SURA YA SITA
II
Baada ya kuzitawala na kuzinyonya sana
nchi zetu nyingi za Kiafrika, na baada ya
'kutoa' uhuru kwa shingo upande,
Uingereza iliendelea kujifanya kuwa baba
na mama wa makoloni yake ya awali.
Falsafa hii ndio chanzo cha kutoa
vijimsaada kadha wakadha. Eti pia
Uingereza ndio mtaalam wa habari
zinazohusu nchi hizi zilizokuwa chini ya
himaya yake.
Na habari ambazo hupata nafasi katika
vyombo vyao mara nyingi huwa ni zile
ambazo si nzuri sana katika masikio ya
wasikilizaji. Yaani habari za aibu,
kushindwa, rushwa udikteta, uzembe na
kadhalika. Uteuzi huu wa habari hizo
mbovu na kuacha zile nzuri nje yao ni
ushahidi mwingine ambao huonyesha
kuwa Uingereza ingependa kuendelea
kuitawala Afrika hadi mwisho wa dunia.
Habari za wizi wa fedha za kigeni katika
Tanzania zilikuwa tamu mno katika
magazeti, redio na televisheni zote za
Uingereza. Habari hizo zilipambwa kwa
wino na rangi mbalimbali na uongo wa
aina tofauti hata zikawa kubwa kuliko
zilivyostahili kuwa. Hiyo ilitokana hasa na
mwizi wa pesa hizo alivyokuwa mtu
maarufu duniani. "Ndivyo walivyo
waafrika..." liliandika gazeti moja. "Kati yao
hakuna mwaminifu..." Gazeti lingine
lilipendekeza kuwa Tanzania isipate
msaada wowote wa kimataifa bila ya fedha
hizo kurejeshwa. "Tunaamini kilicofanyika
ni njama tu, baina ya Joram na viongozi wa
serikali yake", Televishen moja ilitangaza.
Habari hizi zilianza kuwa za kawaida
machoni na masikioni mwa Joram na Nuru.
Hawakuzijali wala kuzishughulikia. Hata
hivyo kuna gazeti hili ambalo liliwashtua
zaidi. Mwandishi wake alikuwa amesafiri
hadi Dar es Salaam Tanzania ambako
alifanya utafiti wake binafsi, akihonga hapa
na kuiba habari pale hata akawa
ameunganisha taarifa ambayo ilidai kuwa
Joram alikuwa ametorokea Nairobi Kenya
kwa ndege ya kukodi. Mwandishi huyo
alisafiri hadi Nairobi ambako utafiti wake
ulimfikisha katika chumba alichokuwa
Joram na Nuru wakitumia majina bandia.
"Kwa kila hali Joram yuko London hivi
sasa", lilieleza gazeti hilo. "Dunia haiwezi
kupumbazwa na hila zake za kujibadili
sura na umbile. Kwa hila ilivyo Joram
atakuwa akiishi katika hoteli kubwa kwa
jina la bandia.
"Imekuwa tabia ya kawaida", liliendelea
kuandika gazeti hilo. "Kila wanapofanya
madhambi yao huko kwao hukimbilia huku.
London imejaa watu weusi wengi ambao
wanaishi wanavyotaka baada ya kufanya
maovu - au mema ambayo yalionekana
maovu - huko makwao. wako wachoyo,
wahujumu, wazembe, wanafiki na
kadhalika. Wengi wameziacha nchi zao
zikiwa masikini zaidi na huku roho za watu
zikiteketea katika vita na mauaji yasiyo na
mwisho. Uingereza tunawakaribisha na
kuishi nao kama binaadamu wenzetu.
Miongoni mwa watu hawa sasa yumo
Joram Kiango, mtu aliyejifanya na
akaaminika kuwa ana roho ya kipekee
yenye upendo na ushujaa kama ngao kwa
jamii yake. Kumbe alikuwa fisi katika ngozi
ya kondoo. Huyu, Uingereza haiwezi
kumstahamili. Lazima apatikane,
ahukumiwe na kupokonywa kila senti
aliyobaki nayo.
