SEHEMU YA 36
ILIPOISHIA:
Harakaharaka mama alienda kupewa taarifa, akaanza kuangua kilio kwa sauti ya juu huku akilitaja jina langu, wanawake wengine nao wakawa wanalia kwa huzuni, vilio vikawa vimeamka upya.
“Unatakiwa kujikaza mdogo wangu,” aliniambia Bonta, wakati tukipelekwa kwenye chumba kilichokuwa na mwili wa marehemu.
SASA ENDELEA...
Tuliingia na kukuta mwili wa baba ukiwa umelala na kutulia kitandani, akiwa tayari ameshavalishwa sanda. Ungeweza kudhani baba amelala tu lakini kumbe ndiyo alikuwa ametutoka.
Baba mkubwa ndiye aliyekuja kutufungulia sanda upande wa kichwani, nikamtazama baba, kiukweli nilijitahidi sana kujikaza kiume kama alivyosema Bonta lakini haikuwezekana.
Nilipiga magoti na kuukumbatia mwili wa baba huku uso wangu ukiwa umejawa na machozi, donge kubwa likawa limenikaba kooni kiasi cha kunifanya nishindwe hata kumeza mate, nikaanza kuangua kilio kwa huzuni kubwa huku nikimuita baba.
Kwa kipindi ambacho baba alikuwa mzima, kabla hajaanza kuumwa, alitulea vizuri sana sisi wanaye, alijitahidi kwa kadiri ya uwezo wake kuhakikisha tunapata malezi bora na elimu bora ingawa mambo yalianza kuharibika alipoanza kuugua na kuishia kulala kitandani.
Pengine hata leo hii angegundua ni kazi gani niliyokuwa naifanya baada ya kushindwa kuendelea na masomo kutokana na ukosefu wa karo, pengine angeumia sana ndani ya moyo wake kwa sababu kila sikuwa alikuwa akitusisitiza wanaye kwamba elimu ndiyo kitu pekee kinachoweza kutukomboa maishani.
Kwa zaidi ya dakika kumi na tano nzima nilikuwa nikiendelea kulia tu huku nikiwa nimemkumbatia baba, ikafika mahali ikabidi niondolewe kwa nguvu kwa sababu ningeweza hata kuzimia kutokana na kulia mfululizo kwa muda mrefu.
Nilipotolewa kule chumbani, nilipokelewa na mama ambaye alinikumbatia huku na yeye akianza upya kulia. Ilikuwa ni siku ya huzuni kubwa sana kwangu, mama akawa ananiambia kwamba lichaya mimi kujitahidi kutafuta fedha za matibabu ya baba, alikuwa amekataa kuendelea kukaa nasi na kuamua kurejea kwa Mungu wake. Ilifika mahali, mwili wangu ukawa umeishiwa nguvu kabisa kwa sababu ya kulia, macho yakiwa yamevimba na kuwa mekundu sana.
“Inabidi upate kitu kitakachokupunguzia uchungu ndani ya moyo wako,” alininong’oneza Bonta, akanishika begani na kunikumbatia, akawa ananipeleka nje ambapo ilibidi tujitenge na waombolezaji wengine na kukaa pembeni kidogo ya nyumba, chini ya mti wa mkorosho.
“Changamsha kichwa mdogo wangu, haya ni mambo ya kawaida kabisa, sisi wote hapa duniani ni wapita njia tu, cha msingi tumuombee apumzike mahali pema peponi,” alisema Bonta huku akitoa kichupa kidogo kilichokuwa na ile pombe kali anayopenda kunywa.
Nilikifungua na kupiga funda moja, nilipomeza nilihisi tumbo lote linawaka moto na muda mfupi baadaye, nikaanza kujisikia vizuri. Bonta akawa anaendelea kunisisitiza kuinywa ile pombe. Japokuwa kichupa kilikuwa kidogo lakini nilipofikisha nusu, tayari nilikuwa nimechangamka kwelikweli.
Kuna wakati nilikuwa nasahau kabisa pale ni wapi na nini kimetokea, tukawa tunaendelea na stori za hapa na pale na Bonta, mara Bonta aliingiza mkono mfukoni na kutoa msokoto, akatazama huku na kule kuhakikisha kwamba hakuna mtu yeyote aliyekuwa akitutazama.
Akauwasha na kuvuta kidogo kisha akanipa, na mimi nikavuta huku safari hii nikiwa nimeshaanza kuzoea, ile hali ya kukohoa ikawa imeisha kabisa, nilipovuta mara kadhaa, ndiyo kabisa nilizidi kujiona kama hakuna chochote kilichotokea.
Hata sijui nini kiliendelea, nilishtukia tu nimepitiwa na usingizi mzito, tulipozinduka tayari ilikuwa ni alfajiri. Unajua tatizo la hivi vilevi, kama pombe na madawa mengine ya kulevya, japokuwa watu wengi huwa wanaamini kwamba vinapoteza mawazo, ukweli ni kwamba huwa vinakusahaulisha kwa muda mfupi tu na vikiisha kichwani, matatizo yanarudi palepale.
Japokuwa usiku ule baada ya kupiga pombe kali na kusindikizia na msokoto nilijiona kama nipo dunia nyingine kabisa, kulipopambazuka tu hali ilikuwa imerudi palepale, moyo wangu ulikuwa ni kama una kidonda. Na jinsi pombe zisivyo na adabu, kama ukinywa usiku wa manane, ukiamka asubuhi japokuwa zinakuwa zimepungua sana kichwani lakini bado zinakuwepo.
Kwa hiyo japokuwa ilikuwa ni siku mpya bado kichwa changu kilikuwa na ‘mawenge’ na kwa mtu ambaye ananifahamu vizuri, angeweza kugundua kwamba sikuwa kwenye hali yangu ya kawaida.
“Hapa ni kwenye umati wa watu na kama unavyojua tena kazi zetu hatutakiwi kufanya jambo lolote linaloweza kuwafanya watu waanze kukutilia mashaka.”
“Mimi hapa ni kwetu, wala usiwe na wasiwasi.”
“Kuwa kwenu siyo sababu, polisi wapo kila sehemu, tunaweza kuja kukamatwa hata hapahapa,” alisema Bonta kwa msisitizo lakini aliyokuwa anayazungumza yalikuwa yakiingilia kwenye sikio moja na kutokea kwenye sikio la pili.
“Hebu nipe kwanza nizimue,” nilimwambia Bonta nikimaanisha anipe tena ile pombe kali, akanitazama kwa muda kisha akashusha pumzi ndefu, kumbe alikuwa na vichupa vingine kadhaa vya ile pombe ya Kizungu ambayo hata sijui inaitwaje, akanipa kimoja na kuendelea kunisisitiza kwamba natakiwa kuwa makini tusije kuibua matatizo yasiyokuwa na msingi.
Nilikipiga kile kimoja kwa kasi na licha ya ukali wake, nilipokishusha chini tayari kilikuwa kimeshafika nusu.
“Hapana Snox, hatuendi hivyo,” alisema Bonta huku akinipokonya kile kichupa, akakifunga vizuri na kukirudisha mfukoni mwake. Sikutaka kubishana naye, nikatulia huku nikiisikilia ile pombe ikisambaa mwilini kwa kasi ya ajabu.
Mara nilianza kuhisi kama lile jeraha langu pale mguuni linaniwasha, nikapandisha suruali na kulitazama, sijui ndiyo akili ya pombe au kitu gani, nilijikuta nikitamani kulichubua na kutoa ngozi ya juu ambayo ilikuwa ikilifanya jeraha lionekane limeanza kupona.
Bonta hakushtukia nilikuwa nafanya nini, nikawa nimetulia naendelea kujichubua na cha ajabu hata sikuwa nasikia maumivu. Alipokuja kushtuka, tayari nilikuwa nimemaliza kulichubua lote na kwa sababu kidonda bado hakikuwa kimepona, damu nyingi zikaanza kunivuja mguuni na kulowanisha suruali na kiatu changu.
“Mambo gani umeanzahayo Snox?” alisema Bonta kwa sauti iliyoonesha kwamba alikasirika, wakati hayo yakiendelea, kule upande wa pili vilio vilikuwa vikiendelea kusikika, huku wanawake wengine wakiendelea kupika chai kwa ajili ya waombolezaji.
“Kenny unaitwa ndani,” alisema mtoto mmoja wa jirani, aliyetumwa kuja kuniita. Kama nilivyoeleza awali, jina nililopewa na wazazi wangu ni Kennedy ila wengi walikuwa wakilifupisha na kuniita Kenny, ingawa upande wa pili kwenye kazi haramu, jina langu lililokuwa linafahamika lilikuwa ni Snox.
Niliinuka na kutaka kuelekea ndani lakini cha ajabu, nilijikuta nikipepesuka sana, ni hapo ndipo nilipoelewa kwamba pombe siyo chai, ile pombe niliyokunywa ilikuwa imenichukua kwelikweli, nilijitahidi kujikaza lakini wapi, nikawa naendelea kupepesuka, hali iliyomshangaza kilammoja.
“Huyu si ndiyo mtoto mkubwa wa merehemu?”
“Ndiyo! Si Kenny huyu?”
“Sasa mbona amelewa asubuhi yote hii wakati maiti ya baba yake ipo ndani hata bado haijaenda kuzikwa?”
“Halafu mbona amelowa damu mguuni?” niliwasikia wazee wa pale mtaani ambao walikuwa wamejumuika pale msibani wakinijadili, sikuwajali, nikapita kwa hatua ndefundefu za kilevi na kuingia mpaka ndani.
