Riwaya: Saa za Giza Totoro

Kanungila Karim

JF-Expert Member
Apr 29, 2016
20,744
25,446
THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO) SEHEMU YA 01
Mtunzi: HASHIMU AZIZI

“Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!”
“Nanii?”
“Fungua!”
“Jitambulishe kwanza, wewe nani?”
“Nimesema fungua! Fungua kwa hiyari yako!”
“Huyo ni nani?”
“Shiii! Rudi ndani kalale!”
“What is going on? Please let me know!” (Nini kinaendelea? Tafadhali naomba nieleweshe).
“Ngo! Ngo! Ngo!”

Kufumba na kufumbua, kishindo kikubwa kilisikika, mlango ukaja kunibamiza kwa nguvu na kunirusha mpaka ukutani, nikajibamiza na kudondoka chini kama mzigo. Wanaume watatu waliokuwa wamevalia makoti meusi, walinifuata na kunikaba pale chini huku wakinimulika kwa tochi zenye mwanga mkali usoni.

“Tulia, vinginevyo tunakumwaga ubongo sasa hivi,” alisema mmoja kati yao, nikashtuka kusikia akikoki bunduki yake na kuninyooshea. Sikuwahi kuona bunduki halisi katika maisha yangu hata mara moja, nilizoea tu kuziona kwenye TV lakini sasa, mtutu ulikuwa ukinitazama.

“She is innocent! Please leave her alone!” (Hana makosa! Tafadhali muacheni) nilisema kwa sauti ya kutetemeka, nikashtukia mmoja kati yao akinipiga kwa nguvu kichwani na kitako cha bunduki kisha akanisindikizia kwa kunipiga na buti gumu alilokuwa amevaa, nikasikia kizunguzungu kikali kisha giza nene likatanda kwenye uso wangu, sikuweza tena kugundua chochote kilichoendelea.

Nilipokuja kuzinduka, tayari kulikuwa kumepambazuka. Nikakurupuka pale chini nilipokuwa nimelala na kusimama, nikasikia kichwa kikiwa kinanigonga kuliko kawaida. Kilichonishtua ni kwamba pale chini nilipokuwa nimelala, palikuwa na damu nyingi ambazo sasa zilikuwa zimekauka.

Nikajishika sehemu mbalimbali za mwili wangu, nikagundua kwamba mdomo wangu ulikuwa umevimba sana, harakaharaka nilisogea kwenye kioo kidogo kilichokuwa ukutani na kujitazama, nikashtuka kwa jinsi nilivyokuwa natisha.
Jicho moja lilikuwa limevimba sana na kuweka kama alama za weusi kwa chini yake, mdomo nao ulikuwa hautamaniki. Kwa jinsi ilivyoonesha, ni kwamba wale wanaume walionivamia usiku uliopita, waliendelea kunipiga tena hata baada ya kuwa nimepoteza fahamu.

“Lakini kwa nini? Why? Nimefanya kosa gani kwa Mungu wangu kustahili adhabu kali kiasi hiki?” nilijisemea huku nikianza kumwaga machozi. Harakaharaka nikaenda mpaka chumbani, macho yangu yakatua juu ya kitanda cha chuma au banco kama wenyewe tulivyokuwa tumezoea kukiita, Saima hakuwepo! Nikageuka kutazama huku na kule, nikagundua kwamba hata begi lake pia halikuwepo, uchungu usioelezeka ukanikaba kooni kiasi cha kunifanya nishindwe hata kumeza mate.

Nilitoka nje huku nikipepesuka maana maumivu ya kicha yalikuwa makali sana, nikatazama huku na kule, hakukuwa na dalili yoyote ya kuwepo kwa Saima, nikarudi ndani huku nikiendelea kulia kwa uchungu usioelezeka. Niliwasha moto kwenye jiko la kuni, nikabandika maji na kuchochea mpaka yalipochemka, nikaanza kujikanda maeneo yote yaliyokuwa na majeraha. Nilikuwa nasikia maumivu makali lakini ilikuwa ni lazima nifanye hivyo.

Nilisukutua mdomo kwa maji yaliyochanganywa na chumvi, maumivu niliyokuwa nayasikia yalikuwa hayaelezeki. Nilijisafisha puani ambako damu ilikuwa imegandia, nikaanza pia kujikanda kwenye jicho. Ama kwa hakika nilikuwa nikisikia maumivu makali sana lakini ilikuwa ni lazima nifanye hivyo ili angalau nipate ahueni. Tangu nifahamiane na Saima, kila kitu changu kilikuwa kimebadilika kabisa, nilishapoteza kila kitu na sasa hata usalama wangu wenyewe ulikuwa ni mtihani mgumu.

Nasema mtihani kwa sababu kama watu wameweza kujua mahali tulipokimbilia na kujificha, tukiishi maisha kama ya wanakijiji kabisa, lakini watu wameingia mpaka ndani, wamenipiga na kunijeruhi vibaya lakini kama hiyo haitoshi wameondoka na Saima, hiyo ilikuwa ni ishara ya hatari sana kwenye maisha yangu.

Sasa kama hata sehemu ya kujificha haipo tena, nini ityakuwa hatma yangu? Nilijiuliza maswali mengi sana wakati nikiendelea kujikanda. Baada ya kumaliza kazi hiyo, nilienda kuanza kurekebisha mlango uliokuwa umevunjwa usiku uliopita na watu wale walioondoka na Saima.

Niliifanya kazi hiyo huku nikiendelea kujiuliza maswali mengi sana ndani ya kichwa changu. Nilipomaliza, tumbo lilikuwa likitetemeka kwa sababu ya njaa, ikabidi nifanye maarifa ili kutuliza njaa yangu. Kwa bahati nzuri, unga tulionunua mjini na Saima siku tulipoamua kufunga safari kwenda kujificha, bado ulikuwepo. Nikapika ugali harakaharaka na kwa sababu kulikuwa na mboga kidogo tulizobakisha usiku uliopita, sikupata tabu.

Baada ya kumaliza kula, nilitoka na kujaa nje, nikawa naendelea kutafakari nini cha kufanya kwa sababu ndani ya muda mfupi tu nilikuwa nimeingia kwenye matatizo makubwa sana ambayo hata sikuwa najua nawezaje kutoka.
Sikuwa na kazi tena, kazi pekee ambayo ndiyo iliyokuwa inanipa jeuri ya kuishi jijini Dar es Salaam kwa uhuru, ilikuwa imeshapotea katika mazingira ya kushangaza sana.

Sikuwahi kuwa na wasiwasi kuhusu utendaji kazi wangu na japokuwa wakati akinipa barua ya kunisimamisha kazi, meneja wetu alisisitiza kwamba wamefikia hatua hiyo kutokana na sababu za kiutendaji, moyoni nilikuwa najua wazi kwamba hiyo siyo sababu bali kuna jambo jingine kubwa ambalo mimi na yeye tulikuwa tunalijua.

Nilikumbuka jinsi nilivyojikuta nikiwa nimezungukwa na watu wanaonitakia mambo mabaya, watu wanaotamani kusikia au kuona nimedondoka na kupoteza maisha papo hapo! Nilishangaa kwa nini watu ambao kipindi cha nyuma ndiyo waliokuwa watu wangu wa karibu, wamenigeuka kiasi hicho?

Uchungu uliponizidia, niliinuka na kuzunguka nyuma ya nyumba yetu, mahali kulipokuwa na makaburi mawili, moja la marehemu baba na lingine la marehemu mama. Nilipiga magoti na kuyainamia, machozi yakawa yananitoka kwa wingi huku uchungu mkali ukizidi kunitesa moyoni mwangu.

