-7-
Imetungwa na kuandikwa na Japhet Nyang'oro
Hivyo isingekuwa sahihi kuwachukua watu muhimu ambao taarifa zao zinategemewa, halafu uwaweke na majasusi wenye uwezo mkubwa wa mapigano. Vinginevyo ni sawa na kuwachanganya kondoo na mbwa mwitu kwenye zizi moja. Hivyo ili kutafuta usawa kwenye kamati hizo, ilibidi kuwaandaa watu wetu kwa namna hiyo. Nadhani sasa umenielewa?”
“Naam! Nimekupata vyema.” Jacob Matata akaitikia huku akitikisa kichwa kuafiki.
“Baada ya miaka kadhaa, hofu ya viongozi wa kijamaa ilikuja kuthibitika kuwa kweli. Baada ya miaka kadhaa, nchi nyingi za kijamaa, ilibidi zifungue mlango kwa mfumo wa uchumi wa kibepari. Ndiyo maana sasa hivi unaona nchi nyingi duniani zinafuata uchumi wa kibepari. Lakini maandalizi yalishafanyika miaka mingi iliyopita.” Bi. Anita akaweka kituo na kushusha pumzi ndefu akifikiri. Baada ya kitambo kifupi cha ukimya wa tafakuri akaendelea.
“Sasa turudi kwenye kisa chetu, kilichokupelekea uniite hapa siku ya leo. Hayo uliyosema yanauhusiano gani na wito wangu?’’ Jacob akauliza huku akipiga mkupuo mkubwa wa sharubati iliyokuwa kwenye bilauri.
"Swali zuri! Miaka kadhaa iliyopita, mchakato wa kutafiti na kupima uwepo na kiwango cha gesi mkoani Mtwara ulianza. Ili kuridhia matakwa ya kimataifa, kuhusiana na nishati zenye mlipuko. Serikali ililazimika kutafuta makampuni makubwa ya kimataifa, yenye uzoefu na kazi ya upimaji na uchimbaji wa gesi Mtwara. Serikali ya Tanzania ikatangaza tenda. Kampuni tatu za kimarekani na mbili za ulaya zikaomba kupewa fursa ya kufanya kazi hiyo. Baada ya kupima na kujulikana kiasi cha gesi inayopatikana hapa nchini, thamani yake ingepatikana. Hapo sasa makampuni ya uchimbani yangeanza kuomba tenda ya kuchimba gesi hiyo.
Kwa vyovyote vile ilivyo, mchakato huu ni mkubwa na hautakuwa na maslahi kwa Tanzania na nchi washirika peke yake. Bali kuna nchi nyingi sana ambazo kwa vyovyote zitaweka mikono yake katika mchakato huo. Hapo ndipo matumizi ya wale watu wetu wawili waliosomeshwa na Mwalimu Nyerere yanapokuja.” Bi. Anita akaweka kituo kabla ya kuendelea.
“Watu wetu hao wanaheshimika na kusifiwa ndani ya Umoja wa Mataifa. Tayari serikali imeshawapa taarifa kuhusu hili suala la kugunduliwa kwa gesi hapa nchini. Taarifa ziliwafikia kupitia Idara ya Usalama wa Nchi yetu. Halikuwa jambo jipya kwa vile tayari walikuwa na tetesi za mchakato huo. Hivyo mapema baada ya kupata taarifa, wakaanza maandalizi ya chini kwa chini.”
“Kwa bahati nzuri mmoja wa hao watu wetu, aliombwa na kampuni moja ya Marekani. Wakimtaka awe kwenye timu yao ya wataalamuu, ambayo ingekuja kufanya kazi nchini. Endapo serikali ya Tanzania ingewapa zabuni ya kupima kiwango cha gesi iliyopo. Mtu huyo ni mwanamke, anaitwa Judith Muga. Mara moja alipotakiwa kuingia kwenye timu hiyo ya kigeni, aliamua kuitaarifu serikali yetu. Kwa kuzingatia hilo, serikali ikaamua kwa makusudi, kuichagua kampuni hiyo kuongoza mchakato huo. Huku wakijua fika kuwa kampuni hiyo itatoa nafasi kwa mtu wetu kufanya nayo kazi. Kampuni hiyo ingefanya kazi na makampuni mengine kutoka nchi kumi, ambazo zingekuwa waangalizi huru wa mchakato mzima.” Bi. Anita akaweka kituo kabla ya kuendelea.
“Kwa sababu hiyo, Judith Muga amekuwa hapa Tanzania kwa zaidi ya mwaka mmoja. Akishirikiana na wataalamuu wa kampuni hiyo ya kigeni pamoja na washika dau wengine muhimu. Amepewa mkataba wa awali, mwaka mmoja uliyopita.” Bi. Anita akaweka kituo kama anayefikiri jambo, kisha akasema.
“Nilikwambia watanzania waliopandikizwa walikuwa wawili. Tayari nimemwongelea Judith Muga. Mtanzania mwingine Ivan Mabala, yeye aliingizwa kwenye Kamati ya Baraza la Umoja wa Mataifa, ambayo inashughulika na usalama wa raia katika matumizi ya nishati. Umoja wa Mataifa kwa kuhofia kuwa malengo ya kibiashara yanaweza kusahau kutazama usalama wa raia, uliweka kitengo hiki. Kazi kubwa ya kitengo hiki ni kuhakiki na kuwakilisha maslahi ya raia popote kunapoanzishwa mradi mkubwa wa kuchimba na kuchakata nishati. Kamati hii ndiyo ambayo huangalia mambo kama vile; uharibifu wa mazingira na kuhakikisha hakuna madhara kwa raia, kutokana na taka zitakazozalishwa na miradi ya kuchakata na kuchimba nishati.” Bi. Anita akaweka kitoa na kumtazama Jacob. Haraka akaridhika kuwa maelezo yake yalimuelea vyema. Kisha akaendelea.
“Hivyo basi, wawakilishi wa kamati hiyo, ilikuwa ni lazima wawepo kwenye shughuli ya Mtwara. Unaweza kujiuliza kisa chetu kinaingiaje hapa? Ni hivi! Kuna mambo matatu yametokea ndani ya wiki tatu zilizopita. Mambo hayo yanatia shaka sana, kiasi kwamba waziri mkuu ameomba kitengo chetu kiingilie kuchunguza. Nimefikiri kwa kina alichosema na nimekubali kuwa, sisi tukiwa kitengo cha ujasusi cha nchi hii, hatutakiwi kunyamaza na kuendelea kusubiri.”
“Nini kimetokea?” Jacob akauliza kwa shauku.
“Hatua ya kupima kiasi cha gesi iliyopo imeshafanyika. Ripoti ya awali ilishaandaliwa. Kilichobaki ni serikali kuipitia rasmi ripoti hiyo na rais kutia saini. Rais akishatia saini, ripoti hiyo itasambazwa kwenye soko la kimataifa kama tangazo rasmi la serikali ya Tanzania, kukaribisha wawekezaji wa kuchimba gesi iliyoko mkoani Mtwara. Hapo ndipo wadau watakaporusha vyema karata zao.” Bi. Anita akaweka kituo na kumtazama Jacob Matata kwa makini. Kisha akaendelea.
“Shida iliyojitokeza sasa, baada ya kazi ngumu ya mwaka mzima, ya kuchunguza na kupima upatikanaji wa gesi ya Mtwara, ripoti hiyo ilikamilika. Japokuwa Judith alikuwa anafanya kazi kwa niaba ya kampuni iliyomuajiri, lakini Tanzania ilikuwa ikimtegemea sana katika maoni yake kabla ya rais hajatia saini. Judith angeshirikiana kwa siri na maafisa wengine wa wizara ya Nishati na Madini, kupitia ripoti hiyo na kisha kuiwasilisha kwa rais. Ushiriki wa Judith, kama mtu muhimu wa serikali, ulikuwa kwa siri kubwa. Lakini ilikuwa wazi kuwa, katika Wizara ya Nishati na Madini, hapakuwa na mtu aliyekuwa na uwezo wa kitaalamuu na uzoefu wa kusimamia mchakato huo. Hivyo kazi hiyo ilimtegemea sana Judith. Sasa jambo la kushangaza ni kuwa, hadi wakati huu tunavyoongea, ripoti ya gesi ya Mtwara imetoweka kwenye mazingira ya kutatanisha.”
“Unamaanisha nini? Kama ripoti halisi haionekani, wadau muhimu wa mchakato huo, kama Judith na wawakilishi wa makampuni shiriki. Si watakuwa na nakala kwenye compyuta zao?’’ Jacob akahoji kwa namna ya kuonesha kuwa hapakuwa na tatizo kubwa.
“Hiyo ndiyo sababu iliyonipelekea kukuitaka uingilie kati kisa hiki cha kusisimua. Judith Muga, ambaye ndiye alikuwa na nakala ya mwisho ya ripoti hiyo. Akiwa na jukumu la kuisoma na kuihakiki, kabla ya kuiwasilisha na hatimaye kupitishwa na rais. Ametoweka, huku juhudi za kujua alipo, zikigonga mwamba.” Bi. Anita akaweka kituo na kupiga mwayo hafifu. Jacob Matata akabaki ametumbua macho huku akili yake ikijenga shauku. Wakati huu, maswali mengi yalipita kichwani mwake na kuibua hoja zenye maswali lukuki. Bi. Anita akaendelea.
“Kuna kosa limefanyika mahali fulani.” Bi. Anita akaongea huku akifikiri.
“Kosa gani?” Jacob akadadisi.
“Hakuna afisa mwingine wa serikali aliyekuwa na nakala ya ripoti hiyo na bahati mbaya haikuwahi kuchapishwa. Sehemu pekee ripoti hiyo ilipokuwa imehifadhiwa ni kwenye kompyuta ya Judith. Hivyo kutoweka kwa Judith, kumetokea sambamba na kutoweka kwa ripoti hiyo ya gesi ya Mtwara.” Bi. Anita akaweka kituo.
“Kwanini tusiwaombe wataalamuu wengine, walioshirika mchakato huo watupatie nakala zao?’’
“Hapo ndiyo suala lingine linapoibuka. Ndege iliyokuwa imebeba wataalamuu, waliokamilisha uchunguzi na mchanganuo wa gesi ya Mtwara, imeangushwa siku kadhaa zilizopita. Bila shaka taarifa unazo, kwani hiyo ndiyo habari ya mjini kwa sasa. Jambo la kushangaza, yule mtanzania mwingine aliyepewa uraia wa Urusi. Bwana Ivan Mabala, ameuawa wiki moja iliyopita. Wakati ambapo taifa linategemea sana uwepo wake kwa siri.” Bi. Anita akaweka kituo, huku macho yake makali yakimtazama Jacob Matata kwa utulivu. Mara hii aliweza kubaini jinsi uso wa Jacob ulivyobadilika na kuchukua uzito unaostahili, kutokana na kile alichokuwa akimwambia.
“Ulisema uhusiano wa Judith Muga na serikali, ulikuwa wa siri sana. Umewahi kufikiri kuwa Judith anaweza kutusaliti? Halafu pamoja na ndege hiyo kuanguka yenyewe ama kuangushwa, bado hainiingii akilini kuwa, hatuwezi kupata ripoti hiyo kutoka kwenye kompyuta za watu hao!’’ Jacob akatia shaka huku akifikiri.
“Judith Muga alitoweka baada ya kutoweka kwa Waziri wa Ulinzi, Sabodo Msumari. Hapo awali haikuwa wazi kama alikuwa ametekwa au ameuawa au vyote kwa pamoja. Lakini baada ya Judith kutoweka, inaonekana Sabodo alitekwa na watu waliotaka kujua taarifa za Judith. Sabodo ndiye mtu pekee aliyekuwa akifahamu mahali anapoishi Judith. Hivyo inawezekana Sabodo aliuawa baada kuhojiwa juu ya wapi alipokuwa akiishi Judith. Hadi sasa hatuwezi kujua, watu hao walifanikiwa kupata taarifa gani kutoka kwa Sabodo.”. Bi. Anita akafafanua zaidi.
Kesho asubuhi tunaendelea sehemu ya 8.
Sent using
Jamii Forums mobile app