Riwaya: UCHU

UCHU
SURA YA KWANZA
ARUSHA II

Musoke aliangalia ndani ya kitabu chake cha
simu, akaipata namba ya Chifu ya nyumbani na
kumpigia simu.
Alipoangalia saa ilikuwa yapata saa tano usiku.
"Hallo", alisikia sauti ya Chifu, ikiwa na nguvu
kama ya kijana wa miaka thelathini.
"Mzee, shikamoo, Musoke hapa".
"Marahaba Musoke, habari za siku nyingi, nini
kinakufaya unipigie simu saa hizi?".
"Umekasirika Mzee?".
"Hapana, shauku".
"Bado tu uko vilevile, utafikiri hujastaafu?".
"Mwili ndio unastaafu lakini nafsi huwa haistaafu
maana nafsi haizeeki isipokuwa mwili".
"Ahsante nitazingatia, huo ushauri, maana nami
naitwa mzee sasa na nafsi yangu imeanza
kukubali".
"Hapana usiruhusu kabisa. Haya, lete habari
zinazokufanya umpigie simu mzee kama mimi
saa hizi kwanza uko wapi?".
"Niko Arusha".
"Aha, nilifikiri uko Kampala".
"Niko Arusha, Chifu". Ilikuwa ukimwita Chifu
mara moja anajuwa kazi imeanza.
"Haya lete hizo habari".
Musoke alimweleza habari zote toka mwanzo
mpaka mwisho. Pia alimweleza jinsi idara za
upelelezi za serikali zilivyokataa kumsaidia kwa
kitu nyeti kama hiki.
"Pole sana", Chifu alimjibu baada ya kuyasikia
yote.
"Tatizo lako ni kubwa, la kuangaliwa kwa makini
sana. Mimi mwenyewe nimekuwa nikishangazwa
sana na mambo yalivyo Rwanda. Enzi zetu sisi
tusingeruhusu hali kama hiyo itokee, wewe
mwenyewe unajuwa msimamo wetu ulivyokuwa".
"Ndio Chifu, lakini serikali zetu za sasa kila mtu
eti na nchi yake, eti hiyo ndio wanaiita
demokrasia", Musoke alijibu.
Wakati wanazungumza kwenye simu mawazo ya
Chifu yalikuwa yanakwenda kama Kompyuta
kutafuta nani angeweza kumsaidia Musoke na
Chama chake cha PAM katika azma yao ya
kutafuta kiini cha matatizo ya Rwanda. Chifu
mwenyewe alikuwa mwana PAM, na aliamini
Umoja katika Afrika.
"Jack", Musoke alishituka kusikia Chifu akimuita
kwa jina lake la kwanza. Hii ilikuwa na maana
amekwisha pata jawabu. "Nafikiri nitakupatia
ufumbuzi wa tatizo lako. Mtu mmoja tu katika
Afrika hii ambaye anaweza kuifanya kazi yako.
Hivi sasa ameacha kazi za kiserikali maana
ameowa na anafanya shughuli zake. Lakini
kutokana na imani yake katika Umoja wa Afrika
anaweza akaifanya kazi hii, huna haja ya kuwa
na kikosi, maana yeye pekee ni kikosi.
Nitazungumza naye, nipe namba yako ya simu
na chumba chako; nitakupigia simu kesho
asubuhi".
"Ahsante Chifu, nilijuwa wewe ndiye
utakayenimalizia matatizo yangu", Musoke
alijibu kisha akampa namba ya simu ya pale
hotelini na namba ya chumba. Alipomaliza tu
akasikia simu ikikatwa. Akajuwa tayari Mzee
yuko kazini.
Chifu alipokata simu ya Musoke, alipiga simu
nyingine.
"Hallo".
"Chifu".
"Aha shikamoo".
"Marahaba, tuonane kusho asubuhi,
tutastafutahi pamoja pale Kili, kama kawaida.
"Sawa Mzee, kesho", Chifu alijibiwa.
"Kesho, ahsante", Chifu alijibu na kukata simu.
ITAENDELEA...
 
