SIRI
episode 15
Mtunzi. Patrick CK
Kama maelekezo ya kazi
aliyopewa yanavyompasa kufanya,
baada ya kunasa maongezi kati ya
Edger na Stanley bila kupoteza
muda Judy akayatuma moja kwa
moja kwa Paul mkuu wake wa kazi
nchini Tanzania.Paul akiwa ofisini
kwake akisubiri taarifa toka kwa
vijana wake aliowatumakumfuatilia Damian Mwamba
akapokea faili lililotumwa na Judy
akalifungua na kutoa tabasamu.
“Judu anafanya kazi nzuri
sana” akawaza na kuanza
kuyasikiliza mazungumzo yale ya
Edger na Stanley.Akarudia kwa
mara ya pili kuyasikiliza kwa
makini sana halafu akampigia simu
Donald Nkebo
“Paul kuna habari gani mpya?
Donald Nkebo akauliza baada ya
kuipokea simu ya Paul
“Mr Donald kuna taarifa
nimeipata sasa hivi toka kwa Judy
ambayo ninadhani unapaswa
kuisikiliza.Ninakutumia sasa hivi”
akasema Paul “Sawa Paul.Nitumie sasa hivi
niisikilze halafu nikuelekeze nini
cha kufanya.” Mr Nkebo akajibu
akiwa na shauku ya kutaka kujua
kilichomo ndani ya maongezi hayo
Kwa haraka Paul akamtumia
Donald Nkebo maongezi yale ya
Edger na Stanley. Kama ilivyokuwa
kwa Paul,Dr Nkebo naye
akayarudia maongezi yale zaidi ya
mara mbili halafu akashika kichwa
akitafakari.
“Huyu kijana anaonekana ana
nia ya dhati ya kugombea urais.Ni
lazima tumdhibiti haraka
iwezekanavyo.Tukimuachia
mwanya hata kidogo anaweza
akatusababishia matatizo makubwa.Anafikiria hata
kuutangazia umma kwamba
aliwekewa sumu na watu kutoka
ndani ya chama chake,hatupaswi
kumuacha akafanya hivi.nadhani
wakati umefika wa
kuwanyamazisha watu hawa
wawili Edger na huyu mwenzake
Stanley anayeonekana kuwa
mshauri wake mkuu.Hii ni kazi ya
haraka ambayo Paul anatakiwa
aifanye haraka sana”akawaza
Donald na kumpigia Paul simu
“Mr Donald” akasema Paul
“Paul nimeyasikiliza
mazungumzo yao.Kwanza kabisa
nimegundua Edger anapata
msaada mkubwa wa kimawazo toka kwa huyu Stanley ambaye
anaonekana ndiye mshauri wake
mkuu.Nataka utumie kila mbinu
unayoijua mpaka leo jioni uwe
umekwisha mfahamu huyo Stanley
ni nani na uanze mara moja
kutafuta namna ya
kumnyamazisha.Edger akimkosa
huyu Stanley atavunjika moyo
kwani yeye ndiye mwenye kusuka
mipango yake yote.Jambo lingine
Edger anaonekana kukubaliana na
ushauri wa Stanley wa kutaka
kuhama chama ili akagombee uraisi
katika chama cha upinzani.Vile vile
anafikiria kuutangazia kwamba
alipewa sumu ili afe na hili si jambo
zuri hata kidogo.Edger anatakiwa adhibtiwe haraka sana kabla
hajatoka hospitali na kuanza
harakati zake za urais.Nataka
mipango ya kumuondoa Edger
ianze haraka sana.Vipi kuhusu
Damiani mmefikia wapi? Akauliza
Donald
“Donald kwanza kuhusu Edger
sishauri kumuondoa kwa
sasa,tuendelee kumchunguza ili
tuufahamu mtandao wake
wote.Huyu Stanley tutamuondoa
haraka sana ili kuzidi kummaliza
nguvu Edger na mipango ya
kumuondoa inaanza haraka
sana.Kuhusu Damiani mwamba
tunaendelea vizuri na leo tunaanza
kupiga hatua ya awali kwa Mr Mwamba.Tunachotaka kukifanya
kwanza ni kutega kifaa maalum
katika simu yake ambacho
kitakuwa kikituonyesha kila
mahala anapokuwa.Nina imani
mpaka jioni ya leo nitakupa taarifa
kamili ya wapi tumefikia kuhusu
Damiani.Vijana wanafanya kazi
usiku na mchana”
“Nanafurahi kusikia hivyo
Paul.Ongeza bidii ili mheshimiwa
rais aanze kusikia hatua
tunazozichukua.”
