Jul 6, 2023
23
28
Imetimia idadi ya mikoa 19 Tanzania bara na mkoa mmoja Tanzania visiwani na wilaya zaidi ya 25 nilizotembelea hadi sasa. Wasalaam ndugu zangu.

Mwezi wa saba mwaka huu 2023 nilibahatika kutembelea mkoa wa Iringa. Ilikuwa ni safari kutembelea mikoa mitano tofauti ndani ya kanda mbili tofauti, kanda ya kati na kanda ya nyanda za juu kusini. Hapa nitaangazia niliyobahatika kujionea na kujifunza kutoka katika safari yangu kutembelea mkoa wa Iringa na baadhi ya wilaya zake.

Safari yangu kuelekea Iringa nilianzia Dodoma. Kutoka Dar es salaam hadi Dodoma mji mkuu wa Tanzania ilikuwa safari nzuri sana, nilifanya safari ya kwanza kuanzia hapo jijini Dar es salaam kupitia barabara kwa kutumia mabasi ya abiria hadi katikati ya Tanzania. Lengo lilikuwa ni kupata uzoefu wa kupita barabara iendayo Iringa kutokea Dodoma, niliambiwa njia hii ni nzuri na inavutia haswaa kutazama Mandhari pembezoni mwa barabara hii.

Nilifanikiwa kupata gari kutoka eneo moja maarufu kwa jina MAGOROFANI hapo Dodoma, nadhani kama sijakosea ni jina maana nilikuwa mgeni na ilikuwa mara yangu ya kwanza kufika eneo hilo. Ni majira ya jioni muda wa saa kumi na moja na nusu ndio nilipata kupanda gari ya abiria kutokea Mwanza. Japo sikupanga kufanya safari hiyo majira ya jioni lakini ilinibidi niondoke mapema jijini Dodoma ili kuweza kuokoa muda wa kutembelea vivutio vingi nilivyopanga kuvifikia ndani ya mkoa wa Iringa.

Njiani safari ilikuwa nzuri na gari kampuni ya Capricorn ilikuwa na mwendo mzuri na salama kabisa kwa abiria wake na watumiaji wengine wa barabara. Safari ilikuwa nzuri tulipita maeneo ya Mkonze, Mpunguzi, na kupitia Google map niliona eneo linaitwa Manzese😁 na jingine likiitwa Fufu, kiukweli nyakati jua likikaribia kutoweka nilibahatika kuona hali ya ujangwa jangwa inayopatikana maeneo yale.

Kuna baadhi ya maeneo ni kame sana kwa kweli, wakati tunakatiza bwawa la Mtera ilishakuwa giza na usiku umeingia rasmi, hivyo kwa uchache niliona eneo la daraja na baadhi ya miundombinu inayotumika kukamilishia uzalishaji wa umeme kwa kutumia maji. Eneo hili nililipenda sana, maana ni kati ya maeneo machache niliyotamani kuyaona hadi ikanifanya nipite njia hiyo.

Tulivuka salama na kuanza kupandisha vilima taratibu, hadi pale nilipoona eneo linaloitwa Nyang'oro kupitia simu yangu ya mkononi. Mwanzo niliona michoro ya kona kona nyingi kwenye ramani ya simu yangu na kisha kwa bahati mbaya sana mwendo mfupi mbele sikuweza tena kupata huduma ya mtandao kutokana na eneo hilo kutokuwa na mtandao wa uhakika. Kiukweli nili_enjoy sana maeneo hayo, fikilia kwa mara ya kwanza kukaa siti ya mbele ya gari tena nyakati za usiku na kuona barabara yenye kona kona nyingi mithili ya alama ya "S" na muonekano mzuri wa mlima Nyang'oro🙂 ulinifanya nione maisha ni ya thamani sana kama utafanya jambo ambalo moyo wako unalitamani zaidi.

Kutoka Nyang'oro tulisogea mbele zaidi na kufika eneo linaloitwa Ismani, nadhani ni eneo maarufu na watu wengi hapa wanalifahamu, kutoka Ismani gari yetu ilisimama Kihesa ambapo kwa msaada wa maelezo kutoka kwa abiria mwenzangu alinishauri nishukie hapo Kihesa kutokana na kuweza kupata huduma nafuu za malazi tofauti na kushukia mjini kati kabisa. Niliona ni wazo zuri na pia kwa kuwa niliona umbali kutoka Kihesa nitakaposhukia hadi kufikia kivutio cha kwanza nitachoanza kutembelea asubuhi yake ni karibu zaidi, basi niliafikia kushuka hapo. Aisee ile kushuka tu nikapokelewa na baridi kaliiiiii🥶🥶 almanusura nirudi ndani ya basi🙃.
Lakini nashukuru Mungu niliandaa koti nzito kwaajiri ya kukabiliana na hali ya baridi ambayo nilitegemea kabisa kukutana nayo huko.

Safari mpya ilianza sasa, kama kawaida kufumba na kufumbua nakuta bodaboda kama kumi hivi wameshanizunguka, ingekuwa kwa mji kama Dar es salaam ningezani ni majambazi maana sio kwa mikoti ile😃😀 ila jamaa ni waaminifu na wenye busala sana. Nilimchagua bodaboda mmoja na kumwomba anipeleke katika lodge moja isiyokuwa na bar wala kelele nyingi, pia isiwe mbali na barabara kuu na yenye ghalama nafuu. Bila hiyana akaniambia kalia sofa mzee!! Kwenye bodaboda baridi inapuliza haswaa, mwendo mfupi tu kama mita mia moja buku yangu ikawa imeshaliwa, yaani sehemu ya kutembea kwa miguu huku umefumba macho ikawa ndio nimeshafika hivyo😀😀.

Nilimshukuru na ukweli alinipeleka sehemu sahihi ambapo vigezo vyangu vyote nilivyovitaka vilikuwepo. Lodge ipo kimya sana, muhudumu wa kiume, na hadi naondoka majira ya asubuhi sikuweza kubahatika kuonana na mteja awaye yeyote hapo😎. Nilionyeshwa chumba changu juu mlangoni kikiwa na jina la Tembo, nikaweka begi langu moja dogo kisha nikarudi mapokezi na kuomba msaada wa kufika eneo la karibu lenye huduma ya vyakula na vinywaji.

Jamaa akanipa maelezo mafupi na muda mfupi baadae nilikuwa ndani ya bar moja kubwa na yenye mziki mkubwaaaa si mchezo. Kwa wale wakazi wa Dar es salaam na mikoa ya Pwani huko ambao hamjawahi kutembelea mikoa yenye baridi msidhani bar na pub za huku zipo waziwazi kama kule Buza, Mabibo sinza au hapo mtaani kwako. Aisee huku ni unaingia ndani ya mjengo, milango ya vioo ni kama unaingia club kwa huko Dar es salaam, hii yote inatokana na hali ya baridi inayokuwa imetawala muda wote huko nje.

(Nitaendelea hapa, muda ujao.)
Kuona zaidi mambo mengi kuhusu safari hii unaweza kutazama #All about Tanzania life kupitia Facebook/ All about Tanzania life.

png_20230717_184944_0000.png
 
Kiukweli nili_enjoy sana maeneo hayo, fikilia kwa mara ya kwanza kukaa siti ya mbele ya gari tena nyakati za usiku na kuona barabara yenye kona kona nyingi mithili ya alama ya "S" na muonekano mzuri wa mlima Nyang'oro ulinifanya nione maisha ni ya thamani sana kama utafanya jambo ambalo moyo wako unalitamani zaidi.

Aloo hii imenigusa sana asee, hongera mkuu uzi mzuri huu, binafsi hakuna kitu duniani nakihusudu kama kusafiri
 
IMG_20230707_210118_489-01.jpeg

Habari. Imenichukua muda mrefu kidogo kuweka hapa mwendelezo wangu wa safari kutembelea mikoa ya nyanda za juu kusini mwa Tanzania kwa sababu kadhaa zilizokuwa nje ya uwezo wangu.

Leo rasmi nimeanza mwendelezo wa masimulizi haya ya safari zangu huku nikiwa naandaa habari mpya kuhusu maeneo kadhaa niliyotembelea katika msimu wangu huu wa tano wa safari kuzunguka Tanzania. Juu nimeweka picha ya pili niliyopiga katika eneo la Gangilonga mkoani Iringa, binafsi huo ndio ulikuwa muonekano wangu katika siku ya kwanza na ya pili pale Iringa mjini na viunga vyake. Tunaendelea...... Usiku ule wa kwanza baada ya kupata sehemu ya kulala na kupata chakula katika bar 🍸 na mgahawa wa jirani na maeneo yale ya Kisesa nilipofikia, nilirudi kwenye Lodge niliyofikia na kama ilivyo kawaida yangu ni kuwa jambo muhimu la kwanza kufanya ni kupitia Google map. Kwa msaada wa Google map huwa naona na kuyajua vizuri maeneo yote yanayonizunguka kwa wakati huo, nitahesabu umbali na kujua njia rahisi za kufikia vivutio ninavyotaka kutembelea na njia hii imekuwa ikilahisisha haswa kujua ghalama na umbali nitakaotumia.

Baada ya kuandaa kila kitu ambacho ningevaa, ningekitumia asubuhi ijayo na kuandika maeneo yote ambayo nataka kuyafikia basi huwa napumzika mapema kabisa ili kuutuliza mwili na uchovu wa safari ya siku hiyo.
Asubuhi imefika, nakumbuka niliamka mapema sana🤭 hii ilitokana na kutamani sana kuona sehemu kubwa ya mji wa Iringa kwa siku mbili pekee na kisha kutembelea katika wilaya ya Mufindi kwa siku kadhaa huko. Nilijiandaa chap, nikakabidhi funguo za chumba na rasmi nikaingia mtaani kuona mazingira na hali ya hewa ya huko. Kutokana na uzoefu wangu haikunichukua muda mrefu sana kupata mwenyeji maeneo hayo, kwani nilitembea umbali wa kama hatua hamsini tu ndipo nikakutana na kijana wa makamo hivi, huyu alikuwa amefuga lasta na kuvaa vizuri kabisa, kwa ufupi ni kuwa aina za uvaaji wa huku ni kama ilivyo maeneo mengine yenye hali ya hewa ya baridi hapa Tanzania. Jamaa alivaa koti kubwa, kofia nzuri, jeans na raba. Ilikuwa siku nzuri hasa baada ya jamaa kujua kuwa nimetokea Dar es salaam na kuja hapa kutembea, alifurahi kwa kuwa yeye pia alikuwa ni mwenyeji wa Magomeni Dar es salaam na alikuwa hapa Iringa kwa miaka miwili sasa kwa shughuli zake za biashara ndogo ndogo ambapo baada ya kumaliza chuo hapo Iringa akajikuta akitamani maisha ya hapa na kuamua kubaki hapa hapa.

IMG_20230624_072625-01.jpeg

(Hii ilikuwa ndio picha ya kwanza kupiga nikiwa ndani ya Iringa mjini. Nilipata picha hii ya kumbukumbu kwa msaada wa rafiki wa kwanza niliyekutana nae hapa)

Basi nilimuuliza maswali machache ya jinsi ya kufika katika eneo la Gangilonga na kwenye shule iliopewa jina la Dr Kleruu, huyu bwana Kleruu nilipata kusoma historia yake hapa hapa jamii forums na nikaahidi siku moja kufika katika mji ambao maisha yake yalitamatika hapo. Ulikuwa ni mwendo mfupi tu kutoka nilipofikia hadi hapo kwenye shule na kuna chuo pia maeneo hayo kama sikosei, na nilisimama eneo hilo kama mtalii wa ndani ninayetaka kuyafikia maeneo yote muhimu kwa miguu yangu😀😄 sikuacha kupiga picha pia katika eneo hilo na baada ya muda mfupi nilianza safari sasa kwenda katika eneo lililopo jiwe la Gangilonga huku yule mwenyeji wangu wa kwanza tukiachana hapo kwenye shule yenye jina la Dr Kleruu. Sikuitaji kupanda bajaji au pikipiki kwa sababu yalikuwa ni maeneo karibu sana. Basi kwa msaada wa maelezo ya mwenyeji wangu na muongozo kutoka katika Google map nilifanikiwa kufika katika maeneo hayo. Lakini kiukweli kabisa nilipita njia ya nyuma na eneo hilo hivyo sikubahatika kuona bango lolote lenye maelezo kuhusu eneo hilo maana nilitokea kwenye eneo lenye nyumba nzuri na Mandhari kama ya maeneo ya Oysterbay au Msasani kule, ulikuwa ni mtaa mzuri na umejengeka vyema.

