SURA YA KUMI NA MOJA
III
Kuanguka kutoka umbali wa zaidi ya mita ishirini kutoka angani hadi juu ya sakafu ngumu si mchezo. Joram bila ya uhodari wake wa kucheza karate na sarakasi, kama asingefikia kichwa basi angefikia mgongo na kuvunjikavunjika. Lakini alijitahidi kusahau uchovu na maumivu aliyokuwa nayo, akaikusanya akili yake pamoja na kujipindua angani hadi akafikia mabega na kubiringika. Hata hivyo fahamu zilimtoka kwa dakika kadhaa .
Uhai ulipomrudia alifumbua macho yake kwa taabu na kutazama pande zote... Akajikuta akiwa amelala katikati ya mizoga mingi ya binadamu. Baadhi ilikuwa mifupa mifupa na mingine ikiwa imevimbiana, huku mingine ikiwa imeoza kabisa. Mara akapatwa na harufu kali ya kutisha. Harufu ambayo iliambatana na inzi wengi wanene wa kutisha, ambao walikuwa katika hali ya kurukaruka wakishangilia mawindo hayo rahisi. Licha ya inzi hao Joram aliwaona panya wakubwa mfano wa paka walioifanya mizoga hiyo kuwa karamu yao. Panya mmoja alikuwa akipita kumzunguka Joram akimtazama kwa namna ambayo ilionyesha kuwa alikuwa akitamani kuanza kumla akiwa hai.
Moyo ulimdunda Joram. Ingawa hakujua au kupata kuhisi hofu katika moyo wake, lakini kitu fulani kilimpanda moyoni na kumtia hasira na kichefuchefu. Alihisi kama mtu aliyeruka majivu na kukanyaga moto. Kama kufa kwa nini afe kifo kibaya kama hiki? Afe huku anaona? Huku akiliwa na panya? Kwanini asingeruhusu lile dude limuue?.
Kisha Joram akajikaza kiume na kujikongoja kusimama wima. Ilikuwa baada ya kujikumbusha ule usemi wake wa mara kwa mara "Binadamu hufa kwa uzee, hufa kwa ajali, hufa kwa maradhi. Lakini kuna binadamu ambao hufa kwa uvivu vilevile. Hususan katika kazi kama za upelelezi" Wazo hilo lilimfanya aanze kutembeatembea humo akitafuta mwanya wa kumtoa ndani ya kaburi hilo. Alizitazama kuta na kubaini kuwa zilijengwa kwa chuma cha pua, chumba kirefu chenye upana wa mita kumi na mbili kwa ishirini. Akatazama juu kuangalia uwezekano wa kupanda hadi huko alikoangukia. Lakini ilikuwa ndoto nyingine. Ukuta ulikuwa laini mfano wa kioo ambacho kingemshinda hata paka.
Akajiuliza afanye nini? aketi kukisubiri kifo?. Hapana, lazima ajitahidi kutafuta mwanya. Lazima kuna mahali pengine penye mlango ambao unatumiwa kuwaleta watu hawa kusubiri kifo. Akaendelea kutembea akiruka mizoga na wakati mwingine hata kulazimika kuikanyaga mifupa, inzi na panya waliomuongezea msukumo kwa kukimbia hapa na pale, bila shaka kwa mshangao wa kuona kitoweo chao kitatembea kwenda huku na huku.
Joram aliuchunguza ukuta kwa umakini wa hali ya juu. Hatimaye aliufikia ukuta ambao ulikuwa mlango wa chuma uliofungwa kwa nje. Alijaribu kuutingisha mlango huo, bila ya mafanikio. Ulikuwa mlango imara kama ukuta huo. Baada ya kutafakari Joram akaupeleka mkono wake ilipolala bastola yake, ambayo aliitumia kuachia risasi. Risasi iliugonga mlango huo na kuanguka ardhini kama gololi. Hata bomu lisingeweza kuubomoa mlango huo. Hali hiyo ilimfanya Joram aduwae kwa mara nyingine, akitafakari nini cha kufanya.
Mara macho yake takavutwa na maiti mmoja aliyekuwa akitikisika. Joram aliisogelea maiti hiyo na kuitazama kwa makini. Naam, alikuwa mtu mwenye uhai kidogo mwilini mwake. Miguu yake ilikuwa imekatwa na Joram aliona vilevile jicho lake moja lilikuwa limeng'olewa. Huyu alikuwa mtu mweupe tofauti na wengine walikuwa weusi. Bila shaka huyu alikuwa Mrusi.
"Pole", Joram alimwambia.
"Wewe ni nani?", mtu huyu aliuliza kwa sauti ya udhaifu.
"Itakusaidia nini kunifahamu?", Joram alimjibu na kuongeza, "Unakaribia kufa".
Mtu huyo alicheka kidogo kabla ya kuanza kujikongoja na kusema polepole, "Kweli huwezi kunisaidia chochote. Hata hivyo wewe utakufa kabla yangu. Mwenzio hii ni siku ya kumi na nne bado naishi".
Joram hakuona kama kulikuwa na umuhimu wowote wa kuendelea kumsikiliza mtu huyo aliyekuwa akikaribia kukata roho. Lakini hakukuwa na jambo muhimu la kufanya na akaendelea kumsikiliza. Haikuchukua muda kabla hajafahamu kuwa Mrusi huyo alikuwa mmoja kati ya watu wengi waliokuwa wakiuawa kinyama baada ya kushukiwa wakifanya upelelezi dhidi ya uwatawala wa makaburu. Pango hili liliandaliwa maalumu kwa ajili ya kuangamiza watu kwa siri baada ya kupata mateso makali. Wengi walikuwa wakiachwa wafe wenyewe kwa majeraha waliyokuwa wamepata. Lakini adhabu kubwa iliyokuwa ikitumika ilikuwa njaa.
"Usishangae", aliambiwa, "Ni njia pekee ya kutuwezesha kuishi". Alipomuona Joram akizidi kushangaa mtu huyo aliongeza, "Au unaogopa kula nyama za maiti? Sikia, unaweza kunila nikiwa hai. Sina dalili ya kupona. Na ninavyokuona unaonyesha kabisa kuwa tuko pamoja katika mapambano dhidi ya utawala haramu wa makaburu. Unaweza kunila ukaishi kwa zaidi ya wiki moja zaidi, pengine muujiza ukakutokea nawe ukapona na kuendelea na mapambano. USiniogope wala kunishukuru. Wala sitaki kujua wewe ni nani. Haitanisaidia.
Joram aliona kama angerukwa na akili endapo angeendelea kuketi hapo akimsikiliza mtu huyo ambaye ilikuwa dhahiri kuwa uhai wake ulikuwa ukielekea ukingoni. Joram akaondoka hapo taratibu na kuurudia mlango huo ambao alitulia tena akiutazama kwa makini. Bado hakujua angefanya nini kuufungua. Ingehitaji muujiza. Harufu ya maiti hao, kelele za panya na inzi waliokuwa wakishangilia bahati zao, vilizidi kumsumbua Joram. Joram alijua kuwa harufu na usumbufu huo vingemuua kabla hajasikia njaa.
Aliutazama tena mlango huo kwa uchungu na hasira. Akatamani apige magoti na kumwomba Mungu ili afanye miujiza mlango ufunguke. Hilo hakulifanya. Ingekuwa unafiki, kwani hakuwa amemuomba Mungu walao kwa kumshukuru kwa miaka mingi sasa. Vipi amukumbuke wakati huu wa shida? Na vipi ategemee muujiza mkubwa kiasi hicho wakati enzi za miujiza ilikwisha pita? Hii ilikuwa enzi nyingine. Enzi ya kutumia akili na nguvu.
Bado hakuona kama alikuwa na lolote ambalo angeweza kufanya na kujitoa katika gereza hilo. Kwani kila hali alijiona kama aliyefikia mwisho wa msafara wake kimaisha.
Kwani mara ya kwanza aliilaani bahati yake. Siku kwa hofu wala uchungu wa mateso aliyopata katika gereza hilo ambalo halikutofautiana na mtu kuzikwa hai. Hasa alijilaumu kwa kuikosa fursa ya kujionea kwa macho yake mwenyewe jinsi utawala wa makaburu na raia wake watakavyotaabika pindi mitego aliyoitega itakavyofyatuka na silaha ambayo waliiandaa kuwateketeza watu wasiokuwa na hatia itakapowageukia. Joram kama alivyo, hakuna ambacho kingemsisimua zaidi ya hicho. Aone macho ya mshangao yatakavyowatoka wakubwa wa utawala wa makaburu na machozi yaliyochanganyika na makamasi yanavyotililika juu ya mashavu yao meupe. Aone majumba yao makubwa waliyojenga kwa jasho la wanyonge yakiteketea na kubomoka kama milima ya barafu. Na hatimaye aione setilaiti yao ikianguka katikati ya mji wao baada ya mitambo waliyoweka angani kulipuka. Ndiyo. Ni hayo tu aliyohitaji Joram. Ni hayo ambayo yalikuwa yamemfanya ayahatarishe maisha yake kwa muda wote huo hata kumwaga damu za watu wasiokuwa na hatia, ili, afanikishe dhamila yake. Hayo, kuyashuhudia kwa macho yake kungempendeza zaidi ya pesa na kusisimua zaidi ya sterehe. Kwanini amekuwa hana bahati hiyo?.