“Nimekuelewa Mr
Donald,tunajitahidi sana na
ninakuahidi kazi nzuri
itakayomfurahisha hata
Mheshimiwa rais”akasema paul na kukata simu
*******************
Blue Lavender hotel ni moja
kati ya hoteli iliyojizolea umaarufu
mkubwa ndani na nje ya nchi kwa
upikaji wa vyakula vya kila aina na
vya mataifa mbali mbali.Ni hoteli
hii ambayo Damiani Mwamba
hufika mara kwa mara hasa nyakati
za asubuhi kupata supu.Kwa siku
kadhaa sasa amekuwa akifuatiliwa
na vijana wa Paul
wanaomchunguza bila yeye
kufahamu.Moja kati ya vitu
walivyovigundua katika uchunguzi
wao waligundua kwamba Damian anapenda sana kufika katika hoteli
hii kupata supi kila siku asubuhi.
Kama kawaida yake alishuka
garini na kuingia katika ukumbi
mzuri ulioezekwa kwa makuti safi
na kuifanya mandhari ya hapa
kuwa ya kuvutia mno,akaenda
katika meza ambayo imezoeleka
kama meza yam zee Damian akakaa
huku akisoma gazeti wakati
akisubiri supu.Hakuwa na haja ya
kuagiza kwani anafahamika sana
hapa.Imekuwa ni kawaida yake kila
siku kununua magazeti na kuja
nayo hapa na kuyasoma huku
wakati akiendelea kupata supu.
Dakika tatu toka awasili katika
hoteli hii,vijana wawili waliovalia suti safi walioonekana kama
wafanya biashara wakubwa nao
wanawasili na kukaa katika meza
ya karibu kabisa na Damian
Mwamba nao hali kadhalika
wakaagiza supu.Damian akiwa
mezani peke yake hakuweza
kung’amua kuwa vijana wale
wawili waliokuwa wamekaa karibu
yake ni vijana hatari waliokuwa
wakifanya kazi ya kumfuatilia usiku
na mchana na kujua nyendo
zake.Vijana wale waliendelea na
maongezi yao kama kwaida huku
wakipata supu waliyokuwa
wameagiza huku Damiani
akiendelea kusoma gazeti lake.
Akiwa amezamisha mawazo yake katika gazeti lile kubwa
lililosheheni habari mbali mbali za
siasa mara ghafla kikatokea
kishindo kikubwa cha mlipuko wa
kitu na kuzua taharuki kubwa huku
wateja wengine waliokuwepo hapo
hotelini wakianguka kwa
mstuko.Kama umeme kijana mmoja
kati ya wale wawili waliokuwa
wakimfuatilia Damiani Mwamba
akajirusha toka pale mahala
alipokuwa amekaa na kumpiga
kichwa kizito Damian Mwamba
akaanguka na kupoteza
fahamu.Kijana ambaye naye
alianguka chini kwa kasi ya aina
yake akaingiza mkono mfukoni kwa
Mr Damiani na kuitoa simu yake.Akaifungua kwa haraka na
kupachika kidude Fulani kidogo
sana chenye muundo kama karatasi
katika mfuniko wa simu ile
ambacho si rahisi kwa mtu kuweza
kuking’amua kuwa kimepachikwa
hapo.Akaifunga simu ile na
kuirudisha mfukoni mwa Mr
Mwamba.Ni kitendo kilichochukua
sekunde zisizozidi ishirini.Hakuna
mtu yeyote aliyeweza kukishuhudia
kitendo kile kwa sababu watu wote
kwa sasa walikuwa ndani ya
taharuki kubwa kutokana na
kishindo kile cha mlipuko na kila
mmoja alikuwa akijaribu
kujiokoa.Ni kitendo kilichofanyika
kwa haraka,wepesi na umakini wa hali ya juu sana kisha vijana wale
wakatoweka.
