SIMULIZI....PENZI CHUNGU
MWANDISHI..HALFANI SUDY
SIMU; 0757 633010
SEHEMU YA 42
"Nimewasiri jana toka Ujerumani. Baada ya kuwasiri tu katika ardhi ya Tanzania, IGP aliniita. Nilitoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Juliuas Nyerere moja moja kwa moja nilienda kituo kikuu cha Polisi. Niliwakuta watu watatu ofisini, wote wamekaa wameshika tama. Wakiwa wamezongwa na mawazo.
Nilimkuta Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, nilimkuta mkuu wa majeshi, pamoja na mkuu wa Polisi Tanzania.
Kwa jinsi nilivyowakuta wamekaa nikajua kuna tatizo kubwa sana lililokuwa linawakabiri.
Mkuu wa Polisi, kamanda John Rondo ndiye aliyenikaribisha na kuniamuru nikae kwenye kiti, nilikaa nikiwa na hofu sana. Sikujua ni kitu gani kilichowakutanisha wakuu wale wakubwa wa nchi, tena wakiwa katika hali ya wasiwasi namna ile, IGP John Rondo alianza kuongea, kabla hata ya kusubiri nitulie vizuri kitini.
Alinambia mambo makubwa sana, mambo ambayo yalikuwa rahisi sana kuingia katika masikio yangu, lakini yalikuwa magumu sana kuyaelewa. Hata John Rondo mwenyewe hakuwa na uhakika sana na alichokuwa anakieleza, lakini mwishoni alinielekeza kwa mtu ambaye anaweza kunifafanulia mambo hayo, alinambia niende kwa usiri mkubwa sana, na nitumie ushawishi mkubwa sana ili aweze kunambia mambo hayo. Ni yeye aloyeyashuhudia mambo hayo, huku akionywa kutotoa siri ya mambo hayo, kutoa siri ni kuweka rehani maisha yake. Mtu huyo ni mwanamke, anaitwa Magdalena Zomba, lakini watu wengi wanamtambua kama mama Suto. Nilitoka pale kituo cha Polisi na kuelekea Tabata, nyumba akiyoishi mama Suto, niliwakuta majirani wachache, walionieleza kuwa mama Suto amefariki siku kadhaa, sasa nikajua kazi imeanza. Ndio nimekuja hapa moja kwa moja kuulizia ripoti ya uchunguzi wa kifo cha mama Suto iko wapi, nami nianze kazi yangu"
Inspekta Jasmine mwili wote ulikuwa unamtetemeka, alikumbuka alivyoidharau na kuipoteza ripoti zile za daktari kizembe, kumbe ripoti zile hasa ya Mama Suto ilikuwa na umuhimu mkubwa sana, ripoti ambayo ingetoa njia kwa kukamatwa kwa hao watu, wenye nia mbaya lakini isiyoeleweka wazi kwa wakuu wale wa Polisi na mkuu wa jeshi.
"Ripoti zilipotea Daniel" Inspekta Jasmine aliingea kwa sauti yenye kitetemezi.
"Zimepotea vipi Inspekta?"
"Kuna kibaka aliiba tukiwa katika foleni, na kufanikiwa kukimbia nazo"
"Come on Inspekta, hatufanyi mambo kiurahisi namna hiyo, alikukimbia vipi kibaka Inspekta ?."
Inspekta Jasmine hakuwa na la kusema, alimuomba radhi Daniel, huku akimuomba taarifa ya kupotea kwa ripoti asiipeleke kwa IGP.
"Sasa insp...." Daniel hakumalizia alichotaka kusema, simu ya Inspekta Jasmine ilikuwa inaita.
Akaipokea.
"Mnafanya kazi gani Inspekta, raia wenye hatia wanaendelea kuuwawa, au unataka tuandike kwamba jeshi la polisi ni wazembe kuliko taasisi yoyote Tanzania" Bila salamu Veronika Baro aliwaka kwenye simu.
"Come down mwandishi, tunalifanyia kazi"
"Hadi lini Afande, tuandikaje sasa kwenye magazeti, tuandike nini zaidi ya uzembe wa jeshi la Polisi ?." Inspekta Jasmine hakutaka kuendelea Kumsikiliza mwandishi yule alikata simu.
Mara, simu yake ilianza kuita tena, hakuipokea, alikuwa anaitazama tu mithili ya mtoto akiungalia kwa makini mdoli wake...
ITAENDELEA KESHO MUNGU AKIPENDA.