Nape mambo mazito
na Martin Malera
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), leo kinaanza kuwachuja vijana wanaoomba kuteuliwa kuwania nafasi za uongozi wa juu ndani ya Jumuiya ya Umoja wa Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), huku mwombaji anayegusa hisia za wengi kwa mitazamo tofauti, Nape Nnauye, akilazimika kukwepa vihunzi saba vya vikao vya mchujo kutokana na utata wa umri wake.
Ingawa vihunzi hivyo saba vinawahusu wagombea wote, lakini jina la Nape huenda likaumiza vichwa vya wajumbe wa vikao hivyo, kwa sababu kubwa mbili.
Mosi, ni kutokana na utata wa umri wake ambao hadi sasa ana umri wa miaka 30, lakini wakati uchaguzi huo utakapofanyika Desemba mwaka huu, atakuwa na miaka 31, umri ambao kimsingi unamwondolea sifa ya kuwania nafasi hiyo.
Sababu ya pili ni hatua yake ya kulipua bomu la ufisadi linalohusu mradi wa ujenzi wa jengo la makao makuu ya umoja huo, jijini Dar es Salaam, huku akimtaka Mwenyekiti wa UVCCM anayemaliza muda wake, Dk. Emmanuel Nchimbi, Katibu Mkuu, Francis Isaac na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Edward Lowassa, kuwajibika.
Habari kutoka ndani ya CCM ambazo Tanzania Daima imezipata, zinasema Sekretarieti ya UVCCM, ndiyo itakayoanza kufungua pazia la mchujo huo katika kikao chake kinachotarajiwa kufanyika leo, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Katiba ya UVCCM, mwenyekiti wa kikao hicho ni Kaimu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Francis Isaac, ambaye Nape amemtaja kama mmoja wa viongozi wanaopaswa kuwajibika kutokana na kashfa ya ufisadi ya mradi huo wa ujenzi. Isaac pia ni Mkurugenzi wa uchaguzi huo.
Isaac, jana aliithibitisha Tanzania Daima kuwapo kwa kikao hicho na kuongeza kuwa kitafuatiwa na kikao kingine cha Kamati ya Utekelezaji ya UVCCM, ambacho kitaongozwa na Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Dk. Nchimbi, ambaye Nape amemtaja kama mmoja wa wahusika wakubwa wa mradi huo unaodaiwa kuwa na harufu ya ufisadi na hauna masilahi kwa jumuiya hiyo.
Isaac alisema kikao hicho cha Kamati ya Utekelezaji, huenda kikafanyika mjini Dodoma au Dar es Salaam, na hadi sasa hakijapangiwa tarehe ya kufanyika hadi hapo watakapokutana na Nchimbi, ili kupanga tarehe ya kufanyika kwa kikao hicho nyeti.
Nchimbi aliyekuwa mpinzani mkubwa wa Nape katika uchaguzi uliopita, pia ataongoza kikao kingine cha Baraza Kuu la Umoja huo, ambacho Isaac alisema hakijapangiwa tarehe, lakini kitafanyika mjini Dodoma.
"Kikao cha Kamati ya Utekelezaji na cha Baraza Kuu la UVCCM, bado havijapangiwa tarehe, lakini vitafanyika hivi karibuni na vitafanyika Dodoma. Tunasubiri kukutana na mwenyekiti tujue vikao hivyo vinafanyika lini," alisema Isaac.
Nape ambaye ni mototo wa mwanasiasa mkongwe nchini, marehemu Moses Nnauye, atakutana na kihunzi kingine cha kikao cha sekretarieti ya CCM mjini Dodoma, kinachotarajiwa kufanyika Agosti 20, mwaka huu na kitaongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Yusuph Makamba.
Katika sakata la ufisadi la mradi huo, Makamba alilazimika kumwita Nape na kumsuta mbele ya vyombo vya habari, akielezea kukerwa na hatua ya mwanasiasa huyo machachari kutoa tuhuma hizo nzito dhidi ya viongozi wa CCM, wakati suala hilo limekabidhiwa kwenye vikao vya juu kwa maamuzi.
Katika mtiririko wa vikao hivyo vya mchujo, Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, ataongoza kikao kingine cha tano cha Kamati ya Maadili ya CCM, kitakachofanyika Agosti 21, mjini Dodoma.
Pia Kikwete ataongoza kikao cha Kamati Kuu (CC), kitakachofanyika Agosti 25 mjini Dodoma, na kikao cha mwisho na cha saba ni cha Halmashauri Kuu (NEC), ambacho pia kitakuwa chini ya Kikwete na kitafanyika mjini Dodoma Septemba 2 hadi 3, katika ukumbi wa White House.
"Katika vikao vyote vya mchujo, Nape anakuwa na ahueni kwenye vikao vitakavyoongozwa na rais na anategemea sana busara ya CC na NEC, lakini vingine vyote vinaongozwa na Nchimbi, Francis na Makamba, ambao amewagusa katika kashfa hiyo ya ufisadi. Hapo kweli atachomoka?" alihoji mmoja wa wajumbe wa Baraza Kuu la UVCCM ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.
Mbali ya Nape, waombaji wengine watakaopitia chekeche hilo ni Jerry Slaa, Zainab Kawawa, Hussein Mohammed Bashe, Hamad Masauni, Issa Haji Ussi na Benno Malisa, ambaye anapewa nafasi ya kuteuliwa, kwa madai ya kuwa kipenzi cha baadhi ya viongozi wa juu wa jumuiya hiyo na ndani ya CCM.
Wengine ni Anthony Mtaka, Said Mtanda, Haule Pangisa, Samuel Marero, Stephen Deya, Godfrey Mwankenja, David Manoti, Mussa Mnyeti, Edson Lubua, Mwamini Lusingu, Asmah Kalokola, Marco Zablon Allute, Harold Adamson, Suleiman Muhsein Haji, Adila Hilal Vuai, Ashura Ismail, Rashid Masalaka na Raha Ahamada.
Wanaowania uteuzi wa nafasi ya makamu mwenyekiti ni Happy Mahava, Raha Ahamada Ally, Riziki Pembe Juma, Michael Bundala, Rabia Hamid Shaka, Nuru Mohammed Ahamed na Twaha Ally Muhaji.
Katika hatua nyingine, waombaji 16 wa nafasi ya mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, wamemaliza kihunzi cha awali cha kikao cha sekretarieti ya mkoa, ambapo watoto wa vigogo, Said Ntimizi na Ben Samuel Sitta, wamepata alama nzuri, na sasa wanasubiri uamuzi wa vikao vya juu vya CCM.