UCHU

SURA YA PILI

KAZI KWAKO

"Umesikia George Foreman amerudi ulingoni na
kutwaa ubingwa", Chifu aliuliza.
"Sikusikia tu, nimeona kwenye televisheni".
"Basi na wewe nataka urudi ulingoni", Chifu
anasema kwa tabasamu huku akiupaka mkate
wake siagi.
"Mimi! mimi nimeoa na mke wangu ana mimba.
Mchezo huo sifanyi, sifanyi ng'o".
Chifu anaangua kicheko kiasi cha kuwafanya
watu wote ndani ya chumba cha mkutano
wamwangalie.
"Kwani mimi sijui umeoa! Kwani mimi sijui mke
wako ana mimba! Najua, lakini nakutaka
ulingoni tena. Kwani George Foreman hana mke,
hana watoto, mbona karudi ulingoni", Chifu
aliendelea kusema kwa kebehi.
"Huenda alikuwa anataka pesa, huenda alikuwa
anatafuta sifa, mimi sitaki vitu vyote hivyo, sirudi
ng'o", Chifu alielezwa kwa busara.
"Sikiliza nikueleze kwanza. Mimi ndiye
niliyekuruhusu uache kazi na kukushauri uoe na
nisingependa uharibu ndoa yako. Najua
unampenda sana mkeo, sasa nasema nisikilize
kwa makini nikueleze, kama utakataa itanibidi
niingie mimi mwenyewe ulingoni", Chifu alijibu
kwa masikitiko kiasi cha kumfanya mwenzake
apoe hasira zake.
"Chifu, hebu nieleze kuna nini? Kitu cha maana
namna hiyo, kiasi cha kusema utafanya kazi
hiyo mimi nisipokubali? Unajua mimi siwezi
kukuruhusu wewe kufanya hivyo.
"Basi sikiliza".
Ilimchukua Chifu saa nzima kumweleza suala la
Rwanda na jinsi msimamo wa PAM
ulivyohusiana pamoja na vipengele vingine vingi
ambavyo hata akina Musoke wasingeweza
kumweleza maana hawavijui.
"Unafikiri Serikali ya sasa ya huko haiwezi
kufanya kazi hiyo", Chifu aliulizwa.
"Haiwezi. Inahitaji ujuzi wa hali ya juu kufanya
kazi hiyo, katika hali ya machafuko namna ile,
maana hata wao hawajui nani ni nani katika
nchi yao. Hawamwamini mtu yeyote na wao
hawaaminiki vilevile na kuweza kupata habari za
kina kama zinavyotakiwa, unahitajika ujuzi wa
juu sana. Na katika Afrika nzima kama si wewe
basi itanibidi mimi mwalimu wako nikaifanye.
"Umenipa mtihani mkubwa sana. Unafikiri kazi
kama hii inaweza kuchukua muda gani?".
Chifu alipoulizwa swali hili, moyo wake ilitulia
akijuwa kazi itafanywa.
"Inategemea na wewe mwenywe, wiki moja au
mbili, mwezi yote yategemea wewe. Kwani Pepe
atajifungua lini?".
"Bado ana miezi miwili".
"Nakutakia heri. Nafikiri utamaliza kazi kabla ya
hapo. Tafadhali, hafadhari iwe kitu cha kwanza
kwako maana huko kuna hatari nyingi, usifanye
mchezo kama unataka kumwona mtoto wako",
Chifu sasa alikuwa amebadilika na kumwasa
mwenzake.
"Nikifa utamlea wewe", Alijibu.
"Sasa nina miaka sabini, nitamlea miaka
mingapi mie", Chifu alijibu.
"Wewe ndiye uliyetaka, shauri yako, damu yangu
itakuwa juu ya kichwa chako".
"Pole sana. Ndege ya Shirika la Ndege Tanzania
inaondoka saa tano na nusu kwenda Kilimanjaro.
Tiketi hii hapa, umepatiwa nafasi kwenye ndage
hiyo. Musoke mtaonana uwanja wa ndege,
atakuja kukupokea, si unamfahamu?".
"Ndio, namfahamu".
"Haya kwa heri. Ukirudi toka Arusha, kabla ya
kwenda Kigali, njoo unione nitakuwa tayari na
taarifa za kukusaidia kule".
"Asante, nitafanya hivyo.
Chifu alilipa wakaondoka.

ITAENDELEA
 
Naomba Willy Gamba 1 uingie jikoni huyu jamaa anaweza kuacha watoto wafe njaa.
 
Back
Top Bottom