RIWAYA: UFUKWE WA MADAGASCAR
SEHEMU: 65
“Sifahamu kitu chochote kuhusu hizo pesa unazosema”. Nikaongea kwa utulivu. Yule kamanda akanitazama huku akiruhusu tabasamu la kifidhuli kuchanua usoni mwake kisha nikamuona akionesha ishara fulani kwa kichwa ambayo sikufahamu maana yake ingawa nilihisi kuwa huwenda alikuwa akiwasiliana na yule mtu aliyekuwa nyuma yangu.
Ghafla nikavalishwa ule mfuko mweusi kichwani kisha nikaanza kuburutwa kibabe kwenye kile kiti nilichofungwa kuelekea kando ya lile eneo. Hatukwenda mbali mara tukasimama na hapo nikabebwa na kuinamishwa chini sehemu fulani. Kufuatia tukio lile nikaanza kuhisi kuwa mambo hayakuwa shwari tena na muda uleule nikaanza kumiminiwa maji mengi usoni huku nikiwa bado nimevikwa ule mfuko mweusi ambao mara hii ulikuwa umekazwa kisawasawa. Hofu ikaniingia pale nilipokumbuka kuwa mtindo ule ulikuwa miongoni mwa mitindo hatari iliyokuwa ikitumika kuwatesa watuhumiwa sugu hususani washukiwa wa ugaidi pale wanapolazimishwa kuzungumza juu ya taarifa fulani. Mtindo ule wa utesaji humpelekea mtuhumiwa kushindwa kuvuta hewa ya kutosha na hali hiyo inapozidi hupelekea kifo.
Niliendelea kumiminiwa maji mengi usoni kwa muda mrefu huku nikijitahidi kufurukuta bila mafanikio. Mapafu yangu yakaanza kusumbuka kutafuta hewa safi ya oksijeni iliyoanza kuwa adimu hata hivyo sikufanikiwa kirahisi. Hatimaye nikaanza kuhisi kizunguzungu, giza zito likaanza kutanda kwenye mboni zangu huku taratibu nguvu zikiniishia mwilini, mwishiwe roho yangu ikafika njia panda.
Wakati hali yangu ikizidi kuwa mbaya mara kwa mbali nikasikia amri kutoka kwa yule kamanda na hapo lile zoezi likasitishwa. Nilipoketishwa vizuri ule mfuko mweusi ukaondoshwa kichwani mwangu hali iliyonipelekea nitapike chakula chote tumboni na kuanza kuhema hivyo kama niliyepishana na kiumbe cha ajabu msituni. Macho yakaniwiva huku mdomo ukinichezacheza kwa hofu. Kwa vile nilivyoketishwa sikuweza kuona nyuma yangu ingawa nilihisi kulikuwa na beseni kubwa la maji na hivyo kunithibitishia kuwa kile kilikuwa chumba cha mateso.
“Bila shaka sasa upo kutueleza pesa ziko wapi”. Yule kamanda akajigamba.
“Ningekuwa nafahamu hizo pesa mnazozizungumzia ningekwisha waambia mahali zilipo kuliko adha hii ya mateso”. Nikaendelea kujitetea huku nikihema kwa pupa.
“Wenzako wako wapi?”. Yule kamanda akaniuliza kwa kujiamini kana kwamba alikuwa na hakika na anachokizungumza.
“Wenzangu akina nani?”
“Wenzako mlioshirikiana katika kupanga mapinduzi ya kijeshi hapa Burundi”
“Mimi sijafika hapa Burundi kushiriki mapinduzi ya kijeshi na wala sifahamu chochote kuhusu hao watu mnaonihusisha nao. Kwa tafsiri nyingine mimi siyo mtu sahihi mnayemtafuta. Yaani ni kama mtego wa nguruwe pori halafu amenasa fisi. Tafadhali naomba mniache niende zangu kama hamtaki wageni katika nchi yenu”. Nikafoka kwa hasira huku nikijitahidi kufurukuta kwenye kile kiti nilichofungwa bila mafanikio. Hata hivyo hila yangu haikufanikiwa kwani nilijikuta nikitulizwa kwa kuzabwa makofi mawili mazito kichwani kutoka kwa yule mtu aliyekuwa nyuma yangu na hivyo kunisababishia maumivu makali kichwani. Yule mtu aliyesimama nyuma yangu alikuwa hodari sana wa kuzaba makofi na viganja vyake vilikuwa vimekomaa kama mbao kavu ya mninga na ingawa kile kilikuwa kipigo cha mara moja lakini maumivu yake hayasimuliki.
Yule kamanda hakunijibu badala yake nikamuona tena akionesha ile ishara ya kichwa kwa yule mtu aliyekuwa nyuma yangu. Muda uleule nikavishwa tena ule mfuko mweusi kisha nikabebwa tena na kuinamishwa kwenye lile beseni nyuma yangu na hapo lile zoezi la kumiminiwa maji usoni likaanza upya. Mara hii yale maji yalikuwa mengi huku muda wa mateso ukiongezwa. Lile zoezi likaendelea huku nikifurukuta tena bila mafanikio hadi ikafikia muda sikuweza tena kuleta matata kwani nguvu zilikuwa zimeniiishia mwilini. Macho yangu yakaanza kufumba taratibu huku mtupo wa mapigo ya moyo wangu ukidorora hatimaye sikuweza kusikia chochote kilichokuwa kikiendelea eneo lile.
_____
Niligundua kuwa fahamu zangu zilikuwa zimenipotea muda mfupi baada ya kupigwa ngumi moja ya tumbo iliyonipelekea nitapike maji mengi niliyoyameza tumboni na hapo nikaanza tena huhema kwa pupa huku maumivu makali yakisambaa mwilini. Lile jopo la wale makamanda wa jeshi bado lilikuwa mbele yangu nyuma ya ile meza na hapo nikagundua kuwa haukuwa umepita muda mrefu tangu kupotewa na fahamu zangu hadi kuzinduka. Nilikuwa nimelowa chapachapa kufuatia yale maji niliyomwagiwa.
“Tueleze Luteni pesa ulizoiba ziko wapi na watu unaoshirikiana nao ni akina nani?”. Yule kamanda akaniuliza huku akinitazama kwa makini usoni.
“Mnadhani nitaukwepesha ukweli kwa kuyageuza maneno yangu. Nimekwisha waambia kuwa sifahamu lolote”. Nikaongea kwa shida huku mawazo mengi yakipita kichwani mwangu. Ukweli ni kwamba moyoni nilishaanza kuhisi juu ya hatari kubwa iliyokuwa ikininyemelea mle ndani. Vile vielelezo vyangu vilikuwa vimenipelekea moja kwa moja niaminike na wale makamanda wa jeshi la wananchi wa Burundi kuwa nilikuwa miongoni mwa wahaini wa serikali na askari mamluki walioingia nchini Burundi kinyemela kwa ajili ya kusadia kufanyika kwa mapinduzi ya kijeshi. Kwa kweli niliishiwa nguvu na kuanza kukata tamaa kwani utetezi wangu ungehitaji ushahidi mkubwa ambao ungeweza kuwashawishi wale makamanda kuwa mimi sikuwa miongozi mwa hao wanamapinduzi wa kijeshi waliokuwa wakisakwa. Ushahidi ambao ili niaminiwe ingelinibidi nizungumze ukweli juu ya misheni yangu yote hadi kufika kwangu pale Burundi.
Labda ningeweza kufanya hivyo lakini maadili ya kazi yangu kamwe hayakuniruhusu. Kwanza sikutaka kuamini kuwa mara baada ya kuzungumza ukweli huo ningeachiwa huru, lah hasha!. Ni dhahiri kuwa baada ya hapo ningeuwawa kama walivyouwawa mahaini wengine. Lakini vilevile kazi yangu ya ujasusi sifa yake moja ni kufanyika katika mazingira ya siri sana kwani hakuna nchi yoyote inayoruhusu kuchunguzwa au kupelelezwa na nchi nyingine kwa sababu za kiusalama. Hivyo endapo ningezungumza ukweli kwa namna moja au nyingine ningeweza kujitenganisha na wingi wa lawama za moja kwa moja kwangu badala yake lawama hizo zingeelekezewa kwa nchi yangu Tanzania iliyonituma na hivyo kuharibu mahusiano mazuri yaliyojengwa kwa muda mrefu. Ingawa kufuatia kukamatwa kwangu nilifahamu kuwa tayari kulishatia dosali mahusiano mazuri yaliyokuwa baina ya nchi hizi mbili lakini niliona nisipalie mkaa suala hilo kwa kuzungumza ukweli. Hivyo nikapanga kushikilia msimamo wangu hata kama ungenigharimu kifo.
“Luteni, mimi naona tukupe kwanza muda wa kutafakari ili baadaye tutakaporudi uweze kuyajibu maswali yetu vizuri”. Yule kamanda akaongea kwa kujiamini huku akiitazama saa yake ya mkononi kama anayekimbizana na muda.
“Muda hauwezi kubadili ukweli kamanda”. Nikaongea kwa hasira nikipingana kikamilifu na hoja ile.
“Muda hauwezi kubadili ukweli lakini unaweza kubadili matokeo”. Yule kamanda akaongea kwa ujivuni huku akiruhusu tabasamu la kihuni usoni mwake kisha nikamsikia akimwambia yule mtu nyuma yangu.
“Mfungue na umuache huru”. Mwanzoni nilidhani kuwa sijasikia vizuri lakini kitendo cha kumuona yule mtu nyuma yangu akianza kunifungua zile kamba mwilini kwenye kile kiti kikanipelekea nistaajabishwe na upendo ule wa mwendo kasi. Wakati yule mtu alipokuwa katika harakati za kunifungua ile kamba mara nikawaona wale makamanda wakisogeza viti vyao nyuma na kusimama kisha pasipo kuzungumza neno wakaanza kuondoka mle ndani kupitia ule mlango tulioingilia.
Yule mtu nyuma yangun alipomaliza kunifungua zile kamba na yeye akaanza kuondoka mle ndani huku akiwa ameongozana na wanajeshi wengine wawili ambao kupitia sare zao niliweza kuwatambua kuwa walikuwa makomandoo wanaonuka ubabe wa kila namna. Wale watu walipotoka mle ndani ule mlango wa kile chumba ukafungwa kwa nje na hapo nikabaki peke yangu mle ndani.
Nikiwa bado nimeketi kwenye kile kiti mawazo mengi yakawa yakipita kichwani mwangu. Maneno ya yule kamanda yalikuwa yakiendelea kuzitaabisha fikra zangu juu mambo yalivyokuwa yakienda. Sasa nilichokuwa nikikifikiria ilikuwa ni kutoroka mapema mle ndani kabla ya wale makamanda hawajarudi mle ndani kunifanyia mahojiano ya awamu ya pili. Taratibu nikaanza kuyatembeza macho yangu kukipeleleza vizuri kile chumba kilichofanana na pango dogo lililochongwa miaka mingi iliyopita kwa ustadi wa hali ya juu. Tatizo likabaki ni kwa namna gani ningeweza kutoroka kwenye kifungo kile kile pasipo kujua ramani ya lile eneo.
Wakati nikiendelea kutafakari ghafla nikashtushwa na sauti hafifu ya mtu anayekohoa nyuma yangu. Baridi nyepesi ya mshtuko wa hofu ikasambaa mwilini, nywele zikanicheza kichwani huku mate yakinikauka kooni. Nikaanza kuhisi jambo la hatari nisilolifahamu lilikuwa likininyemelea taratibu nyuma yangu. Nikapanga kuwa nisigeuke nyuma haraka hata hivyo mawazo yangu yakasalitiwa na hisia na kunipelekea nishindwe kuvumilia na hapo taratibu nikageuka kutazama nyuma.
Kwa sekunde chache nikashikwa na mduwao usioelezeka. Kiasi cha umbali wa hatua moja nyuma yangu alikuwa amesimama mtu ambaye sikuwahi kumuona hapo kabla wala kufahamu kuwa alikuwa ametokea wapi kwa mle ndani. Lilikuwa pandikizi la mtu mweusi na urefu wake ungepelea kidogo kutimia futi saba. Mwili wake ulikuwa imara na ulioshiba misuli ya nguvu. Jitu lile lilikuwa limevaa suruali ya jeshi na buti za jeshi miguuni, kichwani alikuwa amenyoa upara huku kifua wazi na mikono yake alikuwa ameikunjia kifuani. Lile jitu lilikuwa likinitazama kama kiumbe cha ajabu sana kuwahi kuonekana mbele yake. Mara moja nilipomtazama yule mtu mashaka yakaanza kuniingia huku nikianza kunusa harufu ya matata. Nikataka nisimame haraka pale kwenye kiti hata hivyo sikufanikiwa kwani pigo moja la teke la lililoinuliwa na kwa kasi ya umeme na kutua begani mwangu linanirudisha chini na kuniketisha kwenye kile kiti.
“Tulia chini komredi hakuna haja ya kuharakisha mambo”. Lile jitu likanionya huku maumivu makali yakisambaa begani mwangu. Ukubwa wa umbo la lile jitu ukanishangaza sana kama siyo kuniogopesha.
“Wewe ni nani na unashida gani na mimi?”. Nikaliuliza lile jitu huku nikigeuka kiwiziwizi kulitazama tena.
“Usijali utanifahamu hapo baadae”
“Una shida gani na mimi?”. Nikauliza kwa udadisi.
“Wakubwa wamenituma nije kukuhoji”
“Wakubwa gani na kwanini wasije wao wenyewe?”
“Wakubwa wangu wa kazi”
“Kwanini wasije wao wenyewe?”
“Wao wanamajukumu mengine muhimu kwa wakati huu”
“Wewe ndiyo hauna majukumu?”. Nikaliuliza lile jitu na kabla sijaendelea lile jitu likanichapa kofi zito la shingoni ambalo maumivu yake yakanipelekea nimeze funda kubwa la mate huku hasira ikinichemka mwilini.
“Maswali mengine yanafaa umuulize mke wako”. Lile jitu likanifokea na sauti yake nzito ikatengeneza mwangwi mkubwa mle ndani kisha likaniuliza.
“Pesa ulizokwapua ziko wapi na watu unaoshirikiana nao kwenye mapinduzi yenu ya kishenzi ni akina nani?”
“Nimekwisha waambia mabwana zako kuwa sifahamu lolote”. Nikafoka kwa hasira na lile jitu halikuweza kuvumilia tusi lile hivyo likarusha teke usawa wa kichwa changu lakini tayari nilikwishaliona pigo lile hivyo nikainama chini kidogo kulipisha likate upepo. Hata hivyo wakati nikifurahia hila ile lile jitu likaniwahi kwa pigo jingine la teke ambalo lilizama kwenye tundu la mgongo wa kile kiti cha mbao na kunitupa chini kama bwege. Nikawahi kusimama lakini mara hii mateke mawili makini ya lile jitu yakafakinikiwa kunilambisha tope kwenye sakafu ya kile chumba na kunisababishia maumivu makali. Lile jitu kuona vile likaanza kujitapa huku likijipigapiga kifuani kama sokwe mtu na kuangua kicheko cha mahoka.
Haraka nikawahi kusimama kisha nikalifuata lile jitu kulikabili na liliponiona nikilifuata likasimama kama sokwe na kunisubiri. Nilipolifikia nikaanza kulichapa mapigo hatari ya chapchap sehemu tofauti nikipanga kuliangusha chini, lakini ni kama nilikuwa nikilitekenya na hivyo kulipelekea liangue kicheko cha dhihaka. Nilipoona lile jitu halikolei mapigo nikalichapa teke moja la korodani. Likawahi kushtukia pigo lile na kuudaka mguu wangu kisha likanikwida kibabe na kuninyanyua juu kama mwana miereka halafu likaanza kukimbia na mimi mle ndani na kwenda kunibwaga kwenye kona moja ya kile chumba, maumivu yale yakanipekea nipige mayowe. Loh! lile jitu lilikuwa na nguvu nyingi kama lililokunywa viagra. Kabla sijasimama likawahi kupenyeza mkono wake mmoja na kuidaka shingo yangu kisha likaninyanyua juu kwa mkono wake mmoja huku likinitazama kwa hasira. Mara hii nikapata wazo muruwa, haraka nikajikunja na kulitandika lile jitu pigo la kifuti cha pua. Pigo lile makini likauvunja mwamba wa pua yake hapo na hapo lile jitu likapiga yowe kali na kunitupa kando haraka kama lililoshika kaa la moto. Lile jitu likaendelea kupiga yowe kali mle ndani na hivyo kupelekea mtetemo mkali mle ndani kiasi kwamba popo waliokuwa mafichoni wakapagawa na kuanza kuyakimbia maficho yao wakizunguka hovyo mle ndani.
