaingia kwenye mchakato wa uchaguzi kwa sababu yoyote ile, kwani mwenye mamlaka ya mwisho ni NEC."
Alisema Nape ataendelea kujadiliwa katika mchakato huo wote hadi NEC na hata alama anazowekewa katika vikao vya awali vya UV-CCM hazitoshi kumwondoa kwenye uchaguzi huo.
"Sio alama E tu, hata akipewa alama Z, bado haitoshi kumwondoa kwenye kinyang'anyiro. Jina lake litapita katika ngazi zote za uchaguzi hadi NEC, ambayo ndio yenye uamuzi wa mwisho," alisema.
Nape aliiambia Mwananchi juzi kuwa bado anatafakari adhabu hiyo ya Baraza Kuu kabla ya kuamua kukata rufaa kwa kuwa bado hajapewa rasmi barua ya kuvuliwa kwake uanachama.
Naye Emmanuel Nchimbi, mwenyekiti wa UV-CCM, ambaye alimshinda Nape katika uchaguzi uliopita, jana alitoa taarifa kwa vyombo vya habari akisema Nape anayo haki ya kukata rufaa na kwamba alisema uongo kuwa mkataba wa uwekezaji wa jengo la makao makuu ya umoja huo haukujadiliwa na vikao halali ndio maana alitimuliwa.
"Baraza Kuu liliridhika kuwa vikao vyote vya UV-CCM vinavyohusika na mchakato huo vilihusika kikamilifu, ikiwemo Baraza Kuu la tarehe 4/8/2007 na kikao kilichopitisha muhtasari wa Baraza Kuu cha tarehe 9/2/2008 ambacho Nape alishiriki," ameeleza Nchimbi katika taarifa yake.
Alisema kuwa Nape alionekana kwenye televisheni akitoa tuhuma hizo kuwa hakukuwa na vikao halali vilivyopitisha mkataba huo, wajumbe wa Baraza Kuu waliridhika kuwa aliwadanganya kwa kukana maneno hayo.
Hata hivyo, Nchimbi anaonyesha katika maelezo yake kuwa uamuzi wa Baraza Kuu ulikuwa mkubwa kuliko mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya Utekelezaji ya UV-CCM, ambayo ilitaka Nape asimamishwe kushiriki vikao vya umoja huo na CCM imchukulie hatua za kinidhamu kwa mujibu wa taratibu zake. Baraza hilo lilimvua uanachama badala ya kuzingatia mapendekezo hayo.
Kuhusu hatima ya mtoto huyo wa mwanasiasa wa zamani wa CCM, Marehemu Moses Nnauye, Nchimbi alisema Nape anayo haki ya kukata rufaa kwa mujibu wa Ibara ya 89 (e) ya kanuni za UV-CCM.
"Kwa mujibu wa ibara hiyo, suala la uanachama, mamlaka yake ya mwisho ni Baraza Kuu la UV-CCM," anasema Nchimbi katika taarifa hiyo, akipingana na Ferouz ambaye kwake Nape anaweza kugombea uenyekiti iwapo atapitishwa na NEC, licha ya kwamba mamlaka ya mwisho ya suala la uanachama liko Baraza Kuu.
Nchimbi alisema mapendekezo ya kumvua Nape nyadhifa zake zote ndani ya CCM yameshawasilishwa kwa katibu mkuu wa chama hicho tawala na kuongeza: "Uamuzi wa chama katika suala hilo utakuwa wa mwisho."
Source: Mwananchi