GISENYI
VI
Baada ya kupata habari hizi
walikubaliana kuitisha mkutano wa
dharura mnamo saa sita na nusu
mchana. Rais alipiga simu tena kwa
Jenerali Bunyenyezi na kumwambia afike
ofisini kwake haraka akiwa pamoja na
kiongozi wa upinzani wa Zaire, aliyekuwa
akiunganisha vyama vyote vya upinzani
na ambaye askari wake waliwahi
kupigana vita bega kwa bega na majeshi
ya RPF, wakati wa mapambano dhidi ya
Serikali ya Rwanda ili wapate uzoefu
kutoka kwao. Bwana Mpinda ambaye nae
alikuwa mjini Kigali kwa mazungumzo.
Haikuchukua zaidi ya saa moja wote
walifika ofisini kwa Rais.
"Bwana Mpinda karibu sana. Nimekuita
pamoja na Kamanda hapa ili tuzungumze
kama uliyonieleza juzi, maana naona hali
imegeuka, sasa inakupendelea wewe",
Rais alicheka kidogo na wote
wakatabasamu.
"Asante sana Mheshimiwa Rais,
nashukuru Mungu, kama umegeuza
uamuzi wako na uko tayari kutuunga
mkono sisi", Mpinda alijibu.
"Kama nilivyosema naona hali
inakupendelea, kuna mambo ambayo
yametokea na kuashiria tulifikirie kwa
makini ombi lako. Askari wako wote bado
wako kwenye ardhi ya Rwanda?", Rais
aliuliza.
"Hapana Mheshimiwa, wengine wengi
bado wapo lakini baadhi yao wamevuka
wapo mpakani, wakisaidia kufundisha
jeshi la Wabanyamulenge", Mpinda
alimwambia Rais.
"Kamanda Bunyenyezi, nataka basi
ufanye mpango na kiongozi wa
Banyamulenge nae awepo kwenye
mkutano wa saa sita na nusu", Rais
aliagiza.
"Na hilo tumelifikiria, na Col. Rwivanga
ameshatuma Helikopita kwenda
kumchukua", Kamanda Bunyenyezi alijibu.
"Oh, vizuri sana. Sasa bwana Mpinda
unakaribishwa kwenye kikao saa sita na
nusu, na naomba ujieleze vizuri, na kama
ukiweza kuwashawishi mawaziri na
makamanda wangu, basi utakuwa
umefanikiwa. Hii ni nafasi nzuri sana
kwako kwani na sisi sasa tunalazimika
kutumia mpango wako ili nasi tukidhi
lengo letu. Hivyo, kazi kwako
kukishawishi kikao kama kweli una
mipango thabiti ya kuweza kufanya kazi",
Rais alimalizia.
"Mheshimiwa Rais, naenda kukaa na
makamanda wangu, na kwa vile viongozi
wa Banyamulenge nao watakuwepo na
wako upande wenu na wetu, basi naamini
nitaweza kukiridhisha kikao kuwa tuko
tayari kufanya kweli", Mpinda alijibu.
"Haya Bwana Mpinda kwa heri. Kamanda
Bunyenyezi, wewe ngoja kidogo".
Walimtoa nje Bwana Mpinda na
wakamrudisha kwenye nyumba ya wageni
ya Serikali alikokuwa amefikia na
makamanda wake. Rais na makamanda
wake walipobaki nyuma, walitafakari
swala zima kwa undani. Wakaangalia jinsi
ambavyo wangeweza kufaidika kwa
kuwatumia wapinzani wa Serikali ya Zaire
ili waweze kutimiza lengo lao kuwaondoa
Intarahamwe na Wahutu wote wenye
siasa kali pale mpakani kwao ili wasije
wakaivamia Rwanda, huku bila kulaumiwa
na Jumuia ya Kimataifa kuwa wamevamia
nchi nyingine na kuwaua wakimbizi.
"Nafikiri hii ndio nafasi yetu ya pekee
kumaliza tatizo hili. Kwa hiyo, inabidi
tulieleze kwenye mkutano vizuri",
Kamanda Bunyenyezi alieleza.
"Je, hawa wapinzani na waasi wa
Banyamulenge wakishindwa, itakuwaje?
si siri itavuja?", Rais aliuliza.
"Hilo litakuwa jambo jingine, sisi tutakuwa
tumetimiza lengo letu na tutakuwa
tumewaondoa na kuwamaliza kabisa
hawa Intarahamwe karibu na mipaka
yetu. Tutakuwa tumewatokomeza mstuni
huko Zaire. Shida na wasiwasi kwetu
vitakuwa vimemalizika kabisa. Kazi yako
itabaki kujenga nchi na si kupigana tena",
Kamanda Bunyenyezi alijibu.
"Kweli, sasa tumepata kisingizio; Mungu
yuko pamoja nasi, maana chochote
tungefanya serikali ya Zaire na Jumuia ya
Kimataifa visingetupa nafasi. Basi nenda
kajitayarishe, Mkutano utakuwa mgumu
sana, maana najua mawaziri wengi
itakuwa vigumu kukubali", Rais alijibu.
"Asante Mheshimiwa Rais, nafikiri
watatuelewa kwa sababu hii ni kwa faida
ya Taifa la Wanyarwanda ambalo
limeteseka sana, lazima wananchi wapate
muda wa kupumua na si vita kila siku",
Kamanda Bunyenyezi alijibu na
kueondoka kwenda
kujitayarisha.