Sasa nililiona lile jitu likinijia mzima mzima huku limepandwa na hasira kama mbogo aliyeparazwa na risasi ya kichwa ya muwindaji. Sikuwa na nguvu za kutosha za kukabiliana na lile na lile dubwana hivyo nikavisogelea vile viti nyuma ya ile meza mle ndani na kuanza kulitupia lile jitu. Ilikuwa kama mchezo kwani lile jitu lilivipangua vile viti kwa mikono yake huku vingine vikivunjika vunjika vipande vipande na kusambaratika mikononi mwake. Lile jitu liliponifikia nikaanza kulikwepa nikikimbilia upande huu na ule kama bondia anayetafuta nafasi nzuri ya kutupa konde lake kwa mpinzani. Lile jitu likawa likinifuata kila ninapoelekea mle ndani. Nilipopata nafasi nzuri nikaruka kwa ufundi wa hali ya juu na kujikita ukutani kwa mtindo mzuri wa sarakasi kisha nikajitupa hewani na kulinasa vizuri lile jitu shingoni kwa kabari ya miguu yangu, kabari matata ambayo ili mtu aweze kujinasua angepaswa kujikaza vizuri ili shonde lisimtoke.
Sote takapiga mwereka na kuanguka chini huku lile jitu likilalama kwa maumivu. Baada ya kukurukakara kubwa mle ndani huku lile jitu likijitahidi kujinasua hatimaye likanizidi nguvu na kuikamata miguu yangu vyema na kuindoa shingoni mwake kisha likawahi kunichapa makofi mawili ya mgongoni wakati nilipojaribu kujiviringisha mbali naye. Japokuwa lile jitu lilikuwa na mwili mkubwa lakini wepesi wake ulinishangaza sana kwani wakati nilipokuwa nikisimama nilishangaa nikichotwa mtama kwa ufundi ilionishangaza sana. Nikarushwa hewani huku nikiweweseka kwa pigo lile. Nilipotua chini lile jitu likawahi kunidhibiti kwa kabari matata shingoni mwangu kwa mokono yake imara. Nikajitahidi kufurukuta bila mafanikio nikitupa mikono na miguu yangu huku na kule.
Lile dubwana halikuniachia kirahisi badala yake likaendelea kukaza mikono yake kwa nguvu zote na kunipelekea nianze kuhema kwa shida. Sasa mle ndani kulikuwa na patashika ya aina yake katika kuhakikisha kuwa najinasua mapema kutoka katika kabari ile ya kifo. Sikufua dafu kirahisi kwani lile jitu lilikuwa na nguvu nyingi za kunidhibiti hivyo ni kama nilikuwa napoteza muda wangu bure kwani halikuniachia.
Hali yangu ikaanza kuwa mbaya baada ya kuanza kukosa hewa, nikatanua mapafu yangu bila mafanikio huku mishipa yangu shingoni ikituna na macho yameniwiva kama nyanya. Hofu ya kifo ikaanza kuniingia taratibu. Nikajaribu kulipiga lile jitu kwa kichwa cha kinyumenyume hata hivyo sikufanikiwa kwani lile jitu lilinikwepa kwa wepesi wa ajabu. Nikiwa katikati ya kujinasua mara wazo fulani likanijia. Kufumba na kufumbua nikatupa pigo moja makini la kiwiko cha nguvu kwenye jicho la kulia la lile dubwana. Lilikuwa pigo makini lililoniletea majibu muruwa. Lile jitu likapiga yowe kali mle ndani kiasi cha kuniogopesha hata mimi mwenyewe hata hivyo halikuniachia badala yake likaninyanyua juu na kunitupia ukutani na kunisababishia maumivu makali ya bega. Hata hivyo sikuwa na muda wa kujilegeza kwani roho yangu tayari ilikuwa mnadani. Wale popo mle ndani wakaanza tena kurandaranda wakionesha kushtushwa sana na zile kelele.
Wakati lile jitu likinijia pale chini huku limejifunika jicho kwa kiganja chake mimi tayari nilikuwa nimeliona hivyo nikawahi kujiviringisha kando kulikwepa kisha kwa mtindo mzuri wa sarakasi nikalisindikiza kwa teke makini la mgongoni. Lile jitu likaenda kujibamiza ukutani huku tusi zito likimtoka mdomoni huku mimi tayari nikiwa nimeangukia upande wa pili wa kile chumba. Hata hivyo sikufanikiwa haraka kujipanga kwani tayari lile jitu lilikuwa limenifikia hivyo likanichapa teke matata kifuani na maumivu yake yalikuwa ni kama niliyepigwa na kipande cha jabali kifuani. Nikatupwa nyuma vibaya na kuangukia tope sakafuni. Nilijaribu kusimama haraka lakini lile jitu lilikuwa makini sana hivyo haraka likawa limenifikia na kuanza kunitupia mateke mfululuzo, baadhi nikafanikiwa kuyapangua mengine yakanipata hata hivyo sikuacha kujitetea nikihamia upande huu na ule kumpotezea umakini.
Nilipopata nafasi nzuri nikarukia ukutani na kukita vyema miguu yangu kisha kwa mtindo wa sama soti nikajibetua hewani kulifuata lile jitu kwa pigo makini la kifuti cha kichwa. Lilikuwa pigo hatari sana kiasi kwamba mtu yeyote wa kawaida kama angepona basi angekuwa tayari amerukwa na akili lakini kwa lile jitu hali ilikuwa tofauti kidogo kwani nililiona likirudi kinyumenyume kwa mwendo wa kupepesuka kama mlevi huku akipiga yowe kali kama aliyepigwa kwa nyundo ya mawe kichwani. Lakini hatimaye akasimama na kukitikisa kichwa chake huku na kule kukiweka sawa. Nilipomchunguza nikaona damu nyepesi ikimtoka puani na masikioni na hapo nikajua kipigo changu kilianza kumkolea.
Sikutaka kumkawiza haraka nikainuka kule nilipoangukia ili kumkabili. Pigo langu la kwanza la teke lilimpata mbavuni, pigo la pili likamparaza tumboni, pigo la tatu akaudaka mguu wangu kwa mkono wake wa kushoto kisha akanichota matama ulionirusha vibaya hewani huku nikiweweseka na nilipotua chini akanikita mguu wa mgongo, pigo baya zaidi kuwahi kukutana nalo katika harakati zangu. Nikagugumia kiume kwa maumivu makali, akawahi kurusha teke linipate tumboni lakini niliwahi kujiviringisha kando hivyo pigo lile likakata hewa bila mafanikio na kunipelekea lile jitu lipepesuke hovyo kwa kukosa mhimili. Nikamfuata haraka na kumchapa teke la kifua, akalipangua kwa madaha lakini hakuwa ameshtukia hila yangu kwani wakati akifurahi kwa kulipangusa pigo langu mimi tayari nilikwishaufyatua mguu wangu mwingine, nikamchapa teke la shingo, pigo lililompelekea apige chafya kama aliyenusa ugolo.
Lile jitu kuona vile likapandwa na gadhabu likaanza kunitukana matusi ya kila aina huku likinisogolea taratibu kama linalotaka kunikamata mzimamzima. Nikaanza kulikwepa nikahamia upande huu na ule huku macho yangu yakiwa makini katika kuhakikisha kuwa halinifikii. Mbinu za lile jitu kutaka kunikamata mzimamzima zilikuwa zimeanza kunitahadharisha kwani nilifahamu kuwa lilikuwa na nguvu nyingi mno kiasi kwamba lingeweza kunidhibiti bila usumbufu mkubwa. Mara mbili tatu nikafanikiwa kulikwepa lile jitu hata hivyo wakati nikijiandaa kulikwepa kwa mara nyingine kwenye kona ya kile chumba bahati mbaya nikateleza kwenye tope na kujikuta mikononi mwake. Lile jitu likanikumbatia na kunibana kifua na mikono yangu kwa nyuma kisha likaanza kunibana mbavu kama chatu anayejiandaa kunimeza, maumivu yake yalikuwa makali mno huku nikihisi kichomi. Nikiwa nimeanza kuona hatari ya kupoteza maisha nikakusanya nguvu za kutosha kisha nikalitandika lile jitu kichwa cha nguvu cha kinyumenyume. Pigo lile likauchana vibaya mdomo wake na kuyavunja meno yake mawili huku akijing’ata ulimi vibaya. Hata hivyo lile jitu halikuniachia na mimi kuona vile nikarudia pigo lile kwa mara pili mara hii nikafanikiwa kulivunja vibaya taya lake la kulia. Lile jitu likapiga yowe na kuniachia bila kupenda, nikaangukia upande wa pili huku nikiwa nahema kwa pupa baada ya kukosa pumzi ya kutosha kwa kitambo sambamba na maumivu makali mbavuni.
Loh! sikuwa nimegeuka nyuma haraka kulitazama tena lile jitu wakati lilipochomoa kisu kutoka kwenye mkanda wa kombati yake kiunoni na kunitupia. Nikashtushwa na maumivu makali yaliyonipelekea nipige yowe baada ya kisu kile kuzama mgongoni. Kabla sijajihami vizuri kisu kingine kikazama kwenye mnofu wa paja la mguu wangu wa kushoto na kusambaza maumivu makali mwilini. Nikapiga yowe kali kuomba msaada lakini ilikuwa ni sawa na kazi bure. Pigo la tatu la kisu lilinikuta wakati nikijitupa chini upande wa pili wa ile sehemu hivyo kikazama kwenye mnofu wa msuli wa mkono wangu wa kushoto. Hofu ikaziteka haraka hisia zangu, nikaanza kuona kifo kilikuwa karibu sana kunifikia. Lile jitu lilikuwa na shabaha ya hali juu katika mtindo wa mapigano ya visu hata hivyo mimi nilikuwa mwalimu zaidi yake. Hivyo kabla ya pigo la nne la kisu chake halijanifikia mimi tayari nilikwishawahi kukichomoa kile kisu kwenye mnofu wa mkono wangu wa kushoto kisha kwa shabaha makini nikakitupa kile kisu kwa mtindo wa kininja, kikaenda kuzama tumboni kwa lile dubwana na huku mpini wake ukisalia nje. Lile jitu likapiga mayowe ya kutetemesha lile pango hadi wale popo kuanza kurandaranda hovyo mle ndani. Lile jitu likaushika ule mpini wa kisu tumboni mwake huku macho yamemtoka kama mjusi aliyebanwa na mlango huku limesimama, taratibu damu ikaanza kusambaa kwenye viganja vyake mkononi.
Kwa maumivu makali nikajikaza na kuchomoa kile kisu kilichozama kwenye mnofu wa paja langu huku nikipiga yowe la uchungu kisha nikakizungusha na kukitupa kwa lile jitu. Kile kisu kikazama mbavuni mwa lile jitu lakini mara hii lile jitu liliachama mdomo pasipo kupiga kelele kama mtu mwenye kiu mbaya ya maji karibu na kufa. Kisu cha tatu wakati nikikichomoa mgongonim maumivu yake yakanipelekea nipige kelele za woga kwani damu nyingi ilinitoka na mimi kwa hasira nikakitupa kile kisu kwa lile jitu kwa nguvu zangu zote na hapo kikaenda na kuzama kwenye shingo yake. Mara hii nilisikia mguno hafifu kwani lile jitu halikuwa na nguvu ya kupiga mayowe tena badala yake nikaliona taratibu likianguka chini kama mbuyu uliopigwa shoka la mwisho kuanguka.
Mle ndani kukasikika kishindo kikubwa wakati lile dubwana likaanguka chini kwenye tope, wale popo wakatowekea kwenye maficho yao kisha ukimya ukachukua nafasi yake mle ndani. Nilianguka chini bila kupenda huku nikihema kwa tabu kama mwanariadha wa mbio za masafa marefu katika mstari wa mwisho wa ushindi wake. Yale majeraha ya visu mwilini mwangu yalikuwa yakivuja damu nyingi iliyoniogopesha kama siyo kunikatisha tamaa ya kuendelea kuvuta pumzi ya uhai hapa duniani. Hali yangu ilikuwa ikielekea kuwa mbaya zaidi. Pamoja na ushindi nilioupata sikuwahi kupambana na jitu hatari katika harakati zangu za kijasusi kama lile jitu lenye kila tabia za mnyama. Nilianza kuona kizunguzungu huku wingu zito likianza kutanda kwenye mboni zangu. Nikataka kusimama lakini sikufanikiwa kwani kizunguzungu kilinipelekea nipige mweleka wa aina yake. Hata hivyo akili yangu haikuwa imechoka kiasi cha kushindwa kufikiri juu ya hatima yangu.
Nikiwa pale chini nikaanza kusota taratibu kulifuata lile jitu pale lilipoangukia. Nilipolifikia nikaanza kulipekua lile jitu mifukoni. Kwenye mfuko wa kushoto wa suruali yake ya jeshi nikaikuta bastola aina ya Berreta M9 na magazini mbili zilizojaa risasi. Nikaichukua ile bastola za zile magazini mbili kisha taratibu nikasota kwenye tope hadi katika sehemu moja yenye uchochoro wa jiwe la ukuta wa kile chumba ambapo nilipenyeza mkono wangu na kuificha ile bastola huku nikiugulia maumvu makali sana katika majeraha ya vile visu mwilini mwangu.
Damu nyingi ilikuwa ikiendelea kunitoka kwenye yale majeraha hali iliyonipelekea nizidi kusikia kizunguzungu. Hatimaye nikayaacha yale maficho ya bastola na kusota kwenye lile tope sakafuni kuelekea kwenye ile meza waliokuwa wameketi wale makamanda wa jeshi pale awali. Hata hivyo sikufanikiwa kwani nilikuwa nimepoteza damu nyingi sana na hali yangu ilikuwa mbaya. Kizunguzungu kilikuwa kimenizidi kufuatia kupoteza damu nyingi kwenye yale majeraha mwilini. Sikuweza tena kuendelea na safari yangu baada ya kuona giza zito likitanda kwenye mboni zangu, nguvu zikaniishia taratibu nikajilaza chini bila kupenda. Nilijaribu kufungua kinywa changu ili nipige yowe kuomba msaada lakini sikufanikiwa badala yake sauti yangu mwenyewe ilinirudia masikioni kama sauti ya mwangwi usioeleweka. Hatimaye sikuweza tena kuona chochote mbele yangu na kilichofuata baada ya pale sikuweza kufahamu kinachoendelea.
_____
Fahamu zilinirudia kwa haraka na hapo nikapiga chafya mara tatu kisha nikafumbua macho yangu taratibu nikiyatembeza huku na kule. Mara hii nilishtuka zaidi baada ya kujiona kuwa nilikuwa juu ya kitanda cha chuma chenye godoro kuukuu lenye madoa makavu ya damu bila foronya. Nilikuwa kwenye chumba kidogo bila dirisha, upande wa kulia wa kile kitanda kulikuwa na meza fupi chakavu ya mbao, juu ya meza ile kulikuwa na beseni dogo la aluminium lenye vifaa vyote muhimu vya Tibba kama mikasi, bandeji, dawa ya kukaushia vidonda, vidonge vya kutuliza maumivu, mabomba ya sindano, kisu kidogo cha kupasulia mgonjwa wakati wa oparesheni, koleo, glovu na dawa nyingine ambazo sikuzifahamu. Hata hivyo vitu vile tayari vilikuwa baadhi vimetumika kwa namna vilivyokuwa vimefunguliwa.
Nilipoyapeleka macho yangu kutazama upande wa kushoto hapo nikaona stendi ndefu ya chuma ya kitabibu iliyotundikiwa chupa mbili za dripu, chupa moja ya dripu ya maji na nyingine dripu ya damu. Macho yangu yakapata uhai kidogo na nilipoichunguza milija ya zile chupa za dripu nikagundua kuwa zote sindano zake zilikuwa zimechomekwa kwenye mkono wangu wa kushoto.
Haraka nikataka niinuke na kuketi kitandani lakini hilo lilishindikana kwani miguu yangu na mkono wangu wa kushoto uliotundikiwa dripu ilikuwa imefungwa kwa pingu zilizofungwa kwenye pembe za kile kitanda cha chuma.
“Hapa ni wapi?”. Nikajiuliza huku hofu ikiniingia taratibu. Maumivu makali yakaanza kusambaa mwilini sambamba na kichwa kuuma. Nilipojichunguza vizuri nikagundua kuwa nilikuwa nimefungwa bandeji mkononi, mgongoni na pajani. Loh! na hapo ndiyo nikakumbuka vizuri juu ya mambo yote yaliyonisibu wakati nikipambana na lile jitu lenye nguvu za ajabu na hatimaye kuliangamiza. Hata hivyo nilipopeleleza vizuri nikagundua kuwa mandhari yale yalikuwa tofauti na kule kwenye kile chumba nilichopambana na lile jitu.
Hiki kilikuwa chumba kidogo sana hata paa lake lilikuwa fupi sana. Mle ndani hapakuwa na taa ya umeme isipokuwa taa moja ya kandili iliyokuwa juu ya ile meza ya kitabibu pembeni ya kile kitandani nilicholazwa. Mle ndani hapakuwa na mtu yeyote mwingine. Wakati nikizidi kupeleleza mandhari yale kwa macho nikaanza kusikia njaa kali tumboni.
Fahamu ziliponirudia vizuri nikakumbuka kuwa mara ya mwisho nilikuwa nikisota kuelekea kwenye ile meza ya kile chumba nilichopambana na lile jitu. Nikakumbuka kuwa sikuwa nimefanikiwa kuifikia ile meza pale fahamu zangu ziliponitoka baada ya kuzidiwa na kizunguzungu kikali.
Wakati nikiendelea kuwaza pale juu kitandani mara nikasikia mlango wa kile chumba ukifunguliwa nyuma yangu kisha kukafuatia na sauti ya vishindo vya miguu ya watu ambao idadi yao sikuifahamu haraka hadi pale watu hao waliponifikia pale kitandani na kunizunguka. Sikutaka kujitia kuwa bado sijarudiwa na fahamu kwa vile nilikuwa na njaa sana hivyo nilihitaji chakula vinginevyo matibabu yale yasingekuwa na maana yoyote kwani hali yangu ingezidi kuwa mbaya.
Wale watu walipoingia mle ndani wakakizunguka kile kitanda wakinitazama kwa shauku. Sikutia neno lolote badala yake nikayatembeza taratibu macho yangu kuwatazama na kwa kufanya vile nikamtambua mtu mmoja tu miongoni mwao ambaye alikuwa ni yule daktari mbilikimo aliyekuwa ameongozana na wale makamanda wa jeshi kwenye kile chumba tulichokuwa na mateka wengine pamoja na Kepteni Amadou Coulibary Sidibe. Wale wanaume wengine sura zao zilikuwa ngeni kabisa machoni mwangu na walikuwa wamevaa kiraia ingawa nilipowachunguza vizuri nikajiridhisha kuwa walikuwa ni maafisa usalama wa serikali ya Burundi. Wale maafisa walikuwa na sura za kazi na hakuna hata mmoja kati yao aliyeonekana kuwa rafiki. Wale maafisa usalama wakaendelea kunitazama kwa makini pale kitandani huku wakionekana kuridhishwa na maendeleo ya afya yangu. Hatimaye mmoja wao akageuka na kumuuliza yule daktari mfupi kando yake.
“Tunamuhitaji kwa mahojiano mafupi”. Yule afisa usalama akaongea kwa kujiamini huku akimtazama yule daktari na hapo nikajua mtu aliyekuwa akihitajika kwa mahojiano nilikuwa mimi. Hata hivyo sikutia neno lolote.
“Hali yake bado haijatengamaa vizuri, anahitaji siku moja zaidi”. Tule daktari akajibu huku akizitazama kwa makini zile chupa za dripu.
“Kwanini siku moja zaidi?”’. Afisa usalama mwingine akauliza huku akigeuka na kumtazama yule daktari kwa udadisi.
“Mwili wake bado ni dhaifu na amepoteza damu nyingi mwilini. Siku moja zaidi atakuwa amemaliza dripu zote na kupata afueni kama hali yake haitobadilika”. Yule daktari akaitetea taaluma yake na hivyo kunipelekea nifurahi kimoyomoyo.
“Kesho usiku tutakuwa hapa kumchukua hatuwezi kusubiri zaidi. Huyu mtu anataarifa muhimu tunazozihitaji”
“Sawa!”. Daktari yule akaitikia bila kutia pingamizi huku akigeuka na kunitazama kabla ya kuniuliza.
“Vipi unaendeleaje?”
“Nina njaa sana naomba chakula”
“Vipi kuhusu maumivu ya kichwa?”. Yule daktari akaniuliza huku akiyakagua majeraha yangu mwilini.
“Naombeni chakula tafadhali vinginevyo nitafia humu ndani”. Nikaendelee kuwasihi wale watu. Yule daktari hakusema kitu badala yake akafungua droo ya meza iliyokuwa kando ya kile kitanda mle ndani na hapo akatoa chupa ya chai na kikombe cha bati. Nikamuona akiifungua ile chupa na kisha kumimina uji mwepesi wa moto kwenye kile kikombe cha bati na kunipa. Nikakipokea kile kikombe kwa pupa na kuanza kuunywa ule uji wa kwa papara pasipo kusubiri upoe. Ulikuwa uji wa moto sana, mwepesi na usiokuwa na chumvi wala sukari hata hivyo kwangu ilikuwa afadhali. Nikabugia vikombe vinne na nilipomaliza mdomo wangu ulikuwa umeungua vibaya na kusababisha vidonda.
“Endelea kupumzika zaidi utapata nafuu”. Yule daktari akanisisitiza baada ya kumaliza kunihudumia na hapo yule daktari na wale maafisa usalama wakatoka nje ya kile chumba na kufunga mlango. Mle ndani nikabaki tena mpweke huku mawazo mengi yakipita kichwani mwangu nikawa nikizikumbuka sura za wale maafisa usalama waliotoka kuniona muda mfupi uliopita.
Usiku ule sikuweza kupata usingizi badala yake mawazo yangu yalijikita katika kufikiria juu ya hatima yangu mle ndani. Mwisho wangu niliuona ulikuwa karibu kuliko nilivyofikiria hata hivyo niliendelea kumuomba Mungu. Nikameza funda kubwa la mate na kujilaza vizuri huku macho yangu yakitazama darini.
_____
Asubuhi ya siku iliyofuata yule daktari mfupi alikuja tena kunijulia hali na kuniletea kiamsha kinywa cha uji mwepesi wa mahindi uliokolezwa pilipili za kunikomoa, usiyotiwa chumvi wala sukari. Hata hivyo sikuwa na namna ya kufanya hivyo nikakaza roho na kuunywa uji ule huku nikifahamu kuwa nilihitaji nguvu mwilini ili kukabiliana na mateso makali dhidi ya wale maafisa usalama wa Burundi usiku ule kama walivyoniahidi. Japokuwa mwili wangu bado ulikuwa dhaifu lakini nilikuwa nimepata nafuu kiasi cha kuweza kunipa matumaini.
Wakati nilipoitazama saa ya mkononi ya yule daktari nikagundua kuwa ilikuwa ikielekea kutimia saa moja asubuhi vinginevyo giza la milele la mle ndani bado lingekuwa fumbo kubwa la majira yale kwangu.
Yule daktari akamaliza kunihudumia na kunifunga tena vidonda vyangu halafu wakati akijiandaa kuondoka nikamuona akinitazama kwa kunihurumia sana kama mtu aniambiaye buriani na hali ile ikanizidishia mashaka.
“Usiku wa leo utaenda kuhojiwa na pengine huo utakuwa ndiyo mwisho wako”. Yule daktari akanidokeza kwa sauti ya chini ili walinzi wawili makomandoo wa jeshi waliokuwa wamemsindikiza na kuishia nje ya mlango wa kile chumba wasimsikie. Hazikuwa taarifa za kuniogopesha hata kidogo kwa vile wale maafisa usalama walikwisha gusia juu ya mahojiano hayo wakati waliponitembelea siku ya jana. Kitu kilichonivutia ilikuwa ni hali ya huruma ya yule daktari mfupi na namna alivyonitazama.
“Nitaenda kuhojiwa wapi?”. Nikauliza kwa kunong’ona huku nikimkazia macho yule daktari.
“Humu humu ndani lakini sifahamu ni wapi”
“Kwanini unasema baada ya mahojiano hayo ndiyo utakuwa mwisho wangu?”
“Wamepanga kukuua”. Yule daktari akaongea kwa huruma na taarifa ile ikapelekea koo langu likauke kwa hofu.
“Unaweza kuniambia hapa ni wapi?”
“Hata mimi sipafahamu”. Yule daktari akanong’ona na kunishangaza.
“Kwa vipi?”. Nikamuuliza yule daktari kwa mshangao.
“Ninapoletwa humu ndani huwa nafunikwa machoni na ninapoingia humu ndani huondolewa kitambaa machoni ili nisifahamu hapa ni wapi”. Yule daktari akanong’ona huku akimalizia kufunga bandeji kwenye jeraha langu pajani.
“Najitaji msaada wako tafadhali”. Nilinong’ona.
“Msaada gani?”. Yule daktari akaniuliza kwa udadisi.
“Wapelekee ripoti wakubwa zako kuwa hali yangu imebadilika na kuwa mbaya ili leo wasiweze kunihoji nipate nafuu zaidi”. Nilijaribu kumshawishi yule daktari nikipanga kuununua muda wakati nikifikiria namna ya kutoroka lakini haraka daktari yule akatikisa kichwa chake kuonesha kukataa.
“Nina mke na watoto na wote wananitegemea. Sitaki kuiacha familia yangu yatima”. Yule daktari akanong’ona kisha akamalizia kazi yake.
“Muombe Mungu wako”
Yule daktari akaniaga kisha akaelekea mlangoni ambapo aliufungua na kutoka nje. Ule mlango wa kile chumba ulipofungwa nikasikia vishindo vya miguu vikiyoyoma na hatimaye kutoweka kabisa eneo lile na hapo mle ndani kukawa kimya.
_____
Nilikuwa nimepitiwa na usingizi mzito kitandani wakati niliposhtushwa na kelele za kufuli za mlango wa kile chumba zikifunguliwa kwa papara. Nilikuwa nimelala usingizi mtamu kuliko siku zote za maisha yangu, usingizi ulionipelekea niyasahau masaibu yote niliyowahi kupitia. Lakini hofu ya kifo cha kinyama sasa ilikuwa imeziteka haraka hisia zangu baada kushtushwa na kelele za funguo zikitekenya kufuli za mlango wa kile chumba.
Mlango wa kile chumba ulipofunguliwa wanaume saba wakaingia kibabe mle ndani lakini yule daktari mfupi hakuwepo miongoni mwao. Wanaume watatu kati ya wale niliwakumbuka kuwa walikuwa ni wale maafisa usalama walionitembelea siku ya jana. Wanaume wanne waliosalia walikuwa ni wanajeshi makomandoo ambao niliwatambua haraka kufuatia sare zao za kijeshi. Walikuwa wanaume vipande wenye sura za kazi wanaonuka ubabe, yaani watu wanaofurahia vita kuliko amani.
Watu wale walipoingia mle ndani hawakunisemesha kitu badala yake wakanizunguka haraka pale kitandani kisha mmoja wao akaanza kunifungua zile pingu miguuni na mkononi. Wakati zoezi lile likiendelea mara nikamuona komandoo mmoja akichomoa sindano za dripu katika mishipa yangu mkononi pasipo kuzingatia utaalam wa kidaktari na hivyo kunisababishia maumivu makali hata hivyo yule mtu hakuonekana kujali. Yule mwenzake alipomaliza kunifungua pingu makomandoo wawili wakanishika miguu yangu na kunishusha kwa nguvu pale kitandani. Nilipoangua chini wakaanza kuniburuta kibabe kuelekea nje ya kile chumba na wale maafisa wakawa wakifuatia kwa nyuma…ITAENDELEA