Riwaya: 'Njama'

Riwaya: 'Njama'

NJAMA
SURA YA NANE
USIKU WA HEKAHEKA
Tulipofika Kilimanjaro Hoteli ilikuwa yapata saa
tatu kamili. Tulipokuwa njiani kuelekea Kilimanjaro
nilimweleza Eddy mambo yote niliyokuwa nimepata
toka kwa Zabibu, mambo ambayo hata yeye
alisema yalionyesha ufumbuzi wa jambo hili kwa
mtu mwenye kufikiri. Tuliingia hotelini tukapanda
lifti iliyotushusha orofa ya pili. Tulipotoka ndani ya
lifti mara ile hali ya tahadhari ilituingia. Mimi
nilitoa bastola yangu nikaiweka tayari na Eddy
akafanya vile vile.
Tulipofika mlango wa chumba namba 206 tulikuta
umefungwa, niligonga nikiwa nimesimama upande
kabisa. Niligonga mlango mara mbili haraka
haraka, halafu nikatulia kidogo kisha nikagonga
tena, kwani hivi ndivyo Veronika alikuwa
amenielekeza namna ya kujitambulisha lakini
sikusikia kitu. Nilimonyesha ishara Eddy abane
ukutani wakati mimi nafungua.
Nilifungua mlango ghafla. Tishio nililolikuta
sijawahi kulipata tena, kwani Veronika alikuwa
amelala kwenye sofa na kisu chenye mpini
mwekundu kikiwa kimemwingia juu kidogo ya titi la
kushoto. Kidogo ningezimia lakini nilijikaza
nikakimbia pale kwenye sofa huku nikikanyaga
maiti za watu wengine hapo chumbani.
Veronika alikuwa bado ameshikilia mkono wa simu
mikononi mwake. Nilipomfikia nilimkuta bado yuko
hai. Wakati huo Eddy nae alikuwa ameingia akanipa
glasi ya whiski.
"Bosi jikaze, mnyweshe hii whiski mimi naita gari la
hospitali"'
Nilimnywesha Veronika kisha nikamtingisha
akafunua macho akapata fahamu kidogo.
"Vero, Willy hapa, niambie nani amefanya hivi".
"Walikuja.... watatu... nikapam...bana ...nikawaua
nikakupigia simu.... ku...ku...kumbe walikuwepo...
wengine ...wawili ... mmoja ... akamwita ... Shu...
Shu...Shuta muue.... mimi kugeuka ...
akanichoma... ki... kisu... nikawahi ...kumpiga yule
mwingine ...kwa... akafa... Shuta...
akakimbia ...nika...
Hakuweza kusema tena. Nikamwongeza whiski na
kumtingisha.
"Oh Vero, nimeita gari la wagonjwa na mganga
anakuja sasa hivi utapona tu.
"Si...siwezi...nitak-
ufa...nimekufa...ame...moyo...Willy
na...nakufa...na...ku...penda ...hakuna tena...
mwanamume... niliye... mpenda...kama wewe.
Ni...nimefurahi...kukuona ...ma...mara...
ya...mwisho...nikifa ...kwa ajili ya Afrika...
siogopi...kufa...kwani nimekufa ...kwa
sa...sabab...bu...nzuri.
Ende...le..za ...ma...pa...mba...no...
Willy ...Mungu...a...ku...-
sai...die...uni...ku...pi...zie...kisasi Afrika.
Ni...busu...na... ku...
Nilijua Veronika hawezi kuchukua dakika moja
zaidi, niliweka midomo yangu kwenye midomo yake
na kulamba damu yake ambayo sasa ilikuwa
inatoka mdomoni.Alitabasamu na macho yake
yakang'ara kiasi ambacho sikuwahi kuyaona
yanang'ara vile halafu akayapepesa akafariki.
Alikufa huku akitabasamu.
Sikuwahi kulia na kupata uchungu kama wakati wa
kifo cha Veronika. Nilijilaumu. Kama ningekwenda
nae kwa Zabibu asingekufa.
Eddy alinikuta nabubujika machozi kama mama
anayemlilia mtoto wake wa pekee.
"Bosi jikaze", Eddy alinishauri.
"Washenzi hawa, nduli hawa, watanitambua.
Kwanini Mungu anaruhusu mtu kama Veronika kufa
mikononi mwangu?. Eee Mungu nisaidie nilipize
kisasi kwa ajili ya mwanamapinduzi huyu wa Afrika
nzima", niliomba kwa sauti huku machozi
yananitoka. Vero alikuwa amekufa kishujaa.
Alikuwa amewaua maadui wanne pale pale
chumbani.
Niling'oa kile kisu nikasafisha damu yake kwenye
nguo zake.
"Kisu hiki hiki kitawauwa kama walivyomwua
Veronika", nilisema.
"Bosi ninataka toka sasa tuwe pamoja".
"Hapana sasa hivi, fanya mpango wa kuondoa
maiti hizi humu ndani. Na umwarifu Chifu, polisi
wala wakuu wa hoteli wasiingilie. Na halafu
kampashe Sherriff habari hizi za huzuni.
Muushughulikie mwili wa Veronika uweze
kupelekwa kwao. Mwambie Sherriff ashughulike na
habari hiyo tu mambo mengine aniachie. Mwambie
Chifu mambo yote yalivyo mpaka sasa mimi
namfuata Shuta lazima alipe. Fanya hayo kwanza
halafu nitakapokuhitaji nitakujulisha".
Niliondoka na kumwacha Eddy mle ndani ya
chumba nikakimbia kwenye lifti iliyonitelemsha
chini. Nilipita pale mapokezi huku nikikimbia kiasi
cha watu wote kunishangaa.
Niliingia ndani ya gari Eddy alilokuwa amekodi na
kuliacha Kilimanjaro Hoteli nikaondoka kwenda
kumtafuta Shuta.
ITAENDELEA
 
NJAMA
SURA YA NANE
USIKU WA HEKAHEKA
II
Niliondoka na kuelekea nyumbani kwa Eddy
nilikomwacha Zabibu. Njiani nilifikiria uhusiano
wangu na Veronika tokea siku tuliyoonana mwenye
ndege mpaka kifo chake kilipotokea mikononi
mwangu dakika chache zilizopita. Nilisikia uchungu
usio kifani. Hasira na chuki yangu kwa makaburu,
mabeberu na vibaraka wao ilizidi kiwango chake
cha kila siku.
"Kifo peke yake ndicho kitaniachisha kuwawinda
hawa wadhalimu maishani mwangu", niliapa.
Nilipofika nyumbani kwa Eddy nilimkuta Zabibu
amekaa kwenye sofa pale tulipomwacha.
"Kumetokea nini, mbona ulikuwa unalia?", Zabibu
aliniuliza baada ya kuniangalia kwa muda mfupi.
Nilimweleza yaliyompata Veronika, na jinsi urafiki
wetu na Veronika ulivyokuwa umekomaa tangu
kuonana mwenye ndege wakati tukielekea
Freetown. Hakika nilijuta kumfahamu Veronika
afadhali nisingeonana nae.
"Usisikitike sana, sasa tunakuwa watu wawili
tuliopoteza marafiki zetu. Lililopo sasa ni sisi
kutiana moyo na kusaidiana kuwatafuta hawa
waliofanya matendo haya.
Nilijisikia vizuri kidogo Zabibu kuwa pamoja nami.
"Unajua Shuta anapokaa?", niliuliza.
"Ndio, anakaa Oysterbay, Kaunda Drive No. 11230".
"Basi, sasa wewe tulia hapa mimi nitarudi muda si
mrefu".
"Twende sote".
"Hapana. Kazi hii huijui niachie mimi, wewe
pumzika hapa. Ukiona usingizi chumba hicho hapo
kalale. Tutaonana baadaye".
"Lakini jihadhari inaonekana watu hawa ni hatari
kabisa, sitapenda kusikia umeuawa, nikisikia tu na
mimi nitajiua", aliniambia Zazibu akionyesha hali
ya mapenzi kama kwamba tumekuwa marafiki siku
nyingi.
Mimi huwa sielewi kwa nini binadamu hawa
hutokea kunipenda mara tu nionyeshapo uso
wangu. Niliondoka na kuelekea Oysterbay. Niliingia
Kaunda Drive na kuanza kuangalia namba za
nyumba. Niliendesha polepole mpaka nikaona
nyumba. Nilipokuwa napita mbele ya lango la
nyumba hiyo mlango wa mbele ulifunguliwa mimi
nikaendelea mbele kidogo nikaegesha gari langu,
halafu nikarudi kwa miguu.
Nilipofika kwenye ua wa jengo hili nikabana, maana
watu wanne walikuwa wanazungumza hapo nje na
kulikuwa na magari mawili.
Niliposogea nilisikia mtu mmoja anazungumza.
"Hay Shuta, zungumza na mzee halafu utatukuta
Sliver Sands marquuis Du Zaire wanapiga huko
mpaka saa kumi. Baada ya kazi ngumi namna hii
mtu inambidi astarehe kidogo".
"Sawa Mlambo, ngoja nizungumze na mzee nimpe
taarifa yote ilivyo halafu nitampitia msichana
wangu na mnamo saa tano hivi nitakuwa huko",
alijibu Shuta.
"Oke tutaonana", alijibu Mlambo.
Kisha Mlambo na wenzake wakaingia ndani ya gari
aina ya Peugeot 504 na walipotokeza kwenye
mlango nikaona namba zao TZ 66500. Shuta
alirudi na kuingia nyumbani. Mimi niliruka kama
paka nikatua ndani ya ua. Baada ya kutua nikasikia
viatu vinatembea kwa nje. nikarudi haraka haraka
nikabana ndani ya ua wa michongoma.
Nilipoangalia nikaona alikuwa ni askari wa usiku
aliyekuwa analinda ile nyumba. Bila kuniona
alizunguka kunipita kwenye upande huu wa kulia
wa nyumba. Nyumba yenyewe iliwa kushoto mwa
barabara kama unatoka mjini.
Alipotangulia tu mimi nilimnyemelea bila yeye
kunisikia. Nilipokuwa karibu nae nilimrukia na
kumtia kabali, taratibu na bila kupiga kelele
nilimnyonga na kuhakikisha amekufa kisha
nilimsogeza pembeni kwenye giza la michongoma.
Kisha nilizunguka nyumba kuangalia hali ilivyo.
Nyumba yenyewe ilikuwa na vyumba vitatu vya
kulala. Kulikuwa na chumba kimoja kikubwa nikajua
hiki ndicho mwenye nyumba alikuwa akilala.
Madirisha yalikuwa yamefungwa. Nikatoa pete
yangu yenye jiwe la almasi, nikakata tundu katika
kioo kisha nikaingia mkono karibu na mahali pa
kufungulia dirisha. Baada ya kufungua dirisha la
kioo, kulikuwa na dirisha jingine la wavu wa kuzuia
mbu. Nilichukua mkasi nikakata sehemu kiasi cha
kupitisha mkono karibu na mahali pa kufungulia
nikalifungua.
Nilipanda na kutumbukia ndani ya chumba cha
kulala kilichokuwa na bafu ndani yake. Nilifunga
madirisha vizuri nikaacha mapazia kama
yalivyokuwa yamekunjwa. Nilinyata mpaka kwenye
mlango nikasikia mtu anasema kwenye simu.
"Hallo naomba mzee. nimepiga karibu dakika tano
nzima sipati namba hiyo. Mimi Shuta hapa.
Nilisubiri pale kwenye mlango wa kutokea sebuleni.
"Hallo, Shuta hapa".
Mambo hayakwenda vizuri sana yule msichana ni
mpiganaji wa karate na judo sijawahi kuona.
Ameua vijana wetu wanne, watatu aliwaua kabla
ya kuchomwa kisu, lakini hata wakati amekwisha
kuchomwa kisu alimwua Shilonda kwa kumvunja
shingo. Lakini hata hivyo nimemwua.
"Nina uhakika kabisa amekufa palepale maana
nilimchoma kisu kwenye moyo hasa".
"Ndio sasa tumebakiza wawili ndipo tunaweza
kuanza kupakia".
"Haya asante mzee".
Kisha nilisikia anapiga simu tena. "Hallo Sakina
yupo. Shuta hapa".
"Aha kisura jitayarishe nakuja kukupitia twende
kamanyola nasikia siku hizi wana mtindo mpya wa
79 Scania LBT III... tutakwenda ukauone".
"Dakika kumi na tano nitakuwa hapo".
"Haya kwaheri".
Akarudisha simu.
Nilijua atakuja chumbani hivyo mimi nilijibanza
kwenye ukuta karibu na mlango nikamsubiri maana
nilisikia viatu vinakuja. Mkono wa kushoto nilishika
bastola na mkono wa kulia kisu kile kilichomwua
Veronika.
