SEHEMU YA 32
ILIPOISHIA:
“Hebu washa taa zote za ndani dereva,” alisema yule askari, dereva akatii, askari wengine watatu wakaingia, jumla wakawa wanne, wakawa wanapita na kuwatazama abiria vizuri, mmoja baada ya mwingine. Mapigo ya moyo yalianza kunienda mbio kuliko kawaida wakati yule askari mmoja akisogea upande niliokuwa nimekaa huku akiwa amenikazia macho.
SASA ENDELEA...
“Habari yako!”
“Nzuri afande, shika..mooo!” nilimjibu yule askari ambaye sasa alikuwa amenisogelea pale nilipokuwa nimekaa.
“Unatoka wapi?”
“Natoka nyumbani naenda kazini.”
“Unafanya kazi wapi?”
“Mjini.”
“Unafanya kazi gani?”
“Aaa eeh! Naha...ngaika tu afa..nde! Niko gereji!” nilijibu kwa kubabaika, nadhani tayari yule askari alishahisi kwamba kuna kitu hakipo sawa kwa sababu nilipoteza kabisa utulivu.
Hata angekuwa mtu mwingine yeyote katika nafasi yangu, lazima angechanganyikiwa kwa sababu kwanza kiunoni nilikuwa na bastola na kwenye mfuko wa koti, nilikuwa na magazini iliyojaa risasi, achana na zile zilizomo kwenye bastola. Kama hiyo haitoshi, nilikuwa na kiasi kikubwa sana cha fedha nilizokuwa nimezisunda kwenye suruali na kwenye lile koti nililokuwa nimevaa.
“Kitambulisho chako tafadhali,” alisema yule askari, mapigo ya moyo yakawa yanazidi kunienda mbio kuliko kawaida kwa sababu ukweli ni kwamba sikuwa na kitambulisho chochote na kwa kawaida askari akitaka kukutia hatiani, hata kama huna kosa, anakimbilia kukuuliza kitambulisho.
“Afande John, hebu njoo mara moja kuna tatizo huku,” sauti ya askari mwingine ilisikika kutokea kule mbele ya gari, akageuka kuwatazama wenzake. Nadhani yeye ndiye aliyekuwa akiitwa Afande John.
“Nimekwambia toa kitambulisho,” alinisisitiza huku akigeuka na kunipa mgongo, nikajifanya kama najipapasa mwilini kutafuta kitambulisho wakati ukweli ni kwamba sikuwa na kitambulisho chochote, akasogea kule mbele alikoitwa na wenzake. Kule nako kulikuwa na zogo lingine, kumbe kulikuwa na abiria aliyekuwa akisafirisha gunia la mirungi na alikuwa amelichomeka katikati ya siti!
Kwa jinsi yule askari alivyokuwa amenikomalia, nilijua nisipofanya kitu, kweli naweza kujikuta nikiishia pabaya. Nilichokifanya, kwa kasi ya mshali nilivuta kioo na kukisogeza nyuma, kikaachia upenyo ambao naweza kuruka.
Kufumbana kufumbua nilijipindua na kuruka dirishani, huku mkono mmoja ukiwa tayari umeshaichomoa bastola na kuishika, niliamua liwalo na liwe, siwezi kukamatwa kizembe namna hiyo. Kelele walizopiga abiria niliokuwa nimekaa nao kwa mshtuko, ziliwashtua wale askari ambao wote walikuwa wamemzingira yule jamaa aliyekuwa amebeba mirungi.
Kwa kasi ya kimbunga nilikimbia na kuyavuka magari mengine ambayo nayo yalikuwa yamesimamishwa yakiendelea kukaguliwa, nikatokea upande wa pili wa barabara na kuanza kutimua mbio kwa kasi kubwa huku nikihema kwa nguvu. Nilijua kitu pekee kinachoweza kuniokoa kwa wakati huo, ni mbio tu, hakuna kingine.
Kila kitu kilifanyika kwa haraka mno kiasi kwamba mpaka askari wale walipokuja kushtukia ni nini kilichotokea mpaka abiria wengine wakashtuka kiasi kile, tayari nilikuwa nimeshazamia kwenye vichaka vilivyokuwa pembeni ya barabara upande wa pili.
Nikasikia vishindo vikija kwa kasi upande ule niliokimbilia huku askari wakijaribu kumulika kwa tochi zao kali. Ili kuwapunguza kasi, nilifyatua risasi mbili hewani, hali ikachafuka eneo hilo.
Kwa mafunzo niliyokuwa nimeyapata kule kambini, nilikuwa najua kwamba askari wanaposikia mlio wa bunduki, hata kama walikuwa wanakimbia, kwa kawaida ni lazima kwanza walale chini au watafute sehemu ya kujikinga kwanza ili kuepuka kupigwa risasi kizembe na kuangalia ni wapi risasi zinakotokea, kwa hiyo kitendo cha mimi kufyatua risasi ghafla, kiliwachanganya na kuwazubaisha kwa muda, huo ukawa upenyo mzuri kwangu kuzidi kukimbia.
Kwa bahati nzuri, kule nilikokimbilia kulikuwa kama na bonde hivi, kwa hiyo nikawa naporomoka kwa kasi kushuka chini na muda mfupi baadaye, tayari nilikuwa nimetokezea upande wa pili, kutazama nyuma nikaona mwanga wa tochi ukifuata kule nilikokuwa nakimbilia, nikafyatua risasi nyingine mbili na kulenga pale zile tochi zilipokuwa.
Nilijua kwa kitendo kile, hawawezi kuendelea kunifuatilia kwa sababu sasa mimi ndiye niliyekuwa tishio kwao. Niliendelea kukimbia na kiukweli mazoezi magumu ya gamutu yalinisaidia sana kuwa na pumzi, dakika chache baadaye nikawa nimeshawapoteza.
Nilijiona kuwa na mkosi sana kwa sababu kama nisingetumia mbinu hiyo, nilikuwa naenda kunaswa kizembe sana na sijui Bosi Mute angesikia kama nimekamatwa angechukua hatua gani, nikawa nazikumbuka zile sifa alizokuwa ananimwagia wakati akinitambulisha rasmi kwa wenzangu na kunipongeza kwa kazi nzuri niliyoifanya.
Nilichoamua ilikuwa ni kurudi kambini haraka iwezekanavyo kabla hakujapambazuka vizuri kwa sababu tayari ile ilikuwa ni hatari kubwa kwangu. Nilikimbia kwa muda mrefu, nikikatiza kwenye vichaka na mashamba ya korosho na minazi.
Ili kuficha utambulisho wangu kwamba kama wamenimaki kwa mavazi niliyovaa isiwe rahisi kunitambua, nilivua lile koti na shati, nikazifunga fedha zangu vizuri na kuendelea kukimbia nikiwa kifua wazi, mkono mmoja nikiwa nimeshika zile fedha nilizokuwa nimezingirisha kwenye nguo na mkono mwingine nikiwa nimeshika bastola.
Baada ya dakika kadhaa, tayari nilikuwa nimeshafika kwenye barabara inayoelekea Hospitali ya Tumbi, nikaivuka na kuendelea kukimbia kwa kasi utafikiri nashiriki kwenye mashindano ya mita mia moja.
Nilipofika umbali wa kama mita mia mbili hivi, nilisikia muungurumo wa gari likipita kwa kasi kuelekea Hospitali ya Tumbi, ilibidi nijibanze kwenye mti wa mbuyu na kulitazama, lilikuwa ni gari la polisi.
Nadhani walikuwa wameamua kunifukuza kwa gari na kwa mahesabu yao, waliamini kwamba kwa kipindi hicho lazima nitakuwa bado sijavuka barabara kwa sababu walikuwa wakimulika na tochi zao kali upande wa pili wa barabara, mbio zangu zilikuwa zimesaidia kuwazidi akili kwa sababu kama nisingekazana, pengine wangenikuta nikiwa bado sijavuka barabara na kwa jinsi tochi zao zilivyokuwa na mwanga mkali, wangeweza kuniona.
Nilijutia sana uamuzi wangu wa kutosikiliza ushauri, hata wa Bonta aliponiambia kwamba huko mtaani bado hali siyo shwari kwa hiyo nisiende nyumbani badala yake niwatumie hela kwa njia ya simu. Lile gari lilipopita, niliendelea kukimbia, safari hii nikiwa nimeongeza kasi zaidi ya awali, kweli asiyesikia la mkuu huvunjika guu.
Muda mfupi baadaye, nilitokezea sehemu iliyokuwa na makazi ya watu, ikabidi ile bastola niifiche na kuvaa fulana, lile koti nikabaki nimelishika vilevile, nikatokezea kwenye Barabara ya Morogoro na bila kupoteza muda, nilimsimamisha dereva wa bodaboda aliyekuwa akipita, akasimama mita chache mbele.
“Nipeleke machinjioni.”
“Dah! Braza kule siwezi kwenda muda huu, wanatupora sana pikipiki zetu,” alisema huku akipangua gia na kutaka kuondoka, ikabidi nitumie ushawishi wa fedha.
“Nitakupa shilingi elfu thelathini, kuna ng’ombe wetu wameibwa usiku nahisi watakuwa wanachinjwa muda huu, nataka niwahi,” nilimdanganya, kweli akaingia kwenye laini. Nilipanda, harakaharaka akaiondoa pikipiki na tukawa tunaelekea upande wa Mlandizi, kilometa chache mbele akakata kona mkono wa kulia na kuingia kwenye barabara ya vumbi.
Nilimwambia machinjioni kwa sababu kambi yetu ilikuwa upande huo ingawa kulikuwa na umbali mrefu kutoka hapo machinjioni mpaka kufika kambini kwetu, kwa wenyeji wa Kibaha watakuwa wanaelewa machinjio ya zamani ilipo, ni umbali wa kilometa kadhaa kutoka barabara kuu na upande huo hauna shughuli nyingi za kibinadamu na hata nyumba zake zimejengwa mojamoja sana.
Njiani nilikuwa namhimiza aongeze mwendo, wakati mwingine tukawa tunaserereka kwenye mchanga na kunusurika kuanguka, uzuri ni kwamba ilionesha na yeye alikuwa na uzoefu wa kutosha wa kuendesha pikipiki.
Tulipokaribia machinjioni, nilimuelekeza kwamba anishushe, nikamlipa fedha zake na harakaharaka akageuza pikipiki yake na kuondoka, nadhani alihofia kwamba pengine nina lengo la kumkaba na kumnyang’anya pikipiki yake, nikajifanya kama naelekea machinjioni na nilipogeuka na kujiridhisha kwamba yule bodaboda ameshapotea, nilikata kushoto na kuingiakwenye mashamba ya watu, nikaendelea kukimbia kufuata uelekea wa ile barabara inayoelekea kambini.
Mpaka kunapambazuka, bado nilikuwa nikiendelea kukimbia, yaani kama ni adhabu ya ukaidi, nilikuwa nimejipa adhabu kali kwelikweli. Baada ya kukimbia kwa zaidi ya dakika hamsini, hatimaye nilianza kuuona ukuta wa ngome, nikawa najiuliza nitaingiaje na nikionwa itasemaje kwa sababu sasa kulishapambazuka kabisa, moyoni nikajiambia potelea mbali.
Nilikimbia mpaka mwisho kabisa wa ukuta huo, upande wa nyuma, nikaenda mpaka kwenye mti mkubwa wa mkorosho uliokuwa upande wa nyuma, nikapanda na kuanza kuchungulia kwa ndani. Hakukuwa na pilikapilika zozote, nikashuka harakaharaka na kuanza kuhangaika kuruka ukuta.
Ukuta wa nyuma ulikuwa mrefu sana na kwa juu kulikuwa na nyaya za senyenge ambazo ukipita kizembezembe lazima zikunase. Nilitumia akili ya ziada, pembeni kulikuwa na gogo refu la mnazi, nikalisimamisha na kuliegamiza ukutani, kisha nikalitumia kupanda mpaka juu ya ukuta, nikajipenyeza kwa umakini kwenye zile senyenge kisha nikaligeua lile gogo, likadondokea upande wa nje kisha na mimi nikajirusha na kudondokea upande wa ndani.
Kwa bahati mbaya, wakati nikianza kujirusha, suruali ilinasa kwenye zile nyaya, hali iliyosababisha nipoteze ‘taimingi’ ya kuruka, nikajichana mguuni palepale kwenye senyenge na hata nilipotua chini, niliangukia mkono mmoja, nikasikia umelia ‘nkaa!’ kisha ukawa ni kama umekufa ganzi.
“Haya yote ni kwa sababu ya kutomsikiliza Bonta,” nilisema huku nikijikakamua na kuinuka, damu nyingi zikawa zinanitoka pale nilipojichuna na senyenge huku mkono nao ukianza kuniuma kwelikweli, eneo la kiwiko. Narudia tena, kama ni adhabu, nilikuwa nimepata adhabu ya kutosha kwa ukaidi wangu. Japokuwa nilikuwa nasikia maumivu makali, nilijikongoja na kupita nyumanyuma kuelekea kwenye chumba changu.
Wakati mwenyewe nikiamini kwamba hakuna aliyeniona, kumbe kule nilikokuwa napita, damu zilikuwa zikichuruzika na kuweka alama bila mimi mwenyewe kushtukia.
Nilipoingia ndani, nilikimbilia bafuni kwanza, nikavua nguo zote na kuzitupa koridoni, nikaanza kujimwagia maji huku nikiendelea kuugulia maumivu makali ya mkono na lile jeraha la mguuni, ilifika hatua nikawa siwezi tena kuvumilia maumivu, machozi yakawa yananitoka huku nikijilaumu sana kwa uzembe nilioufanya.
Nilikaa bafuni kwa zaidi ya dakika kumi na tano mpaka nilipohakikisha jeraha limeacha kutoa damu, nilipotoka ndiyo nikashtuka kuona kuna alama za damu kuanzia mlangoni mpaka bafuni, nikiwa bado nimepigwa na butwaa, nilisikiamlango wangu ukigongwa kwa nguvu.
“Fungua!” nilisikia sauti nzito ambayo sikugundua haraka ni ya nani kwa sababu kama ni Gamutu, tayari sauti yake nilikuwa naijua.
“Ngo! Ngo! Ngo!” mlango uligongwa tena kwa nguvu zaidi ya mara ya kwanza, nikazidi kuchanganyikiwa, nikiwa hata sijui nifanye nini.
Je, nini kitafuatia?