Date::8/2/2008
Wagombea UVCCM wawekewa kitanzi cha umri
*Kinawalenga Mnauye Nape, Bhashe
*Mbinu ya kuchomeka wanawake yaiva
Na Mwandishi wetu
Mwananchi
BAADA ya wagombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi kukwepa kitanzi cha kura tatu mwaka 2005, safari hii Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC)ya chama hicho inadaiwa kuwaandalia vijana wa chama hicho zengwe la umri kama njia ya kuengua baadi ya wagombea, Mwananchi Jumapili imeelezwa.
Taarifa mbalimbali zilizofikia gazeti hili zinaeleza kwamba NEC iliamua kwamba kanuni ya wagombea wasiwe wamevuka umri wa miaka 30 itumike kwenye uchaguzi wa mwaka huu wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM).
Zengwe la umri ni kanuni iliyoingizwa kwenye taratibu za uchaguzi wa UVCCM mwaka 2003 wakati Mwenyekiti wa sasa, Dk Emmanuel Nchimbi, anawania nafasi hiyo kwa mara ya pili, ikilenga kumuengua, lakini busara ya Kamati Kuu ya CCM iliiweka pembeni kwa muda.
Kulingana na kanuni hiyo umri wa mwisho wa kugombea ni miaka 30 ili kiongozi husika asizidi miaka 35 akiwa madarakani umri ambao ni wa mwisho wa uanachma wa UVCCM.
Zengwe la umri safari hii linalekea kuwalenga baadhi ya wagombea machachari katika uchaguzi wa UVCCM, ambao ni pamoja na Nape Mnauye, na Hussein Bhashe ambao wamejitosa kuusaka uenyekiti.
Uchunguzi wa Mwananchi Jumapili, umebaini kwamba kama utaratibu wa kura tatu uliokuwa utumike kuamua nani atakuwa mgombea wa CCM kwenye NEC, ikionekana zaidi kumlenga Rais Jakaya Kikwete, wakati huo akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ni dhahiri baadhi ya wakubwa ndani ya chama hawafurahishwi na misimamo ya watu kama Nape na Bhashe.
Habari za ukahakika zanasema kwamba baada ya hoja ya umri wa miaka 30 kuahirishwa mwaka 2003, kabla ya kutumika ilipaswa kwanza kupata baraka za vikao vya UVCCM kunzia kwenye sekretariati, Kamati ya Utekelezaji na mwishowe kwenye Baraza Kuu. Hatua hizi hazikufuatwa ila ni NEC iliagiza tu kuanza kutumika.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa UVCCM ambaye pia ni Kaimu Katibu Mkuu wa umoja huo, Francis Isaac, aliambia Mwananchi Jumapili kwamba kanuni ya umri ilipitishwa na Kamati Kuu ya CCM miaka mitano ilyopita.
Isaac alisema haikuweza kutumika katika uchaguzi wa UVCCM uliopita kwa sababu wakati uamuzi unapitshwa wa kanuni hiyo tayari uchaguzi ngazi ya wilaya ulikwisha kufanyika na hivyo kuamuliwa ianze kutumike katika uchaguzi huu.
"Kwa mujibu wa kanuni hiyo mgombea anayefaa kuchukua fomu kwa ajili ya kugombea ni yule ambaye amezaliwa chini ya Januari mosi, 1978 kama atachaguliwa atamaliza muda wake wa uongozi akiwa na miaka 35," alisema na akaongeza:
"Kanuni hii imeacha majeruhi watu wengi, kuna vijana wazuri sana, tuliwapenda wachukue fomu lakini umri wao wa miaka 32 na 33 umewafanya waende kugombea uongozi kwenye Jumuiya ya Wazazi."
Isaac pia alisema kwamba mchakato wa kutungwa kwa kanuni hiyo ulifuata taratibu zote kuanzia kwenye sekreteriati, Baraza Kuu, Kamati Kuu ya CCM, NEC na baadaye mkutano mkuu wa CCM uliofanyika miaka mitano iliyopita.
Hata hivyo alipotakiwa kueleza ilikuwaje ikashindikana kutumika wakati huo kama ilikuwa imekwisha kutunga na ikalenga kwenye viongozi wa kitaifa tu wa UVCCM mwaka 2003, alisema wakati uamuzi unatolewa uchaguzi ngazi ya wilaya ulikuwa umekwisha kufanyika.
Nape aliyezaliwa Novemba 26, 1977, aliwasha moto ndani ya chama hicho siku amechukua fomu ya kuwania nafasi hiyo, baada ya kulipua bomu kwamba mkataba wa kujenga jengo jipya la UVCCM umegubikwa na ufisadi.
Mbali na Nape, Bhashe amekuwa majeruhi wa siasa za fitina ndani ya CCM, kwani katika uchaguzi wa wajumbe wa NEC ya CCM mwaka 2007 kura wala jina lake havikutokea baada ya kura kupigwa, hali iliyozua maswali mengi.
Bhashe ni mjumbe wa Baraza Kuu UVCCM mkoa wa Tabora na mjumbe wa Mkutano Mkuu UVCCM. Kama ilivyo kwa Nape, Bhashe naye anapigwa zengwe la umri akiwa amezaliwa Agosti 26, 1978.
Hoja ya umri ikiendelea kuandaliwa kama silaha ya kuwamaliza vijana hao wawili ili majina yao yasipitishwe, makundi kinzani ndani ya chama hicho yanazidi kujiimarisha na kuongeza mikakati ya kumalizana.
Habari zilizopatikana zinaeleza kuwa mvutano wa makundi haya yanayoongozwa na makanda wa siku nyingi wa chama hicho yanataka kila moja kuweka mgombea wake ili aweze kuibuka mwenyekiti wa umoja huo ambaye kwa nafasi yake ataingia katika vikoa vya juu ya vya chama, kikiwamo kikoa cha Kamati Kuu (CC) ambacho ni muhimu katika maamuzi ya chama.
Katika siasa hizi za makundi, Nape anaonekana kupaniwa zaidi hasa kutokana na uamuzi wake wa kushupalia kashfa ya mkataba wa ujenzi wa jengo la UVCCM unaodaiwa kuwa kufanywa kinyemela.
Baada ya Nauye kutoa tuhuma hizo, si tu Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba alikosa uvumilivu na kumshambulia kupitia vyombo vya habari, ila ndani kwa ndani kuna mikakati ya kutaka hata kumnyang'ana kadi Nape akidaiwa kwamba amekiuka maadili ya chama kwa kumshambulia Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa UVCCM, Edward Lowassa, anayedaiwa kusaini mkataba unaoelezwa kutokuwa na maslahi kwa chama.
Makamba pia alimtuhumu Nape kwamba amevunja taratibu za uongozi kwani kwa nafasi yake kama mjumbe wa NEC na kiongozi ndani ya UVCCM, alitakiwa kuzungumza mambo hayo kwenye vikao halali vya chama na si barabarani.
Ingawa zengwe hilo linajengwa juu ya umri, hoja pia imekuwa ikielezwa kwamba viongozi hao wawili wanaonekana kuwa wa msimamo mkali ambao watakataa kuwa daraja la watu waliozoea kuutumia umoja huo kwa maslahi binafsi ya kisiasa.
Kutokana na kuweka mikakati huo, kundi linalopingana na Nape na Hussein wanaamini kwamba karata yao inaweza kupita kama pia wakichomeka suala la jinsia, ili kuonekana kwamba wanajali nafasi za wanawake katika ngazi za juu za uongozi kwenye chama. UVCCM haijawahi kuwa na mwenyekiti mwanamke.
Lakini pia nafsi ya mgombea huyo kutoka visiwani hasa wakati huu wa mjadala tete wa hadhi ya Zanzibar, mgombea wa ngazi ya mwenyekiti akitoka huko ni mbinu ya kusaka kuungwa mkono zaidi.
Chanzo kimoja kutoka ndani ya CCM kinaeleza kuwa baada ya kubaini mbinu hiyo , kundi la Nape nalo limeamua kumchukua mgombea mwanamke kutoka Pemba ili kama suala la jinsia litaibuliwa basi anayeweza kukubalika zaidi ni wa Pemba ambako wanachama wa chama hicho wanaeleza kuwa wametengwa.
Baadhi ya wagombea wa kike waliochukua fomu kuwania nafasi hiyo kutoka Zanzibar ni Raha Ahmada Ali na Adila Hilal Vuai, wote kutoka Unguja na Ashura Ismail Abdallah kutoka Pemba.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Umoja huo, Francis Isaac aliiambia Mwananchi Jumapili vikoa vya kuanza kuwajadilia waliochukua fomu vitaanza kufanyika mwezi huu.
Alisema jumla ya wagombea 27 wamechukua fomu za kugombea nafasi hiyo, 18 kutoka Bara na 9 kutoka Zanzibar.
Uchaguzi wa viongozi wa UVCCM nafasi ya wilaya utafanyika Oktoba 25, mwaka huu na ule wa mkoa utafanyika Novemba 4, mwaka huu na kumalizia na wa taifa utakaofanyika Desemba 27, mwaka huu.