“Naomba mnisamehe wazazi wangu! Yawezekana napitia haya kwa sababu sikuyatilia maanani mafundisho yenu, nateseka mtoto wenu, sina mahali pa kuegamia, imefika mahali sioni tena sababu ya kuendelea kuishi,” nilisema huku machozi yakiendelea kunitoka kwa wingi sana.

Waliosema kulia ni dawa hawakukosea, baada ya kulia kwa muda mrefu angalau nilianza kujihisi kama kuna mzigo fulani mkubwa umepungua ingawa macho nayo sasa yalikuwa yamevimba na kuwa mekundu sana. Niliinuka na kuanza kutembea taratibu kurudi ndani huku moyoni nikijiambia kwamba sikuzaliwa kufeli.

Haiwezekani nisome kwa taabu, baadaye Mungu anisaidie nipate kazi nzuri, niwe na familia nzuri na kupata kila ninachokitaka lakini baadaye kila kitu kigeuke na kunifanya nirudi tena kwenye mateso! Niliona ni kitu kisichowezekana na kutoka ndani kabisa ya moyo wangu, niliamua kupambana kiume.

Kwanza nilipata ujasiri wa kukabiliana na tatizo kubwa la Saima, ambaye mpaka muda huo nilikuwa sijui huko aliko kama yuko hai au la! Lakini pia ilikuwa ni lazima nipambane kurejesha kila kilichokuwa changu kisha kikapotea. Ilikuwa ni kazi ya hatari lakini hakukuwa na jinsi, sikuwa tayari kurudi kwenye mateso yale niliyokulia tangu nikiwa mdogo. Nilikuwa naijua hatari ambayo naenda kukabiliana nayo lakini sikuwa na namna, ilikuwa ni lazima nipambane.

Kwa jinsi nilivyokuwa nimeamua kuishi, sikuwa mtu wa matatizo kabisa na niliamua kuwa hivyo kutokana na historia yangu kutokuwa nzuri kwenye suala zima la maisha yangu binafsi lakini hiki kilichokuwa kinaendelea kwa sasa, kilinikumbusha maisha yangu ya nyuma, nikajikuta nikitamani kurudi kwenye maisha yangu ya zamani, ambayo huwa ni chukizo kubwa kwa wanadamu mpaka kwa Mungu.

“Hata Mungu wangu utakuwa shahidi wangu kwa hili, sina namna! Itabidi tu iwe hivyo,” niliwaza huku machozi yakinitoka tena. Nilisimama na kutembea kikakamavu mpaka nyuma ya nyumba yetu ambayo sasa ilikuwa imechakaa sana.
Nikasogea mpaka pembeni ya mti wa mjohoro, nikaanza kufukua kwa kutumia panga nililokuwa nimelishika. Baada ya kufukua kwa muda, hatimaye nilikutana na kitu nilichokuwa nakitafuta. Nilikitoa kisanduku kidogo cha plastiki, nikageuka na kutazama huku na kule, nilipohakikisha hakuna anayeniona, harakaharaka nilikibeba kisanduku hicho mpaka ndani.
Nikakiweka mezani, nikakifutafuta udongo kwa sababu kilikuwa kimekaa kwa muda mrefu ardhini na baada ya kuridhika na hali yake, hatimaye nilikifungua.

Bado nilikuwa nazikumbuka namba za siri nilizotumia kukifunga, macho yangu yakatua juu ya kitu kilichosababisha nitabasamu! Siyo tabasamu la furaha, la hasha! Tabasamu la kifo, tabasamu ambalo huwa linaonekana usiku wa giza totoro pekee.

Je, nini kitafuatia?

2309838_IMG_4061.jpg

Hard copy ni Tsh 10000 kwa order, softcopy ni Tsh 5000/= papo kwa hapo!
0719401968 unatumiwa PDF kwa WhatsApp au email mwanzo hadi mwisho in PDF Format unasoma hata kwenye simu!
Poleni kwa inconviniences




Sent using Jamii Forums mobile app
 
SEHEMU YA 02

ILIPOISHIA:
Bado nilikuwa nazikumbuka namba za siri nilizotumia kukifunga, macho yangu yakatua juu ya kitu kilichosababisha nitabasamu! Siyo tabasamu la furaha, la hasha! Tabasamu la kifo, tabasamu ambalo huwa linaonekana usiku wa giza totoro pekee.

SASA ENDELEA...

Unaweza kujiuliza nilikuwa nimeona nini kilichosababisha nitoe tabasamu la aina hiyo? Kihulka mimi ni mpole sana na pengine upole wangu wa nje ndiyo unaosababisha wakati mwingine watu kunionea waziwazi, wakiwa hawajui ndani ya moyo wangu kumejificha kitu.

Ilikuwa ni bunduki ninayoipenda sana, AK47 ambayo ilikuwa imekatwa kitako na mtutu na kuifanya iwe na uwezo wa kubebeka vizuri mikononi. Jinsi nilivyoipata silaha hii hatari, ambayo kisheria haitakiwi kabisa kumilikiwa na raia, isipokuwa wanajeshi tu, ni stori ndefu sana na yenye kusisimua kwelikweli.

Wakati mwingine binadamu wanakuwa wepesi wa kuwalaumu wenzao kwa matokeo ya mwisho, lakini ni wachache wanaokuwa wanaujua ukweli wa nini kinachosababisha mtu fulani akafanya tukio fulani. Sikuwahi kudhani hata mara moja kwamba itafika siku nitakuwa nikiutegemea mtutu wa bunduki kufanya kile ninachokitaka.

Kwa kipindi kirefu ndoto zangu zilikuwa ni kusoma na kuja kuwa daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na watoto, na nilisukumwa kuupenda udaktari kutokana na jinsi nilivyokuwa namuona mama yangu akiteseka kwa kipindi kirefu kitandani, akiwa hana uwezo wa kufanya kitu chochote kutokana na maradhi yaliyokuwa yanamsumbua.
Hata hivyo, ndoto zote hizo ziliyeyuka kutokana na matatizo niliyopitia na japokuwa baadaye niliamua kuachana na mambo hayo, siku hiyo nilijikuta nimetamani tena kufanya jambo kwa ajili ya kujitetea.

Hakuna kitu ambacho nilikuwa nakichukia kwenye maisha yangu kama kuonewa, shida na matatizo niliyopitia maishani mwangu vilinifanya niwe na roho ya aina yake, ambayo wakati mwingine nikikasirika utaona ni bora ukutane na mnyama mkali wa porini kuliko mimi.

Niliendelea kuitazama ile bunduki huku tabasamu la kifo likiwa bado limetanda kwenye uso wangu, nikainua macho na kutazama juu angani huku ile bunduki nikiwa nimeishikilia vilevile, nikaitazama tena na kujaribu kuikoki, ikakubali na kutoa mlio fulani ambao kwa kipindi kirefu ulikuwa unaashiria jambo baya na kila nilipousikia ujue kuna jambo baya lilikuwa linaenda kutokea.

Unaweza kujiuliza, nini hasa kilichotokea kwenye maisha yangu kiasi cha kufanya ndoto zangu za udaktari ziyeyuke na kujikuta nikiishia kuwa mtumiaji mzuri wa bunduki za kivita wakati hata jeshini sijawahi kupitia?
Nikisema mtumiaji mzuri wa bunduki namaanisha hivyo, kwenye suala zima la kulenga shabaha na kufanya mashambulizi ya kushtukiza, wenyewe wanaita ‘ambush’ nilikuwa vizuri kwelikweli kiasi kwamba kipindi nilipoamua kujikita kwa asilimia mia moja kwenye kazi hiyo, licha ya umri wangu mdogo nilikuwa tegemeo kwelikweli.

