Riwaya: Tutarudi na roho zetu?

SURA YA KUMI NA MBILI

II

"Dakika yoyote kuanzia sasa! ama kweli tumekwisha", Kombora aliwaza akitoka dirishani baada ya kusimama hapo kwa muda akichungulia nje na kisha kukirudia kiti chake. Mzee huyu alikuwa ameamua lolote ambalo lingetokea limkute akiwa ofisini kwake. Hakuona sababu ya kutaabika ama kwenda kushuhudia maisha ya wanawe wanavyokata roho na kufa kikatili endapo nyumba yake ingekuwa miongoni mwa nyumba zizizo na bahati kusalimika.

Mara mawazo ambayo hakutaka yamjie akilini yakamtokea. Mawazo ya upweke, unyonge na msiba mkubwa. Mawazo ambayo yalikuwa yakimfunulia hali ambayo angekuwa nayo endapo ingetokea yeye kuwa mmoja kati ya wale watakaosalimika na familia yake nzima kuteketea, angewezaje kuishi bila ya mama watoto wake, yule mwanamke mpole ambaye hajaacha kumuonea haya kwa kiwango kile kile walipokuwa wachumba hadi leo wamekuwa pamoja kwa zaidi ya miaka thelathini. Angeishi vipi bila ya watoto wake wanne, mmoja akiwa wa kiume aliyehitimu Chuo Kikuu na kupata ajira mwaka jana na wale wa kike ambao wote wameolewa na kumpatia wajukuu watano. Maisha yangekuwa vipi endapo yote hayo yangebadilika ghafla kwa ajili ya ukatili wa utawala dhalimu wa weupe wachache huko Kusini.

Kisha akaikumbuka saa yake. Dakika kumi zilikuwa zimepita! Hakuyaamini macho yake. Akainuka na kupiga hatua mbili tatu akilirudia tena dirisha. Akachungulia chini. Mitaa yote ya Dar es Salaam ilikuwa kimya kabisa. Kelele zilisikika kwa mbali kutoka katika viwanda kadhaa vilivyokuwa vikiendelea na kazi. Inspekta Kombora akakirudia kiti chake na kuketi. Masikio yake yalikuwa wazi yakisubiri kwa hofu kudaka mlio wowote wa mashaka ambao ungesikika. Macho pia yalikuwa wazi yakitazama angani kupitia dirishani.

Dakika ishirini!

"Wakati wo..." alipotaka kusema sauti yake ikataishwa na ukelele wa ghafla ambao ulivuka kutoka angani. Bila kutegemea Inspekta Kombora akayafumba macho yake kwa nguvu huku akitamani kuweka vidole masikioni ili asisikie zaidi. Kelele ziliendelea kwa mvumo mkubwa zaidi. Hisia zilimfanya Kombora aamini kuwa zilikuwa kelele za kushangilia badala ya vilio na maombolezo kama alivyotarajia. Akasikia kwa makini zaidi. Wananchi walikuwa wakipiga kelele za kushangilia na kucheka kwa nguvu.
Watu wote!

Kuna waliopatwa na wazimu!

Dakika moja baadaye Kombora alikuwa miongoni mwa wananchi wengine katika chumba cha habari, ghorofa ya mwisho. Askari walikuwa wakitokwa na machozi ya furaha huku wakisikiliza redio BBC, iliyokuwa ikiendelea kutoa taarifa.

..."Tunawaletea habari hii kutoka BBC. Hadi sasa inaaminika kuwa utawala wa makaburu wa Afrika Kusini haujafanikiwa kuuzima moto huo mkali ambao unaendelea kuyateketeza majumba mbalimbali katika mji wa Johannesburg. Kadhalika haijafahamika watu wangapi wamepoteza maisha na wangapi wamejeruhiwa katika tukio hilo la kusikitisha japo inaaminika kuwa idadi ya vifo na majeruhi inaweza kuwa kubwa zaidi".

"Kadhalika mtambo wa siri uliokuwa umejengwa na utawala wa makaburu kwa ajili ya kuendesha setelaiti ya aina yake angani isiyoonekana kwa macho, umelipuliwa na wahandisi wake wote kuangamia. Inasemekana kuwa baada ya mtambo huo kulipuliwa chombo hicho cha ajabu kimeanguka katikati ya mji wa Johannesburg na kusababisha madhara makubwa kwa maisha na mali za wananchi. Pia inaaminika kuwa afya za wananchi katika mji huo zitakuwa mashakani kutokana na nguvu za nuklia zilizotumika kuunda chombo hicho".

..."Kwa kila hali imeonyesha dhahiri kuwa Joram Kiango akishirikiana na mwenzake yule msichana mrembo Nuru wameshiriki kwa njia moja ama nyingine kuhakikisha mtambo huo hauleti madhala kwa nchi za Kiafrika kama makaburu walivyokusudiwa. Na endepo vijana hao wasingeweza kufanya kazi ya ziada kama walivyofanya kwa utawala wa makaburu, dakika hii BBC tungekuwa tunatangaza msiba mkubwa kwa Afrika nzima kwani kulikuwa na mpango na mkakati kabambe wa kuzishambulia nchi zote zilizoko mstari wa mbele kwa wakati mmoja.

Kombora hakuweza kustahamili. Machozi mengi yalimtoka na kuteleza juu ya mashavu yake. Machozi ya furaha. Joram Kiango tena! Kwa mara nyingine ameliokoa taifa na Afrika nzima kuepuka kipigo cha kikatili kutoka kwa makaburu, kipigo ambacho kisingesahaulika. Joram ambaye alimfikiria vibaya kwa kutoweka kwake na fedha nyingi za umma ambazo alizichezea kote duniani.

Ghafla ikampambazukia Kombora. Joram hakuwa ameziiba zile pesa. Alikuwa amezichukua kwa mtondo ule ili ionekane kama ameziiba. Ili azitumie kwa shughuli hii pamoja na kuaminika kama msaliti mara aingiapo nchini Afrika Kusini. Angeweza kuchua hata pesa zote! Kombora aliwaza. Angeweza kuzitumia apendavyo! Kijana huyu ni nani katika Afrika kama sio malaika aliyeletwa kuishi kama binadamu kwa manufaa ya binadamu wengine?.

Kombora alirejea ofisini kwake. Mara tu alipoketi simu zilianza kumsumbua. Nyingi zikiwa za waandishi wa habari zikiuliza hili na lile. Swali kubwa lilikuwa kutaka kujua kama kweli ni Joram Kiango aliyefanya kazi hiyo ambayo majeshi yote ya nchi za Kiafrika yasingeweza kuifanya. Zaidi walitaka kufahamu Joram yuko wapi.

Simu ambayo ilimsumbua Kombora kuliko zote ni ile iliyotoka Ikulu. Alizungumza na Rais mwenyewe. "Tunamtaka haraka kijana huyo Inspekta Kombora. Kuna tuzo maalumu la ushujaa ambalo linamsubiri..."

Kwa jinsi Kombora alivyomfahamu Joram hakuamini kama angeweza kupatikana kwa urahisi kiasi hicho, na hasa kujitokeza aipokee tuzo hiyo hadharani.

Siku mbili baadaye uhai ulilirudia jiji la Dar es Salaam kama kawaida. Pilikapilika za mitaani, viwandani na maofisini ziliendelea mtindo mmoja. Kila uso ulikuwa na furaha, tabasamu likiwa karibu. Jina la Joram lilikuwa katika fikra za kila mmoja. Ambao hawakupata kumfahamu waliulizia ni nani huyo Joram Kiango?.

"Humfahamu?", waliulizwa huku wakitazamwa kama wapumbavu.

Tawi la Benki ya City Drive lilikuwa na uhai vilevile. wateja wengi walifurika kama kawaida wakiweka na kuchukua pesa, kuangalia mahesabu yao na shughuli nyingine mbalimbali. Pilikapilika hizo ziliwafanya wasimtazame zaidi ya kawaida mzee huyu aliyevaa kanzu nyeupe na koti jeusi, ambaye alikuwa na nywele na ndevu nyingi nyeupe kwa wingi wa mvi. Mkononi akiwa amebeba mfuko mnene wa ngozi. Aliwapita wateja wote, akipokea shikamoo zake hadi ofisini kwa meneja ambaye pia alimpokea kwa heshima zote, kwani haikuwa mara kwa mara kutembelewa na watu wenye umri kama huo.