Alifungua mlango akawasha taa huku akipiga mluzi
kisha alifululiza kwenda kwenye kabati la nguo bila
hata kuniona. Mimi nilirudisha mlango kwa mguu,
ndipo akageuka kuniona. Sijaona mtu anastuka
namna hii maana palepale jasho lilimtoka, akataka
kukaa chini akashindwa, akaanza kugwaya. Nilifikiri
atazirai.
"Kumbe wewe unaona kuuwa wenzako ni rahisi na
kumbe wewe mwenyewe unaogopa kifo namna hii".
"Niache niache, mimi ninakujua wewe ni nani,
nisamehe".
Kuomba kwake msamaha kulinifanya mimi
nikasirike zaidi.
"Kabla sijafikiria kukusamehe nataka kujua kiongozi
wenu ni nani?".
"Mimi simjui; mimi ni mtu mdogo tu".
"Si unasema mimi unanijua?".
"Ndiyo nakujua wewe ni Willy Gamba, mpelelezi
mkuu wa Afrika. Mimi niliwaambia waaache kama
wewe wamekuingiza katika upelelezi lakini
walikataa".
"Wakina nani?".
"Akina Mlambo".
"Mlambo ndiye nani?".
"Ndiye mkuu wetu sisi kwa upande wa kuua
wapinzani".
"Na yeye ni mwanachama wa SANP?".
Alitoa macho na kushitushwa sana na swali langu
hili, kisha nikaona anaanza kutokuwa na mshituko.
"Sitasema maneno zaidi nifanye unavyotaka".
"Ahaa, mimi huwa napenda watu shujaa kama
wewe".
Niliweka bastola yangu ndani ya mkoba wake
nikaweka kisu vizuri kwenye mkanda nikamfuata.
Aliponiona sina silaha akaona ajaribu bahati yake.
Palepale aligeuka mbogo na kuanza kunishambulia
kwa makonde. Alitupa konde la kwanza nikaliona.
Akatupa la pili nikaliona. Akatupa la tatu nikashika
mkono wake nikamchukua judo na kumtupa upande
mwingine wa chumba akaanguka kama papai bovu.
Haraka haraka nikamfuata pale chini nikampiga
teke la mbavuni na lingine la tumboni akalainika.
Kisha nikamkunja vizuri sana. Nikatoa kisu
nikachana shati lake akabaki tumbo wazi.
"Sasa utanieleza. Usiponieleza nitakutumbua
matumbo na Sakina hutamwona tena. Niambie
nani mkubwa wenu?".
Macho ya kutisha yalimtoka kwa kukiangalia kisu
na kuona kuwa nilikuwa sitanii.
"Niache, niache nitakwambia mkubwa wetu ni...
Kabla hajamaliza kusema mlango ulipigwa teke na
mtu mmoja akaingia ndani na kabla hajafyatua
risasi pale tulipokuwa nilijirusha upande mwingine
risasi zake zikanikosa ila zikamwingia Shuta
tumboni, na mimi wakati ule ule nikamtupia kisu
kilichompata katikati ya koo akaanguka chini huku
risasi zinatoka ovyo.
Nilisikia vurumai nyingine sebuleni nikajua wako
wengi. Kama umeme nilitoa bastola yangu tayari
kukabiliana na matatizo.
"Mashuka umempata?", nilisikia sauti inauliza kwa
woga.
"Ndiyo", nilijibu kwa sauti ya chini.
Kabla sijampa nafasi nilijirusha na kujiviringisha
ndani ya sebule ambamo nilikuta watu wawili
mmoja akiwa na bastola. Na kwa vile hakutegemea
hatua kama ile alishikwa na bumbuwazi palepale
nikapata nafasi ya kumpiga risasi ya katikati ya
paji la uso akaanguka chini. Kabla sijawahi
kusimama yule mwingine alipiga teke bastola
yangu ikaanguka chini, palepale akanipa teke la
tumboni nikaanguka chini. Wakati ule ule nikaona
anaangalia kule bastola ya yule mwenzake
niliyempiga risasi ilikoangukia na akaruka
kuichukua. Mimi nikitumia ujuzi wangu wa miaka
mingi nilimwahi wakati ndipo anafikisha vidole
vyake kwenye bastola nikampiga kichwa kimoja cha
sisimizi akaona nyota na kujiviringisha mbali na
bastola. Kwa vile alikuwa tayari amenitia mori
nilimfuata wakati naye anasimama. Nikaona
anajikunja tayari kupigana karate, mimi nikaona
ndipo ananipeleka nyumbani.
"Aisee mlambo-iiiiji mjukuu wa Chaka mwana Zulu
fanya kazi yako", alijitia mori.
"Ungekuwa mjukuu wa Chaka ufanye jambo la aibu
kama kuwa kibaraka wa Makaburu - tazama
Mwafrika asiye na aibu".
Aliruka na kutupa karate nikaikinga kwa mikono.
Akatupa tena nami nikaizuia, halafu akageuza mara
moja, akanipata, kisha akanipata tena, nikajua huyu
alikuwa na ujuzi wa kutosha hivyo mimi ilinibidi
nibadili na kujaribu Kung-fu. Na hapo hapo
nikasikia mwili mzima unasisimka nikamwingia.
Kwa sababu ya hasira na baada ya kukumbuka
mauaji ya Veronika chuki kubwa iliniingia hivyo
nilitupa wimbi la kwanza nikatupa la pili likampata
la tatu nilipopeleka kiganja changu kikamtoboa
chini kidogo ya kifua na kutoka na vipande vya
matumbo na vitu vingine vya ndani. Alipiga kelele
"Eeeeeeeeeeeeenakufa, eeeeeeee.
Akaanguka chini akafa.
Nilirudi chumbani nikamkuta Shuta yu hai,
anajaribu kusimama lakini anashindwa sababu ya
risasi zilizomwingia tumboni. Nilichomoa kisu
kutoka kwenye maiti ya yule mtu niliyekuwa
nimemchoma kooni nikamfuata.
"Kama ulivyomwua Veronika na mimi nakuua hivyo
hivyo, maana nilimwahidi aliponiomba nimlipizie
kisasi"
"Nisamehe, nipeleke hospitali".
Kusikia hivi roho ilinichemka, nikamchoma kisu
katikati ya moyo huku analia hovyo.
"Kwa heri Shuta, mtaonana sasa hivi na Veronika
mbele ya Mungu, ukajibu vizuri kwanini umemwua".
Niligeuka na kumwacha anakufa.
Nilipofika sebuleni tu nikasikia gari linapiga breki
pale nje. Niliruka nikachukua bastola yangu na
kuokota nyingine hapo sebuleni nikabana karibu na
mlango wa kutokea nje nikasubiri.
Mlango ulipigwa teke na hapo hapo wakaingia
watu wawili kama risasi, bastola mkononi,
wakajiviringisha mmoja akiwa tayari kupambana na
kitu chochote mbele yake na mwingine
akajiviringisha na kuegeka nyuma. Mimi nilikuwa
tayari kwa lolote.
"Ni mimi usiftatue", nilipiga kelele.
Kumbe hawa walikuwa ni Eddy na Sherriff.
Oh Bosi, samahani", Eddy alisema huku akiruka.
"Siku nyingine kutatokea ajali namna hii",
nilimwambia.
"Tunaomba isitokee", Sherriff alijibu naye
akisimama.
"Umefanya kazi kubwa sana Bosi", Eddy
alinipongeza baada ya wao kuangalia maiti zote
ndani ya nyumba hii.
"Ninastahili kazi kama hii", nilijibu.
"Sisi tulipongojea kwa muda mrefu tukaona
tukufuate baada ya kujua kutoka kwa Zabibu kuwa
umekuja huku. Tulihisi kuwa kuchelewa kwako
unaweza ukawa katika matatizo. Tulipokuja
tulikuta gari lako na gari jingine hapo mbele
yameegeshwa. gari lako lilikuwa limetolewa upepo
ndani ya tairi zote, hivyo hii ilituhakikishia kuwa
uko msambweni", alieleza Eddy huku tukielekea
kwenye gari lao. Ndani ya gari nilimkuta Zabibu.
"Oh Willy mpenzi uko salama?".
Alifungua mlango na kunirukia akiweka mikono
shingoni mwangu na kunibusu.
"Na wewe umefuata nini?", nilimwuliza.
Nilimkarisha ndani ya gari kwenye viti vya nyuma
mimi nikakaa huku Sherriff na Eddy wakaingia
mbele, Eddy akatia gari gea tukaondoka.
"Nilikuja nikuone kama ni kufa tufe wote. Maana
sijui nini kimeniingia nakuona wewe ndiye
mwenzangu sasa. Nikiwa karibu na wewe nasahau
yote yaliyopita".
"Usizoee kutembea na sisi mtoto kama wewe, hufai
hata kujeruhiwa kidogo. tuachie sisi hatari ndiyo
kazi yetu. Sitaki kupatwa mkasa kama niliopatwa
nao kwa Veronika".
Kisha nikamweleza toka mwanzo mpaka mwisho
wa mapambano yangu nyumbani kwa Shuta.
"Naona huyu Mlambo na wenzake walitia shaka
walipoona gari langu. Hivyo walirudi kuhakikisha.
Lazima niseme Mlambo alikuwa na mafunzo ya hali
ya juu ya jeshi hata mimi alinitoa jasho".
Tulielekea nyumbani kwa Eddy.
ITAENDELEA
 
NJAMA
SURA YA NANE
USIKU WA HEKAHEKA
III
Tulipofika nyumbani kwa Eddy ilikuwa saa tano za
usiku. Tuliingia tukaa kwenye viti. Eddy akaleta
vinywaji.
"Kifo cha Veronika kimeniuma sana, tokea sasa
mimi nimeahidi nitakuwa bega kwa bega na wewe
mpaka nione mwisho wa mambo haya", Sherriff
aliniambia huku machozi yakimtoka.
"Sijui nikwambie nini Sherriff, maana hali niliyonayo
mimi siwezi kuieleza. Afadhali tuiachie hapo hapo".
"Basi, mambo yote tumetengeneza. Chifu amesema
mwili wa Veronika hauwezi kusafirishwa mpaka
mwisho wa mambo yote ili aweze kupewa heshima
zote za kijeshi. Hivyo mwili wake umetunzwa huko
kwenye chumba cha maiti katika hospitali ya
Muhimbili mpaka hapo tutakapojua mwisho wa
mambo haya. Mwili wake utapewa uangalizi wa
pekee hivyo hata tukichukua mwezi mzima utakuwa
katika hali safi tu", Eddy alieleza.
"Jambo hili haliwezi kuchukua siku mbili zaidi.
Nimeshapata mwanga mkubwa wa kutosha. Kuna
kitu kidogo
tu ambacho bado kinakosekana lakini naamini
kesho haiishi bila kukupata kitu hicho", niliwaeleza.
Kisha
nikawaeleza jinsi nilivyokuwa ninafikiria mambo
yalivyo toka mwanzo mpaka mwisho.
"Sasa ninachotafuta ni yale magari waliyapata
wapi?.Nguo ni rahisi pamoja na vyeo kama
nilivyowaeleza. nikishajua hilo basi jambo hili
tutakuwa tumelitatua. Itabaki sasa kufanya
shughuli ya mwisho ambayo ni kuzikamata hizi
silaha na kuwakamata vibaraka hawa".
Wote walitingisha vichwa kuonyesha wamenielewa.
"Ray Sikazwe anakaa wapi?", nilimwuliza Zabibu.
"Anakaa Oysterbay, Kenyata Drive nyumba Nambari
1000/D".
"Oke, Eddy tokea sasa hivi weka vijana wa
kumfuata Ray Sikazwe kila mahali anapokwenda.
Ifikapo asubuhi nataka nataka nijue nyendo zake
zote na sisi tutawasaidia tokea hapo. Tukiweza
kufanya hivyo kazi itakuwa rahisi. Baada ya
mambo yote yaliyotokea leo lazima akipata habari
atakuwa na wasiwasi, hivyo lazima tu atafanya kitu
cha kujinasa. Wote tutalala hapa maana ndiko
mahali hapafahamiki.
"Tutaonana asubuhi", niliwaaga. Nyumba ya Eddy
ilikuwa na vyumba vitatu vya kulala. Kwa vile
Zabibu alikuwa na huzuni nyingi na kwa vile mimi
pia nilikuwa na huzuni tulionelea afadhali tukalala
pamja ili tuweze kuliwazana mioyo.
 
NJAMA
SURA YA TISA
MAPAMBANO NA VIBARAKA
Ilikuwa saa kumi na mbili na nusu za asubuhi
wakati nilipokuwa nakaribia kumaliza kunyoa
ndevu. Nilikiangakia kidevu changu kwenye kioo
nikaona nilikuwa sijajinyoa vizuri. Kila wakati
nilipokuwa na mawazo mengi kitu kama hiki
kilikuwa kinanitokea. Lakini hata hivyo nia yangu
nionekane nadhifu hivyo nilichukua tena mashine
ya ndevu na kuanza kujinyoa. Nilipoona mambo
yanakuwa mazuri kwenye kidevu changu, nikaanza
kuoga.
Nilitoka maliwatoni na kurudi chumbani nilikokuwa
nimelala. Zabibu bado alikuwa hajaamka, hivyo
nilivaa taratibu ili nisije nikamshtua toka usingizini.
Alikuwa na sura ya mtoto mchanga isiyokuwa na
maneno. Nilimwangalia huku nikivaa. Nilipomaliza
kuvaa na kuweka kila kitu changu tayari, nilikwenda
nikambusu Zabibu usingizini nikaondoka ndani ya
chumba na kufunga mlango taratibu.
Niliwakuta Sherriff na Eddy wamekaa sebuleni
wanakunywa kahawa.
"Karibu bosi, habari za kuamka?".
"Nzuri", nilijibu, nikaa kwenye kiti cha meza ya
kulia nikavuta kikombe cha chai na kujiwekea
kahawa ya kutosha.
"Lazima iwe nzuri", Sherriff alijibu huku
akitabasamu nikajua alikuwa na maana gani
kusema hivyo.
"Usinionee wivu".
"Lazima tukuonee wivu, maana chuma kama hicho
si cha kawaida.
"Bosi, vijana wameleta habari kama ulivyoomba",
Eddy alisema huku akibadilisha mazungumzo.
"Ndio, wamesemaje.
"Wamesema hawakuweza kumwona Sikazwe
mpaka saa tisa za usiku. Walimpata akitokea
kwenye barabara ya Bagamaoyo na akielekea
nyumbani kwake. Hawakuweza kujua alikuwa
anatokea wapi. Na mpaka sasa hivi bado yuko
nyumbani amelala. Wamenieleza kuwa ofisi za
SANP hazifanyi kazi siku za Jumamosi. Na kama
unavyojua leo ni Jumamosi".
"Basi waambie waendelee na wahakikishe kuwa
hawapotezi hata dakika moja. Atakapoondoka
nyumbani nataka kujua anaelekea wapi. Sawa?".
"Hamna taabu".
"Sasa hivi mimi ninakwenda kumwona Chifu maana
nilipata habari kuwa anataka ripoti toka kwangu,
maana anasumbuliwa sana na Serikali".
"Nafikiri Sherriff anaweza kuendelea kupumzika
hapa, mimi nitakujulisha wakati nitakapokuhitaji".
"Sawa", alijibu Sherriff kwa mkato.
"Naomba unipatie 'machine gun' inayoweza
kuchukua risasi zaidi ya mia. Niliwahi kuzitumia
nilipokuwa jeshini.
"Aina gani".
"Zilizotengenezwa Urusi".
"Zipo".
"Oke niletee moja ya aina hiyo. Ikiwezekana tuma
mtu aniletee mapema kusudi niishughulikie".
"Hamna taabu, utapata.
Baada ya kuzungumza na hawa vijana tuliagana
kisha nikaondoka. Nilitembea kwa mguu mpaka
nyumbani kwangu, ili nikabadilishe nguo. Nilifika
nikafungua mlango, nikaangalia saa yangu nikaona
ilikuwa yapata saa mbili kasoro robo. Nilipoingia tu
ndani, roho yangu ikashtuka lakini nilikuwa
nimechelewa, nilipigwa na mfuko wa mchanga
kisogoni nikaanguka.
ITAENDELEA
 
NJAMA
SURA YA TISA
MAPAMBANO NA VIBARAKA
II
Nilisikia sauti ikisema ni saa tisa sasa. Sauti hiyo
ndiyo ilikuwa imenizindua. Nilijikuta nimelazwa
kwenye kitanda cha chuma bila godoro, na nilijikuta
nimefungwa kwenye kitanda mikono na miguu.
Kichwa kilikuwa kinaniuma sana, na kwa chati
nilifunua nilikuta nimo kwenye chumba kidogo cha
giza tupu.
Nikatuliza mawazo nikaanza kufikiri nini kimetokea.
Ndipo nikatambua kuwa nilipokuwa nakwenda
nyumbani kwangu saa mbili kasorobo nilipigwa na
kitu nilichohisi ni mfuko wa mchanga nikaanguka
chini. Tokea hapo mpaka sasa sikujua chochote.
Hii ina maana kuwa nilizimia. Nikakumbuka yule
mtu alisema ilikuwa saa tisa, hii ina maana
nilikuwa nimezimia kwa zaidi ya masaa sita.
Nilifikiri jinsi akina Eddy, Sherriff, zabibu na Chifu
walivyokuwa wamehangaika huu kujaribu
kunitafuta. Hata mimi mwenyewe nilikuwa sijui
hapa ni wapi. Ila nilikuwa nasikia kelele nyingi nje
ya chumba hiki. Hivyo nilifikiri kuwa huenda ikawa
ni sehemu ya viwanda. Sikujua ile sauti iliyosema
sasa ni saa tisa ilitokea wapi, maana kulionekana
kana kwamba hakukuwa na mtu ndani ya chumba
hiki.
"Zaidi ya saa tisa sasa lazima waje kutupokea sisi
twende tukapate chochote", nilisikia tena mtu
anazungumza.
"Washa taa", sauti nyingine ikajibu.
Hivyo nikajua kuwa nilikuwa nalindwa na watu
wawili ila sikuweza kuwaona kwa sababu ya giza.
Taa ilipowashwa mimi nikajifanya kana kwamba
bado nimezimia kabisa.
"Bado kazimia kabisa", alisema mmoja wao.
"Daktari alisema hawezi kuamka mpaka saa kumi
na mbili au baada ya hapo", alijibu mwingine.
"Kama ni hivyo basi twende tukawaambie
watupokee njaa inauma sana".
"Oke twende, zima taa".
Walifungua mlango na kuzima taa halafu
wakafunga mlango na funguo wakaondoka. Mimi
nilijinyanyua ili nione nimefungwa kiasi gani.
Nilikuta ni mikono na miguu tu iliyofungwa kwenye
kitanda cha chuma kipatacho futi tatu upana.
Miguu ilifungwa kwa ustadi sana kiasi kuwa
nilisikia kama damu haipiti na sehemu za nyayo
zimekufa ganzi. Kwa upande wa mikono, mkono wa
upande wa ukutani nilipoujaribu nikaona
haukufungwa kwa ustadi sana, ule wa upande
mwingine ndio ulifungwa kwa ustadi sana.
Nilinyanyua kichwa changu nikasikia kinauma sana,
nikakirudisha chini. nilianza kufikiri namna gani
nitajiokoa. Baada ya kufikiri sana nikaona njia
pekee ni kujaribu kufungua hizi kamba kabla walinzi
hawa hawajarudi. Hivyo nilionelea nijikaze.
Ingawaje kichwani nilisikia maumivu makali. Kwa
vile sehemu zote tokea tumbo, kifua na kichwa
zilikuwa hazikufungwa, na kitanda kilikuwa cha futi
tatu nilijikunja ili mdomo wangu ufikie kamba za
mkono wa upande wa ukutani ambao haukuwa
umefungwa sana.
Nilitulia tena nikamwomba Mungu. Niliupeleka
mdomo wangu kwenye fundo la kamba walilokuwa
wamenifungia. Kwa bahati mdomo wangu ulifika
nikaanza kupitisha meno yangu kwenye kamba ili
niweze kujua wamefungaje. Katika hii tafuta tafuta
huku maumivu karibu yananitoa fahamu, niliuma
ncha moja ya kamba, nikaivuta na fundo lote la
kamba likafunguka na mkono wangu wa kulia
ukawa huru.
Ilibidi nirudishe kichwa changu kipumzike maana
maumivu yangu yangeweza kunifanya nizimie.
Nikiwa na mkono mmoja huru, nilipata tumaini na
nguvu mpya. Nilichoomba sasa ni watu hawa
wasije upesi. Kwa vile walikuwa wamesema daktari
aliwaambia siwezi kuamka kabla ya saa kumi na
mbili nilijua watadharau kuja ndani ya chumba hiki
cha joto la kuweza kuua kabla haijakaribia saa
kumi na mbili wakati wananitegemea kuamka.
Nguvu mpya zilizoletwa na mawazo kuwa
nimechelewa mambo mengi zilinifanya nisahau
kabisa maumivu yangu.
Niliutumia mkono wangu wa kulia kufungua mkono
wa kushoto. Nikiwa sasa nimeweza kufikia hatua
hii niliingiwa na furaha nikaanza kushambulia
kamba nilizofungwa miguuni. Kwa mtu mwenye
ujuzi kama wangu hii haikunipa taabu na mara
nikawa huru tayari kupambana na wadhalimu
hawa.
Nilirudi nikajilaza nikaziweka kamba kijanja kana
kwamba bado hazijafunguliwa. Nikawa katika hali
ya kusubiri. Nilivyokuwa na bahati haikupita muda
mrefu nikasikia funguo zinaingia ndani ya kufuri la
mlango. Mara mlango ukafunguliwa na taa
zikawashwa. Mimi nilijilaza vile vile na kujifanya
bado nimezirai.
"Bado sana huyu, niliwaambia daktari alisema saa
kumi na mbili. Angekuwa mtu wa hivi hivi asiye na
mazoezi pigo lile lingemuua pale pale", nilisikia
sauti ikisema.
"Sawa. Akiamka saa kumi na mbili itakuwa vizuri
maana ndipo wakati wazee watakapomhitaji", sauti
nyingine ilijibu.
"Haya shika funguo, mwangalie kwa makini
akionyesha dalili ya kupata fahamu tupashe habari
mara moja. Sisi tuko chumba kingine tukisubiri
maelekezo zaidi kutoka kwa wazee.
"Haya asante, lakini naomba asiamke wakati nikiwa
peke yangu. Nasikia mtu huyu ni hatari kubwa
kabisa'.
"Wewe mwoga sana. Mtu aliyefungwa kiasi hiki
unafikiri atafanya nini hata akiamka, labda awe na
nguvu za kishetani".
"Huenda anazo".
"Kama anazo basi pole, yatakuwa matatizo yako".
Nikiwa katika kusikiliza mazungumza haya kidogo
nicheke. Yule mtu mwingine alitoka, akabaki mlinzi
mmoja ambaye alifunga mlango na kuzima taa,
halafu akakaa kwenye kiti. Nilisubiri kama dakika
kumi hivi nikaanza kukoroma. Yule mlinzi aliinuka
na kuwasha taa na kunisogelea kitandani wakati
mimi bado nimefumba mamcho. Kule kuhema
kwake ndiko kulinifanya nijue yuko karibu.
"Wewe umeamka", aliuliza kwa wasiwasi, nilifungua
macho yangu kwa chati nikaona alikuwa ameshika
bastola akiwa amelenga kifuani pangu. Nilifanya
mahesabu ya namna ya kumwingia mtu huyu
nikapata.
"Ndiyo', nilijibu kwa unyonge.
Niliona macho yanamtoka, nikaona mtu huyu
ameingiwa na woga na anaweza kunipiga risasi
shauri ya woga nisipomwahi. Hivyo kama chui
nilimrukia na wakati ule ule nikawa nimepiga
bastola yake ikaanguka upande mwingine na
nikampiga pigo la mkono la karate katikati ya
kichwa akafa bila kujua nini kimemwua. Niliiendea
bastola yake, nikamvua joho lake jekundu,
nikalivaa, kisha nilifungua bastola nikakuta funguo
na risasi za bastola hii. Nilifungua bastola nikakuta
ina risasi tatu tu nayo ina uwezo wa kubeba kumi.
Hivyo niliijaza risasi, kisha nikachemsha kidogo
viungo vyangu tayari kwa kupambana na watu
walioko chumba kingine. Kichwa kilikuwa bado
kinaniuma lakini hakikuwa tishio kubwa.
Nilizima taa, nikajaribu kufikiri nilipo lakini nikaona
bila kwenda nje haingenisaidia. chumba hiki
kilionekana kilikuwa ni stoo ya vitu, hivyo nilihisi
hapo nje kuna ofisi na nilifikiri kuwa ndicho chumba
cha pili alichokuwa amezungjumzia yule mlinzi wa
pili. Nilifungua mlango taratibu, niliangalia hali
mara moja nikajua hizi zilikuwa sehemu za nyuma
za bohari, au ofisi. Maana kulikuwa na chumba
kinatazamana na stoo hii, halafu kulikuwa na
vyumba vitatu mbele tena kwa upande wa kulia.
Upande wa kushoto kulikuwa na mlango wa
kutokea uwani.
Nilisikia watu wanazungumza kwenye chumba
kilichokuwa kinaangaliana na mahabusu yangu.
Nikajua ni hiki chumba alichozungumza yule mlinzi.
Nilijiweka tayari kisha nikagonga. Mimi niliamini
watajua ni mwenzao hivyo wangekuja bila tahadari
kufungua mlango.
"Ngwishe", nilisikia sauti ikiita.
"Ndiyo", nilijibu kwa sauti nzito.
"Ameamka?".
"Bado".
"Funguo tu mlango haukufungwa", nilijibiwa.
Basi bastola yangu ikiwa tayari mkononi, nilifungua
mlango na kuingia ndani. Kweli watu wote sita
walikuwa wamwezunguka meza wanakula.
Waliponiangalia na kunitambua mimi ni nani
wengine chakula kiliwadondoka toka midomoni.
"Endeleeni kula, mbona mnaacha", niliwatania.
Mmoja wao alimkonyeza mwenziwe wakifikiri mimi
sikuona kumbe hawakujua macho ya Willy
yamefundishwa kuangalia kila mahali kwa wakati
mmoja utafikiri kinyonga. Yule aliyekonyezwa alitoa
bastola haraka sana lakini mimi nilijua anataka
kufanya nini na kabla hata sijamtahadhalisha
alikuwa tayari kufyatua, lakini mimi nilikuwa
mwepesi zaidi nikampata. Wakati yeye alipofyatua
risasi alimpiga mwenzake na kumwua. wawili tayari
walikuwa wamekufa.
Pale pale wengine wote walisimama kila mtu akitoa
bastola. Lakini niliwawahi watatu halafu nikaona
yule wa nne macho yake yanaangalia mlango.
Mara moja nikaanguka chini na risasi ikanikosa
kwa nyuma ikapita na kumpiga yule wa nne na
kummaliza, mimi pale pale nikajiviringisha na
kumwahi yule wa nje. Lo nilikuwa nimeponea chupu
chupu, maana kama nisingewahi kulala chini, vile
vile ningekwenda kuonana na Veronika mpenzi
wangu kama kweli watu huwa wanaonana tena
huko ahera.
Nilitoka ndani ya jengo hili upesi upesi. Nilipofika
nje nikaona niko kwenye mabohari ya Chang'ombe.
Bohari hii ilikuwa imezungukwa na ua wa matofali.
Nilivua joho jekundu nikapanda ua nikatokea katika
uchochoro nikaanza kukimbia. Nilikadilia kuwa
ilikuwa yapata saa kumi na moja. Nilipofika mbele
ya bohari nilikuta ni mali ya Kampuni moja ya
matairi ya magari iitwayo "Trans World Tyres", kwa
sababu sikutaka kufanya uchunguzi zaidi kutokana
na hali niliyokuwemo niliona teksi nikaipungia
ikasimama na kumwamuru dereva anipeleke
Independence Avenue haraka.
ITAENDELEA
 
NJAMA
MAPAMBANO NI VIBARAKA
III
"Ohuu. Bosi umetokea wapi?". Linda aliuliza huku
akitoa pumzi ndefu ya kuonyesha wasi wasi
aliokuwa nao umemtoka.
"Nimetoka mahabusu".
"Pole sana bosi".
"Usinipe pole sasa hivi, mapambano bado kabisa
yanaendelea, utanipa pole nikiweza kumaliza
mapambano haya kwa usalama. Eddy yuko wapi?".
"Yuko katika shughuli za kujaribu kukutafuta apate
kujua uliko. Lakini kila baada ya muda mchache
anauliza hapa".
"Akipiga tena simu mwambie arudi haraka. Je
Sherriff yuko wapi?".
"Wote wako pamoja".
"Haya kaniletee Sandwich za nyama ya kuku na
niwekee glasi ya whiski ofisini kwangu. ninakwenda
kunawa kidogo".
Baada ya kumaliza kunawa niliingia ofisini kwangu
na kuanza kunywa whiski na Sandwich alizokuwa
ameleta Linda.
"Chifu yuko?", niliuliza.
"Amesema muonane saa moja bila kukosa", Linda
alijibu.
Mara simu ililia ofisini kwa Linda. Linda akashika
simu yangu iliyokuwa imeunganishwa na yake.
Alibonyeza kidude kimoja baada ya kuinua mkono
wa simu.
"Hello nani hapo?", Linda aliuliza".
"Oh Eddy, rudi hapa haraka Bosi yuko hapa. Yuko
hai kabisa ameketi kwenye kiti chake anakunywa
whiski"....
"Haya asanhte", Linda aliweka simu huku akicheka.
"Nakwambia bosi ungesikia sauti ya Eddy
niliposema uko hapa. utafikiri mtu aliyekwamwa na
mwiba wa samaki".
Simu iliita tena ofisini kwa Linda na Linda
akachukua simu.
"Hello nani hapo?", Linda aliuliza. "Ehe Unasemaje
Issack... Eddy bado hajafika hapa, lakini atafika
muda si mrefu, na kama una habari muhimu Bosi
yuko hapa". "Oke, njoo haraka sana", Linda alijibu
na kukata simu.
"Vijana wa Eddy aliokuwa amewasambaza, huyu
Issack na mwenziwe ndio walikuwa na jukumu la
kuangalia mienendo ya Sikazwe", alisema Linda.
"Ghafla mlango wa ofisi yangu ulifunguliwa,
Sherriff, Eddy na Zabibu wakaingia ndani.
"Pole sana Bosi, sisi tulijua kwa uhakika kuwa
utakuwa msambweni", Eddy alitoa pole.
Linda na Zabibu waliangaliana kwa jicho baya.
Inaonekana Linda hakunda Zabibu kuja ofisini kwa
bosi wake.
"Huyu anakuja kufanya nini, si afadhali angalikaa
nyumbani, akawaachia wanaume hawa kazi hii.
Mara nyingine kutembea na wanawake katika
mapambano kama haya kunaweza kuleta mkosi".
"Mimi sina mkosi. Pilipili usiyokuwa inakuwashia
nini?. Shughulika na mambo yako dada na mimi
nitashughulika na yangu, usinijue kabisa", alijibu
Zabibu kwa hasira.
"Haya basi yaacheni hayo mambo ya kitoto hapa
tuko kazini. Sitaki kusikia uchafu mwingine
wowote", niliwaonya.
Nilianza kuwaeleza yaliyonipata toka mwanzo
mpaka mwisho. Nilipomaliza kuzungumza tu Issack
akaingia.
"Ehe tupe maelezo", Eddy alimdai.
"Nitaanza toka jana usiku kwa faida ya wale
ambao hawakupata habari hizo toka mwanzo.
Sikazwe tulianza kumwona mnamo saa tisa za
usiku akitokea barabara ya Bagamoyo. Alielekea
moja kwa moja nyumbani kwake na hakutoka tena
mpaka saa sita za mchana. Mnamo saa sita hivi
aliondoka akaenda kula chakula cha mchana.
Aliporudi mnamo saa saba hivi alikuja na lori dogo
tani tatu likimfuata nyuma. Alifungua mlango na
kuanza kutoa mizigo iliyofungwa kama mtu
anayehama. Baada ya kujaza gari hili, liliondoka na
nikamwambia Ismail alifuate. Ismail aliporudi
alisema mizigo hiyo imetelemshwa kwenye bandari
ndogo yaani pale ngalawa na meli ndogo ndogo
zinapopakia mizigo yao.
"Yaani mizigo hiyo ilikuwa imefungwa kisafari?'.
"Ndio".
"Haya endelea".
"Kiasi cha saa tisa hivi walikuja watu wawili ndani
ya gari, mmoja Mzungu mwingine mwafrika.
Walikaa kama dakika tano tu wakaondoka.
Nilimwambia Ismail awafuate. Walielekea barabara
ya Bagamoyo, Ismail aliporudi alisema watu hawa
waliingia barabara ya Kilimani na kuingia nyumba
moja inayotazamana na Hosteli ya Tazara. Sikazwe
hakutoka. Mnamo saa kumi na moja hivi alikuja
mtu mwingine na gari akazungumza nae mlangoni.
Maneno aliyosema yalionyesha kumkasirisha
Sikazwe maana alimsukuma, na yule mtu haraka
haraka akaingia ndani ya gari na kuondoka....
"Ismail alimfuata huyu mtu lakini mtu huyu aliingia
Estiennes Hoteli na kuanza kunywa pombe, hivyo
akamwacha akarudi. Wakati natoka Sikazwe
alikuwa bado yuko ndani lakini nafikiri atatoka
maana alichukua debe la mafuta ya petrol akajaza
gari lake".
"Kazi nzuri umefanya".
"Asante", alijibu kwa furaha sana.
"Eddy nitayarishie gari, hapana Issack nitatumia
gari lako mimi na wewe tutakwenda kumfuata
Sikazwe, popote atakapokwenda. Sherriff Eddy na
wengine mnisubiri hapa hapa nitarudi ila
mjitayarishe kwa usiku wa kazi", niliwaeleza lakini
niliona wanashangaa.
Kabla hawajaanza kusema mengi nilimwambia
Linda. "Mwambie Chifu anisubiri kidogo nikichelewa
kufika saa moja".
Nikatoka nje pamoja na Issack nikawaacha
wamepigwa na butaa.
Niliangalia saa yangu ilikuwa saa kumi na mbili na
dakika tano na kwa majira ya wakati huu ya Dar es
Salaam giza lilikuwa limeingia. Tulipofika kwa
Sikazwe tu tulimwona naye anafungua mlango wa
gari akaweka mkoba wake ndani, kisha akaingia na
kuwasha gari moto. Sisi tuliegesha gari letu kama
watu wanaopunga hewa pwani saa za jioni kwani
vile vile kulikuwa na magari mengine. Alipoondoka
tu Sikazwe sisi taratibu tulimfuata.
Mimi ninapomfuata mtu hata awe na ujuzi wa
namna gani hawezi kunitambua. Sikazwe
alituongoza mpaka kwenye nyumba hii ambayo
Issack alisema ilikuwa karibu na Hosteli ya tazara.
Alipiga honi mbele ya lango kubwa. Tukaona askari
anakuja kumfungulia akaingia ndani. Majibwa
mawili makubwa yaliandamana na askari huyu. Sisi
tulienda na kuegesha gari letu mbele ya baa ya
Hosteli ya Tazara. Mtu yeyote angedhani tuko
humo katika baa, tunakunywa.
"Unayo bastola yenye seilensa?", nilimwuliza
Issack.
"Ndiyo".
"Nipe. Wewe ningoje hapa lakini uwe katika
tahadhari kitu chochote kikitokea njoo haraka,
umenielewa.
"Hamna wasiwasi bosi".
"Kazi ninayokwenda kuifanya ni ndogo ila majibu
ndio yananipa wasiwasi".
"Nakutakia kheri, bosi".
"Nafikiri nitaihitaji".
Nakutakia kheri, bosi".
"Nafikiri nitaihitaji".
Niliondoka na kwenda kwenye nyumba ile. Mbwa
walikuwa wanabweka kila gari linapopita mbele ya
ile nyumba. Niliona hii itanisaidia maana hata
wakibweka halitakuwa jambo la ajabu. Niliangalia
wapi upepe unatoka nikaona ulikuwa unatoka
mashariki kwenda magharibi, hivi nikaamua kuingia
nyumba hii kutoka magharibi kuzuia mbwa wasije
wakaninusa. Nyumba ilikuwa imezungushiwa ua
wenye seng'eng'e zenye miba upatao urefu wa futi
sita kwenda juu. Kati ya mafunzo yangu makubwa
kuruka ilikuwa mojawapo. Nilikuwa naweza kuruka
futi saba wakati mwingine nane. Hivyo nilirudi
nyuma nikaruka juu ya seng'eng'e na kutumbukia
ndani ya ua bila kishindo maana nilitanguliza
mabega.
Nilikumbuka kuwa kibao nje la lango kubwa
kilikuwa kimeandikwa jina la Tony Harrison, hivi
nilijua huyu ndiye mwakilishi wa Euro-Afro. Zabibu
aliwahi kunieleza habari hizi. Walivyokuwa
wanahusiana na Sikazwe ndicho nilikuwa nimekuja
kutafuta. Kwanza ilinibidi nitoe kikwazo kimoja
yaani askari mlinzi na mbwa. Nilisikia mbwa
wanabweka mbele ya nyumba, hivyo nilijibanza
kwenye ukuta wa upande huu wa magharibi halafu
nikanyata pole pole mpaka kwenye kona ya ukuta
na mbele. Nilichungulia nikaona askari mlinzi
pamoja na mbwa wake wawili. Nilikohoa yule
askari akastuka akaangaza huku na huko asione
kitu maana mimi nilikuwa nimeganda kama kupe
kwenye ukuta. Ili kuridhisha mashaka yake alikuja
upande niliokuwa akifuatana na mbwa. Alikuwa na
bunduki mkononi, kwa umbo lake nikajua ni 'SAR'.
Alipofika karibu kabisa na mimi niliona mbwa
wanainua mikia nikajua tayari wameninusa.
Nililenga bastola yangu nikawaua wale mbwa kwa
kuwapiga katikati ya vichwa kwa upesi sana
kwamba yule askari alishangaa kuona mbwa
wanaanguka hata bila kubweka. Alipogeuka na
kuniona tayari alikuwa amechelewa, nilimrukia
nikamkaba kabali taratibu mpaka alipokufa bila
kutoa sauti. Nilivuta mizoga ya majibwa haya na
maiti ya yule askari na kuyaweka kando ya ua
upande wa magharibi kwenye seng'eng'e. Nikiwa
nimeridhika na hatua yangu ya kwanza. Sasa
nilichukua hatua ya pili.
Nilianza kuzunguka nyumba kwa nyuma nikielekea
mashariki. Sikwenda mwendo mrefu kabla sijafika
mahali nilipokuwa ninapahitaji. Nilikuwa nimefika
nje ya sebule na dirisha la nyumba lilikuwa wazi,
na nikasikia mazungumzo ya huko ndani kama
nami niko pale pale. Hivyo nilibana tena kwenye
ukuta nikaanza kusikiliza mazungumzo.
"Lakini Tonny, mimi nimrjitshidi sana lakini huyu
mdudu Gamba na kundi lake amewaua watu wangu
wengi sana. Fikiria Shuta na Mlambo wameuawa.
Nadhani nisingejitahidi zaidi ya hapo. Lakini hata
hivyo bado nina watu wa kutosha kutekeleza kazi
hii. Usiku huu huu itakwisha, usiwe na shaka.
Hii ilikuwa sauti ya Sikazwe.
"Sawa Ray, lakini naona ungejitahidi zaidi ya hapo
maana lazima ile meli ndogo iondoke saa tisa za
usiku ili kuwahi meli yetu ya Euro-Afro Mtwara
usiku wa kesho. Tayari rubani wa meli hiyo ana
habari na mpango wa kutoa mizigo ndani ya meli
ndogo (scooner) na kuingiza katika meli hiyo huko
Mtwara haina uangalizi sana kama bandari ya Dar
es Salaam", Tonny alisema.
"Vizuri mimi nitajitahidi, tayari mizigo yote
imefungwa vizuri, imebaki kusafirisha tu kwenda
kwenye bandari ya meli ndogo".
"Nimepata habari kuwa unangojewa kwa shangwe
na wakuu wa serikali ya Afrika Kusini. Nimewaeleza
mipango yote, na wao wako tayari kuzungumza na
chama chako ili damu isimwagike Nchini.
Wamefurahi sana kwa kazi yetu ya kuweza kuziiba
silaha za hatari ambazo zingeua wananchi wa
Afrika Kusini bure, kumbe mnaweza kufikia
maafikiano ya kubadilisha siasa ya Serikali ya
Afrika Kusini kwa mazungumzo", Tonny Harrison
alieleza.
"Na mimi nimeona ni wenda wazimu kuendeleza
vita dhidi ya Afrika Kusini kwa njia ya
mapambano.Lakini bado chama cha PLF
kitaendeleza mapambano. Chimalamo ni mtu
mwenye nia ya kuuza ubaguzi wa rangi kwa
mapambano na mtutu". Sikazwe alionya.
"Si wewe unajua vitu vyao vyote na namba ya
askari wao na mafunzo waliyopata askari wao
pamoja na silaha walizonazo.
"Ndiyo, najua kila mbinu ya jeshi lake maana
mwaka jana Kamati ya Ukombozi ya OAU ilitaka
kutuunganisha. Hivyo tulipewa fursa ya kuelezana
kikamilifu hali ya mali ya kila Chama kwa
mwenzake. Tulikuwa wote tumekubali kuungana
tukaelezana siri zote za vyama vyetu. Ni wakati tu
tulipokuja na maoni ya namna ya kuweza kufikia
hali ya kubadili siasa ya ubaguzi bila kumwaga
damu, ndipo nilipokataa tena mpango huo wa
kuunganisha vyama. Nilidai kuwa siasa ya Chama
cha PLF na chama changu zilikuwa na tofauti za
kimsingi ambazo hatukuweza kukubaliana. Huu
ulikuwa uongo lakini ulikubalika ikaonekana
tuendelee hivi tulivyo ili mradi wote tuna nia moja
kwa hivyo siri zote za PLF ninazo.
"Kwa hiyo siri zote za PLF unazijua na kwa sababu
wewe umejiunga na serikali ya Afrika Kusini
itakuwa rahisi sana kuwateketeza wapigania uhuru
wa PLF wasijaribu tena. Yaani litakuwa pigo kubwa
kiasi kuwa kuweza kuimarisha chama chao kianze
mapambano tena, lazima itawachukua muda mrefu,
na wakati huo Ray utakuwa uanatawala pamoja na
wazungu huko Afrika Kusini". Sikazwe alitoa
kicheko.
"Msiwe na wasiwasi mimi nitakuwa nao bega kwa
bega kuleta hali nzuri katika Afrika Kusini na
nitakuwa mstari wa mbele kupinga harakati za
ukombozi ambazo wakati huo zitakuwa hazina
maana".
"Kesho ndiyo siku kubwa kwako utakapoingia
Pretoria na kuwekewa zulia jekundu", Tonny
alisema kwa sauti ya kejeli.
Bila kutambua ile kejeli Sikazwe alijibu. "Ninaisubiri
kwa hamu sana. Magari yale yaliyofanya kazi
tayari yamebadilishwa rangi za jeshi la Tanzania.
Kwa hiyo saa nne inaweza kupitia Intercontinental
Motors na kuyachukua ili kubeba ile mizigo toka
bohari mpaka bandari ndogo".
"Tayari Max ameisha waarifu, au siyo ?', Tonny
aliuliza.
Niliinuka taratibu kumwangalia huyu Max
nikamtambua; ni yule aliyetukimbia kule kwenye
uwanja wa Saba Saba.
"Mara hii nitakupata", nilijisemea moyoni maana
mara moja alinikumbusha Veronika.
"Ndiyo, gari ziko tayari", Max alijibu.
"Oke mimi ninakwenda kijitayarisha saa tatu unusu
ndipo nitatoka nyumbani kwangu kuelekea kwenye
shughuli.
"Je kuna wasiwasi wowote?", aliuliza Tonny.
"Hamna taabu, tayari watu wa Forodha wanajua
tunapeleka spea za magari Mtwara na tumeisha
zungumza nao vizuri hamna taabu".
"Lakini usimsahau Gamba na wenzake", Tonny
alikumbusha.
"Usiwe na wasiwasi nina askari zaidi ya mia
ambao wamefundishwa mafunzo ya juu hapa hapa
Tanzania. Kama Gamba na wenzake wanataka kifo
vema, na waje watuingilie watakiona kilichomtoa
kanga manyoya shingoni".
"Oke nakutakia upakuzi mwema".
"Max, kwa sababu wewe ndiye kiongozi wa meli hii
ndogo uwe macho kusije kukatokea kosa", Tonny
alimwonya.
"Wewe unanijua sifanyi kosa mara mbili",
alijigamba Max.
"Haya Sikazwe nafikiri saa tisa na nusu tutaonana
hapa sitalala nitakusubiri".
"Usiwe na shaka", alijibu Sikazwe huku akisimama.
"Lo, nipe tiketi yangu ya ndege kabisa".
"Chukua hii hapa imelipiwa na serikali yako
unakokwenda kuwa kati ya watu wakubwa
watakaoongoza nchi yenye nguvu kuzidi zote katika
Afrika".
Sikazwe na Max walimwaga wakafungua mlango
wakatoka nje. Tonny Harrison alibaki ameketi
kwenye kiti. Kwa vile nilikuwa na wasiwasi kuwa
wangeshangaa kutomwona askari mlinzi na mbwa
wake, nilitoka pale dirishani nikazunguka mbele.
Kwa bahati nzuri hawakushughulika kumwita
askari, ila Max alikwenda akafungua mlango,
Sikazwe akapitisha gari langoni, halafu Max
akarudisha mlango na kuingia ndani ya gari
wakaondoka.
Mimi nikaona nimepata wakati mzuri wa
kuzungumza na Tonny Harrison. Nilipoangalia saa
yangu nikaona ni saa moja na nusu. Saa mbili
zilikuwa zinatosha kumaliza shughuli zangu na
Tonny Harrison kabla sijamfuata Sikazwe hapo saa
tatu na nusu. Nilifungua mlango taratibu maana
ulikuwa umerudishiwa tu bila kufungwa kwa
ufunguo. Nikiwa na bastola mkononi niliingia
sebuleni na kumkuta Tonny Harrison ameinamia
meza anasoma faili.
"Habari za kazi Tonny Harrison?".

Harrison aligeuka na kujikuta anaangalia katikati
ya mdomo wa mtutu wa bastola. Pale pale
aligeuka sura. Kwanza ikawa ya manjano kisha
ikageuka ikawa nyekundu kama mtu aliyechapwa
kofi usoni. Unajua hawa wenzetu weupe akichapwa
kofi muruwa uso hugeuka na kuwa mwekundu.
Alitaka kutamka neno akashindwa. Niliona alikuwa
hategemei kabisa maisha mwake kukutana na
wakati kama huu ambao alijikuta anatazama
mdomo wa kifo.
"Habari gani?. Au umekuwa bubu?".
Nilisogea taratibu huku bastola yangu ikiwa
imemlenga katikati ya uso wake. Kwa kigugumizi
alijibu. "Nzuri....".
"Telemka hapo kwenye meza njoo tukae hapa
kwenye makochi nina mazungumzo ya maana na
wewe kabla sijaondoka".
Bila kusita aliinuka kwenye kiti na kwenda kukaa
kwenye kochi. Wakati wote huu mdomo wa bastola
haukumwachia hata chembe ya nafasi. Nilikwenda
pale mezani alipokuwa ameacha faili nikalichukua.
Nilikaa upande mwingine wa makochi tukawa
tunaangaliana ana kwa ana.
"Bwana Harrison natumaini tumewahi kuonana?".
"Ndiyo, nafikiri tulionana kwenye tafrija
iliyoandaliwa na Lion Club Hotelini Kilimanjaro".
Nikaweka bastola yangu kwenye paja huku macho
yangu yakiwa yanamwangalia kwa makini.
"Na si mara moja au mbili?".
"Nafikiri ni mara nyingi".
"Nasikitika kusema kwamba leo sikuja kwenye
tafrija ila nimekuja kuzungumza nawe kwa ajili ya
suala la hatari ambalo wewe unalijua vizuri zaidi.
Faili niliyoichukua kwenye meza ilikuwa
imeandikwa "SIRI" halafu kichwa cha faili kiliitwa
"OPERESHENI HUJUMA". Mara moja nikajua katika
faili hili ndimo kulikuwa na maelezo yote ya jinsi
tukio hili lilivyofanywa na hawa majahiri. Ule
ulikuwa ni ushindi thabiti hivyo niliweka faili kwenye
mapaja yangu.
"Sina haja ya kujitambulisha kwako kuwa sasa hivi
nimekuja kukuona kama nani, kwa sababu
natambua unaelewa, au sivyo".
Ndiyo".
"Bila kupoteza muda ningependa kujua, bwana
Harrison, wazo la kuziiba silaha za wapigania
uhuru mkiwatumia wapigania uhuru wenyewe
limetoka kwa Makaburu au kwa mataifa ya
Magharibi?".
"Kwanza kabla sijajibu swali lako nataka kutoa
mshangao wangu kwako jinsi ambavyo umeweza
kupeleleza na kugundua jambo hili ambalo
lilitayarishwa kwa mbinu za hali ya juu. Mimi
ningependa unieleze kwanza jinsi ulivyoweza
kupeleleza mpaka kunifikia mimi kitu ambacho
sikutegemea kabisa. Nafikiri baada ya hapo
unaweza kunifanya unavyotaka kwani hili faili
uliloshika lina kila kitu. Sina hata haya ya
kukueleza mengi; yote utayakuta humo".
Mpaka sasa nilishatambua kuwa Harrison hakuwa
mtu mwenye ujuzi wowote katika mambo ya
kijasusi ila alikuwa ametumiwa tu kwa sababu
ndiye mtu pekee ambaye angeweza kutekeleza
jambo hili bila kushukiwa, na kweli kwa muda wa
miezi sita alikuwa amefaulu kutotambulikana.
"Sawa, bwana Harrison. Nafikiri nitaanzia toka
mwanzo ninavyofikiri ndivyo mambo yalivyokuwa
mpaka kufikia hali hii.
"Mnamo miezi sita iliyopita Rais wa Chama cha
wapigania uhuru kiitwacho PLF, Ndugu Cicil
Chimalamo, alitembelea Urusi kwa nia ya kutafuta
msaada wa kijeshi; yaani silaha kwa ajili ya
mapambano yaliyokuwa yameanza dhidi ya serikali
ya Afrika Kusini.
"Kwa vile Ndugu Chimalamo alikuwa na habari zote
kuhusu nguvu za kijeshi za serikali ya Afrika Kusini
ilizonazo alitoa maombi yake kwa serikali ya Urusi
ili aweze kupatiwa msaada wa silaha za kisasa
walizonazo Makaburu. Ombi hili la Ndugu
Chimalamo lilikubaliwa na serikali ya Urusi na
akaahidiwa kupatiwa silaha hizi katika muda wa
miezi sita. Na kwamba katika muda huo silaha hizi
zitakuwa zimewasili Dar es Salaam".
Akiniangalia kwa makini, nilitoa pakiti yangu ya
sigara ya aina ya Tropicana, nikatoa sigara mbili,
moja nikampa na nyingine nikavuta mwenyewe,
kisha nikaendelea.
"Kwa kutokana na mbinu za kisasa za kijasusi za
mashirika ya kijasusi ya nchi za Magharibi habari
hizi zilinaswa. Ziliponaswa habari hizi ndipo nchi
za Magharibi zilipopasha habari serikali ya
Makaburu tishio lililokuwa linakuja dhidi yao. Hapo
ndipo serikali ya Makaburu ilipokaa chini na kufikiri
nini la kufanya. Uamuzi wa Makaburu ukawa wa
kufanya ujahiri huu ndilo lilikuwa tatizo. Lakini
baada ya kulishughulikia suala hili ambalo nafikiri
walitupiwa wakuu wa shirika la ujasusi, yaani
"BOSI", walifikiria mbinu za hali ya juu na kuamua
kuwa kwa kutumia mbinu hizi wangeweza kufaulu
kuziteka silaha hizi kabla hazijafika mikononi mwa
wapigania uhuru. Bashiri yangu ni sawa na vipi?'.
"Mpaka sasa hujakosea kitu", alijibu.
"Makaburu ni wajanja sana na wanawajua wakuu
wa vyama vya wapigania uhuru vizuri sana. Hivyo
waliamua kumtumia mkuu mmoja wa wapigania
uhuru ambaye walikuwa wanajua kuwa hakuwa na
msimamo kamili, kwa vile walimjua alikuwa
hapiganii hasa ukombozi wa waafrika wanaoonewa
huko Afrika Kusini bali alikuwa akipigana ili apate
cheo. Ukubwa na kujaza tumbo lake ndio ilikuwa
nia yake. Hivyo waliamua kumtumia bwana Ray
Sikazwe wa Chama cha SANP, ambaye ndiye
alipatikana na sifa hizi walizozitaka. Walipofikia
hapa kilichokuwa kimebaki ni namna gani
watamwingia na kuweza kumridhisha kweli
akisaidiana nao katika kuhujumu vyama vingine
angepata kila alichokitaka. Hapa ndipo walipohitaji
msaada wa nchi za Magharibi na hapo ndipo wewe
Harrison ulipoingizwa katika njama hizi".
Nilinyamaza kidogo kiasi chs kupitisha mate.
"Kampuni yenu ya Euro-Afro ni kampuni kubwa
sana, na ina rasilimali nyingi katika Afrika Kusini.
Inamiliki madini ya maangamizi, chromiumu na
platinumu katika Afrika Kusini. Na Afrika Kusini
ndiyo nchi pekee isiyo ya kikomunisti inayotoa
madini haya ambayo yanahitajika sana katika
viwanda vya nchi za Magharibi. Hivyo serikali ya
Makaburu ilizungumza na nchi za Magharibi
zizungumze na kampuni yenu ikiwa na kisingizio
kuwa kama wapigania uhuru hawa wakipata silaha
hizi si serikali ya makaburu tu itaangamia, bali nchi
za Magharibi zilizo na rasilimali zao nchini humo
nazo zitapoteza mali zao. Kwa hivyo swala hili
lilikuwa muhimu kwa nchi za Magharibi kama ilivyo
kwa serikali ya Makaburu.
"Kwa vile Kampuni yenu inamiliki makampuni mengi
katika nchi mbalimbali za kiafrika na mojawapo
ikiwa ni Tanzania, hivyo ilionekana ndiyo kampuni
pekee ambayo ingeweza kusaidia katika suala hili.
Hivyo wakubwa wako waliarifiwa juu ya suala hili
na hatari zake kama halitaweza kushughulikiwa
haraka na kwa kikamilifu. Kwani hatari hii
isingekuwa kwa Afrika Kusini tu ila pia Kampuni hii
ya Kibepari ingeweza kupoteza mali zake zote ikiwa
wazalendo watashinda vita vya ukombozi.
Kutokana na sababu hizi wakubwa zako
walikubaliana na Makaburu kuwa kulikuwa na haja
ya kushirikiana ili kulinda maslahi ya Makaburu na
nchi za Magharibi. Hapo ndipo ulipopashwa habari
namna utakavyoshughulikia suala hili. Mpaka hapo
maelezo yangu ni sawa au vipi?'.
"Sijui ulijuaje?, endelea maana nashangaa sana
jinsi Afrika huru ilivyoendelea katika upelelezi".
"Habari zilipokufikia pamoja na plani yote ndipo
ulipomwita bwana Ray Sikazwe na kumweleza
kama ulivyoelekezwa. Ndipo ulipomdanganya kuwa
serikali ya Makaburu iko tayari kufanya
mazungumzo na chama chake ili wafikie uhuru wa
walio wengi kwa mazungumzo bila mapambano, ila
kwanza atimize sharti moja. Sharti hilo ni
kusaidiana kati ya majasusi wa "BOSI" ambao
wataingia Tanzania kama wanachama wa chama
chake na kundi lake la wapigania uhuru lililokwisha
kufundishwa mbinu za vita katika kuziteka silaha
za chama cha PLF ambazo zilikuwa zikitegemewa
kuwasili mjini Dar es Salaam mnamo miezi sita
hivi".
"Kwani unadhani Makaburu hawawezi kutafuta
suluhisho la namna hii, baada ya kutambua kuwa
umefika sasa wakati wa kuanza kuwachukulia
waafrika kama binadamu wenzao?", Harrison
aliuliza.
"Mimi najibu kuwa baso, kwani kama nia yao
ingekuwa hiyo wasingetaka suluhisho na chama
kimoja tu na kwa siri, wangeliutangazia ulimwengu
na kuomba vyama vyote vinavyohusika na tatizo la
Afrika kusini vishiriki vyote kwa ujumla bila sharti
lolote, la hasha, Harrison. Hizi zilikuwa mbinu tu za
kuhujumu harakati za mapambano ya chama cha
PLF ambacho kinaendelea na mapambano makali
dhidi ya serikali ya Makaburu".
"Sawa nafikiri umenipa msingi wa mambo kama
yalivyopangwa na serikali ya Afrika Kusini
ikisaidiwa na nchi za Magharibi ambao ndio sisi.
Lakini tulifaulu katika kuziteka nyara silaha hizi bila
tatizo, je umekuja kugundua ni nani wanahusika?,
ingawaje juzi tulipata habari kuwa wewe ni
mpelelezi hatari lakini hatukuamini ungeweza
kugundua kitu".
"Nitakueleza sasa. Nilipoanza upelelezi wangu siku
ya kwanza tu niliona mwanga kwani mlikuwa
mmefanya kosa. Kosa lenyewe lilikuwa ni kumwua
kiki. Nilipokuta Kiki amekufa, tulianza kuchunguza
habari zake tukakuta mambo yote aliyokuwa
ameeleza juu yake si kweli, hivyo tukagundua
alikuwa jasusi wa Makaburu waliokuwa wamefaulu
kumweka katika ofisi ya za kamati ya Ukombozi ya
OAU, na ni yeye aliyeweza kufanikisha jambo hili".
"Na mlijuaje kuwa mimi na sikazwe tunahusika?".
"Kosa jingine. Sikazwe nilipomwuliza kama
anamfahamu Kiki alisema aliwahi kumwona mara
moja tu wakati alipofika ofisini kwake na
kumpeleka kwenye kamati ya Ukombozi ya OAU ili
wamsaidie kazi. Sasa tulipofahamu kuwa Kiki
alikuwa na rafiki msichana aitwae Zabibu
nilimtafuta.
"Nilipofika kwake wakati mmemtuma mtu wa
kwenda kumwua nikamkomboa. Yeye huyu binti
alinieleza kuwa Sikazwe alikuwa rafiki mpenzi wa
Kiki pamoja na wewe. Hii ilidhihilisha kuwa Sikazwe
alisema uongo hivyo mara moja nikaanza kumhisi
kuwa yumo katika mpango huu. Nilipojua kuwa kati
ya makampuni yaliyo chini ya Euro-Afro ni pamoja
na Intercontinental Motors ambao ni wakala wa
magari ya "Benzi" nchini hapa nikawa na uhakika
kabisa wewe unahusika. Maana magari
yaliyotumiwa yalikuwa maloli makubwa ya aina ya
Benzi ambayo ni sawa na yanayotumiwa na jeshi
letu. Na magari yote ya jeshi kwa siku ile
yameweza kufahamika yalikuwa wapi. Hivyo
ikaacha sababu moja tu magari yaliyobeba zile
silaha yalitoka kwenye kampuni yenu ya
Intercontenental Motors ya jeshi pamoja na
kuyaweka namba za bandia. Juu ya mavazi ya
kijeshi wapigania uhuru wengi wanayo hivyo, hilo
halikuwa tatizo kwenu. Una swali jingine?".
"Nafikiri umenielewesha vya kutosha na ninakupa
hongera kwani kweli wewe ni mpelelezi maarufu si
Afrika tu ila Ulimwengu mzima. Maswali mengine
niliyokuwa nayo nimekwishajua majibu yake baada
ya kuzungumza na wewe na kuamini mimi
mwenyewe kuwa wewe huwezekani".
Ghafla mlango ulifunguliwa na Issack akaingia
bastola mkononi.
"Karibu Issack samahani kwa kuchelewa nilikuwa
na Bwana Tonny Harrison hapa ambaye ni
mwakilishi wa kampuni ya Euro-Afro ambaye ndiye
alikuwa kiongozi wa tukio la bandarini".
Niliangalia saa yangu nikaona ni saa mbili.
"SWali na mwisho Harrison, silaha mmezificha
wapi?".
"Sikazwe ndiye anajua, na kama umeweza kufikia
hapa sidhani utashindwa hatua ya mwisho".
"Haya simama twende zetu. Issack kalete gari
hapo mbele ya mlango".
Issack alitoka na Harrison bila matatizo alisimama
na kuangalia sebule na vitu vilivyokuwemo kwa
huzuni. Alitangulia mimi nikafuata nyuma. Nilipofika
mlangoni nilizima taa, nikawa na faili kwapani na
bastola ikiwa imemlenga Harrison. Nilirudisha
mlango na kuelekea kwenye lango.
"Askari na mbwa wangu wako wapi?", Harrison
aliuliza tulipofika kwenye lango.
"Sasa hivi wako sehemu ambayo mimi na wewe
hatujafika lakini siku moja tutafika".
Issack alikuwa ameegesha gari mbele ya lango,
Harrison alifunga mlango wa nyuma mimi
nikamfuata na kukaa naye.
"Kwa usalama wako usijaribu kitu chochote",
nilimweleza huku Issack anaondoa gari.
"Mimi hata bastola sijui kuinua, watu hawa
waliniahidi ulinzi mkali na kwamba ingekuwa
vigumu operesheni hii kushindwa. Kumbe
wameniuza. Usiwe na wasiwasi na mimi, sijui
mbinu yoyote mbele ya bastola".
Nikajua wakati wake wa kusema ukweli umefika.
"Vipi bosi?", Issack aliuliza.
"Kituo cha usalama kwa watu kama hawa".
Issack kwa sababu alielewa ni kituo gani cha
usalama alikwenda moja kwa moja na kupiga honi
tulipofika kwenye lango. Mlinzi alikuja akafungua
lango sisi wote wawili tukatoa vitambulisho vyetu.
Akastuka mara moja na kuturuhusu kuingia.
Nilimwongoza Harrison mpaka kwenye ofisi ya
kituo hiki cha usalama.
Nilipofika nilimkuta afisa wa zamu nikatoa
kitambulisho changu, naye akastuka.
"Ndio Mzee".
"Huyu mtu awekwe chini ya ulinzi mkali mpaka
utakapopata maelezo tena".
Niliomba kitambulisho chake nikachukua jina,
namba na cheo chake.
Alikuwa na cheo kikubwa. Kisha nilirudi ndani ya
gari.
"Moja kwa moja ofisini, maana saa tatu na nusu
ndipo kazi kubwa ya kukata na shoka inaanza".
ITAENDELEA
 
NJAMA
SURA YA KUMI
"UHURU UTALETWA KWA MTUTU TU"
Tulipoingia ofisini tulikuta wanatusubiri kwa hamu.
"Chifu anataka kukuona", Eddy alinieleza.
"Mwambie Maselina haiwezekani, nitamwona
baadaye. Sasa hivi hakuna nafasi maana
tukichelewa hapa mambo yote yatakuwa
yameharibika. Mwambie asitoke ofisini mpaka saa
sita. Asipotuona ajue basi makubwa yametupata,
akituona ajue tumerudi na ushindi. Umesikia
Linda?".
"Nimesikia".
"Sherriff, Eddy na Isaack mko tayari kwenda
kwenye uwanja wa mapambano", niliwauliza.
"Bila wasiwasi", walijibu kwa pamoja.
"Na mimi?", Zabibu aliuliza.
"Wewe utabaki hapa na Linda. Tutaonana saa sita
kama tukiwa salama.
"Mimi nataka twende wote, kama ni kufa tukafe
wote"
"Kwanini unataka ukafe naye kwani yeye ni nani
wako", Linda alimuuliza kwa ukali.
"Acheni upuuzi, nyinyi bakini hapa, haya mambo ya
kuleteana haraha, mtatupa mkosi bure".
"Twendeni zetu", niliwaeleza wenzangu nasi
tukaondoka ndani ya ofisi na kuingia ndani ya gari.
Eddy ndiye alichukua usukani na Isaack akaa naye
mbele. Mimi na Sherriff tulikaa nyuma.
"Twende moja kwa moja nyumbani kwangu
tukachukue silaha zaidi. Halafu tutapita nyumbani
kwa Eddy kuchukua silaha tulizoacha kule. Tuna
saa moja ya kujitayarisha kabla ya kuingia kwenye
uwanja wa mapambano.
"Itabidi tutoke kwa Eddy mnamo saa tatu na nusu.
Hii itatupa nafasi ya kuwa nje ya nyumba ya
Sikazwe saa tatu na nusu. Maana ndipo yeye
ataondoka kuelekea huko walikoziweka silaha".
"Kisha niliwaeleza mazungumzo yote niliyoyasikia
kati ya Harrison, Sikazwe na Max.
Kwa hiyo tutakuwa watu wanne tukikabiriana na
zaidi ya watu mia", Isaack alisema kwa mshangao.
"Ndiyo sababu watu kama sisi tunaitwa ni hatari.
Siku moja Isaack utakapokuwa komando kama
mimi utakuwa na uwezo wa kukabiliana na maadui
mia peke yako. Kwa hiyo mimi naona kama ni
afadhali sana kama tuko watu wanne dhidi ya watu
mia. Tukitumia hamasa na maadili na moyo wa
kimapinduzi sina shaka Mungu atatusaidia na
tutashinda na kufichua hizi njama za Makaburu na
mabeberu ya jumuia ya ulimwengu", niliwatia
moyo.
"Nikiwa niko na wewe bosi, huna sina wasiwasi
wowote", Eddy alisema.
"Hata mimi", Sherriff aliongeza.
"Kama ni hivyo, hata mimi ninafurahi kuwa nina
jeshi lililohai na kamanda wake".
"Kutokana na ulivyoeleza komredi, watu hawa
walikuwa wamepanga kuzichukua silaha hizi kwa
meli ndogo kama spea ziendazo Mtwara", Sherriff
alieleza.
"Sawa'.
"Baada ya kufika Mtwara wangefanya nini?",
aliuliza.
"Swali zuri. Watu hawa walikuwa wamejitayarisha
vizuri sana. Hili kampuni kubwa la Euro-Afro lina
meli zake. Meli yake moja itakuwa inapakua mizigo
Mtwara kuingia kesho. Hivyo walikuwa wamepanga
kutoa silaha hizi kwenye hii meli ndogo na
kuzipakia katika meli kubwa ambayo ingelikwenda
kuzitelemsha Afrika Kusini...
"Mipango yote hii iko ndani ya faili nililompa Linda
ampelekee Chifu. Meli hiyo ingekuwa inangojwa
bandari ya East London kutelemsha zana hizi.
Sikazwe angeondoka kesho kwa ndege akidai
anakwenda Botswana lakini angekwenda Pretoria
ambako mimi nafikiri wangemtia ndani mana nia
yao haikuwa kufanya kama walivyomdanganya ila
tu walitaka awasaidie kuziiba silaha kwa sababu
ilikuwa rahisi kwake".
"Kwa hiyo mpaka sasa Sikazwe anakazana bure
tu", Isaack alisema huku akicheka.
"Wajinga ndio waliwao", Eddy alijibu. Tulifika
nyumbani kwangu, nikabadilisha mavazi kuvaa
mavazi ya kikazi yaani koti na suruali yenye mifuko
mingi ili kuweza kubeba silaha za kutosha.
Baada ya hapo tukaelekea kwa Eddy ambako
tulijitayarisha kwa kikamilifu. Kwa bahati nzuri
tulikuwa na majoho mekundu matano tuliyoyateka
kwa hawa majahili. Kila mtu alichukua joho moja,
maana hii ingetusaidia kuwaingilia wakidhani ni
wenzao. Tulipata vile vile kofia tatu ambazo
niliwagawia wenzangu. Nakwambia tulipojaribu
kuvaa tulifanana na wao kabisa. Hivyo tulichoomba
ni kuwa tukute bado hawajabadili mvao wao
unaowatambulisha. Baada ya kuona kila kitu
kimekamilika tulijiandaa kuondoka huku roho zetu
zikipiga haraka haraka.
ITAENDELEA
 
NJAMA
SURA YA KUMI
"UHURU UTALETWA KWA MTUTU TU"
III
Tulitoka kwenye kichochoro kimoja kati ya
mabohari ya sehemu hii na kujikuta uso kwa uso
na bohari ya intercontinental Motors. Tulikuta nje
kuna malori matatu yanapakiwa kwa pamoja.
Kulikuwa na watu wasiopungua ishirini, walikuwa
wanapakia mizigo kwa kupeana. Tuliona gari la
Sikazwe lakini yeye hakuwemo, hali hii ilitujulisha
kuwa yumo ndani.
Penbeni kidogo ya magari haya kulikuwa na
walinzi. Walikuwa hatua kama ishirini kutoka
kwenye magari yaliyokuwa yanapakia kwa kila
upande; baadhi yao walikuwa wamejibanza kwenye
ukuta wa mabohari haya na mengine wote wakiwa
na bunduki mkononi. Habari nzuri wote walivaa
majoho mekundu na kofia. Nilihisi kuwa kulikuwa
na askari wasiopungua ishirini hapa nje.
"Nafikiri wote mmeona ulinzi ulivyo. Kitu
ninachotaka ni kufanya mashambulizi kimya
kwanza mpaka tutakapolazimika kuwashambuliwa
watu wa ndani. Kwa upande huu giza linatusaidia
hivyo walinzi wa huku haitakuwa taabu kuwapata.
kuna walinzi kama sita waliobana upande huu.
Mimi na Isaack tutashambulia kushoto, Nyinyi
Sherriff na Eddy mtashambulia upande wa kulia.
Nawatakia kheri".
Tulipeana mikono kimya kimya kwani hatukujua
nini kitatokea. Mimi nilikuwa wa kwanza kujitokeza
kwenye michongoma na kubana kwenye huu ukuta
wa bohari jingine. Kama hatua tatu kulikuwa na
mlinzi anavuta sigara huku macho yake yakiwa
kwenye gari. Nilimsogelea kimya kimya. Nilipokuwa
karibu kabisa nilimsemesha.
"Sijui watamaliza saa ngapi kupakia, mimi najisikia
kuchoka".
"Sijui hata..." Aligeuza uso kunijibu, nikamkata
karate ya shingo upesi upesi na kumlaza chini.
Nikamwashiria Isaack alipojitokeza nikamwona
Eddy naye ananyata kwenda upande wa kulia.
Nilimnyooshea kidole kimoja kumweleza mmoja
tayari nimepata. Yeye akanitolea alama ya vidole
ya V kuonyesha ushindi.
"Wewe Isaack simama hapa hapa uwe kama wewe
ndiye mlinzi wa hapa, mpaka nitakapokuonyesha
ishara nyingine".
"Sawa", alijibu.
Mlinzi mwingine alikuwa hatua kumi hivi na
hakujua nini kimetokea. Kwa vile nilikuwa nimevaa
kama yeye alifikiri mimi ni mwenzake hivyo
nilikwenda tu kama mmoja wao mpaka
nilipomfikia.
"Vipi kuna wasiwasi wote?", nilimwuliza.
Aliinua kichwa.
"Hakuna....."
Kabla hajamaliza nilimkata karate ya katikati ya
kichwa akafa palepale. Nilimwegemeza vizuri
kwenye ukuta nikamwacha kama mtu aliye hai.
Nilimwunulia Isaack vidole viwili na yeye
akawainulia Eddy na Sherriff ambao sasa nilikuwa
siwaoni. Kumbe Eddy na Sherriff walikuwa
wameenda kwa haraka zaidi, maana Isaack
alinionyesha vidole vitatu kuonyesha wenzetu tayari
walikuwa wameua watatu.
Hii ilinitia moyo sana. Upakiaji uliendelea bila
wasiwasi. Mtu wa mwisho kwa upande huu
alikuwa amebana kwenye kona kabisa ya ukuta wa
bohari hii. Nilimwendea huku nikiwasha sigara. Na
yeye alipoiona aliweka bunduki yake chini akatoa
sigara.
"Sina moto afadhali umepita huku", aliniambia.
Mimi niliwasha kiberiti akaimana ili kuwasha
sigara. Palepale nikamkata karate ya shingo. Bila
hata kukoroma akakata roho. Nikamwegemeza
ukutani halafu nikamfanyia ishara Isaack aje.
"Sawa wewe utasimama hapa mimi nawafuata
walinzi wale watatu waliosimama mbele ya magari.
Kama watashtuka mimi nitajitupa chini wewe
wawahi". Halafu nikatoa funguo za gari.
"Pita hapa kichochoroni panda gari mpaka ofisini
mwambie Chifu aje pamoja na Mkuu wa Polisi
pamoja na askari watakaokuja kulinda na
kuzihifadhi zana hizi baada ya mapambano.
Umenielewa?".
"Sana. Nakutakia kheri".
Nilianza kutembea kuelekea kwa wale watu. Kabla
hata sijafika nilisikia mlio wa 'SMG' kwa upande
wa akina Sherriff. Nikajua mambo yameiva.
Nikainua SMG yangu na kuwateketeza hawa walinzi
waliokuwa mbele ya magari. Isaack hakupata hata
muda wa kupiga risasi ila nilimwona anaingia
uchochoroni na kupotea. Mimi niliruka juu ya gari
lililokuwa karibu, nikakuta watu wanne walikuwa
wanapanga masanduki ya silaha.
"Kumetokea nini?", niliwauliza.
Wote waligeuka na kuniangalia. Pale pale
nikawaachia risasi za kuwaua kisha nikaruka chini.
Milio ya bunduki ilifanya watu wote watoke ndani
ya bohari na kusambaratika hovyo. Watu wote
waliokuwa hapa juu walikuwa wamesharuka chini.
Niliweka sanduku moja kama kinga nikaanza
kutungua mtu mmoja mmoja na bastola yangu
nyenye sailensa.
Kwa vile hawakusikia mlio kutoka sehemu yangu
watu walipiga risasi zao kuelekea upande kwa
upande wa akina Sherriff. Nilipoangalia juu ya lile
gari jingine nilimwona sherriff ameseimama juu na
kuwashambulia adui kwa namna ya ajabu.
Nilimfanyia ishara akaiona na yeye akanifanyia
ishara ya kuonyesha kuwa Eddy alikuwa chini
anajaribu kuingia ndani. Kuona hivyo nilimfanyia
ishara kuwa na mimi nakwenda ndani hivyo
atuchunge wote. Tulikuwa tumeuwa idadi kubwa ya
askari waliokuwa wamebaki ni wachache tu.
Niliruka chini huku nikiachia risasi ovyo hata
niliweza kufika kwenye ukuta wa bohari lao.
Nilitupa SMG nikajitupa kwenye mlango na
kujiviringisha mpaka ndani ya bohari na kama
umeme nikarukia nyuma ya sanduku kubwa na
kuanza kujaza risasi bastola yangu. Huko nje
nilisikia bado Sherriff anaendelea kumimina risasi ili
kuwazuia wasitoke nje.
Nilipoinuka niliona kama kumebaki watu kumi tu
ndani; wengine wote tulikuwa tumewateketeza.
Nilimwona Eddy anaviringisha na kuingia ndani.
Wale watu walimwona na kabla hawajapiga risasi
niliwahi wawili, wengine wote wakarudi kujificha
nyuma ya masanduku.
Eddy aliruka mpaka nilipokuwa.
"Asante bosi umeniponya",
"Usinishukru ndio sababu tuko wote. Kwanza kazi
mliyoifanya wewe na Sherriff sikuitegemea. Kazi
imekuwa rahis kabisa".
"Kuna watu kama wangapi humu ndani?".
"Hawazidi kumi, na wote wako upande wa
mashariki. Nafikiri wanamlinda Sikazwe na Max".
Huko nje kulikuwa kimya; Tukajua Sherriff anasubiri
sasa kashi kashi kutoka kwetu.
"Sasa Eddy lazima tuwafanyie ujanja ili
tuwapunguze. Mimi nitasimama juu ya hili sanduku
ili niwadanganye. Walivyo wajinga walinzi wao
watainuka ili wanipige risasi. Mimi nikiita tu jina
kaa tayari na hii SMG yako kisha anza kumimina
risasi. Mimi nitakuwa nimeisharuka kitambo, hivyo
utawapata kama mchezo. Usiogopea kuwa
unaweza kuniumiza ninakuhakikishia kuwa
nitakuwa sipo".
"Lolote usemalo bosi", Eddy alijibu huku
anatayarisha bunduki yake.
Niliinuka kama umeme juu ya sanduku nikawaona
wote mara moja.
Nikaita
"Sikazwe?".
Hapo hapo kama umeme nikaruka nyuma ya
sanduku jingine. Walinzi wanne wainuka ili
kunitupia risasi huku wakiwa wamejitokeza hadi
vifua. Eddy alimimina risasi na kuwashindilia wote
risasi katikati ya vifua vyao wakafa pale pale.
Nilimwonyesha Eddy vidole kuwa wamebaki watatu,
kwani nilipokuwa nimeruka juu ya sanduku niliona
wako watu saba.
"Gamba, nilisikia sauti ya Sikazwe anaita.
"Unasemaje?", nilimwuliza.
"Naomba tuzungumze, vita umeshinda.
"Sawa Sikazwe, lazima ujuwe kuwa ukombozi wa
Afrika Kusini utaletwa kwa mtutu wa bunduki tu, si
mazungumzo.
"Walinidanganya".
"Hawakukudanganya, shida yako ni kwamba wewe
ni kibaraka; yaani unapenda cheo kuliko watu
wako. Matokeo yake ndiyo haya. Hata Makaburu
wafanye njama za namna gani, mwisho wake
wazalendo watashinda.
Wakati tukijibishana na Sikazwe, Eddy alikuwa
anatambaa chini kuelekea pale walipokuwa.
"Tafadhali tuzungumze?", aliomba.
"Umechelewa, maana umeshaipaka matope Afrika,
hivyo tutakupeleka mbele ya wanamapinduzi wa
Afrika ndio watakao kuhukumu".
"Huwezi kunichukua hai".
Kumbe wakati huu tunajibishana Max naye na
askari mwingine walikuwa wamejivuta karibu
kabisa na mimi. Ghafla nikahisi kuna kitu karibu
nami.
"Bosi", Eddy aliita ambaye pia alikuwa amewaona.
Kusikia tu hivyo niliruka pale nilipokuwa na wakati
huo nikawaona Max na yule kijana mwingine karibu
kabisa na mimi wameinua bastola tayari kufyatua.
Nilijiviringisha hewani namna ambayo hata wao
walishangaa risasi zao zote zikanikosa, wakati ule
ule nikaachia za kwangu nikawapata wote nao
wakaanguka chini.
Sikazwe aliinuka akasimama juu ya sanduku
akachukua bastola akataka kujipiga risasi. Bastola
tatu zililia kwa wakati mmoja na kuupiga mkono
wake. Kumbe Sherriff nae alikuwa amefika
mlangoni na kuona kitendo alichotaka kukifanya
akakizuia. Eddy nae aliona akazuia wakati na mimi
niliona nikazuia asijipige risasi.
"Bado tunakutaka Sikazwe ukiwa hai ili ukajibu
maswali ya wanamapinduzi na wapenda maendeleo
ya Afrika", nilimwambia huku bado anashangaa
jinsi risasi tatu zikitoka pande tofauti zilivyoweza
kupiga kiganja chake tu.
Mara tunasikia usiku mzima umejaa kelele za milio
ya magari ya polisi.
"Chifu yuko njiani", niliwaambia wenzangu ambao
sasa tulikuwa tumemzunguka Sikazwe.
Lo, Bosi ile jiviringisha uliyotoa pale hewani sijaona
hata ndani ya sinema", Eddy alinisifu.
"Mimi nilichoka kabisa; sasa naamini yote
niliyoelewa. Nilifikiri mengine wanakuongezea",
Sherriff alisema.
"Kuwa komandoo siyo mchezo", niliwajibu
nikatabasamu.
Milio wa tahadhali ya magari ya polisi ulisogea
kabisa.
"Ndio sababu sikumwona Isaack", Eddy alisema.
"Ndio sababu", nilijibu.
Tulisikia milango ya magari inafungwa kwa nguvu.
Mara tukamwona Chifu na Mkuu wa Polisi
wanaingia.
"Karibu Chifu, kazi imekwisha. Na mtu wenu huyu
hapa na mwingine nafikiri tayari una habari naye.
Ndani ya malori hapo nje kumejaa silaha, na
zingine zimo humu. Mkienda bandari ndogo (dhow
wharf) mtakuta meli ndogo iliyotayarishwa kwa ajili
ya kusafirisha silaha hizi, sisi hatuna zaidi",
nilimweleza kwa niaba ya wenzangu.
"Kazi nzuri vijana, mmeokoa jina la Tanzania, na
mmeitoa Afrika katika aibu", Chifu alijibu huku
wakitupa mikono ya pongezi.
Mkuu wa polisi alitoa pingu akamfunga Sikazwe
huku sura yake ikionyesha ukali.
Mara nikamwona Zabibu anakuja anakimbia
akifuatiwa nyuma na Isaack. Niliwakonyeza Sherriff
na Eddy, tukatoka pale haraka haraka tukawaacha
Chifu na wenzake wanamshughulikia Sikazwe.
"Oh mpenzi Willy", Zabibu alinirukia shingoni.
"Hamna taabu wote tu wazima", nilimjibu.
"Ashukuriwe Mungu", Zabibu alijibu.
"Isaack gari liko wapi?".
"Oh Bosi, linakusubiri wewe".
"Twendeni zetu, acheni wazee hao wafanye
shughuli zao sisi yetu tumemaliza", niliwaeleza
wenzangu.
Sherriff, Eddy, Isaack, Zabibu na mimi tuliondoka
na kwenda kwenye gari letu huku askari polisi
tuliowapita wakitushangaa na kutupigia saluti.
Tuliingia ndani ya gari letu, huku gari moja la polisi
lenye mlio wa tahadhali limetutangulia.
"Je unajua tunakwenda wapi?", aliuliza.
"Sijui lakini nafikiri imebidi tupewe heshima ya 'VIP'
Isaack alijubu.
Mara gari nyingine ya polisi ikatusindikiza kwa
nyuma.
"Lo, utafikiri Marais", Sherriff alitania.
"Mara moja kwa miaka si mbaya", nilijibu.
"Mimi mnitelemshe kwa Margaret", Sherriff alisema.
"Ala, mipango imeshafanywa nini?", niliuliza.
"Oh, mwenzangu siku nyingi", Eddy alijibu.
"Sawa baba, kazi na dawa", nilijibu huku nikimbusu
Zabibu.
Nilipoangalia saa yangu nikaona ilikuwa yapata saa
sita kasoro robo.
Ilikuwa asubuhi ya Jumapili. Jua lilichomoza
kutokea baharini huku miali yake ya asubuhi
ikichukua rangi ya maji ya bahari na kuipitisha
kwenye vioo vya chumba changu cha kulala.
Mwanga huu ulimmulika Zabibu usoni ambaye
alikuwa bado amelala. Hakika mwanga huu wa
asubuhi ulimfanya azidi kupendeza. Asubuhi vile
vile kulikuwa na upepo baridi uliotoka baharini na
kutufikia sehemu hizi za Upanga. Kwa kifupi ilikuwa
asubuhi njema ambayo sitaisahau.
Niliangalia saa yangu nikaona inapata saa moja
kasoro dakika tatu. Nilinyanyuka na kufungua radio
ili kusikia taarifa ya habari ya saa moja.
Kunyanyuka kwangu kulimwamusha Zabibu
ambaye alinitolea tabasamu la kukata na shoka.
Na mimi nikamrudishia lile la pekee ambalo huwa
nalitoa kwa nadra sana.
"Tusikilize taarifa ya habari", nilimwambia.
Baada ya mlio wa tindo sauti ya kike ikasema.
"Sasa ni saa moja kamili". Halafu ikafuatiwa ya
kiume.
"Ifuatayo ni taarifa ya habari kutoka Radio
Tanzania Dar es Salaam msomaji Godfrey
Chalamila. Kwanza habari kwa ufupi. Majasusi
wawili walioshiriki katika njama za kuiba silaha za
chama cha PLF bandarini wamekamatwa.
Mwili wa msichana mwanamapinduzi Veronika
Amadu aliyeuawa katika harakati za kufichua
njama za wizi wa silaha utasafirishwa kwenda
Freetown, Sierra Leone.
Serikali imetaifisha makampuni yote yaliyokuwa
chini ya Kampuni la kibepari la Euro-Afro.
Habari kamili; Wapelelezi shupavu wa Afrika jana
usiku waliwakamata majasusi wawili na kuuwa
wengine wengi na kuzikomboa silaha na
kuzikomboa silaha za chama cha PLF zilizokuwa
zimetekwa na majasusi waliokuwa wakiifanyia kazi
Afrika Kusini. Majasusi hawa ni Ray Sikazwe,
aliyekuwa rais wa chama cha SANP na Tonny
Harrison aliyekuwa mwakilishi wa kampuni ya
Euro-Afro.
Serikali imetamka kuwa watu hawa watafikishwa
mahakamani siku ya Jumatatu kujibu mashitaka ya
ujasusi na hujuma. Wakati huo huo kamati ya
ukombozi ya OAU imelaani njama hizi za Makaburu
na kusema kuwa lazima Makaburu wajue kuwa
Afrika iko macho na haiko tayari kuchezewa.
Taarifa hiyo iliendelea kusema kuwa chama cha
PLF kitaongeza harakati za mapambano huko
Afrika Kusini ambayo ndiyo njia pekee ya kuweza
kupata uhuru wa walio wengi. Vile vile taarifa hiyo
imesema kutakuwa na kikao cha kamati ndogo ya
siasa mjini Dar es Salaam ili kutafuta njia ya
kuviunganisha vyama vyote vya ukombozi vya
Afrika Kusini, ili moto wa mapambano uweze
kuwaka zaidi.
Mwili wa mwanamapinduzi shupavu hayati
Veronika Amadu aliyeuawa katika harakati za
kupambana na majasusi wa Makaburu ili kukomboa
silaha zilizokuwa zimeibiwa bandarini utasafirishwa
kwenda MJINI Freetown, Sierra Leon ambako ndiko
kwao. Serikali imetoa ndege aina ya Boeng 737
ambayo itachukua na ujumbe wa kijeshi
utakaosindikiza maiti hiyo pamoja na
wanamapinduzi wengine. Imefahamika toka mjini
Freetown kuwa mwanamapinduzi huyu atazikwa
kwa heshima zote za kijeshi. Vyama vya
wanamapinduzi na wapenda maendeleo duniani
kote vimesema vitapeleka wawakilishi wao kwenye
mazishi ya shujaa huyo.
Serikali imetaifisha makampuni yote yaliyokuwa
chini ya kampuni ya kibepari ya Euro-Afro, kwa kile
ilichokiita "Kujihusisha kwa kampuni hiyo na
serikali ya Makaburu ili kupiga vita harakati za
ukombozi. Hakuna fidia itakayotolewa. Na huo ndio
mwisho wa taarifa ya habari".
Nilifunga radio baada ya taarifa ya habari maana
ilinikumbusha Veronika.
"Utakwenda kwenye mazishi?", Zabibu aliuliza.
"Ndio".
"Tutakwenda wote?".
"Hamna taabu. Mambo yatatengenezwa.
TAMATI
 
R.I.P Musiba ulikuwa na kipaji cha ajabu, hii ingekuwa kwa wenzetu tungepata muvi kali kama ya 007...
 
Back
Top Bottom