SURA YA NANE
II
Kwa Afrika Kusini ilikuwa kama nafasi ya dhahabu. Vyombo vyote vya habari nchini Afrika Kusini viliandika na kushangilia kwa nguvu kuwasili kwa Joram na Nuru katika nchi yao. Waliipamba habari hiyo kwa maandishi makubwa na kuyatia chumvi nyingi juu ya wizi wa pesa za umma. Walieleza jinsi alivyopokonya pesa hizo, alivyozitumia kwa starehe sehemu mbalimbali ulimwenguni, alivyofaulu kuwalaghai polisi wote duniani, na mwisho alivyoona hana hila tena zaidi ya kukimbilia Afrika Kusini, ili ajisalimishe na kujificha maisha.
"Huu ni mfano hai kwa watu weusi kote ulimwenguni", alieleza mtangaji mmoja wa televisheni. "Hakuna asiyemfahamu huyo Joram Kiango. Alijifanya mpigania haki, usawa na usalama wa watu weusi. Amesababisha vifo vya watu wengi ambao walikuwa na nia njema ya kuzikomboa nchi zao. Ndivyo walivyo watu weusi wote. Wanawalaghai wenzao na kuwafanya wote waote mikia misituni eti wakidai haki na uhuru. Matokeo yake ni kuwafanya, hao wenzao, kuwa vijakazi wakati wao wakitunisha matumbo yao mara baada tu ya kupata madaraka. Natumaini weusi wote mnaodanganywa mtaitumia nafasi hii kuuona ukweli wa mambo. Bila hekima na uongozi wa mtu mweupe Afrika ingekuwa bado gizani, na endapo ataondoka mtu mweupe Afrika giza litarudi...".
Hayo yalisemwa baada ya watu kuwatazama Joram na Nuru wakitoka katika ndege waliyoiteka kuwaleta Afrika Kusini, huku wakiwa wametanguliwa na rubani ambaye walikuwa wamemshikia bastola. Nje ya ndege Joram aliitupa chini bastola yake na kuweka mikono yake juu. Ndipo Polisi wa makaburu waliokuwa wameuzingira uwanja wakiwasubiri, walijitokeza na kuwakamata na kuwakagua haraka haraka. Walipoona hawana silaha nyingine zaidi ya ile iliyotupwa waliwaongoza hadi kwenye gari lililokuwa likiwasubiri. Muda wote huo kamera za waandishi wa televisheni na zile za wapigapicha wa magazeti zilikuwa zikiwaelekea Joram na Nuru kwa ukamilifu. Kama kuna chochote kilichowashangaza watazamaji ni jinsi sura za vijana hawa zilivyoonekana tulivu, nzuri, zisizo na dalili zozote za ugangwe kama walivyotegemea kuwaona.
Msafara wa gari lililowabeba uliishia katika jumba moja kubwa lenye ghorofa kadhaa. Humo baada ya lifti waliyoingia kuwapandisha juu walijikuta katika chumba kilichoelekea kuwa maalum kwa ajili ya kuhoji mateka. Askari waliokuwa nao waliamuru kusubiri, kisha wakatoka zao na kuufunga mlango nyuma yao. Baada ya muda waliletewa chakula na vinywaji. Wakala na kunywa.
Baada ya muda kama walivyotegemea, walianza kutembelewa na maafisa wa upelelezi, ambao waliwauliza maswali kemkem. Maswali yote Joram na Nuru waliyajibu kwa ukamilifu kama walivyojiandaa; kwamba walikuwa wameishiwa na hila za kuwakwepa INTERPOL wakaona hawana njia nyingine zaidi ya kukimbilia Afrika Kusini ambako wangepata hifadhi. Baada ya maswali yalifuata mawaidha na badala ya mawadha ikawa kashfa.
"Wewe kama Joram Kiango ambaye nchi yako na Afrika nzima ilikutegemea huoni aibu kufanya ulivyofanya na kumbilia huku Afrika Kusini?"
"...Utajisikiaje utakapolazimika kufuata matakwa yote ya ubaguzi wa rangi na kulazimika kushuhudia Waafrika wanavyonyanyaswa?", Joram aliulizwa.
"...Unaweza kukiri hadharani kuwa viongozi wote wa Afrika ni wadanganyifu na hawajui watendalo?", lilikuwa swali lingine la maudh kwa Joram.
"...Ukipewa bastola ili umuue mpigania uhuru yeyote atakayematwa utafanyaje?", aliulizwa kwa mara nyingine.
"...Huyu msichana na uzuri wake wote ni malaya?, mbona anakubali kuandamana na mwizi".
Yalisemwa mengi zaidi ya hayo. yapo ambayo Joram aliyajibu kwa namna ambayo alijua kama walitegemea atajibu. Mengine hakuyajibu, akijua kuwa walimtegemea kutojibu. Mengine ilimlazimu kuinama kwa haya wakitarajia kuwa aone aibu. Baadhi ya maswali haya aliyakwepa kijanja akijua ni mitego iliyokusudiwa kumnasa.
Kutoka hapo walipelekwa katika chumba ambacho kilikuwa na mitambo mingi ambao eti ingeonyesha kama walikuwa wakisema ukweli au la. Waliwekwa katika mitambo hiyo na kuanza kuulizwa tena maswali. Yote hayo Joram alikuwa ameyafafanua kwa Nuru kabla hawajaondoka Paris kuelekea Kinsasa Zaire ambako waliiteka nyara ndege ile ya kukodi. Alimweleza kuwa ambacho mtambo kama unaweza kuonyesha ni dalili za moyo kudunda na damu kuchemka mara unapoulizwa swali ambalo litakushitua au utakapobuni uongo. Hivyo endapo utazungumza kwa kujiamini haitaonekana dalili zozote.
Ndivyo ilivyotokea. Saa chache baadaye walikuwa wamechukukuliwa na gari kutoka katika chumba hicho na kupelekwa katikati ya maji ambako waliingizwa katika nyumba moja kubwa na kuelekezwa katika chumba kilichokuwa na vitanda viwili. Humo walikuta mizigo yao yote. Ingawa mizigo yao ilikuwa kama ilivyokuwa, Joram hakusita kugundua kuwa tayari ilikuwa imekaguliwa kwa ukamilifu. Hilo alilithibitisha baada ya kufungua na kukuta kila kitu kimo isipokuwa furushi la pesa zilizokuwa zimesalia. Hilo pia alilitegemea. Hivyo hakubabaika. Akamwendea Nuru na kumvuta mkono akimwelekeza kitandani ambako alimketisha ili ampumzike kidogo.
"Pole", Joram alimwambia Nuru.
"Kwa".
"Usumbufu".
"Mbona bado sijasumbuka. Naamini huu ni mwanzo tu, kuna mengi yanayokuja na nitakuwa tayari kuyakabiri yote...".
"Shii", Joram alimnyamazisha. Usijisikie huru kiasi hicho", alinong'ona. "Bado tuko chini ya ulinzi mkali. Yawezekana wanatutazama na kutusikia. Kiswahili si lugha ngumu kiasi hicho. Endelea kujihadhari".
Moyoni Joram alikuwa na sherehe kubwa. Alikuwa akishangilia mafanikio ya msafara huo ambao ulienda kama alivyokusudia kuelekea kuzaa matunda. Kufika Afrika Kusini na kupata mapokezi yenye hadhi kwa kiwango hiki ilikuwa jambo pekee la pili ambalo alilihitaji sana. Jambo la awali ambalo alihakikisha limefanikiwa kabla hajabandua mguu wakekuiacha dunia huru na kujitosa jehanamu kiasi hiki ilikuwa kulisafirisha sanduku lake ambalo lilikuwa na kila kitu alichohitaji katika jukumu lililokuwa mbele yake. Kati ya vitu vilivyokuwemo ni pamoja na pesa za matumizi muhimu, silaha aina aina, madawa ya kila aina, ramani mbalimbali, ngozi na sura za bandia ambazo zingemfanya aonekane mtu mweupe, na zaidi ya yote ni vile vijigololi maalumu ambavyo alivipata kutoka kwa hayati Chonde.
Ilikuwa imemgharimu uongo mkubwa na pesa kuweza kulifikisha sanduku lile katika nchi hii. Alikuwa ametumia hila za kumwendea mfanyabiashara wa Kimarekani ambaye alikuwa akisafirisha mizigo yake moja kwa moja kutoka Ufaransa. Baada ya kujijenga kwake kwa urafiki bandia alimhadaa kuwa amepata oda ya kuuza madawa ya kulevya nchini Afrika Kusini. Mmarekani huyo alikataa kabisa kujihusisha kwa hali yoyote katika biashara ya aina hiyo. Joram alikazimika kumpigia magoti kwa maneno huku akimpa pesa nyingi na kumwahidi sehemu kubwa ya faida. Ndipo sanduku hilo liliposafiri pamoja na mizigo mingine muhimu ya Joram. Na aliarifiwa kuwa sanduku hilo limefika salama. Ilimpendeza sana Joram kuona kati ya watu wengi waliokuja kiwanjani kushuhudia wateka nyara hao wakitelemka kutoka ndani ya ndege, mmoja wao alikuwa Mmarekani huyo aliyeitwa Moore. Ilimpendeza zaidi kuwa Moore hakuweza kufahamu kuwa mteka nyara huyo ndiye yule aliyekuwa rafiki yake siku tatu zilizopita nchini Ufaransa. Joram akiwa amekariri ramani ya nyumba ya Moore kama anavyovifahamu viganja vyake vya mkono, alikuwa akiisubiri kwa kiu kibwa fursa ya kuweka mikononi mwake mizigo yake.
Kabla ya kuoga kama alivyohitaji kufanya, Joram alijitia shughuli na kufanya kama anayepanga vitu chumbani kwake vizuri. Alichokuwa akifanya hasa ni kitu au vitu fulani na haukupita muda kabla ya kukiona alichokuwa akitafuta. Kipande kidogo sana cha kioo kilichokuwa kimejitokeza sakafuni katika pembe moja ya chumba kama kilichosahauriwa na waashi kwa bahati mbaya. Joram alijua kuwa nyuma yake kipande hicho kulikuwa na nyaya ambazo zilisafiri hadi kwenye mtambo ambao ulikuwa na jukumu la kupeperusha kila wanachoongea au hata kuwaona. Baada ya kuona hayo Joram alilidhika, akijua kuwa alikuwa hana haraka ya kuwa msiri. Alihitaji faragha kwa usiku mmoja tu, na katika usiku huo alijua ambacho angefanya kuufanya mtambo huo ushindwe kuwajibika kwa dakika kadhaa.
Wakaoga.
Wakalala.