TUTARUDI NA ROHO ZETU?
SURA YA KUMI
Mkoba mdogo wa Joram Kiongo,
uliosheheni vifaa vyake muhimu kama
silaha ulitulia vizuri kwenye bega lake la
kushoto, akiwa mtulivu na mwenye
uhakika wa kile anachokwenda kukifanya,
alionekana kama mtu aliyechukua mzigo
wa kawaida kabisa ambao haukukuwa na
chochote cha hatari. Alizipiga hatua moja
baada ya nyingine akiipita baadhi ya
mitaa ya mji mkuu wa Afrika Kusini.
Alipishana na watu wengi, akaambatana
na wengine waliokuwa katika safari zao
za kawaida kama alivyokuwa yeye.
Kitu fulani katika damu yake
kilimnong'oneza kuwa anafuatwa. Hilo
halikumshangaza. Kwani tangu
alipoachana na Nuru alifahamu fika kuwa
asingekubaliana na ushauri wake wa
kwenda kumsubiri mahali ambapo
alipomwelekeza mpaka atakapomaliza
awamu hii ya mwisho ambayo ilikuwa ya
hatari mno. Akiwa ameshangazwa na
ushupavu wa msichana huyu, jinsi
alivyokuwa tayari kuihatarisha roho yake
kwa hiari yake mwenyewe, Joram aliamini
kuwa Nuru asingekubali kabisa kubaki na
kuikosa fursa hii ya mwisho. Fursa
ambayo endapo itafanikiwa isingefutika
katika kurasa za historia ya matukio
muhimu katika duniani.
Ushindi katika operesheni hii
ungewafanya Joram na Nuru kuingizwa
katika historia ya Afrika, kwani kama
watafanikiwa katika mpango wao
watakuwa wameinusuru Afrika nzima
kuteketezwa na makaburu.
Hivyo Joram hakujishughulisha kugeuka
nyuma, kwa hofu ya kuwafanya
makachero ambao aliamini kuwa
wamezagaa kote mitaani wakimtafuta
wakamshuku. Badala yake aliendelea na
safari yake huku akitafuta nafasi na
wasaa wa kumtia Nuru chenga ya mwili.
Hakumaliza mtaa huo kabla fursa hiyo
haijajitokeza. Katika kona ya mtaa huo
Joram alikuta mahali ambapo palikuwa
na ajali ya magari matatu yaliyogongana.
Watu wengi walikuwa wamekusanyika
kutazama ajali hiyo. Kati yao Joram
aliweza kuwaona baadhi ya watu wenye
dalili ya ukachero na uaskari. Hakuwajali.
Badala yake akajitia kama mmoja kati ya
raia waliokuwa wakitazama miili ya
madereva wawili ambao hawakuwa na
dalili ya uhai.
Aliitumia fursa hiyo kutoa kofia mfukoni
na kuiweka kichwani, pamoja na
kuyafunika macho yake kwa miwani ya
jua. Kisha akajipenyeza katika kundi hilo
na kutokea upande mwingine, hapo
akawa tayari amemchanganya Nuru.
Hivyo akaendelea na safari yake kama
alivyokusudia. Mluzi mdomoni, tabasam
usoni na tahadhari moyoni. Baada ya
mitaa kadhaa aliumaliza mji. Kwa mbali
aliweza kuona jengo lenye mtambo
aliokuwa akiuhitaji. Ili kuthibitisha
alitumia hila kuitazama ramani yake.
Hakuwa amekosea. Akaendelea na
msafara wake. Akaanza kujikumbusha
kwa mara nyingine mpango ambao
aliuandaa ili umwezeshe kufanyikisha
kazi iliyokuwa mbele yake.
Moyoni alijua kabisa kuwa alikuwa
amekaribia mbele ya domo la mauti lililo
wazi; kuingia ilikuwa rahisi na wajibu
wake, lakini kutoka kinywani humo akiwa
hai ni jambo ambalo hakuwa na uhakika
nalo kabisa. Alipiga moyo konde,
akakubali kufa kishujaa kwa ajili ya
Afrika, kutoka hai ilikuwa vigumu. Hata
hivyo Joram hakuogopa. Lakini
kutokuogpa hakukumfanya astahimili
adgabu, akajikuta akitokwa na sala ndefu
kimoyomoyo. Jambo ambalo hakumbuki
kwa mara ya mwisho alishiriki lini au
alishiriki wakati gani...
ITAENDELEA 0784296253