Kiyama cha Nape CCM leo
Na John Daniel, Dodoma
KAMATI Kuu ya CCM, inayokutana leo mjini hapa, inakabiliwa na mtihani wa kukubali au kukataa mapendekezo ya Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama hicho (UVCCM) ya kumvua madaraka yote, Bw. Nape Nnauye, kwa kilichoelezwa kuwa ni kuvunja kanuni za Umoja huo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa kikao hicho chenye nguvu na kinachotoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama (NEC), kitachofanyika mijini hapa keshokutwa, kuna mgawanyiko huku baadhi yao wakionesha wasiwasi wao kama Bw. Nape ametendewa haki au amehukumiwa kwa sababu za ugomvi kati yake na viongozi wa UVCCM na wadhamini wake.
"Nafikiri bado kuna maswali mengi ya kujiuliza kuhusu huyo Bwana (Nape), inawezekana kulikuwa na shinikizo kubwa kutoka kwa hao wakubwa wake na wadhamini, unajua wana nguvu na ushawishi mkubwa, sasa sijui wajumbe wa CC na NEC watamua vipi," alisema moja wa wajumbe wa Halmashauri Kuu.
Kanuni kwanza
Hata hivyo baadhi ya wana CCM waandamizi waliipongeza hatua ya Baraza la UVCCM dhidi ya Nnauye, wakisema imezingatia kanuni za msingi za Jumuiya hiyo na hivyo kilichotakiwa ni kuzifuata na kuchukua hatua.
"Watu wanaweza kusema mengi kuhusiana na hatua hii, lakini ieleweke kuwa siasa za siku hizi nchini zinaelekea katika watu kutafuta umaarufu na hivyo kujikuta wakivunja kanuni walizokubaliana, lakini wakibanwa huanza kulia na kutafuta visingizio vya kuonewa," alisema kiongozi wa CCM ambaye hakutaka kutajwa jina.
Alisema kimsingi CCM inakubali kukosolewa na kujikosoa, lakini hata hivyo ina kanuni zake na mahali pake pa kutolea ushauri au malalamiko au kukosoa na si popote kama ilivyofanywa na Bw. Nape.
Alisema Bw. Nnauye kiumri alijua kabisa asingestahili kugombea nafasi ya uenyekiti wa UVCCM kwa kuzingatia umri wake, kwani angefikisha miaka 35 akiwa bado mwanachama wa UVCCM wakati anajua kanuni hazimruhusu.
"Sasa alipoona hata yeye kwamba hawezi kugombea, akatafuta upenyo wa kutafuta umaarufu ndipo akachukua fomu kugombea na kuanza kutafuta kinga nje ya kishabiki na kutoa kauli za kupotosha na hata kutukana viongozi, sasa amebanwa analalamika, asubiri uamuzi wa vikao vya juu," alisema.
Uchunguzi uliofanywa na Majira mjini hapa ulionesha kwamba suala la kuondolewa kwa Bw. Nape kumeleta mawazo tofauti huku baadhi yao, wakidai kuwa kumetokana na yeye mwenyewe kuweka mawazo yake mapema kabla ya kufikia hatua ya kuongoza UVCCM, jambo lililosababisha watu kujua mwelekeo wake hivyo kufanya maadui zake kupata mwanya wa kummaliza.
Baadhi yao walidai kwamba licha ya kuondolewa kwake katika Umoja huo na kinyang'anyiro cha uenyekiti, lakini bado suala la uchunguzi kuhusu mradi wa UVCCM katika kiwanja namba 1081/2 Dar es Salaam ni muhimu hasa katika kipengele cha uwekezaji na muda wa wawekezaji.
Pamoja na mambo mengine CC katika kikao chake cha leo itajadili na kumteua rasmi mgombea wa CCM katika Jimbo la Tarime iliyoachwa wazi na marehemu Chacha Wangwe.
Habari kutoka ndani ya CCM, ilieleza kwamba jina la mgombea huyo litatangazwa rasmi Septemba 13 mwaka huu, siku mbili baada ya kumalizika kwa kikao cha NEC mjini hapa.
Pia CC itajadili majina yaliyopitishwa na UVCCM kuwania uenyekiti wa umoja huo baada ya Bw. Nnauye kuenguliwa rasmi juzi kwa kuvunja kanuni ya 17(c) na Ibara ya 18(b) ya kanuni ya Umoja huo kwa kuzungumza nje ya vikao halali.
Aapa kuendeleza mapambano
Siku moja baada ya Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kutangaza kumfuta uanachama, Bw. Nape amesisitiza kuwa ataendelea kusimama kidete kutetea anachokiamini kuhusiana na ujenzi wa mradi wa Jumuiya hiyo, wanaripoti Reuben Kagaruki na Said Mwishehe.
Bw. Nape ambaye alikuwa akigombea uenyekiti wa UVCCM kabla ya kufutwa uanachama, alisisitiza kuwa kauli zinazotolewa na viongozi wa umoja huo, kuwa alikana kutoa taarifa hizo, si za kweli bali wanataka kupotosha ukweli.
Akizungumza na gazeti ili kwa simu Dar es Salaam jana, Bw. Nape alisema ataendelea kusimama na kutetea kile alichokisema kuhusiana na ujenzi wa mradi huo.
Alisisitiza kuwa amesikitishwa na kauli iliyotolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Bw. Francis Isack, kuwa alipoulizwa kama alitoa taarifa zilikuwa zikiripotiwa na vyombo vya habari, alikanusha.
Jana vyombo vya habari vilimkariri Bw. Isack akisema Bw. Nape alipoulizwa kuhusu taarifa zilizokuwa zikiandikwa kwenye vyombo vya habari, alikanusha kuhusika nazo na kusema magazeti yalilenga kufanya biashara.
Alisema mali za UVCCM zinasimamiwa na Bodi ya Wadhamini hivyo kama kuna matatizo wa kuulizwa ni wao (Bodi).
Alipoulizwa amepokeaje uamuzi wa UVCCM kumvua uanachama, Bw. Nape alisema Baraza Kuu si kikao cha mwisho ndani ya CCM, hivyo ana matumaini vikao vingine vitatoa uamuzi utakaomtendea haki.
Bw. Nape alitaja vikao ambavyo vinaweza kubatilisha uamuzi wa UVCCM kuwa ni Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), Kamati Kuu (CC), Kamati ya Maadili na Sekretarieti.
"Bado nina imani na vikao hivi, wao kama vijana wana uhuru wa kutoa uamuzi wao," alisisitiza. Alipoulizwa kama ataendelea kubaki ndani ya CCM iwapo uamuzi utaendelea kama ulivyo, alijibu kuwa kwa sasa ni mapema mno kutangaza hatua atakazochukua.
"Kwa sasa bado vikao vinaendelea, vikishamalizika nitasema ni nini kitafuata," alisema na kuwataka wafuasi wake kuendelea kumuunga mkono, kwani siasa ni lazima mtu avuke milima na mabonde.
Bw. Nape alipoulizwa kama kufutwa kwake uanachama kunatokana na yeye kuwa tishio kwenye kinyang'anyiro cha kuwania nafasi ya uenyekiti, alisema hawezi kujua kilichomo ndani ya moyo wa kila mmoja.
Alisema hadi jana alikuwa hajapewa taarifa za kuvuliwa uanachama kwa maandishi. Alipoulizwa kama alipewa nafasi ya kusikilizwa, Bw. Nape alijibu kuwa juzi aliitwa na Kamati ya Utekelezaji ya UVCCM na kueleza kile alichokisema na hakukuwa na maswali.
Hivi karibuni, Bw. Nape alikaririwa na vyombo vya habari akiwatuhumu Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la UVCCM, Bw. Edward Lowassa, mbunge wa Monduli na aliyekuwa Waziri Mkuu kuwa anahusika na mkataba tata wa mradi wa ujenzi wa jengo la makao makuu ya umoja huo.
Wengine waliokuwa wametajwa katika tuhuma hizo ni Mwenyekiti wa UVCCM, Dkt.Emmanuel Nchimbi na aliyekuwa Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Bw. Amos Makalla, ambaye kwa sasa ni Mweka Hazina wa CCM.
Kutokana na kauli hizo, Baraza Kuu la UVCCM lililokutana juzi liliamua kumvua uanachama kwa kile kinachodaiwa alivunja kanuni ya 17(C) ya umoja huo kwa kutoa taarifa za uongo.
Katika hatua nyingine, uamuzi uliotolewa na UVCCM dhidi ya Bw. Nape umeonekana kuwaudhi baadhi ya viongozi wa CCM na kueleza kuwa umoja huo umekurupuka kwa kuchukua uamuzi wa kumfuta uanachama na kupendekeza avuliwe madaraka aliyonayo chini ya mwavuli wa CCM.
Kiongozi wa CCM aliyezungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa jina, alisema jana kuwa uamuzi uliotolewa na umoja huo unaweza kutafsiriwa vingine na wabaya wa chama hicho.
"Wangeweza kusubiri kwa kuheshimu mawazo yake, leo hii mtu anagombea ndani ya kipindi hicho hicho anaadhibiwa kwa kufutwa uanachama, unadhani hiyo inaleta picha gani?," alihoji
Aliongeza kuwa kauli za Bw. Nape ziligusa chama chote na si UVCCM tu, hivyo walipaswa kusubiri ili chama kitoe uamuzi wake.
Aliongeza kusema kuwa "Mbona wabunge wanawasema mawaziri na wengine wanafikia hatua ya kujiuzulu nyadhifa zao hawachukuliwi hatua za kinidhamu na chama?," alihoji kiongozi huyo na kuongeza kuwa iweje adhabu hizo aanze kupewa Bw. Nape.
Alisema kitendo hicho kinalenga kuonesha kuwa Bw. Nape amefanya kosa kubwa ndani ya CCM. Kiongozi huyo alisisitiza kuwa uamuzi wa UVCCM kumfuta uanachama Bw. Nape, unalenga kufananisha chama hicho na CHADEMA ambacho kilimsimamisha uongozi aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wake marehemu Chacha Wangwe, baada ya kuhoji mapato na matumizi ya fedha za ruzuku.
Kiongozi huyo alisisitiza kuwa umoja huo umekurupuka na unataka kuwapa nafasi wapinzani kukisema vibaya chama hicho.
Kwa upande wao, viongozi wa vyama vya upinzani waliozungumza na gazeti hili, walisema uamuzi wa kumfuta uanachama UVCCM Bw. Nape, unalenga kuonesha jinsi chama hicho kisivyopenda kukosolewa.
Wapinzani wachekelea
Mwenyekiti wa TLP, Bw. Augustino Mrema, alisema CCM imemtoa kafara kijana huyo. "Ufisadi ndani ya CCM umeota mizizi, iweje leo hii wamtoe kafara kijana mdogo kama Nape?," alihoji.
Alisema haiwezekani waliohusika kwenye 'ujambazi' wa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) iliyokuwa chini ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wapewe muda wa kulipa fedha walizoiba huku wanaosimama na kutaka mabadiliko ndani ya CCM akifukuzwa.
Alisema inashangaza kuona mtu anayetaka mabadiliko ndani ya CCM akifukuzwa na kuwataka wabunge wa CCM wanaokemea maovu ndani ya Serikali ya chama hicho kuwa makini kwani uamuzi uliotolewa dhidi ya Bw. Nape ni salamu kwao.
"Hii ni message (ujumbe) imetumwa kwa wabunge wa CCM watambue kuwa mtu anayetikisa uhai wa CCM ataishia pabaya," alisema Bw. Mrema na kumtaka Bw. Nape kuhama chama hicho kwani CCM si baba wala mama yake.
"Nape ni kijana mdogo asidhani kuwa akihama CCM ndio mwisho wa maisha yake," alisisiza Bw. Mrema.
Naye Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Wilbroad Slaa, alisema alishawahi kusoma magazeti yakimnukuu Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Yusuf Makamba, akiwataka vijana waache kuchafua chama kwa kusema hadharani.
Alisema kauli hiyo ilikuwa inalenga kuficha uchafu ndani ya chama hicho. "Wanachofanya ni kukigeuza chama hicho cha mafisadi kwa kuwafukuza wanaosema ukweli," alisema.
Alipoulizwa kama chama hicho kitakuwa tayari kumpokea Bw. Nape iwapo atatangaza uamuzi huo alijibu; "Mtu akitoka kwenye Ukristo na kwenda kwa Waislamu huwa anapokewa".