Riwaya: Saa za Giza Totoro

Riwaya: Saa za Giza Totoro

Msaada wa vocha wasomaji.
Kama una vocha ya Halotel,VodaCom au TTCL nisaidieni niendeleze hadithi
 
SEHEMU YA 35

ILIPOISHIA:
Katika hali ambayo ilimshangaza kila mmoja aliyekuwa anashuhudia tukio hilo, Bonta alimkunja yule askari aliyekuwa amempiga na kitako cha bunduki kichwani, sijawahi kuona mtu anayeweza kuwa na ujasiri wa kumkwida mtu aliyeshika bunduki mkononi, nadhani ujasiri huo uliwatisha hata wale askari wenyewe, purukushani kubwa ikatokea.
SASA ENDELEA...
“Ana bunduki! Ana bunduki!” alisema askari mmoja kwa sauti ya juu baada ya kuiona bastola ya Bonta pale kiunoni alipokuwa ameichomeka. Hali hiyo ilisababisha askari wote wamvamie kwa lengo la kumpokonya ile bastola, wakawa wanamgombea kama mpira wa kona.
“Kumbe jambazi! Hebu sogeeni tumalize kazi,” alisema askari mmoja huku akiikoki bunduki yake na kumnyooshea Bonta ambaye sasa alikuwa ameanza kuzidiwa nguvu kwani walikuwa wakimpiga kwa kumchangia.
Kwa jinsi hali ilivyokuwa, nilijua kweli yule askari anaweza kumtwanga risasi Bonta kwa sababu hakuwa na hata chembe ya masihara, nikaona nisipofanya kitu, kweli anaweza kuuawa mbele ya macho yangu. Kosa kubwa ambalo walilifanya wale askari, lilikuwa ni kunidharau na kuelekeza nguvu zao zote kupambana na Bonta.
Kwa kasi ya umeme nilichomoa bastola, nikaikoki na kufyatua risasi iliyompiga bega yule askari aliyekuwa amemnyooshea Bonta bunduki, akadondoka chini kama bunduki, nikawa nimechokoza moto.
Askari wote waliruka na kubingirika chini kama wanasarakasi kwa lengo la kuangalia risasi iliyompiga mwenzao imetokea wapi, na mimi nikajirusha na kubingirikia kwenye ukingo wa barabara, kama ningechelewa kidogo sijui nini kingetokea, pengine huo ndiyo ungekuwa mwisho wangu kwani mvua ya risasi ilimwagika kwa nguvu.
Watu waliokuwa jirani na eneo hilo wakawa wanakimbia kuokoa maisha yao, huku madereva wengine wakishuka kwenye magari yao na kukimbia wakiyaacha barabarani.
Sijui Bonta aliondokaje pale chini, nilishtukia na yeye akiwa upande ule wa ukingo wa barabara nilikokuwa mimi, huku ile bastola yake ikiwa mkononi, akanipa ishara kisha akawa anahesabu vidole. Nilimuelewa vizuri, alimaanisha kwamba tunatakiwa kujibu mapigo kwa pamoja, akahesabu, moja, mbili, alipofika tatu tuliinuka kwa pamoja na kushambulia kwa nguvu.
Lilikuwa ni pigo takatifu, sijui wale askari walikuwa wamezubaa na nini kwa sababu wote walikuwa wamesimama huku wakiwa wameelekeza bunduki zao kule tulikokuwa, huku yule mwingine akiwa chini, damu nyingi zikimtoka, kwa hiyo tulipoinuka na kushambulia, hawakuwa na sehemu ya kujificha, wakadondoka chini kama mizigo huku damu nyingi zikivuja.
Bonta alisimama, akanipa na mimi ishara nisimame, akamsogelea yule aliyekuwa wa kwanza kudondoka, akamuongeza risasi ya kichwa, damu zikaruka kwa wingi mithili ya bomba lililopasuka. Harakaharaka akaiinua pikipiki ambayo katika ile purukushani ilianguka, akajaribu kuiwasha, ikawaka.
Akaigeuza kwa kasi na kunisogelea, nikapanda kisha akaiondoa kwa kasi kubwa, tukipita upande ambao hatustahili kupita tukawa tunarudi upande wa Mwenge, watu wengi wakawa wanakimbilia pale eneo la tukio.
Sijui ni kwa sababu watu hawajazoea kusikia milio ya risasi au sijui ni ushamba, lakini watu wengi wana kawaida ya kupenda kwenda kushuhudia kilichotokea, yaani mtu akisikia risasi zinanguruma, anajificha ila zikitulia tu, sekunde chache anatoka na kukimbilia eneo la tukio kwenda kushuhudia.
Hili ni kosa kubwa sana na kuna siku limewahi kusababisha madhara makubwa sana, watu wasio na hatia wakapigwa risasi kwa sababu ya uzembe wao, nitakuja kulielezea tukio hilo.
Basi watu wengi walizidi kukimbilia eneo la tukio na sisi tukawa tunazidi kutokomea na pikipiki yetu, nikiwa nimejishikilia vizuri nisije kuanguka, mara kwa mara nikigeuka nyuma kuangalia kama kuna mtu alikuwa akitufuatilia kama Bonta alivyoniambia.
Tulienda mpaka pale barabara ya vumbi ya kuingilia kwenye kituo cha daladala cha Mawasiliano inapoanzia, Bonta akakata kona kwa kasi utafikiri tupo kwenye mashindano, almanusra tulivae daladala la Mbezi lililokuwa linapakia abiria, kwa bahati nzuri Bonta alikuwa na uzoefu sana na pikipiki, akaweza kuimudu vizuri.
“Washenzi sana wale, wanajua kila mtu ni wa kumchezea,” alisema Bonta huku akizidi kuvuta pikipiki kwa kasi kubwa, sikumjibu kitu kwa sababu bado na mimi nilikuwa ni kama nimepigwa na bumbuwazi kwa kile kilichofanyika pale Ubungo.
Dakika chache baadaye, tayari tulikuwa tumeshafika Sinza, tukavuka Barabara ya Shekilango na kuingia barabara ya vumbi ya mtaani, dakika chache baadaye tulikuwa tumeshafika pale nyumbani kwangu. Akaizima pikipiki na kunipa ishara kwamba niteremke.
“Ulibeba funguo?”
“Huwa natembea nayo,” nilisema huku nikilegeza mkanda wa suruali yangu, nikatoa kamba ya bukta ambayo ndiyo huwa naifunga funguo ya geti la nje na ya mlango mkubwa.
“Una akili sana,” alisema Bonta huku akitazama huku na kule kuhakikisha usalama, harakaharaka nikafungua geti, tukasaidiana kuiingiza pikipiki mpaka ndani.
“Umefanya kazi nzuri sana,” alisema huku akinipa mkono baada ya kuwa tumeingia ndani, na mimi nikampa mkono.
“Kama usingemuwahi yule mshenzi kweli angenipiga risasi,” alisema huku akienda kufungua friji, hakukuwa na chochote zaidi ya maji, ambayo nayo yalikuwa ya moto kwa sababu nilizima friji. Sikuamini kama tumerudi kwangu.
“Inabidi tuzugezuge kwanza hapa mpaka mambo yatulie, tutatoka baadaye,” alisema huku akivua fulana yake ambayo ilikuwa na damu.
“Yule mshenzi ameniumiza sana, hebu niangalie sijapasuka,” alisema huku akiinamisha kichwa chake pale alipopigwa na kitako cha bunduki. Alikuwa amepasuka na hata damu zilizokuwa zimeilowanisha fulana yake, zilikuwa zikichuruzika kutoka kwenye jeraha hilo, ingawa nyingine zilimrukia pale eneo la tukio.
“Mbona bado unatetemeka?” aliniuliza, nikakosa cha kumjibu kwa sababu ni kweli bado nilikuwa natetemeka, lile tukio la pale Ubungo lilikuwa limeniogopesha sana kwa sababu lilitokea ghafla sana, halafu nilikuwa najua kwamba linaweza kutusababishia matatizo makubwa zaidi kwa sababu askari wasingekubali kirahisi kuona wenzao wamepigwa risasi.
“Piga kidogo uondoe hofu,” alisema Bonta huku akifungua kichupa kidogo cha pombe kali ambacho kumbe alikuwa amekibeba. Nilifanya hivyo na kweli baada ya kupiga kidogo, nilianza kujisikia ile hali ya mikono kutetemeka ikipungua.
“Mwagia kidogo hapo kwenye kidonda,” alisema Bonta, kweli nikammwagia kidogo ile pombe kali pale kichwani, nikamuona akiuma meno kwa nguvu, nadhani ni kwa sababu ya maumivu.
Ilibidi mimi nikaoge kwanza, nikabadilisha na nguo, na yeye akaenda kuoga na kufua ile fulana yake iliyokuwa imechafuka kwa damu, hakuwa na nguo nyingine ya kuvaa kwa sababu zangu zilikuwa ndogo na yeye alikuwa pande la mtu kwelikweli, alipomaliza alitoka nayo na kuchukua pasi, akawa anaikausha.
Kwenye kama saa sita hivi za usiku, tulijiandaa na kutoka, safari hii hatukuondoka na pikipiki tena, tukaenda mpaka barabarani na kusimamisha teksi, tukaingia na safari ikaendelea. Tulikubaliana na dereva kwamba atupeleke mpaka nyumbani Msanga, japo alitutajia bei kubwa lakini Bonta alisema kwamba ni bora tumlipe tu.
Mimi nilikaa siti ya mbele, Bonta akawa amejilaza kwenye siti ya nyuma, nadhani lile jeraha pale kichwani lilikuwa limemmaliza nguvu kwa sababu alipigwa sehemu mbaya na kama angekuwa legelege, angeweza hata kupoteza fahamu. Safari iliendelea na baadaye, akili kwamba nyumbani kuna msiba zikanirudia, huwezi kuamini zile purukushani zilisababisha nisipate kabisa muda wa kufikiria kuhusu msiba wababa.
Moyo wangu ulikuwa na huzuni kubwa sana lakini kwa upande mwingine, nilimshukuru Mungu kwani kazi yake haina makosa, baba alikuwa ameteseka kwa kipindi kirefu sana.
Mpaka tunawasili Msanga, ilikuwa ni tayari saa tisa za usiku, kwa sababu za kiusalama Bonta akasema yule dereva asitupeleke mpaka nyumbani, akatushusha stendi kisha tukasubiri mpaka alipogeuza gari lake na kuondoka ndiyo na sisi tukaanza kuondoka kuelekea nyumbani.
“Hawa madereva teksi siyo watu wa kuwaamini, wanaweza kukuchuuza kirahisi sana,” alisema Bonta wakati tukikatiza mitaa kuelekea nyumbani. Kadiri tulivyokuwa tunakaribia nyumbani ndivyo huzuni ilivyokuwa inanizidi, sikutaka kabisa kuamini kama sitakuja kumuona tena baba maishani mwangu.
Tulipofika, tulikuta watu wengi wakiwa wamekaa nje, wengine wakiota moto na wengine wakipiga soga za hapa na pale, kama kawaida ya msibani watu huwa wanakesha mpaka marehemu akazikwe.
Walipotuona tunakuja, kila mtu alishtuka hasa baada ya kugundua kwamba ni mimi, na nadhani maswali ambayo kila mtu alikuwa akijiuliza kichwani mwake, ni ‘wametoka wapi usiku wote huu?’.
Harakaharaka mama alienda kupewa taarifa, akaanza kuangua kilio kwa sauti ya juu huku akilitaja jina langu, wanawake wengine nao wakawa wanalia kwa huzuni, vilio vikawa vimeamka upya.
“Unatakiwa kujikaza mdogo wangu,” aliniambia Bonta, wakati tukipelekwa kwenye chumba kilichokuwa na mwili wa marehemu.
Je, nini kitafuatia?
 
SEHEMU YA 36

Tuliingia na kukuta mwili wa baba ukiwa umelala na kutulia kitandani, akiwa tayari ameshavalishwa sanda. Ungeweza kudhani baba amelala tu lakini kumbe ndiyo alikuwa ametutoka.
Baba mkubwa ndiye aliyekuja kutufungulia sanda upande wa kichwani, nikamtazama baba, kiukweli nilijitahidi sana kujikaza kiume kama alivyosema Bonta lakini haikuwezekana.
Nilipiga magoti na kuukumbatia mwili wa baba huku uso wangu ukiwa umejawa na machozi, donge kubwa likawa limenikaba kooni kiasi cha kunifanya nishindwe hata kumeza mate, nikaanza kuangua kilio kwa huzuni kubwa huku nikimuita baba.
Kwa kipindi ambacho baba alikuwa mzima, kabla hajaanza kuumwa, alitulea vizuri sana sisi wanaye, alijitahidi kwa kadiri ya uwezo wake kuhakikisha tunapata malezi bora na elimu bora ingawa mambo yalianza kuharibika alipoanza kuugua na kuishia kulala kitandani.
Pengine hata leo hii angegundua ni kazi gani niliyokuwa naifanya baada ya kushindwa kuendelea na masomo kutokana na ukosefu wa karo, pengine angeumia sana ndani ya moyo wake kwa sababu kila sikuwa alikuwa akitusisitiza wanaye kwamba elimu ndiyo kitu pekee kinachoweza kutukomboa maishani.
Kwa zaidi ya dakika kumi na tano nzima nilikuwa nikiendelea kulia tu huku nikiwa nimemkumbatia baba, ikafika mahali ikabidi niondolewe kwa nguvu kwa sababu ningeweza hata kuzimia kutokana na kulia mfululizo kwa muda mrefu.
Nilipotolewa kule chumbani, nilipokelewa na mama ambaye alinikumbatia huku na yeye akianza upya kulia. Ilikuwa ni siku ya huzuni kubwa sana kwangu, mama akawa ananiambia kwamba lichaya mimi kujitahidi kutafuta fedha za matibabu ya baba, alikuwa amekataa kuendelea kukaa nasi na kuamua kurejea kwa Mungu wake. Ilifika mahali, mwili wangu ukawa umeishiwa nguvu kabisa kwa sababu ya kulia, macho yakiwa yamevimba na kuwa mekundu sana.
“Inabidi upate kitu kitakachokupunguzia uchungu ndani ya moyo wako,” alininong’oneza Bonta, akanishika begani na kunikumbatia, akawa ananipeleka nje ambapo ilibidi tujitenge na waombolezaji wengine na kukaa pembeni kidogo ya nyumba, chini ya mti wa mkorosho.
“Changamsha kichwa mdogo wangu, haya ni mambo ya kawaida kabisa, sisi wote hapa duniani ni wapita njia tu, cha msingi tumuombee apumzike mahali pema peponi,” alisema Bonta huku akitoa kichupa kidogo kilichokuwa na ile pombe kali anayopenda kunywa.
Nilikifungua na kupiga funda moja, nilipomeza nilihisi tumbo lote linawaka moto na muda mfupi baadaye, nikaanza kujisikia vizuri. Bonta akawa anaendelea kunisisitiza kuinywa ile pombe. Japokuwa kichupa kilikuwa kidogo lakini nilipofikisha nusu, tayari nilikuwa nimechangamka kwelikweli.
Kuna wakati nilikuwa nasahau kabisa pale ni wapi na nini kimetokea, tukawa tunaendelea na stori za hapa na pale na Bonta, mara Bonta aliingiza mkono mfukoni na kutoa msokoto, akatazama huku na kule kuhakikisha kwamba hakuna mtu yeyote aliyekuwa akitutazama.
Akauwasha na kuvuta kidogo kisha akanipa, na mimi nikavuta huku safari hii nikiwa nimeshaanza kuzoea, ile hali ya kukohoa ikawa imeisha kabisa, nilipovuta mara kadhaa, ndiyo kabisa nilizidi kujiona kama hakuna chochote kilichotokea.
Hata sijui nini kiliendelea, nilishtukia tu nimepitiwa na usingizi mzito, tulipozinduka tayari ilikuwa ni alfajiri. Unajua tatizo la hivi vilevi, kama pombe na madawa mengine ya kulevya, japokuwa watu wengi huwa wanaamini kwamba vinapoteza mawazo, ukweli ni kwamba huwa vinakusahaulisha kwa muda mfupi tu na vikiisha kichwani, matatizo yanarudi palepale.
Japokuwa usiku ule baada ya kupiga pombe kali na kusindikizia na msokoto nilijiona kama nipo dunia nyingine kabisa, kulipopambazuka tu hali ilikuwa imerudi palepale, moyo wangu ulikuwa ni kama una kidonda. Na jinsi pombe zisivyo na adabu, kama ukinywa usiku wa manane, ukiamka asubuhi japokuwa zinakuwa zimepungua sana kichwani lakini bado zinakuwepo.
Kwa hiyo japokuwa ilikuwa ni siku mpya bado kichwa changu kilikuwa na ‘mawenge’ na kwa mtu ambaye ananifahamu vizuri, angeweza kugundua kwamba sikuwa kwenye hali yangu ya kawaida.
“Hapa ni kwenye umati wa watu na kama unavyojua tena kazi zetu hatutakiwi kufanya jambo lolote linaloweza kuwafanya watu waanze kukutilia mashaka.”
“Mimi hapa ni kwetu, wala usiwe na wasiwasi.”
“Kuwa kwenu siyo sababu, polisi wapo kila sehemu, tunaweza kuja kukamatwa hata hapahapa,” alisema Bonta kwa msisitizo lakini aliyokuwa anayazungumza yalikuwa yakiingilia kwenye sikio moja na kutokea kwenye sikio la pili.
“Hebu nipe kwanza nizimue,” nilimwambia Bonta nikimaanisha anipe tena ile pombe kali, akanitazama kwa muda kisha akashusha pumzi ndefu, kumbe alikuwa na vichupa vingine kadhaa vya ile pombe ya Kizungu ambayo hata sijui inaitwaje, akanipa kimoja na kuendelea kunisisitiza kwamba natakiwa kuwa makini tusije kuibua matatizo yasiyokuwa na msingi.
Nilikipiga kile kimoja kwa kasi na licha ya ukali wake, nilipokishusha chini tayari kilikuwa kimeshafika nusu.
“Hapana Snox, hatuendi hivyo,” alisema Bonta huku akinipokonya kile kichupa, akakifunga vizuri na kukirudisha mfukoni mwake. Sikutaka kubishana naye, nikatulia huku nikiisikilia ile pombe ikisambaa mwilini kwa kasi ya ajabu.
Mara nilianza kuhisi kama lile jeraha langu pale mguuni linaniwasha, nikapandisha suruali na kulitazama, sijui ndiyo akili ya pombe au kitu gani, nilijikuta nikitamani kulichubua na kutoa ngozi ya juu ambayo ilikuwa ikilifanya jeraha lionekane limeanza kupona.
Bonta hakushtukia nilikuwa nafanya nini, nikawa nimetulia naendelea kujichubua na cha ajabu hata sikuwa nasikia maumivu. Alipokuja kushtuka, tayari nilikuwa nimemaliza kulichubua lote na kwa sababu kidonda bado hakikuwa kimepona, damu nyingi zikaanza kunivuja mguuni na kulowanisha suruali na kiatu changu.
“Mambo gani umeanzahayo Snox?” alisema Bonta kwa sauti iliyoonesha kwamba alikasirika, wakati hayo yakiendelea, kule upande wa pili vilio vilikuwa vikiendelea kusikika, huku wanawake wengine wakiendelea kupika chai kwa ajili ya waombolezaji.
“Kenny unaitwa ndani,” alisema mtoto mmoja wa jirani, aliyetumwa kuja kuniita. Kama nilivyoeleza awali, jina nililopewa na wazazi wangu ni Kennedy ila wengi walikuwa wakilifupisha na kuniita Kenny, ingawa upande wa pili kwenye kazi haramu, jina langu lililokuwa linafahamika lilikuwa ni Snox.
Niliinuka na kutaka kuelekea ndani lakini cha ajabu, nilijikuta nikipepesuka sana, ni hapo ndipo nilipoelewa kwamba pombe siyo chai, ile pombe niliyokunywa ilikuwa imenichukua kwelikweli, nilijitahidi kujikaza lakini wapi, nikawa naendelea kupepesuka, hali iliyomshangaza kilammoja.
“Huyu si ndiyo mtoto mkubwa wa merehemu?”
“Ndiyo! Si Kenny huyu?”
“Sasa mbona amelewa asubuhi yote hii wakati maiti ya baba yake ipo ndani hata bado haijaenda kuzikwa?”
“Halafu mbona amelowa damu mguuni?” niliwasikia wazee wa pale mtaani ambao walikuwa wamejumuika pale msibani wakinijadili, sikuwajali, nikapita kwa hatua ndefundefu za kilevi na kuingia mpaka ndani.
Japokuwa mama alikuwa kwenye huzuni kubwa, alishtuka sana na hali niliyokuwa nayo, akaacha kulia na kuanza kunitolea macho, akiwa ni kama haamini alichokuwa anakiona.
“Umeanza lini kunywa pombe?” aliniuliza mama kwa mshangao, uso wake ukiwa umelowa kwa machozi na macho yake yakiwa yamevimba na kuwa mekundu kwa sababu ya kumlilia baba.
“Sijanywa pombe!” nilisema kilevi huku nikijitahidi kusimama kikakamavu, kumbe ndiyo nilikuwa nazidi kuharibu.
“Halafu kumbe ile harufu ya bangi iliyokuwa inasikika wewe ndiye uliyekuwa unavuta?”
“Ha..pa...na mama,” nilisema kwa kubabaika, baba zangu wadogo na ndugu zangu wengine waliokuwa wamekusanyika kwenye chumba kimoja kwa ajili ya majadiliano ya kifamilia, walikaa kimya wakisikiliza mazungumzo yangu na mama.
“Tuachane na hayo mwanangu,” alisema mama huku akianza tena kuangua kilio, watu wote wakawa kimya mle ndani, baba mdogo akavunja ukimya.
“Tumeitana kama familia kwa ajili ya kujadili taratibu za mazishi, je, tunataka baba akazikwe makaburini au hapahapa nyumbani, lakini pia tumejipangaje kuhusu gharama za jeneza na matumizi mengine ya msibani?” alisema baba mdogo ambaye ndiye aliyekuwa amepewa jukumu la kuwa msemaji wa familia kwenye msiba huo.
“Nitafanya kila kitu mimi, jeneza shilingi ngapi kwani?” nilisema kwa sauti iliyoonesha wazi kwamba mdomo wangu ulikuwa mzito kwa sababu ya pombe, hakuna aliyenijibu, nikaingiza mkono mfukoni na kutoa burungutu la noti za shilingi elfu kumikumi, hata sikuhesabu nikamkabidhi mama lakini alikataa kuzipokea, akawa anaendelea kulia, ikabidi baba mdogo ndiyo azipokee.
Sijui nini kilitokea, wakati nikijiweka vizuri suruali yangu, bastola iliponyoka kutoka pale kiunoni nilipokuwa nimeificha na kudondoka chini, watu wote wakapigwa na butwaa, kwanza kugundua kwamba nilikuwa na bastola kaini pia kugundua kwamba mguu wangu ulikuwa umelowa damu kuonesha kwamba nilikuwana jeraha kubwa.
Hata mama aliyekuwa akiendelea kulia, alinyamaza nakubaki amepigwa na butwaa, harakaharaka nikainama kwa lengo al kutaka kuiokota ile bastola lakini kwa sababu nilikuwa nimelewa, nilishindwa kuiokota, badala yake nikapepesuka na kutaka kuanguka.
Nilirudia tena kujaribu kuiokota, kweli nikafanikiwa kuiokota na kuirudisha pale kiunoni, bado wote wakawa wanautazama mguu wangu.
“Unatembea na bunduki Kenny? Umepatwa na nini mwanangu? Mbona umebadilika ndani ya muda mfupi na kuwa mtu wa ajabuajabu?” alisema mama, akaanza tena kuangua kilio, nikaona hapo ndani siyo sehemu ya kukaa tena kwani ilionesha ni kama hali niliyokuwa nayo ilikuwa ikimuongezea mama huzuni.
“Mjomba mbona unatudhalilisha?” mambo gani tena haya unayafanya? Kwa nini usisubiri tukamzike baba ndiyo uendelee na mambo yako?” aliniambia mzee mmoja tuliyezoea kumuita mjomba, kauli ambayo iliugusa moyo wangu, nikichanganya na hali niliyomuacha nayo mama chumbani, nilijikuta huzuni kali ikinizonga, nikaanza kulia kwa sauti ya juu. Wasichokijua watu wengi ni kwamba kama umelewa halafu ukaanza kulia, unaweza kulia kwa uchungu mpaka watu wote wakakushangaa, ndicho kilichotokea kwangu.
Nikiwa naendelea kulia kwa nguvu na kuwafanya vijana wa pale mtaani pamoja na wazee wa mtaani wapate kazi ya kunituliza, nilishtuka baada ya kuona gari la polisi likija pale nyumbani, pombe zote ni kama ziliyeyuka kichwani, nilipogeuka na kutazama pale Bonta alipokuwepo, sikumuona, moyo ukawa unadunda kwa nguvu kuliko kawaida, ni nikiwa ni kama siamini kilichokuwa kinatokea.
Je, nini kitafuatia
 
SEHEMU YA 37

Naomba maji ya kunywa, ngojeni nikanywe maji,” nilisema huku nikiinuka, uso wangu ukiwa umejawa machozi na kamasi maana nilikuwa nalia kwelikweli ingawa kilio chote kilikatika ghafla baada ya kuwaona wale polisi.
Ujio wao ulionesha wazi kwamba haukuwa wa kawaida, si kawaida polisi kwenda misibani labda katika yale matukio ambayo kifo kimetokea katika mazingira ya kutatanisha, baba hakuwa amekufa kifo cha kutatanisha kwa hiyo ujio huo ulikuwa ni kwa lengo maalum.
Nilitembea harakaharaka huku safari hii hata ile hali ya kupepesuka ikiwa imeisha kabisa, watu wakawa wananitazama huku pia wakitazama kilichonifanya niwe kwenye hali hiyo.
Nilipoingia ndani, nilienda mpaka kwenye dirisha lililokuwa pembeni ya mlango, sikujali waombolezaji waliokuwa wakiendelea kulia, nilijisogeza na kuanza kuchungulia kule nje.
Niliwaona wale polisi wakisogea mpaka pale walipokuwa wamekaa waombolezaji wengine, muda mfupi baadaye nilimuona mwenyekiti wa serikali ya mtaa ambaye naye alikuwa pale msibani, akisimama na kuwafuata wale polisi.
Wakasalimiana kisha wakawa wanazungumza kitu ambacho hata sikuelewa ni nini, nikamuona yule mwenyekiti akigeuka na kuwaoneshea kule ndani, wakaanza kuja. Nilitamani dunia ipasuke na kunimeza, watu wote pale msibani walitulia wakiwa na shauku kubwa ya kutaka kuona nini kilichowaleta askari hao hapo msibani.
Bado sikuwa na majibu, wamefuata nini? Wamejuaje kama nipo pale? Akili za harakaharaka zilinituma kukimbilia kule kwenye chumba kilichokuwa na mwili wa marehemu baba, huko ndiyo mahali pekee ambako hakukuwa na watu. Niliingia mbiombio na kwenda kujifungia mlango kwa ndani, nikawa nautazama mwili wa baba uliokuwa umelala kitandani huku ukiwa umefunikwa sanda, sikuwa najua nini cha kufanya.
Mara nilipata wazo, nililitazama dirisha la chumba hicho ambalo halikuwa limejengwa kwa uimara, nikasogea na kujaribu kulitingisha, niliona likianza kutingishika, nikaona hiyo ndiyo njia pekee ya mimi kujiokoa.
Kumbe wakati mimi nikiwaza hivyo, wale askari tayari walikuwa wameenda mbele zaidi kiakili kuliko mimi, kumbe wakati wengine wakija kule ndani wengine walizunguka upande wa nyuma wa nyuma yetu, wakati nikiendelea kulitingisha kwa lengo la kulivunja ili nitoke na kukimbia, nilimuona askari mmoja akiwa amesimama na bunduki huku akiwa ameilengesha palepale dirishani, kama anayesubiri nitoke tu amalize kazi.
“Mungu wangu, nimekwisha,” nilijisemea huku nikisogea ukutani haraka, mara nikaanza kusikia mlango ukigongwa kwa nguvu.
“Kenny! Kennedy,” nilisikia yule mwenyekiti akiniita, nikajua mwisho wangu umewadia. Kitu pekee nilichoweza kukifanya, ilikuwa ni kutoa bastola pale kiunoni nilipokuwa nimeificha pamoja na zile fedha nyingine ambazo nilikuwa nazo mfukoni, achilia zile nyingine ambazo nilipofika tu nilienda kuzificha kwenye chumba kilichokuwa kinatumiwa na ndugu zetu wa kike hapo nyumbani.
“Sasa nitaificha wapi?” niliwaza wakati mlango ukiendelea kugongwa, nilimtazama marehemu baba ambaye bado alikuwa pale kitandani, nikapata wazo la kwenda kuficha vitu hivyo kwenye sanda aliyokuwa amefungwa.
Nilijua hata kama polisi watakuwa na machale kiasi gani, hakuna anayeweza kwenda kuipekua maiti, ndani ya sekunde chache nilikuwa nimeshaifunua ile sanda, nikaichomeka bastola na zile fedha kisha nikairudishia vizuri.
Mungu anisamehe kwa kitendo hicho na hata baba huko aliko naamini atakuwa amenisamehe kwa sababu sikwa na kitu kingine cha kufanya kwa wakati huo, kwani kama ningesema niirushe ile bastola nje, wale askari wangeiona, kama ningesema niifiche sehemu nyingie yoyote mle ndani, lazima wangenipekua na kuiona! Nasisitiza tena sikuwa na cha kufanya.
Baada ya kuhakikisha nimeirudishia ile sanda vizuri, nilisogea pale mlangoni na kufungua mlango huku nikijikamua machozi, nikakutana uso kwa uso na mwenyekiti na wale askari.
“Kijana mwenyewe ndiyo huyu!” alisema mwenyekiti huku akiwaonesha wale askari kwangu, mmoja kati yao akanisalimu kwa kuniita jina langu kisha akaniambia wana mazungumzo na mimi na kabla hata sijajibu chochote, nilishtukia nikivalishwa pingu kwenye mikono yangu kwa mbele.
“Kwa nini unanifunga pingu? Nimefanya kosa gani? Halafu mna mazungumzo gani wakati mimi nipo kwenye msiba wa baba yangu?” nilisema huku nikiendelea kujivisha sura ya majonzi ambayo ilificha kabisa uhalisia uliokuwa nyuma ya pazia.
“Kwani kuna nini? Afande kwani kuna nini baba zangu, mbona mmemfunga mwanangu pingu?” mama aliingilia kati na kuwauliza wale askari huku uso wake ukiwa umejawa na huzuni kubwa kutokana na majonzi ya kuondokewa na mumewe, macho yake yakiwa yanazitazama zile pingu nilizofungwa.
“Tunahitaji kuzungumza na huyu kijana lakini naona analeta ubishi.”
“Mnazungumza naye nini baba zangu wakati mnajua tupo msibani, na mwili wa baba yake bado hata haujaenda kuzikwa? Halafu kwa nini mumfunge pingu? Kwani mmeambiwa huyu jambazi?”
“Mama, siyo kwamba tunamuonea mwanao, tunatekeleza kazi zetu za kisheria, wala hatujafika hapa kwa kubahatisha. Huyu mwanao ni mhalifu, hebu ngoja kwanza tumpekue huku na wewe ukishuhudia,” alisema yule askari, nadhani walishakuwa na uhakika kwamba kuna kitu watanikuta nacho.
Akanishika mikono ambayo tayari ilikuwa na pingu na kuiinua kwa upande wa mbele kisha akaanza kunipapasa mwili mzima lakini hakukuta chochote. Alirudia zaidi ya mara tatu lakini majibu yalikuwa ni yaleyale, wale askari wakawa wanatazamana kisha wakamgeukia yule mwenyekiti.
Mpaka hapo nilishakuwa naelewa ni nini kinachoendelea, ile hofu niliyokuwa nayo ikapungua moyoni kwa sababu niligundua kwamba kumbe wale askari hawanifahamu na hawajui lolote kuhusu mimi isipokuwa kuna ‘mshakunaku’ mmoja amewapigia simu ili waje kunikamata na moyo wangu ulinituma kumhisi yule mwenyekiti.
“Kenny hebu nenda kazungumze nao nje, sitaki mniharibie msiba wa mume wangu, samahani sana,” alisema mama huku akianza tena kulia, sikutaka kumuona mama akilia kwa hiyo ikabidi nikubali haraka kuepusha shari, nikatoka nao hadi nje huku pia tukiwa tumeongozana na yule mwenyekiti ambaye mara kwa mara nilikuwa namkata jicho.
Watu wote pale nje waliacha kila walichokuwa wanakifanya na kuanza kushangaa kuona natolewa na polisi tena nikiwa nimefungwa pingu na kukokotwa mzobemzobe. Niliwasikai baadhi ya akina mama wakianza kuangua vilio kwa sababu ulikuwa ni msiba juu ya msiba.
“Yule mzee mnoko sana yule, sijui anataka mwenzake asimzike baba yake,” nilimsikia kijana mmoja wa pale mtaani akiongea wakati mimi nikitolewa mzobemzobe, wenzake wakawa wanamuunga mkono, hisia zangu kwamba mwenyekiti alikuwa amenichoma kwa polisi zikazidi kuongezeka.
“Halafu umekunywa sana pombe! Yaani asubuhi yote hii umelewa wakati upo kwenye msiba wa baba yako?”
“Nilikunywa jana usiku, siyo asubuhi.”
“Kijana mdogo kama wewe kwa nini unakuwa mlevi kiasi hiki? Halafu hata midomo yako imebadilika rangi na kuwa myeusi, unavuta bangi wewe si ndiyo?”
“Afande eeh! Tuheshimiane basi,” nilimkoromea askari mmoja niliyeona sasa ameanza kuvuka mipaka na kuniuliza maswali yasiyo nakichwa wala miguu. Jambo ambalo walikuwa hawalijui ni kwamba nikiwa kwenye anga zangu, huwa siwaogopi kabisa askari na nilishawafanyia mambo mabaya sana wenzao kadhaa na hata usiku uliopita tu, tulifanya tukio Ubungo tukiwa na Bonta.
Kichwani nilishajengewa itikadi kwamba askari yoyote yule ni adui yangu, awe mwanamke au mwanaume, kijana au mzee, ilimradi ni askari basi hakuna urafikikati yetu.
“Unabishana na chombo cha dola si ndiyo,” alisema yule askari niliyemkoromea huku akigeuka huku na kule kuangalia kama bado watu walikuwa wakitutazama. Ilivyoonesha, kama kusingekuwa na watu wanaotutazama angeweza kunifanyizia kitu kibaya sana.
Na hapa ndipo askari wengi wanapokosea, wapo baadhi ambao wanaamini kwa sababu wamepitia mafunzo ya kiaskari, basi wanayo haki ya kuwaonea au kuwanyanyasa raia na matokeo yake, hata raia wa kawaida, achana na wahalifu kama mimi, wanakuwa na vinyongo na askari na ndiyo maana hata wakisikia wamepatwa na jambo baya, wanachekelea! Hii ni kwa sababu ya ubabe wa baadhi yao.
“Chombo cha dola utakuwa wewe bwana!” nilizidi kumjibu mbovu yule askari, akawa ananitazama kwa kunitamani kwelikweli huku na mimi nikimtazama vizuri kwa lengo la kumkariri sura yake.
Waliniondoa pale msibani mpaka kwenye kituo kidogo ambacho hakikuwa mbali na pale nyumbani, nikaingizwa ndani na kuanza kuhojiwa, madaiyao eti walisema wamepigiwa simu na msamaria mwema kwamba nilikuwa nafanya fujo msibani na kutishia watu bastola.
“Usalama wako utueleze hiyo bastola iko wapi, vinginevyo kazi unayo.”
“Bastola? Bastola gani, umenipa bastola wewe? Halafu we mzee nimekuona kuanzia kule unanifuatafuata sana, sasa dawa yako inachemka,” nilisema kwa kujiamini, uzoefu wa kutumia bunduki, mazoezi niliyokuwa nayafanya kule ngome ukichanganya na pombe kali niliyokuwa nimekunywa na mibange niliyovuta usiku uliopita, vilinipa ujasiri usio wa kawaida ambao uliwafanya wale askari uvumilivu wao ufike mwisho.
“Unasemaje dogo? Mpeni chai huyu maana naona anatuzoea sasa,” alisema mwingine aliyeonekana kuwa na cheo, yule askari ambaye kuanzia kule nyumbani tulikuwa tukijibizana ‘fyongo’, akawa wa kwanza kunisogelea huku akikenua meno yake kama anayeshangilia kwamba hatimaye amepewa ruhusa ya kunishughulikia.
Kufumba na kufumbua, alinipiga ngumi mbili nzito tumboni zilizosababisha nikohoe damu. Je, nini kitafuatia?
 
Story nzuri sana ingawa Msanga hakuna kituo cha polisi.
 
Similar Discussions

Back
Top Bottom