Makamba: Si dhambi kuchangia Chademahttp://www.mwananchi.co.tz/habari/5-habari-za-siasa/3226-makamba-si-dhambi-kuchangia-chadema
Wednesday, 14 July 2010 08:18
gazeti la mwananchi.
Ramadhan Semtawa
KATIBU mkuu wa CCM, Yusuph Makamba amesema kitendo cha kada wake maarufu na bilionea Mustafa Sabodo kuichangia Chadema, si dhambi kwa kuwa hata "Waislamu huchangia Wakristo" katika shughuli mbalimbali.
Sabodo, ambaye ni mfuasi mkubwa wa falsafa za muasisi wa taifa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, alitoa hadharani hundi ya Sh100 milioni na kuweka bayana kuwa lengo lake ni kuwezesha wapinzani kupata wabunge wengi zaidi, kitu ambacho si cha kawaida katika duru za kisiasa nchini.
Lakini, akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana Makamba alisema kitendo hicho si dhambi wala cha ajabu kwa sababu Sabodo alitoa fedha kutoka mfukoni mwake na si za CCM.
"Kwani wewe dini gani," alimuuliza mwandishi. "Mimi dini yangu ya Mwislamu, lakini nimewahi sana kuchangia Wakristo. Kwani nilivyochangia Wakristo nilibadili dini kuwa Mkristo?
"Kwani ni kosa gani kwa Mkristo pia kumchangia Mwislamu? Huu ni upendo na ukifanya hivyo haimaanishi umebadili dini bwana weee.."
Akikabidhi fedha hizo, Sabodo alisema: "Kambi ya upinzani ikiimarika na kupata wabunge wengi, itasaidia kuimarisha demokrasia nchini na kuliletea taifa maendeleo ya kweli.
Akifafanua zaidi, bilionea Sabodo alisema kwamba kuongezeka kwa wabunge wa upinzani bungeni ni jambo la muhimu katika kuweka upinzani kwa CCM na kusukuma gurudumu la maendeleo kwa wananchi wake.
Makamba alisema Sabodo bado ni mwanachama wao na kwamba kitendo chake cha kuisaidia Chadema hakiwezi kufungua mlango wa kutokea kwa wanachama ambao wanaona chama hicho kinakwenda tofauti na misingi iliyowekwa na waasisi.
"Tumeacha misingi ipi bwana mbona unataka kuongeza mambo....! mimi nakwambia hicho ni kitendo cha kawaida tu," alisema.
Alijifariji kwamba Sabodo hatajatangaza kuondoka CCM pamoja na kuichangia Chadema.
"Kwani CCM ni nini na Chadema ni nini? Hivi vyote ni vyama vya siasa kama ilivyo dini, hivyo kuchangia Chadema haimaanishi yuko Chadema," alisisitiza Makamba.
"Kuna sababu kuu za mtu kujiondoa katika chama; moja ni kunyang'anywa kadi au kurudisha kadi, sisi hatujamnyang'anya kadi wala yeye hajarudisha kadi," alisisitiza Makamba.
Kwa mujibu wa Makamba, CCM haina tatizo na mchango huo wa Sabodo kwa Chadema.
Sabodo kwa muda mrefu amekuwa kimya hasa tangu kuingia madarakani serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete.
Katika uongozi wa awamu ya tatu, Sabodo amewahi kushutumu baadhi ya mambo ndani ya serikali na chama ambayo yalikwenda kinyume na misingi iliyowekwa na Nyerere.
-mwisho-
wana jf mnasemaje kuhusu uweledi huu unaooneshwa na bw. sabodo na koment ya katibu mkuu wa chama chake?