Riwaya: Tutarudi na roho zetu?

Riwaya: Tutarudi na roho zetu?

SURA YA NNE II

Ulikuwa usiku mfupi sana kwa Joram. Alikuwa na mengi ya kufanya ambayo hakuweza kuyatekeleza wakati huo. Ilimchukua muda wa kutosha kumshawishi Nuru kwa vinywaji na mahaba ili asahau hofu yake ya kuua mtu. Baada ya usiku wa manane ndipo Nuru alipoacha kuweweseka na kupitiwa na usingizi mzito. Lakini alikuwa kamkumbatia Joram kwa nguvu. Ilimrazimu Joram kutumia hila fulani na kujitoa mikononi mwake na kumfanya Nuru akumbatie mto.
Aliinuka kutoka kitandani, akanyata kwa utulivu, Joram aliliendea sanduku la marehemu Chonde na kutazama uwezekano wa kulifungua. Isingekuwa kazi rahisi. Ilihitaji utaalamu wa hali ya juu au risasi ya bastola ili kulifungua sanduku hilo. Joram hakuwa tayari kutumia risasi kwa hofu ya kumwamsha Nuru. Na utaalamu siyo jambo ambalo lingepatikana kwa dakika moja. Hivyo aliliweka kando sanduku hilo na kuchukua mfuko wa Chonde ambao haukumchukua muda kuufungua na kuangalia mifuko yake ya siri ambamo alitoa nyaraka mbalimbali na kuzisoma kwa makini.
Yale maandishi wa kijasusi ni jambo lingine ambalo lilihitaji muda na utulivu mkubwa ili kueleweka. Hivyo hakupoteza muda kujaribu kuyasoma. Badala yake alichukua hati ya kusafiria ya Chonde, kile kijisanduku na nyaraka zote alizoziona muhimu. Vitu vingine alivifungafunga katika mfuko na kuvificha mahali ambapo aliamini kuwa visingepatikana kwa urahisi.
Baada ya hapo alichukua begi lake na kutoa vitu vyote vilivyokuwemo. Alichukua kinyago fulani cha hoteli na kukifunga katika mfuko wa nailoni na kuutumbukiza katika begi lake. Akalinyanyua kupima uzito wake. Kisha aliweka mezani, na kuacha albam ambayo ilikuwa ikitoa nuru nyekundu iendelee kuwaka. Akaitupa taulo iliyokuwa kiunoni mwake na kujilaza kitandani kwa utulivu akiutoa mto aliokuwa ameukumbatia Nuru na kuichukua nafasi hiyo. Akaiinua mikono ya Nuru na kuifanya ituwe kiunoni mwake. Akayafumba macho yake na kujifanya kulala.
Lakini asingeweza kulala alikuwa akiyasubiri mapambano kwa hamu. Joram hakujua kuwa alikuwa amepitiwa na usingizi mzito. Alipoamka alikutana na macho mazuri ya Nuru yakimtazama kwa utulivu.
"Za asubuhi, mpenzi".
"Nadhani siyo mbaya".
Nuru alitulia kidogo kabla ya kuongeza, "Nilikuwa nikisubiri uamke ili tuzungumze mpenzi. Nadhani haya yatakuwa maongezi yetu ya mwisho".
"Kwa vipi?".
"Unajua jana nimeua mtu? wakati wowote polisi watafika hapa na kunitia pingu. Endapo nitanusurika kitanzi siwezi kunusurika kifungo cha maisha". Akasita tena na kuongeza, "Leo nimeota mpenzi. Nimeota nikining'inia juu ya kitanzi. Wewe na watu wengine mkiwa kando mkinicheka. Nilijaribu kukuita unisaidie lakini sauti haikuweza kutoka".
Joram akacheka. "Nani aliyekwambia kuwa utafungwa? Polisi wangemfahamu mtu aliyemuua bila shaka wangepata medali ya dhahabu badala ya kukuvika pingu. Pamoja na hayo hawawezi kabisa kufahamu nani alimuua. Unajua uliingia hotelini mle ukiwa mwanaume?, ni mimi tu niliyeweza kukufahamu", Joram akacheka tena. "Lakini yote hayo ya nini? Leo tunaenda zetu Nairobi".
"Kufanya nini?".
"Kutumia".
Nuru akashikwa na mshangao. "Nilidhani umeingia kazini Joram".
Joram alitabasamu kabla ya kumjibu. "Kuna mpelelezi mwenzangu maarufu anayeitwa Willy Gamba, aliwahi kusema kazi na dawa. Mpelelezi ni binadamu vilevile. Lazima astarehe na kuburudika. Yawezekana tutaenda Nairobi tukiwa kazini. Sasa sikia Nuru. Nitafunga mizigo yetu yote na kukutaka ukanisubiri Uwanja wa ndege. Hapana usiende Terminal II nenda kanisubiri Terminal I uwanja wa zamani. Nataka twende kwa ndege ya kukodi".
"Ndege ya kukodi!", Nuru hakustahamili kuficha mshangao wake. "Kwa kweli suala zima linanitatanisha. Kwanza nadhani hatuna pesa za kutosha kutuweka hotelini kwa siku tatu
zaidi".
"Nani aliyesema kuwa hatuna pesa?".
Saa mbili baadaye Joram alikuwa mtaa wa Sokoine akielekea benki ya City Drive. Mkononi alikuwa na mfuko wake mkubwa ambao ulionekana mzito. Alipoingia benki alimfuata meneja aliyeongea nae jana ambaye alimpokea katika hali ya kujuana. Baada ya salamu za kawaida Joram alipewa fomu alizotakiwa kujaza. Akazijaza kwa makini na kuzirejesha kwa meneja ambaye alizipitia. Kisha alitakiwa kuonyesha mali yake aliyohitaji kuhifadhi kwa utaratibu wa Self Custody. Akafungua begi lake na kutoa kunyago.
"Ni hicho tu?", meneja aliuliza. "Nilidhani una kidani cha almasi". Akamjibu kwa sauti ya mzaha. Moyoni meneja huyu aliamini kabisa kuwa ndani ya kinyago hicho kulikuwa na kipande cha almasi au Tanzanite. Kwanini hakuona sababu nyingine ambayo ingemfanya Joram ajiingize katika gharama kubwa kwa ajili ya kinyago cha Mmakonde mmoja.
"Hiki kina thamani kama roho yangu", Joram alimjibu meneja. "Ni kumbukumbu ambayo iliachwa na babu mzaa babu yangu ambayo inalinda ukoo wetu. Niliwahi kuzani kwamba ni utamaduni wa kipuuzi nikakidharau, lakini yalinipata makubwa. Nusura nipoteze roho. Tangu nianze kukithamini na kuwa nacho, mambo yameniendea kama ninavyotaka".
Meneja huyo alielekea kumwamini. Wakaninuka na kuelekea shimoni. Waliwapatia wafanyakazi wanaotunza akaunti za watu, ambao hawakujishughurisha kuwatazama zaidi ya ule mtazamo wa kawaida. Wakatelemka ngazi na kuingia vyumba vya chini. Ni hapo Joram alipomgusa meneja begani na kumwambia.
"Sikia bwana meneja. Sihitaji kuhifadhi kinyago hiki wala kitu kingine. Nahitaji pesa. Za kigeni", Sauti yake ikiwa ileile, makini, iliyotulia, ikamfanya meneja huyo kudhani kuwa huo ulikuwa utani mwingine wa Joram. Hivyo aligeuka akitabasamu. Lakini tabasamu lake liliyeyuka ghafla na nafasi yake kumezwa na hofu iliyochanganyika na mshangao mara alipokutana na bastola kubwa ikimwangalia kifuani.
"My god", meneja aliropoka kwa hofu.
"Usiogope", Joram alimnongoneza meneja. "Endapo utakuwa mbishi utaumia. Kwanza pesa hizi siyo zako. Nifunguliea nichukue kidogo na kuondoka zangu".
"Sina ufunguo", meneja alijibu. "Zaidi ya hayo, vitasa hivi hufunguliwa na watu wawili kwa pamoja. Sioni unavyoweza kuzichukua", akavuta pumzi kwa nguvu kabla ya kuongeza, "Pamoja na hayo ndugu Joram, Nashindwa kuamini kama kweli unadiliki kufanya kitendo hicho. “Unajuwa wewe ni mtu mwenye hadhi kubwa hapa nchini na duniani kote. Kwanini uichafua hadhi hiyo? Kama unataka pesa hata ukiiomba serikali ungepewa. Hakuna asiyeujua mchango wako katika kuilinda nchi hii".
"Yawezekana hufahamu ubahili wa serikali hii wewe", Joram alimcheka meneja. "Sasa tusipoteza muda. Mimi ninazo funguo ambazo zinafungua kila aina ya kufuli. Sidhani kama kufuli zenu zitashindikana. Nitakupa funguo hizi ujaribu mmoja baada ya mwingine nitakuwa
nyuma yako nikikutazama. Ukifanya ujinga utapoteza maisha yako". Juhudi hizi hazikufua dafu. Ndipo Joram alipoamua kufumua kitasa kwa risasi. Bastola ilikuwa na kiwambo cha kupoteza sauti, na kwa hivyo, ulitokea mlio wa kawaida tu. Dakika iliyofuata walikuwa ndani ya chumba cha fedha za kigeni, Joram akiwa amemsimamia meneja ambaye alimwamru kutoa kinyago kwenye begi na kuanza kupakia mabunda ya noti za Dollars, Paunds na nyinginezo. Mfuko uliposhiba, Joram alimwamru meneja huyo kuondoka. Aliuchukua mfuko na kumtaka atangulie.
"Tutatokea mlango wa uani na kwenda nje kupitia geti. Bastola itakuwa mfukoni lakini tayari kuvunja mgongo wako endapo utafanya ujanja au ujinga wowote. Tembea kama kawaida bila kugeuka nyuma".
Walitoka na kuelekea uwani badala ya ofisini. Wafanyakazi wawili watatu waliwatazama kwa mshangao lakini tabasamu la Joram liliufanya mshangao wao utoweke. Tabasamu hilohilo liliwafanya askari wa getini wasishituke kwa lolote kumuona meneja wao katangulia akitokea mlango ambao hutumika kwa nadra sana.
Barabarani Joram alimtaka meneja huyo kuendelea na safari akifuata barabara ya Samora bila kugeuka nyuma. Meneja alitembea kwa dakika kadhaa. Alipita benki ya nyumba na kuifikia barabara ya Samora. Hapo alisimama kusubiri amri nyingine. Hakusikia. Akatulia kwa muda akiogopa kugeuka nyuma. Alipoona macho ya wapita njia yakianza kumtazama kwa maswali ndipo alipojitahidi kugeuka nyuma. Akajikuta akiwa peke yake. Hakujuwa Joram yuko wapi. Kwanza aliduaa kwa muda. Kisha akarudiwa na fahamu akainuka na kuondoka mbio kurudi ofisini.
"Tumeibiwa", alimwambia mfanyakazi wa kwanza aliyekutana nae. Akaingia ofisini kwake na kuvuta king'ola cha ishala ya hatari. Dakika chache baadaye polisi waliwasili na kuanza kuuliza maswali yao.
Wakati huo Joram alikwisha badili mavazi yake na kuvaa mavazi ya kizee pamoja na ndevu za bandia zilizojumuisha na miwani kumfanya aonekane mtu mwingine kabisa. Kadhalika alikwisha badili teksi mbili ambazo zilimtelemsha sehemu mbalimbali. Hii ya tatu alikuwa amemwambia dereva, "Airport, tafadhali. Fanya mwendo wa kuruka".
Dereva hakumwangusha. Wakati polisi walipoanza kuweka vizuizi vya njiani, Joram alikuwa akimalizia kulipia fedha za ndege ya kukodi kwa ajili ya kuelekea Nairobi.
ITAENDELEA
 
duh! Joram anaiba! sipati fundisho hapa, kidi kudi fanya fasta kipande kinachofuata maana hii sasa ni zaidi ya kushangaza!
 
Kulikua hakuna namna nyingine ya kupata pesa. Alishakataa kufanya kazi angepata wapi pesa ya starehe? Ila kwa upande mwingine wakubwa zake hawajui kama yuko mzigoni kama kawaida.
 
Kasomeni "Uchu" ishaisha. Hii tusubiri Sana maana Kidi Kudi yupo na yeye anafuatilia "Msako wa Hayawani"
 
Kasomeni "Uchu" ishaisha. Hii tusubiri Sana maana Kidi Kudi yupo na yeye anafuatilia "Msako wa Hayawani"

uchu, njama, kisasi, balaa, hofu zote tushamaliza. labda tuzirudie maana hakuna namna
 
Back
Top Bottom