Japokuwa mama alikuwa kwenye huzuni kubwa, alishtuka sana na hali niliyokuwa nayo, akaacha kulia na kuanza kunitolea macho, akiwa ni kama haamini alichokuwa anakiona.
“Umeanza lini kunywa pombe?” aliniuliza mama kwa mshangao, uso wake ukiwa umelowa kwa machozi na macho yake yakiwa yamevimba na kuwa mekundu kwa sababu ya kumlilia baba.
“Sijanywa pombe!” nilisema kilevi huku nikijitahidi kusimama kikakamavu, kumbe ndiyo nilikuwa nazidi kuharibu.
“Halafu kumbe ile harufu ya bangi iliyokuwa inasikika wewe ndiye uliyekuwa unavuta?”
“Ha..pa...na mama,” nilisema kwa kubabaika, baba zangu wadogo na ndugu zangu wengine waliokuwa wamekusanyika kwenye chumba kimoja kwa ajili ya majadiliano ya kifamilia, walikaa kimya wakisikiliza mazungumzo yangu na mama.
“Tuachane na hayo mwanangu,” alisema mama huku akianza tena kuangua kilio, watu wote wakawa kimya mle ndani, baba mdogo akavunja ukimya.
“Tumeitana kama familia kwa ajili ya kujadili taratibu za mazishi, je, tunataka baba akazikwe makaburini au hapahapa nyumbani, lakini pia tumejipangaje kuhusu gharama za jeneza na matumizi mengine ya msibani?” alisema baba mdogo ambaye ndiye aliyekuwa amepewa jukumu la kuwa msemaji wa familia kwenye msiba huo.
“Nitafanya kila kitu mimi, jeneza shilingi ngapi kwani?” nilisema kwa sauti iliyoonesha wazi kwamba mdomo wangu ulikuwa mzito kwa sababu ya pombe, hakuna aliyenijibu, nikaingiza mkono mfukoni na kutoa burungutu la noti za shilingi elfu kumikumi, hata sikuhesabu nikamkabidhi mama lakini alikataa kuzipokea, akawa anaendelea kulia, ikabidi baba mdogo ndiyo azipokee.
Sijui nini kilitokea, wakati nikijiweka vizuri suruali yangu, bastola iliponyoka kutoka pale kiunoni nilipokuwa nimeificha na kudondoka chini, watu wote wakapigwa na butwaa, kwanza kugundua kwamba nilikuwa na bastola kaini pia kugundua kwamba mguu wangu ulikuwa umelowa damu kuonesha kwamba nilikuwana jeraha kubwa.
Hata mama aliyekuwa akiendelea kulia, alinyamaza nakubaki amepigwa na butwaa, harakaharaka nikainama kwa lengo al kutaka kuiokota ile bastola lakini kwa sababu nilikuwa nimelewa, nilishindwa kuiokota, badala yake nikapepesuka na kutaka kuanguka.
Nilirudia tena kujaribu kuiokota, kweli nikafanikiwa kuiokota na kuirudisha pale kiunoni, bado wote wakawa wanautazama mguu wangu.
“Unatembea na bunduki Kenny? Umepatwa na nini mwanangu? Mbona umebadilika ndani ya muda mfupi na kuwa mtu wa ajabuajabu?” alisema mama, akaanza tena kuangua kilio, nikaona hapo ndani siyo sehemu ya kukaa tena kwani ilionesha ni kama hali niliyokuwa nayo ilikuwa ikimuongezea mama huzuni.
“Mjomba mbona unatudhalilisha?” mambo gani tena haya unayafanya? Kwa nini usisubiri tukamzike baba ndiyo uendelee na mambo yako?” aliniambia mzee mmoja tuliyezoea kumuita mjomba, kauli ambayo iliugusa moyo wangu, nikichanganya na hali niliyomuacha nayo mama chumbani, nilijikuta huzuni kali ikinizonga, nikaanza kulia kwa sauti ya juu. Wasichokijua watu wengi ni kwamba kama umelewa halafu ukaanza kulia, unaweza kulia kwa uchungu mpaka watu wote wakakushangaa, ndicho kilichotokea kwangu.
Nikiwa naendelea kulia kwa nguvu na kuwafanya vijana wa pale mtaani pamoja na wazee wa mtaani wapate kazi ya kunituliza, nilishtuka baada ya kuona gari la polisi likija pale nyumbani, pombe zote ni kama ziliyeyuka kichwani, nilipogeuka na kutazama pale Bonta alipokuwepo, sikumuona, moyo ukawa unadunda kwa nguvu kuliko kawaida, ni nikiwa ni kama siamini kilichokuwa kinatokea.
Je, nini kitafuatia