Riwaya: 'Njama'

Riwaya: 'Njama'

Mimi nimesoma haya mavitabu ya hadithi mpaka basi. Kina Ben Mtobwa, sss Simbamwene, Hammie Rajabu Musiba mwenyewe vote vi4....lakini vyooote kilichonishika ni Sofia wa Gongo la mboto. Pili pilipili na pumbazo la moyo....dah kitambo kweli

Una nakala yoyote unisaidie nami nisome.????
 
Ayaaa,rusheni nondo moja moja jama,mtatuchanganya,tufatilie kikomo,kisha mwenye kufa n's kupona,kijasho chembamba,hofu na uchu waturushie kimoja kimoja!dah,hii ni zaidi ya utamu
 
Kuna mdau kajitokeza kule jukwaa la Sports and entertainment specifically entertainment ameanza kuweka riwaya ya HOFU
Cc. MAPIKIPIKI pono

Ahsante mkuu,ngoja nijikumbushe hofu,kisha utumwagie KK yaani kikosi cha kisasi,halafu ulee uhondo wa wizi wa almas mwadui(Elungata),mkuu katika novel zote za willy gamba,sijasoma novel moja ya kijasho chembamba,chonde chonde mwenye hiyo novel atumwagie humu,
 
Last edited by a moderator:
NJAMA....
SURA YA NNE
FUNUNU
"Samahani binti tunaomba kumuona Meneja",
nilimwambia mwandishi mahsusi wa Meneja wa
Bandari.
"Sijui nyinyi ni akina nani?", aliuliza msichana huyu
aliyeonekana amechoka choka.
"Mwambie ni Willy Gamba na wateja wake kutoka
gazeti la Afrika".
Meneja wa Bandari tulikuwa tunafahamiana kikazi,
hasa kutokana na shughuli zingine tulizokuwa
tunazifanya katika kampuni yetu ya Afrika
Internation Agencies.
Yule msichana alizungumza na bosi wake kwa
simu, alipomaliza alinyanyuka na kutufungulia
mlango tukaingia ndani. Tulimkuta Issack Mlingi
ambaye ndiye Meneja wa Bandari aliyehusika na
tukio hili akionyesha hali ya kuchoka sana. Nafikiri
hii ilitokana na bughudha alizopata toka kwa polisi
na watu wengine wanaohusika na upelelezi wa
tukio hili. Macho yake yalikuwa mekundu na
yamevimba.
"Karibuni ndani", alisema huku akinyanyuka ili
tusalimiane.
"Samahani ndugu Mlingi, naamini una shughuli
nyingi sana", nilimuomba radhi.
"Si kitu Gamba, karibuni".
"Hawa ni wateja wangu Sherriff na Veronika kutoka
gazeti la Afrika ambalo kampuni yangu ni wakala
wake, na jamani huyu ni Issack Mlingi, Meneja wa
Bandari", walipeana mikono kisha wote tukavuta
viti tukakaa.
"Ndugu Mlingi ni imani yangu kuwa umeisha ulizwa
maswali mengi juu ya tukio hili lililotokea hapa
bandarini. Lakini naamini hatutakuwa
tumekuhangaisha kama tutakuuliza maswali. Kama
nilivyokwisha kwambia hawa waandishi wa gazeti
la Afrika na ni waandishi pekee walioruhusiwa
kuingia hapa nchini kuandika juu ya tukio hili,
naamini unajua msimamo wa gazeti la Afrika. Hata
hivyo tutakuuliza maswali kidogo tu kusudi
tusikuchoshe sana".
"Hebu nipeni vitambulisho vyenu niviangalie",
aliomba.
Sherriff na Veronika walimpa vitambulisho,
akaviangalia na aliporidhika akavirudisha.
"Haya ulizeni maswali yenu, maana ikiendelea hivi
naweza kupata wazimu", alisema huku akitoa
tabasamu la uchovu.
"Tumesoma maelezo yako uliyotoa polisi, ila
tumekuja hapa kukuuliza maswali machache juu ya
mambo ambayo hatukuwa tumeyaelewa vizuri",
alisema Sherriff.
"Ulieleza kuwa ulipata simu kutoka kwa Jones
Mantare ambaye umezoea sana sauti yake, kiasi
kwamba huwezi kuikosea ukiisikia. Lakini jambo la
kushangaza ni kwamba, Mantare anasema hakuwa
amekupigia simu kwani alikuwa na mkutano na
Mwenyekiti wa Kamati na Mwenyekiti amethibitisha
kuwa ni kweli walikuwa wote toka saa tisa hadi saa
kumi na moja. Baada ya kupata maelezo hayo
bado unaweza kusema kuwa sauti ile ni sawa
kabisa na ya Mantare?".
"Kwa sababu wakati ule nilikuwa sina wasiwasi
kuwa kuna jambo baya roho yangu iliridhika kuwa
ni Mantare. Lakini sasa kwa sababu Mantare
anasema hakupiga simu, ndipo nakumbuka kuwa
nilimwuliza kama ana mafua, maana kwa mbali
alikuwa akizungumzia puani, na yeye alijibu kweli
mafua yalikuwa yamemkaba sana. Lakini maelezo
mengine, mathalani ambayo huwa tunataniana na
Jonas, yalikuwa yote sawa. Kusema kweli
inawezekana kabisa alikuwa mtu mwingine
anayemfahamu sana, lazima niseme sana maana
isingekuwa hili jambo la mafua bado ningeendelea
kung'ang'ania alikuwa Jones. Lakini Jones
amekuja hapa hana mafua hata kidogo kwa siku
nyingi".
"Hebu fikiria tena kidogo juu ya sura na sauti au
umbile na tabia ya huyu mtu aliyekuwa akijiita Meja
Paul Liboi, unaweza kuwa na uhakika kabisa kuwa
mtu huyu ni mzalendo wa Tanzania?", Veronika
aliuliza.
Ndugu Mlingi alisita kidogo kujibu swali hili na uso
wake ukakunjamana kidogo. Baada ya kufikiri sana
akasema.
"Nafikiri anaweza asiwe mzalendo".
Wote tukamwangalia.
"Kwanini unafikiri hivyo?", mimi nilimuuliza.
"Wazo hili lilikuwa halijaingia kichwani mwangu,
lakini sasa baada ya kuuliza swali hili inawezekana
mtu huyu asiwe mtanzania maana kwanza
kiswahili chake hakikuwa kimenyooka na alipenda
sana kuchanganya na kiingereza. Mimi nilimfikiria
kuwa huenda ni Mjaruo, lakini alikuwa hajang'oa
meno. Vile vile alikuwa na haraka haraka na
maneno ya mkato mkato. Nikifiri sana hakuna na
ile hali ya kirafiki waliyonayo watanzania wengine
wengi. Lakini kwa sababu nilijuwa ni mwanajeshi
nikafikiri ndio sababu aikuwa na tabia ya namna
hiyo".
"Una jambo jingine ambalo huenda sasa unafikiri
halikuwa lakawaida juu ya tukio lolote baada ya
kujuwa watu hawa walikuwa majahiri?".
"Nafikiri nimeshasema yote, ila tu huenda kitu
kimoja, sijui kama kinahusika ama vipi".
"Ehe, kitu gani".
"Baada ya kuzungumza na huyo anayejiita Jones
Mantare, simu za jengo hili hazikufanya kazi tena.
Tulipowaeleza Posta kesho yake, walikuja mafundi
na kusema waya inayounganisha jengo hili na
waya zinazokwenda Posta ilikuwa imekatika kwa
kuangukiwa na mti. Sasa nilianza kuona picha
kidogo ya tukio hili. Nilijua mara moja kuwa watu
waliokuwa wameshughulikia tukio hili ni watu
wenye kujua ujasusi wa hali ya juu; kwani
walihakikisha kuwa kila hatua wanayoichukua na
nyayo zake wanazifuta ili asiwepo mtu wa
kuzifuatiia".
TUjikuta tumeridhishwa sana na safari yetu ya
bandarini hivyo tukaona tuondoke.
"Asante sana ndugu Mlingi, kama tukihitaji mambo
zaidi tutakuona tena, na kama utakumbuka kitu
cochote kinachoweza kutusaidia nipigie simu.
Nafikiri simu yangu unayo?", nilimuuliza.
"Ndio ninayo", alijibu.
"Na tahadhali usizungumze ovyo juu ya tukio hili,
maana si tukio zuri", nilimwonya.
"Bila shaka nitajitahidi".
Tuliagana nae, tukaondoka kuelekea mjini.
Nilijaribu nilivyoweza kuangalia kama naweza
kumwona Eddy na mwenzake, lakini wapi hakika
vijana walikuwa wanafanya kazi nzuri sana, maana
kama mimi Willy sikuweza kuwatambua basi
hakuna mtu mwingine tena, si kama najisifu ila huo
ndio ukweli, mtu akitaka kunitafuta mimi basi
ajiweke sawa, la sivyo shauri lake.
"Kamara kama ulivyomjua alikuwa mtu wa namna
gani, unafiri anaweza kwa njia yoyote akawa
kajiingiza katika jambo hili?", nilimuuliza Sherriff
huku tukiwa tumesimama kungojea kuingia
barabara ya site drive, tukutokea bandarini.
"Mimi nakuhakikishia komredi kuwa Kamara
alikuwa hawezi kufanya jambo kama hilo, ni lazima
tu iko namna ambayo alishambuliwa na
kunyang'anywa karatasi hizo, alinihakikishia
Sherriff.
"Oke, naona sasa twende kwenye ofisi ya kamati