Ilikuwa ikitokea ‘kazi’, basi lazima nitakuwa miongoni mwa watu wawili au watatu ambao ndiyo wanaoongoza msafara. Baada ya hapo, niligeuka huku na kule kutazama kama kuna mtu alikuwa ananitazama, nilipogundua kwamba niko peke yangu, harakaharaka nililirudisha lile sanduku palepale lilipokuwa na kulifunga vizuri, kwa kutumia ‘chepe’ nikafukia na kuparudishia kama palivyokuwa awali.

Kwa muda wote huo, zana yangu nilikiwa nimeivaa begani. Nilirudishia miche ya mipapai ambayo ilikuwa juu ya eneo hilo kama njia ya ‘kuwazuga’ askari wasijue chochote kilichokuwa kinaendelea kisha harakaharaka nikarudi mpaka ndani, nikachukua begi dogo lililokuwa darini na kutoka nje.

Begi hilo lilikuwa na vifaa maalum ambavyo kwa harakaharaka ungeweza kudhani labda ni vya ufundi wa umeme, lakini kimsingi vilikuwa ni vifaa kwa ajili ya kusafishia bunduki.
Harakaharaka nilianza kuifungua silaha hiyo na kwa sababu tayari nilikuwa na uzoefu wa namna ya kuifungua na kuifunga upya kwa muda mfupi, ndani ya dakika chache tu nilikuwa nimeshaifungua, nikaanza kuisafisha kwani haikuwa imetumika kwa muda mrefu kiasi.

Wakati nikiendelea na kazi hiyo, kwa mbali nilianza kusikia muungurumo kama wa gari au pikipiki kubwa ukija kwa kasi kubwa. Kengele ya hatari ikalia ndani ya kichwa changu, kwa kuwa nilikuwa nakaribia kumaliza, niliamua kuifunga hivyohivyo, harakaharaka nikairudishia na kuivaa begani.

Nikachukua koti langu la kazi, refu na jeusi kisha nikafunga mlango na kuzunguka nyuma ya nyumba, nikakimbia na kuyapita yale makaburi na kutokomea kwenye vichaka vilivyokuwa mita kadhaa kutoka pale nyumbani. Nikaenda kupanda juu ya mti mrefu wa mkaratusi, nikawa natazama kwa mbali kuangalia muungurumo niliokuwa nausikia ulikuwa unatokea wapi kwa sababu haikuwa kawaida kwa magari kuja huko tulikokuwa tunaishi. Nilichokuwa nimekihisi ndicho kilichokuwa kimetokea, niliona pikipiki mbili aina ya Honda, zile kubwa kama zinazotumika kwenye mashindano zikija kwa kasi kubwa huku wanaume wanne wenye miili mikubwa wakiwa wamepakizana wawili wawili.

Walikuja kwa kasi kubwa mpaka pale nyumbani kwetu, ile pikipiki ya kwanza ikasimama upande wa kulia na ile nyingine upande wa kushoto kisha wote wanne wakateremka huku wakiwa wamevaa kofia maalum za kuficha nyuso zao.
Japokuwa walikuwa wamejiziba nyuso zao, niliweza kuhisi moja kwa moja kwamba ni watu niliokuwa nawafahamu kwa jinsi miili yao ilivyokuwa na jinsi walivyokuwa wakitembea. Unajua kama mtu umewahi kufanya naye kazi kwa karibu, hata ikitokea akajaribu kujibadilisha, ni rahisi sana kumgundua, hivyo ndivyo ilivyotokea kwangu.

Nitakuja kueleza kwa kirefu baadaye ni kwa namna gani mimi na watu hawa tulifahamiana lakini chanzo cha yote, kilikuwa ni mtu mmoja tu. Mtu ambaye awali niliamini kwamba anaweza kunisaidia kuutua mzigo mzito niliokuwa nao kichwani lakini mwisho akaishia kunibadilisha na kuwa kiumbe mwingine tofauti kabisa. Basi nikiwa pale juu ya mti, niliwashuhudia watu wale wakigonga mlango kwa fujo kama walivyofanya jana yake, na walipoona kimya, walivunja mlango na kuingia ndani kibabe.

Nikiwa sielewi hili wala lile, nilimuona mmoja kati yao akirudi pale kwenye pikipiki, nikamuona akifungua kidumu kilichokuwa na kimiminika ndani yake ambacho kwa mbali sikuweza kugundua ni nini. Akarudi ndani kwa wenzake na kufumba na kufumbua, nilishtuka kuona moshi mwingi ukianza kutokea madirishani napembeni ya paa. Wale watu wakatoka haraka nje, wakadandia pikipiki zao na kuziwasha, wakasogea mita kadhaa na kugeuka tena nyuma, nadhani ili kuhakikisha kama walichokusudia kukifanya kinaenda kama walivyokuwa wamepanga.

Nilishindwa kujizuia pale juu ya mti kutokwa machozi, baada ya kuona nyumba yetu kuukuu ikiteketea kwa moto huku wale washenzi wakigongesheana mikono kwa furaha na kuondoka kwa kasi kubwa na pikipiki zao.
Nilikuwa na uwezo wa kufanya kitu lakini niliona si busara kwa sababu naweza kujikuta naharibu zaidi mambo. Basi niliendelea kushuhudia nyumba yetu ikiteketea huku moshi mkubwa ukiwa umetanda angani, na kwa jinsi moto ulivyokuwa mkali, sikuweza kuokoa chochote.

Nilishuka na kukaa nje, mita kadhaa kutoka moto ulipokuwa unawaka kwa nguvu, nikawa nimejishika tama huku moyoni nikiwa na uchungu usiomithilika. Kwa ilivyoonesha, mtu aliyekuwa nyumaya matukio yote hayo, alikuwa akitamani kuniona napata shida kubwa pengine kuliko binadamu yeyote aliyewahi kuishi.

Kilichonifikirisha zaidi, kama mtu au watu waliokuwa wanayafanya haya walikuwa na lengo la kuniua, kwa nini jana yake walipokuja hapo nyumbani na kumteka Saima, hawakunipiga risasi na kuniua kabisa wakati walikuwa na uwezo wa kufanya hivyo? Kwa nini waliniacha niendelee kuishi?

Kwa jinsi nyumba zilivyokuwa zimejengwa hapo kijijini kwetu, na kwa sababu sikupiga kelele zozote za kuomba msaada, wanakijiji walikuja kuanza kukusanyika wakati moto ukiwa unaelekea kuzimika baada ya kuwa umeteketeza kila kitu. Kwa sababu ninazozijua mwenyewe, sikutaka kuzungumza na mtu yeyote, nikawahi kuondoka kabla hawajafika na kurudi kule vichakani.

Nilikuwa nahitaji muda wa kukaa peke yangu, kutafakari juu ya kilichotokea na kuchukua uamuzi wa nini cha kufanya. Kwa hiyo niliendelea kujichimbia kule vichakani, machozi yakinitoka na kuulowanisha uso wangu, nikawa natafakari nini cha kufanya. Nilikaa huko mpaka giza lilipoanza kuingia, nikavaa koti langu na kuhakikisha kama kitendea kazi changu kipo kwenye hali nzuri, nikaianza safari ya kuelekea mjini kwa sababu katika kutafakari, niliamua kwamba dawa ya tatizo siyo kulikimbia, ni kukabiliana nalo.

Kwa kuwa nilikuwa na picha ya watu waliokuja kuchoma ile nyumba yetu na nilikuwa nafahamu wapi kwa kuwapata, niliamua kuwafuata hukohuko ili kama mbwai iwe mbwai! Huu ni uamuzi wa kijasiri sana ambao unahitaji kweli uwe na moyo wa kishujaa kuuchukua kwa sababu watu niliokuwa nawafuata hawakuwa wa mchezomchezo lakini ilikuwa ni lazima niende. Niliamua kutembea kwa miguu kwa sababu kwa hali niliyokuwa nayo, kama ningeamua kupanda gari basi ingekuwa rahisi kwa watu kunishtukia kwamba nilikuwa na chuma begani na pengine kunikamatisha kwa polisi.

Baada ya kutembea kwa muda mrefu, hatimaye niliwasili jijini Dar es Salaam na moja kwa moja nilienda Manzese Tip Top, kwenye maskani ya mmoja kati ya wale vijana aitwaye Ismail au Suma Baunsa kama tulivyozoea kumuita.
Suma alikuwa akiendesha biashara ya kuuza vinywaji kwenye grosari moja pale Manzese Tip Top na sifa kubwa ya grosari yake ilikuwa ni kuuza kila aina ya pombe unayoitaka, kwa saa ishirini na nne. Kwa nje ungeweza kudhani kwamba ni nyumba ya mtu lakini kumbe ndani kulikuwa na ukumbi mkubwa ambako pombe zinauzwa usiku kucha na mchana kutwa.

Nilijua kwa vyovyote lazima Suma atakuwa kwenye ofisi yake akisherehekea na wenzake kwa sababu mara zote, hata kipindi ambacho tulikuwa tukishiriana nao kabla sijaamua kuachana na hayo mambo na kuendelea na maisha yangu, tulikuwa tukipiga ‘ishu’, tunakaa nao kwenye chimbo hilo kuwakwepa polisi na kiukweli hapo ndipo nilipojifunzia kunywa pombe, kula mirungi na kuvuta bangi.

Baada ya kufika eneo hilo, nilijua nikipitia mlango wa mbele, ni rahisi mabaunsa wake kunishtukia na pengine kunizuia kuingia, kwa hiyo kwa sababu nilikuwa nazijua njia za mkato za kuingilia ndani, nilitazama huku na kule na nilipojiridhisha kwamba hakuna aliyekuwa akinifuatilia, niliruka ukuta mrefu wa uani, nikatua ndani kimyakimya.

Nikaingia kwenye moja kati ya vyoo vya wanaume vilivyokuwa huko uani, nikaikoki vizuri bunduki yangu na kuikamata vizuri mkononi, nikatoka huku nikitembea kwa staili ya kuyumbayumba ili watu waamini nilikuwa miongoni mwa wateja na nilikuwa nimelewa. Muziki ulikuwa ukipigwa kwa sauti ya juu huku watu wengi wakiwa wanakunywa pombe, kutafuna mirungi, kujidunga madawa ya kulevya na kila aina ya ufuska, huku wengine wakifanya matendo yasiyostahili kufanywa hadharani na wanawake waliokuwa ndani ya grosari hiyo ya aina yake.

Nilichezesha macho kwa kasi kubwa na hatimaye nilifanikiwa kumuona Suma akiwa amekaa na mwanamke mmoja mnene aliyevalia nusu utupu, wakiwa wananyonyana ndimi. Nikateleza kama nyoka na kumfikia, kufumba na kufumbua tulikuwa tukitazamana naye, ana kwa ana huku bomba la AK47 nikiwa nimelikandamiza kwenye ubavu wake wa kushoto.

“Inuka na ufanye ninachokueleza, ukizingua unajua nini kitatokea,” nilisema kwa sauti ya chini lakini yenye mamlaka, yule mwanamke akakurupuka akiwa ni kama haamini kilichotokea, Suma naye akawa anatetemeka akiwa haelewi nimeingiaje pale.

Je, nini kitafuatia?

Sent using Jamii Forums mobile app
 
SEHEMU YA 03

“Inuka na ufanye ninachokueleza, ukizingua unajua nini kitatokea,” nilisema kwa sauti ya chini lakini yenye mamlaka, yule mwanamke akakurupuka akiwa ni kama haamini kilichotokea, Suma naye akawa anatetemeka akiwa haelewi nimeingiaje pale

SASA ENDELEA...

“Snox! Nakuomba mdogo wangu, please show me some mercy!” (Nionee huruma tafadhali) alisema Suma huku akiwa anatetemeka kuliko kawaida lakini sikumjali.
“Look at my face!” (Nitazame usoni), nilimwambia kwa Kiingereza kilichonyooka, akanitazama usoni halafu akawa ni kama ameshtuka kidogo.

“Mlikuja mkanipiga na kunijeruhi kiasi hiki, mkamteka Saima wangu na kama hiyo haitoshi, mmekuja kuchoma moto nyumba yetu. Bado unategemea kwamba nitakuonea huruma?” nilisema huku na mimi nikitetemeka kwa hasira.
”No! Nisikilize kwanza Snox,” alisema huku akiniita kwa jina langu la kazi. Watu wengi mitaani huwa wanaamini Snox ni jina langu halisi kwa sababu kila ninakoenda ndilo linalotumika lakini ukweli ni kwamba halikuwa jina langu halisi wala halikuwa na uhusiano wowote na jina langu halisi.

Kiuhalisia jina langu naitwa Keneth au Kenny lakini kama nilivyosema, waliokuwa wakinijua kwa jina hilo, walikuwa wachache mno, tena wale wanaonijua tangu nikiwa mdogo lakini wengine wote walikuwa wakiniita Snox.
“Najua mlitumwa, nataka kujua mhusika ni nani,” nilisema huku nikimkokota taratibu kuelekea kule uani. Yaani ungeshuhudia kilichokuwa kinaendelea, pengine ungepata picha halisi ya kile wanachosema ‘sungura kamkaba tembo’.
Suma alikuwa na mwili mkubwa uliojengeka kimazoezi lakini licha ya ukweli kwamba mimi nilikuwa na kamwili kadogo ka wastani, nilikuwa namkokota kama ng’ombe anayepelekwa machinjioni.

Kwa jinsi nilivyoingia eneo lile mpaka kumpata, bado alikuwa amepigwa na butwaa na hiyo pekee ilitosha kumchanganya kichwa na kibaya alikuwa anafahamu akili zangu nikishika ‘mashine’ zinakuwaje kwani tumewahi kufanya ‘kazi’ pamoja.
“Nataka jibu, sitaki blaah! Blaah!” nilisema huku nikizidi kulikandamiza bomba la AK47 kwenye ubavu wake, nikaikoki na kumfanya ashtuke.
“Nitakwambia Snox, mimi na wewe tumeshakuwa kama ndugu, huna haja ya kutumia nguvu kwangu,” alisema Suma kwa upole, nikatega masikio kwa makini kumsikiliza.
“Mzee anasema umemsaliti, anataka kuhakikisha unapata taabu mpaka mwenyewe ukome.”
“Mzee gani?”
“Aah Snox, kwani nikisema mzee wewe unaelewaje? Kuna mwingine tena zaidi ya bosi?”
“Nimemsaliti kivipi?”
“Kitendo cha kukataa kazi bila sababu za msingi, kimemkasirisha sana na anasema atahakikisha anakomaa na wewe mpaka aone mwisho wako,” alisema Suma lakini maneno yake hayakuniingia akilini. Nilijua kabisa kwamba ananidanganya kwa sababu alichokisema hakikuwa na uzito wowote wa kumfanya mtu aniwinde kwa kiasi kile.
“Saima yuko wapi?”
“Sijui chochote kuhusu Saima, sikuhusika kwenye hiyo kazi.”
“Unanificha si ndiyo?”
“Snox, sina sababu ya kukuficha chochote ndugu yangu, ila labda Seba anaweza kuwa anajua chochote maana siku hizi ndiyo mtu wa karibu zaidi na mzee.”
“Nitampata wapi?”
“Lazima muda huu atakuwa anakula bata Trace Element, kule Masaki,” alisema Suma akitegemea kwamba baada ya maelezo hayo nitamuachia.
Kwa walichonifanyia, japokuwa sikuwa na nia ya kukatisha maisha ya mtu yeyote, lakini ilikuwa ni lazima niwashikishe adabu wote waliohusika halafu mwisho nitamalizia na huyo aliyewatuma, ambaye nilikuwa na hasira kali sana juu yake kwa alichonifanyia maishani mwangu.

Nilimsukuma Suma kwa nguvu, akakimbia na kusimama mbele hatua kadhaa mbele, akanigeukia haraka huku akiwa ameinua mikono juu maana alikuwa anajua ni nini ninachotaka kukifanya. Mara nyingi kama mtu amekuteka na mkononi ana silaha ya moto, anapokwambia ukimbie, au anapokusukumia mbali na yeye, usidhani anafanya hivyo kwa sababu kweli amekusamehe, mara nyingi ni kwa sabahu anataka apate nafasi ya kukulenga vizuri ili akupige risasi. Suma alilijua hilo na ndiyo maana alifikia hata hatua ya kunipigia magoti akiomba nisimfanyie chochote.

Sikutaka kusikiliza la muadhini wala mchota maji, nilifanya kile nilichoona kinafaa, mlio mkali wa bunduki ulisikika, na hasa ukizingatia kwamba ilikuwa imekatwa mtutu, mlio wake ulikuwa mkubwa na wa kutisha sana.
Sikupoteza muda, nilimruka pale chini alipokuwa ameangukia akitokwa na damu nyingi, nikachumpa kwenye ukuta na muda mfupi baadaye, nilikuwa nikiteremka upande wa pili wa ukuta. Nilijua kwa vyovyote lazima mlio huo urtasikika kwa polisi waliokuwa doria ambao lazima watakuja eneo hilo kwa hiyo nilipita njia tofauti na niliyojia.

Wateja waliokuwa wakiendelea kuburudika mle ndani kwa vinywaji na muziki, walishtuka mno kusikia mlio wa bunduki, tena kutokea ndani kabisa ya ‘chimbo’ lao, kila mmoja akaanza kutimua mbio kuokoa maisha yake, wengine wakikanyagana hovyo na kusababisha madhara yawe makubwa.

Zile purukushani zilinisaidia hata mimi kuondoka eneo hilo kwa urahisi zaidi kwani nilijichanganya na kujifanya na mimi naogopa mlio wa risasi, nikawa nakimbia ‘mdogo-mdogo’. Ungeniona wala usingeweza kuhisi kwamba mimi ndiyo nilikuwa chanzo cha mshike-mshike uliokuwa unaendelea.
Nilitokezea Sinza ya Mugabe baada ya kuwa nimekatiza sana vichochoro ili nisionekane na mtu yeyote. Nilisimama kando ya barabara na muda mfupi baadaye, bodaboda moja ilikuja, nikaipungia mkono na hatimaye ikasimama.
‘Duh, baba umepiga pigo za kijambazi kabisa! Niuzie hilo koti,” alisema dereva wa bodaboda huku akichekacheka, nikanyamaza tu kwani ninapokuwa nimeivaa sura ya kazi huwa sipendi kucheka kwa sababu nimewahi kufundishwa kwamba unapocheka, unaondoa uzingativu wa akili.

“Nipeleke Trace Element.”
“Trace Element au Element?”
“Nimekwambia Trace Element,” nilisema kwa msisitizo, yule dereva wa bodaboda akanywea na nikamuona kama ananitazama kwa macho ya kuibia hivi. Basi aliwasha pikipiki na tukaondoka huku kila mtu akiwa kimya kabisa. Njia nzima nilikuwa namsisitiza kuongeza kasi nadhani mpaka mwenyewe baadaye alikoma.

Basi baada ya kama dakika thelathini, tayari tulikuwa tumewasili Masaki, nikateremka kwenye bodaboda na kumlipa fedha zake kisha harakaharaka nikajichanganya na kuelekea kwenye chimbo lingine liitwalo Trace Element.
Unajua watu wengi wanapajua Club Element lakini hawajui kwamba kuna chimbo lingine la kijanja liitwalo Trace Element, ambalo ndani yake kuna watu wabaya wa kila aina.

Mara nyingi, wau wabaya huwa hawachangamani na watu wazuri mara kwa mara, hata wanapokunywa pombe, huwa wanatenga kujificha kwenye machimbo yao ambayo wanakutana wenyewe kwa wenyewe, hapo ndipo wanapokuwa na amani ndani ya mioyo yao kwani wakijichanganya na watu wasiowajua, kila anayemuona anahisi ni polisi au mpelelezi.
Kwa sababu mara kwa mara nilikuwa nakuja eneo hilo na wenzangu wakati nikiwa mwanachama kamili, nilikuwa nazijua njia nyepesi za kutoroka, hasa polisi wanapokuja kwa lengo al kufanya ukaguzi, niliamua kutumia njia hizohizo kuingilia kwa sababu nilikuwana uhakika pale getini nisingeruhusiwa kuingia.

Basi nilizunguka upande wa pili na kukwea juu ya mti uliokuwa jirani na fensi, nikatambaa na kujivuta juu kwa juu mpaka nilipopanda juu kabisa ya fensi, nikatafuta sehemu nzuri ya kurukia, nikadondokea ndani kimyakimya bila mtu yeyote kujua.

Unaweza kushangaa huu umahiri wa kuparamia kuta za watu, taha ndefu kiasi gani bila kushtukiwa na mtu yeyote nimeupata wapi? Katika kipindi chote nilichokuwa nafanya kazi za uhalifu, mimi ndiyo nilikuwa nategemewa zaidi kwenye masuala ya kuruka fensi na kwenda kufungua mageti kwa ndani.

Mara nyingi ili majambazi waingie ndani kwa urahisi, lazima mmoja atangulie ndani kupitia ukuta na akiingia, anaenda kufungua geti kwa ndani ili wote waliopo nje waingie na huko ndiko nilikopata ujuzi huo.

“Kumbe wakati napanda kwenye ule mti, mmoja kati ya walinzi wa eneo hilo, alikuwa ameshaniona na akawa anasubiri aone mwisho wangu. Nikiwa pale chini, nilishtukia bomba la baridi likinigusa shingoni, likifuatiwa na sauti ya ‘tulia hivyohivyo kwa usalama wako)’, nikajua nimepatikana.

Je, nini kitafuatia?

Sent using Jamii Forums mobile app
 
SEHEMU YA 04




ILIPOISHIA:
“Kumbe wakati napanda kwenye ule mti, mmoja kati ya walinzi wa eneo hilo, alikuwa ameshaniona na akawa anasubiri aone mwisho wangu. Nikiwa pale chini, nilishtukia bomba la baridi likinigusa shingoni, likifuatiwa na sauti ya ‘tulia hivyohivyo kwa usalama wako)’, nikajua nimepatikana.

SASA ENDELEA…

Miongoni mwa vitu ambavyo Mungu amenijaalia, ni kutokuwa na hofu au woga ndani ya moyo wangu na pengine hiyo ndiyo sifa iliyokuwa inawafanya watu wote wanaonijua wawe wananiogopa au kuniheshimu, yaani kama huniheshimu basi uniogope kwani sikuwa na hata chembe ya woga.

Licha ya yule mtu kunigusisha bomba ambalo bila hata kuuliza nilijua lazima litakuwa ni mtutu wa bunduki, kwa jinsi ninavyowajua walinzi wengi wa Kibongo, huwa hawafanyi kazi kwa weledi.

Unaweza ukashangaa kwa nini nasema hivyo, lakini nikiri tu kwamba nimepitia mambo mengi sana hapa duniani, mengine makubwa na ya kutisha mno ambayo hata nikikusimulia, unaweza usiamini kwa haraka utakachokisikia.
Na miongoni mwa matukio mengi niliyoyafanya, yalikuwa yakiwahusu zaidi walinzi kwa hiyo nilikuwa najua jinsi walivyo wazembe.

Miongoni mwa sheria ambazo serikali inatakiwa kuzibadilisha mapema sana, ni hili suala la kampuni za ulinzi kukabidhiwa dhamana ya kulinda kwenye maeneo yenye mali za gharama, na kibaya zaidi kampuni hizi nyingi huwaajili wazee ambao hawawezi kupambana na majambazi wenye njaa, mwisho wanaishia kuuawa kama kuku.
Kwa hiyo nilichokifanya, nilijifanya kama nasalimu amri na kuinua mikono juu kisha kwa kasi ya kimbunga nikageuka na kumrukia yule mlinzi mwilini huku mikono yangu ikiwahi kuushika mtutu wa bunduki na kuugeuzia juu.

Kwa jinsi nilivyojirusha kwa nguvu, yule mlinzi hakutegemea kabisa kwa hiyo tukadondoka wote mpaka chini kama mizigo, tukawa tunagombea ile bunduki. Katika zile purukushani, nilifanikiwa kumzidi nguvu, nikampiga na kitako cha bunduki yake mwenyewe, akapoteza fahamu.

Harakaharaka nilimburuta mpaka pembeni, nikamfunga mikono na miguu na kumjaza matambara mdomoni kisha nikaanza kuutafuta mlango wa kuingilia ndani. Kwa nje kulikuwa na utulivu wa hali ya juu mno, usingeweza kuamini kwamba ndani kulikuwa na ulimwengu mwingine wa tofauti kabisa.

Basi nilifanikiwa kufika kwenye mlango wa nyuma na kwa kuwa ulikuwa umefungwa kwa ndani, nilitumia mbinu ya kufyatua kitasa kwa kutumia sindano niliyokuwa natembea nayo.

Kwa watu waliowahi kushiriki kwenye haya mambo ya uhalifu, nadhani watakuwa wananielewa vizuri ninapozungumzia masuala ya sindano na vitasa. Hakuna kitasa kinachoweza kufua dafu kwa mtumiaji mzuri wa sindano na mafuta ya breki.

Basi niliingia ndani kimyakimya na nikaiweka vizuri bunduki yangu, tayari kwa chochote. Basi nilienda moja kwa moja mpaka kwenye vyoo vya uani, nikaingia kwenye moja kati ya vyoo hivyo na kujibanza humo, wakati nikitafakari nini cha kufanya.

Mara nilisikia vishindo vya mtu akija kule chooni, nikaikamata vizuri bunduki yangu, tayari kwa chochote. Kwa bahati nzuri, aliingia kwenye choo cha pili, akajisaidia na muda mfupi baadaye, akawa anatoka.

Niliamua kumtumia kama chambo kwa sababu wasichokijua watu wengi, ni kwamba milango miwili mikubwa ya kutokea kwenye jengo lile, kuanzia mlango wa nyuma hadi mlango wa mbele, ilikuwa ikifunguliwa kwa kadi maalum za ‘ku-swap’.
Kwa jinsi jengo hilo lilivyokuwa limejengwa, kadi moja ilikuwa inatakiwa kutumika na mtu mmoja tu na bila kadi hiyo, uwezekano wa kuingia ndani ulikuwa mgumu na hiyo ndiyo sababu iliyonifanya nijibanze kule chooni kusubiri mzembe mmoja nipambane naye.

“Samahani,” nilisema huku nikimgusa begani yule mtu baada ya kuwa nimenyata na kumsogelea, nikamuwahi wakati anataka kuswap kadi ili mlango ufunguke. Alipogeuka tu, nilimtwisha kitako cha bunduki, damu zikaruka hewani kisha akadondoka mpaka chini kama mzigo huku kadi ikigeukia pembeni.

Unajua wakati mwingine ninapokumbuka mambo niliyoyafanya, najisikia vibaya sana kwa sababu watu wengi wasio na hatia walikuwa wakiteseka na wengine kuuawa kwenye mikono yangu. Wasichokijua watu wengi, kitako cha bunduki ni silaha mbaya sana, kiwe kimekatwa au kipo kizima. Mtu yeyote ukimpiga na kitako cha bunduki kichwani, hata kama awe nunda vipi, lazima apoteze fahamu, hasa kama unajua namna ya kutumia .

Basi harakaharaka nilimburuza na kumlaza kwenye maua, damu zikawa zinaendelea kumtoka lakini sikujali. Ilikuwa ni lazima nimfikie Seba ambaye naye kama alivyokuwa Suma, alikuwa pande la mtu la miraba minne, ambalo kazi yake ni kufanya michezo ya hatarihatari.

Niliswap ile kadi na kuingia ndani huku nikijitahidi sana kujichanganya ili asiwepo yeyote anayeweza kunihisi kwamba nimevamia nikiwa na nia ovu ndani ya klabu hiyo ambayo wateja wake ni watu maalum pekee.

Nilikaa kwenye moja kati ya kona zilicojificha, nikawa naangaza macho huku na kule kumtafuta Seba na baada ya dakika kadhaa, macho yangu yalimnasa akiwa anacheza kamari na wenzake. Miongoni mwa matatizo aliyokuwa nayo Seba, ambayo nahisi ndiyo yaliyomfanya akaingia kwenye kazi za kutumia silaha za moto, ni kupenda sana kamari.
Hata akipata fedha nyingi kiasi gani, Seba alikuwa na tabia ya kukesha hata siku mbili mfululizo akicheza kamari, yaani mpaka fedha zimuishie ndiyo akili zinamrudia laikini vinginevyo, hawezi kutulia.

Niliamua kumfuata palepale alipokuwa akiendelea kucheza mchezo maarufu wa kamari uitwao ‘poker’, kwa wale wazungukaji wa kwenye kumbi za starehe watakuwa wanaujua mchezo huu maarufu.

Nilifika kimyakimya na kusimama nyuma yake, sikutaka mtu yeyote ajue kinachoendelea kwa hiyo nikawa najipanga namna ya kumteka kimyakimya bila mtu kujua.

“Tulia hivyohivyo, hii ni bunduki, tena AK47, ukileta ujuaji nakumwaga kinyesi sasa hivi,” nilimnong’oneza Seba, kwa sababu na yeye ni mhuni aliyekubuhu, aliamua kunisaidia kazi yangu, akajifanya eti anataka kwenda toilet ili wale wenzake wasishtukie chochote.

Akanitazama usoni kama anayeuliza nini cha kufanya, nikampa ishara ya kusimama, kweli akasimama, nikampa ishara ya kuelekea kule nyuma, kweli akakubali kirahisi. Nimewahi pia kufanya kazi na Seba na miongoni mwa sifa zake kubwa, alikuwa siyo mwepesi wa kukubali kushindwa.

Ukichanganya na ukubwa wa mwili wake uliojengeka vyema kimazoezi, nilijua lazima anaweza kuleta ubishi lakini nikawa nimejiandaa kukabiliana naye. Alitembea harakaharaka mpaka alipoufikia mlango, akawa anataka kusap ili kufungua na kutoka nje lakini nikamzuia.

Nilijua akitoka nje atamuona yule mtu aliyekuwa amepoteza fahamu baada ya kupigwa na kitako cha bunduki lakini pia anaweza kumuona yule mlinzi ambaye naye nilikuwa nimemtwanga na kumfunga kamba.
“Nataka usimame hapohapo,” nilimwambia, akageuka taratibu na kunitazama huku akionesha kutokuwa na hata chemba ya masihara.

“Yaani wewe ndiyo wa kunishikia bomba mimi?”
“Unajifanya mjanja si ndiyo? Sitaki kujua kwa nini mmechoma nyumba yetu, nataka kujua mahalia liko Saima.”
“Kinachokupa ujeuri ni hiyo bunduki uliyoshika mkononi si ndiyo?”

“Ukijibu vizuri hakuna kitakachoharibika. Huu siyo muda wa mchezo, nitakufumua ubongo sasa hivi,” nilisema huku nikiwa sina hata chembe ya masihara na ili kumuonesha kwamba kweli licha ya mwili mkubwa aliokuwa nao ambao nilikuwa simfikii hata nusu yake, kweli nilikua nimevurugwa na nilikuwa tayari kufanya chochote, nilikoki bunduki na kuikamata vizuri huku nikimtazama machoni.

“Mdogo wangu, nakuomba tuliza mashetani yako. Nakujua wewe ukishavuta mibange yako hakuna anayeweza kukuzuia, nakuomba shusha ‘chuma’ chini,” alisema, nikaona kama ananichanganya kichwa.
“Saima yuko wapi?”

“Sasa mdogo wangu, wewe si unajua kabisa kwamba sisi ni vibaraka tu tunatumwa?”
“Narudia kwa mara ya tatu, Saima yuko wapi?” nilisema, safari hii nikiwa natetemeka kwa jazba. Kwa watu wote waliowahi kufanya na mimi dili chafu huwa wananielewa nikifikia hatua ya kutetemeka huwa nini kinafuatia. Tayari nilishaanza kusikia harufu ya damu kwenye pua zangu na kilichokuwa kinafuatia, hakikuwa kizuri hata kidogo.
“Kibaha! Tumempeleka Kibaha kwenye shamba la bosi, lakini yupo salama.”

“Shamba lipi?”
“La machinjioni,” alisema na kwa sababu alinisumbua, sikutaka kumuacha Seba hivihivi, nilitaka kutuma salamu kupitia yeye kwa hiyo nilichokifanya, nilivuta ‘trigger’ kwa ufundi, risasi moja ikapiga kwenye mguu wake wa kushoto upande wa chini, katikati ya vidole na kisigino.

Kelele za mlio wa risasi kutoka kwenye bunduki iliyokatwa mtutu na kelele alizozipiga Seba, ziliwashtua watu wengine waliokuwa wakiendelea kula raha, wakiwa hawajui chochote kinachoendelea, wakaanza kukimbia huku an kule huku Seba akiwa ameshaanguka chini, damu nyingi zikiwa zinamtoka pale nilipompiga risasi.

Nilifungua mlango na kutoka na ili kuzuia wasije wakatokana kunifuata, nilipiga risasi kwenye eneo la kuscan kadi za kufungulia mlango, nikawa na uhakika kwamba hakuna mtu anayeweza kuingia wala kutoka kwa kutumia mlango huo.
Harakaharaka niliruka ukuta na kudondokea upande wa nje, nikaanza kukimbia kutokomea gizani.

Kumbe kulikuwa na askari waliokuwa doria jirani na eneo hilo kwa hiyop ule mlio wa risasi, uliwafanya wafike eneo la tukio haraka sana.

Kwa bahati mbaya, wakati nikikimbia kuvuka barabara, taa za gari la polisi lililokuwa linakimbia kwa kasi kuelekea eneo la tukio, zilinimulika na kunifanya nichanganyikiwe kidogo, unajua ukimulikwa gizani na mwanga mkali lazima uchanganyikiwe.

Nilisikia gari hilo likifunga breki kali, hapo ndiyo na mimi nikapata akili za kukimbia kwa sababu kwanza mwili wangu ulikuwa na damu lakini kibaya zaidi, nilikuwa na bunduki hatari ambayo kama ningekamatwa na polisi, huenda maisha yangu yote yaliyosalia ningeyamalizia gerezani.

Nilikimbia na kujaribu kuruka ukuta lakini kabla sijaruka, nikasikia wale askari wakifungua milango na kuruka kwenye gari lao kwa kasi kubwa, mmoja kati yao akatoa amri ya kunitaka nisimame na kuinua mikono juu, jambo ambalo niliona kama haliwezekani.
Je, nini kitafuatia?

Sent using Jamii Forums mobile app
 
SEHEMU YA 05

ILIPOISHIA:
Nilikimbia na kujaribu kuruka ukuta lakini kabla sijaruka, nikasikia wale askari wakifungua milango na kuruka kwenye gari lao kwa kasi kubwa, mmoja kati yao akatoa amri ya kunitaka nisimame na kuinua mikono juu, jambo ambalo niliona kama haliwezekani.

SASA ENDELEA...
Yaani nisalimu amri kirahisi namna hiyo? Nijivalishe mwenyewe kitanzi kwenye shingo yangu? Lilikuwa ni jambo lisilowezekana kwa hiyo ilikuwa ni lazima nifanye kitu, tena haraka iwezekanavyo.
Pale nilipokuwa nimesimama, karibu na ukuta, kulikuwa na mtaro, ile inayochimbwa kandokando ya barabara. Kwa sababu maeneo mengi ya Masaki na Mikocheni yana kama asili ya majimaji, mitaro mingi iliyochimbwa ni mirefu na ina maji.

Kwa kasi ya kimbunga, nilijirusha kwenye mtaro, nikasikia risasi kadhaa zikipita mita chache kutoka pale nilipo, nikaangukia ndani ya mtaro. Kwa jinsi nilivyochukua uamuzi huo kwa kasi kubwa, nadhani hata polisi wenyewe hawakutegemea.

Katika medani za kivita, adui anapokuwa sehemu ambayo yupo chini kuliko wewe, kama kwenye shimo au handaki na ana silaha ya moto, huwa ni hatari sana kwa wewe uliyesimama juu ya ardhi kwa sababu yeye anaweza kukupiga risasi lakini wewe huwezi.

Wale polisi walilitambua hilo kwa sababu nadhani huwa wanafundishwa, kwa hiyo walichokifanya, ilikuwa ni kukimbia haraka kurudi nyuma ili kutafuta sehemu ya kujikinga na mashambulizi ya wazi ya risasi.
Nilikuwa na uwezo wa kufanya chochote lakini sikuona sababu ya msingi ya kuingia kwenye matatizo na polisi kwa muda huo, kwa hiyo nilichokifanya, nilifyatua risasi moja hewani ili kuwatisha wasije kichwakichwa kisha nikautumia muda huo kutambaa kwa kasi kama nyoka kwenye ule mtaro.

Nilifanikiwa kuibukia mita kadhaa mbele na kwa sababu wao waliamini lazima nitakuwa palepale niliporukia, waliendelea kufyatua risasi huku wakisogea, safari hii wakiwa makini zaidi. Nikatoka kwenye mtaro na kukimbia huku nikiwa nimeinama, nikatokezea kwenye ukuta wa jengo lingine ambalo linatumika kama ‘godauni’ la kuhifadhia mizigo, nikaruka ukuta mrefu na kuangukia kwa ndani.

Niliona ni afadhali kupambana na walinzi wa godauni hilo kuliko kupambana na polisi ambao kila mmoja alikuwa na silaha.Kama nilivyoeleza awali, uzembe uleule wa walinzi, ambao sijui kwa wakati huo walikuwa wapi, pengine nao walijificha baada ya kusikia milio ya risasi, uliniwezesha kukatiza eneo lote la godauni bila kuonwa, nikaenda kuruka ukuta wa upande wa pili na kutokea mtaa wa pili, nikawa nakimbia huku mwili wangu wote ukiwa umelowa kwa maji machafu ya ule mtaro.

Nilikimbia kwa tahadhari kubwa huku nikiendelea kusikia milio ya risasi kule nilikotoka, nadhani polisi bado walikuwa wakijiaminisha kwamba nipo palepale niliporukia. Baada ya dakika kadhaa, nilitokezea kwenye Barabara ya Cocacola, ile inayotokea Mwenge kwenda Mikocheni. Nilijua kabisa kwamba nikiwa nakimbia pembeni ya barabara ni rahisi kuonekana, kwa hiyo nikavuka na kuingia upande wa pili wenye viwanda na magodauni mengi, ambao kwa wakati huo ulikuwa kimya kabisa.

Nilikimbia kwa umbali mrefu huku nikimuomba Mungu wasishtukie nilikokimbilia, lengo langu likiwa ni kufanya kila kinachowezekana kufika Kibaha usiku huohuo. Baada ya kukimbia kwa umbali mrefu, niliona mwanga wa bodaboda ikija kwa kasi mbele yangu, nikajua hiyo ndiyo nafasi yangu ya kujiokoa. Nilijitokeza na kusimama katikati ya barabara na kuinua bunduki juu huku mkono mmoja nikimuamuru dereva wa bodaboda kusimama. Nilipoona anaongeza mwendo, niliikamata bunduki vizuri na kumnyooshea, nikiwa tayari kufanya lolote kumsimamisha kama atakaidi ninachokitaka.
Akiwa ni kama hakutegemea alichokuwa anakiona mbele yake, dereva alifunga breki za ghafla, akaruka kwenye bodaboda na kuiacha ianguke, akaanza kukimbia kurudi kule alikotoka huku akiwa ameinua mikono juu, nadhani aliogopa zaidi baada ya kugundua kwamba nilikuwa na bunduki.

Sikutaka kushughulika naye, harakaharaka niliifuata ile bodaboda ambayo bado ilikuwa inanguruma pale chini huku taa zikiwa zimewaka, nikaiinua na kuhakikisha kama ipo salama, nikapanda na kuiondoa kwa kasi kubwa huku bunduki yako nikiwa nimeivaa begani.

Niliendesha kwa kasi kubwa mno, kwenye matuta nikawa nainuka bila kupunguza mwendo na kuyafukia kama ‘nimesimama’, muda mfupi baadaye nikawa tayari nimeshafika Afrikana.
Nilikunja kona kushoto, nikawa narudi upande wa mjini kwa sababu awali nilikuwa kwenye ile Barabara ya Old Bagamoyo, ile inayopita kule kwenye Ofisi za Times FM.

Nilirudi mpaka njia panda ya... nikakata kona na kuingia upande wa kulia, nikawa nakimbia kwa kasi kubwa kwenye barabara ya kuelekea Mbezi, ambayo kipindi hocho bado ilikuwa haijawekwa lami kama ilivyo sasa hivi. Kwa wanaoijua barabara hii, inaenda kukutana na Morogoro Road eneo la Mbezi Mwisho.

Basi nilikamua kwelikweli, sikuwa na uhakika kama mafuta yaliyomo kwenye bodaboda hiyo yatatosha kunifikisha ninakoenda kwa sababu pale yule dereva alipoitupa na kukimbia, mafuta yalimwagikia barabarani.
Baada ya kama dakika ishirini hivi, tayari nilikuwa nimeshafika Mbezi, nikaingia kwenye barabara ya lami na kuendelea kukimbia kwa kasi kubwa, mpaka ikafika mahali nikawa nahisi bodaboda inaweza kulipuka. Sikuwa dereva mzuri wa bodaboda lakini nilikuwa na uelewa wa kutosha wa namna ya kuendesha na kwa sababu usiku huo hakukuwa na magari mengi barabarani, basi sikupata sana shida.

Baada ya kukimbia kwa muda mrefu, hatimaye niliwasili Kibaha Maili Moja, nikapita na mbele kidogo, nilikunja upande wa kulia kwenye viwanda, nikanyoosha na barabara na kuanza kupandisha kuelekea Machinjio ya Zamani, wenyeji wa Bagamoyo watakuwa wanakufahamu vizuri. Ni nje kabisa ya Mji wa Kibaha.

Muda ulikuwa umeyoyoma sana na kwa mbali nikaanza kuona kama ule mwanga wa alfajiri umeanza kulifukuzia mbali giza totoro la usiku. Niliendelea kusonga mbele, nikipita kwa kasi kwenye barabara yenye mchanga mwingi na kusababisha muda mwingine pikipiki iwe inaniyumbisha kwa nguvu.

Mpaka nafika Machinjioni, tayari kulikuwa kumeshaanza kupambazuka na nikajua fika kwamba sitaweza kuikamilisha kazi hiyo kwa siku hiyo, kwa sababu muda mzuri ulikuwa ni usiku wa giza totoro.
Kwa kuwa nilikuwa nalifahamu vizuri shamba nilikoelekezwa kwamba Saima ndiko alikopelekwa, nilitafuta sehemu ya kuificha pikipiki, nikaiingiza ndanindani kabisa kwenye mashamba ya mikorosho na kuipaki, nikashuka na kukaa chini kwa sababu upepo uliosababishwa na spidi kubwa niliyokuwa naendeshea pikipiki hiyo, ulisababisha kifua changu kiwe ni kama kinataka kupasuka.

Tayari mapambazuko yalishawadia kwa hiyo nilichokifanya, ilikuwa ni kuhakikisha hakuna mtu anayeweza kuiona pikipiki hiyo, nikaanza kutembea kwa miguu kuelekea kwenye shamba kubwa lenye zaidi ya ekari hamsini, ambalo ndiko yalikokuwa maficho niliyoelekezwa kwamba Saima atakuwa amefichwa akiteswa.

Mmiliki wa shamba hilo kubwa, alikuwa ni mfanyabiashara mkubwa, Mutesigwa au maarufu kama Bosi Mute, ambaye naweza kukiri kwamba licha ya awali kuwa msaada mkubwa kwangu wakati nafika mjini kwa mara ya kwanza, sasa alikuwa ndiyo adui yangu mkubwa na nilishajiapiza kwamba popote nitakapopata bahati ya kukutana naye kwenye kumi na nane zangu, lazima nimuue, tena kwa mikono yangu mwenyewe.
Kwa nje lilikuwa linaonekana kama ni shamba, likiwa limezungushiwa uzio mrefu wa matofali na nyaya lakini kwa ndani, ilikuwa ni kama kambi ya waasi.

Mipango yote michafu ilikuwa ikifanyikia ndani ya shamba hilo, mali nyingi za wizi, yakiwemo magari, yalikuwa yakifichwa ndani ya shamba hilo na kwa sababu Mutesigwa alikuwa anajua namna ya kula na wakubwa, hakuna mtu yeyote aliyekuwa anaweza kulisogelea shamba lake.

Miongoni mwa makosa makubwa aliyoyafanya, ilikuwa ni kuanza kuniandama, akiamini sina cha kumfanya. Nilishamtumikia kwa kipindi kirefu, kwa hiyo nilikuwa namjua kuliko mtu mwingine yeyote na siyo kumjua yeye tu, bali mpaka familia yake na watu wote aliokuwa akishirikiana nao. Kwa kuwa yeye alikuwa amenianza, nilijiapiza kummaliza kwa sababu wahenga wanasema akuanzaye mmalize.

Maisha yangu na kila nilichokuwa nakipitia, ilikuwa ni kwa sababu yake, yeye ndiye aliyenibadilisha kutoka kuwa kijana mzuri, mpole na mstaarabu mpaka kuja kuwa mnyama na sasa silaha aliyoitengeneza, ilikuwa inarudi kumuangamiza yeye mwenyewe.

Nilitafuta sehemu nzuri, upande wa nyuma kabisa wa shamba hilo kubwa, nikajificha na kuanza kupanga namna ya kwenda kutimiza azma yangu. Ilikuwa ni lazima nimuokoe Saima kwa gharama yoyote, hasa ukizingatia kwamba ndani ya tumbo lake, alikuwa na kiumbe, mwanangu mtarajiwa, ambaye angekuja kuyabadilisha kabisa maisha yangu na kunifanya na mimi nianze kuitwa baba.

Je, nini kitafuatia?
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom