SIMULIZI; PENZI CHUNGU
MWANDISHI; HALFANI SUDY
SEHEMU YA 58
Zile gari kumi za askari ziliwasiri Tegeta kwa fujo. Askari wote walishuka kabla ya zile gari hazijasimama. Kila mmoja akiwa na bunduki mkononi. Waligawa vizuri, na kila askari akiwa analijua vizuri jukumu lililomleta Tegeta.
"Kumpiga risasi Suto Sutani kisha kumkamata, na kumuuwa siyo mbaya pia" Ilikuwa ni kauli toka kwa Mkuu wa Operesheni ile. Kamanda wa kanda maalum ya Dar es salaam, Elvis Lema.
Askari waliingia kazini, huku maneno ya kamanda wao yakiwa kichwani mwao. Askari walitafuta sana, kwenye hoteli , kwenye mabaa, kwenye nyumba za kulala wageni lakini ilikuwa kazi bure. Hawakufanikiwa kumuona Suto Sutani.
Kwa mara nyingine tena Suto Sutani aliyeyuka!
Polisi sasa waliuhamishia msako wao mtaani, watembeaji usiku walikoma sana siku hiyo. Ilikuwa ni lazima uhojiwe, na ukijibu kisichoeleweka lazima upigwe kidogo na ikiwezekana uwekwe ndani. Ulikuwa usiku mbaya sana kwa walevi.
Inspekta Jasmine na Daniel Mwaseba nao walikuwa wanaenda kwa kasi kubwa sana Tegeta. Kwa lengo moja tu, kumkamata huyo Suto Sutani. Mwanamke aliyekuwa anatafutwa mithili ya gaidi kwa sasa.
Baada ya muda mchache nao walijiunga na wenzao pale Tegeta, walienda kuongeza nguvu, na nguvu iliongezeka hasa. Lakini nguvu hiyo haikusaidia kabisa katika kumkata Suto Sutani.
Wakati Polisi wakiigeuza Tegeta nje ndani, kumsaka Suto Sutani. Suto Sutani mwenyewe alikuwa katika kituo cha kujazia mafuta kama mlinzi Tegeta ileile.
Suto Sutani alivyotoka pale kwa mshona viatu, alitembea huku akiwaza wapi itakuwa sehemu salama kwake. Hakutaka kabisa kulala katika nyumba za kulala wageni, alijua huko atakamatwa haraka sana. Suto Sutani aliongoza barabara akienda asikokujua, mara akaiona sheli pembeni mwa barabara, hapo ndipo alipata fikra mpya, fikra ya kuupitisha usiku ule pale sheli, alihisi ni sehemu salama zaidi.
Alichunguza kwa makini mazingira ya sheli ile. Aligundua kuna mlinzi mmoja tu wa kike. Mlinzi aliyekuwa anasinzia gizani pembeni kabisa mwa sheli ile. Kwa mwendo wa kunyata alimsogelea mlinzi yule wa kike. Pigo moja tu la Suto Sutani aliyebadirika lilimfanya mlinzi yule azimie. Alimburuza hadi kichakani, alimbadirisha nguo, alimvesha nguo zake yake yeye, na Suto Sutani akavaa nguo za kilinzi. Alirudi tena kule sheli na kukaa kiti kile kile cha mlinzi, Suto nae alisinzia.
Inspekta Jasmine na Daniel walizunguka sana mtaani, mafuta ya gari yao yalipungua, wakaiona sheli. Wakawa wanaelekea kujaza mafuta sheli ileile aliyolinda Suto Sutani.
ITAENDELEA KESHO MUNGU AKIPENDA