Kisha akamkumbuka NUru. Kiasi hofu ilimrudia alajiuliza kama Nuru angefanikiwa kunusurika katika mapambano haya angewezaje kurejea Dar es Salaam. Alikuwa amempa maelezo yote muhimu na kumsisitiza wakati gani Nuru aanze safari ya kutoroka zake kurudi nyumbani Tanzania endapo asingemwona. Bila shaka hakuna atakayeweza kuhangaika kumtafuta msichana mmoja ambaye hana tofauti na wasichana wengine wakati mamia ya watu watakapokuwa wakiungua moto, maelfu wakikimbia kwa fujo na mamilioni wakiwa wamepigwa na butwaa. Wakati majumba makubwa na viwanda vya makaburu vikiteketea kwa moto mkali ambao mfano wake haujapata kutokea katika historia ya taifa hili na dunia kwa ujumla. Wakati chombo kisichoonekana kwa macho ya kawaida kitakapokuwa kikielea angani, na baadae kuanguka, baada ya nguvu yake inayokifanya kielee na madini yanayokifanya kisionekane kuishiwa nguvu. Hapana, Joram hakuona kama Nuru angeshindwa kuitumia fursa hiyo. Bila shaka baada ya kumchanganya kwa hila na kumtoroka alipokuwa akimfuata kwa siri, angerudi na kuyafuata maelezo aliyopewa awali. Joram, aliamini hivyo.
Joram asingejisamehe endapo lolote baya lingemtokea Nuru na kusababisha maisha yake kupotea. Licha ya kwamba uzuri wa Nuru haukustahili kuharibiwa na mkono wa kaburu yeyote katili, Ushujaa wa Nuru ilikuwa nguzo iliyotegemewa sana na Joram. Yote aliyokuwa ameyatenda, hekima na juhudi za Nuru vilikuwa vimemsaidia. "Ee Mungu msaidie Nuru aweze kurudi nyumbani", Joram alimwombea Nuru.
Utulivu aliokuwa nao wakati akiwaza hili na lile, ulimfanya panya mmoja amrukie kifuani na kujaribu kumuuma. Lakini Joram aliweza kumkwepa na kuachia teke moja dhaifu ambalo yule panya aliweza kulikwepa pia. Hata hivyo panya huyo alimfanya Joram ayatoe mawazo yake nje na kuyarejesha katika pango hilo la mauti. Harufu mbaya sana ya binadamu waliooza, ikamrudia tena akilini na moyoni. Akajisikia kutapika. Hata hivyo alijikaza kisabuni.
Kisha akakumbuka kumtupia jicho yule Mrusi. Akashangaa kuona kundi dogo la panya wakiwa juu ya uso wake, wakimla, kwanza Joram alishangaa; kisha akaelewa, Mrusi huyo alikuwa tayari amekata roho!- Kichefuchefu kilimrudia tena Joram. Alitamani kufumba macho ili asiendelee kuona ukatili wa panya hao wakimla mtu ambaye dakika chache zilizopita walikuwa wakizungumza nae. Mtu ambaye bila shaka ni mwema sana. Vinginevyo asingeweza kujitolea aliwe akiwa hai? Joram alijiuliza.
Ghafra muujiza ukatokea.
Joram alishangaa kuona mlango ukitingishika na hatimaye kufunguka. Alikuwa makini kuangalia yeyote ambaye angeingia ndani ya kaburi hilo, Joram alijipanga kumteka na kumlazimisha ama amuue kwa risasi au amtoe katika chumba hicho. Hakuwa tayari kufia humo. Hivyo alisubiri muujiza huo kwa shauku, akiutazama mlango kwa makini, lakini akiwa tayari kwa lolote, la heri au shari.
Wakati Joram akijipanga kukabiliana na hali hiyo, Bastola ilionekana katika mkono wa msichana. Halafu ukafuata uso mzuri wenye jasho na damu. Huyu alikuwa Nuru.
"Joram?" Nuru alipiga ukelele wa furaha baada ya kumuona Joram aliyekuwa amesimama kando akiwamwangalia, akiyaamini macho yake.
"Naweza kuyaamini macho yangu?", Joram alimuuliza Nuru akiwa bado amesimama pale. "Wewe ni Nuru kweli au malaika?", Joram aliuliza kwa msisitizo.
Nuru hakupata muda wa kujibu swali la Joram. Tayari alikuwa kifuani kwa, akiwa amemkumbatia kwa nguvu huku akilia kwa sauti ndogo. Wakati wakijipambanua kikamilifu kuwa haikuwa ndoto bali kweli-huyo alikuwa Nuru halisi aliyekuja kumuokoa-alianza kuinua mikono yake ili naye amkumbatie. Lakini Nuru alikuwa tayari amejitoa mikononi mwa Joram na kumtaka watoke eneo hilo haraka haraka huku akisema, "Twende zetu. Wakati umewadia.
Joram alimfuata Nuru kikondoo.
Wakawa nje, baada ya kupigwa na hewa safi fahamu zilimrudia Joram kikamilifu. Saa yake ya mkononi ilikuwa imevunjwa wakati wa mapambano na jitu lile, baada ya kutazama saa ya Nuru Joram akaelewa sababu za kuelezwa kuwa wakati umewadia. Uhai ukamrudia mara moja rohoni, ingawa kimwili alikuwa bado ghaifu. "Niambie Nuru tafadhali. Niambie, mitego tuliyotega haijafyatuka tu?, mji huu haujaanza kuteketea?".
Badala ya kujibu, Nuru alimwambia Joram. "Sililiza tuliza akili".
Kwa mbali walisikia kelele nyingi za hofu, vilio na milipuko ya kutisha ikisikika kutoka kila upande. Walisikiliza kwa muda wa nusu dakika hivi, Joram akatabasamu na kusema polepole; "Nadhani inatosha. Watakufa wenye hatia na wasio na hatia. Sasa iliyobaki ni ile kazi moja ya mwisho. Kuulipua huu mtambo".
Haraka Joram aliushika tena mkono wa Nuru wakaanza kukielekea chumba cha mtambo. Nuru akiwa na ramani halisi ya jengo hilo, alimshauri Joram wapi wapitie. Dakika mbili baadaye tayari walikuwa wamewasili katika chumba hicho.
Kulikuwa na wahandisi watatu katika chumba hicho, jasho likiwatoka kwa jinsi walivyokuwa wakishughulika, wakiwa hawaelewi kinachoendelea zaidi ya kuona mambo yanabadilika, hawakuweza kuwaona Joram na Nuru walioingia ghafra. Walipowasabahi bastola mbili zilikuwa tayari zikiwangalia. Wakabaki wameduwaa. Mshangao wao ulikoma baada tu ya risasi kupenya katika miili yao na kuwafanya waangukiane huku damu nyingi zikiwavuja.
Joram aliikimbilia mitambo hiyo na kuanza kuikoroga kama alivyokusudia. Alipotosheka aliyatoa mabomu yake ya mkono na kuyatega sehemu mbalimbali za mtambo huo. Mara tu alipomaliza alimshika Nuru mkono wakatoka ndani wakikimbia mbio.
Joram aliduwaa kidogo akijiuliza lipi wafanye. Kurudi ndani ya jumba hilo isingewezekana kwani wakati wowote jumba hilo pia lingelipuka. Na kukimbia ingewachukua hatua chache tu kabla ya kukamatwa na risasi za askari wa eneo hilo. Lakini Nuru alijua la kufanya. Alimwongoza Joram katika upenyo aliokuwa amepita na Von hadi nje ya ua ambako walikimbia tena wakitegemea kumkuta rubani wa helikopta akiwemo, ili wamlazimishe kwa bastola awaendeshe kutoka nchini humo na kurudi nyumbani Dar es Salaam. Hakuwemo. Bila shaka miujiza iliyokuwa ikitokea ilimtia kiwewe hata akalazimika kuingia mitini, huwenda alilazimika kuikimbilia familia yake akiamini kuwa anaweza kuiokoa, baada ya kusikia hali ya mji imebadilika na kuwa ya vurugu na vurumai. Hivyo kiasi fulani Nuru alianza kukata tamaa. Lakini Joram alimrejeshea matumaini alipomwambia wapande, wakaingia ndani ya helikopta.
Joram alikuwa na ujuzi wa nadharia kuhusu kuendesha helikopta. Alilazimika kujikumbusha ujuzi huo kwa vitendo, jambo hilo liliwagharimu dakika zaidi ya mbili hivi. Wakati huo askari wa doria walikwisha kuwaona na kuanza kuwafuata kwa kasi zaidi. Mmoja wa askari hao aliilenga helikopta kwa bunduki yake na kujiandaa ili kuipiga risasi. Wakati huo huo jambo lingine la kushangaza likatokea. Jumba hilo lililokuwa hifadhi ya mitambo haramu ya makaburu likalipuka na kusababisha kishindo kikubwa katika eneo hilo. Moto wa kutisha ulipanda juu na kusambaa kote.
Wakati askari hao wakitazamana kwa mshangao wasijue nini kimetokea. Helikopta tayari ilikuwa angani. Walipokumbuka kuirushia risasi. Helikopita ilikuwa ndio kwanza ikibadili uelekeo kuelekea nchini Botswana, halafu Dar es Salaam, nchini Tanzania.