ya Ukombozi ya OAU", nilimweleza huku nageuza
gari kuingia site drive na kuelekea kwenye ofisi ya
kamati.
Tulipofika kwenye mapokezi ya ofisi hii ya kamati
na kumkuta msichana mmoja akizungumza kwenye
simu, ikatubidi tumsubiri kidogo amalize
kuzungumza, niliangalia saa yangu ilikuwa yapata
saa sita na dakika tano.
"Samani jamani, sijui niwasaidie nini", msichana
alituuliza.
"Bila samahani binti, sisi tunaomba kumwona
Jones Mantare", nilijibu.
"Mna ahadi naye?", binti aliuliza.
"Hapa, lakini nafikiri ukimwambia Willy Gamba wa
AIA na wageni toka gazeti la Afrika, ambao
wanataka kumwona, anaweza kutuona",
nilimweleza.
"Msubiri basi", huyo msichana alijibu kisha akainua
simu na kuanza kuzungumza na ofisi ya Mantare.
Jones Mantare alikuwa ananifahamu, maana
nilikuwa nimehakikisha kuwa nafahamiana karibu
na kila mtu katika ofisi hii ya kamati, yeye alikuwa
akinifahamu kama mfanyabiashara, maana ndivyo
nilivyojulishwa kwake. Tokea hapo tulikuwa
tunaonana mara kwa mara sehemu za starehe na
kujenga uelewano wa kutosha, hivyo nilihisi kuwa
asingeweza kunikatalia nisimuone, ingawa nilijuwa
atakuwa katika hali isiyokuwa ya kawaida. Baada
ya kuzungumza kwa muda kwenye simu msichana
alitwambia.
"Mnaweza kwenda kumwona, ofisi yake ipo mwisho
wa ujia mkono wa kulia".
"Asante sana binti", nilimjibu.
Tulimwacha tukaelekea alikotuelekeza. Tulibisha
mlango pale tulipokuwa tumeelekezwa.
"Karibu", tulisikia sauti ya msichana ikitoka ndani.
Nilifungua mlango tukaingia na tujikuta katika ofisi
kubwa ya mwandishi mahsusi wa Mantare.
"Habari zako bibie", nilimsalimia kwa niaba ya
mwenzangu.
"Nzuri, ni Gamba na wenzake nafikiri?", aliuliza.
"Hasa", nilijibu.
"Ingieni moja kwa moja anawasubiri", alisema huku
akisimama na kutufungulia mlango wa bosi wake.
Tulipoingia tu Mantare alisimama.
"Ahaa ndugu Willy, karibuni".
"Asante, asante Jones".
"Nafikiri niwajulishe, huyu ni ndugu Jones Mantare,
ofisa katika kamati hii ya ukombozi, na hawa ni
komredi Ahmedi Sherriff na komredi Veronika
Amadu. Ni waandishi wa habari wa gazeti la
"AFRIKA".
Walipeana mikono kwa mara nyingine.
"Ehe, mlitaka kuniona, sijui niwasaidie nini?",
aliuliza.
"Hawa makomredi ni wateja wangu, kampuni yangu
ndio wakala wa gazeti la Afrika hapa nchini. Hasa
kitu kilichotueta hapa ni kutokana na tukio hili la
juzi. Nafikiri unaelewa msimamo wa gazeti la Afrika
katika ukombozi, na kutokana na msimamo huo
wameiomba serikali kama wanaweza kuandika
habari za kuaminika juu ya tukio hili. Ni wasiwasi
wao kuwa magazeti mengi ya kibeberu yataandika
habari za kupotosha, na wao wako hapa ili waweze
kueleza jumuia ya ulimwengu ukweli mtupu. Kwa
hiyo tutashukuru sana ukiweza kutusaidia katika
kujibu maswali machache. Hatutataka kupoteza
muda wako kutueleza mengi, maana nakala ya
maelezo yako tumeipata toka polisi. Hivi ni nia
yetu uweze kutufafanulia katika sehemu ambazo
hazieleweki katika tukio hili".
Niliona kule kutaja nakala ya maelezo yake kutoka
polisi kulimtoa wasiwasi aliokuwa ameuonyesha
usoni mwake. Niliona macho ya Veronika yakiwaka
kuonyesha kuwa nilivyoeleza nimeeleza vizuri sana
na Sherriff alitingisha kichwa kuonyesha kuwa
niliyoyasema ni sawa kabisa.
"Sawa ndugu Willy, nitakuwa tayari kuwajibu
mwaswali yenu, kusema kweli kama ulivyosema,
radio za kibeberu zimekwisha tangaza uongo ili
kuridhisha maslahi yao. Kwa jinsi hii tutakuwa
radhi kuona ukweli unaandikwa na gazeti hili. Haya
sijui mna maswali gani?".
"Inasemekana kuwa hayati Kamara Franki ndiye
alikuwa anashughulikia suala hili la silaha. Na
amekutwa ameuawa. Nafikiria hizi karatasi
zilitokatokaje mikononi mwa marehemu na kuingia
mikononi mwa hawa majahiri?. Maana kutokana na
maelezo ya Polisi ofisi yenu hii haikuvunjwa mahali
popote", Sherriff aliuliza.
"Sawa kabisa?, kutokana na maelezo ya mwandishi
mahsusi wa marehemu, anasema ya kwamba?,
wakati marehemu anatoka ofisini alimweleza aweke
zile karatasi za kuchukulia silaha ndani ya mkoba
wake, kwa sababu alikuwa anategemea kwenda
kwenye kikosi cha Jeshi kinachoshughulikia silaha
za wapigania uhuru kesho yake, kabla hajaja
ofisini. Kwa hiyo, jibu kwa swali lako ni kwamba
watu hawa walimnyang'anya marehemu karatasi
hizo na ndio sababu wamemuua."
"Watu hawa unafikiri walijuajuaje kuwa marehemu
atakuwa na karatasi hizi ndani ya mkoba wake?",
Veronika aliuliza.
"Hapo ndipo hata sisi tumekwama".
"Huyu mwandishi mahsusi wa marehemu yupo",
nilimuuliza.
"Ndio yupo".
"Unaweza kumwita tukazungumza nae kidogo?".
"Hali yake si nzuri sana, bado ana mshituko kwa
ajili ya marehemu. Unajua mnapofanya kazi kwa
uhusiano ulio karibu na mtu mnakuwa na urafiki wa
hali ya juu sana. Hata hivyo nitajaribu kuwaitieni".
Alishika simu na kuzungumza na mwandishi wake.
Wakati tukimsubiri Veronika alimuuliza tena. "Ofisa
wa kule bandarini Ndugu Mlingi anasema mtu
aliyempigia simu alikuwa na sauti kama yako,
mathalani mambo mnayotaniana yalikuwa vile vile,
unaweza kufikiri mtu yeyote hapa ofisini au hata
nje anayeweza kuigiza sauti yako kiasi hicho?".
"Ni imani yangu kuwa mtu kukuigiza kiasi hicho
lazima awe mtu aliyekuzoea, na mtu aliyekusikia
ukizungumza mara kwa mara, hasa na huyu ndugu
Mlingi".
"Kuesema kweli, nimefikiria kweli juu ya mtu huyu
mpaka nimechoka, nitazidi kumfikiria kama wazo
likinijia nitakupigia simu."
Mara mlango ulifunguliwa akaingia msichana mrefu
mwembamba mwenye nywele nyingi. Kama
unapenda wasichana warefu na wembamba, basi
hapa pana msichana wa namna hiyo, jina lake
Margreth. Ni mzuri kiasi chake.
"Karibu Margreth", Mantare alimkaribisha, wote
tukasimama akatujulisha kwake. Mwandishi
mahsusi alileta kiti kingine na Margreth akaketi.
"Samahani Margreth", hawa ndugu wana maswali
kidogo ya kukuuliza," Mantare alimwambia.
Margreth hakujibu kiti bali alituangalia tu.
"Samahani sana binti, sisi wote yunaelewa hali
uliyonayo, ila imetubidi tukuone tuweze
kuzungumza nawe huenda utatusaidia kutatua huu
mkasa uliompata bosi wako", nilimwelezea.
"Niko tayari kuwaelezea chochote kama kitasidia
kuwapata watu waliomuua bosi wangu." Magreth
alijibu huku machozi yakimlengalenga.
"Jaribu kukumbuka, nilimwambia, "wakati
marehemu anakueleza uweke zile karatasi za
kuchukulia silaha kulikuwa na mtu mwingine
yeyote?".
Alikaa kimya kwa muda kisha akajibu, "Hapana",
harafu kama amegutuka akasema, "Ndio
nakumbuka sasa, alikuwepo tarishi wetu wa hapa
ofisini".
Nikasikia kengere ya tahadhari inalia kichwani
mwangu. Wote tulitazamana.
"Tarishi huyu yuko hapa?", niliuliza.
"Hapana, ni mgonjwa anaumwa na ameandikiwa
kulala siku tano', Margreth alijibu.
"Toka lini?".
"Toka tarehe nne".
"Yaani siku ambayo ilibainika kuwa silaha
zimeibiwa na bosi wako ameuawa?".
"Ndio".
"Yaani atakuwa kazini tarehe tisa".
"Ndio".
"Una uhakika kabisa alikuwepo?".
"Ndio".
Habari kama hizi mimi ndizo huwa zinanitibua,
maana wakati kifo kinatokea haafu kinatokea kitu
kingine chenye uhusiano wa karibu namna hii, basi
hapo ndipo huwa naanza kujumulisha moja kwa
moja na kupata mbili.
Nilimgeukia Mantare na kumwuliza, "Huyu tarishi
ndiye alikuwa tarishi wa ofisi nzima?".
"Ndio'.
"Anaitwa nani?".
"Anaitwa George Kiki".
"Mmekuwa naye muda gari?".
"Yapata miezi sita sasa".
"Ni MTANZANIA!".
"Hapana ni mkimbizi kutoka Afrika Kusini, aliletwa
kwenye ofisi yetu na chama cha wapigania uhuru
cha Afrika Kusini kilichopo hapa mjini cha SANP. Ili
tumsaidie. Alipokuja hapa alitupa maelezo yake na
kuonekana ni kati ya vijana walioanzisha
maandamano ya kitongoji cha Soweto huko Afrika
Kusini. Alieleza kuwa yeye alipata mwanya wa
kutoroka gerezani ndipo akakimbia na kuweza
kufika hapa baada ya safari ndefu ya taabu. Kwa
vile alikuwa hana kisomo cha kutosha jinsi yeye
alivyojieleza tuliamua kumpa kazi ya utarishi ili
kumsaidia. Kusema kweli amekuwa kijana mwenye
bidii sana, na anapendwa na kila mfanyakazi wa
hapa, hasa kwa nidhamu yake, na utekelezaji wa
kazi yake".
"Kwa hivi alikuwa na fursa ya kuingia ndani ya ofisi
ya mtu yeyote wakati waowote ili kuchukua mafaili
na mambo kama hayo?".
"Hasa ndivyo ilivyokuwa".
"Anaishi wapi?".
"Anaishi huko Kinondoni sehemu za Hananasifu
Estate katika nyumba za shirika la nyumba".
"Nyumba yenyewe unaijuwa?".
"Mimi nimewahi kufika kwake; tumewahi
kumpeleka na marehemu", alisema Margret huku
tena machozi yakimlengalenga.
"Samahani Mantare, sijui unaweza kumruhusu
Margret akatuelekeza kwa Ndugu Kiki?".
"Bila wasiwasi mnaweza kwenda nae".
Niliwaangalia wenzangu nikaona wameridhika na
maswali na majibu ya hapa, hivyo kwa niaba yao
nikamshukuru ndugu Mantare.
"Ikiwa tutahitaji jambo lolote tutarudi tena au
tutapiga simu. Na wewe ukipata jambo lolote
usisite kutufahamisha".
"Hamna tabu, nitafurahi kuwasaidia".
Tuliagana tukaondoka kuelekea Kinondoni.
ITAENDEEA....
NJAMA
SURA YA NNE
FUNUNU III
"Mimi naona tukapate chakula cha mchana
kwanza", Sherriff alishauri.
"Sawa", walijibu kwa pamoja. Sherriff alikaa nyuma
pamoja na Margret na wakati huo mimi naendesha
nikiwa katika mafikara mengi, Sherriff alichukua
jukumu la kumtuliza Margret akimweleza mambo
mengi juu ya matatizo ya binadamu na kumwambia
kuwa asihuzunike sana maana ndiyo binadamu.
Kadiri Sherriff alivyozidi kusema ndivyo Margret uso
wake ulizidi kutokwa na huzuni kwani mimi
nilikuwa nawaangalia katika kioo cha kuendeshea.
Hata Sherriff alipofika kusema yeye huwa anaamini
kuwa kwa kila linalotendeka linatendeka kwa ajili
ya uzuri, nilimwona Margret anamwemwesa kwa
mara ya kwanza, na ndipo sura yake ilionyesha
uzuri aliokuwa nao. Niliona hata Sherriff aligundua
uzuri huo, kwani uso wake ulibadilika kiasi cha
kwamba moyo wake uliguswa.
Tulifika New Afrika Hoteli, nikaegesha gari wote
tukatoka nje. Basi, moja kwa moja tulifuliza
kwenda kwenye lifti ya kutupeleka orofa ya kwanza
ambapo ndipo Bandari Grill ilipo. Mbele yangu
nilimwona Eddy anavuka sehemu ya mapokezi,
halafu akazungusha kichwa akaingia kwenye choo
kilichopo hapa chini. Hii ilikuwa ishara kuwa alitaka
kuniona.
"Samahani jamani nasikia nimebanwa haja ndogo,
tangulieni nakuja sasa hivi. Margret, we ndiye
mwenyeji washughulikie wagaeni".
"Bila wasiwasi", alijibu akiwa anaanza kupona
kutoka katika mshituko alioupata.
Niliingia maliwatoni nikamkuta Eddy ananisubiri.
"Mpaka dakika hii hakuna chochote", aliniambia
bila kuniangalia.
"Sawa, nendeni mkale halafu nenda ofisini
nitakukuta huko kiasi cha saa kumi hivi".
"Oke", alisema huku akielekea kwenye mlango wa
kutokea.
Mimi nilimaliZa haja yangu ya uongo na kweli
nikaondoka kujiunga na wenzangu. Tulipata muro
safi sana hapa Bandari Grill, na kwa sababu kila
mtu alikuwa na njaa tulikula kimya kimya.
"Nasikia kichwa kinaniuma", Veronika alilalamika.
"Nafikiri kwa ajili ya hali ya hewa. Joto jingi sana
kuliko ulilozoea", nilimjibu.
"Kama ni hivyo afadhali ukameze dawa upumzike,
sisi tutakwenda kumwona Kiki halafu tutakuja
kukuona", Sherriff alishauri.
"Naona hivyo ni sawa", alijibu.
Basi tulikubaliana Veronika apumzike sisi tuendelee
na shughuli. Tuliondoka New Afrika na
kumtelemsha Veronika Kilimanajaro.
"Vero mpenzi, kuna gari lile pale unaweza kulitumia
wakati wowote. swichi iko chini ya zulia",
nilimuonyesha gari ambalo Eddy alikuwa ameliacha
hapo. Sisi tuliondoka na kuendelea na safari yetu
ya Kinondoni.
"Twende kupitia barabara ya Upanga moja kwa
moja, halafu tukivuka Salendar briji mbele kuna
barabara ya Kinondoni hivyo tutaingia kushoto.
Sehemu iko mbele ya makaburi. Baada ya
makaburi kuna barabara la vumbi, linakatisha
barabara hii. Tukiacha hilo na kuendelea mbele
tukakuta barabara nyingine ya vumbi inaingia
kushoto na kuna kibao kimeandikwa Bamboo Baa
and Restauranti, basi hapo ndipo tutakapoingia",
alieleza Margret kwa ufasaha kabisa.
Mimi hupenda maelezo ya namna hii, siyo mtu
amefika mahali pa kukata kona ndipo anasema,
kata hapa kushoto. Maelekezo hayo ni ya kihuni na
ndiyo anayosababisha ajali nyingi.
Nilifuata maelezo ya Margret vizuri kabisa,
nilipotaka kuingia kushoto pale kwenye bao la
tangazo la Bamboo Baa and Restauranti, Margret
alisema, 'Njia hapa si nzuri twende pole pole,
halafu mbele kidogo utakata kushoto tena tuelekee
kwenye nyumba hizo pale", alinielekeza na
kuonyesha kwa kidole.
Niliendesha pole pole nikaikuta njia na kuifuata
kuelekea kwenye nyumba hizi za shirika la nyumba.
"Baada ya nyumba hiyo yenye bendera ya CCM,
ambayo ndiyo ya mjumbe, ya pili yake".
"Hapa?".
"Ndio, mlango huu huu".
Nyumba hizi zinakaa familia mbili mbili, lakini
zimetengwa katikati kiasi kwamba kila familia ina
sehemu yake kamili. Tulitoka ndani ya gari,
Margret akatangulia na kibisha hodi. Lakini
hatukupata jibu. Nilisikia moyo wangu unapiga
haraka haraka, hii ni sirika niliyozaliwa nayo, na
ilikuwa ni ishara kuwa kuna hatari.
"Hebu ngoja Margret", nilimwambia nikimrudisha
nyuma.
Niliujaribu mlango ukafunguka nikamwita Sherriff
na kumwambia hakuna mtu, tulifungua mlango
mwingine uliokuwa unaelekea jikoni, bafuni na
chumba cha kulala. Tukiwa wote na wasiwasi
tukibisha hodi kwenye mlango wa chumba cha
kulala. Lakini hatukupata jibu. Nilitoa Bastola
yangu, na kusukuma mlango wazi.
Tulimkuta mtu ambaye tuliamini ni Kiki
amechomwa kisu kifuani!, nilipomshika nikajua
alikuwa amekwisha kufa saa nyingi sana. Kisu
kilikuwa kimeachwa pale kifuani. Kilikuwa kisu
kikubwa na mpini wake mwekundu. Tulimwita
Margret aje atuhakikishie.
Akiwa anatetemeka kwa woga alikuja na kusema,
"Ndiye yeye masikini", akaanza kulia tena
tulimbembeleza na kumvuta na kuondoka haraka
haraka ndani ya nyumba hiyo. Tuliingia katika gari
langu na kuelekea mjini. Sasa nilianza kuongeza
hesabu kwamba mbili na mbili na kupata nne. Na
vile vile majahiri hawa walianza kunitisha kwani
mbinu zao zilikuwa kubwa. Lakini hata hivyo mbinu
za Willy ni kubwa zaidi.
"Mapambano yameanza Sherriff", nilisema kwa
sauti ambayo sikuamini ilikuwa yangu.
"Na kweli yameanza", Sherriff alijibu.
Wakati huo tulikuwa tumesimama kwenye taa za
usalama barabarani za salendar briji tukuelekea
New Afrika. Saa yangu ilisema ni saa kumi na
dakika mbili.
"Naona mimi mnifikishe nyumbani", Margret
aliomba.
"Unakaa wapi".
"Ninakaa kwenye orofa pale nyuma ya Rex Hoteli".
"Nazijua orofa hizo, uko orofa ya ngapi, maana
tunaweza kukuhitaji ama kikazi ama katika hali ya
kustarehe, unasemaje?".
"Karibu mimi niko orofa ya pili chumba namba
kumi na nane. Simu yangu ni 22221".
Basi wakati huo tulikuwa tumefika Posta ya
Azikiwe, tulipofika kwenye sanamu ya Bisimini,
tukaingia Independent Evenue.
"Unajua", Margret alitugutusha.
"Ehee", nilijibu na kumwangalia ndani ya kioo cha
kuendeshea, maana yeye alikuwa amekaa nyuma.
"Sijui ni mafikara yangu, ila tu limekuja kama wazo
la kunishangaza, maana baada ya kutokea mambo
haya kila kitu nakiona si cha kawaida
kinanigutusha".
"Nini kimekugutuusha?", Sherriff aliuliza akionesha
msisimko.
"Unajua pale kwenye lango la kuingia ndani ya ofisi
yetu kumekuwa na mwendawazimu ambaye
amekaa pale zaidi ya mwezi mzima. Amekuwa
amevaa matambalatambala tu na amebeba
makopo mengi, sijui mmemuona?".
"Mimi nilimwona", Sherriff alijibu.
"Mimi sikumwona".
"Polisi walikuja kumchukua siku moja, na
kumpeleka kunakohusika lakini hazikupita saa tatu
akarudi. Alikuwa hatoki pale hata dakika moja,
usiku na mchana kutokana na walinzi wa usiku
wanavyosema. Leo mlipokuja alikuwepo maana
mimi niliona gari lenu linaingia wakati natoka
kunywa chai. Gari lenu lilipoingia na yeye alivuka
lango akaingia ndani. Hii ni kawaida yake, kwani
huwa anaombaomba kwa kila mgeni anayefika pale
ofisini na ndio sababu aliitiwa polisi kwa sababu
anawafadhaisha wageni wetu. Gari lenu mliliegesha
mbele kabisa ya mlango wa kuingia mapokezi na
kutoka ndani ya gari haraka hivyo hakuwahi. Mimi
nilipoingia pale mapokezi nilikuta nyinyi
mmekwisha kwenda ofisini kwa Mantare ila
nilimkuta yule kichaa anamuuliza yule msichana
wa mapokezi. Hawa watu wanasema wanatoka
katika gazeti la Afrika. Yule msichana wa mapokezi
alikasirika na kumfokea, Toka hapa! kama
wanatoka gazeti la Afrika watakufaa nini wewe?,
wana kazi ya maana kuliko kuonana na
mwendawazimu kama wewe. Toka!".
"Kitu cha kushangaza ni kwamba wakati
tunaondoka pale ofisini kwetu nakumbuka
sikumuona wala makopo yake na kilago chake
hakikuwepo, sijui jambo hili lina maana yoyote au
mnaonaje nyinyi wenyewe?", alimalizia Margret.
"Unasema alikuja hajawahi kutoka pale hata dakika
moja, ila tu siku ile aliyochukuliwa na polisi kwa
muda wa masaa matatu?", nilimuuliza.
"Nina uhakika kabisa maana mimi damu yangu
ilikuwa haipatani na yule mtu kabisa, na ni mimi
niliyefanya kampeni ya kumuitia polisi lakini
aliporudi alionekana kuwa maafisa wote walidharau
kumchukulia hatua tena".
"Ukimwangalia alikuwa anaonekana kichaa au
unafikiri anajifanya tu?", nilimuuliza.
"Kitu kilichonikosanisha naye ni kwa sababu siku
moja aliniambia yeye si kichaa ila anajifanya tu ili
kujipatia pesa bila jasho. maana ilikuwa
ukimwangalia sana wakati yeye hana habari
anakuwa kama si mtu kichaa, ila huwa anapoona
watu anakuwa kichaa kabisa".
"Asante sana, kumbuka jambo hili linaweza likawa
na msingi tutaliangalia".
"Asante".
Niliegesha gari mbele ya Rex Hoteli.
"Wakati wowote tutegemee", nilimweleza huku
akitelemka.
"Mnakaribishwa", akiwa zaidi anamwangalia
Sherriff. Sherriff alitoa mkono wake wakapeana
mikono. Tayari kulikuwa na kitu kinapita kati yao,
maana nyuso zilikuwa wakati wanapeana mikono,
mimi ndiye najua, maana hata mimi hali hii
inanitokea. Walikuwa wameanguka katika penzi.
"Mimi naona turudi pale ofisi ya kamati
tukahakikishe kama kweli hayupo pale yule kichaa",
nikimwambia Sherriff.
"Sawa".
Tulikwenda kimya kimya kila mtu akichambua
mambo, tuliyokuwa tumeyapata na kuyaona,
tulipofika pale ofisini tulimkuta mlinzi wa jioni
anayeingia kazini saa tisa wanapofunga kazi mpaka
saa kumi na mbili asubuhi, ilionekana alikuwa
anafanyakazi masaa mengi sana, lakini yeye
alipenda kazi yake na kuridhika na kipato
alichokuwa anakipata, baada ya kutusalimia na
kutueleza hizo saa zake za kazi, nilimuuliza.
"Unajua kulikuwa na mzee mmoja kichaa hapa sijui
amehamia wapi?'.
"Hata mimi nashangaa, kichaa huyu alikuwa hatoki
hapa hata dakika moja. Hata haja zake alikuwa
akiifanya hapa hapa karibu. Polisi walimchukua
hapa akawachenga akarudi mwishowe
wakamwachia akae tu. sasa leo nafika nakuta
kiisha ondoka na wala harufu yake hakuna.
Nimeshangaa sana. Amekaa karibu mwezi mzima".
"Ulikuwa unapata fursa ya kuzungumza nae?".
"Si mara nyingi, ila tu siku moja nilikuja
na ..........akasita kusema.
"Sema tu usiogope, hata kama ni siri, sisi
tutakufichia".
"Lakini nyinyi ni akina nani?".
"Sisi tunashughulikia wagonjwa wa akili, tumepata
habari toka polisi kuwa kuna mwendawazimu hapa,
hivyo unaweza kutueleza tabia yake ili tuweze
kumtafuta. Kwa hiyo usisite kutueleza",
nilidanganya.
Baada ya kutafakari mambo haya aliendelea, "Siku
moja kulikuwa na tafrija hapa ofisini jioni. Mimi
niliweza kwa mbinu zangu kujipatia mzinga mzima
wa whiski aina ya 'Dimple' nikauficha wagaeni
wote walipoondoka, nilitoka nje ya lango na kuanza
kunywa huu mzinga wa whiski. yeye alipoona
ninakunywa hii whiski alikuja na kopo lake
akaniomba kwa vile nilikuwa najuwa siwezi
kumaliza chupa nzima nilimgawia nusu basi
alikunywa ile pombe kama maji. Basi ilipomkolea
akaanza kuzungumza Kiingereza ila mara kwa
mara alisema neno sijui 'Sazafrika' neno hili
alilirudia mara nyingi. Na nyinyi mnajua vichaa
mimi niliachana nae nikaendelea na shughuli zangu.
Sasa sielewi kama kilikuwa Kiingereza sawa sawa.
Lakini kitu kilichonivutia ni kule kutamka hicho
Kiingereza chake kama mzungu. Lakini husema
kichaa ana mashetani saba, anaweza kuzungumza
lugha saba tofauti."
"Asante sana, na samahani sana kwa
kukubugudhi", Sherriff alitoa mfukoni shilingi
arobaini akampa. Yule Mzee alifurahi sana.
"Mungu awaongezee wanangu".
Tuliingia ndani ya gari tukaondoka zetu.
"Unaona mambo yalivyo Sherriff?, hii inaonyesha
wazi kuwa George Kiki alikuwa ni jasusi
aliyepachikwa hapa na mabeberu na wakafanikiwa.
Mimi simulaumu mtu yeyote, hata mimi huenda
ningemsaidia kupata kazi. Baada ya mabeberu
kujua mkataba wa silaha kati ya PLF na Urusi
miezi sita iliyopita walichukua hatua ya kuhakikisha
hizo silaha haziwafikii wapigania uhuru wa PLF
maana inasemekana ni silaha za kisasa kabisa.
Tutakapoonana na kiongozi wa PLF atatueleza
zaidi, kuajiliwa kwa kiki miezi sita iliyopita
kunaoana kabisa na nyakati za mkataba huo.
Inaonekana kazi ya jasusi huyo ni kujua mambo
yote yanayotendeka juu ya huo ili mwishowe aweze
kuiba hizo karatasi za kuchukulia silaha, jambo hili
amefanikiwa", nilinyamazi kidogo.
"Kwanini wamwue?", Sherriff aliuliza.
"Kwa sababu hawakuwa na haja nae tena, asije
akashikwa na kutoa siri. Hii inanionyesha jinsi watu
hawa walivyo wajuzi katika kazi yao, hawataki
kufanya makosa".
Wakati huu tukizungumza tulikuwa tukielekea mjini.
"Juu ya huyu kichaa unasemaje?".
"Huyu kichaa nae ni jasusi. Ninavyoona mimi huyu
aliwekwa pale ofisini kusudi aweze kuona nini
kitatokea hapo ofisini baada ya silaha kuibwa.
Aliwekwa mwezi mmoja ili kuondoa mashaka.
Hivyo alikuwa anangoja kuona baada ya polisi na
maofisa wa usalama ni nani mwingine aliyekuwa
na dukuduku juu ya jambo hili. Aliposikia waandishi
wa habari wa gazeti la Afrika nao wamejiingiza
akawa amemaliza kazi, akaondoka kwenda
kupeleka ujumbe, ni wazi kabisa wao walijuwa
polisi na maofisa wa usalama watalishughulikia
jambo hili na ninafikiri walishapima uzito na kuona
wanaweza kukabiliana nao. Hivyo walingoja wajue
kama kuna kundi jingine litakalojiingiza katika
katika upelelezi wa tukio hili. Sasa wamejua; kwa
hivyo waandishi wa gazeti lazima muwe macho.
Tokea sasa kaeni katika tahadhari; lolote linaweza
kutokea. Unaonaje maoni yangu?'.
"Lo Willy, ndio maana wewe ni mpelelezi maarufu
katika Afrika. Maelezo yako yanaeleza hali halisi
kabisa. Na swali ulilomuuliza Margret kama kuna
mtu mwingine aliyeweza kuona akiweka karatasi
ndani ya mkoba, mimi nilikuwa silifikilii kabisa na
ndilo swali lililotupa mwanga. Kweli kila mtu na
kazi yake", alisifu Sherriff.
"Lakini maswali mliyouliza ninyi vile vile ni ya
maana sana, nafikiri kuliko waliyoulizwa na Polisi.
Sidhani Polisi wameishafikia hii tuliyofikia kwa
muda huu mfupi".
Mara wazo likanijia.
"Lile jambo lililokuwa linakutatanisha nimepata jibu
lake. Swali la nani aliyepiga simu kwa Mlingi akiiga
sauti ya Mantare na maneno ya Mantare aliyozoea
kuzungumza na Mlingi".
"George kiki", alijibu Sharriff.
"Kabisa, unajuwa Kiki alikuwa anaingia ndani ya
kila ofisi ya ofisa akiwa kama tarishi. Swali hili
nilimuuliza Mantare akakubali. Hivyo Kiki akiwa
jasusi aliyefundishwa, ninavyofikilia, haikuwa kazi
kumsiliza Mantare katika simu zake nyingi na
ninafikiri alifanya kila njia kusikiliza simu kati ya
Mantare na Mlingi. Hii inaonekana wazi kabisa".
"Lo tunaanza kuona mwanga sasa", Sherriff
alisema.
"Kweli tumeona mwanga, lakini ni mwanga
unaotufikisha kwenye giza nene. Maana Kiki
ambaye angetupa fununu ya watu hawa amekufa,
yule kichaa lazima ameshapotea hewani, gtumerudi
pale pale".
"Watu hawa ni akina nani na silaha hizi ziko
wapi?", niliuliza swali hili wakati naegesha gari
New Afrika.
"Hilo ndio swali gumu lakini afadhali tunajua Afrika
Kusini inahusika, maana Kiki katokea huko. Na yule
kichaa alipolewa alizungumzia Sozafrika ambayo
nasadiki ni South Afrika".
"Sawa kabisa, lazima tujuwe tunapambana na
South Afrika na haikosi shirika lao la ujasusi
'BOSS', linasaidiwa na mashirika mengine ya
ujasusi ya nchi za kibeberu. Hivyo tutakuwa na
kazi ngumu maana watu hawa nimewahi
kupambana nao ni watu hatari kabisa".
"Tumwombe Mungu atasaidia".
"Na wewe ukijisaidia", nilijibu.
Wote tukacheka na kutoka ndani ya gari. Ilikuwa
saa kumi na moja. Hivyo kabla hatujavuka
barabara nilionelea nifike ofisini kidogo halafu
niende nyumbani.
"Sherriff mimi nafika nyumbani kidogo, nitakuona
saa kumi na mbili kamili".
"Sawa nitakusubiri hapa duka la kahawa".
oke basi saa kumi na mbili".
Niliingia ndani ya gari na kuondoka. Nilipofika
ofisini nilimkuta Eddy na vijana wengine. Linda
alikuwa ameshaondoka.
"Eddy kuna mtu mmoja anaitwa George Kiki,
alikuwa akifanyakazi kwenye ofisi ya Kamati ya
ukombozi kama tarishi?, hapa aliingia kama
mkimbizi baada ya kutoroka Afrika Kusini. Alifika
ofisi za chama cha SANP, ambao walimpeleka
kwenye Kamati ya Ukombozi waweze kumsaidia
angalau kazi yoyote. Inawezekana hana kisomo cha
kutosha. Nataka ukague habari hii kwa kutumia njia
zetu za kawaida. Unaweza kuwajulisha makomredi
wetu kule Soweto, nadhani watakuwa na maelezo
kamili. Habari hizi nazitaka haraka. Kila kitu,
aliingiaje hapa alikwendaje kwenye ofisi za SANP
alikuwa anaishi namna gani, nani walikuwa rafiki
zake nk. wewe unajua".
Eddy aliyekuwa anachuku maelezo haya alijibu.
"Atashughulikiwa bosi, usiwe na wasiwasi".
"Chifu yuko?".
"Kaondoka".
"Haya asante, usitoke mpaka nitakapokujulisha
tena".
"Mimi nipo".
Ndio sababu nilimpenda mtoto huyu. Nidhamu yake
kwangu ilizidi ya mdogo wangu ambaye tumetoka
ndani ya tumbo la Mama Willy. Niliingia ndani ya
gari nikaelekea zangu Upanga.
Niliposimamisha gari mbele ya mlango, moja kwa
moja macho yangu macho yangu yakaangukia
kwenye kitu kilichokuwa kwenye ubao wa juu ya
mlango mkubwa wa kutokea nje. Nilitoka nje ya
gari haraka haraka nikiwa tayari kwa mapambano.
Nilikuta ni kisu chenye mpini mwekundu kama kile
tulichokikuta kwenye kifua cha maiti Kiki; ncha
yake ilitumiwa kama kipini cha kubandika kipande
cha karatasi pale mlangoni.
Niliking'oa nikachukua karatasi na kusoma
yaliyobandikwa hapo yalisema.
Willy Gamba, kama unathamini maisha yako
achana na hao watu wa gazeti la Afrika. na kama
ni rafiki zako waambie waondoke hapa mjini
tunawapa mpaka saa kumi na mbili jioni wawe
uwanja wa ndege. Vinginevyo yaliyompata Kamara
Frank yatawapata na nyinyi. Hili ni onyo kali na si
mchezo. Shughulika na mambo yako usishughulike
na mambo ya watu wengine. Wapo wenyewe
wanaohusika waachie. Nasema tena saa kumi na
mbili jioni leo wawe uwanja wa ndege na wewe
baada ya kuwafikishia habari hizi tusikuone
unashughulika zaidi ya kazi yako ya kawaida ya
AIA Subiani.
Kwanza nilicheka maana niliona kazi sasa inaanza.
Hii inaonyesha upelelezi wetu ulikuwa umewashitua
kuliko wa Polisi. Nilijua yule kichaa alifanya kazi
yake vizuri sana, maana ni yeye tu
aliyetufahamisha kwa majahiri wenzake. Hiki kisu
chenye mpini mwekundu ilimaanisha damu. Nami
niljua damu imeanza kunuka.
Nilifungua mlango nikaingia ndani, nikakoga haraka
haraka kisha nikabadilisha nguo nilifungua sanduku
langu la silaha na kuchukua bastola zingine mbili
kwa madhumuni ya kuwapa Sharriff na Verokika
kwani hakukuwa na mchezo tena, maana upatapo
onyo toka kwa watu kama hawa huwa hawatanii.
Kisha niliinua simu na kupiga kituo cha Polisi cha
Salendar Bridge.
"Hallo kituo cha Polisi hapa".
"Sikiliza, nenda Kinondoni Hananasifu, Estate
kwenye nyumba ndogo ndogo za shirika la Nyumba
nambari IIC utakuta kuna maiti ambayo ina zaidi
ya masaa ishirini na nne", kabla hajatamka neno
nilikata simu. Niliangalia saa yangu muda ulikuwa
umekimbia na ilikuwa saa kumi na mbili kamili.
Niliingia ndani ya gari nikakimbilia New Afrika.
Nilipoingia duka la kahawa sikumwona Sherriff
nikapata wasiwasi. Nikaenda mapokezi kuuliza
wakaniambia aliacha habari kuwa amekwenda
dukani mara moja nimsubiri. Nilirudi nikasimama
nje pale magari yanapoleta watu New Afrika
yanapozungukia. Niliangaza huku na huku na mara
nikamwona Sharriff anakuja akiwa anavuka tawi la
Benki ya nyumba. ghafla alipokuwa anataka kuvuka
barabara ilitokea gari sijui wapi ikapiga breki,
wakatoka watu wawili haraka kama umeme,
wakamvuta Sharriff ndani ya kiti cha nyuma cha
gari, na gari hilo likaondoka tena kama umeme.
Kitendo hiki hakikuchukua hata nukta tano.
Watu wote waliduwaa wasijue cha kufanya, lakini
mimi Willy nilijua la kufanya. Nilikimbia kwenye gari
Eddy alilokuwa amekodi na kuliacha New Afrika.
Kwa vile alikuwa ameliegesha vizuri niliingia na
kuondoka kama umeme. Nilikuwa nimeona lile gari
linakata kulia kutoka barabara ya Azikiwe kuingia
Azania Front. Nilipoingia Azania Front niliona gari
lao linafika kwenye ofisi za NASACO nikacheka.
ITAENDELEA
 
Gamba kwa kujipendelea!hofu alikuwa na nyaso,njama na veronica amadu toto la freetown alipouawa akahamia kwa zawadi kikosi cha kisasi akawa na tete kisha uchu akawa na bibiana vyote vinono.
 
Gamba kwa kujipendelea!hofu alikuwa na nyaso,njama na veronica amadu toto la freetown alipouawa akahamia kwa zawadi kikosi cha kisasi akawa na tete kisha uchu akawa na bibiana vyote vinono.
Good observation. Njama anasema hapendi kupika kwenye Hofu huko Rwanda anasema anapenda kupika........!
 
[QUOTE="kidi kudi, post: 11543553vitaburvya huyo]Riwaya; 'NJAMA' Mtunzi; A.E MUSIBA (Willy Gamba) NAONANA NA CHIFU Ndege ilitua kwenye uwanja wa ndege wa mjini Dar es Salaam kiasi cha saa moja na nusu asubuhi. Nilipita harakaharaka katika sehemu za afya, uhamiaji na ushuru wa forodha, kisha nikachukua teksi iliyonipeleka moja kwa moja katika ofisi yangu ya 'Afrika International Agencies', iliyoko mtaa wa Independence karibu na ofisi kuu za shirika la Bima la Taifa. "Hallo bosi, umerudi!", Rose mfanyakazi wetu sehemu ya mapokezi alisema. "Naam nimepata ujumbe wa teleksi kutoka kwa Marcelina kuwa mama anakufa". "Na kweli nenda ofisi kwako mwandishi wako mahususi alikuwa na wasi wasi maana huko juu wanakuulizia kila baada ya dakika kumi.

Ama kweli huko juu kuna kitu kikubwa kinawawasha". Nilielekea ofisini kwangu, nilipofika nikafungua mlango wa mwandishi wangu mahsusi, Linda. Oh, Mungu wangu, afadhali umefika, kidogo nipate wazimu maana huko juu hawanipi nafasi hata ya kupumua. Naulizwa kila wakati kwanini hujafika, utafikiri mimi ndiye nakufuga". "Poa sasa nimefika mwenyewe.

Vipi shughuli hapa?". "Mambo shwali, isipokuwa toka juzi kuna jambo limeharibika, maana jana nzima ofisi inawaka moto. Chifu huko juu ametingwa na mambo. Na afadhali uende sasa hivi, mimi nawajulisha kuwa uko kwenye lifti unaelekea ofisini kwake". "Yaa fanya hivyo". Niliacha mzigo wangu kwa Linda, nikaelekea ofisini kwa Chifu ambaye ofisi yake ilikuwa orofa ya tatu, na sisi tulikuwa chini katika jengo hilo hilo.

Nilifungua mlango bila kubisha hodi. Nikaingia ndani ya ofisi ya mwandishi mahsusi wa Chifu. "Ooh, Mungu wangu! Afadhali umekuja!", Maselina alisema kwa moyo wa furaha. "Hujambo lakini?". "Sijambo ila wasiwasi ni juu yako tu. Pole sana, nafikiri tumekukatishia likizo murua kabisa". "Wacha kusema. Tayari nilikuwa nimeshapata kipande cha msichana.

Nilipopata ujumbe wako kidogo nipate ugonjwa wa moyo. Je kuna nini huku kinacholeta wasiwasi hivi?". "Atakueleza mwenyewe kinachompandisha damu yake. Nakwambia amekuwa anakuhitaji kwa haraka sana, hata hivi anaona umechelewa. hivi sasa nilikuwa nataka kutuma teleksi nyingine". "Mama yangu mzazi! mtafikiri nina roketi yangu mwenyewe!". "Ngoja nimwambie kwamba umefika. Akifungua mlango kisha atukute tunapga soga sijui atafanya nini. Huenda atapasuka!". "Mwache apasuke! Mnafikiri kunikatisha likizo yangu nilijisikiaje.

Utadhani moyo wangu umetengenezwa kwa chuma, na wake kwa udongo". "Kamwambie mwenyewe hayo huko ndani", Maselina alijibu akimwemwesa huku akiinua simu. Huyu Maselina tumefanya kazi pamoja kwa muda mrefu kiasi ya kwamba uelewano wetu hauwezi kuelezeka kwa maneno. Huenda siku moja nitapata maneno ya kueleza, ila tu kwa leo naweza kusema ni rafiki yangu mkubwa. "Chifu, namba moja yuko hapa", Maselina alitamka katika simu. Nambari moja, ndivyo nilikuwa najulikana kikazi.

Katika kazi yetu sisi hutumia namba, mimi nilikuwa namba moja hivyo unaweza mwenyewe kuchekecha ukajuwa kwa nini. Mimi Willy si mtu wa majivuno. Watu wengi, hasa wakubwa wa serikali walinijua kwa hii namba yangu. Wengi walikuwa hawajui namba moja ni Willy Gamba, ila kwa watu wachache sana. Hii ilinipa fursa hata nyumbani Dar es Salaam nijulikane kama mfanyabiashara wa kawaida tu, na si Willy Gamba ambaye ni namba moja katika Idara ya Usalama, Tanzania. Maselina aliweka simu chini. "Nenda ndani mara moja". Nilifungua mlango, na nikamkuta Chifu akitembea toka kona moja ya chumba hadi kona nyingine.

Kwa mtu ninayemfahamu nikajua hapo alipo alikuwa na matatizo makubwa sana yaliyomsakama rohoni mwake. "Kaa chini namba moja', Chifu aliamru. Chifu anaponiita kwa namba yangu ya kazi ujue kuna jambo kubwa. nilivuta kiti nikaa, yeye akazidi kutembea kona hadi kona nyingine, hatimaye akasimama nyuma ya kiti chake. "Nashukuru kwa kufika kwako mapema, namba moja ndio sababu nakutegemea sana". "Asante", nilijibu halafu nikaendelea. "Mbona hivi, nini kinakuwasha?". Alichukuwa mtemba uliokuwa mezani, akafungua mkebe wa tumbaku akaijaza, kisha akawasha na kuanza kupuliza.

Alipuliza mara mbili, halafu akazungusha kiti chake ambacho kinazunguka kwenye tendegu, akaketi. "Kina jambo kubwa limetokea!". Aliweka mtemba wake mezani na kuweka mikono yake kwenye mezani. Akaniangalia machoni, huku macho yake yakionesha ukali wake. Akili yangu ikiwa tayari kusikiliza jambo hili huku moyo ukinidunda.

Utanisikiliza, utauliza maswali baadaye". Sawa". "Nafikiri nitaanza toka mwanzo. Ingawaje mambo mengine unayajua, nitayarudia tu kwa ajili ya umuhimu wa habari yenyewe ilivyo, unaonaje?". "Utakavyoona wewe Chifu". "Unajua nchi yetu inalea vyama vingi vya wapigania uhuru. Kama vile vyama vya wapigania uhuru toka Zimbabwe, Afrika Kusini n.k. Pamoja n a kulea vyama hivi tunawapatia vijana wao ya kijeshi. Kwa vile mafunzo mengi yanapatikana hapa na makao makuu ya vyama hivi yapo hapa, basi silaha zao vile vile zinapitia hapa na sisi tunazipokea toka nchi rafiki na kuwapa wanaohusika. "Hapa tuna vyama viwili vya wapigania uhuru katika Afrika kusini.

Vyama hivi ni 'The Peoples liberetion Front, of South Afrika (PLF)" kinachoongozwa na Ndugu Cecil Chimalamo na South Afrika National Party (SANP) kinachoongozwa na Ndugu Ray Simbuche. Miezi sita iliyopita Ndugu Cecil Chimalamo wa PLF alikwenda Urusi ambako alioba msaada wa silaha na akaahidiwa kupewa silaha hizo ambazo zingepelekwa Dar es Salaam mnamo muda wa miezi sita. "Wiki iliyopita Ubalozi wa Urusi wa hapa mjini ulipata karatasi za maelezo ya silaha hizi ambazo tayari zilikuwa zimeshapakiwa kwenye meli siku nyingi na zilikuwa njiani kuwasili Dar es Salaam.

Na makaratasi haya yalisema meli hiyo itawasili mjini hapa mnamo wiki hii'. "Basi yalipofika, ubalozi uliyashughulikia kikamilifu kwa upande wake, kisha ukayapitisha kwenye kamati ya ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), maana kamati hii ndiyo inashughulikia mambo haya kama unavyofahamu. Kamati nayo ilianza kuzishughulikia karatasi hizi mpaka zikawa tayari, wakawa sasa wanangoja meli kufika.

Habari kutoka kwenye Wakala wa Meli zilieleza kuwa meli hiyo itaingia bandarini Dar es Salaam tarehe tatu mwezi huu ambayo ilikuwa juzi ile". "Baada ya kupata habari hizi kamati ilipanga pamoja na ofisi ya mambo ya silaha za wapigania uhuru pia na maofisa wa bandari wanaohusika kuwa mizigo hiyo ipakuliwe usiku wa tarehe nne yaani juzi kuamkia jana. Kwa sababu karatasi zote zilikuwa zimekamilika na sehemu zote zikiwa na habari kamili, pande zote zilikaa zikisubiri silaha hizo mnamo siku hiyo kama ulivyopangwa".

Chifu alichukua mtemba wake tena akavuta kidogo kisha akauweka juu ya meza. "Nafikiri umenielewa mpaka hapo?". "Wakati huo mpango hii yote ya kupakua mizigo hii, ofisi ya PLF ilikuwa ikishirikishwa?", niliuliza. "Ndio, kwa sababu huwa wanaelezwa mambo yote yanavyokwenda, hivyo huwa wana habari kamili ya mambo yote.

Naweza kuendelea?". "Unaweza". "Sasa jambo la kushangaza likatokea juzi. Maofisa wa ofisi ya jshi la ulinzi inayoshughulikia silaha za wapigania uhuru walikwenda kwenye ofisi ya kamati ya ukombozi juzi mnamo saa nne ili kuchukua karatasi hizo za mizigo, wapate kijitayarisha kwa upakuaji wa mizigo hiyo wakati wa usiku.

Walipofika kwenye ofisi hii wakakuta ofisa anayehusika hajafika kazini. Ikabidi wamwone ofisa wa juu katika ofisi hiyo kumweleza umuhimu uliopo wa kuandaa kupakua silaha hizo usiku. "Huyu ofisa wa juu katika ofisi hii ya kamati naye alisema kuwa alikuwa ameshangazwa kwanini ofisa huyo alikuwa hajafika kazini. Hivyo wote kwa ujumla wakaondoka kuelekea nyumbani kwa ofisa huyo kuona kama anaumwa aweze kuwaelekeza wapi walipoziweka karatasi hizo. Huyu ofisa alikuwa akikaa sehemu za Upanga, Barabara ya Umoja wa mataifa, nyumba namba 1168". "Walipofika nyumbani kwa ofisa huyo walimkuta mfanyakazi wake akiwa nje. Walipomuuliza kama wenye nyumba wapo aliwajibu kuwa yeye hakai hapo ila huwa anakuja kila asubuhi lakini alipofika asubuhi hii alikuta milango yote ya kuingilia ndani ya nyumba imefungwa.

Hivyo mpaka muda huo alikuwa anasubiri kwani alifikiri wametoka. Ofisa huyo alikuwa anakaa yeye pamoja na mke wake na walikuwa bado hawajapata watoto. Ofisa mmoja wa jeshi alikwenda kuangalia gereji akakuta gari la ofisa huyu lipo na lilikuwa bado halijatoka. Kitu hiki kilimtia mashaka akawaeleza wenzake na akashauri wajaribu kuingia ndani ya nyumba huenda walikuwa bado wamo ndani.

Kwani kama kutoka wangekuwa wametoka na gari lao, walikubaliane wavunje mlango wa kuingilia ndani". Chifu alinyamaza kidogo akainua macho yake kuniangalia. "Walishtushwa kwa kumkuta ofisa huyu amepigwa risasi amekufa sebuleni, huku akiwa amevalia vizuri kabisa kuonyesha kuwa alikuwa anatoka matembezini.

Halafu ukumbini walimkuta mke wa ofisa huyo naye amepigwa risasi amekufa huku akiwa amevalia nguo za kulia. Haapo hapo wakanyanyua simu na kutoa ripoti ya vifo hivi kituo cha polisi Oysterbay ambacho hakikuchelewa kutuma maofisa wao kwenye nyumba hiyo. Baada ya polisi kufika, maofisa hao wa jeshi na ofisa kutoka kamati ya ukombozi ilibidi warudi upesi kwenye ofisi ya kamati, maana vifo hivi vilileta wasiwasi". Wakati wote huu akieleza, mimi nilikuwa kimya kabisa na akili yangu ilichemka niliposikia habari hizi za mauaji. "Halafu ikawaje?". "Walirudi ofisi za kamati upesi upesi, na kuanza kutafuta makaratasi haya ya mizigo kila mahali ofisini hapa, lakini hawakuona kitu.

Hapo ndipo jasho lilipowatoka. Jambo hili liliwapa wasiwasi zaidi ikabidi wakimbilie bandarini kutoa habari kwa maofisa wa bandari kuwa karatasi zimepotea". Chifu macho yake yaliwaka nikajua karibu anasema kitu cha kustua. "Walipofika katika ofisi za bandari, ofisa anayehusika na habari hizi, walipomweleza kuwa makaratasi yamepotea, alishangaa sana, ndipo mwishoni akawaeleza kuwa silaha zilikuwa zimeisha chukuliwa usiku uliokuwa umepita na wanajeshi waliovalia nguo za jeshi la ulinzi na wakiwa na karatasi zote za kuchukulia silaha, zikiwa kamili kabisa. Walikuwa wamefika na magari ya jeshi la wananchi, hata akawatolea namba za magari.

Kundi hili lililochukua silaha liliongozwa na mtui aliyevalia nguo za cheo cha meja. Kusikia hivi kundi lote lililofika kwenye ofisi ya bandari lilichoka kabisa. "Lakini si walikuwa wamekubaliana na ofisi ya bandari kuwa watapakua usiku wa juzi kuamkia jana, ilikuwaje yeye akaruhusu mizigo ipakuliwe usiku wa juzi ile kuamkia juzi?". "Huko ndiko nakuja kufafanua. Ofisa wa bandari alieleza kuwa mnamo terehe tatu mwezi huu ambayo ni juzi ile kiasi cha saa kumi alipata simu toka ofisi ya Kamati ya Ukombozi.
 
Nilikisoma hiki kitabu miaka zamani sana wakati huko hata Dar sijui vzr nilikuwa nakuja likizo tuu, lkn Leo nimeirudia na kujua sehemu zoote zilizotajwa Asante kwa kunirudisha shule ya msingi na sekondari.
 
Nilikisoma hiki kitabu miaka zamani sana wakati huko hata Dar sijui vzr nilikuwa nakuja likizo tuu, lkn Leo nimeirudia na kujua sehemu zoote zilizotajwa Asante kwa kunirudisha shule ya msingi na sekondari.
Hata mn nilikisoma nikiwa mdogo dar siifahamu hivyo leo nime enjoy sana . Hv New Africa hotel ndo ipo pale posta jirani na NBC Corporate eeh? Kumbe zamani ilikuwa Bank ya Nyumba daaah.
 
Hata mn nilikisoma nikiwa mdogo dar siifahamu hivyo leo nime enjoy sana . Hv New Africa hotel ndo ipo pale posta jirani na NBC Corporate eeh? Kumbe zamani ilikuwa Bank ya Nyumba daaah.
Hawa watunzi noma sana imebidi veronica afe ili amwachie Zabibu nafasi ya kutafunwa na Gamba
 
Back
Top Bottom