Hatua chache mbele yangu nikaanza kuuona mwinuko wa jiwe hilo kuubwa nililozoea kuliona kupitia Tanzania safari channel 😃 aisee nilipata msisimko wa ajabu kuona kitu ambacho nilitamani kukiona kwa macho yangu nje ya nionavyo kwenye televisheni. Basi kiufupi ni kuwa eneo lile ni tulivu sana na nilipata kusikia habari kuwa kuna nyakati baadhi ya watu waliokuwa wakitembelea hapo walikumbana na vikundi vya vijana wahuni na kuwaletea shida na wizi. Lakini hadi wakati huo nilipotembelea mimi nilikuta jitihada za kuwakabili wahuni hao zilishafanyika na eneo kuwa na usalama kama kawaida. Sasa shida ilikuwa ni kuwa mimi nilifika eneo hilo mapema zaidi, ilikuwa ni saa mbili kamili hivi asubuhi na wahusika wa hapo sidhani kama wamezoea kupata wageni kwa muda huo, hivyo sikubahatika kuwakuta kabisa maeneo hayo na hali hiyo ilinifanya nisogee kwenye nyumba moja wapo karibu na eneo hilo na kuomba mwenyeji atakayenisaidia kuniongoza hadi kufika juu kabisa ya jiwe hilo. Nashukuru haikuwa shida sana wenyeji wa familia ile walinisikia na kunipa vijana wao wawili kunisaidia kufika eneo hilo na maajabu ni kuwa kati ya vijana hao kuna mmoja wapo Ana zaidi ya miaka kumi hapo hapo chini ya jiwe hilo na hakuwahi kabisa kukanyaga huko juu🧐

Basi tulianza safari kupanda kimwinuko kidogo na kisha kupanda baadhi ya mawemawe na kusogea eneo la juu kabisa kwenye jiwe kuu na kuuona mji wote wa Iringa chini yetu. Aisee usipange kukosa kufika eneo hilo siku ukitembelea Iringa kwa kweli ni eneo zuri na kulikuwa na baridi sana siku hiyo, upepo ulikuwa wa kutosha na Mandhari yote ya mji ilionekana vizuri kabisa
IMG_20230624_080710-01.jpeg

(Hapo pichani ni wakati nikiwa nusu ya safari kupanda juu ya jiwe la Gangilonga)
20230624_080046-01-01.jpeg

(Picha hii nilipiga nikiwa juu kabisa kwenye jiwe hilo na eneo ambapo Mandhari yote ya mji wa Iringa inaonekana vizuri kwa upande wa chini.)

Sikuweza kukaa hapo juu kwa muda mrwfu sana kutokana na kulinda muda wa wenyeji wangu waliosaidia kunileta hapo na pia nilikuwa na mpango wa kuendelea kuyafikia maeneo mengine zaidi ndani ya siku hiyo, hivyo baada ya kupata picha kadhaa za kumbukumbu tulianza kutelemka chini na sikusahau kulipa fadhila kidogo🙂😀 ya angalau pesa kidogo ya kununulia soda kwa wenyeji wangu na kuwahamasisha pia kutembelea vivutio vilivyopo karibu na maeneo yao.
Niliendelea na safari yangu hadi kufika tena katika eneo lile nililopita mwanza lenye shule na kisha kuanzia hapo nikapanda bajaji sasa safari ikiwa ni kufika katika jengo la makumbusho la Iringa Boma. Ikumbukwe pia maeneo hayo yote ndio ilikuwa mara yangu ya kwanza kabisa kufika lakini ilikuwa ili ujue kuwa mimi ni mgeni ni hadi niamue mwenyewe kukuambia, kwani kupitia kiongozi wangu mkuu Google map na maelezo toka mtandaoni yalinisaidia kujua kila kitu katika eneo ninalofikia. Baada ya muda mchache tu nilifika katika eneo maarufu zaidi kama alama ya mkoa wa Iringa, na kuelekea lilipo jengo la Iringa Boma.

(Mwendelezo utakuwa hapa. Kuona zaidi habari kuhusu safari hii tembelea hapa All about Tanzania life.
 
Back
Top Bottom