Dakika kama kumi hivi tangu
kishindo kile cha mlipuko
kitokee,gari nne za polisi zikafika
kwa kasi zikiwa zimesheheni askari
wenye silaha waliojizatiti vilivyo
,nyuma yao kulikuwa na gari
kubwa la kuzima moto.Haraka
haraka na kwa umakini wa aina
yake polisi wakaanza kudhibiti hali
ya usalama na kuanza zoezi la
kuwaondoa watu waliokuwamo
hapo hotelini ambao wengine
walikuwa wamejeruhiwa kwa
kukatwa na vitu kama chupa au
kuunguzwa na vitu vya moto.Wapo
watu wachache waliokuwa wamepoteza fahamu kutokana na
kishindo cha mlipuko ule.Gari tatu
za wagonjwa zilikuwa tayari
zimefika na kuwapakia wale
wagonjwa waliokuwa wameumia
na wengine kupoteza fahamu
wakakimbizwa katika hospitali ya
karibu kwa matibabu.Miongoni
mwa watu waliokuwa wamepoteza
fahamu alikuwapo Damiani
Mwamba .
Katika maegesho ya magari
kulikuwa na magari matatu
yaliyokuwa yakiwaka moto na
kikosi cha zimamoto kilikuwa
kikiendelea na kazi ya kuuzima
moto ule ili usije ukasambaa katika
magari mengine na kusababisha maafa makubwa zaidi.Watu wote
walikwisha tolewa mahala hapa
ambapo kwa sasa palionekana
kama si mahala salama .Wataalamu
wa milipuko kutoka jeshi la
wananachi wa Tanzania
wakishirikiana na wale wa jeshi la
polisi waliwasili na kuanza mara
moja kazi ya kuchunguza chanzo
cha mlipuko ule na kuangalia kama
kuna dalili zozote za kutokea
milipuko zaidi.
*******************
Sekunde ambayo yule kijana
,aliweka kile kifaa kilicho kama
karatasi katika simu ya Damian Mwamba,Paul akaiona taa ya kijani
ikiwaka katika mitambo yake
ishara kwamba kifaa kile kinafanya
kazi akatabasamu.Muda huo huo
akachukua simu na kumpigia
Damian Nkebo
“Paul kuna habari gani mpya?
Donald Nkebo akauliza
“Mr Nkebo ,nimeona
nikutaarifu habari nzuri kwamba
dakika kadhaa zilizopita vijana
wangu wamefanikiwa kuweka kifaa
maalum katika simu ya Damian
mwamba ambacho kitakuwa
kikitupa mwelekeo kamili wa kila
mahala anapokuwa Mr
Mwamba.Kama unavyofahamu yule
ni mfanyabiashara mkubwa kwa hiyo kila mahala aendapo ni lazima
awe na simu yake kwa maana hiyo
hivi sasa tutakuwa tukimfuatilia
kwa masaa ishirini na
manne.Tutaweza kujua yuko
wapi,anaongea na nani na
anaongea nini.Nina imani baada ya
muda mfupi ujao tutakuwa
tumepata kitu cha kuweza
kumwondoa kabisa katika
ulimwengu huu wa siasa.”
“Kazi nzuri sana Paul”akasema
Donald Nkebo
“Hata hivyo Mr Donald wakati
wa kutekeleza jambo hilo
tulilazimika kufanya tukio dogo ili
kufanikisha shughuli nzima”
“Tukio dogo? Hebu nifafanulie”akauliza Donald
akionekana kuwa na wasiwasi
kidogo
“Tulilazimika kufanya mlipuko
mdogo ndani ya gari moja
tulilokuwa tumeliegesha pale kwa
zaidi ya siku mbili.Damian
Mwamba ana mazoea ya kwenda
kupata supu katika hoteli ile kila
siku hivyo tukalazimika kufanya
tukio dogo ili kuweza kufanikisha
mpango wetu”
“Paul hakuna madhara yoyote
yaliyotokea?Nina uliza hivyo kwa
sababu lazima uchunguzi
utafanyika.Nataka nipate picha
kamili ili na mimi nije kitu cha
kufanya”akasema Donald “Ulikuwa ni mlipuko ambao
haukusababisha kifo au madhara
makubwa kwa hoteli zaidi ya gari
mbili zilizokuwa karibu na gari letu
lililokuwa limebeba mlipuko ule
kuwaka moto.Vijana wetu wote
wako salama salimini na kwa hivi
sasa wako njiani wanarudi ofisini
baada ya kuikamilisha kazi.Nitazidi
kukupa taarifa kadiri tunavyopiga
hatua.Nimeona nikujulishe ili kama
kutatokea tatizo lolote basi uwe
tayari kulimaliza haraka”
“Sawa Paul,kazi nzuri sana
Paul.Endelea kunipa taarifa ya kila
tukio linalotokea.Na kama una
tatizo lolote lile usisite
kunifahamisha.Ukumbuke katika operesheni hii tunao mkono wenye
nguvu wa mheshimiwa rais kwa
hiyo usiwe na wasi wasi na kitu
chochote kile.”
“Nalielewa hilo Mr Nkebo na
nitakueleza iwapo kuna mahala
tumekwama au la”
Paul akakata simu akaigeukia
mitambo yake.
“Sasa umeingia katika mikono
yetu Damian.Kiama chako
kimefika.Taratibu sana
tutakupoteza katika uwanja wa
siasa” akawaza Paul huku akicheza
na kompyuta
******************** Taratibu Mr Damiani Mwamba
alianza kurejewa na
fahamu.Akapepesa macho ili
kutazama vizuri akagundua
alikuwa katika chumba kilichokuwa
na harufu kali ya dawa.Mara moja
akapata picha kuwa mahala hapa ni
hospitali.
“Mzee mwamba unajisikiaje
sasa? Daktari aliyekuwa pembeni
akauliza baada ya kugundua mzee
Damiani mwamba tayari
amekwisha rejewa na fahamu zake.
“Kichwa kinaniuma
sana.Siwezi hata kukiinua” Akajibu
Mr Mwamba kwa taabu.
“Pole sana.Inaonekana
uligonga kichwa chako katiak sehemu ngumu baada ya mlipuko
kutokea” Daktari na kumbukumbu
ya tukio lililotokea Blue lavender
hotel ikarejea kichwani
“Daktari vipimo vyako
vinaonyesha nimeumia kiasi gani?
Akauliza Damian kwa wasiwasi
“Mr Mwamba vipimo
vinaonyesha kuwa haukuumia sana
zaidi ya kupoteza fahamu baada ya
kugongesha kichwa katika kitu
kigumu na mstuko ule ukakufanya
upoteze fahamu”
“Kwa hiyo ninaweza
kuruhusiwa kurudi nyumbani
leo?akauliza Damian
“Ndiyo Mr
Mwamba.Tutakufanyia tena vipimo kwa mara ya pili na kama
hatutaona tatizo lolote
tutakuruhusu uende
nyumbani”akasema daktari.Damian
mwamba akarejesha kumbu kumbu
hotelini ulikotokea mlipuko ule.
“Kitu gani kilisababisha
mlipuko ule?Lilikuwa ni bomu au ni
mtungi wa gesi? Akajiuliza
“Lakini kishindo kilikuwa
kikubwa sana na sina hakika kama
kishindo kile kilikuwa ni cha
mtungi wa gesi. Yawezekana likawa
ni bomu.Kama ni bomu lilikuwa la
kutegwa?Na kama lilitegwa nini
hasa malengo yake?akaendelea
kujiuliza
“Nisiumize kichwa sana kwa sasa.Nikitoka hapa nitapata ripoti
kamili ya kilichotokea.Nashukuru
Mungu niko salama.” Akawaza Mr
Mwamba
HAIFA - ISRAEL
Baada ya kutoka hospitalini Dr
Olivia akarejea tena hotelini kwake
kupumzika.Alipojilaza kitandani
akaanza kutafakari juu ya
kilichotokea hospitali
“Nahisi Edger hakufurahishwa
na Christopher na ndiyo maana
alionyesha mabadiliko ya ghafla
mara tu Chris alipokuja kukaa nasi
pale bustanini.Wakati
nikizungumza na Chris alikuwa
mkimya na hakutaka kuzungumza chochote,na mara tu baada ya Chris
kuondoka Edger aliomba
nimrudishe ndani na hakutaka tena
kukaa na mimi.Kuna kitu
kinamsumbua yule jamaa” akawaza
Dr Olivia na kutabasamu baada ya
sura ya Christopher kumjia
kichwani
“Christopher ni kijana
mzuri,anayevutia kukaa na
kuongea naye.Amenivutia
sana.Nitajaribu kumshawishi aje
Tanzania. Akikubali nitafurahi
sana” akaendelea kuwaza Dr Olivia
“Lakini kwa nini nisimpigie
simu na kuongea naye sasa
hivi?Nadhani hili ni wazo zuri sana
ngoja nipige simu pale hospitali niombe kuzungumza na
Christopher” Dr Olivia akawaza
huku akiinuka na kuiendea simu
iliyokuwapo pale
mezani,akabonyeza namba za
hospitali ile alimolazwa
Christopher ,na simu ikapokelewa
na mwanadada mwenye sauti nzuri
Olivia akaomba aunganishwe na
chumba cha Christopher.Baada ya
sekunde kadhaa akaisikia sauti
nzuri ya kiume ikiita
“Halloo Dr Olivia”
“Hallo Chris unajisikiaje?
Olivia akauliza
“Najisikia vizuri,maendeleo
yangu ni mazuri sana.Uko wapi
sasa hivi Olivia,hotelini?akauliza Christopher
“Ndiyo niko hotelini
nilikofikia.Sina mtu wa
kuzungumza naye naye nikaona
nikupigie japo tuongee machache
kama sintakuwa nakusumbua.” Dr
Sanda akasema
“Ni kama ulikuwa katika
mawazo yangu Olivia kwani hata
mimi ninajisikia mpweke sana hapa
hospitalini na nilitamani kupata
mtu wa kuzungumza naye.Nafurahi
sana kukutana na waafrika
wenzangu japokuwa hatutoki
katika nchi moja lakini tunaweza
kuishi kama ndugu ndugu
moja”akasema Christopher na
sekunde kadhaa zikapita halafu akasema
“Dr Olivia hoteli ulikofikia ni
mbali sana na hapa
hospitali?akauliza Christopher
“Hapana hakuna umbali mrefu
ni mwendo wa dakika kumi tu.Kuna
nini Christopher?akauliza Dr Olivia
“Olivia kama hutajali,na kama
unayo nafasi kwa nini usije hapa
hospitali tukakaa ,tukaongea na
kufahamiana zaidi kwa sababu
naona kama siku imesimama masaa
hayaendi”akasema Christopher
“Wazo lako zuri Chris.Nitafika
hapo si muda mrefu kwani hata
mimi nimeboreka sana hapa
hotelini”
Dr Olivia akasimama akiwa ni mwingi wa furaha.
“Kwa kuwa Edger alisema
anahitaji kuwa mwenyewe leo
apumzike,ngoja niitumie nafasi hii
kwenda kuongea na Chris.Ni kijana
mchangamfu,anayefurahisha na
ambaye huchoki unapokuwa
naye.Nimeboreka sana peke yangu
hapa hotelini,Judy yeye anapenda
kujifungia chumbani kwake”
Dr Olivia akawaza huku
akifungua mkebe wake wa
vipodozi.Haraka haraka bila
kupoteza muda akajiweka vizuri
halafu akamfuata Judy chumbani
kwake akamuaga kuwa anakwenda
hospitali.
Dakika kumi na tano baadae akawasili hospitalini akaenda
mapokezi akaomba Chris ataarifiwe
kwamba amekwisha fika na
atamkuta bustanini.Dakika tano
baadae Chris akashuka na kukutana
na Olivia
“Nashukuru kwa kufika kwako
Dr Olivia.Siku yangu nahisi kama
ilikuwa imesimama.Sehemu kama
hii ni nadra sana kukutana na mtu
kutoka afrika na ikitokea bahati
umekutana naye inakuwa ni faraja
kubwa sana.Nasikia furaha
kukutana nawe Dr Olivia.Najihisi
kama niko nyumbani”akasema
Christopher
Dr Olivia huku akitabasamu
akajibu “Hata mimi nafurahi sana
kukutana nawe.Mara ya kwanza
kufika hapa nilikuwa mpweke sana
kwa sababu Edger hakuwa na
fahamu na sikuwa na mtu yeyote
wa kutoka nyumbani wa kuongea
naye.Baadae akatumwa Judy kuja
kunisaidia kumuuguza Chris kidogo
nikafarijika” akasema Dr Olivia
“Dr Olivia samahani kwa
kuuliza swali hili je wewe na Edger
mna mahusiano yoyote ya
kimapenzi?
Dr Olivia akacheka tena
kicheko kikubwa kilichomfanya
Christopher atabasamu.
“Kwa nini umeuliza hivyo
Chris? Dr Olivia akacheka huku akitabasamu
“Kwa sababu niliona dalili
Fulani za wivu machoni mwa Edger
wakati nimekaa na ninyi asubuhi ya
leo hapa bustanini.”
Dr Olivia akacheka kidogo na
kusema
“Mimi na Edger,hatuna
mahusiano yoyote ya
kimapenzi.Edger ni mgonjwa
wangu na ni mimi ndiye niliyemleta
hapa Israel kwa matibabu.Sikuwa
nikifahaiana naye hadi alipoletwa
katika hospitali yetu akiwa
mgonjwa hajitambui.Yeye ni
mwanasiasa na mimi ni
daktari”akasema Dr Olivia
“Niliogopa kwa namna Edger alivyokuwa ananitazama nikajual
labda wewe nay eye mna
mahusiano ya kimapenzi.Lini
unategemea kurudi nyumbani
Tanzania?”
“Kurudi nyumbani inategemea
na hali ya ugonjwa wa Edger
inavyoendelea.Iwapo atapata nafuu
kwa haraka basi nitarejea
nyumbani hivi karibuni.Siwezi
kumuacha Edger peke yake wakati
mimi ndiye niliyemleta huku
Israel.Ungependa kuja kutembea
Tanzania siku moja?
“Lazima nitakuja Tanzania
mara tu baada ya
kupona.Ninaipenda sana Tanzania.”
“Nitafurahi sana kama utafika kutembea Tanzania.lakini
ningefurahi zaidi iwapo ukija
Tanzania ufike katika hospitali yetu
na mimi niwe daktari wako”
Christopher akacheka baada
ya kauli ile ya Dr Olivia
“Hata mimi ningefurahi sana
kama ungekuwa daktari
wangu.Ningejua mapema
kama kuna hospitali nzuri Tanzania
inayotibu maradhi haya ya moyo
nisingepoteza wakati wangu kuja
kutibiwa huku Israel,ningekuja
moja kwa moja Tanzania”
“Muda wowote karibu sana
Tanzania.Nitakuwa mwenyeji
wako”
Maongezi kati ya Chris na Dr Olivia yakaendelea hadi usiku wa
saa nne .Ni mara ya kwanza kwao
kukutana lakini kwa muda huu
mfupi walitokea kuzoeana kupita
kiasi.