Saturday, June 27, 2015
Imechapishwa na Maseypr kwa 7:17 AM
TUTARUDI NA ROHO ZETU?
SURA YA NANE
Katika Jumba fulani, mtaa fulani, katikati
ya jiji la Johannesburg, Nchini Afrika
Kusini, Makaburu wanne waliketi katika
ofisi moja wakisikiliza taarifa za kijasusi
kutoka Tanzania. Jasusi mmoja alikuwa
akiwataarifu kwa kutumia chombo
maalumu juu ya msafara wake na
mafanikio ya kazi zake.
"Nimefika salama na kuwakabiri nikiwa
katika hali ya kusikitisha iliyowafanya
waniamini kama mmoja wao. Wameumeza
kabisa uongo wangu. Sasa wananiamini
sana. Wameniuliza mwaswali mengi na
nimewajibu kiume nikiwapa taarifa za
uongo. Nadhani wamekusudia kuwatuma
wapelelezi wao huko, ingawa
hawakupenda kunishirikisha moja kwa
moja. Hata hivyo msijali, nitakuwa macho
kutoa taarifa sahihi hatua baada ya
hatua..."
Makaburu wakatazamana tena na
kutabasamu kwa namna ya kupongezana.
Mmoja wao hakuona kama tabasamu
linamtosha. Yeye aliangua kicheko. Kisha
aliona kicheko hakitoshi. Akainuka na
kuliendea kabati lililokuwa nyuma yake
ambamo alitoa chupa kubwa ya pombe
kali aina ya John Walker na glasi nne.
Akazileta mezani na kuziweka mbele ya
kila mmoja. Akafungua na kumimina.
"Labda tusherehekee ushindi". Baadae
akaongeza, "Sitoi ruhusa ya kunywa ofisini
isipokuwa inapobidi kufurahi. Mwanadamu
hana budi... Cheers..."
Kaburu huyu kwa jina aliitwa Von Iron, kwa
sura hakutofautiana sana na mtoto
mchanga ingawa kwa umbo alikaribiana
na kiboko aliyeshiba vizuri. Yeye ndiye
aliyekuwa kiongozi wa kamati hii maalumu
ya BOSS ambayo iliundwa kuzishughulikia
kikamilifu nchi za kiafrika 'zinazojitia
kichwa ngumu'. Amekuwa Mkurugenzi
Mtendaji wa shirika hili la kijasusi tangu
lilipoundwa miaka mingi iliyopita. Mara
kwa mara kazi yake imekuwa nzuri kwa
wakubwa zake. Haikupata kutokea
mpango aliouandaa yeye ukashindwa
kutoa mafanikio. Jambo ambalo lilimpa
hadhi na heshima machoni mwa watu
weupe na kumfanya jazanda ya mauti
katika fikra za weusi. Ni yeye aliyebuni
uwezekano wa kuitumia nguvu ya nyuklia
kuwaangamiza Waafrika.
Hakuwa Mwanasayansi, lakini alipewa
jukumu la kushirikiana nao, akiwa na
uhuru wa kutumia kiasi chochote cha pesa
hadi majaribio yalipofanyika na kutoa
matunda ya kupendeza. Kadhalika mi yeye
aliyebuni mpango wa kuwawekea ngozi
nyeusi baadhi ya wapelelezi wao, kwa
kupoteza pesa nyingi katika hospitali
zinazofanya Plastic Surgery. Wapelelezi
hao waliingizwa kwa hila katika vikundi
vya wapigania uhuru na kujifanya wenzao
huku wakitoa siri zote hata kuua inapobidi.
Mmoja wa watu hawo ni huyu aliyekuwa
akiwafurahisha sana kwa taarifa zake
kutoka Tanzania. Yeye alifanya mabadiliko
ya ngozi yake miaka mitano iliyopita,
akawa mweusi na kutibua mambo mengi
katika vyama vya SWAPO na ANC.
Majuzi alirudishwa Ulaya ambako
alirudishiwa ngozi ya mtu mweupe usoni
na mikononi, kisha akatumwa Tanzania
ambako waliona ni chimbuko la
misukosuko yote dhidi ya utawala wa
makaburu, na hasa wajue nini kinafanyika
katika kutapatapa kwa Serikali na
wananchi wa Tanzania juu ya mtambo wao
wa aina yake ulioko angani baada ya
kutoeleweka kilichomtokea mtu wao
Chonde hata akafa katika hoteli ya New
Afrika. Zaidi huyu alikuwa amepewa akiba
ya kutosha ya zile gololi zinazouongoza
mtambo huo kulipua miradi teule ili wakati
utakapowadia waachie hili walilokusudia
kulifanya, "Pigo la mwisho".
Umaarufu wa Von Iron dhidi ya ngozi
nyeusi ulikuwa umechipua katika roho
yake tangu utotoni baada ya kuzaliwa na
kukulia katika familia ya kitajiri ambayo
iliwatenda waafrika kama wanyama.