"Marahaba", babu huyo aliitika. "Wewe ndiye mejeja mwenyewe?" alihoji mzee huyo aliyefika benki akisaidiwa na mkongojo wake.

"Ndiyo mimi babu, nikusaidie nini".

"Ndiye wewe uliyeibiwa zile pesa nyingi za kigeni?".

"Ni mimi mzee wangu, kuna tatizo gani tana babu".

"Basi pole sana kijana wangu na huu hapa mzigo wako", mzee huyo alisema huku akiufungua mfuko wake na kutoa mabunda ya noti. Pesa za kigeni na shilingi chache za Tanzania. "Nimetumwa na kijana mmoja anasema anaitwa Joram Kiango nikuletee. Amesema nikuombe radhi sana kwa kuzichukua bila ridhaa yako. Alikusudia kuzitumia kwa safari yake lakini alipata pesa nyingine kutoka kwa jasusi moja ambalo alilikamata kule New Afrika Hoteli hivyo alizitumia pesa zile badala ya hizi. Hata hivyo amesema zimepungua kidogo lakini atazilipa..."

Meneja alikuwa hamsikilizi kwa makini. Mshangao ulikuwa umemshika. Alimtazama mzee huyo kwa muda kisha akainama na kuanza kuzihesabu kwa mabunda. Katika hesabu ya haraka haraka zilipungua dola mia mbili. Akazirudisha katika mfuko wake na kuinua macho ili amshukuru mzee na kumwambia la kufanya. Hakumuona. Mzee alikuwa ameondoka bila ya kuaga wakati akihesabu pesa.

Meneja aliduwaa. Kisha alikumbuka la kufanya. Akauchukua mfuko wa pesa na kuondoka nao hadi katika gari lake. Akalitia moto hadi katika ofisi za Inspekta Kombora ambako alimwona moja kwa moja na kumsimulia mkasa mzima.

"My god", Kombora alifoka. "Aliyezileta pesa hizo kwako hakuwa mzee. Alikuwa kijana sana, Joram Kiango mwenyewe.

Meneja alizidi kushangaa. "Mbona alikuwa mzee sana Inspekta?, hata sauti yake ilionyesha".

"Huyo ni Joram Kiango", Kombora alimkatisha meneja. Ametumia moja ya mbinu zake ili asipatikane na kupewa heshima yake. Amejifanya mkongwe kama alivyofanya katika mkasa ule ulioitwa SALAMU TOKA KUZIMU", Kombora alijiinamia kwa muda. "Tulimhitaji sana", alisema kama aliyemsahau meneja huyo wa benki na badala yake kujisemea peke yake. "Anahitajika. Kumtafuta haitasaidia kitu. Kwa jinsi ninavyomfahamu hatajitokeza hivi karibuni hadi hapo mchango wake utakaposahaulika, au litakapotokea suala lingine linalohitaji ushujaa.-

'IWE ZAWADI YANGU KWA KILA MWANAMAPINDUZI WA KWELI KATIKA AFRIKA'. MWALIMU NYERERE ALIWAHI KUSEMA KABURU NI KABURU TU AWE MWEUPE AU MWEUSI NI KABURU TU. KUTOKANA NA MATENDO.

-TAMATI-- 0659-230-273
 
Asanteni kwenu wote mliofanikisha kukamilika kwa Riwaya hii tamu na ya kusisimua. Much love
 
Asanteni nyote kwa kutuletea kisa hiki cha kusisimua, Mwenyezi Mungu awabariki nyote!
 
Buriani Ben Mtobwa, hata sasa kaburini ungali ukinena
KABURU NI KABURU TU.AWE MWEUPE AU MWEUSI NI KABURU TU.KUTOKANA NA MATENDO!!!!
Shukran kwa wawasilishaji?
 
SALAMU KUTOKA KUZIMU



KIFO kaja duniani kwa kazi moja tu. Akikukuta umekwisha... Akikusalimia umekwisha... Hana mdhaha. Lakini sasa huyu anataka watu mashuhuri, watu wakubwa zaidi. Anataka kuifanya Afrika nzima iangue kilio na maombolezo ambayo hayajapata kutokea duniani. Na anataka hilo litokee siku moja, saa moja... "Bendera zote duniani zipepee nusu mlingoti", anasema huku akichekelea. "Sijawahi kushindwa..." Jasho linawatoka watu mashuhuri. Damu inamwagika kama mchezo. Inspekta Kombora machozi yanamtoka. Joram Kiango anabaki kaduwaa.


SURA YA KWANZA


"Bado nasisitiza kuwa tusithubutu wala kujaribu kufanya lolote kabla ya kuhakikisha kuwa Joram Kiango yu marehemu", ilidai sauti moja nzito.


"Naam, lazima afe", sauti nyingine iliunga mkono. "Afe kabla hatujainua mikono kufanya lolote tulilokusudia. Hakuna asiyefahamu jinsi kijana huyu alivyo hatari anusaye shari na kuingilia kati kuharibu harakati zote. Hajasahaulika alivyowakorofisha wale mashujaa waliotaka kuuangusha utawala wa nchi ya Ngoko katika tukio lile lililoitwa Dimbwi la damu. Kadhalika bado hatujasahau alivyosababisha vifo na kuharibu mipango ya majasusi waliotaka kuiharibu nchi hii katika mkasa ambao mtu mmoja aliuandikia kitabu na kuuita Najisikia kuua tena. Kwa kila hali Joram Kiango ni mtu hatari zaidi ya hatari zote zinazoweza kutokea, Hana budi kufa".


Kicheko kikavu kikasikika kidogo, kikafuatwa na sauti iliyokwaruza ikisema.


"Atakufa. Lazima afe. Na atakufa kifo cha kisayansi kabisa. Mpango huu tumeuandaa kwa uangalifu mkubwa, Na watekelezaji wake pia ni watu ambao wamehitimu vizuri katika nyanja zote zinazohusika na kazi hii, Tuondoe shaka kabisa. Mpango huu utafanikiwa kwa asilimia mia".


"Kwa hiyo ndugu Mwemyekiti", ilisema sauti ya mtu wa kwanza. "Niwie radhi kwa kukukata kauli. Ninachokuomba ni kuuahilisha mkutano huu na tusisubutu kukutana tena hadi hapo Joram Kiango atakapokuwa kaburini, Pengine mtaniona mwoga kupindukia, Lakni mimi sipedi kabisa kufanya jambo lolote wakati kijana yule akiwa hai. Mnajua jinsi alivyo na miujiza. Anaweza kuwa hapa akisikiliza mazungumzo yetu, kesho tukajikuta mahakamani bila kutegemea".


Ilizuka minong'ono, sauti mbili tatu zilimuunga mkono msemaji aliyemaliza kusema. Jina la Joram liliamsha hofu katika mioyo yao. Wakatazamana...


Walipenda pia kumwona Mwenyekiti wao uso kwa uso. Kwa bahati mbaya, hawakuweza kuona uso wake isipokuwa kiwiliwili tu, ambacho kilifunikwa kwa mavazi ya thamani kama walivyokuwa wamevaa wao. Mwanga mkali uliotokana na taa ya umeme iliyowekwa kwa namna iliwachoma macho kila walipotamani kumtazama Mwenyekiti usoni. Ni yeye tu aliyekuwa na nafasi nzuri ya kuwatazama wote mmoja baada ya mwinginge kikamilifu na kuwasoma nyuso zao. Wakati wa kumtambua Mwenyekiti ulikuwa bado haujawadia hivyo hawakupaswa kumuona kabisa isipokuwa sauti yake tu.


Mkutano huo ulifanyika katika chumba cha siri, chini ya ardhi katika mojawapo ya majumba ya kifahari yaliyoko Jijini Dar es salaam.


Kila aina ya tahadhari iliwekwa kuhakikisha usalama wa mkutano huu wa awali. Mkutano ambao ulikuwa umeitishwa ghafla, kwa njia za kutatanisha, hata wajumbe hao walijikuta wamefika kwenye mkutano bila kufahamu kilichowaleta hapo.


Mwenyekiti akaufungua mkutano huo kwa maneno machache akisema: "Tunataka kuitetemesha Afrika na kuishangaza dunia. Tunataka kuachia pigo ambalo halitafutika katika historia ya Ulimwengu". Wajumbe wakaelewa kinachoendelea. Ndipo mjume mmoja alipotoa rai ya kumaliza kikao hadi watakaposikia Joram Kiango amekuwa marehemu.


Tahadhari kubwa ilikuwa imechukuliwa wakati wa kuandaa mkutano huo. Wajumbe waliingia kwa siri kubwa wakipita milango tofauti, katika eneo hilo vilitegwa vifaa vya kisasa kwa ajili ya kuhakikisha kila mshiriki wa mkutano huo wa siri anahusika kwa njia moja ama nyingine. Walihakikisha pia hakuna kifaa au chombo chochote cha kunasa sauti ama kusikiliza maongezi hayo ya siri. Vinginevyo chumba hicho kingeweza kutoweka kisayansi kisionekane mlango wowote zaidi ya kuta za kawaida. Zaidi ya yote silaha za kisasa, hewa za sumu, buduki zisizotoa mlio, madawa ya kulevya na mbinu zingine zilikuwa tayari kutumika endapo lolote lingetokea. Kwa bahati mbaya, ni Mwenyekiti peke yake ndiye aliyejua mpango mzima kuhusu mkanda huo.


Kulikuwa na kila sababu ya kuweka tahadhari au uangalifu huo. Watu waliokutana katika mkutano huu hawakuwa watu wenye njaa ya pesa wala kiu ya utajiri. Ni watu mashuhuri walioshiba na kudhamiria kulinda shibe yao. Wote walikuwa na hadhi mitaani, nyadhifa serikalini, na heshima katika chama. Waliokutana hapa wote walikuwa na matarajio ya kuvuna matunda matamu. Matunda ambayo yangetokana na mkutano huo. Hakuna mjumbe aliyependa kukosa utamu wa matunda hayo. Hivyo wote walikuwa na dhamira moja.


"Inaonyesha kuwa Joram ni tishio kwa kila mtu hapa", Sauti nzito ya Mwenyekiti ilisema. "Hilo linanifanya nizidi kuwa na imani juu ya dhamira yenu. Joram anaogopwa kuliko Polisi na jeshi zima la nchi hii, Kwanini? Wanajeshi mko hapa, polisi mko hapa, Chama tawala kiko hapa. Serikali iko hapa. Anayekosekana hapa ni mtu huyo anayejiita Joram Kiango. Mtu mtundu sana, ambaye utundu wake ni madhara kwa watu wenye dhamira maalumu. Hakuna atakayeshuku kuwa kauawa. Daktari atampima na kuona kafa kwa kansa ya moyo. Atauawa kitaalamu na kufa kistaarabu. Msiwe na shaka".


Kimya kifupi kikafuata. Wajumbe wakatazamana usoni. Kimya kilimezwa na sauti ya Mwenyekiti alipoongeza maneno.


"Kwa hiyo, naahirisha kikao hiki kama alivyoshauri mjumbe. Tutakutana tena hapa baada ya wiki mbili, siku na saa kama za leo, kwa njia zetu zile zile, bila kusahau kuwa joram Kiango hatakuwa Joram tena ila hayati Joram Kiango. Na ifahamike kuwa kuitoa nje siri hii ni sawa na kujiwekea saini ya kifo chako mwenyewe".


"Ni kweli Mwenyekiti", sauti mbili tatu za wajumbe wenye hofu, ziliitikia.


ITAENDELEA 0784296253

Maseypr-kwa-1:24 AM
 
Nielekeze jinsi ya kuanzisha Uzi mpya kirchhoff

mkuu mnapewa ruhusa na wenyewe kuziandika RIWAYA zao humu??? isije ikawa mnafanya hivi bila ruhusa yoyote na kuwadidimiza waandishi wetu.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom