Riwaya: Penzi chungu

Riwaya: Penzi chungu

SIMULIZI..... PENZI CHUNGU
MWANDISHI.. HALFANI SUDY

SEHEMU YA 28

Hamadi! Kumbe alikuwa Mhudumu wa Guest ile.
Mhudumu yule wa kiume wa nyumba ile ya kulala wageni aliingia kwa kasi sana, akiwa na gazeti la Dumizi mkononi. Sasa alikuwa anatazamana na Suto uso kwa uso. Macho ya Suto yalitua katika lile gazeti. Akajua kuna hatari!

"Bila shaka ni Suto Sutani"
Mhudumu alisema kwa dharau kidogo. Suto aliuficha kwa nyuma mkono wake wa kushoto, akificha kile kisu.

"Suto umefanya hapa ndio kichaka wauaji, ufanye mauaji huko na kuja kujificha hapa" Mhudumu alisema huku akibonyazabonyaza simu yake, bila shaka akitafuta namba fulani za kupiga.
Suto alijua licha ya kuvaa kofia na miwani lakini yule Mhudumu alikuwa ameshamgundua. Akamwangalia yule mhudumu huku akisikitika, Akijua Mhudumu kajiongeza mwenyewe kwenye orodha isiyomhusu, orodha ya kifo ! Suto hakujibu, Suto alitenda.
Kwa kasi ya haraka aliutoa ule mkono wenye kisu kule nyuma, na kwa kasi ileile na nguvu zake zote alididimiza kile kisu katika tumbo pana la yule Mhudumu, Mhudumu alishikwa na mshangao sambamba na maumivu, hakutegemea kama Suto ana kisu, hakutegemea kama Suto atafanya kitendo kama kile kwa muda ule na kwa kasi ile. Mhudumu alishikilia tumbo lake lililobaki na jeraha baya sana. Mhudumu yule alikufa akiwa anashangaa uwezo wa Suto katika uuaji.

Suto Sutani aliona pale siyo sehemu salama tena kwake. Alichukua begi lake dogo la visu, alipita mlango wa nyuma wa nyumba ile ya kulala wageni na kutokomea. Akiuacha ndani mwili usio na roho wa Mhudumu yule mbea.

***************

Inspekta Jasmine alikuwa ofisini kwake ndani ya makao makuu ya Polisi, Posta. Mara simu ya mezani iliita.

"Hallo Afande"
"Hallo Afande"
"Yametokea mauaji Gongo la mboto"
" Saa ngapi?"Inspekta Jasmine aliuliza kwa fadhaha.
" Kama masaa matatu yaliyopita"
"Naelekea huko, ramani sahihi ya nyumba yalikofanyika mauaji utanipa njiani"
"Sawa Afande"
Simu ikakatwa.

Inspekta Jasmine alichukua gari na askari watano, walielekea Gongo la mboto.
Waliwasiri Gongo la mboto, na kwa msaada wa yule askari aliyekuwa anakaa jirani na ile Guest, walifika hadi katika nyumba ya wageni yalipotokea mauaji. Nyumba aliyokuwepo Suto Sutani, adui namba moja wa Inspekta Jasmine masaa matatu yaliyopita. Walikuta kundi dogo la watu.

Inspekta Jasmine na wale askari watano waliingia moja kwa moja ndani ya nyumba ile ya kulala wageni. Walimkuta Mhudumu pale kaunta na yule askari aliyepiga simu. Askari aliyeamini kuwa muuaji kwa kadri ya sifa alizopewa na Mhudumu ni Suto, na kuamua kumpigia moja kwa moja Inspekta Jasmine.

"Habari yako"
"Nzuri Afande"
"Meneja yuko wapi"
"Hapana Meneja hapa nipo mimi tu"
"Hebu nielezee mazingira ya tukio"
"Tuliamka asubuhi vizuri na Mhudumu mwenzangu wa kiume anayeitwa Jerry, baada ya kufanya usafi wa nje, Jerry aliniaga kuwa anaenda kununua gazeti, baada ya muda mfupi alirudi anakimbia na kuelekea uwani, mimi nilidhani kashikwa na tumbo la kuhara, kwahiyo anakimbilia chooni. Yalipita masaa kadhaa Jerry sikumuona. Ilivyofika saa nne asubuhi, muda wa wateja kukabidhi vyumba. Nikaanza kupita chumba kimoja baada ya kingine. Nilipofika chumba namba nane niliukuta mlango ukiwa wazi, nilipoingia ndani, ndipo nilikutana na maiti ya Jery sakafuni......Jerry aliuwawa kwa kuchomwa kisuuu oooooh masikini Jery" Mhudumu alisimulia kwa uchungu na simanzi, huku machozi yakimtiririka. Inspekta Jasmine hakujari kabisa kilio cha Mhudumu yule. Pamoja na kilio chake aliendelea kumhoji.

"Uliandika jina la mteja aliyepanga katika chumba namba nane?"
"Ndio afande"
"Anaitwa nani?"
Mhudumu akipekua kitabu harakaharaka.
"Ana...anaitwa Susa Zamani"

Hii Simulizi ndio kwanza inaanza.....

ITAENDELEA KESHO
 
SIMULIZI.. PENZI CHUNGU
MWANDISHI.. HALFANI SUDY

SEHEMU YA 29

"Suso Zamani?"
"Ndio afande , hili hapa" Mhudumu alisema huku akimuonesha Inspekta lile jina kwa kidole katika daftari la wateja .
"Susa Zamani" Inspekta Jasmine alijisemea kwa sauti aliyojisikia mwenyewe.
Inspekta Jasmine alilipokea lile daftari, kuliangalia vizuri lile jina.
"Susa Zamani "
"Ni nani aliandika hapa ?" Inspekta Jasmine aliuliza swali huku akimwangalia usoni yuke Mhudumu.
"Niliandika mimi, baada ya kutajiwa jina na mteja mwenyewe" Mhudumu alijibu akiwa na hofu kidogo.
"Alikwambia anaitwa?" Ghafla Inspekta Jasmine aliuliza tena.
"Susa Zamani" Safari hii Mhudumu alijibu kwa uhakika zaidi.
"No ni mwanaharamu huyo, ni Suto Sutani !" Inspekta Jasmine aliropoka.
Yule Mhudumu kusikia jina hilo alistuka sana, na kuanza kutetemeka, nani aliyekuwa hajawahi kulisikia jina la Suto Sutani ? Mwanamke aliyeaminika kuwa muuaji, mwenye roho mbaya. Aliyeweza kutoroka katika kuta nne nene za Gereza imara la Segerea.
"Sutoooo"
"Bila shaka, yupoje?"
"Hata sikumuona vizuri muonekano wake, mara nyingi alikuwa anavaa miwani na kofia. Ila ni maji ya kunde na kwa urefu mnalingana na wewe"
"Huyohuyo, ni Suto, bado anaendelea kuuwa mwanaharamu, ana dhamira gani lakini ?" Inspekta Jasmine aliuliza swali, hakukuwa na wa kumjibu.

Inspekta Jasmine na wale askari wengine walienda katika chumba namba nane, chumba alichokuwa Suto Sutani muda mfupi uliopita. Zaidi ya mwili wa yule Mhudumu uliolala bila uhai pale sakafuni, hawakupata lengine la maana. Suto hakuacha alama yoyote mle chumbani.

Inspekta Jasmine aliomba msaada wa kuongezewa Polisi. Polisi ambao walijitahidi kumsaka Suto katika Guest na Baa zote za Gongo la mboto, lakini Suto Sutani hakuonekana. Gongo la mboto iligeuzwa nje ndani, hawakuambulia kitu. Suto Sutani alifanya mauaji na kutoweka kwa mara nyingine.

Asubuhi ya siku iliyofuata ilimkuta Inspekta Jasmine mbele ya meza ya Mkuu wa upelelezi na makosa ya jinai kanda ya Dar es salaam. Lililompeleka ni moja tu, na la aibu. Kwa mara ya kwanza katika maisha yake ya kulitumikia jeshi la Polisi, Inspekta Jasmine alikubali mbele ya Mkuu wake kuwa ameshindwa kazi ya kumkamata muuaji. Ilikuwa aibu kwake, aibu kubwa sana kwa jeshi la Polisi pia.

"Inspekta Jasmine"
"Ndio mkuu"
"Unasema umeshindwa kazi ya kumkamata muuaji ?"
"Ndio Afande"
"Nani ataweza sasa?"
"Naomba uchague askari mwengine Mkuu"
"Hilo linawezekana, ilaa naomba unikabidhi mkanda na kofia, hivyo ni mali ya jeshi la Polisi"
"Sijakuelewa Mkuu"
"Umeshindwa kazi Inspekta, sasa kwanini tulikupeleka CCP Moshi? tulikupeleka Moshi ili uje kushindwa kazi?"
"Sina maana nimeshindwa kazi...."
"Sasa umeshindwa nini, nitajie kazi kuu za askari"
"Lakini Mku...."
"Lakini nini afande! Naomba ukaandike barua ya kuacha kazi leo. Kesho asubuhi niikute mezani kwangu !"
Hali ilikuwa tete kwa Inspekta Jasmine.
"Basi nisamehe Mkuu, nitamsaka Suto !"
"Nakupa wiki moja, Suto awe amekamatwa, la sivyo ombi lako la leo, litakuwa limepita bila kipingamizi"
"Ombi gani Mkuu?"
"Ombi lako la kuacha kazi !"
"Sijaomba kuacha kazi mkuu" Inspekta Jasmine maji sasa yalikuwa yamemvuka shingo na kuamua kumzamisha taratibu...

ITAENDELEA BAADAE
 
SIMULIZI ..PENZI CHUNGU
MWANDISHI.. HALFANI SUDY

SEHEMU YA 30

"Ulikuja kufanya nini sasa hapa ofisini?"
"Naomba nisamehe Afande"
"Nakupa wiki moja Suto awe amekamatwa. Nitakupa msaada wowote unaoutaka kwa kipindi hiko, nimemaliza, waweza kwenda "

Inspekta Jasmine alipiga saluti na kutoka nje akiwa na hasira zisizo na kifani.

***********

Beji na Zura walipata kashikashi kubwa kazini kwao, baada ya uchunguzi walionekana wao ndio wazembe kazini. Na wote walifukuzwa kazi. Ilikuwa ni huzuni sana kwao, huzuni hiyo ilizidisha hasira kwa dada wale wawili, sasa walirudi mtaani wakiwa na hasira isiyo na kifani dhidi ya Suto Sutani. Waliapa lazima wamkamate Suto, lazima wamuuwe Suto Sutani.

***********

Wakati Inspekta Jasmine akigomewa na Bosi wake kuhusu Suto Sutani, na Beji na Zura wakifukuzwa kazi baada ya kuzembea kazini na Suto Sutani kutoroka gerezani.

Suto Sutani, alikuwa nje kidogo ya Jiji la Dar es salaam. Alikuwa amejificha katika kibanda kidogo katika kijiji cha Mwanambaya, kilichopo wilaya ya Mkuranga. Alijificha katika kibanda hicho kidogo tangu alivyofanya mauaji kule Gongo la mboto. Alipanda daladala inayoelekea Mbagala tena kutokea kule Gongo la mboto, alipofika Mbagala alipanda gari linaelekea Mkuranga na kushuka Mwanambaya. Hakuna mtu aliyemtambua katika magari aliyopanda. Bahati ilikuwa upande wake, alopofika Mwanambaya alikikuta kibanda dhaifu cha nyasi na kujihifadhi humo. Kibanda kilichohamwa na wenyewe kwa kuwa kipindi hiko hakikuwa kipindi cha kilimo.

Jiji Dar es salaam ilikuwa patashika. Baada ya kumkosa Suto Gongo la mboto, Inspekta Jasmine aliomba msaada kwa Bosi wake. Aliomba kuweka askari wa kutosha barabarani ili magari yote yawe yanakaguliwa kumtafuta Suto, nyumba za wageni zote zipekuliwe Dar es salaam nzima kumtafuta Suto, lakini Suto hakupatikana, Suto hakuwa Dar es salaam, Suto alishafika Mwanambaya kabla ya msako wa katika magari haujaanza.
Kutoonekana kwa Suto kulimuumiza sana Inspekta Jasmine. Aliona kazi yake inakaa rehani, kwa ajili ya Suto Sutani, hakutaka kabisa kukubali kushindwa, lakini alielekea kushindwa.

************

Wakati Suto Sutani akiwa katika kibanda dhaifu huko Mwanambaya, katika hoteli moja huko Mwenge kulikuwa na kikao. Kikao kilichoitishwa na mama Bruno, katika kikao hiko pia walikuwemo Manka, Dungu, Banda, Beji, Zura, Veronica Baro, Banda na wanaume wengine wawili. Kilikuwa kikao cha watu kumi wenye dhamira ya mbaya ya kumuua Suto Sutani....

ITAENDELEA Baadae....sorry jana cm ilizima chaji...
 
SIMULIZI.... PENZI CHUNGU
MWANDISHI.. HALFANI SUDY
SIMU; 0757 633010

SEHEMU YA 31

"Habari zenu jamani" Mama Bruno alisalimia.
"Nzuri" wote waliitikia.
"Hapa tuna agenda kuu moja tu, hakuna kufungua kikao wala kufunga kikao, agenda ni kumuua Suto Sutani kwa njia yoyote ile na haraka iwezekanavyo, kikao hiki ni kwa ajili ya kupanga mipango kujua tunaanza vipi na tunamaliza vipi. Lakini tuhakikishe Suto Sutani anakufa !" Mama Bruno alisema kwa kirefu.
"Mpango siyo kumuua Suto, mpango kwanza ni kujua Suto Sutani yupo wapi kwa sasa, Suto Sutani amekuwa mwiba mkali sana, jeshi la Polisi lenyewe linahaha usiku na mchana kumsaka Suto. Sasa sisi tunapanga kumuua, tutamuonea wapi, hapa tujipange kumtafuta kwanza, ili tujue anaishi wapi" Manka nae alichangia.
"Ni kweli kabisa Manka. Kujua Suto Sutani yuko wapi ni kazi ngumu kuliko tunavyofikiria, jeshi la Polisi lenyewe limeshindwa kuvumbua kitendawili hiko mpaka leo wanahaha kumsaka Suto, mama Bruno kama unadhani kazi ya kumuua Suto ni rahisi, unajidanganya mama, Mimi ndiye naziona nyuso za maaskari zilivyo na woga, Inspekta Jasmine mwenyewe tunayemuamini wananchi wote, huku nchi ikimtegemea, anastuka ukimtajia jina la Suto Sutani, Veronica mimi najuta kujiingiza katika kadhia hii, pesa zenu haramu zimeniponza, kuitumia vibaya kalamu yangu kumeniponza, sijui... ."
"Nyamazaaaaa...huu siyo wakati wa kulaumiana, siyo wakati wa kulalamika, kama pesa ushachukua, kama kalamu yako ushaitumia vibaya, lakini ushukuru bado upo kazini, bado ni mwandishi wa gazeti la Dumizi, sisi tumekosa kazi Veronica, kutokana na Suto, kutokana na pesa unazoziita haramu. Cha muhimu hapa ni kutafuta namna ipi tunampata Suto Sutani na kumuua, basi !" Beji aliyasema maneno hayo kwa hasira. Na wengine wote walitikisa vichwa, ishara ya kukubaliana nae.
"Eeh tunafanyaje sasa" Dungu kwa mara ya kwanza alichangia.
"Naona mnagombana sana, kumkamata Suto na kumuua siyo tatizo kabisa. Suto atamatwa na atauwawa!. Kumkamata Suto ni kazi ndogo sana kwa Kurwa na Doto. Kwakuwa mmetushirikisha katika hili hakuna litakaloshindikana. Mnastaajabu Polisi kushindwa, Polisi hawana akili za kutufikia sisi, Kulwa na Doto" Kurwa kijana mpya katika kikao kile alisema kwa kujigamba.
Sasa kikao kilipata uhai, Kurwa alirejesha hali ya kujiamini kwa wanakikao.
"Tunaanzaje sasa msako wetu?" Dungu aliuliza.
"Mwelekeo wetu unategemea mwelekeo wa Polisi, lazima tujue Polisi wanahisi Suto yuko wapi,nasi tunaelekea huko. Kwa hilo tunategemea sana mchango wako Veronica, ukaribu wako wa Polisi utatusaidia sana. Lazima tuhakikishe Suto anakufa kabla hajaingia mikononi mwa Polisi, Polisi wakimkamata tu, atakutajeni ninyi, nanyi mtaangia matatani. Lazima tuwe makini, na tufanye kazi kwa haraka mara mbili au tatu zaidi ya Polisi. Kulwa alieleza kwa kirefu.
" Tunawategemea sana jamani" Manka alisema kwa sauti yenye uwoga.
"Usijari, tutafanya kazi mliyotutuma kwa haraka sana"

Mama Bruno alifunga kikao, kila mtu akiwa na matumaini mapya, huku wakisubiri taarifa toka kwa mwandishi Veronica Baro, ili Kurwa na Doto wakafanye kazi.....

ITAENDELEA. ........
 
SIMULIZI......PENZI CHUNGU
MWANDISHI..HALFANI SUDY

SEHEMU YA 32

Usiku ulimkuta Suto Sutani akiwa Mwanambaya porini. Suto alikuwa anajisikia njaa. Hakukuwa na chakula chochote kule porini alikokuwa, ilimlazimu aende kijijini Mwanambaya aone jinsi ya kupata chochote cha kutia tumboni. Lakini kwenda kula kule kijijini ilimaanisha kuukaribia mkono wa adui. Suto alijua sasa sura yake ilikuwa maarufu sana ndani ya Tanzania nzima. Hakutaka kabisa kujidanganya eti kwa kuwa ni kijijini basi watakuwa hawajui lolote kuhusu msako wake, pamoja na yote hayo Suto hakuwa na jinsi. Ilikuwa ni lazima aende kijijini kula.

Alitoka taratibu toka katika kile kibanda, alibeba begi lake dogo lililojaa visu, na kuifuata njia nyembamba iliyokuwa inaelekea kijijini Mwanambaya.
Baada ya mwendo mrefu kidogo, alianza kuona ishara ya mwanga, ishara ya uhai, vilikuwa vibatari. Pamoja na muda kutaradadi, lakini baadhi ya watu wa kijiji kile walikuwa bado hawajalala. Hasa wafanyabiashara ndogondogo.
Suto alisogea taratibu, huku umakini wake ukiongezeka kadri ya anavyopiga hatua kukikaribia kijiji.
Hatimaye alifika kijijini.

Suto alimwona Mzee mmoja akiuza mahindi ya kuchoma pembeni kidogo na wenzie, alimfata kwa mwendo wa taratibu.

"Habari Mzee"
"Nzuri, hujambo" Mzee alijibu huku alimwangalia Suto usoni.
"Suto akainama kidogo, ili asiangaliane na yule mzee moja kwa moja.
" Nataka mahindi matatu Mzee" Suto alisema huku akiiweka kofia yake vizuri .
"Mia tisa" Mzee alijibu bila kumwangalia Suto safari hii.
Suto alinunua mahindi, na kuifata ile njia aliyotokea muda mfupi.
Yule Mzee alikuwa ni Mzee maarufu sana Mwanambaya. Umaarufu wake ulitokana na sababu kuu mbili, kwanza ni kuuza mahindi na umaarufu wake wa pili ni kwa ajili ya kusoma magazeti. Pale alivyomtazama tu Suto kwa mara ya kwanza, aligundua ndiye muuaji anayetafutwa. Aliiona sana sura ile kwenye magazeti na sasa alikuwa ameshaizora. Akavuta gunia lake la mahindi. Akatoa kipande cha gazeti la Dumizi.

"Ndiye muuaji !"

Alisema kwa sauti kubwa. Mzee yule kwa mwendo wa haraka alienda nyumbani kwa mtendaji wa kijiji, muda uleule ikapigwa mbiu. Wanakijiji wote walikusanyika. Wakaambiwa taarifa ya kuonekana muuaji kijijini kwao. Taarifa iliyowastua sana. Huku wakisisitizwa wawe makini sana. Eti muuaji kaingia kijijini kwao.
Afisa mtendaji akapiga hatua moja mbele zaidi, alipiga simu kituo cha Polisi Mkuranga, kuomba msaada wa Polisi.
OCD wa Mkuranga aliipokea taarifa ile kwa hofu sana. Naye alipiga simu makao makuu ya Polisi, makao makuu wakamtaarifu askari anayehusika na kesi ile, Inspekta Jasmine yupo njiani. Kutoka kwa Inspekta Jasmine taarifa zilimfikia Veronica Baro, kutoka kwa Veronica Baro taarifa zikawafikia kina Kulwa na Doto. Wakati Inspekta Jasmine akiwa ndani ya gari lilikuwa linaenda kwa kasi kuelekea Mwanambaya. Kulwa, Doto na Dungu, nao walikuwa kwenye gari wakielekea huko kwa kasi kubwa zaidi.
Wote wakimuwahi Suto Sutani. Kina Kulwa kwa lengo la kumuua, wakati Polisi kwa lengo la kumkamata...

ITAENDELEA KESHO MUNGU AKIPENDA.
 
SIMULIZI.....PENZI CHUNGU
MWANDISHI..HALFANI SUDY
SIMU; 0757 633010

SEHEMU YA 33

Gari ya kina Kulwa ilikuwa inaendeshwa kwa kasi sana. Nyuma ya usukani alikuwepo kijana wa kihuni, na akiendesha gari kihuni pia, alikuwa anaitwa Dungu, na alikuwa analitungua gari.

Suto Sutani, kwa mwendo wa taratibu alielekea kwenye ficho lake jipya. Bila kujua kuna hatari kubwa sana iliyokuwa inamkimbilia kwa kasi. Jambo usilolijua......
Aliingia katika kibanda chake , na kujilaza.

Kule kijijini Mwanambaya kulikuwa na taharuki kubwa sana. Wanakijiji walikuwa na hofu kubwa sana. Suto sasa alikuwa tishio. Wanakijiji wengi walikuwa wamekaa kwa mafungu wakimuongelea Suto Sutani huku wakionesha uwoga wao dhahiri.

Ghafla gari ya kina Dungu iliingia kwa kasi kubwa na kufunga breki kali, gari ile ilizidisha hofu kwa wanakijiji. Walianza kupiga kelele hovyo na kukimbia. Kelele zile zilitua moja kwa moja katika masikio ya Suto Sutani kule porini.

"Hapa siyo sehemu salama tena"
Alisema kwa sauti ndogo. Hakujishauri mara mbili, alibeba begi lake na kutokomea porini zaidi.

Kule kijijini ilikuwa patashika, Kulwa, Doto na Dungu walileta patashika kijijini. Waliingia kwa Mtindo mbaya, Mtindo ambao uliwafanya wakose ushirikiano toka kwa wanakijiji. Kila mmoja na bastola yake, walikuwa wanamtafuta Suto Sutani kwenye nyumba za watu.

Muda mfupi, vilisikika ving'ora kwa mbali, ishara kuwa Inspekta Jasmine na askari wengine walikuwa wanawasiri kijijini pale. Hali ya taharuki iliongezeka Mwanambaya !

Sasa kina Dungu nao iliwaingia hofu, walikimbia mbio na kupanda katika gari yao, waliifata barabara inayoelekea Mkuranga. Wale askari nao kufika Mwanambaya waliikuta taharuki kubwa, huku vumbi likiwa hewani, wanakijiji wote wakionesha kwa kidole njia inayoelekea Mkuranga. Bila kuuliza zaidi gari la Polisi lilielekea huko wakijua ndipo alipoelekea Suto Sutani.
Gari ya kina Dungu ilikuwa inaenda kwa kasi kubwa sana. Liliiacha mbali sana gari ya Polisi.
Dungu alikuwa mtoto wa kihuni mwenye kujua kweli kuliendesha gari kihuni. Walipokaribia jaribu, walipunguza mwendo wa gari. Na walipofika kijijini Jaribu, walisimamisha kabisa gari. Wakalipaki huku wenyewe wakikaa pembeni. Baada ya dakika kumi, waliliona gari ya Polisi ikipita kwa kasi kubwa sana. Huku king'ora cha hatari kikilia. Wakina Dungu walitabasamu, walipanda kwenye gari yao na kurejea kijijini Mwanambaya.
Walikaribia kijiji cha Mwanambaya, waliliacha gari na kuelekea Mwanambaya kwa miguu. Safari hii walibadiri mbinu, walikuwa wapole sana. Walikutana na mwanakijiji mmoja aliyawaeleza kila kitu kuhusu Suto Sutani, na mahali inaposemekana yupo kule porini. Kina Dungu, Kulwa na Doto walielekea huko...

ITAENDELEA BAADAE MUNGU AKIPENDA
 
SIMULIZI... PENZI CHUNGU
MWANDISHI.. HALFANI SUDY
SIMU.... 0757 633010

SEHEMU YA 34

Dungu na wenzake waliingia porini. Huku wakijilaumu kwa mbinu mbaya waliyoitumia mwanzoni walipofika pale kijijini. Porini kulikuwa na Giza la kutisha sana, la kumuogopesha mtu yeyote wa kawaida. Lakini Dungu, Kulwa na Doto hawakuwa watu wa kawaida kama mimi na wewe. Walikuwa manunda, walikuwa wameshindikana, walikuwa hawaogopi lolote, walisonga mbele kule porini bila wasiwasi wowote.

Inspekta Jasmine, pamoja na Polisi wake sasa walikuwa wanaingia Kibiti. Kwa kasi ileile na king'ora chao chenye sauti kali sana. Hawakubahatika kuliona gari lolote, kwa mara nyingine tena walihisi Suto Sutani kawazidi kete. Wao walikuwa wanajua mbio zile wanamkimbiza Suto. Walipofika Kibiti kijijini walisimama, waliwauliza watu na kuambiwa kuwa haijapita gari yoyote kijijini hapo, Inspekta Jasmine alifura kwa hasira. Alitamani kumkaba yule mtu aliyewapa taarifa ya kutoonekana kwa gari walilohisi anaendesha Suto Sutani. Waliamua kurejea Mwanambaya.

Wakati kina Dungu wakihangaika kule porini, Inspekta Jasmine na mapolisi wakihangaika kule Kibiti, Suto Sutani alikuwa Tandika. Alitembea kwa miguu pori kwa pori usiku ule akatokea Kisemvule, Kisemvule alipanda daladala iliyomteremsha Mbagala. Ulikuwa usiku hakukuwa na mtu aliyekuwa makini na Suto ndani ya gari. Kwa kutumia faida ya giza alipanda na kutulia katika gari ya Mbagala inayoelekea tandika bila kujulikana na mtu yeyote. Na sasa alikuwa amekaa katika darasa moja la shule ya Sekondari Maarifa.

Kule porini kina Dungu hawakumuona Suto. Walitafuta sana, lakini hawakumuona kabisa Suto. Waliamua kurejea kijijini.
wakati ule wakati kina Dungu wanaamua kurejea kijijini, kina Inspekta Jasmine nao ndio walikuwa wanaingia kijijini Mwanambaya.

Kina Dungu walikuja taratibu, walipokaribia kijijini waliona kitu kilichowastua sana.
Askari !
Askari zaidi ya kumi walikuwa wanakuja upande waliokuwa wao, kule porini. Kwa kasi ya ajabu vijana wale waliingia vichakani, walijificha.
Inspekta Jasmine na askari wake walipita pale bila kuhisi kitu chochote na kuelekea porini, askari walivyopita kina Dungu wao walinyanyuka na kuelekea kijijini. Walipofika waliongoza kule walikoliacha gari yao, walilichukua na kurejea mjini. Walifanikiwa kuwakwepa Polisi, lakini hawakufanikiwa kumkamata Suto Sutani ambaye ndiye alikuwa dhamira yao kuu...

ITAENDELEA TENA BAADAE
 
SIMULIZI.....PENZI CHUNGU
MWANDISHI..HALFANI SUDY
SIMU... 0757 633010

SEHEMU YA 35

Mapolisi nao walitafuta sana kule porini, hawakufanikiwa kumpata Suto. Ilikuwa kama hakuwahi kuwepo sehemu ile. Maaskari walirejea kijijini. Wakiwa mikono mitupu. Waliamua kuacha askari wawili kulinda kijijini pale, huku Inspekta Jasmine na askari wengine wakirejea mjini.

Alfajiri Suto Sutani ilimkuta mle darasani, aliupitisha usiku wa siku ile mlemle.
Aliamka.
Kutokana na mateso aliyoyapitia usiku ule dhamira yake ya kulipa kisasi ilizidi kushamiri. Aliteseka sana kule porini, aliteseka sana pale darasani. Aliamua kuyarejesha mateso aliyoyapata kwa waliomsababishia mateso hayo. Aliwakumbuka, Beji na Zura, askari Polisi waliomtesa sana gerezani, askari waliochangia kwa kiasi kikubwa kumpandikiza roho mbaya ya kikatili aliyokuwa nayo leo. Suto sasa aliamua kwenda kuwaonesha Beji na Zura matokeo ya kazi waliomfundisha. Aliamua kwenda kuwauwa Beji na Zura hukohuko Segerea. Alinunua kanga pale Tandika sokoni, akaongeza na idadi ya visu. Alivyovihifadhi vizuri katika begi dogo.
Alijifunga zile kanga mbili mwilini, kiunoni na kifuani, kanga iliyomsaidia kumfunika hadi kichwani. Sasa Suto alibadirika sana, alikuwa na taswira nyingine, taswira ya kimama, tofauti kabisa na taswira waliyokuwa nayo wakina Inspekta Jasmine na Polisi wenzie.

Aliingia katika daladala na kuelekea Segerea.
Gari liliondoka kwa mbwembwe nyingi za dereva pale Tandika sokoni. Safari ya kuelekea Segerea ilianza.

Walipofika njiani walikutana na askari wengi sana barabarani. Wakiosimamisha kila gari linalopita.
Na gari alilopanda Suto nalo lilisimamishwa. Kule ndani ilikuwa taharuki kubwa sana kwa Suto. Alipata mstuko mkubwa sana, alijua arobaini zake zimefika. Suto alianza kulia kwa uchungu, kilio kilichotokana na kushindwa kutekeleza kwa aliyoyapanga. Aliona huu ndio ulikuwa mwisho wa kisasi chake kwa watu waliomsababishia mateso makali sana duniani. Hakuwa anahofia kukamatwa Suto, ila alihofia kukamatwa kabla hajakamilisha kisasi chake, na hilo ndilo lililokuwa linamliza kwa uchungu mkubwa, kukamatwa kabla hajaimaliza orodha yake ya kifo !
Sasa askari walikuwa wanalisogelea gari alilopanda Suto Sutani....

ITAENDELEA USIKU SANA
 
SIMULIZI...PENZI CHUNGU
MWANDISHI..HALFANI SUDY
SIMU: 0757 633010

SEHEMU YA 36

Askari mmoja alilisogelea lile gari alilopanda Suto Sutani. Alienda upande wa kulia anaokaa dereva, na kuongea nae kidogo, kwakuwa Suto Sutani alikuwa amekaa katika siti za nyuma za ile daladala hakusikia lolote. Wakati yule askari akiongea na dereva alimuona askari mwengine akielekea ulipo mlango wa daladala ile.
Aliingia ndani !.
Suto Sutani aliinamia kiti, akijifanya amelala usingizi mzito. Askari alisogea hadi siti za mwisho za daladala ile. Akawa amesimama jirani kabisa na Suto Sutani, aliyekuwa ametopea katika usingizi mkali wa kuigiza huku jicho moja likiona kila kitu kinachoendelea.
Daladala ile ilisogezwa pembeni na kupaki, na kuzimwa kabisa na dereva.
Askari wengine wawili walilifuata daladala lile.

Ghafla!, msafara mkubwa wa magari ulipita, Suto Sutani kwa kutumia jicho lake moja aliushuhudia msafara ule. Gari la nne katika msafara ule ndio lililorejesha matumaini katika moyo wa Suto Sutani, alimuona Raisi wa jamhuri ya muungano wa Tanzania akiwa na mkewe, wakiwa wametulia katika siti za kati za gari lile la kifahari. Suto sasa akaijua sababu ya kusimamishwa, kumbe msafara wa Raisi wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikuwa anapita katika njia ile. Suto alipumua pumzi ndefu sana, huku akimshukuru Mungu kimoyomoyo. Baada ya msafara wa raisi kupita,waliruhusiwa kuendelea na safari. Laiti trafki wangeijua dhamira iliyopo katika moyo wa Suto Sutani, wasingeiruhusu daladala ile iendelee na safari yake.

Daladala ilimfikisha Suto Sutani Segerea, aliwaona watoto wa maaskari wakicheza mpira wa manailoni katika uwanja mdogo wenye mchanga mwingi, Suto alimuita mtoto mmoja na kumuuliza.
"Hujambo mtoto"
"Sijambo, shikamoo"
"Ngoja nikuulize kitu mtoto mzuri, Dada Beji na Zura wanakaa nyumba gani?"
"Ngoja nikuitie Bakari mimi siwajui"
Mtoto ambaye aliyetambulika kama Bakari aliitwa, alikuwa mtoto mwenye umri mkubwa kidogo tofauti na yule aliyemuuliza Suto awali.
"Eti Bakari,Dada Beji na Zura wanakaa nyumba gani?"
"Walihama hapa siku nyingi, ila leo nimemuona Beji kwa mkuu wa gereza. Moyo wa Suto uliruka sarakasi !

ITAENDELEA KESHO MUNGU AKIPENDA
 
SIMULIZI... PENZI CHUNGU
MWANDISHI.. HALFANI SUDY

SEHEMU YA 37

Suto alimuaga harakaharaka yule mtoto, na kuelekea mahali ilipokuwa ofisi ya mkuu wa Gereza. Alikuwa anaijua vizuri sana ofisi hiyo.

Beji alikuwa ameleta malalamiko yake ya madai ya mafao kwa mkuu wa Gereza. Alishayapeleka katika Wizara ya mambo ya ndani, na nakala aliileta kwa mkuu wa Gereza la Segerea. Gereza alilokuwa anafanyia kazi. Kabla ya kisanga kile cha usiku kilichoondoka na kazi yake, kilichoondoka na mafao yake.
Beji na Zura hawakukubali!

Kazi kama hii ya kuleta nakala ya madai aliifanya Zura siku iliyopita. Ingawa sheria zilikuwa wazi kwa mtu aliyefukuzwa kazi, lakini Beji na Zura walikuwa vichwa ngumu!

Sasa Beji alikuwa anatoka katika ofisi ya mkuu wa Gereza baada ya kumkabidhi ile nakala.
Walikutana na Suto Sutani katika korido ndefu ya kutoka kule ofisini kwa mkuu wa Gereza. Beji hakumtambua kabisa Suto Sutani, wakati Suto alimtambua Beji vizuri sana. Huku akificha kwa ile kanga aliyovaa alikiweka kisu chake vizuri, kikiwa amekishika imara kwa mkono wake wa kulia. Huku lile begi lake lenye visu likibembea katika bega lake la kushoto.
Korido yote ilikuwa kimya. Msuguo wa viatu vya watu wawili tu ndio vilikuwa vinasikika, viatu vya Suto Sutani na msuguano wa viatu vya Beji. Walikaribiana kabisa sasa, walikuwa na tofauti kama ya hatua mbili hivi.

Mara, kwa kasi ya ajabu na nguvu zake zote Suto alipiga hatua kubwa kumkaribia Beji na kukididimiza kile kisu kirefu shingoni kwa Beji. Beji alistuka sana, alipata maumivu makali na mstuko mkubwa sana!. Suto aliishusha kabisa ile kanga iliyomfunika kichwani. Sasa alionekana vizuri sana.
"Suto ume-ni-u--a..." Beji aliongea kwa sauti ya kukatakata. Suto alipiga kofi la nguvu juu ya ule mpini wa kisu! Beji alitoa ukelele dhaifu wa kukata tamaa.
"Ndio, naitwa Suto Sutani!"
Suto Sutani alivaa vizuri ile kanga yake na kurudi kwa kasi kule alikotoka.
Akijua tayari kashaua!.

Beji hakutegemea kabisa kitendo alichofanyiwa na mwanamke yule katili. Kwa taabu alijishika pale shingoni kilipoingizwa kisu,
alistaajabu!.
Aliushika mpini tu wa kisu, kisu chote kilikuwa kimezama ndani ya shingo yake!
Beji alikosa nguvu, aliyumba, akajiegemeza katika ukuta wa Gereza lile, damu sasa ikawa inatoka shingoni mithili ya chemchem ya maji. Beji alijitahidi kupiga kelele, lakini alijisikia mwenyewe, sauti haikutoka kabisa. Mara aliona macho yake yamekuwa mazito, macho yalikuwa yanajifumba yenyewe taratibu huku yakishuhudia kwa mbali damu nyingi sana pale ukutani.
Beji alizimia !

Wakati Beji akipitia katika mateso makali na hatimaye kuzimia, Suto Sutani alikuwa katika daladala inayoelekea kariakoo. Alikuwa amesimama hakupata siti ya kukaa. Alikuwa mtulivu sana kama hajafanya tukio la kutisha sana dakika chache zilizopita. Alikuwa anaelekea kariakoo, akiamini wingi wa watu wa Kariakoo utakuwa faida kwake na kutokamatwa kwa urahisi na askari.

Akiwa amesimama wima, ghafla macho yake yakatua kwa kondakta wa daladala ile.
"Ndiye mwenyewe" Suto alisema kimoyomoyo, kondakta wa daladala ile alikuwa Banda mlevi. Mlevi aliyejaribu kutaka kumuua na kumbaka kwa mara ya kwanza Suto Sutani pale gerezani Segerea, pamoja na Giza la usiku ule haikuwa sababu ya Suto kutomtambua, alikumbuka vizuri sana umbo la mtu aliyepambana nae usiku gerezani, alikumbuka vizuri....

Banda na Suto daladalani, nini kitatokea?

Itaendelea usiku sana....si yakukosa
 
Back
Top Bottom