Hayati baba yake mzazi alikuwa na mgodi
wa dhahabu, watumishi wake walikuwa
wakifanya kazi na kulipwa ujira hafifu mno
kiasi cha kuwafanya washindwe kuyamudu
maisha, jambo ambalo hakuna
aliyeonekana kulijali, hata ikajengeka
katika fikra za Von kwamba mtu mweusi ni
chombo cha mtu mweusi ambacho hakina
haki wala thamani.
Halafu yakatokea maafa katika mgodi.
Baba yake alikuwa katika moja ya ziara
zake adimu wakati ilipotokea hitilafu hii
ambayo hadi leo chanzo chake
hakijafahamika. Hitilafu ambayo
ilisababisha maafa makubwa kwa
wafanyakazi wengi, weusi kwa weupe.
Hayati Iron mwenyewe aliponea
chupuchupu. Kama asingejitokeza
mtumishi wa Kiafrika, mzee mkongwe,
ambaye alitumia nguvu zake zote kumtoa
katika chumba ambacho kilikuwa
kimefunikwa na mawe, siku hiyo
angeyapoteza maisha yake kutokana na
majeraha mabaya aliyopata. Vifo hivyo
vilimsikitisha sana mzee Iron hata
akajitolea kuishi na mtoto pekee wa mzee
huyo ambaye alikuwa msichana mzuri,
ingawa uzuri huo ulipotoshwa na unyonge
aliokuwa nao rohoni. Uamzi wa Iron kuishi
na Mwafrika katika nyumba moja, likiwa
jambo geni sana wakati huo, ulileta
mgogoro mkubwa sana kwa familia yake,
hasa mkewe. Lakini hilo Iron hakulikubali
asilani. Badala yake akazidisha mapenzi
kwa msichana huyo huku akiahidi
kumpeleka masomoni nje ya nchi.
Halafu ikatokea mzee Iron akafumaniwa
na msichana huyo. Ilikuwa habari iliyojaa
aibu kubwa masikioni mwa kila mtu
mweupe. Lakini Iron hakuona aibu.
Alikitetea kitendo chake na kukataa
matakwa ya mkewe kwamba msichana
huyo yatima afukuzwe. Hata mkewe
alipotishia kujiua Iron hakukubali kumtupia
msichana huyo lawama ambazo
hazikumstahili. Ikatokea tena.
Wakafumaniwa kwa mara ya tatu. Hapo
mkewe hakustahamili zaidi. Alirudi
chumbani ambako alichukua bastola na
kumwua msicha yule mweusi. Mzee Iron
alizirai kwa hasira. Fahamu zilipomrudia
alipokonya bastola hiyo kutoka mikononi
mwa mkewe na kumpiga risasi mbili
kifuani. Kisha akajilenga kifuani na
kujifyatulia risasi zote zilizokuwa
zimesalia. Vifo hivyo vilizusha simulizi
kubwa mitaani kwa muda mrefu.
Vilimwacha Von katika msiba wa uyatima.
Msiba ambao ulizaa hasira zaidi kwa mtu
mweusi, akijua kuwa ni mtu mweusi
aliyemnyima haki ya kuwa na wazazi.
Jambo ambalo lilimfanya siku zote awe
mstari wa mbele katika kutukuza na
kutekeleza taratibu zote za ubaguzi. Daima
alikuwa mkatili, kuliko wakatili, mnyama
kuliko wanyama dhidi ya mtu mweusi.
Matokeo yake yakawa kupata vyeo
ambavyo vilimwezesha kuwa na mamlaka
juu ya uhai na kifo kwa kila mtu mweusi
katika shirika hili la kijasusi. Wengi
waliuawa kwa ajili yake, mengi yaliendelea
kufanyika ili kumkomoa mtu mweusi
kutokana na mapendekezo yake. Lakini
hakukoma kuendelea kubuni. Mtambo
uliokuwa angani ukisubiri kuiharibu Afrika
huru ulikuwa moja tu kati ya ubunifu wake.
Pamoja na kuwatendea mengi ya kikatili,
pamoja na kuhakikisha kuwa weusi wengi
wasio na hatia wakipoteza maisha yao
kwa kuuawa, bado Von hakuona kama
viumbe hawa walielekea kumpigia mtu
mweusi magoti. Badala yake alishangaa
kuona weusi wakiendelea kusimama kiume
wakitetea haki yao. Alipokufa huyu
alizaliwa huyu, wimbo uleule ukiwa
midomoni. Hata Mandela ambaye alikuwa
kifungoni, alipoteswa bado alikuwa na
msimamo uleule. Hilo kiasi fulani lilimtisha
sana kaburu Von. Hakuwaelewa kabisa
watu hawa. Wana nini katika damu zao?.