Nuru alimaliza kuisoma habari hii huku
akitetemeka kidogo. Lakini ilimshangaza
alipoinua uso na kukutana na uso wa
Joram ambao ulikuwa ukichekelea. Hilo
lilimshangaza. Akiwa mtu aliyeishi na
Joram kwa kipindi cha kutosha, alikuwa na
hakika kuwa amemfahamu Joram vya
jutosha. Asingelaghaika kama watu
wengine kung'amua lini anacheka kwa
hasira na wakati upi anajifanya kuchukia
wakati amefurahi. Tabasamu hilo ambalo
huutembelea uso huu kwa nadra sana.
Hivyo ilimshangaza sana Nuru.
Alimtegemea Joram kujisingizia kucheka
huku rohoni akibabaika na kukata tamaa.
Si kushangilia kama aliyepata tuzo au
ushindi mkubwa baada ya shindano gumu.
"Sijakuelewa Joram, sidhani kama hii ni
habari njema", Nuru alimwambia Joram.
"Wala sidhani kama una haki ya kutegemea
habari njema tangu ulipokubali
kuandamana na mwizi mkubwa kama
huyu", Joram alimjibu Nuru taratibu.
Alipoona uso wa Nuru bado una maswali
na dalili za kutoridhika, aliongeza,
"Kinachonichekesha ni huyu Mwingereza
anavyojinya ana uchungu na nchi yetu
kuliko sisi wenyewe. Utafiti aliofanya
hautokani na moyo wake wa kuwajibika
bali ni nguvu alizonazo kiuchumi. Uwezo
ambao ameuiba kutoka katika makoloni
yao miaka nenda rudi".
Joram alikohoa kidogo kabla ya kuongeza,
Hawawezi kunitisha kabisa. Nitaishi hapa
nikistarehe katika jiji kubwa ambalo
linapendeza kwa madini yaliyoibiwa kwetu,
yaliyochimbwa kwa jaso la babu zetu.
Nitaondoka hapa tu nitakapokuwa tayari
kuondoka. Sivyo dada Nuru?".
"Ninachosema ni jinsi unavyoifurahia
habari hii badala ya kuionea aibu.
Sikutegemea. Au pengine hili ni fumbo
jingine?". Joram hakumjibu.
Maisha jioni ile yaliendelea kama kawaida.
Joram alijipitisha hapa na pale akifanya hili
na lile. Sasa ilikuwa dhahili shahili kwa
Nuru kuwa alikuwa katika shughuli kubwa
na ngumu kinyume na jinsi alivyoiruhusu
sura na sauti yake kuonyesha. Nuru
hakujisumbua tena kumuuliza Joram lolote
akichelea kupoteza muda wake kwani
ingekuwa sawa na kumpigia mbuzi gitaa
ukimtegemea kucheza rumba. Hata hivyo
Nuru alipopata wasaa mwingine alimkabiri
Joram na kumwambia kwa utaratibu,
"Unadhani mwandishi yule anatania
anaposema watafanya juu chini kututafuta?
Huoni kama tunaweza kukamatwa? Hila
hizi za kujibadili sura si imekuwa
teknolojia ya kawaida siku hizi? Sidhani
kama zinaweza kutusaidia".
"Najua, mpenzi. Ninachojivunia ni wingi wa
watu na ukubwa wa jiji hili. Itawachukua
muda hadi watakapofika hapa na
kutukamata. Wakati huo hatutakuwa hapa
tena, bali tutakuwa angani tukimalizia
kuitembelea nchi ya mwisho ya dunia.
Usijali Nuru. Starehe bila hofu yoyote..."
Joram hakuumaliza usemi wake kabla ya
kuusikia mlango ukigongwa.
Wakatazamana huku wakisikiliza. Mlango
ulipogongwa tena kwa nguvu kuliko
mwanzo. Joram hakuwa mgeni wa
ugongaji wa polisi. Kwa mara ya kwanza
akajikuta kuwa alikuwa amekosea sana
kuwadharau polisi wa Uingereza kiasi
hicho. Akamtumia Nuru jicho ambalo
lilibeba ujumbe ambao masikioni mwa
Nuru ulieleza waziwazi "Cheza nao". Papo
hapo Joram akatoka na kuingia bafuni
huku akiufunga mlango nyuma yake.
Mlango ulipogongwa tena Nuru aliinuka na
kuufungua. Kama walivyotegemea mlango
ulipofunguka aliingia askari mmoja
mwenye cheo cha Sajenti akifuatana na
mmoja kati ya maofisa wa hoteli hiyo.
"Samahani sana dada", afisa huyo alieleza.
"Tumelazimika kukusumbua kidogo.
Nadhani utatuwia radhi. Huyu hapa ni
Sajini Brown kutoka Scotland Yard, yuko
katika ziara ya kuwatembelea wageni wote
wa hoteli hii ili kutazama hati zao za
kusafiria pamoja na kuwauliza maswali
madogo madogo ambayo nadhani
utamjibu. Ni mzunguko wa kawaida tu kwa
ajili ya tukio dogo ambalo wangependa
kulikamilisha ili wasirudi tena katika hoteli
hii".
"Bila samahani", akimgeukia yule polisi
ambaye wakati huo alikuwa akitoa
kitambulisho chake.
"Kwa kawaida hapa kwetu hatupendi
kusumbua wageni", alieleza askari huyo.
Tunatimiza ombi la INTERPOL tu", alisita
akamtazama Nuru kwa makini zaidi. Sijui
dada unaitwa nani?".
"Mrs Prosy Godwin".
"Kutoka?"
"Naijeria".
"Yuko wapi bwana Godwin?"
"Ametoka, nadhani atarudi baada ya dakika
chache".
"Naweza kuona hati zenu za kusafriria
pamoja na nyaraka zingine kama zipo?"
"Bila shaka", Nuru alimjibu huku akiuendea
mfuko ambao aliufungua na kutoa hati.
Akazikabidhi kwa askari huyo ambaye
alianza kuzipekua.
Dakika hiyo hiyo mlango wa bafuni
ulifunguka. Askari alipogeuka kutazama
alikutana na pigo lililokusudiwa
kumumaliza, lakini halikutimiza wajibu
wake. Pigo hilo lilimfanya apepesuke na
kuegemea ukuta. Mkono wake ukapaa
kukinga pigo la pili huku mkono wake wa
pili ukisafiri haraka kuitafuta bastola yake.
Joram hakuruhusu mkono huo utoke na
bastola. Aliachia judo ambayo ilitua
ubavuni mwa askari huyo na kumlegeza.
Pigo lililofuata lilimlazimisha kuanguka
sakafuni. Baada ya kazi hiyo ndipo Joram
alipomgeukia afisa wa hoteli ambaye
wakati huo alikuwa ameduwaa, mdomo
wazi, kama asiyeyaamini macho yake.
"Mwinue ndugu yake na umpeleke bafuni",
Joram alimwamru.
"Vipi bwana Godwin? nadhani
hukumwelewa huyu bwana. Alikuwa hana
nia mbaya zaidi ya... ya..." Joram hakuwa
na muda wa kuchezea. Alijua afisa huyo
wa hoteli alihitaji nini kumtoa mshangao,
pigo moja tu, ambalo halikutegemewa
lilimfanya afisa huyo aanguke chini kama
gunia la mkaa. Hima Joram alianza
kuwavutia bafuni mmoja baada ya
mwingine. Kisha aliufunga mlango wa bafu
kwa funguo na kumfuata Nuru ambaye pia
alikuwa ameshangaa.
"Kwanini umefanya hivyo Joram?
Haikuwepo kabisa sababu ya
kuwashambulia. Askari huyo
asingegundua lolote. Sasa watajua kuwa
uko hapa na wataanza kututafuta kwa udi
na uvumba".
Si kitu. Kwa nini tujikombekombe kwao?
London si mji mzuri pekee yake katika
dunia hii. Bado tuna haja ya kuiona miji
mingine". Joram alimwambia Nuru kwa
tabasamu lenye dalili ya hasira.
ITAENDELEA