ROHO ZETU?
SURA YA SABA
Walikuwa wameitembelea miji mingine
maarufu ya dunia. Walikuwa wameonja
anasa na starehe za kila mji. Baada ya
kutoroka London walikwenda Ufaransa
ambako walipitia miji mbalimbali na
kuingia Paris. Toka Paris walikwenda
New York ambako hawakukaa sana kabla
ya kuruka tena hadi Washington, Hong
Kong, Moscow na kwingineko.
Ingawa ilikuwa ziara ya starehe lakini
ilikuwa ziara ngumu kiasi cha
kumtatanisha Nuru na kumsisimua
Joram. Safari zao zilikuwa za
kujifichaficha usiku na mchana
kuwaepuka polisi na wapelelezi ambao
ama walimhitaji Joram kwa makosa ama
kuzishuku hati zao za kusafiria ambazo
mara kwa mara walitumia za bandia. Hila
za hali ya juu pamoja na ruswa nzito ni
njia pekee iliyowafanya wafanikiwe
kuiepuka mitego yote ya CID, KGB,
INTERPOL na wapelelezi wa nchi
mbalimbali.
Katika tukio moja kwenye mji mmoja,
ilimlazimu Joram kujifanya mwanamke
malaya ili kuwaepuka polisi walioizingira
hoteli ambayo alikuwemo. Polisi hao
walipoingia kwenye chumba ambamo
waliamini kumnasa Joram walijikuta
wakirudi nje kwa aibu baada ya kukuta
wasichana wawili, waliofanana kwa uzuri,
wakiwa nusu uchi juu ya kitanda chao
kwa namna ya kufanya mapenzi ya wao
kwa wao. Polisi hawakujuwa kuwa kati ya
wasichana hao mmoja alikuwa Joram
Kiango ambaye aliifunika miguu yake ya
kiume kwa soksi maalum zinazobadili
mwili na kujivika nywele na matiti bandia.
Wakati askari hao wakisubiri nje ili
kuwahoji vizuri; Joram na Nuru walitumia
dirisha kuondoka zao na kila kilichokuwa
chao.
Katika tukio lingine Joram alilazimika
kuteka nyara ngege ndogo ya abiria na
kuilazimisha kutua katika uwanja ambao
haukukusudiwa jijini New York. Kutoka
uwanjani hapo walipata kinga kutoka kwa
askari waliokuwa wameizingira ndege
hiyo kwa kuwachukua rubani na msaidizi
wake huku wakizielekeza bastola zao
katika vichwa vyao. Polisi walikuwa
wakiwafuata kwa mbali, televisheni
ikiwaona na kuwaonyesha kwa kila mtu.
Lakini ilifika mahali ambapo si polisi wala
rubani aliojua kilichotokea. Polisi walikuta
ndege hiyo ikiwa imesimama kando ya
nyumba, marubani wakiwa usingizini kwa
kunusa dawa fulani bila kutarajia. Watu
walioshuhudia tukio hilo wakiwa hawajui
kinachotokea, walidai kuwa waliona
"vijana wazuri" msichana kwa mvulana
wakishuka kutoka ndege hiyo na mizigo
yao na kuingia katika jumba la jirani
ambamo hawakuonekana wakitoka tena.
Harakati na machachari yao katika miji
mbalimbali ziliondokea kuwa habari
ambazo ziliwavutia sana waandishi wa
habari. Mara kwa mara televisheni, redio
na magazeti zilitoa habari zinazowahusu,
Leo kaonekana hapa, hapa kafanya hivi,
pale alifanya vile na kadharika.
Habari hizo zilipambwa kwa picha zao
zinazovutia, kurudiwarudiwa ka historia
ya maisha ya Joram kiango pamoja na
kutiwa chumvi nyingi ili kugusa masikio
ya watu wote na kuisisimua kila mmoja.
Hivyo jina lilipanuka na kuhadhari
kuneemeka. Ilikuwa kama dunia imesita
kushughulikia masuala yaliyo muhimu na
kuandamana na Joram katika ziara yake
hii ndefu. Jambo ambalo lilimfanya kila
mpelelezi kuwa na hamu ya kubahatika
kumtia Joram mikononi na kumfikisha
kunakohusika.
Jambo ambalo lilimshangaza Neema
katika mkasa huo mzima ni jinsi ambavyo
alielekea kufurahishwa na jinsi habari
hizo za aibu juu yake zilivyopata nafasi
kubwa katika vyombo vya habari.
Iliendelea kumfurahisha Joram badala ya
kumchukiza. Nuru ambaye alimfahamu
Joram asivyopenda sifa alijikuta akijawa
na msgangao kwa mabadiliko hayo ya
Joram.
Hata hivyo mshangao wake ulianza
kupungua pale Joram alipoanza au
alipolazimika kumshirikisha katika baadhi
ya mambo aliyokuwa akiyafanya. Jambo
la kwanza lilikuwa mazoezi ya viungo.
walifanya kila starehe, lakini baada ya
starehe, wakiwa chumbani kwao,
walifanya mazoezi makali ya viungo.
Mazoezi ambayo awali yalimtoa Nuru
jasho, machozi na damu. Lakini baada ya
muda machozi na damu vilikoma na
jasho kupungua. Akawa hodari, akiwa
bega kwa bega na Joram katika kila
jambo. Zoezi la pili lilikuwa la matumizi
ya silaha mbalimbali ambazo Joram
alikuwa akizinunua kwa siri sana.
Alimwelekeza Nuru namna ya kuzificha
mwilini, namna ya kuzitumia na
kumfundisha jinsi ya kulenga shabaha
kwa ukamilifu. Nuru alikuwa mwepesi wa
kuelimika.
Hayo yaliufanya moyo wa Nuru uwe na
tumaini kubwa. Sasa aliamini kuwa
Joram alikuwa na jambo fulani zito la
muhimu ambalo alikuwa akishughulikia.
Pengine katika safari hiZo za mji hadi mji
alikuwa akimhitaji mtu kwa madhambi
fulani. Mtu gani huyo? Na ni madhambi
gani aliyoyafanya?
Maswali ambayo yaliimarika hasa
kutokana na simu nyingi ambazo Joram
alikuwa akipiga kwa rafiki zake sehemu
mbalimbali ulimwenguni, ambazo mara
kwa mara zilikuwa katika mafumbo ya
aina aina. Japo alimsikiliza kwa makini
Nuru hakuambua chochote cha haja, zaidi
ya kuishia kuhisi tu. Wakati wote huo
Joram hakukoma kujifungia.
Halafu ikaja jioni ya leo, ambapo Joram
alionekana mtulivu kuliko ilivyokuwa siku
zote. Sigara ziliteketea mdomoni mwake
moja baada ya nyingine, macho yake
yakimtazama Nuru ambaye alikuwa
ameketi juu ya meza ya kuvalia
akishughulikia nywele zake. Joram
alimtazama kwa makini kwa dakika
kadhaa, kisha alimsogelea na kumshika
bega.
"Nilichoshika hapa ni kipande murua cha
kazi ya sanaa ambayo ni mfano halisi wa
kazi ya Muumba. Nadhani hana budi
kujivunia mafanikio yake", alisema
akitabasamu.
Nuru aliinua uso kumtazama.
"Kwa bahati mbaya kazi hii ya sanaa iki
katika hatari ya kuharibika endapo
itandelea kuandamana na binadamu
wenye akili mbaya kama Joram Kiango".
Hilo lilimfanya Nuru atabasamu. Alijua
Joram anaelekea wapi. Siku hizi mbili
alikuwa akimchunguza kwa makini na
kuona mabadiliko katika fikira zake.
Alikuwa akiona na kushuhudia kutoweka
kwa ile starehe ya kujisingizia katika nafsi
ya Joram na badala yake starehe kamili
kuchukua nafasi yake. Mfano wa mtu
ambaye yuko katika jahazi hafifu katikati
ya bahari iliyochafuka anapobahatika
kufika pwani salama. Hivyo alijua kuwa
Joram ana neno. Akamhimiza kulisema
kwa kumwambia, "Unachotaka kufanya
Joram ni kunitisha... Lazima uelewe kuwa
sitishiki ng'oo. Tumekuwa nawe katika
heri na shari. Tutakuwa pamoja jehanamu
na peponi. Usijisumbue kuniambia lolote
lenye dhamira ya kututenga".
Joram akacheka. "Una akili nyepesi sana
Nuru", akamwambia. "Nilichokuwa
nikielekea kukuomba ni kukushauri urudi
nyumbani, uniachie kazi iliyoko mbele
yangu. Ni kazi chafu, ya hatari, yenye
nuksi, ambayo sidhani kama itanifanya
nirudi nyumbani na roho yangu".
"Nimekwisha sema usijisumbue
kunitenga. Nina hamu na kazi nzito, chafu
yenye damu. Sijasahaun
nilivyoshirikishwa kuwaangamiza wakuu
wa nchi wasio na hatia. Nahitaji
kujitakasa. Ni damu pekee
itakayonitakasa. damu ya adui wa Afrika.
Joram aliduwaa huku akimtazama
msichana huyo. Hakuwa na shaka kuwa
msichana huyo ni shujaa. Lakini hakujua
kuwa ni shujaa kiasi hicho. Ndiyo,
alimtegemea sana katika msafara wake.
Lakini hakukusudia kumwingiza katika
mkasa ambao ilikuwa dhahiri kuwa
pamoja na ugumu wa maandalizi yake ya
muda mrefu hadi sasa matekeo yake
yalikuwa gizani. Yeye alikuwa tayari
kwenda, tayari kufanya kazi
inayompeleka; uwezekano wa kurudi
haukumsumbua. Kufa kusingemtisha
sana mradi atakuwa ameifanya kazi yake.
Kifo chake ni jambo moja, kusababisha
kifo cha mtoto wa watu, mzuri kama
Nuru, ni jambo jingine.
"Sikia Nuru. Labda huelewi... Nakusudia
kwenda toka hapa sio nchi ya kawaida. Ni
nchi ambayo kuna watu wenye kiu kubwa
ya damu ya mtu mweusi na njaa kubwa
ya roho zetu. Na ninahitaji kujipeleka
moja kwa moja mikononi mwao. Kwa
ufupi nategemea kwenda Afrika Kusini...".
"Tutakwenda pamoja".
...Na ninachokwenda kufanya ni hujuma.
Wakinigundua watanitafuna mbichi".
"Watatutafuna pamoja".
Joram akaduwaa. "Labda nikufunulie kila
kitu kilivyo Nuru", Joram akamwambia.
""Nisubiri", alisema akiliendea begi lake
lililokuwa limefurika kwa vitabu aina aina
pamoja na encyclopedia ambazo Joram
alikuwa akizitumia kwa muda mrefu
kujaribu kuyasoma yake maandishi ya
kijasusi ambayo aliyapata katika mfuko
wa hayati Chonde. Humo alitoa karatasi
ndefu, iliyoandikwa kwa mashine, ikiwa
tafsiri ya maandishi hayo. Alimkabidhi
Nuru na kumwabia asome haraka haraka.
MPANGO KABAMBE WA KUIFANYA
AFRIKA ITUPIGIE MAGOTI
Taarifa hii ni siri kubwa miongoni mwa
watu wachache sana, wa ngazi za juu
katika serikali yetu. Ni taarifa ya
mafanikio ya jaribio lililofanyika muda
mrefu, kwa gharama kubwa, baina ya
wana sayansi wetu na waliotoka katika
nchi marafiki duniani; juu ya uwezekano
wa kufanya nguvu za nukria zitusaidie
katika kuwaweka Waafrika, na
ikiwezekana dunia nzima katika kwato
zetu.
Itakumbukwa kuwa kifungu kikubwa cha
pesa kilitengwa ili kufanyia majaribio
haya. Kwa siri kubwa sana mtambo
madhubuti ulijengwa na setilaiti kutupwa
angani. Mbili kati ya setilaiti hizo
zilidondoka katika nbahari ya Hindi kabla
ya kuonyesha matokeao. Lakini setilaiti
ya tatu imetimiza majibu. Majaribio
yamefanywa na kuleta matokeo ya
kuridhisha kabisa. Mtu wetu alitumwa
Lagos na kutega gololi maalumu ambazo
baada ya kufyatuliwa zimeifanya setilaiti
hiyo iliyoundwa kwa madini yanayoifanya
isionekane kwa macho iweze kuingia
katika anga la nchi hiyo na kuachia
bomba la moto mkali ambao uliteketeza
uwanja na watu kadhaa. Jaribio la pili
lilifanywa huko Harare ambako maghala
yaliteketea. Jaribio la tatu na la mwisho
linakusudiwa kufanywa Tanzania, katika
jengo la Benki Kuu inayojengwa. Hatuna
shaka kuwa jaribio hilo litafanikiwa.
Baada ya jaribio hilo ndipo tutaanzisha
mpango wa kuzifanya nchi zote
zinazojiita za mstari wa mbele, kutupigia
magoti. Mtu wetu anayekwenda Tanzania
ni mtu wa kutegemewa, aliyeishi huko
miaka mingi. Atapewa pesa nyingi
zitakazomwezesha kwenda mahala
popote duniani, na kumnunua mtu yeyote.
Huyu atakuwa na jukumu la kusubiri amri
yetu ili aachie vipigo vingine ambavyo
vitaifanya Afrika itokwe na machozi huku
dunia ikilalamika...
Nuru aliinua kichwa ghafla kumtazama
Joram. Tayari uso wake ulikuwa umelowa
jasho la hofu na mshangao. "Joram" Nuru
alifoka, "Mungu wangu. Huoni kama hii ni
habari ya kutisha kuliko zote?
Tunawezaje kustarehe hivi huku nchi yetu
ikiwa mashakani?".
"Imenichukua siku nyingi kuigundua.
Waliyaficha maandishi hayo kwa hila
ambazo zingemtoa jasho mtu yeyote
mwenye akili timamu. Hata hivyo
ugunduzi huu hautatusaidia chochote.
Kama ulivyosoma setilaiti hiyo iko angani
na haionekani kwa macho. Inaendeshwa
na mtambo ambao uko katika himaya
yao, bila shaka ukilindwa kwa hali na
mali. Hakuna njia nyingine zaidi ya
kuubomoa mtambo huo".
"Je. Tukitoa siri hii kwa dunia?", Nuru
alimuuliza Joram.
"Haisaidii. Umoja wa Mataifa utalalamika
na kuilaani Afrika Kusini. Pengine
watawekewa vikwazo vya kiuchumi.
Unadhani hayo yatawafanya
watuhurumie?". Mara ngapi
wamelaaniwa? Mara ngapi wamewekewa
vikwazo? Hapana Nuru. Lazima nifike
Afrika Kusini. Dawa ya moto ni moto".
Nuru alitulia kwa muda akiitafakari
taarifa hii kwa makini. Mara aliinuka na
kumwendea Joram. Akamkumbatia na
kumnong'oneza masikioni. "Samahani
sana mpenzi. Nilikuelewa vibaya sana
ulipoiba pesa benki. Vilevile nilishangaa
unavyozitumia pesa hizo vibaya kwenda
huku na kule ukuwa hujali matusi ya
waandishi wa habari. Sasa nimekuelewa.
Nimeelewa kwanini ulifanya vile. Ulikuwa
ukijiandaa kwenda Afrika Kusini.
Ulichofanya ilikuwa kuilaghai dunia ili
uonekane mhalifu na mkimbizi asiyeweza
kuishi popote isipokuwa Afrika Kusini.
"Sivyo mpenzi?". Joram alipochelewa
kujibu Nuru aliongeza, "Mpenzi. Wewe ni
shujaa kuliko mashujaa wengine niliopata
kuwasikia. Tutakwenda pamoja Afrika
Kusini...".
"Tatizo siyo kwenda Nuru. Tatizo ni
kurudi. Unaoneje, tutarudi na zoho zetu?".
ITAENDELEA 0784296253
Share