Swali hilo lilikuwa likimletea maswali
mengine ambayo yalijenga hisia fulani.
Maswali yaligongana kichwani mwake.
Alijiuliza baba yake alikuwa ameona nini
katika nywele kavu, ngozi nyeusi na sura
ya kusikitisha ya yule msichana wa
Kiafrika hata akadiriki kumwua mkewe na
kujiua mwenyewe! alisikia hadithi ya mtu
mwingine ambaye alimwacha mkewe na
kukimbia na msichana mweusi hadi
Marekani ambako walifunga ndoa. Wana
nini watu hawa? Iko siri gani ndani ya
ngozi zao zinazotisha? Labda ingebidi
alifumbue fumbo hili kwa kumpata mmoja
ili aonje? Lakini...mweusi... Hapana. Mara
kwa mara aliyafukuzia mbali maswali hayo
ambayo yalimjia bila taarifa hasa
alipoukumbuka uyatima wake.
"Cheers", Von aliropoka tena
Wenzake wakageuka na kumtazama kwa
mshangao. Kisha akatabasamu
kimyakimya wakiendelea kunywa taratibu.
Baada ya vinywaji hivyo, Von aliamua
waendelee na kikao chao.
Walivuta mafaili ya suala la Chonde na
kuangalia wamefikia wapi kuhusu kisa cha
kifo chake na wapi zilielekea mali zake.
Bado haikueleweka nani alimuua Chonde
na maiti ya pili chumbani mle
haikujulikana ilikuwa ya nani. Zaidi
haikufahamika wapi vilienda vitu ambavyo
alikuwa navyo, ambavyo ni vya hatari na
siri kubwa. Kitu kimoja walikuwa na hakika
nacho. Vitu hivyo vilikuwa havikufika
mikononi mwa polisi. Jambo ambalo
liliwafanya waafiki kuwa watu waliomwua
Chonde na kumwibia pesa nyingi na vitu
alivyokuwa navyo ni majambazi wa
kawaida, ambao wangeweza kuvitupa
vifaa vile muhimu kama takataka na
nyaraka za siri kama uchafu. Ambacho
wangejua kutumia ni pesa za Tanzania na
za kigeni ambazo zingewachukua muda
mrefu kabla ya kuzimaliza.
Pesa lilikuwa si tatizo kwa akina Von.
Walilitupa suala hilo kando bila kinyongo
hasa wakijua kuwa tayari mtu wao
mwingine Clay alikuwa nchini Tanzania
akiwa na kila kitu kilichohitajika akiwa
tayari kwa yote waliyohitaji kufanya.
Alikuwa na nafasi nzuri zaidi ya Chonde
kwani uongo aliokwenda nao ungemfanya,
aonekane kama almasi.
"Nadhani kilichobaki ni kuongeza ulinzi
kwenye mtambo wetu", Von alikuwa
akiendelea. Ingawa Clay yuko kwao na
atatuarifu kila wanachokusudia kufanya,
lakini kuna mengine watakayoshindwa
kumwambia. Ni wazi kuwa watatumwa
wapelelezi waje, lakini itaki warudi.
Nadhani tunaelewana".
Akaungwa mkono.
Mara simu ya dharura ikaanza kulia. Ikiwa
simu ambayo hulia kwa nadira sana, Von
aliinua mkono na kuidaka mara moja. "Von
hapa", akaunguruma katika chombo cha
kusemea.
"Bosi, hapa ni kikosi cha ulinzi wa anga.
Ndege zetu za ulinzi zimeizunguka ndege
moja ambayo ina watu wanne tu. Rubani
na msaidizi wake na abiria wawili ambao
ni mwanamke na mwanaume. Rubani wa
ndege hiyo anamboa kutua, akidai kuwa
ametekwa nyara na abiria hao ambao
wamejitambulisha kama Joram Kiango na
mpenzi wake Nuru. Tunauliza kama
tuwaruhusu kutua au tuwalipue".
"Nani, Joram?" Von aliuliza.
"Ndiyo. Joram Kiango. Yule..."
Mara Von akalikumbuka jina hilo vizuri.
Joram Kiango. Halikuwa jina la kupendeza
hata chembe masikioni mwake, ingawa
siku mbili tatu zilizopita limesikika kwa
namna ya kupendeza kiasi. Joram kuja
Afrika Kusini! Bila shaka ni kujaribu
kujificha baada ya kuibia nchi yake akiba
yote ya pesa za kigeni. Vizuri. Tutampa
hifadhi ya kudumu. Anaweza kujificha
milele katika makaburi yetu. Hatuna roho
mbaya.
"Umesema Joram siyo? Sikia. Huna haja
ya kutumia silaha kubwa kumuu. Anaweza
kufa polepole. Mwambie atue haraka".
ITAENDELEA 0784296253
Notify me
Comment as:
Publish Preview
Create a Link
No comments: