SURA YA NNE
Asubuhi hiyo, baada ya kuoga na kufungua
kinywa Joram alichukua simu na kupiga namba
mbili tatu hivi, akizungumza na rafiki zake wa
zamani. Alipowapata aliwapa maekelezo fulani
fulani kwa lugha ambayo wangeweza kuielewa
wao tu. Baada ya hapo alijitosa mitaani na
kuanza matembezi. Akiwa amevaa vizuri suti
yake ya rangi ya kijivu aina ya three peace
huku kofia ikiwa imezifunika nywele zake vizuri
kuficha michubuko upande wa kushoto na miwani
mweusi iliyolificha jicho lake lililokuwa halijatii
dawa kikamilifu, alionekana kama alivyotaka,
muungwana ambaye hana tatizo lolote akilini
wala mwilini.
Msafara wake wa kwanza uliishia barabara ya
Sokoine katika tawi la Benki ya Taifa ya
Biashara City Drive. Aliingia ndani na kuomba
kuonana na meneja. Alielekezwa katika chumba
hicho ambamo alikaribishwa vizuri na afisa huyo
ambaye uso wake ulimdhihilishia Joram kuwa
hakuwa akiwajibika ili kuitikiwa wito bali
kuwajibika kulikuwemo katika damu yake toka
alipozaliwa.
"Nikusaidie nini ndugu yangu?".
"Naitwa Joram Kiango. Ninayo akaunti hapa".
"Nakufahamu sana, ingawa ni mara yangu ya
kwanza kukuona ukija huku kwetu. Mara
nyingine unaishia huko huko kwenye pesa".
Baada ya kutabasamu kidogo kwa mzaha huo
aliongeza.
"Umefuata mkopo?".
"Hapana mzee", Joram alijibu. "Nikikopa
nitashindwa kulipa. Ninachohitaji ni kutazama
uwezekano wa kuweka mali yangu yenye
thamani katika akaunti mnayoita Self Custody.
Ningependa mnifahamishe utaratibu ulivyo".
Meneja alitikisa kichwa huku akisema. "Hilo tu,
kwanini wamekusumbua hadi huku, utaratibu
wake si mrefu sana. Ziko fomu maalumu ambazo
utazijaza. Baada ya hapo utakabidhiwa ufunguo
wako mmoja, ufunguo wa pili nitakuwa nao.
Utakwenda huko chini na kuhifadhi mali yako
hadi siku utakayopenda kuikagua au kuichukua.
Malipo yake ....".
Joram alimsikiliza meneja kwa makini, akitupa
swali moja moja. Kisha alimuomba meneja
amruhusu kutizama hali ilivyo huko chini kabla
hajajaza fomu zozote. Meneja akainuka na
kushuka nae hadi shimoni. Walipita vyumbo hivyo
vya kuhifadhi nyaraka, baadhi vinahifadhi
fedha na kimoja aliambiwa kuwa kiliazimwa na
Benki Kuu baada ya jengo lao kuharibika kwa
moto. Baada ya kupewa picha kamili ya ulinzi na
usalama wa hifadhi hiyo Joram aliaga na
kuahidi kuwa angerudi kwa ajili ya kukamilisha
kazi hiyo.
Toka hapo Joram alipita hapa na pale akifanya
hili na lile huku sigara baada ya sigara
zikiteketea mdomoni, mwendo wake ukiwa wa
utulivu kama mtu asiye na tatizo lolote
ulimwenguni. Ungemwona kamwe usingefikiria
kamwe ni mtu ambaye usiku wa jana mpenzi
wake alitekwa nyara bila shaka baada ya
kuteswa sana.
Ni hali yake hiyo ya utulivu ambayo
ilimshangaza Inspekta Kombora alipokutana nae
katika mtaa wa Samora. Kombora alisimamisha
gari lake na kumfuata Joram katika duka
alipokuwa. "Joram", Kombora aliita baada ya
kumsalimu. "Nasikia yule msichana wake Nuru
ametekwa nyara".
"Hata mimi nasikia hivyo", lilikuwa jibu la Joram.
"Mbona hufanyi lolote".
"Nifanye nini, barua imenionya nisithubutu
kufanya lolote. Vinginevyo msichana wa watu
atauawa. Unapenda Nuru afe Inspekta",
Kombora alitikisa kichwa kwa mshangao. "Joram
niliyemfahamu mimi alikuwa hapokei amri kutoka
kwa watu kama hao. Hasa katika suala hili
ambalo ni la uhai wa mtu na taifa kwa ujumla.
Mimi nilidhani wamekuchokoza. Nikategemea
kuwa wangejutia uamzi wao. Nilikosea".
"Umekosea sana Inspekta. Joram unayezungumza
naye si yule wa awali. Usishangae Inspekta.
Usiupoteze bure mshangao wako. Bado kuna
mambo utayasikia juu ya Joram huyu ambayo
yatakushangaza zaidi", Joram alisema huku
akitupa kipande cha sigara na kuwasha kingine.
Alipomuona Kombora kama mtu asiyejuwa la
kufanya ama asiyeamini maneno yake aliamua
kuondoka. Kombora alimsindikiza kwa macho
yake yaliyojaa mshangao na huzuni. Baada ya
pitapita hii ya hapa na pale, Joram alirejea
chumbani kwake ambako alijipumzisha kwa muda.
Wafanyakazi na baadhi ya wapangaji wenzake
waliokuwa wamwemzoea Nuru walimsumbua Joram
kwa kutomuona.
"Anaumwa".
"Hapana. Kapata safari ya ghafla".
"Bila kuaga".
"Ilikuwa ghafla".
Aliujenga vema uongo wake huo hadi ukafanana
na ukweli. Jioni hiyo, baada ya kula, kuoga na
kupiga simu nyingine alijitokeza mitaani na
kuanza matembezi yake. Safari hii matembezi
haya yaliishia Ilala nyumbani kwake. Alielekea
chooni ambako alifungua mahali fulani pa siri
akatoa kijisanduku kidogo alichokuwa amekificha
hapo. Alishangaa kukuta kikiwa kitupu bila
bastola na risasi zake ambazo alikuwa ameziweka
huko. Hifadhi hii ilikuwa siri yake binafsi. Mtu
pekee ambaye alikuwa anafahamu siri hii ni
Neema Iddy ambaye sasa ni Marehemu. Mtu
mwingine ambaye angeweza kufahamu ni Nuru.
Uko usiku mmoja, kati ya zile chache ambazo
waliwahi kulala katika nyumba hii, alimtoroka
Nuru akidhani yuko usingizini, akaja hapa na
kusafisa bastola hiyo. Pengine Nuru aliwahi
kumchungulia. Lakini Nuru huyo sasa yuko
mikononi mwa wateka nyara. Nani mwingine
aliyejua siri hii, Joram alijiuliza kwa hasira.
Hasira ambazo zilimfanya atupe kasha hilo na
kutoka nje baada ya kuifunga milango yote kwa
ukamilifu. Msafara wake uliishia katika hoteli
ya Embassy. Akaagiza vinywaji akaanza kunywa.
Baada ya bia mbili akaenda kaunta kuzungumza
na yule msichana wa mapokezi.
"Shem, za kutwa".
"Nzuri sana shemeji", msichana huyo
alizungumza kwa furaha huku akimtazama
Joram kwa mshangao. "Pole sana shemeji",
aliongeza msichana huyo wa mapokezi.
"Kwa".
"Ule mchezo wa jana. Unajua mimi mpaka sasa
siami kama mlikuwa mnacheza tu. Nilidhani
mlikuwa mnapigana. Yule bwana kashikiria kuwa
mlikuwa mnacheza tu".
"Ulikuwa mchezo. Mazoezi ya viungo. Wazungu
huita rehearsal".
"Mpaka mtoane damu".
Hakujua Joram alivyoisherehekea habari hii
alitupa maneno mengine mawili, matatu kisha
akairudia meza yake. Akaendelea kunywa na
kuvuta. Japo alionekana katika hali ya utulivu,
macho yake yalikuwa makini, yakimtazama kila
anayeingia na kutoka. Aliwaona wengi. Na kati
yao alikuwemo yule ambaye alihitaji kumuona.
Alikuwa rafiki au adui yake Chonde. Aliingia na
kuifuata meza ambayo haikuwa na mtu,
akaketi. Mara tu Joram alipomuona aliinuka na
kwenda kupiga simu ambayo alizungumza maneno
machache sana kisha alikirudia kiti chake na
kumwita mhudumu ambaye aliombwa kuleta bia
nne. Mhudumu huyo alipozifikisha bia hizo Joram
alimwelekeza azipeleke kwa Chonde. Kisha
alitulia akimtazama Chonde alivyokuwa
akibishana na mtumishi huyo kwa zawadi hiyo
ambayo hakujua ilikotoka hadi alipoelekezwa na
kumuona Joram. Akazipokea na kuanza kunywa.
Lakini baada ya dakika kumi meza ya Joram
ilikuwa imefurika kwa chupa kumi zilizoletwa na
mtumishi yuleyule kwa niaba ya Chonde.
Walitazamana kwa muda. Baada ya muda
Chonde alihamia kwenye meza ya Joram.
"Za tangu jana".
"Siyo mbaya".
Wakaendelea kunywa kwa muda. Kila mmoja
akimsoma mwenzake. Kisha Chonde alitokwa na
kicheko chembamba. Joram aliungana naye kwa
tabasam kidogo.
"Pole sana".
"Kwa".
"Yale ya jana".
"Lilikuwa zoezi tu, usijali".
Kikafuata kimya kingine. Kimya ambacho Joram
alikivunja kwa kuanzisha maongezi ambayo
Chonge alizungumza kwa uangalifu akiepuka
lolote ambalo Joram alihitaji juu yake. Pamoja na
Joram kuzungumza kwa ujanja na hila za kila
aina bado Chonde ilimfanya ajione mtoto katika
dunia ya upelelezi na mzembe katika elimu ya
Saikolojia. Ni hapo alipozidi kuamini kuwa
Chonde hakuwa mtu wa kawaida na kama
alikuwa jasusi basi hakuwa jasusi wa kawaida.
Alikuwa zaidi. Jambo ambalo liliongeza hasira za
Joram dhidi ya mtu huyu. Vipi amshinde katika
pambano la mwili na halafu amshinde tena
katika pambano la akili, hata hivyo Joram
hakujali sana, akijua kuwa dakika hii ambayo
anaipoteza na Chonde yupo mtu, mahali fulani
ambaye anaifanya kazi ile ambayo yeye
alishindwa kuifanya jana.
Kazi ya kufungua kile kijaruba cha Chonde na
kuona kimehifadhi nini hata kilindwe kwa
kiwango kama kile. Hivyo akaamua, kumruhusu
Chonde aendelee kumlaghai na kumdhihaki.
"Mwanamapinduzi aliyekata tamaa", Chonde
alikuwa akisema.
"Aibu iliyojo kukata tamaa hali nchi yako iko
mashakani, si ungejaribu kutoa mchango wako",
Joram hakumjibu.
Kisha kama aliyekumbuka jambo Chonde alisema
ghafla.
"Nasikia msichana wako ametekwa nyara".
wapi?".
"Kwani ulidhani siri".
Hilo lilimshitua Joram. Alishangaa kuona mtu huyo
alivyo mwepesi wa kupata habari. Baada ya
kuisoma barua hiyo Joram hakuwa ameipeleka
Polisi wala kuchukua hatua zozote zaidi ya
kutabasamu tu. Lililomfanya asifanye loloye hasa
ni kule kuwa kwake na hakika kuwa barua ile
alikuwa ameielewa zaidi ya mwandishi wake
alivyotaka aielewe. Bila shaka mtu huyo alikuwa
amezidokoa habari hizi kituo cha polisi. Jambo
ambalo lilimfanya azidi kumfanya Joram kuamini
kuwa hakuwa mtu mwenye mkono mrefu tu bali
alikuwa na masikio mapana. Yeyote ambaye
angeketi kando akiwatazama watu hawa wawili
wakiongea angeamini kuwa ni kikao cha
marafiki wa siku nyingi. Asingeamini kuwa
yalikuwa kama maongezi baina ya Chatu na
Mbwa, au baina ya Malaika Gabriel na Ibirisi.
Yule msichana wa mapokezi alikuwa mmoja kati
ya watu walioamini hivyo. Alikuwa amewatazama
kwa muda mrefu na kushuhudia wanavyocheka
na kutabasamu akayasahau mashaka yote
aliyokuwa nayo juu ya urafiki wao na kuamini
kuwa pambano la jana lilikuwa mazoezi ya viungo.
Hivyo alizama katika shughuli zake na
kuwatupia jicho mara moja moja.
Chonde alikuwa akifunua mdomo kuongea wakati
saa yake ilitoa mlio ambao haukuwa wa kawaida.
Ulikuwa mlio wa sauti nyembamba sana, ulimfikia
Joram kwa taabu sana. Chonde aliitazama saa
hiyo kwa utulivu, kisha akamtazama Joram kwa
umakini zaidi. Dakika mbili baadae aliendelea
kunywa kwa utulivu. Dakika ya tatu aliinuka na
kuaga kuwa anaelekea msalaani. Joram alisubiri
dakika tano, kisha akamfuata. Hakumkuta.
Akafahamu kuwa mlio katika saa ya chonde
ulimkumbusha kitu fulani. Jambo ambalo
lilimfanya Joram kuhofia mtu wake ambaye
wakati huu alikuwa katika chumba cha Chonde.
Hivyo Joram alikiendea kibanda cha simu na
kuzungusha namba za simu ya chumba hicho.
Haikupokelewa. Toka kwenye simu, Joram alitoka
nje na kukodi gari ambalo lilimpeleka New
Afrika. Akajipenyeza kwa hila hadi ghorofani,
mbele ya chumba hicho. Akatega sikio na
kusikiliza kwa makini. Chumba kilikuwa kimya
kabisa. Ukimya huo ulimtisha sana Joram.
Aliyaamini sana masikio yake na kwa vyovyote
alitegemea kuwa na mtu chumbani humo.
Akasikiliza kwa makini zaidi. Bado hakusikia
chochote. Akaufubngua mlango taraibu na
kuchungulia ndani.
Macho yake alivutiwa na mtu aliyelala chini juu
ya sakafuni utumbo wake ukiwa nje. Macho
yake yakidhihilisha kuwa roho ya mtu huyu pia
ilikuwa nje. Kabla Joram hajajua kuwa ilimpasa
kuingia chumbani humo au la, mara sauti nzito
aliyoifahamu sana ilisikika ikisema.
"Usiogope ndugu. Karibu ndani".
Msemaji alikuwa kajificha nyuma ya mlango,
bastola kubwa ikiwa mkononi mwake ikimtazama
Joram kwa uchu.
"Ingia na ufunge mlango. Nadhani hutapenda
kufia hapo mlangoni kwama paka. Njoo ndani ufe
kistaarabu kidogo", Joram akaingia ndani.
Hakujishughulisha kumtazama Chonde
aliyesimama nyuma ya mlango. Badala yake
alimtazama marehemu jinsi alivyouawa kinyama.
Tumbo lake lilikuwa limebomolewa na kitu
ambacho hakikuwa risasi wala kisu. Bila shaka
ulikuwa mlipuko wa bomu. Kifo hicho kilimsikitisha
sana Joram. Huzuni ikampata. Kwa huzuni hiyo
Joram alimgeukia Chonde na kufoka kwa hasira
akisema. "Shetani mkubwa. Kwanini umemuua
mtu huyu asiye na hatia?".
"Ni wewe uliyemuua", Chonde alimjibu Joram.
"Mimi nimemuua vipi?".
"Usijifanye hufahamu. Bila shaka ni wewe
uliyemtuma kuifanya ile kazi ambayo wewe
ilikushinda. Kazi ya kujua katika kisanduku
hicho mna nini. Nami nikifahamu kuwa pamoja
na kukuadhibu kama nilivyokuadhibu usiku wa
jana ndipo nilipoamua kutega bomu katika
kisanduku hicho. Wakati huo huo mtu yeyote
anayekigusa saa yangu inaniashiria. Hivyo
tulivyokuwa tukinywa nilishangaa kuona dalili za
mtu. Nikafahamu kuwa mtu asiye na hatia
anakufa. Nimemkuta kisha kata roho. Akageuka
kumtazama marehemu kwa muda. Kisha
akarejesha macho katika uso wa Joram na
kusema, "Ni wewe uliyestahili kuwa chali,
utumbo nje, badala ya mtu huyu.
Joram asingeweza kukanusha. Ilimsikitisha sana
kifo cha kijana huyu. Alikuwa mmoja kati ya
vijana wake smart ambao aliwatumia kwa kazi
hizi na hizi kijana ambaye alikuwa amesaidia
sana katika harakati zake zilizokuwa zimepita.
Hakupata kushidwa hata mara moja ambapo
ameyapoteza maisha yake. Joram akajilaumu
kumtuma katika kazi hiyo. Hamu yake ilikuwa ni
kumshinda na kuutawanya ubongo wake
sakafuni... Kama aliyekuwa akiyasoma mawazo
yake, vilevile Chonde aliongeza kwa sauti nzito,
"Hata mimi sikufahamu kama wewe ni mtu
hatari sana Joram. Unastahili kufa mara moja".
Maisha yakiwa ukingoni Joram alijua kuwa
alihitaji kuikusanya akili yake yote ili ajiokoe.
Hakujua angefanya nini. Walikuwa na bastola
moja tu, na ilikuwa katika mikono ya Chonde.
Kuipata bastola hilo ilikuwa ndoto ya mchana.
Chonde alikuwa macho kama kipepeo. Na bado
uwezo wake wa kuitumia mikono yake Joram
asingemudu. Hata hivyo alitegemea kitu kimoja
tu kimsaidie kuokoa maisha yake. Muda. Muda
waweza kufanya maajabu. Hata asipookoka, si
inapendeza endapo ataufaidi uhai wa dakika
chache zaidi kabla ya kifo chake.
"Najua nitakufa", alisema Joram, "Nadhani
unafahamu vizuri kuwa nakufa kwa ajili ya
tamaa ya kufahamu siri iliyomo katika kisanduki
hicho. Nifanyie basi wema wa mwisho. Nifungulie
kisanduki hicho nione kilichomo ili nife nikijua
kilichomo".
Chonde alicheka, "Tatizo lako Joram ni kule
kufikiria kuwa unacheza na mtoto mdogo.
Unachojaribu kufanya ni kuvuta muda. Wakati
huo huo ukithubutu kuendelea na upelelezi wako
ili lolote likitokea- kitu ambacho siamini- utoroke
na kuitoa siri hiyo nje. Kwa taarifa yako siri
iliyomo katika kisanduku hicho ni nzito kuliko
bara zima la Afrika. Kwa maneno mengi ni siri
ambayo dunia nzima inapigania kujua. Kwa
bahati mbaya watu tunaoifahamu siri hii ni
wachache sana. Na tumeshonana midomo. Hata
maiti siwezi kuisimulia siri hiyo. Nadhani hilo
linakutosha. Sasa jiandae kufa. Ungependelea
risasi ya kichwa ama kifuani?".
Joram alimtazama usoni na kuliona tabasamu la
kifedhuri katika macho ya Chonde. Tabasamu
ambalo halikuwa na mzaha. Akajaribu kuicheza
tena karata yake ya mwisho.
"Jana ulinishinda kwa judo. Vipi ukiniua kwa
mikono", Joram alisema Chonde akacheka.
"Ningependa kukua kwa mikono mitupu. Hata
hivyo sina muda wa kutosha. Umebaki na nusu
dakika ya kuishi. Utapenda kufa ukiwa
umefumba macho ama ukiniangalia?".
Sasa mzaha ulikuwa mbali na sauti ya Chonde.
Mauaji yalikuwa wazi katika macho yake. Joram
akaamini kuwa maisha yake yalikuwa yamefika
ukingoni. Akiwa ameshuhudia vifo vingi vya risasi
alitabasamu kimoyomoyo na kuamini kuwa zamu
yake ilikuwa imefika.
Hata hivyo bado aliyapenda maisha. Bado
aliipenda dunia. Na alikuwa akiiacha moja kwa
moja. Hivyo badala ya kuyafumba macho yake
kwa nguvu na kuyakaza usoni. Hiyo pia aliifanya
kuwa karata yake ya mwisho. Kwani kuua si
mchezo. Hasa kumWua kiumbe asiye na uwezo
wa kujitetea.
Ilimsaidia. Nusu ya dakika ilipita Chonde
akielekeza bastola katika kichwa cha Joram,
kidole chake kikigusa kiwambo cha kufyatulia
risasi, lakini alisita kuifyatua. Mara mlipuko wa
risasi ukasikika. Joram akajirusha kando na
kutua chini ambapo aliruka tena hadi upande
wa pili wa kitanda. Risasi mbili tatu zaidi
zikasikika, kama zinazopigwa bila shabaha.
Kisha kimya kikafuata. Kimya ambacho
kilitoweka kwa mkoromo wa mtu aliyekuwa
akikata roho. Ndipo Joram alipojiinua na
kuchungulia. Ikamshangaza kumuoa Chonde
kalala chini kifudifudi, damu zikimvuja katika
tundu kubwa la risasi katika uso wake. Joram
alichupa na kuirukia bastola iliyokuwa mikononi
mwa Chonde. Akajicheka kwa kuona akipokonya
bastola kutoka mikononi mwa marehemu
aliyekata roho kitambo. Akaikimbilia suit case ya
chonde pamoja na kile kisanduku. Akavichukua
na kuanza kutoka.
Mara mlango ulifunguka ukifuatwa na bastola
ambalo ilichungulia kwa uangalifu, ikiingia
ikifuatwa na binadamu ambaye alifunika uso
wake kwa kofia kubwa na miwani. Alikuwa kavaa
suruali na koti la kiume katika hali ambayo
ingemfanya mtu yeyote amfikirie kuwa pande
la mwanaume. Lakini Joram alimfahamu mara
moja akaitelemsha bastola yake na kumkimbilia
huku akisema kwa furaha. "Nuru nawezaje
kukushukuru Nuru".
Walikumbatiana na kubusiana kwa furaha.
Kisha walitengana mara moja na kutazamana.
"Umewezaje kunifahamu mara moja kwa urahisi
kiasi hiki, tangu nimetoweka watu wanashindwa
kunifahamu".
"Nadhani nakufahamu zaidi ya wanawake wote.
Zaidi ya hayo nami mwingine ambaye anaweza
kuhatarisha maisha yake kuipenyeza risasi
katika tundu la ufunguo wa mlango kumuua mtu
ambaye alikuwa tayari kuniangamiza, kwa kweli
sijui namna ya kukushukuru". Wakakumbatiana
tena.
"Nuru niliwahi kukwambia kuwa u mzuri, niliwahi
kukwambia kuwa hawakukosea waliposema kuwa
wewe ni binadamu aliyekuja duniani kwa makosa
badala ya kuwa malaika kama ulivyokusudiwa,
nadhani walikukosea Nuru. Wewe ni Malaika.
Tazama ulivyo mzuri tazama ulivyotokea na
kuipokonya roho yangu kutoka katika kinywa
cha mauti. Nuru, nawezaje kukushukuru Nuru".
Hayo yalipita katika kichwa cha Joram wakiwa
wamekumbatiana. Joram alitamani kuyatamka
kwa sauti, lakini hakufanya hivyo.
"Nakupenda", alisema badala yake.
Ilikuwa mara ya kwanza Nusu kumsikia Joram
akitamka neno hilo. Mara kwa mara alimtesa
kwa kutojua kama kweli Joram alikuwa
akimpenda au la. Ingawa walikuwa wakifanya
mapenzi, bado Joram hakuwahi kulitamka neno
hilo kwa sauti ambayo ingelipa uzito jambo hilo.
Kadhalika macho yake hayakufichua mapenzi
yake kwa hali yoyote. Hivyo ilikuwa kwake zaidi
ya habari. Hata hivyo bado alikuwa na la
kusema.
"Sikuamini Joram", alimnong'oneza. "Pamoja na
kutoweka kwangu nikiwa nimetekwa nyara
hukujishughulisha kunitafuta. Walau kutoa
taarifa kituo cha polisi".
Joram akaanguka kicheko. "Usinichekeshe
Nuru. Waweza kuwa ulifanikiwa kuwalaghai
watu wote pamoja na polisi, lakini mimi
hukunidanganya. Nilijua kuwa ilikuwa hila tu
uliyoiandaa ili kunishawishi niingie katika vita.
Mwandiko wa barua ile pamoja na
kuuvurugavuruga, kwa mtu aliyesomea miandiko
kama mimi, nilifahamu kuwa ni wako. Vilevile ile
damu iliyodondoka pale haikuwa na uzito wowote.
Nilijua umejikata kidole makusudi na ile vurugu
iliyofanyika chumbani haikuwa na umuhimu. Kwa
vyovyote majasusi katili wasingefanya mchezo
kama ule. Hivyo nilikuwa nikikusubiri nikitegemea
utokee tuendelee na starehe zetu".
"Starehe", Nuru aliuliza kwa mshangao. Alikuwa
ameshangaa kuona Joram alivyogundua hila yake
kwa urahisi. Ilimshangaza zaidi alipodai starehe
wakati wamesimama kando ya maiti mbili
zilizolala chini hata bado hazijapoa kwa ajili yao.
"Starehe Joram, nilidhani tumeingia kazini".
Joram akatabasamu. "sikia Nuru, siyo tabia
nzuri kuzungumza kando ya maiti za binadamu.
Pamoja na kwamba bastola zilizotumika zilikuwa
na viwambo vya kupoteza sauti bado mtu yeyote
anaweza kutokea na kutukuta katika hali hii.
Nasi hatuna muda wa kuyajibu maswali ya polisi.
Twende zetu mara moja", Joram alimaliza
akichukua mizigo yake wakaanza kutoka.
"Nifuate. Twende kwa utulivu kama tutokao
chumbani kwetu".
"Kumbuka tu wanaume wawili", Nuru alisema
akitabasamu. Walitelemka na kuiacha hoteli bila
tatizo lolote. Watu wawili watatu waliokutana
nao walikuwa wamewatazama kikawaida. Baada
ya kuingia mitaani Nuru aliifichua bastola na
kumpatia Joram akisema.
"Chukua bastola yako. Samahani kwa kuichukua
bila idhini yako. Nadhani uliihitaji sana.
Ningeweza kukupotezea maisha".
Tabasamu likamtoka Joram.
"Hata hivyo umeniokoa. Kama ningeingia nayo
pengine Chonde angeniua na kunisimanga
baadaye", Joram alijibu. "Nimepata nyingine. Hii
umeipataje".
"Nilikwenda kwako kuichukua".
"Na umewezaje kunusa kuwa niko katika
chumba kile nikisubiri kufa hata ukaja
kuniokoa".
"Ni rafiki yako aliyekuokoa. Hayati Edward
ambaye kwa bahati mbaya mshenzi yule
amemwua. Unajua nilipotoka hotelini kwa
kisingizio cha kutekwa nyara, nilikwenda
kujificha nyumbani kwake, tulijadiliana nae
namna ya kurudisha moyo wako katika msimamo
unaotakiwa. mara ukampigia simu na kumpa
maelekezo ya kwenda kufungua kisanduku hicho.
Aliponieleza maelezo yako na jinsi ulivyoponea
chupuchupu mara ya kwanza ndipo nilijua kuwa
umerudi kazini. Nilitaka nije kwako mara moja.
Lakini yeye aliniomba nisifanye pupa. Akaniomba
nifuatane nae katika hoteli hii nikae kando
nikimlinda. Nilifanya hivyo. Mara nikaona mtu
mwenye dalili za kikatili akiingia chumbani
humo, akiwa na bastola mkononi, ingawa ilifichwa
sana. Kabla sijafahamu cha kufanya nilikuona
wewe pia ukinyatia na kuingia. Ndipo nilipojivuta
mlangoni na kuchungulia katika tundu la
ufunguo. Nikamuona Chonde akiwa tayari
kukuua. Sikuwa na la kufanya zaidi ya
kumlenga na...na ...".
Mara Nuru aliangua kilio. Akamgeukia Joram na
kumkumbatia kwa nguvu akisema, "Nimeua mtu...
nimeua mtu, Joram...".
"Watu huuawa", Joram alimnongoneza Nuru.
"Hebu jitahidi kuwa msichana shujaa kama
ulivyo, Nuru. Usingemuua angeniua. Watu
watakusikia. Twende zetu chumbani".
"Lakini nimeua, Joram... nimeua...".
ITAENDELEA