Riwaya: 'Njama'

Riwaya: 'Njama'

Kwa anayeweza kunipatia hivi vitabu vya Msiba pls ani PM niko Dar
 
NJAMA....
SURA YA NNE
FUNUNU
"Samahani binti tunaomba kumuona Meneja",
nilimwambia mwandishi mahsusi wa Meneja wa
Bandari.
"Sijui nyinyi ni akina nani?", aliuliza msichana huyu
aliyeonekana amechoka choka.
"Mwambie ni Willy Gamba na wateja wake kutoka
gazeti la Afrika".
Meneja wa Bandari tulikuwa tunafahamiana kikazi,
hasa kutokana na shughuli zingine tulizokuwa
tunazifanya katika kampuni yetu ya Afrika
Internation Agencies.
Yule msichana alizungumza na bosi wake kwa
simu, alipomaliza alinyanyuka na kutufungulia
mlango tukaingia ndani. Tulimkuta Issack Mlingi
ambaye ndiye Meneja wa Bandari aliyehusika na
tukio hili akionyesha hali ya kuchoka sana. Nafikiri
hii ilitokana na bughudha alizopata toka kwa polisi
na watu wengine wanaohusika na upelelezi wa
tukio hili. Macho yake yalikuwa mekundu na
yamevimba.
"Karibuni ndani", alisema huku akinyanyuka ili
tusalimiane.
"Samahani ndugu Mlingi, naamini una shughuli
nyingi sana", nilimuomba radhi.
"Si kitu Gamba, karibuni".
"Hawa ni wateja wangu Sherriff na Veronika kutoka
gazeti la Afrika ambalo kampuni yangu ni wakala
wake, na jamani huyu ni Issack Mlingi, Meneja wa
Bandari", walipeana mikono kisha wote tukavuta
viti tukakaa.
"Ndugu Mlingi ni imani yangu kuwa umeisha ulizwa
maswali mengi juu ya tukio hili lililotokea hapa
bandarini. Lakini naamini hatutakuwa
tumekuhangaisha kama tutakuuliza maswali. Kama
nilivyokwisha kwambia hawa waandishi wa gazeti
la Afrika na ni waandishi pekee walioruhusiwa
kuingia hapa nchini kuandika juu ya tukio hili,
naamini unajua msimamo wa gazeti la Afrika. Hata
hivyo tutakuuliza maswali kidogo tu kusudi
tusikuchoshe sana".
"Hebu nipeni vitambulisho vyenu niviangalie",
aliomba.
Sherriff na Veronika walimpa vitambulisho,
akaviangalia na aliporidhika akavirudisha.
"Haya ulizeni maswali yenu, maana ikiendelea hivi
naweza kupata wazimu", alisema huku akitoa
tabasamu la uchovu.
"Tumesoma maelezo yako uliyotoa polisi, ila
tumekuja hapa kukuuliza maswali machache juu ya
mambo ambayo hatukuwa tumeyaelewa vizuri",
alisema Sherriff.
"Ulieleza kuwa ulipata simu kutoka kwa Jones
Mantare ambaye umezoea sana sauti yake, kiasi
kwamba huwezi kuikosea ukiisikia. Lakini jambo la
kushangaza ni kwamba, Mantare anasema hakuwa
amekupigia simu kwani alikuwa na mkutano na
Mwenyekiti wa Kamati na Mwenyekiti amethibitisha
kuwa ni kweli walikuwa wote toka saa tisa hadi saa
kumi na moja. Baada ya kupata maelezo hayo
bado unaweza kusema kuwa sauti ile ni sawa
kabisa na ya Mantare?".
"Kwa sababu wakati ule nilikuwa sina wasiwasi
kuwa kuna jambo baya roho yangu iliridhika kuwa
ni Mantare. Lakini sasa kwa sababu Mantare
anasema hakupiga simu, ndipo nakumbuka kuwa
nilimwuliza kama ana mafua, maana kwa mbali
alikuwa akizungumzia puani, na yeye alijibu kweli
mafua yalikuwa yamemkaba sana. Lakini maelezo
mengine, mathalani ambayo huwa tunataniana na
Jonas, yalikuwa yote sawa. Kusema kweli
inawezekana kabisa alikuwa mtu mwingine
anayemfahamu sana, lazima niseme sana maana
isingekuwa hili jambo la mafua bado ningeendelea
kung'ang'ania alikuwa Jones. Lakini Jones
amekuja hapa hana mafua hata kidogo kwa siku
nyingi".
"Hebu fikiria tena kidogo juu ya sura na sauti au
umbile na tabia ya huyu mtu aliyekuwa akijiita Meja
Paul Liboi, unaweza kuwa na uhakika kabisa kuwa
mtu huyu ni mzalendo wa Tanzania?", Veronika
aliuliza.
Ndugu Mlingi alisita kidogo kujibu swali hili na uso
wake ukakunjamana kidogo. Baada ya kufikiri sana
akasema.
"Nafikiri anaweza asiwe mzalendo".
Wote tukamwangalia.
"Kwanini unafikiri hivyo?", mimi nilimuuliza.
"Wazo hili lilikuwa halijaingia kichwani mwangu,
lakini sasa baada ya kuuliza swali hili inawezekana
mtu huyu asiwe mtanzania maana kwanza
kiswahili chake hakikuwa kimenyooka na alipenda
sana kuchanganya na kiingereza. Mimi nilimfikiria
kuwa huenda ni Mjaruo, lakini alikuwa hajang'oa
meno. Vile vile alikuwa na haraka haraka na
maneno ya mkato mkato. Nikifiri sana hakuna na
ile hali ya kirafiki waliyonayo watanzania wengine
wengi. Lakini kwa sababu nilijuwa ni mwanajeshi
nikafikiri ndio sababu aikuwa na tabia ya namna
hiyo".
"Una jambo jingine ambalo huenda sasa unafikiri
halikuwa lakawaida juu ya tukio lolote baada ya
kujuwa watu hawa walikuwa majahiri?".
"Nafikiri nimeshasema yote, ila tu huenda kitu
kimoja, sijui kama kinahusika ama vipi".
"Ehe, kitu gani".
"Baada ya kuzungumza na huyo anayejiita Jones
Mantare, simu za jengo hili hazikufanya kazi tena.
Tulipowaeleza Posta kesho yake, walikuja mafundi
na kusema waya inayounganisha jengo hili na
waya zinazokwenda Posta ilikuwa imekatika kwa
kuangukiwa na mti. Sasa nilianza kuona picha
kidogo ya tukio hili. Nilijua mara moja kuwa watu
waliokuwa wameshughulikia tukio hili ni watu
wenye kujua ujasusi wa hali ya juu; kwani
walihakikisha kuwa kila hatua wanayoichukua na
nyayo zake wanazifuta ili asiwepo mtu wa
kuzifuatiia".
TUjikuta tumeridhishwa sana na safari yetu ya
bandarini hivyo tukaona tuondoke.
"Asante sana ndugu Mlingi, kama tukihitaji mambo
zaidi tutakuona tena, na kama utakumbuka kitu
cochote kinachoweza kutusaidia nipigie simu.
Nafikiri simu yangu unayo?", nilimuuliza.
"Ndio ninayo", alijibu.
"Na tahadhali usizungumze ovyo juu ya tukio hili,
maana si tukio zuri", nilimwonya.
"Bila shaka nitajitahidi".
Tuliagana nae, tukaondoka kuelekea mjini.
Nilijaribu nilivyoweza kuangalia kama naweza
kumwona Eddy na mwenzake, lakini wapi hakika
vijana walikuwa wanafanya kazi nzuri sana, maana
kama mimi Willy sikuweza kuwatambua basi
hakuna mtu mwingine tena, si kama najisifu ila huo
ndio ukweli, mtu akitaka kunitafuta mimi basi
ajiweke sawa, la sivyo shauri lake.
"Kamara kama ulivyomjua alikuwa mtu wa namna
gani, unafiri anaweza kwa njia yoyote akawa
kajiingiza katika jambo hili?", nilimuuliza Sherriff
huku tukiwa tumesimama kungojea kuingia
barabara ya site drive, tukutokea bandarini.
"Mimi nakuhakikishia komredi kuwa Kamara
alikuwa hawezi kufanya jambo kama hilo, ni lazima
tu iko namna ambayo alishambuliwa na
kunyang'anywa karatasi hizo, alinihakikishia
Sherriff.
"Oke, naona sasa twende kwenye ofisi ya kamati
ya Ukombozi ya OAU", nilimweleza huku nageuza
gari kuingia site drive na kuelekea kwenye ofisi ya
kamati.
Tulipofika kwenye mapokezi ya ofisi hii ya kamati
na kumkuta msichana mmoja akizungumza kwenye
simu, ikatubidi tumsubiri kidogo amalize
kuzungumza, niliangalia saa yangu ilikuwa yapata
saa sita na dakika tano.
"Samani jamani, sijui niwasaidie nini", msichana
alituuliza.
"Bila samahani binti, sisi tunaomba kumwona
Jones Mantare", nilijibu.
"Mna ahadi naye?", binti aliuliza.
"Hapa, lakini nafikiri ukimwambia Willy Gamba wa
AIA na wageni toka gazeti la Afrika, ambao
wanataka kumwona, anaweza kutuona",
nilimweleza.
"Msubiri basi", huyo msichana alijibu kisha akainua
simu na kuanza kuzungumza na ofisi ya Mantare.
Jones Mantare alikuwa ananifahamu, maana
nilikuwa nimehakikisha kuwa nafahamiana karibu
na kila mtu katika ofisi hii ya kamati, yeye alikuwa
akinifahamu kama mfanyabiashara, maana ndivyo
nilivyojulishwa kwake. Tokea hapo tulikuwa
tunaonana mara kwa mara sehemu za starehe na
kujenga uelewano wa kutosha, hivyo nilihisi kuwa
asingeweza kunikatalia nisimuone, ingawa nilijuwa
atakuwa katika hali isiyokuwa ya kawaida. Baada
ya kuzungumza kwa muda kwenye simu msichana
alitwambia.
"Mnaweza kwenda kumwona, ofisi yake ipo mwisho
wa ujia mkono wa kulia".
"Asante sana binti", nilimjibu.
Tulimwacha tukaelekea alikotuelekeza. Tulibisha
mlango pale tulipokuwa tumeelekezwa.
"Karibu", tulisikia sauti ya msichana ikitoka ndani.
Nilifungua mlango tukaingia na tujikuta katika ofisi
kubwa ya mwandishi mahsusi wa Mantare.
"Habari zako bibie", nilimsalimia kwa niaba ya
mwenzangu.
"Nzuri, ni Gamba na wenzake nafikiri?", aliuliza.
"Hasa", nilijibu.
"Ingieni moja kwa moja anawasubiri", alisema huku
akisimama na kutufungulia mlango wa bosi wake.
Tulipoingia tu Mantare alisimama.
"Ahaa ndugu Willy, karibuni".
"Asante, asante Jones".
"Nafikiri niwajulishe, huyu ni ndugu Jones Mantare,
ofisa katika kamati hii ya ukombozi, na hawa ni
komredi Ahmedi Sherriff na komredi Veronika
Amadu. Ni waandishi wa habari wa gazeti la
"AFRIKA".
Walipeana mikono kwa mara nyingine.
"Ehe, mlitaka kuniona, sijui niwasaidie nini?",
aliuliza.
"Hawa makomredi ni wateja wangu, kampuni yangu
ndio wakala wa gazeti la Afrika hapa nchini. Hasa
kitu kilichotueta hapa ni kutokana na tukio hili la
juzi. Nafikiri unaelewa msimamo wa gazeti la Afrika
katika ukombozi, na kutokana na msimamo huo
wameiomba serikali kama wanaweza kuandika
habari za kuaminika juu ya tukio hili. Ni wasiwasi
wao kuwa magazeti mengi ya kibeberu yataandika
habari za kupotosha, na wao wako hapa ili waweze
kueleza jumuia ya ulimwengu ukweli mtupu. Kwa
hiyo tutashukuru sana ukiweza kutusaidia katika
kujibu maswali machache. Hatutataka kupoteza
muda wako kutueleza mengi, maana nakala ya
maelezo yako tumeipata toka polisi. Hivi ni nia
yetu uweze kutufafanulia katika sehemu ambazo
hazieleweki katika tukio hili".
Niliona kule kutaja nakala ya maelezo yake kutoka
polisi kulimtoa wasiwasi aliokuwa ameuonyesha
usoni mwake. Niliona macho ya Veronika yakiwaka
kuonyesha kuwa nilivyoeleza nimeeleza vizuri sana
na Sherriff alitingisha kichwa kuonyesha kuwa
niliyoyasema ni sawa kabisa.
"Sawa ndugu Willy, nitakuwa tayari kuwajibu
mwaswali yenu, kusema kweli kama ulivyosema,
radio za kibeberu zimekwisha tangaza uongo ili
kuridhisha maslahi yao. Kwa jinsi hii tutakuwa
radhi kuona ukweli unaandikwa na gazeti hili. Haya
sijui mna maswali gani?".
"Inasemekana kuwa hayati Kamara Franki ndiye
alikuwa anashughulikia suala hili la silaha. Na
amekutwa ameuawa. Nafikiria hizi karatasi
zilitokatokaje mikononi mwa marehemu na kuingia
mikononi mwa hawa majahiri?. Maana kutokana na
maelezo ya Polisi ofisi yenu hii haikuvunjwa mahali
popote", Sherriff aliuliza.
"Sawa kabisa?, kutokana na maelezo ya mwandishi
mahsusi wa marehemu, anasema ya kwamba?,
wakati marehemu anatoka ofisini alimweleza aweke
zile karatasi za kuchukulia silaha ndani ya mkoba
wake, kwa sababu alikuwa anategemea kwenda
kwenye kikosi cha Jeshi kinachoshughulikia silaha
za wapigania uhuru kesho yake, kabla hajaja
ofisini. Kwa hiyo, jibu kwa swali lako ni kwamba
watu hawa walimnyang'anya marehemu karatasi
hizo na ndio sababu wamemuua."
"Watu hawa unafikiri walijuajuaje kuwa marehemu
atakuwa na karatasi hizi ndani ya mkoba wake?",
Veronika aliuliza.
"Hapo ndipo hata sisi tumekwama".
"Huyu mwandishi mahsusi wa marehemu yupo",
nilimuuliza.
"Ndio yupo".
"Unaweza kumwita tukazungumza nae kidogo?".
"Hali yake si nzuri sana, bado ana mshituko kwa
ajili ya marehemu. Unajua mnapofanya kazi kwa
uhusiano ulio karibu na mtu mnakuwa na urafiki wa
hali ya juu sana. Hata hivyo nitajaribu kuwaitieni".
Alishika simu na kuzungumza na mwandishi wake.
Wakati tukimsubiri Veronika alimuuliza tena. "Ofisa
wa kule bandarini Ndugu Mlingi anasema mtu
aliyempigia simu alikuwa na sauti kama yako,
mathalani mambo mnayotaniana yalikuwa vile vile,
unaweza kufikiri mtu yeyote hapa ofisini au hata
nje anayeweza kuigiza sauti yako kiasi hicho?".
"Ni imani yangu kuwa mtu kukuigiza kiasi hicho
lazima awe mtu aliyekuzoea, na mtu aliyekusikia
ukizungumza mara kwa mara, hasa na huyu ndugu
Mlingi".
"Kuesema kweli, nimefikiria kweli juu ya mtu huyu
mpaka nimechoka, nitazidi kumfikiria kama wazo
likinijia nitakupigia simu."
Mara mlango ulifunguliwa akaingia msichana mrefu
mwembamba mwenye nywele nyingi. Kama
unapenda wasichana warefu na wembamba, basi
hapa pana msichana wa namna hiyo, jina lake
Margreth. Ni mzuri kiasi chake.
"Karibu Margreth", Mantare alimkaribisha, wote
tukasimama akatujulisha kwake. Mwandishi
mahsusi alileta kiti kingine na Margreth akaketi.
"Samahani Margreth", hawa ndugu wana maswali
kidogo ya kukuuliza," Mantare alimwambia.
Margreth hakujibu kiti bali alituangalia tu.
"Samahani sana binti, sisi wote yunaelewa hali
uliyonayo, ila imetubidi tukuone tuweze
kuzungumza nawe huenda utatusaidia kutatua huu
mkasa uliompata bosi wako", nilimwelezea.
"Niko tayari kuwaelezea chochote kama kitasidia
kuwapata watu waliomuua bosi wangu." Magreth
alijibu huku machozi yakimlengalenga.
"Jaribu kukumbuka, nilimwambia, "wakati
marehemu anakueleza uweke zile karatasi za
kuchukulia silaha kulikuwa na mtu mwingine
yeyote?".
Alikaa kimya kwa muda kisha akajibu, "Hapana",
harafu kama amegutuka akasema, "Ndio
nakumbuka sasa, alikuwepo tarishi wetu wa hapa
ofisini".
Nikasikia kengere ya tahadhari inalia kichwani
mwangu. Wote tulitazamana.
"Tarishi huyu yuko hapa?", niliuliza.
"Hapana, ni mgonjwa anaumwa na ameandikiwa
kulala siku tano', Margreth alijibu.
"Toka lini?".
"Toka tarehe nne".
"Yaani siku ambayo ilibainika kuwa silaha
zimeibiwa na bosi wako ameuawa?".
"Ndio".
"Yaani atakuwa kazini tarehe tisa".
"Ndio".
"Una uhakika kabisa alikuwepo?".
"Ndio".
Habari kama hizi mimi ndizo huwa zinanitibua,
maana wakati kifo kinatokea haafu kinatokea kitu
kingine chenye uhusiano wa karibu namna hii, basi
hapo ndipo huwa naanza kujumulisha moja kwa
moja na kupata mbili.
Nilimgeukia Mantare na kumwuliza, "Huyu tarishi
ndiye alikuwa tarishi wa ofisi nzima?".
"Ndio'.
"Anaitwa nani?".
"Anaitwa George Kiki".
"Mmekuwa naye muda gari?".
"Yapata miezi sita sasa".
"Ni MTANZANIA!".
"Hapana ni mkimbizi kutoka Afrika Kusini, aliletwa
kwenye ofisi yetu na chama cha wapigania uhuru
cha Afrika Kusini kilichopo hapa mjini cha SANP. Ili
tumsaidie. Alipokuja hapa alitupa maelezo yake na
kuonekana ni kati ya vijana walioanzisha
maandamano ya kitongoji cha Soweto huko Afrika
Kusini. Alieleza kuwa yeye alipata mwanya wa
kutoroka gerezani ndipo akakimbia na kuweza
kufika hapa baada ya safari ndefu ya taabu. Kwa
vile alikuwa hana kisomo cha kutosha jinsi yeye
alivyojieleza tuliamua kumpa kazi ya utarishi ili
kumsaidia. Kusema kweli amekuwa kijana mwenye
bidii sana, na anapendwa na kila mfanyakazi wa
hapa, hasa kwa nidhamu yake, na utekelezaji wa
kazi yake".
"Kwa hivi alikuwa na fursa ya kuingia ndani ya ofisi
ya mtu yeyote wakati waowote ili kuchukua mafaili
na mambo kama hayo?".
"Hasa ndivyo ilivyokuwa".
"Anaishi wapi?".
"Anaishi huko Kinondoni sehemu za Hananasifu
Estate katika nyumba za shirika la nyumba".
"Nyumba yenyewe unaijuwa?".
"Mimi nimewahi kufika kwake; tumewahi
kumpeleka na marehemu", alisema Margret huku
tena machozi yakimlengalenga.
"Samahani Mantare, sijui unaweza kumruhusu
Margret akatuelekeza kwa Ndugu Kiki?".
"Bila wasiwasi mnaweza kwenda nae".
Niliwaangalia wenzangu nikaona wameridhika na
maswali na majibu ya hapa, hivyo kwa niaba yao
nikamshukuru ndugu Mantare.
"Ikiwa tutahitaji jambo lolote tutarudi tena au
tutapiga simu. Na wewe ukipata jambo lolote
usisite kutufahamisha".
"Hamna tabu, nitafurahi kuwasaidia".
Tuliagana tukaondoka kuelekea Kinondoni.
ITAENDEEA....
 
NJAMA
SURA YA NNE
FUNUNU III
"Mimi naona tukapate chakula cha mchana
kwanza", Sherriff alishauri.
"Sawa", walijibu kwa pamoja. Sherriff alikaa nyuma
pamoja na Margret na wakati huo mimi naendesha
nikiwa katika mafikara mengi, Sherriff alichukua
jukumu la kumtuliza Margret akimweleza mambo
mengi juu ya matatizo ya binadamu na kumwambia
kuwa asihuzunike sana maana ndiyo binadamu.
Kadiri Sherriff alivyozidi kusema ndivyo Margret uso
wake ulizidi kutokwa na huzuni kwani mimi
nilikuwa nawaangalia katika kioo cha kuendeshea.
Hata Sherriff alipofika kusema yeye huwa anaamini
kuwa kwa kila linalotendeka linatendeka kwa ajili
ya uzuri, nilimwona Margret anamwemwesa kwa
mara ya kwanza, na ndipo sura yake ilionyesha
uzuri aliokuwa nao. Niliona hata Sherriff aligundua
uzuri huo, kwani uso wake ulibadilika kiasi cha
kwamba moyo wake uliguswa.
Tulifika New Afrika Hoteli, nikaegesha gari wote
tukatoka nje. Basi, moja kwa moja tulifuliza
kwenda kwenye lifti ya kutupeleka orofa ya kwanza
ambapo ndipo Bandari Grill ilipo. Mbele yangu
nilimwona Eddy anavuka sehemu ya mapokezi,
halafu akazungusha kichwa akaingia kwenye choo
kilichopo hapa chini. Hii ilikuwa ishara kuwa alitaka
kuniona.
"Samahani jamani nasikia nimebanwa haja ndogo,
tangulieni nakuja sasa hivi. Margret, we ndiye
mwenyeji washughulikie wagaeni".
"Bila wasiwasi", alijibu akiwa anaanza kupona
kutoka katika mshituko alioupata.
Niliingia maliwatoni nikamkuta Eddy ananisubiri.
"Mpaka dakika hii hakuna chochote", aliniambia
bila kuniangalia.
"Sawa, nendeni mkale halafu nenda ofisini
nitakukuta huko kiasi cha saa kumi hivi".
"Oke", alisema huku akielekea kwenye mlango wa
kutokea.
Mimi nilimaliZa haja yangu ya uongo na kweli
nikaondoka kujiunga na wenzangu. Tulipata muro
safi sana hapa Bandari Grill, na kwa sababu kila
mtu alikuwa na njaa tulikula kimya kimya.
"Nasikia kichwa kinaniuma", Veronika alilalamika.
"Nafikiri kwa ajili ya hali ya hewa. Joto jingi sana
kuliko ulilozoea", nilimjibu.
"Kama ni hivyo afadhali ukameze dawa upumzike,
sisi tutakwenda kumwona Kiki halafu tutakuja
kukuona", Sherriff alishauri.
"Naona hivyo ni sawa", alijibu.
Basi tulikubaliana Veronika apumzike sisi tuendelee
na shughuli. Tuliondoka New Afrika na
kumtelemsha Veronika Kilimanajaro.
"Vero mpenzi, kuna gari lile pale unaweza kulitumia
wakati wowote. swichi iko chini ya zulia",
nilimuonyesha gari ambalo Eddy alikuwa ameliacha
hapo. Sisi tuliondoka na kuendelea na safari yetu
ya Kinondoni.
"Twende kupitia barabara ya Upanga moja kwa
moja, halafu tukivuka Salendar briji mbele kuna
barabara ya Kinondoni hivyo tutaingia kushoto.
Sehemu iko mbele ya makaburi. Baada ya
makaburi kuna barabara la vumbi, linakatisha
barabara hii. Tukiacha hilo na kuendelea mbele
tukakuta barabara nyingine ya vumbi inaingia
kushoto na kuna kibao kimeandikwa Bamboo Baa
and Restauranti, basi hapo ndipo tutakapoingia",
alieleza Margret kwa ufasaha kabisa.
Mimi hupenda maelezo ya namna hii, siyo mtu
amefika mahali pa kukata kona ndipo anasema,
kata hapa kushoto. Maelekezo hayo ni ya kihuni na
ndiyo anayosababisha ajali nyingi.
Nilifuata maelezo ya Margret vizuri kabisa,
nilipotaka kuingia kushoto pale kwenye bao la
tangazo la Bamboo Baa and Restauranti, Margret
alisema, 'Njia hapa si nzuri twende pole pole,
halafu mbele kidogo utakata kushoto tena tuelekee
kwenye nyumba hizo pale", alinielekeza na
kuonyesha kwa kidole.
Niliendesha pole pole nikaikuta njia na kuifuata
kuelekea kwenye nyumba hizi za shirika la nyumba.
"Baada ya nyumba hiyo yenye bendera ya CCM,
ambayo ndiyo ya mjumbe, ya pili yake".
"Hapa?".
"Ndio, mlango huu huu".
Nyumba hizi zinakaa familia mbili mbili, lakini
zimetengwa katikati kiasi kwamba kila familia ina
sehemu yake kamili. Tulitoka ndani ya gari,
Margret akatangulia na kibisha hodi. Lakini
hatukupata jibu. Nilisikia moyo wangu unapiga
haraka haraka, hii ni sirika niliyozaliwa nayo, na
ilikuwa ni ishara kuwa kuna hatari.
"Hebu ngoja Margret", nilimwambia nikimrudisha
nyuma.
Niliujaribu mlango ukafunguka nikamwita Sherriff
na kumwambia hakuna mtu, tulifungua mlango
mwingine uliokuwa unaelekea jikoni, bafuni na
chumba cha kulala. Tukiwa wote na wasiwasi
tukibisha hodi kwenye mlango wa chumba cha
kulala. Lakini hatukupata jibu. Nilitoa Bastola
yangu, na kusukuma mlango wazi.
Tulimkuta mtu ambaye tuliamini ni Kiki
amechomwa kisu kifuani!, nilipomshika nikajua
alikuwa amekwisha kufa saa nyingi sana. Kisu
kilikuwa kimeachwa pale kifuani. Kilikuwa kisu
kikubwa na mpini wake mwekundu. Tulimwita
Margret aje atuhakikishie.
Akiwa anatetemeka kwa woga alikuja na kusema,
"Ndiye yeye masikini", akaanza kulia tena
tulimbembeleza na kumvuta na kuondoka haraka
haraka ndani ya nyumba hiyo. Tuliingia katika gari
langu na kuelekea mjini. Sasa nilianza kuongeza
hesabu kwamba mbili na mbili na kupata nne. Na
vile vile majahiri hawa walianza kunitisha kwani
mbinu zao zilikuwa kubwa. Lakini hata hivyo mbinu
za Willy ni kubwa zaidi.
"Mapambano yameanza Sherriff", nilisema kwa
sauti ambayo sikuamini ilikuwa yangu.
"Na kweli yameanza", Sherriff alijibu.
Wakati huo tulikuwa tumesimama kwenye taa za
usalama barabarani za salendar briji tukuelekea
New Afrika. Saa yangu ilisema ni saa kumi na
dakika mbili.
"Naona mimi mnifikishe nyumbani", Margret
aliomba.
"Unakaa wapi".
"Ninakaa kwenye orofa pale nyuma ya Rex Hoteli".
"Nazijua orofa hizo, uko orofa ya ngapi, maana
tunaweza kukuhitaji ama kikazi ama katika hali ya
kustarehe, unasemaje?".
"Karibu mimi niko orofa ya pili chumba namba
kumi na nane. Simu yangu ni 22221".
Basi wakati huo tulikuwa tumefika Posta ya
Azikiwe, tulipofika kwenye sanamu ya Bisimini,
tukaingia Independent Evenue.
"Unajua", Margret alitugutusha.
"Ehee", nilijibu na kumwangalia ndani ya kioo cha
kuendeshea, maana yeye alikuwa amekaa nyuma.
"Sijui ni mafikara yangu, ila tu limekuja kama wazo
la kunishangaza, maana baada ya kutokea mambo
haya kila kitu nakiona si cha kawaida
kinanigutusha".
"Nini kimekugutuusha?", Sherriff aliuliza akionesha
msisimko.
"Unajua pale kwenye lango la kuingia ndani ya ofisi
yetu kumekuwa na mwendawazimu ambaye
amekaa pale zaidi ya mwezi mzima. Amekuwa
amevaa matambalatambala tu na amebeba
makopo mengi, sijui mmemuona?".
"Mimi nilimwona", Sherriff alijibu.
"Mimi sikumwona".
"Polisi walikuja kumchukua siku moja, na
kumpeleka kunakohusika lakini hazikupita saa tatu
akarudi. Alikuwa hatoki pale hata dakika moja,
usiku na mchana kutokana na walinzi wa usiku
wanavyosema. Leo mlipokuja alikuwepo maana
mimi niliona gari lenu linaingia wakati natoka
kunywa chai. Gari lenu lilipoingia na yeye alivuka
lango akaingia ndani. Hii ni kawaida yake, kwani
huwa anaombaomba kwa kila mgeni anayefika pale
ofisini na ndio sababu aliitiwa polisi kwa sababu
anawafadhaisha wageni wetu. Gari lenu mliliegesha
mbele kabisa ya mlango wa kuingia mapokezi na
kutoka ndani ya gari haraka hivyo hakuwahi. Mimi
nilipoingia pale mapokezi nilikuta nyinyi
mmekwisha kwenda ofisini kwa Mantare ila
nilimkuta yule kichaa anamuuliza yule msichana
wa mapokezi. Hawa watu wanasema wanatoka
katika gazeti la Afrika. Yule msichana wa mapokezi
alikasirika na kumfokea, Toka hapa! kama
wanatoka gazeti la Afrika watakufaa nini wewe?,
wana kazi ya maana kuliko kuonana na
mwendawazimu kama wewe. Toka!".
"Kitu cha kushangaza ni kwamba wakati
tunaondoka pale ofisini kwetu nakumbuka
sikumuona wala makopo yake na kilago chake
hakikuwepo, sijui jambo hili lina maana yoyote au
mnaonaje nyinyi wenyewe?", alimalizia Margret.
"Unasema alikuja hajawahi kutoka pale hata dakika
moja, ila tu siku ile aliyochukuliwa na polisi kwa
muda wa masaa matatu?", nilimuuliza.
"Nina uhakika kabisa maana mimi damu yangu
ilikuwa haipatani na yule mtu kabisa, na ni mimi
niliyefanya kampeni ya kumuitia polisi lakini
aliporudi alionekana kuwa maafisa wote walidharau
kumchukulia hatua tena".
"Ukimwangalia alikuwa anaonekana kichaa au
unafikiri anajifanya tu?", nilimuuliza.
"Kitu kilichonikosanisha naye ni kwa sababu siku
moja aliniambia yeye si kichaa ila anajifanya tu ili
kujipatia pesa bila jasho. maana ilikuwa
ukimwangalia sana wakati yeye hana habari
anakuwa kama si mtu kichaa, ila huwa anapoona
watu anakuwa kichaa kabisa".
"Asante sana, kumbuka jambo hili linaweza likawa
na msingi tutaliangalia".
"Asante".
Niliegesha gari mbele ya Rex Hoteli.
"Wakati wowote tutegemee", nilimweleza huku
akitelemka.
"Mnakaribishwa", akiwa zaidi anamwangalia
Sherriff. Sherriff alitoa mkono wake wakapeana
mikono. Tayari kulikuwa na kitu kinapita kati yao,
maana nyuso zilikuwa wakati wanapeana mikono,
mimi ndiye najua, maana hata mimi hali hii
inanitokea. Walikuwa wameanguka katika penzi.
"Mimi naona turudi pale ofisi ya kamati
tukahakikishe kama kweli hayupo pale yule kichaa",
nikimwambia Sherriff.
"Sawa".
Tulikwenda kimya kimya kila mtu akichambua
mambo, tuliyokuwa tumeyapata na kuyaona,
tulipofika pale ofisini tulimkuta mlinzi wa jioni
anayeingia kazini saa tisa wanapofunga kazi mpaka
saa kumi na mbili asubuhi, ilionekana alikuwa
anafanyakazi masaa mengi sana, lakini yeye
alipenda kazi yake na kuridhika na kipato
alichokuwa anakipata, baada ya kutusalimia na
kutueleza hizo saa zake za kazi, nilimuuliza.
"Unajua kulikuwa na mzee mmoja kichaa hapa sijui
amehamia wapi?'.
"Hata mimi nashangaa, kichaa huyu alikuwa hatoki
hapa hata dakika moja. Hata haja zake alikuwa
akiifanya hapa hapa karibu. Polisi walimchukua
hapa akawachenga akarudi mwishowe
wakamwachia akae tu. sasa leo nafika nakuta
kiisha ondoka na wala harufu yake hakuna.
Nimeshangaa sana. Amekaa karibu mwezi mzima".
"Ulikuwa unapata fursa ya kuzungumza nae?".
"Si mara nyingi, ila tu siku moja nilikuja
na ..........akasita kusema.
"Sema tu usiogope, hata kama ni siri, sisi
tutakufichia".
"Lakini nyinyi ni akina nani?".
"Sisi tunashughulikia wagonjwa wa akili, tumepata
habari toka polisi kuwa kuna mwendawazimu hapa,
hivyo unaweza kutueleza tabia yake ili tuweze
kumtafuta. Kwa hiyo usisite kutueleza",
nilidanganya.
Baada ya kutafakari mambo haya aliendelea, "Siku
moja kulikuwa na tafrija hapa ofisini jioni. Mimi
niliweza kwa mbinu zangu kujipatia mzinga mzima
wa whiski aina ya 'Dimple' nikauficha wagaeni
wote walipoondoka, nilitoka nje ya lango na kuanza
kunywa huu mzinga wa whiski. yeye alipoona
ninakunywa hii whiski alikuja na kopo lake
akaniomba kwa vile nilikuwa najuwa siwezi
kumaliza chupa nzima nilimgawia nusu basi
alikunywa ile pombe kama maji. Basi ilipomkolea
akaanza kuzungumza Kiingereza ila mara kwa
mara alisema neno sijui 'Sazafrika' neno hili
alilirudia mara nyingi. Na nyinyi mnajua vichaa
mimi niliachana nae nikaendelea na shughuli zangu.
Sasa sielewi kama kilikuwa Kiingereza sawa sawa.
Lakini kitu kilichonivutia ni kule kutamka hicho
Kiingereza chake kama mzungu. Lakini husema
kichaa ana mashetani saba, anaweza kuzungumza
lugha saba tofauti."
"Asante sana, na samahani sana kwa
kukubugudhi", Sherriff alitoa mfukoni shilingi
arobaini akampa. Yule Mzee alifurahi sana.
"Mungu awaongezee wanangu".
Tuliingia ndani ya gari tukaondoka zetu.
"Unaona mambo yalivyo Sherriff?, hii inaonyesha
wazi kuwa George Kiki alikuwa ni jasusi
aliyepachikwa hapa na mabeberu na wakafanikiwa.
Mimi simulaumu mtu yeyote, hata mimi huenda
ningemsaidia kupata kazi. Baada ya mabeberu
kujua mkataba wa silaha kati ya PLF na Urusi
miezi sita iliyopita walichukua hatua ya kuhakikisha
hizo silaha haziwafikii wapigania uhuru wa PLF
maana inasemekana ni silaha za kisasa kabisa.
Tutakapoonana na kiongozi wa PLF atatueleza
zaidi, kuajiliwa kwa kiki miezi sita iliyopita
kunaoana kabisa na nyakati za mkataba huo.
Inaonekana kazi ya jasusi huyo ni kujua mambo
yote yanayotendeka juu ya huo ili mwishowe aweze
kuiba hizo karatasi za kuchukulia silaha, jambo hili
amefanikiwa", nilinyamazi kidogo.
"Kwanini wamwue?", Sherriff aliuliza.
"Kwa sababu hawakuwa na haja nae tena, asije
akashikwa na kutoa siri. Hii inanionyesha jinsi watu
hawa walivyo wajuzi katika kazi yao, hawataki
kufanya makosa".
Wakati huu tukizungumza tulikuwa tukielekea mjini.
"Juu ya huyu kichaa unasemaje?".
"Huyu kichaa nae ni jasusi. Ninavyoona mimi huyu
aliwekwa pale ofisini kusudi aweze kuona nini
kitatokea hapo ofisini baada ya silaha kuibwa.
Aliwekwa mwezi mmoja ili kuondoa mashaka.
Hivyo alikuwa anangoja kuona baada ya polisi na
maofisa wa usalama ni nani mwingine aliyekuwa
na dukuduku juu ya jambo hili. Aliposikia waandishi
wa habari wa gazeti la Afrika nao wamejiingiza
akawa amemaliza kazi, akaondoka kwenda
kupeleka ujumbe, ni wazi kabisa wao walijuwa
polisi na maofisa wa usalama watalishughulikia
jambo hili na ninafikiri walishapima uzito na kuona
wanaweza kukabiliana nao. Hivyo walingoja wajue
kama kuna kundi jingine litakalojiingiza katika
katika upelelezi wa tukio hili. Sasa wamejua; kwa
hivyo waandishi wa gazeti lazima muwe macho.
Tokea sasa kaeni katika tahadhari; lolote linaweza
kutokea. Unaonaje maoni yangu?'.
"Lo Willy, ndio maana wewe ni mpelelezi maarufu
katika Afrika. Maelezo yako yanaeleza hali halisi
kabisa. Na swali ulilomuuliza Margret kama kuna
mtu mwingine aliyeweza kuona akiweka karatasi
ndani ya mkoba, mimi nilikuwa silifikilii kabisa na
ndilo swali lililotupa mwanga. Kweli kila mtu na
kazi yake", alisifu Sherriff.
"Lakini maswali mliyouliza ninyi vile vile ni ya
maana sana, nafikiri kuliko waliyoulizwa na Polisi.
Sidhani Polisi wameishafikia hii tuliyofikia kwa
muda huu mfupi".
Mara wazo likanijia.
"Lile jambo lililokuwa linakutatanisha nimepata jibu
lake. Swali la nani aliyepiga simu kwa Mlingi akiiga
sauti ya Mantare na maneno ya Mantare aliyozoea
kuzungumza na Mlingi".
"George kiki", alijibu Sharriff.
"Kabisa, unajuwa Kiki alikuwa anaingia ndani ya
kila ofisi ya ofisa akiwa kama tarishi. Swali hili
nilimuuliza Mantare akakubali. Hivyo Kiki akiwa
jasusi aliyefundishwa, ninavyofikilia, haikuwa kazi
kumsiliza Mantare katika simu zake nyingi na
ninafikiri alifanya kila njia kusikiliza simu kati ya
Mantare na Mlingi. Hii inaonekana wazi kabisa".
"Lo tunaanza kuona mwanga sasa", Sherriff
alisema.
"Kweli tumeona mwanga, lakini ni mwanga
unaotufikisha kwenye giza nene. Maana Kiki
ambaye angetupa fununu ya watu hawa amekufa,
yule kichaa lazima ameshapotea hewani, gtumerudi
pale pale".
"Watu hawa ni akina nani na silaha hizi ziko
wapi?", niliuliza swali hili wakati naegesha gari
New Afrika.
"Hilo ndio swali gumu lakini afadhali tunajua Afrika
Kusini inahusika, maana Kiki katokea huko. Na yule
kichaa alipolewa alizungumzia Sozafrika ambayo
nasadiki ni South Afrika".
"Sawa kabisa, lazima tujuwe tunapambana na
South Afrika na haikosi shirika lao la ujasusi
'BOSS', linasaidiwa na mashirika mengine ya
ujasusi ya nchi za kibeberu. Hivyo tutakuwa na
kazi ngumu maana watu hawa nimewahi
kupambana nao ni watu hatari kabisa".
"Tumwombe Mungu atasaidia".
"Na wewe ukijisaidia", nilijibu.
Wote tukacheka na kutoka ndani ya gari. Ilikuwa
saa kumi na moja. Hivyo kabla hatujavuka
barabara nilionelea nifike ofisini kidogo halafu
niende nyumbani.
"Sherriff mimi nafika nyumbani kidogo, nitakuona
saa kumi na mbili kamili".
"Sawa nitakusubiri hapa duka la kahawa".
oke basi saa kumi na mbili".
Niliingia ndani ya gari na kuondoka. Nilipofika
ofisini nilimkuta Eddy na vijana wengine. Linda
alikuwa ameshaondoka.
"Eddy kuna mtu mmoja anaitwa George Kiki,
alikuwa akifanyakazi kwenye ofisi ya Kamati ya
ukombozi kama tarishi?, hapa aliingia kama
mkimbizi baada ya kutoroka Afrika Kusini. Alifika
ofisi za chama cha SANP, ambao walimpeleka
kwenye Kamati ya Ukombozi waweze kumsaidia
angalau kazi yoyote. Inawezekana hana kisomo cha
kutosha. Nataka ukague habari hii kwa kutumia njia
zetu za kawaida. Unaweza kuwajulisha makomredi
wetu kule Soweto, nadhani watakuwa na maelezo
kamili. Habari hizi nazitaka haraka. Kila kitu,
aliingiaje hapa alikwendaje kwenye ofisi za SANP
alikuwa anaishi namna gani, nani walikuwa rafiki
zake nk. wewe unajua".
Eddy aliyekuwa anachuku maelezo haya alijibu.
"Atashughulikiwa bosi, usiwe na wasiwasi".
"Chifu yuko?".
"Kaondoka".
"Haya asante, usitoke mpaka nitakapokujulisha
tena".
"Mimi nipo".
Ndio sababu nilimpenda mtoto huyu. Nidhamu yake
kwangu ilizidi ya mdogo wangu ambaye tumetoka
ndani ya tumbo la Mama Willy. Niliingia ndani ya
gari nikaelekea zangu Upanga.
Niliposimamisha gari mbele ya mlango, moja kwa
moja macho yangu macho yangu yakaangukia
kwenye kitu kilichokuwa kwenye ubao wa juu ya
mlango mkubwa wa kutokea nje. Nilitoka nje ya
gari haraka haraka nikiwa tayari kwa mapambano.
Nilikuta ni kisu chenye mpini mwekundu kama kile
tulichokikuta kwenye kifua cha maiti Kiki; ncha
yake ilitumiwa kama kipini cha kubandika kipande
cha karatasi pale mlangoni.
Niliking'oa nikachukua karatasi na kusoma
yaliyobandikwa hapo yalisema.
Willy Gamba, kama unathamini maisha yako
achana na hao watu wa gazeti la Afrika. na kama
ni rafiki zako waambie waondoke hapa mjini
tunawapa mpaka saa kumi na mbili jioni wawe
uwanja wa ndege. Vinginevyo yaliyompata Kamara
Frank yatawapata na nyinyi. Hili ni onyo kali na si
mchezo. Shughulika na mambo yako usishughulike
na mambo ya watu wengine. Wapo wenyewe
wanaohusika waachie. Nasema tena saa kumi na
mbili jioni leo wawe uwanja wa ndege na wewe
baada ya kuwafikishia habari hizi tusikuone
unashughulika zaidi ya kazi yako ya kawaida ya
AIA Subiani.
Kwanza nilicheka maana niliona kazi sasa inaanza.
Hii inaonyesha upelelezi wetu ulikuwa umewashitua
kuliko wa Polisi. Nilijua yule kichaa alifanya kazi
yake vizuri sana, maana ni yeye tu
aliyetufahamisha kwa majahiri wenzake. Hiki kisu
chenye mpini mwekundu ilimaanisha damu. Nami
niljua damu imeanza kunuka.
Nilifungua mlango nikaingia ndani, nikakoga haraka
haraka kisha nikabadilisha nguo nilifungua sanduku
langu la silaha na kuchukua bastola zingine mbili
kwa madhumuni ya kuwapa Sharriff na Verokika
kwani hakukuwa na mchezo tena, maana upatapo
onyo toka kwa watu kama hawa huwa hawatanii.
Kisha niliinua simu na kupiga kituo cha Polisi cha
Salendar Bridge.
"Hallo kituo cha Polisi hapa".
"Sikiliza, nenda Kinondoni Hananasifu, Estate
kwenye nyumba ndogo ndogo za shirika la Nyumba
nambari IIC utakuta kuna maiti ambayo ina zaidi
ya masaa ishirini na nne", kabla hajatamka neno
nilikata simu. Niliangalia saa yangu muda ulikuwa
umekimbia na ilikuwa saa kumi na mbili kamili.
Niliingia ndani ya gari nikakimbilia New Afrika.
Nilipoingia duka la kahawa sikumwona Sherriff
nikapata wasiwasi. Nikaenda mapokezi kuuliza
wakaniambia aliacha habari kuwa amekwenda
dukani mara moja nimsubiri. Nilirudi nikasimama
nje pale magari yanapoleta watu New Afrika
yanapozungukia. Niliangaza huku na huku na mara
nikamwona Sharriff anakuja akiwa anavuka tawi la
Benki ya nyumba. ghafla alipokuwa anataka kuvuka
barabara ilitokea gari sijui wapi ikapiga breki,
wakatoka watu wawili haraka kama umeme,
wakamvuta Sharriff ndani ya kiti cha nyuma cha
gari, na gari hilo likaondoka tena kama umeme.
Kitendo hiki hakikuchukua hata nukta tano.
Watu wote waliduwaa wasijue cha kufanya, lakini
mimi Willy nilijua la kufanya. Nilikimbia kwenye gari
Eddy alilokuwa amekodi na kuliacha New Afrika.
Kwa vile alikuwa ameliegesha vizuri niliingia na
kuondoka kama umeme. Nilikuwa nimeona lile gari
linakata kulia kutoka barabara ya Azikiwe kuingia
Azania Front. Nilipoingia Azania Front niliona gari
lao linafika kwenye ofisi za NASACO nikacheka.
ITAENDELEA
 
NJAMA
SURA YA TANO
TWATOANA JASHO
Niliongeza gari moto ili wasije kunipotea. walikata
kulia wakaingia mtaa wa Railway, nilipoingia mimi
mtaa huu wao walikuwa wamefika kwenye
mzunguko wa 'Clock Tower' na kuingia mtaa wa
Nkurumah.
Kwenye mtaa huu wa Nkurumah niliwakaribia
kabisa, nikiwa nimeacha gari mbili tu kati yangu na
wao. Niliona mmoja katika gari lao akitoa kichwa
nje na kuangalia nyuma, nadhani wanadhani
nitawafuata na gari langu ambalo wanalijua sana.
Lakini hawajui Willy ni mtu wa namna gani. Wakati
huo nilikuwa naendesha gari aina ya Fiat 132 GLS,
na si Colt Gallant Sports kama ambavyo walikuwa
wanafikiria.
Walikwenda moja kwa moja na kushika barabara
ya Pugu. Walipofika kwenye njia panda ya barabara
ya chang'ombe na Pugu, walikata kushoto na
kuingia barabara ya Chang'ombe. Saa hizi magari
hayakuwa mengi hivyo kila gari lilikwenda kasi.
Nilikuwa na bahati kuwa magari yale mawili
yaliyokuwa kati yangu na wao nayo yalikata na
kuingia barabara hiyo hiyo kuzidi kunificha.
Walipofika kwenye sehemu ambayo barabara ya
Mbozi inagongana na Chang'ombe walikata kulia
na kufuata barabara hiyo. hizi gari mbili mbele
yangu zilionyesha kuwa zilikuwa zinaendelea na
barabara ya Chang'ombe. Nilipunguza mwendo ili
wasije wajanitambua. Mara nilisikia wanapiga honi
ya namna ya pekee kabla ya kufika kwenye jengo
la Kampuni ya rangi ya Sadolins.
Ghafla lango la uwa la bohari moja lilifunguliwa na
bila hata kupunguza mwendo, gari hii ilikata
kushoto na kuingia ndani na hapo lango
likafungwa. Mimi nilipitiliza kama kwamba sina
habari na watu hawa. Ilikuwa inakaribia saa moja
za jioni, hivyo giza lilikuwa limeanza kuingia.
Nilisimamisha gari langu kama mita mia mbili hivi,
nikaanza kurudi haraka kwa miguu.
Bohari hili ambalo lilikuwa limezungukwa na ukuta
wa matofali ya saruji, lilikuwa limeandikwa
'Mamlaka ya Pamba'. Mimi nilishangaa sana kwani
sikujua hii ni maana gani. Ukuta wa uwa huu
ulikuwa na urefu usiozidi futi kumi na mbili, hivyo
kwangu ukuta kama huu kuupanda ni kazi ndogo.
Nilikwenda kwenye upande wa lango kubwa,
nikazunguka pembe ya kushoto ya uwa huu. Ukuta
huu ulikuwa unapakana na ukuta wa bohari
nyingine la namna hiyo hiyo kwa upande huu wa
kushoto.
Nilikwenda kama hatua tatu hivi kwenye nafasi hii
ya kati ya mabohari haya, nikavua viatu, nikarudi
nyuma kidogo halafu nikaurukia huu ukuta na
kuukwea huku mikono yangu ikikamata juu yake.
nilivuta mwili wangu wote kimya kimya kama paka
nikachungulia ndani ya uwa.
Pale karibu na mlango nilimwona mtu amevaa koti
refu la khaki rangi nyekundu lililokuwa linavuka
magoti yake kidogo huku ameshikilia bunduki ya
aina ya 'SMG' na akiangalia mlangoni. Bila kufanya
hata chembe ya kelele nilivuta mwili wangu wote
na kutambaa kama nyoka juuya ukuta huu
uliokuwa na upana wa futi moja. Nilitambaa mpaka
nikawa karibu kabisa na mtu huyu kwa juu yake
bila yeye kufahamu. Nilijirusha chini na kufanya
kishindo kidogo nae akageuka. Mimi nilikuwa tayari
nikamkata karate ya shingo kabla hajajua nini
kinamjia. Akazilai. Nikamshikilia na kumlaza chini
taratibu. Muda kitambo aloikufa.
Nilimvua lile koti lake nikalivaa mimi, halafu
nikamnyanyua tena nikamlalisha chini na
kumwegemeza kwenye ukuta. Nilichukua bunduki
yake ambayo ilikuwa imejazwa risasi, nikafurahi
sana kishika silaha namna ile. Mimi nikiwa na
silaha namna ile hata likija jeshi la watu mia
hawaniwezi. Nilijidhatiti tayari kwa mapambano
zaidi nikanyata kwenda nyuma ya jengo la bohari
ambako niliamini kuna mlango mwingine. Nilipofika
kwenye pembe ya ukuta wa kushoto nilichungulia.
Niliona kuna mlango wa mbele wa mlango
alisimama mlinzi mwingine akiwa amevaa
sawasawa na yule wa kwanza; koti refu jekundu.
Alikuwa nae ameshika bunduki ina ya 'SMG',
niliona anafungua mlango anasema kwa sauti kali
"Fanhyeni haraka bwana, kama hataki kueleza si
niambieni mimi akaonane na babu zake huko
ahera". Alirudisha mlango akaangaza huku na
huku. Kutokana na maelezo yake ni kwamba
Sherriff alikuwa anaswalishwa na majahiri na bila
shaka alikuwa akipata kipigo kikubwa.
Nilitumbukiza mkono ndani ya mifuko ya koti
nililovaa nikakuta mna sigara na hamna kiberiti.
Wazo likanijua nikamfanyia yule mlinzi 'sss'
aligeuka akaniona akidhani ni mwenzake,
nilimuonyesha sigara na kuwa nataka moto. Bila
kusita akaja akatoa kiberiti na kwa ajili ya giza
sasa hakuweza kunitambua sababu ya lile koti.
Aliponyoosha mkono kunipa kiberiti. Kama radi
nilimrukia na kumpiga karate ya mikono miwili
shingoni. Sikuwa na haja ya kumwangalia maana
nilijua kwa kipigo hicho hawezi kuishi. Nilimvutia
upande huu wa kushoto na kumwegemeza kwenye
gari lao. Nilichukua bunduki yake iliyokuwa na
ukanda mrefu nikaingika begani na kuiweka
mgongoni.
Sasa njia ilikuwa wazi kwenda mpaka mlangoni,
kwa kutokana na ujuzi wangu wa kuiga sauti ya
yule mlinzi wa nje kwa maneno yake aliyosema
mimi nilisema. 'Vipi hajasema lolote?," nikiwa
nimefungua mlango kidogo na kuchungulia ndani.
Bohari lilikuwa limejaa robo tu ya marobota ya
pamba. Sherriff alikuwa ameshikwa na watu wawili
na mmoja alikuwa amebeba bao akimtandika
tumboni kwa nguvu sana.
"Sema nyie si waandishi wa magazeti ila ni
wapelelezi, ndio".
"Yote ya kweli nimeshaeleza ".
Kabla hajaanza kumpigab tena nilisema. "Mmoja
wenu aje hapa, mimi mnanijua hivyo hatachukua
dakika kabla hajasema uweli wake".
Shomvi alikuja akikimbia, nikamfungulia mlango na
kurudisha mara moja. Alipoangalia ba kutambua
mimi si Luis akataka kupiga kelele lakini nilimwahi
karate ya katikati ya kichwa akafa bila kelele. Watu
wa mle ndani waliokuwa wamemshikilia Sherriff
walikuwa hawana bastola mikononi ila zilionekana
kwenye mapaja. Nilifungua mlango ghafla SMG
mkononi nikamwahi mmoja wao kabla hata
hawajaelewa nini kinatokea.
"Ukijaribu chochote umekufa", nilisema kwa sauti
ya kutetemesha.
Sherriff alishangaa kuniona akaruka ile maiti
akasimama upande mwingine. Niliona ile SMG ya
pili nikampa, akatabasamu. Jinsi alivyoijaribu
mkononi nilikua huyu mtu anajua kuitumia.
"Chukua hizo silaha zake", Sherriff alimkagua
akatoa bastola mbili zenye sailensa na visu viwili
vyenye mpini mwekundu.
"Ah, ni wakati wako sasa kujibu maswali yetu,
nyinyi ni nani", nilimwuliza.
"Mimi sijui, mimi niliajiriwa tu leo hii asubuhi na
Kimkondo, huyu uliyemwua hapo chini, kuwa kuna
kazi ya kumkamata mtu mwenye habari ambazo
wakubwa wake wanataka. Pesa tulizolipwa zilikuwa
nyingi, shilingi elfu kumi kwa kila mtu kwa kazi ya
masaa machache tu nami nikakubali, kusema
ukweli sijui lolote".
"Yeye Kimkondo anafanya kazi gani?".
"Yeye ni jambazi tu anayepewa kazi ya ujambazi
hapa na pale".
Kutokana na maelezo ya huyu mtu nikajua
anasema kweli. Nilijilaumu kumwua Kimkondo
maana yeye huenda angetupa mwanga zaidi. Lakini
hii yote inaonyesha jinsi majahiri hawa yalivyokuwa
yamepanga ujahili wao kwa ufundi.
"Lo Willy asante sana".
"Sahau", nilimjibu kwa mkato.
Ile sura ya kikatili ilikuwa tayari imekuja usoni
mwangu. Katika hali kama hii sura yangu
hubadilika na kuwa mtu tofauti kabisa. Hivyo
nilipomwambia Sherriff sahau niliona anashituka
kidogo.
"Twende zetu tutoke hapa Sherriff, huyu nitajua
mahali ya kumpeleka".
Tulimtangulia, tukafungua mlango wa bohari tayari
kurudi mjini. Tulipokuwa tumefika kwenye kona
niliyotokea, tukasikia honi ya gari ya namna ile ile
waliokuwa wamepiga hawa majahili wa kwanza.
"Sherriff na wewe mtu mjifiche nyuma ya hili gari,
kwa vile mimi nimevalia koti lao ambalo naona
ndicho kitambulisho chao nitakwenda kufungua
lango, unayo ile bastola uliyochukua kwake?".
"Ndio".
"Basi akifanya ushenzi unajua la kufanya; maiti
hazisemi'.
Niliwaacha nikakimbia mpaka kwenye lango
nikafungua. Gari aina ya VW Kombi iliingia imejaa
watu wamevalia makoti kama langu, Gari hili
lilisimama nyuma ya lile gari la kwanza. Milango
ikafunguliwa wakaanza kutoka. Mimi nilikuwa
tayari na SMG yangu.
"Rudini ndani......." niliona yule mtu tuliyekuwa
tumemshika ameruka juu ya gari na kutoa onyo,
lakini kabla hajamaliza Sherriff alimlamba risasi ya
kichwa akaanguka juu ya gari, mimi nikajua tayari
mambo yametibuka, hivyo sasa ni kazi.
Dereva wa gari hii na watu wengine waliokuwa
bado ndani ya gari walifunga mlango ili waondoke.
Wale waliotoka nje walianguka chini na kutoa
bastola tayari kwa mapambano. Mimi nilikuwa
nimeishavua koti nimerukia ukutani na tayari SMG
mkononi. Nilikuwa nimelalia tumbo juu kabisa ya
ukuta. Lile gari lilipopiga moto, nililenga mlango wa
dereva na kuachia risasi mfululizo kama mchezo.
Sherriff alikuwa bado kimya hajaanza shughuli.
Wale watu watano waliokuwa wametoka ndani ya
gari nao walikuwa wametambaa upande mwingine
wa kombi. Kumbe mmoja wao aliniona kule juu
baada ya kuona risasi zilizoua wenzake zikitokea
juu. Mimi nilikuwa bado sijamwona hivyo akainuka
kunimaliza. Lakini kumbe Sherriff alimwona kabla
hajafyatua risasi, akamwahi. Nilipomwona Sherriff
akanionyesha ishara. Alikunja kiganja halafu
akainua kidole kimoja kuonyesha kuwa ni watano
na mmoja tayari kafa.
Mimi nilijirusha chini toka ukutani na kujiviringisha
huku nakoswa koswa risasi za maadui.
Niliposimama huku nikikimbia zigizaga na wakati
huo nikipiga risasi ovyo kuwazuia wasipige. Nilifika
mlango na kufungua kama ninakimbia nje. Wale
kwa woga wao walipoona hivi nao walianza
kukimbia kuwahi mlangoni.
Kumbe ndipo walikuwa wanampa fursa Sherriff
kuwachukua mmoja mmoja vizuri sana. Na mimi
ghafla nilijitokeza tena na kumimina risasi kwa
wawili waliokuwa mbele. Bahati nzuri Sherriff
alijitupa chini la sivyo ingetokea ajali kwani yeye
alifikiri nitawasubiri nje hivyo naye alikuwa
anawafuata nyuma.
"Kazi nzuri Sherriff, la sivyo ningekuua, pole sana",
nilimpa mkono.
"Hali kama hizi nimezizoea sana hivyo huwa niko
tayari katika tahadhari kila mara kwani lazima
kama huna uhakika mwenzako atafanya nini
baadaye tegemea lolote", Sherriff alijibu.
Tulikimbia kutoka pale mpaka kwenye gari langu.
Tuliingia na kuwasha gari moto na kuelekea zetu
mjini.
"Mimi nilijua ndio mwisho wangu", Sherriff
aliniambia.
"Kwa nini?".
"Maana walivyonivamia hata nilishindwa la kufanya
halafu nilijua wewe utakuwa unanisubiri New Afrika
na kumbe mimi nimeshauawa. Na kweli
wangeniua".
Alitoa shati lake kuonyesha uvimbe mbaya sana
kwenye tumbo lake.
"Nasikia maumivu ya ajabu. Watu hawa ni katili
sana".
"Pole sana. Jambo la kusikitisha ni kwamba imebidi
tuwaue wote. Hivyo bado tumerudi pale pale;
hatujui lolote, isipokuwa tu kwamba watu hawa ni
majahili wa hatari sana wanaovaa makoti mekundu
na bunduki wanazotumia ni SMG za kichina,
bastola za kirusi zenye sailensa. Zaidi ya hapo
bado tuko mbali sana na ukweli wa mambo. Ila
kinachonifurahisha ni kwamba sasa watashtuka
baada ya mapambano haya ambamo tumeua watu
wao karibu kumi na tano. Kule kushtuka ndiko
kutatusaidia maana lazima watahaha na kufanya
makosa".
"Sawa kabisa. Lakini mimi nataka kujua jinsi
ulivyojua nimekamatwa na namna ya gari
umeweza kuniokoa. Maana mimi sikuamini
nilipokuona, nilidhani huenda ni malaika kashuka
toka mbinguni katika sura yako".
Tukiwa bado tunaelekea mjini nilimweleza jinsi
nilivyofanya.
"Lo ndio sababu wewe ni mpelelezi namba moja
katika Afrika; mimi sasa nadhani hata katika dunia.
Tukirudi London salama nitailisha komputa
maelezo zaidi juu yako tuone itakuonyesha katika
nafasi gani katika wapelelezi wa ulimwengu".
Mimi nilicheka tu sikujibu kitu.
"Na kule kubadili gari kulisaidia sana maana
walipochungulia na kulikosa gari lako walinidhihaki
kwa kusema kuwa sasa nitakufa peke yangu hata
rafiki zangu hawatathubutu kuja hata kama
wangeniona wakati ninakamatwa".
"Mimi ni mjuzi zaidi yao; lazima tuzidiane maarifa".
Tuliingia barabara ya Independece Avenue.
"Nitakupeleka kwa daktari wangu hapa Zanaki
Street, na utalala hapo. Nafikiri kesho utakuwa
katika hali nzuri, kwa leo lala hapo usirudi New
Afrika ili daktari aweze kukupa matibabu kwanza.
Nitakuja kukupitia asubuhi".
"Sawa wewe ndiye bosi", Sherriff alijibu.
Nilimpeleka kwenye zahati ya rafiki yangu Dk.
Kiluwa na kumweleza amtibu na malipo yatalipwa
na AIA. Nilimwacha nikawaahidi kuwaona asubuhi
yake.
ITAENDELEA
 
NJAMA
SURA YA TANO
TWATOANA JASHO
II
"Eddy nafikiri unaweza kwenda kupumzika. Acha
vijana wa zamu waendelee, maana kesho tunaweza
kuwa na kazi nyingi sana".
"Asante tutaonana asubuhi", alijibu huku
akikusanya kusanya karatasi zake.
Mimi niilimuaga nikaondoka zangu kuelekea New
Afrika tayari kuonana na Veronika. Nilipofika New
Afrika nilikuta duka la kahawa limejaa watu na ile
sehemu ya Patio Baa ndio usiseme, maana vijana
walikuwa wamejazana wakifurahia saa zao za
baada ya kazi.
Nilishikashika mfukoni, nikachukua funguo za gari
mkononi nikaelekea kwenye gari langu, niliona Vero
alikuwa bado hajafika kwani hamkuwa na mtu
ndani ya gari. Nilifungua mlango wa upande wa
dereva ili nikae nimsubiri, maana nilijua
asingechukua muda mwingi.
Nilipoingia na kukaa kitini na kuanza kutelemsha
kioo, nilisikia kama kuna kitu kwenye viti vya
nyuma vya gari langu. Nilipotaka kugeuka
kuangalia nilisikia sauti ikisema. "Usigeuke la sivyo
utakuwa ndio mwisho wako. Washa gari ondoka,
na ufuate maelezo yangu".
Nilisikia mdomo baridi wa bastola ukigusa shingo
yangu.
"Sawa mzee", nilijibu huku nikijifanya kama sijali.
"Siyo mzee, sema wazee. Tuko wawili na wote tuna
bastola na tunajua kuzitumia hivyo usijaribu kitu
chochote cha kuleta matatizo".
"Mimi sina wasiwasi, maana sijui kwanini natekwa
nyara, kama nia yenu ni gari niambieni niwaachie.
Mimi ni mfanyabiashara nitapata gari nyingine,
kwangu pesa si tatizo".
"Funga domo lako, sisi hatuna haja na gari lako
wala pesa yako, sisi tuna pesa kuliko wewe".
Kabla sijasema lolote aliniambia. "Kata kushoto
ingia Independence Avenue, halafu ukifika 'Clock
Tower' ingia mtaa wa Railway halafu shika
barabara inayopita kwenye kituo cha polisi wa
usalama barabarani, halafu ukifika kwenye
mzunguko ingia kushoto, fuata barabara ya Kilwa
mpaka nitakapo kueleza tena. Nasema tena ujanja
wowote utakutokea puani".
"Usiwe na wasiwasi", nilijibu kiume.
"Nyamaza", alijibu kwa sauti ya ukali.
Nilijilaumu sana kwa kutochukua tahadhari zaidi
kwa watu hawa.
Nilifikiria kama naweza kufanya lolote sasa
nitakuwa kwenye upande wa hasara hivyo nikakata
shauri la kufuata maelekezo mpaka mwisho ndipo
nione la kufanya. Maana nafikiri kama nia yao
ilikuwa ni kuniua wasingesita, walikuwa na mwanya
mzuri sana nilipoingia bila tahadhari ndani ya gari.
Nilijua nia yao si kuniua ila kuna habari
walizozitaka. Nilimfikilia Veronika nikajua
atahangaika sana kwani hatanikuta halafu hatajua
Sherriff aliko.
Tulipokaribia uwanja wa Sabasaba aliniamuru
nikate kushoto kwenye njia inayoelekea kwenye
ofisi mojawapo za reli ya Tazara ya Kurasini.
Tulipotelemka kidogo aliniamuru nikate kulia na
kuingia kwenye mlango wa pembeni wa uwanja wa
Monyesho ya Sabasaba.
Tulipofika kwenye mlango huu aliniamuru nipige
honi. Nilipopiga honi mlango ulifunguliwa. Taa
zangu zikamwulika mlinzi aliyevaa joho jekundu,
nikajua mara moja ni nani nimepambana nae tena.
Tena huyu mtu aliongeza na kofia nyekundu juu.
Nilishangazwa sana na mbinu za watu hawa,
maana sehemu zo walizokuwa wanazitumia kama
kambi zao za kufanyia uovu zilikuwa sehemu za
kiserikali. Hii ilionyesha jinsi mbinu za watu hawa
zilivyozidi kiwango.
"Ingia ndani moja kwa moja, fuata barabara mpaka
nitakapokuabia simama", niliamriwa.
Uwanja ulikuwa kimya kabisa. Giza lilitanda kote
ila taa za gari langu peke yake. Tulikwenda mpaka
katikati ya vibanda.
"Simama hapa, zima taa na telemka taratibu.
Ukifanya makosa usinilaumu", alinieleza. Nilipozima
taa tu niliona vivuli vya watu vikinyata polepole
kuja kwenye gari. Nilipokanyaga nje tu gari likawa
limezungukwa na watu watatu. Wale waliokuwa
ndani ya gari walitelemka.
"Mmemleta?", mmoja wa wale waliozunguka gari
aliuliza.
"Ndio", alijibu yule mtu aliyekuwa ananipa amri".
"Kazi nzuri, haya twendeni".
Yule mtu aliyezungumza alitangulia mbele mimi
nikaambiwa nimfuate huku nimezingirwa na watu
wanne. Yaani wale wawili walioniteka, na wengine
wawili waliokuwa wamebeba bunduki aina ile ile ya
SMG, ilionekana hawa watu walitumia sana aina hii
ya bunduki.
Niliongozwa moja kwa moja mpaka kwenye
kibanda kimoja katikati kabisa ya uwanja wa
maonyesho wa Sabasaba. Nilikumbuka kuwa
kibanda hiki kilikuwa kinatumiwa na nchi za
Zambia katika maonyesho ya Kimataifa. Mlango
ulifunguliwa tukaingia. Ndani tulimkuta mtu
mwingine anavuta mtemba amekaa kwenye kiti
huku akitabasamu. Watu hawa wote walivalia
majoho mekundu. Na hawa wanne niliowakuta
huku kiwanjani walivaa kofia nyekundu isipokuwa
wale walioniteka ndio hawakuwa na kofia.
"Karibu Willy Gamba, keti chini kwenye kiti",
aliniambia yule mtu tuliyemkuta ndani.
"Asante, mimi ningependa kusimama", nilijibu.
"Mimi sitaki kukukarisha kwa nguvu, lakini kama
unaona ni lazima nifanye hivyo ninao uwezo, Willy",
aliniambia taratibu huku wale watu wengine
wakinisogelea. Niliona hakuna haja kuchachamaa
hapa hivyo niliketi kwenye kiti.
Chumba hiki kilikuwa kimewekwa fenicha nzuri
sana, hata nikashangaa saa ngapi watu hawa
waliweza kuaandaa chumba hiki kama ofisi na
huku uwanja huu siku zote unalindwa.
"Romano na Charles mnaweza kwenda nje kusudi
muwe tayari kukabiri jambo lolote linaloweza
kutokea hapo nje wakati nikiwa na mazungumzo
mafupi na Willy hapa", alitoa amri polepole kiasi
kwamba ungeweza kuamini kuwa ni mtu mzuri
sana, lakini macho yake yalionyesha uovu usio
kifani.
NIlifurahi sana kwani nilijua kuwa sasa ninaonana
na mtu wa maana katika kundi hili la majahili.
Macho yetu yalipokutana ana kwa ana mara moja
tukatambuana, maana huyu alikuwa jasusi wa hali
ya juu. Sisi tuko kama mbwa tunajuana kwa
harufu. Wale watu wawili wenye SMG walitoka nje
tukabaki na wale watu walioniteka nyara, yule mtu
aliyetupokea na huyu mtu tuliyemkuta humu ndani.
Walipotoka nje waliufunga mlango.
"Bwana Gamba, mimi ni mtu nisiyependa kuumiza
kwa sababu mimi huwa sijisikii vizuri nikiona mtu
anaumizwa. Lakini nikilazimika kufanya hivyo, basi
mimi hufumba macho. Nisingependa nifumbe
macho kwako kwa hiyo naomba sana uwe mtu
mwungwana katika kujibu maswa yangu".
"Nadhani ungependa kujua sisi ambao tuko hapa ni
nani, sisi ni WANAMAPINDUZI WAPINGA
MAPINDUZI".
"Wanamapinduzi wapinga mapinduzi maana yake
nini?. Sikuelewi.
"Ni kwamba sisi tunapinga watu wanaojiita Wana
mapinduzi, wanaofikiri wataleta uhuru Afrika Kusini
kwa njia ya vita. Sisi ni wanamapinduzi ambao
tuna imani kuwa tutaleta uhuru Afrika Kusini kwa
mazungumzo bila kuua mtu hata mmoja. Sasa
swali langu ni hili; Wewe na rafiki zako mna nia
gani katika kupeleleza upoteaji wa silaha?, Kwanini
msiwaachie watu wanaohusika?".
"Mimi si mwana siasa hivyo unayonieleza juu ya
namna gani uhuru utakavyopatikana huko Afrika
Kusini sina haja ya kujua. Lakini wageni wangu ni
waandishi wa habari na kumetokea hapa mjini Dar
es Salaam wizi wa silaha uliotingisha
ulimwengu.Hivyo wakiwa waandishi lazima
wapeleleze wapate kueleza ulimwengu mambo haya
yametokeaje. Sidhani kama kitu hocho ni dhambi.
Ni kitu cha kawaida". Nilimjibu taratibu nikijaribu
kupima hali ndani ya chumba hiki.
"Imeonekana hawa waandishi wa habari
wamekwenda zaidi ya kiwango cha upelelezi wa
kigazeti, kiasi cha sisi kuamini kuwa si waandishi
wa gazeti ila wapelelezi. Jioni hii kama huna habari
rafiki yako Sherriff ameua vijana wangu zaidi ya
kumi. Mtu mmoja, Willy, mtu mmoja?, siamini
kabisa kuwa yeye ni mwandishi".
"Swali langu la pili nataka nujue yeye ni nani na
sasa hivi yuko wapi?. Ukijibu maswali haya
nitakuachia, usipojibu jua ya kwamba kesho
huioni".
"Mimi ninavyojua ni kwamba yeye ni mwandishi wa
habari, kama ni mpelelezi haya ni maneno yako,
Kampuni yangu ni wakala, hivyo nilivyofanya
mkataba na gazeti la Afrika na watu hawa
walipokuja nilijuwa ni waandishi. Pili sijui aliko
sasa hivi, tuliachana saa nyingi na tulipanga
tuonane saa kumi na mbili New Afrika Hoteli lakini
sikumkuta.
Baada ya kufikiri kidogo akasema, "La hasa,
unajua".
"Sijui".
"Au unataka mpaka nifumbe macho".
"Hata kama ukifumba macho, sijui".
"Lucas na Moshi hebu mmwonyesheni huyu namna
ya kujibu", alisema tena pole pole.
"Simama", alisema Lucas.
Sikusimama. Basi walinijia wote pale kitini kama
faru, na mimi Willy tayari nilikuwa nawashwa
kumwonyesha huyu mkubwa wa kuwa Willy
hasukumwi ovyo.
Kama umeme nilisimama upesi na kukwepa ngumi
ya Lucas na kwa sababu alikuwa ameitupa kwa
nguvu sana alipepesuka mimi nikampiga teke
kwenye mapumbu akalia kama nguruwe na wkati
huo shoto langu lilimfikia Moshi singoni nae
akapepesuka mpaka chini. Yule mtu mwingine
aliyetuongoza toka mwenye gari alitoa bastola
yake lakini mimi niliona hatua hiyo nikaruka upande
mwingine wa chumba na risasi zikanikosa, na
wakati huo mlango nao ulifunguliwa na mtu
aliyevaa joho jekundu na kofia nyekundu akiwa na
SMG mkononi akampiga risasi ya mgongo kabla
hajanimaliza pale niliporukia, na yule mtu akafa
pale pale. Huyu mtu wa SMG alimimina risasi kwa
wale wengine waliokuwa wanajaribu kutoa silaha
zao na kuwamaliza hapo hapo. Mimi katika
harakati za kujiokoa niona yule mkubwa wao
anaruka nyuma ya kiti, nikatoa bastola yangu,
lakini nikawa nimechelewa, kwani nyuma ya kiti
chake kulikuwa na mlango mdogo kimo cha urefu
wa kochi. Hivyo alijitumbukiza.
"Anaondoka huyo Willy", nilisikia sauti nya Veronika
akimimina risasi pale kwenye mlango lakini yule
mtu alikuwa anajua nini anachofanya, hazikumpata
akakimbia nje.
Mimi nilishangaa sana kumwona Veronika katika
joho jekundu na kofia nyekundu na SMG mkononi
amefika wakati kabisa uliohitajika kuniokoa.
"Oh Vero mkombozi wangu, umetokea kama
malaika vile".
Alitupa bunduki akavua kofia na joho, haraka hara
akaja akanirukia shingoni na kuanza kunibusu,
kisha akaniachia.
"Tutoke hapa mpenzi, nitakueleza baadae",
alininong'oneza.
Tulitoka ndani ya banda hilo na kusikia gari
linaondoka.
"Mshenzi amepona", Veronika alisema.
"Iko siku yake", nilijibu.
Niliokota bunduki mbili pale nje. tukaenda kwenye
gari letu tukaziweka ndani. Tukawasha gari na
kuelekea mjini. Tulipofika Kilwa Road Veronika
alianza kunisimulia,
ITAENDELEA...
 
Back
Top Bottom